Wakati mama anaendelea
kunithibitishia yale aliyonihadithia babu , kila mara akili yangu ilikuwa ikiyakumbuka
maelezo ya babu, jinsi alivyokutwa siku hiyo baada ya kupoteza fahamu, akasema;
`Mama yako alinikuta nimepoteza fahamu, na walinihangaikia
hadi nikazindukana, na nilipozindukana, nikawa sijiamini, kwani niliyoyaona
hadi nikapoteza fahamu, yalikuwa yakiniandama kichwani;
‘Baba kulitokea nini…’akaniuliza mama yako.
‘Hata sijui, ….nahisi ni mauza uza ya kuondoka kwa mke
wangu, …’nikamwambai nikiogopa kuongea kile nilichokiona.
‘Baba mbona inaonekana kama ulikuwa ukipigana na mtu , maana
vitu humu ndani vimetawanyika, ….?’ Nikamuuliza babu yako na mume akaulia hivyo
hivyo.
Nikawa najiuliza mengi, je ina maana ni kweli hayo
yaliyonitokea ni kweli sio ndoto, maana kama vitu vimetawanyika, ina maana
kweli nilikuwa nikipambana na mtu, nikaanza kukumbuka yaliyotokea ;
********
Babu aliendelea
kuelezea na ukumbuke kuwa hizi zilikuwa kumbukumbu nikiwa nipo na mama
Siku hiyo nilipanga kwenda milimani, huko kuna jamaa mmoja
ninaye mfahamu, jamaa huyo ana utaalmu wa kupambana na wachawi, na huwa
mkimuita kijijini, anawafichua wale wote wenye vitendo hivyo. Nilikuwa
nimefikia uamuzi huu baada ya kuona nashikwa na majinamizi ya kila siku.
Basi nilipoamuka asubuhi , nikawa najiandaa, niliamua
kuondoka pale tu hawo watoto wakiondoka sikutaka kuwaambia wapi nilipokusudia
kwenda, kwani wasingelinikubalia. Nikaweka vitu vyangu tayari, na nikiwa
nasubiri, nikajilaza kwenye kitanda change, na mara kausingizi kamang’amu
ng’amu kakanijia.
Niliona kitu kama kivuli cha mtu, kikinijia, na huwa
kinanitokea mara kwa mara, baada ya kipindi hicho cha kufariki mke wangu. Na
nilijua kikinijia kinachofuata ni kukabwa, na nisipojitahidi ninakuwa kama
napoteza fahamu kabisa, safari hii sikukubali, nikajitutumua
‘Leo nimekuja rasmi kukumaliza, maana nimekukuanya
hunisikii, …’sauti ya kufifia ikasema
Mimi sikumjibu, ikawa kama kwenye ndoto, nikainuka na
kujiandaa kwa mapambano. Kile kivuli ambacho sasa kilionekana kam mtu, ambaye
sikuweza kumuona sura yake ikacheka kwa dharau;
‘Ndio unataka kufanya nini wewe…’ikasema
‘Nitajilinda na wewe mwanga mkubwa….’nikasema na sauti ya
kicheko ya dharau ikasikika, na kilichofuata hapo ni dhoruba, maana hilo
lijamaa, lililokuwa na umbao kubwa lilinizoa zoa na kunirusha hewani.
Nilihisi nikidonoka kwenye viti, na maumivu yakajaa mwilini
kuonyesha kuwa nimeumia, sikukubali, nikainuka na huku nikikumbuka dua
nlizofudishwa za kujilinda na watu hawa. Tatizo ni kuwa japokuwa nilikuwa
nazifahamu hizo dua, lakini kila nilipokuwa nikitaka kuzitaja, ilikuwa kama kumbukumbu
zimepotea.
‘Nitahakikisha kuwa leo unasalimu amri kwangu….’hilo jitu
likasema.
‘Mimi siwezi kukubali kuwa mtumwa wako, kamwe…’nikasema na
sikujua kwanini nilisema hivyo, ila inavyoonyesha hilo jitu lilitaka nifanye
yale ambayo sikukubaliana nayo.
‘Wewe utakubali tu, wenzako walikuwa wakaidi kama wewe sasa
hivi wahaonekani tena, …’likasema hilo dude, na mimi hapo nikakumbuka baadhi ya
maneno ya hiyo dua, na kila nilipotamka neno moja lile dua likawa kama
linaumia.
‘Oh, ..kumbe ..oh…’likawa linasema huku likionyesha
kupepesuka, na kila hatua nikawa naingiwa na kumbukumbu. Nilipoona limeishiwa
nguvu, nikainuka, na kuchukua kiti. Huwezi amini, kitu ambacho nilikuwa
sikuwezi kukiinua kirahisi, niliweza kukiinua kama chombo kidogo tu,
nikambamiza huyo jamaa.
‘Oh, unajifanya kuwa uan nguvu sio…’likasema hilo dubushwa
na mimi nikawa nimekumbuka ile dua niliyofundishwa na lile lidubwana
likatoweka. Nikayumba na kudondoka chini. Na ndivyo walivyonikuta wazazi wako.
‘Je huyo alikuwa ni nani ananichezea’nikajiuliza pale
walipoondoka wazazi wako, na hapo hapo, nikaamua kwenda huko milimani.
*****
Safari ya milimani haikuwa rahisi, maana ilionekana kuwa
huyo adui yangu alikuwa akijua kuwa safari hiyo ni ya kumwangamiza, basi akawa
ananiandama, kwa kunikabili kwa maajabu ya kila namna, lakini kwa vile
nilishazamiria kupambana naye sikuogopa. Na kila aliponitokea nilikumbua hiyo
dua, na kila nilipoisoma jitu hilo hutoweka.
Nilifika sehemu yanye mto, na hapo nikataka kunywa maji na
wakati naima, nikashitukia nimepigwa na kitu nyuma ya kisogo, kilikuwa kigumu
kama chuma, na nikadondokea kwenye maji, na nilipoamuaka nilijikuta nipe kwenye
chumba kidogo, huku nikiwa nimefungwa kamba za ngozi ya wanyama mikono na
miguu.
Nikiwa nimening’inizwa hewani na chini kuna mijoka ya kila
namna imelala, na mingine ikiwa imeinua vichwa ikiniangalia, kwa uchu, na kila
mara kamba ile niliyofungwa ilikuwa ikiisha nguvu, na kuonekana kunisogeza
karibu na ile mijoka.
‘Sisi hatuna zaidi ni wewe
kukubalina na matakwa yetu..’nikasikia sauti ikisema.
‘Matakwa gani…..hayo. mbona mimi
siwaelewi…’nikawauliza.
‘Kwanza achana na huo mpango wako
wa kwenda huko milimani kwa huyo muhuni anayeingilia kazi zetu, sio kwamba
tunamuogopa sana, …..ila hatutaki kuharibiana katika shughuli zatu, na pili
tunakuhitajia uungane na sisi ….’ile sauti ikasema.
‘Na kama nisipokubalina na hayo
…?’ nikauliza.
‘Basi hatuna budi, …hawo nyoka
wanakuhitaji kwa hamu….na kesho utakutwa ukiwa umeungua kama mishikaki…je umesahau yaliyotokea kwa mkeo, hebu mwangalia kule akiwa katikati ya mto...’ile
sauti ikasema na mara nikamuona mke wangu akiwa kati kati ya moto akionekana kupiga kelele ya kuomba msaada.....'hapo moyo wa uwoga, hasira....ukaniingia
Wakati natafakari hayo, akili
ikanijia kuwa nikubali kwa kudanganya, lakini mara akili nyngina ikanijia, na
nikakumbuka yale maneno ya ile dua, nikaanza kuiomba, na mara nilihisi uvumi
mkali ukienea mle ndani ndani, vumbi, na hilo vumbi likawa linazitawanya zile
nyoka, na moja moja ikaanza kukimbia.
‘Muueni haraka, msimuachie…’sauti
ikasema na mimi sikuacah kuiomba ile dua, huku moyoni nkikumbuka yale mema
niliyowahi kuyatenda kwa watu, maana moja ya amsharto ya hiyo dua ni kuwa
wakati unaisoma unatakiwa ukumbuke yale mema uliyowahi kuyatenda, na mimi mema
yalikuwa mengi hata sikuweza kuyamaliza, na mara nikawa nimesimama peke yangu.
Nikaanza safari ya kupanda milima
na ambonde, hadi nikafika nyika, ambayo ndio makazi ya huko ninapokwenda, na
hapo, nikahisi nipo kwenye dunia nyingine, maana watu wa huko kwetu wandai kuwa
eneo hilo wanaishi watu wasio na dhambi,…ndio maana eneo hilo muda wote lina
rutuba, majani yake ni kijani, matunda ya kila namna yalionekana kila kona.
Nilisimama kwa muda nikishangaa
eneo hilo, na hapo nikakumbuka zile duwa na nikazisoma na nikaiona ile njia
iliyonipeleka hadi kwa huyo mtu niliyemuhitaji, Nikafika kwake, na alioniona
alinikaribisha na hata kabla sijamaliza kuongea akasema;
‘Rudi, huko kwenu matatizo yako
yamesikilizwa,….ila watu wa kijiji chako wataandamwa na misuko suko, kwa yale
waliyoyafanya, wewe utaokoka, kwa maendo yako mema, na kila ukumbuke kuomba na
kuyakumbuka matendo yako mema, kwani ndiyo yatakayo kulinda…nenda haraka…
Basi nikareeja huku kwetu, na
nilipofika nilisikia taarifa ya moto mkali uliozuka, na kuteketeza nyumba ya
yule wanayemuita mtalaamu, na yeye hajulikani wapi alipo, na wengine walidai
huenda aliteketea kama alivyokuwa akiwaamrisha watu kuwatekeza wale aliowaita
ni wachawi…
*******
Kumbukumbu za babu
zikanitoka, na sasa nikawa namsikiliza mama anavyoelezea jinsi ilivyotokea
walipokwenda hospitalini
Kilichonishangaza ni jinsi mtoto wetu alivyopona kwa haraka,
hata madakitari wenyewe walishikwa na mshangao, kwani tulipofika hapo
hospitalini alikuwa na hali mbaya sana, alikuwa amelegea na macho yalishaanza
kugeuka meupe kama mtu asiyekuwa na
damu. Alikuwa katapika sana, na joto la homa lilikuwa kali sana.
‘Kwanza inabidi tumpunguze joto la homa….’akasema docta na
wakataka kumpiga sindano ya kushusha homa, akatuelekeza kwenda wodini, ambapo
matibabu hayo yatafanyika, kwani kwa jinsi walivyomuona waliona ni bora alazwe…wakachukua
vipimo vya kwanza lakini cha ajabu hawakuona tatizo lolote, na mtoto akawa
amezidiwa, na wakaona ni vyema alazwe kwanza, huku akiendelea na matibabu …
‘Sasa tutafanyaje, …kwani mmoja ni lazima abakie na mtoto,….’nikamwambia
mume wangu.
‘Mimi mwenyewe ni mgonjwa, kwahiyo ni vyema nikabakia na
mtoto huku nikiendelea kutibiwa…’akapendekeza mume wangu, lakini sikulipenda
wazo, kwani matatizo yake yanaweza yakamuambukiza mgonjwa, kwani tulishahisi
kuwa huenda ana kifua kikuu.
‘Mgonjwa kweli ataweza kumhudumia mgonjwa….ngoja tuskilizie
matibabu yako kuwa watasemaje, ….nikasema na mume wangu akaelekea kwenye
matibabu yake. Ni kipindi hicho wakati mume anakwenda chukuliwa vipimo, nikabakia
na mttoto, akiwa kalegea, kalala kwenye kitanda cha wodi, na mimi nikajikuta
mwili haina nguvu..
Nilishangaa jinsi gani nilivyojisikia vile kwa ghafla,
nikawa kama nipo kwenye ulevi wa mdawa, nikawa najitahidi kuizuia ile hali,
nikashika macho kuondoa giza lilokuwa liktanda usoni, na hapo nikakumbuka dua
aliyonifundisha babu yako, kuwa nikijis vibaya noisome, ….nikaanza kuisoma huku
nimeweka vidoke kwenye macho, mtoto akiwa kalala kitandani, nikimsubiria docta
aje pale kitandani, kwani alikuwa akiendelea kuhudumia wenzangu na zamu yangu
ilikuwa haijafikia.
Ni wakati huo tunasubiria
matibabu ya mume wangu, na nikiwa namsubiria docta afike kwenye kitanda chetu mara
nikamuona mtoto akiinuka na kutaka kutoka nje,
‘Unataka kwenda wapi?’ tukamuuliza tukiwa tumeshikwa na
mshangao, na wakati huo dakitari wa kumpiga sindano ya kupunguza homa, alikuwa
anakaribia kitanda nilipokuwa nimemlaza mtoto. Nikahisi huenda mtoto anaogopa
sindano
‘Kwenda cheza….’akawa anaongea kitoto.
Docta akafika na kumshika shavuni, akatugeukia na
kutuangalia, na kusema;
‘Mbona hana homa tena..home imeshuka, haina haja, ya kupigwa
sindano, ila chukueni vidonge hivi, mumnyweshe, na kama anataka kucheza, tokeni
naye nje, halafu baadaye mrejee , ili tumchukue vipimo vingine….’akasema na
sisi tukamshika mtoto mkono na kumshusha kitandani, alikuwa amekonda kweli na
mwili ulikuwa mdhaifu lakini alijitahidi na kusimama
Basi tukamshusha kutoka kitandani, kwani alishaanza
kutembea, na akawa anatoka nje, na sisi tukawa tunamfuatilia kwa nyuma, na
alipofika nje,kweli akaanza kucheza, anakimbia huku na kule, na docta alipokuja
wodini ambapo tulishapangiwa, akatukuta hatujarudi , akatufuatilia nje, na
kutukuta katika hiyo hali.
‘Vipi mgonjwa amepona?’ akauliza huku akimwangalia
anavyocheza.
‘Ndio…naona imekuwa hivyo, hata sisi tunashangaa….’tukasema
‘Kuna vipimo nataka kumchukua, mnaonaje tukarudi ndani,
huenda dawa alizokunywa zimefanya kazi yake….’akasema docta.
‘Lakini bado, tulikuwa hatujamnywesha hizo dawa….’nikasema
na docta akamwangalia yule mtoto kwa mshangao, hata hivyo akasema twende ndani
tukachukue vipimo vingine. Na hata vipimo vilivyochukuliwa tena havikuonyesha
tatizo lolote.
Docta akatugeukia na kusema;
‘Kama isingelikuwa ni mimi nimempokea awali, ningewaambia
kuwa mumemleta mtoto, akiwa hana tatizo lolote, labda kama mlitaka kumchunguza
hali yake kwa vile amekonda, lakini mimi mwenyewe ndiye niliyempokea, na
niliona hali yake ilivyokuwa mbaya…nashangaa sasa anaonekana mzima kabisa, na
hata vipimo vinaonyesha hivyo, je hali kama hii inatoka mara kwa mara?’
akauliza
‘Hapana,…hii ni mara ya kwanza kuonekana kupona, siku zote
amekuwa na hali mbaya, joto la homa halishuki, kutapika , hapendi kula kabisa….’nikamwamba
docta.
‘Basi huenda ugonjwa umeogopa umekimbia, baada ya mtoto
kufika hapa hospitalini…’akasema docta kwa mzaha.
‘Kwahiyo docta, unasema hana tatizo lolote,..na hajapata
dawa yoyote…?’ akauliza mume wangu
‘Mimi kwa hali ninayoiona kwasasa kwa mgonjwa, sioni kama
kuna haja ya kubakia hapa hospitalini, ….hana tatizo lolote kwa sasa, na kwa
jinsi mnavyomuona, …..ondokeni naye, na kama hali itarejea kuwa mbaya, basi
mrejesheni….’akasema docta.
‘Sawa docta….’nikasema na docta akamgeukia mume wangu na
kusema;
‘Ila kwa baba yake inabidi arudi kesho kuja kuchukua majibu
yake…sioni kama kuna haja ya kumlaza, au mnasemaje?.’akasema dakitari kama
anauliza.
‘Sisi tunakusikiliza wewe…..’akasema mume wangu ambaye mwili
wake ulikuwa umepungua sana, na alikuwa kikohoa mfululizo, na tulijua kabisa,
kuwa huenda kaathirika na kifua kikuu.
‘Haina haja ya kumlaza, hali yake sio mbaya sana, ila
atakunywa hivi vidonge, ….vitamsaidia huku tukisubiria majibu ya vipimo vyake.
Halafu akamgeukia mtoto na kumwangalia kwa makini, alikuwa akionyesha mshangao
mkubwa usoni jinsi mtoto alivyobadilika kwa haraka kiasi kile.
Basi mimi na mume wangu tukakubaliana yeye atafute sehemu
abakie hapo akisubiria hayo majibu ya vipimo vyake, na mimi na mtoto tukarudi
nyumbani.
Niliporudi nyumbani babu yako alikuwa hayupo, na nikawa na
wasiwasi sana tukikumbuka kuwa tulimuacha akiwa mgonjwa, kwahiyo huenda
kazidiwa kapelekwa hospitali, lakini hata tulipouliza watu , hakuna hata mmoja
aliyefamu kuwa kaenda wapi, tulihangaika huku na kule, lakini hatukupata
maelezo yoyote,sisi tukaona tusubiri, kwani hatukuwa na la kufanya.
Ghafla tukasikia mayowe ya watu, na watu wakawa wanakimbilia
huko mayowe yalipotokea, na kwa mawazo yangu ya haraka, nikamuwazia babu yako,
huenda wamemkuta akiwa kafariki au lolote limetokea ….ikabidi nifuatilie huko
mayowe aylipotokea.
Ilikuwa ni maeneo ya yule wanayemuita mtaalamu, nyumba yake
ilikuwa inateketea, na moto ulikuwa mkubwa sana….
NB: Je ni nini kilimtokea `mtaalamu..'
WAZO LA LEO : Ni
kweli yote yawezekana, wapo walipoona kwa njia hizo, kwa kile tunachoweza
kukiita ni miujiza, wapo waliopona kwa imani zao, hata bila kutumia dawa. Na
hapo ndipo tunapoamini kuwa mungu yupo na akitaka liwe litakuwa.
Imani hizi
hotofautiana, kutegemeana na dini za watu mbali mbali. Kutofautiana huku kwa
imani kusiwe kigezo cha kujenga uhasama uadui na chuki, ….kwani sote ni waja
wake muumba, sote ni watoto wa
Adamu na Hawa, kwanini tusjione hivyo, kuwa sisis
ni ndugu wa baba na mama mmoja, kwanini tusipendane, kwanini tusioneane huruma,
kwanini tunapenda kutafuta vyanzo vya kufarakana, ambavyo hata havipo kwenye
imani za dini, bali ni hisia za uchoyo wetu….vyovyote tutakavyofanya au
kujisikia, katu hatubadili hilo, kuwa
sote ni wana-wa-Adamu.
Ni mimi:
emu-three
7 comments :
Tumekupata mkuu kazi yako ni hazina kubwa
Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli
Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli
Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli
Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli
Hii ni zaidi ya mtandao wa kijamii ni bora uifanye iwe e-book
I used to be able to find good information from your blog articles.
Also visit my blog - Cyclepress.Co.Jp
Post a Comment