Maua akiwa njiani kuelekea hospitali baada ya kupokea simu
kuwa anahitajika haraka, alichukua bajaji, na hakumuaga mama yake mdogo, kwani
hakufahamu wapi alipokuwa kaelekea. Yeye alipoamuka asubuhi, akawa anafanya
shughuli zake, akijua mama yake yupo ndani kapumzika, na mara simu yake ikawa
anaita, akakimbilia chumbani kwake kuichukua simu yake;
‘Wewe ni Maua?’ sauti ikauliza.
‘Kwani wewe ni nani?’ na yeye akauliza kwa mashaka, kwani
namba hiyo ilikuwa ngeni kwenye simu yake.
‘Mimi napiga simu toka hospitali kwa Docta, …ambaye jana
uliongea naye mkaahidiana kukutana naye, ....’akasema huyo mwanadada.
‘Kwahiyo kumbe unanifahamu,…,kuna nini kimetokea, au docta
hana nafasi ya kukutana na mimi tena?’ akauliza Maua.
‘Naomba usipoteze muda, docta anakuhitaji ufike nyumbani
kwake haraka, ….kanipigia simu jana, akaniambai nikifika leo kazini nikupigie
simu, uwahi kwake asubuhi na mapema….’akatulia, halafu akasema;
‘Huwa mimi nina
taratibu za kupitia kwake asubuhi, lakini leo sikuweza kupitia kwake,…ila
alinisisitizia kuwa uwahi kwake, mmalizane, kwani akifika kazini hatakuwa na
muda na mongezi na wewe, natumai umenielewa….’akasema.
‘Nyumbani kwake ni wapi…!?’ akauliza kwa mshangao.
‘Ndio ,….aliniambia kuwa leo atakuwa na maongezi na wewe, na
hayo maongezi anahitaji mkayafanyie nyumbani kwake,…..njoo hapa hospitalini nitakuelekeza wapi anapoishi
kwani sio mbali na hapa hospitalini…’akaambiwa.
‘Haya nakuja…’Maua akasema akiwa na hamasa ya kuongea na
huyo docta, na moyoni alisema safari hii atahakikisha anamuelezea kile
alichokihitajia, hatakubali ampotezee muda na maelezo mengo yasiyomsaidia kitu.
Maua ikabidi aache kazi za nyumbani alizokuwa anazifanya kwa
muda ule na kukimbilia ndani kujiandaa. Na kabla hajafanay hilo akaona ni vyema
amuelezee mama yake mdogo,kuhusu hiyo taarifa, alifahamu kuwa huenda
hataruhusiwa kuondoka mapema, lakini kwa jinsi alivyokuwa na umuhimu na huyo
docta, akijipanga kuwa hata kama mama yake mdogo atamkataza yeye ataondoka tu.
‘Mama mdogooh…’akawa anaita, na alifanay hivyo mara tatu,
lakini hakusikia mama yake akiitika,….kulikuwa kimiya, akaamua kufungua mlango
wa chumba cha mama yake mdogo, ..chumba kilikuwa kitupu,…na ilionyesha kuwa
mama yake huyo hakulala humo ndani, au aliamuka mapema sana na kutandika
kitanda…
‘Haiwezekani mama mdogo, atandike kitanda haraka hivyo, na
kupanda kila kitu,….huyu mtu hakulala hapa, kalala wapi,…’akawa anaongea peke
yake. Alipohakikisha kuwa mama yake mdogo hayupo akachukua simu yake ili
kumpigia mama yake huyo, lakini simu ilisema huyo mtu hapatikani.
‘Huyu mama kaenda wapi, hii tabia yake ya kuondoka bila
kuaga, sio nzuri, hata likitokea tatizo hutaelewa kaelekea wapi…’akawa anaongea
peke yake huku akifunga chumba cha mama yake huyo na kuelekea chumbani kwake
kujiandaa kuondoka.
‘Ngoja niondoke maana huko kwa docta nao kuna umuhimu
wake…’akasema.
Alipomaliza kujiandaa, akaona njia rahisi na ya haraka ya
kufika kwa docta ni kuchukua boda boda,…, akasimamisha boda boda na iliyompeleka
huko Sinza, kwenye zahanati ya huyo docta.
‘Nyumbani kwake ni mtaa wa pili, ukifika kwenye bara bara
kuu ya huo mtaa wapili, ulizia nyumbani kwa dakitari bingwa utaonyeshwa nyumba
yake…au utaiona, ipo kwenye kona ya kuingia barabara ndogo, ina rangi ya
michirizi ya kibuluu kwenye geti lake’akaelekezwa na yule mwanadada, nesi wa
hospitali ya huyo dakitari, na Maua akaondoka na ile ile boda boda hadi huko
alipoelekezwa.
Alipofika eneo hilo, kwa jinsi alivyoelekezwa, akaigundua
haraka, na hakuhitajia kumuulizia mtu, akaisogelea ile nyumba, na kugonga
kwenye geti la hiyo nyumba, akagonga mara nyingi bila kusikia dalili ya mtu
kufungua, kulikuwa kimiya kabisa, akaona isiwe taabu, akafungua mlango wa geti,
mlango ukafunguka, haikuwa umefungwa kwa ndani, na kwa tahadhari akaingia
ndani.
Kulikuwa kimya kabisa, akaisogelea ile nyumba na kugonga
mlango, mara tatu, lakini kulikuwa kimiya,..akatulia na kuginga tena, na tena, hakukuonekana
mtu wa kufungua mlango,kulikuwa kimiya kabisa. Maua akahisi nywele
zikimsisimuka,…akagonga tena mlango, akaona kimiya, akageuka nyuma, akitaka
kuondoka;
‘Hapa kweli panaishi mtu..?’ akajikuta akijiuliza. Na mara
simu yake ikaita, alipoangalia aliona ni namba ya mama yake, na kwa haraka
akaipokea, na kuanza kusalimiana na mama yake….akajisahau kuwa yupo nyumbani
kwa mtu.
Mama yake alionekana alikuwa na kitu cha muhimu cha
kumwambia Maua, alikuwa akiongea kwa sauti ya upole, akaanza kuongea kusudio
lake,akasema;
‘Mwanangu, nimeamua kukupigia simu, maana leo hii nimepokea
simu ya mke wa mzee, akinisisitizia kuwa wewe usije ukaenda kumuibia mume
wake….anasema mume wake, hali yake ni mbaya , na kila akipata nafuu kidogo
anakutaja wewe….akitaka wewe uende huko’akasema mama yake.
‘Mama huoni mimi mnaniweka katika wakati mgumu, kwani nikienda
na kama akiniona atapona, kuna ubaya gani, yeye akishapona, kama ndivyo ilivyo,
nageuza narudi zangu kutakuwa na ubaya gani?’ akauliza.
‘Usiende huko kabisa…..huyo mama kazamiria ubaya, kwani
yaliyotokea huko nasikia ni makubwa zaidi, huyo mama keshaondolewa huko na
watoto wake, kwani wamegundua kuwa alikuwa na dhamira ya kumuua mumewe…yeye
anadi yote ni kwasababu yako’akasema mama yeka
‘Oh, ina mama yule mama ni mbaya kiasi hicho?’ akauliza
Maua.
‘Huyo mama na ukoo wake huku kijijini wanaogopwa….na
nakuomba sana mwanangu, kwa hali kama hiyo, usijiingize tena kwenye hiyo
familia, kwa upande wa huyo mzee hakuna shida, wao tatizo lao ni majivuno tu,…’akatulia.
‘Majivuno, wanajivunia nini?’ akauliza Maua.
‘Utajiri…wao wanajivunia utajiri, kuwa ukoo wao ni wa
kitajiri..’akasema
‘Mama mimi sina nia ya kwenda kuolewa na huyo mzee, kama
walivyovumisha watu, mimi nilikuwa na lengo moja, la kutafuta jinsi gani
watakavyowajibika kwa hujuma waliyonifanyia. Na kama nilivyokuelezea, muhusika mkuu
ambaye ndiye chanzo cha haya yote alikuwa huyo Tajiri, na sasa keshafariki…lakini
kama ulivyosikia mwenyewe alidai kuwa sio yeye aliyenipa huo uja
uzito…’akasema.
‘Mwanangu na bora imekuwa hivyo..sijui ungeliuweka wapi uso
wako kama angelikuwa ndio yeye kafanya hivyo, …ni kwa vile keshatangulia mbele
za haki, ningelikutana naye akiwa mzima,…sijui tungeongea nini, lakini yote ni
mapenzi ya mungu, ninachokuomba uwe mbali kabisa na hawo watu, nakuomba sana
mwanangu..’akasema mama yeka.
‘Kwanini unasema hivyo, kuwa ningeliuweka wapi uso wangu….?’
Akauliza Maua, na kabla hawajaendelea zaidi mara king’ora cha polisi kikasikika
nje barabarani, akeuka kuangalia barabarani, na huku kwenye simu mama yake,
akasikia sauti ya hicho king’ora, akauliza
‘Mbona nasikia sauti ya king’ora cha polisi kuna nini huko?’
akauliza mama kwenye simu na Maua alikuwa kaduwaa, kwani king’ora hicho
kilikuwa kimekaribia hiyo nyumba na kilipofika eneo la hapo kwenye nyumba ,
gari hilo likasimama, na kabla hajamjibu mama yake geti la ile nyumba
likafungulia.
‘Maua kuna nini huko….?’ Mama yake akaendelea kuuliza kwenye
simu, na Maua alikuwa bado kashikilia ile simu masikioni hakuweza kuiondoa, na
hakuweza kumjibu mama yake, hadi askari walipomkaribia na mmoja akauliza;
‘Wewe ndiye uliyetupigia simu?’ akaulizwa.
‘Kuwapiga simu!’ akasema Maua huku akionyesha mshangao,
hakujua ni nini kimetokea.
‘Kuna mtu kapiga simu, kutoka hapa nyumbani kwa docta,
akisema kuwa kumkuta docta kalala chini, na damu zikimvuja huenda kapigwa risasi…’akasema
huyo askari.
‘Mimi sijui chochote, nilifika hapa nikiwa nimepigiwa simu
kuwa nije haraka maana huyu dakitari ananihitajia…wala sijaweza kuingia huko
ndani…’akasema Maua akiwa na wasiwasi.
‘Ulipofika hapa hukumuona mtu mwingine yoyote ulipofika hapa,…?’ akaulizwa.
‘Hapana, ndio nilikuwa nagonga mlango, na mara simu yangu
ikaita na nilikuwa naongea na simu nikisubiri kama huyo docta atafuungua
mlango, na mara nyie mkatokea, ….’akasema na yule askari, akamuacha Maua na
kuelekea kwenye mlango wa ile nyumba, na kujaribu kuzungusha kitasa, mlango akaufunguka
na kuingia ndani, akiwa na wenzake.
Alitoka askari mwingine, na kumwambia Maua asiondoke, kwani
watamuhitaji kuongea naye, na Maua akabakia amesimama pale pale.
Maua alisimama pale kwa muda, hakujua afanyeje kitu gani,
mwili wote ulikuwa umekwisha nguvu, na baadaye akakumbuka kuwa alikuwa akiongea
na mama yake, akakuta simu imeshakatika, akajaribu kumpigia mama yake lakini,
simu ilisema kuwa unayempigia hapatikani.
‘Oh, ni balaa gani hili tena, kwanini kila ninapomkaribia mtu
atakayenifungulia siri ….atakayeniambia ni nani aliyenipa huu ujauzito,
nakutana na mikasa mibaya..’akajiuliza na akachukua simu na kumpigia mama yake
mdogo, na yeye alikuwa hayupo hewani.
‘Ooh, siku ya kufa nyani miti yote huteleza,…..naona sasa ni
bora nisihangaike, ishara hii ya mikasa ya ajabu inaniashiria vibaya, ni bora
niilee hii mimba mwenyewe, na kama yupo ambaye anahusika ..ipo siku
atatambulikana….’akawa anaongea kwa sauti ndogo, na mara akawaona wale askari
wakimjia.
‘Inaonakana huyu aliyepiga simu kaondoka…kama sio wewe, hatujui
ni kwanini hakutusubiri hadi tuje, ilikuwa ni suti ya mwanamke ndio maana
tulipokuona wewe tukujua ndio wewe uliyetupigia simu…’akasema huyo askari.
‘Sio mimi…sijawapigia simu polisi, kwanini niwapigia, maana
hata hko ndani sijaingia..’akasema Maua.
‘Unauhakika kweli…maana hii sasa ni kesi ya mauaji,….sema
ukweli wako, ili ujiweke kwenye mazingira mazuri, …’akasema huyo askari.
‘Mnataka ukweli gani zaidi ya huo?’ akauliza Maua.
‘Muite huyo binti nataka kuongea na yeye..’sauti kali
ikasikika huko ndani. Na mara yule askari aliyekuwa kiongea na Maua,
akamsogelea Maua na kwambiwa waingie ndani.
‘Twende ndani, usiguse kitu kingine chochote, japokuwa
tumeshachukua alama za vidole, lakkini tunaweza kuja tena,….’akasema huyo askari.
Maua hakusema kitu, mwili mzima ulikuwa umkimtetemeka,
hakuelewa ni kwanini, akasogea hadi alipokuwa amesimama askari, ambaye aliongea
naye awali kule nje, …
‘Sasa binti,… kiutaratibu wetu, kwa vile wewe ndiye
tumekukuta hapa inabidi ukaisaidie polisi,…sio kwamba wewe tumekushikilia kama
muuaji…hapana, hiyo itafuta baadaye…’akaambiwa.
‘Lakini mimi sijui lolote, hata mkiwauliza wafanyakazi wake
wa kule hospitalini kwake, …mimi hapa nilikuwa hata sipajui, wao ndio
walinielekeza nifike…na nilikuwa hata sijaingia ndani….’akawa analalamika.
‘Huo ni utaratibu wa kipolisi, tunachojaribu ni kutafuta ni
nani aliyefanya haya mauaji, ..kukuchukua wewe kwa ajili ya kukuhoji,ni
taratibu za kawaida,….usiwe na wasiwasi …’akaambiwa na baadaye polisi
walipomaliza kazi zao , wakaanza kumhoji, na baadaye wakaamua kuondoka naye
hadi kituo chao cha polisi.
*******
‘Unaweza kutuambia kwanini ulipigiwa simu uende kumuona huyo
docta?’ Wakawa wanamuhoji Maua, na alijiona akiulizwa maswali yale yale mara
nyingi, mpaka akajikuta anashikwa na hasira.
‘Siwezi kujua,…’akasema Maua kwa hasira.
‘Invyoonekana hilo jambo alilotaka kukuambia wewe, huyo
muuaji au wauaji hawakutaka uambiwe, kwahiyo ni muhimu sana kama
ungetufahamisha lolote unalohisi ‘akasema askari.
‘Kwakweli siwezi kufahamu, …’Maua akasema huku akizuoa mdomo
kupiga miayo.
‘Huyu docta alikuwa docta wa Mzee mmoja kule Arusha, …na kwa
maelezo tuliyoyapata, wewe uliwahi kwenda kwa huyo mzee,…ni kweli au sio
kweli?’ akaulizwa.
‘Ni kweli….’akasema Maua.
‘Sasa kwanini akakuhitajia kwa haraka kiasi hicho?’
akaulizwa.
‘Mimi nimeshawaamboa sijui, nitajuaje kilichopo kichwa ni mwa
mtu mwingine, kama ni hivyo, hata nyie mnaweza mkakisia muonavyo nyie, lakini kwangu
mimi siwezi kujua ni kwanini akanihitaji kwa haraka hivyo’akasema Maua.
‘Je kwa mara ya mwisho mlionana na y eye lini?’ akaulizwa.
‘Juzi,…na nilikuwa na miadi ya kuonana na yeye leo, mchana,…’akasema
Maua, na wale maaskari wakaangaliana.
‘Wewe umesema kuwa hujui ni kwanini alikuhitaji, na sasa
hivi unasema ulikuwa na miadi naye, huoni kuna kitu unatuficha hapo?’ akauliza
polisi.
‘Umeniuliza kuwa ninajua lolote kuhusu hicho docta
alichoniitia,…hilo ndilo swali lenu, au sio, na jibu lake ni kuwa sijui…mlataka
niseme nini, ningelijuaje kuwa hicho
ndichoo alichokuwa akiniitia kiharaka hivyo,….na hakikuhitaji uharaka huo…’akasema
Maua.
‘Hayo maongezi yenu ya mchana yalihusu nini, matibabu au
kuna kitu gani milipanga kuja kuongea naye,…?’akasema Maua.
‘Hayo ni maswala binafsi,….siwezi kuwaambia, …’akasema Maua
‘Maua,….. isingelikuwa huu ushahidi wa kanda za video
zilizokuwa zimewekwa kwenye hiyo nyumba, ungelikuwa umejiweka kwenye ushukiwa
mkuu, maana unavyojibu maswali yako inaonyesha kuna kitu unatuficha, lakini
tunashukuru kuwa docta alikuwa kaweka, huduma ya ulizindi kwenye nyumba yake,
na kila tukio huwa linanakiliwa kwenye huduma hiyo ya ulinzi…na imeonyesha kila
kitu….’akasema huyo askari.
‘Kumbe ndio maana mnawashika watu wasio na hatia na kuwaweka
ndani,…..hamsubiri uchunguzi, mnakimbilia kuwafunga, …baadaye mnagundua hawana
hatia, mtawalipa nini hawo watu?’ akauliza Maua.
‘Wewe huoni tusipofanya hivyo, tunaweza tusimpate mshukiwa….hizo
ni taratibu za kuwezeha kupata ukweli, ….’akasema huyo askari.
‘Kwahiyo mumegundua muuaji ni nani?’ akauliza Maua
‘Humo tumemgundua muuaji….na yupo mbioni kuwekwa mikononi
mwa polisi, ….na hata huyo aliyetupigia simu ni mfanyakazi wake wa ndani,
aliyefika subuhi, na alipomuona bosi wake katika ile hali, akatupigia simu na
kukimbia…’akasema huyo askari.
‘Kwakweli inatisha kuona mtu kauwawa, hata mimi sizani kama
ningeliweza kusubiria….’akasema Maua.
‘Hapo ndipo mnapofanya makosa, ukikimbia unajishuku,….maana
sisi polisi tukifika, tutakimbilia kukushuku vibaya, …usiwe mwoga kama huna
makosa…’akasema huyo askari.
‘Wewe unasema tu kwa vile ni askari…sasa mimi nataka
kuondoka..’akasema Maua.
‘Mbona una haraka hivyo, hatujamalizana na wewe…’akasema
huyo askari, na Maua akabakia kumwangalia tu.
‘Katika hiyo kanda ya kumbukumbu za matukio iliyowekwa
kwenye hiyo nyumba ya docta,kuna mwanamama mwingine ambaye alikuwa akiongea na
docta,…kabla docta hajapigwa risasi, tunataka umuone, huenda unamfahamu’akasema
huyo askari.
‘Yupo wapi huyo mwanamama?’ akauliza Maua.
‘Utamuona kwenye hii video, …..’akasema huku akimuelekeza
kwenye komputa iliyokuwa mbele yake, na Maua akasogea na kuangali, kwanza
alimuona yule mfanyakazi wa nyumbani akiingia ndani, na alipomuona bosi wake
akiwa kwenye hiyo hali, kalala kwenye kochi, huku damu zinamtoka, akawa
ameshika mdomo, akitaka kupiga yowe,….’huyo ni mfanyakazi wake, uliwahi kumuona
kabla?’ akaulizwa.
‘Hapana mimi huyo simjui…mbona hafanani kama mfanyakazi wa ndani.’akasema Maua, kama anauliza na yule askari akamwangalia Maua kwa haraka usoni, halafu akageuka kuangalia komputa yake na kusema;
‘Na huyo…..’akaambiwa wakati sura ya mwanamke mwingine
ikionekana, huyo mwanamke mwingine alikuwa akiongea na docta ,...na mara docta akawa kashikilia kifuani na damu zikaanza kumtoka,.... ' Yule askari akaipekeka haraharaka ha sura ya yule mwanamke aliyekuwa akiongea na docta, ikaonekana kwa uwazi zaidi.
Maua alipoiona ile sura,..kwanza alitulia kimiya, akiwa kama haamini,...kwani kwa jinsi ilivyoonekana awali, haikuonyesha ni nani alimpiga bastola huyo docta, inawezekana akawa huyo mwanamama aliyekuwa akiongea naye, japokuwa hakuwa na bastola mkononi,.....Na kama huyo aliyempiga docta bastola hakupatikana ina maana huyu mwanamke atakuwa hatarini.
'Oh,....'Maua akaguna, lakini akajitahidi kukaa kimiya, huku mwili na mapigo ya
moyo yakimuenda mbio, …akahisi joo likiongezeka mwilini, na mwishowe alishindwa kujizuia
akasema;
‘Oh,...mama mdogo….’akasema
‘Kumbe unamfahamu ehe….sasa utaongea vizuri, …na utatuambia
wapi alipojificha, tulijua lazima utakuwa unahusika kwa namna moja au nyingine.’akasema
huyo askari
WAZO LA LEO: Tunaweza kukwepa maisha ya kuishi na wasiwasi, na uwoga, kama tutakuwa tunatenda yale yaliyosahihina kuwa wakweli katima shughuli zetu za kila siku. Uwoga, wasiwasi hupelekea kuwa sababu ya kupatwa na magonjwa mabaya kama ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment