Maua alikaribia kile kitanda huku mwili mzima ukitetemeka,
hakujua kwanini alifikia hali ya kujisikia hivyo, kwani japokuwa anajua kuwa
huyo ni baba wa mtoto wake, lakini hakuwahi katika moyo wake kujenga ukaribu wa
hadi kujisikia kama alivyojisikia hivyo leo…, ilikuwa kama mtu anamkaribia mtu
wake wa karibu ambaye hali yake ni mbaya na wala hujui kuwa yupo hai au
ameshakufa;
‘Maua unahitajika hospitalini haraka, Tajiri anataka kuonana
na wewe’akakumbuka alivyoambiwa, pale alipokuwa kijiandaa kuonana na wale
Mabinti wawili kwa ajili ya mazungumzo yao, ambayo hakupenda aendelee kuongea
nao bila ya Tajiri kuwepo, lakini taarifa zilizopatikana ni kuwa Tajiri kapigwa
risasai, na hali yake ni mbaya sana.
‘Mimi….?’ Maua akajikuta anauliza.
‘Ndio wewe, kama mtu yupo mahututi, ni bora ukamuone haraka,
ili ujue hatima yako, hawezi akaondoka hivi hivi, na kukuachai huo mzigo..’akasema
mama yake mdogo.
‘Mama ni kauli gani hiyo tena?’ akauliza Maua kwa hamaki.
‘Maua nkuambie ukweli, huyo Tajiri akiondoka, na lako
limekwisha, ndio maana naona tusimamie kuwa hiyo mimba ni ya huyo mzee, mimi
nimeshaongea naye na kumtishia,….anaonekana kukubali kuwa hiyo mimba ni yako’akasema
mama mdogo.
‘Mama kwanini unafanya hivyo, na lini ulionana naye?’akauliza
Maua.
‘Baada tu ya kupata hiyo taarifa kuwa Tajiri kapigwa
risasai, nikaona sasa hatutapata kitu maana muhusika mwenyewe keshaondoka, ….akili
ikanijia, sikupoteza muda, nikamwendea mzee mzima, nilimkuta yupo peke yake, …nikamweleza,….’akasema
mama mdogo.
‘Mama unajua hayo mimi siyataki, inaonekana kama hii mimba
ni mradi, na hata uhalali wake hauna maana, mimi hayo uliyoongea naye simo
kabisa, na naomba usinihusishe, ulishauri nisiseme lolote kuhusu nani kanipa
hii mimba kwa wale mabinti, na nikafanya hivyo, lakini tangu siku ile nimekuwa
nikijisikia vibaya sana, ….’akasema Maua.
‘Shauri lako,…mimi nafanya haya kwa ajili yako,….kwani
ukiolewa na huyo mzee, ni nani atakayefaidi utajiri wake, ni wewe mwenyewe,
sisi tutakuwa tunadowea tu, na ole wako uolewe na yeye, halafu uje kuniletea
nyodo,…..nitakuumbua, unajua kuumbuliwa, …..basi mimi ni mtaalamu wa kuumbua,…’akasema
huyo mama.
‘Mimi wala sina mpangio wa kuolewa na yeye, na sijisikii
kabisa, eti nikalale kitanda kimoja na yule mzee, haiwezekani,…’akasema.
‘Ulale naye mara ngapi…..?’ akasema mama yake na kugeukia
nje.
‘Una maana gani kusema hivyo, ..unafikiri mimi kuwa naye
karibu, …ndio nimefanya hivyo unavyofikiria wewe, hayo ni mawazo yenu mabaya,….ndio
maana unatangaza kuwa mzee huyo ni mshikaji wangu, sijui nini….mama hebu
angalia nafasi yako kwangu mimi,…mimi ni sawa na binti yako, sijui kweli nyie
mumechangai damu na mama yangu mzazi, maana nakuona upo tofauti ..’akasema
Maua.
‘Mimi ni mtoto majini bwana, harakisha twende huko
hospitalini, na mama yako alisema atafika leo, inahitajika kumuachia ujumbe
kuwa akija atusubiri hapa nyumbani, nimjuavyo kwa kiherehere chake anatataka
kuja huko hospitalini..’akasema mama mdogo.
‘Sio kwa kiherehere chake, ni uchnugu mwa mwana,…..nitafurahi
sana akija na kuwa karibu nami, maana tangu nipete hiyo taarifa kuwa huyo
Tajiri ananihitaji mwili wangu wote umekwisha nguvu , najisikia vibaya…..’akasema.
‘Hicho ni kimimba chako kinakupa shida, hakuna lolote, kama
ungekuwa unamjali huyo Tajiri, ungelishafunga ndoa naye mapema, lakini
unaringa,….sijui unachoringia ni nini, …..maana umasikini upo hadi kwenye kope
za macho, sasa unapata bahati, unaichezea, nakumabia, utakuja kujuta,..hasa
kama hutafuta nitakavyokuelekeza’akasema mamd mdogo.
‘Umenielekeza nini tena?’ akauliza Maua.
‘Umeshasahau….unaona ulivyo, …nakuambia hivi, sasa hivi
hicho kimimba ni cha mzee mwenyewe, Tajiri hana lake, kwahiyo ukifika kwake,….sijui
atakuambieje, lakini vyovyote iwavyo, kuanzia sasa kauli yetu, pamoja, ….na
mama yako ndivyo anavyojua, kuwa mimba hiyo ni yam zee, sio ya Tajiri tena, …huyo
keshakufa, ……..’akasema mama mdogo.
Maua akamwangalia mama yake mdogo, lakini akili yake haikuwa
kwa huyo mama yake, akili yake ilikuwa kwa huyo anayekwenda kukutana naye, je
atamkuta yupo hai, na kama yupo hai, yupo katika hali gani, na kwanini amuite
huko hospitalini, ni kwa ajili ya hiyo mimba au kuna jingine la zaidi…
‘Haya mama twende, …..’akasema Maua
*********
Maua alikisogelea kile kitanda, na alipokaribia akasimama,
hakufika karibu kabisa, kwanza macho yake yakaangalia yale mashine
yanayoonyesha mtiririko wa mapigo ya moyo, akaona jinsi gani ile michirizi,
inavyopanda na kushuka, na hapo akawa an uhakika kuwa huyo mtu bado yupo hai, …..akasogea
hatua nyingine..
Akatupa jicho pale kitandani, alimuona huyo mgonjwa,akiwa na
mipita iliyotoka mwilini mwake, na alipomwangalia usoni, alijua kuwa huyo
mgonjwa kalala, na mgonjwa kama huyo kama kalala hahitajiki kusumbuliwa, akaona
ni heri kwake, kwani kwanza katimiza wajibu, pili kahakikisha kuwa bado yupo
mzima, na tatu, hakuweza kuongea naye, kwani hakutaka iwe hivyo, asije akajawa
na simanzi za kumbukumbu ya maongezi yao, hasa kama itatokea kuwa hatapona.
‘Lakini atapona….mungu wangu msaidie apone, mbona ataniachia
mtihani mkubwa…’akajikuta akisema kwa sauti bila kujitambua.
‘Sitapona Maua….muda uliobakia kwangu ni mfupi sana,….nakuomba
usogee hapa karibu kwani nina mengi ya kutaka kukuelezea, kabla pumzi yangu ya
mwisho haijaisha…nakuambia haya, maana wewe nakuamini, na wewe unaweza
kumsaidia mzee, mjomba wangu….’akashituliwa na sauti iliyotokea pale kitandani,
…
‘Oh,…nilijua kuwa umelala, sikutaka kukusumbua…’akasema
Maua.
‘Usipoteze muda, sogea hapa karibu, kwani ninayotaka
kukuambia ni muhimu sana, …..ni kuhusu hiyo mimba uliyo nayo…na chanzo chake’akasikia
hiyo sauti tena, iliyokuwa ikitoka kwa shida, na Maua aliposikia hiyo kaulii
kuwa ni kuhusu hiyo mimba, akajikuta akisogea kwa haraka na kuja kusimama
karibu na kitanda, lakini hakutaka kukaa
‘Kaa karibu yangu, ili usikie kila kitu…’ile sauti ikasema,
na Maua akasita, lakini akasogea pale kitandani na kukaa karibu na huyu
mgonjwa. Aligeuka, kumwangalia , lakini hakugeuza kichwa kizima , alikuwa kama
anaogopa kuangalia kitu cha kutisha.
‘Maua usiniogope,….bado sijafa, sura yangu ni ile ile….huenda
baada ya saa moja ndio unaweza kuniogopa maana sitakuwa kama mimi tena,
mtatanguliza sifa yangu, ….sifa ambayo najua kila mtu atakuja kuwa nayo, ni
swala la muda tu…’akatulia.
‘Kwanza naomba nikuombe msamaha kwa yote niliyowahi
kukutendea, najua usingelifikia hiyo hali kama isingelikuwa ni mimi….na yote
hayo ni kwasababu ya tamaa ya kutafuta utajiri,….na ushawishi wa hawo wanaoitwa
wataalamu, au waganga wa kienyeji, na wasomi, wanatumia elimu yai vibaya……lakini
ni kweli tulipofuata hayo waliyotuelekeza tulifanikiwa…..japokuwa kiukweli
utajiri huo haukuwa na raha…sijawahi kupata raha,….hilo nakuambia ukweli….’akatulia.
‘Utajiri wa haramu, hauna raha yoyote, unakuwa na mali,
unakuwa na kila kitu, lakini moyoni, hakuna raha, kila muda unawaza ubaya
uliowahi kuufanya, kila muda, unajishuku,……hakuna raha,……na madhambi mengi
niliyoyatenda, yamenifanya niwe kama mtumwa wa shetani….’akatulia.
‘Wengi wanajua kuwa mzee yaani babu yangu ndiye aliyenipa
yote hayo, lakini….nakuhakikishia kuwa mjomba wangu, …ni tajiri ndio, lakini
mambo kama haya, nilikuja kumshirikisha kinamna tu, na yeye hakukubali moja kwa
moja, ila aliona anipe nafasi nifanye nijuavyo mimi….baada ya kumshurutisha, na
najua aliamua kunipa kila nilichomshurutisha, ili baadaye aje kunisuta…’akatulia.
Wengi wanajua kuwa mjomba utajiri wake ni …..wakishirikina…..lakini
nikuambie ukweli, kwake yeye mambo hayo alikuwa akiyapinga sana,…unajua kwanini
alimuacha mke wake?’ akauliza, na Maua alitaka kusema kitu, lakini huyo jamaa
akaendelea kuongea;
‘Ni kwasababu mke wake aliendekeza sana mambo hayo….na
mwanzoni kwa sababu ya upendo, mzee wa watu , kipindi hicho alikuwa sio mzee
hivyo, ni mbaba, akawa anamfuata mke wake anavyotaka, kwa shingo upande,
akajikuta anatumbukia kwenye lindi la kufuatilia mambo hayo ya kishirikina, na
hata akajulikana kuwa ni mtindo wake, na utajiri wake umepatikana kwa njia
hiyo,…lakini nafsini mwake alikuwa hapendi, hadi ikafikia mahali akashindwa, na
kusema mimi sitaki tena mambo hayo….
‘Wengi wanajua kuwa mzee huyo aliniita na kunikabidhi mikoba
ya utajiri wake….lakini sio kweli, mimi mwenyewe ndiye nilikwenda kwake na
kumshinikiza kuwa nataka hayo mambo aliyofanya hadi akawa tajiri…nilijaribu
mara nyingi, lakini mjomba alinikatalia kata kata, …lakini sikukata tamaa,..ikawa
kila siku nipo na yeye . Na baadaye nikaona niwasiliane na mkewe, na hapo ndipo
nilipofanikiwa. Mkewe akanifichulia siri ya huo mkoba, lakini…aliniambia kuwa
yeye kwa vile hayupo karibu naye tena, hawezi kujua mumewe kauweka wapi.
‘Nenda kamwambia wewe unauhitaji huo mkoba kwa vile yeye
hautaki,…na ukiupata huo, nitakuelekeza jinsi gani ya kufanya, maana mengi ya
masharti yake, yanawahusu wanaume…..’akanimabia mkewe
Mjomba aliposikia kuwa nimepata maelekezo hayo toka kwa
mkewe, akaona kweli nimezamiria, na kwa kipindi hicho walishaanza
kukorofishana, akaona isiwe shida, akaniambai nimpe muda autafute huo mkoba upo
wapi,…na kweli siku moja nikafika kwake, akaniuliza mara mbili, tatu, kuwa
kweli nahitajia mamb hayo…
‘Maana mambo hayo mimi siyataki tena….kama kweli una ubavu
huo, mimi nitakupa, kwa msharti kwamba, mimi sitabeba lawama yoyote, na kwa
kukuhakikishia hilo, nenda na huo mkoba kwa mke wangu, yeye atakuelekeza
mwenyewe, mimi sijui, na nimesahau jinsi gani ilivyotakiwa iwe…’akasema.
‘Wewe mjomba usijali….nataka na mimi niwe tajiri, kwa njia
yoyote ile…’nikamwamba, basi njoo kesho, kwa leo siwezi kukupa, ila nilitaka
kujua kweli una dhamira hiyo. Nikasema ninayo, na nikaondoka, na kurudi kwake
siku ya pili yake.
Nilipofika kwake, ndio akaniambia kuwa kuna mambo mkewe
alikuwa akiyafanya akiamini kuwa ndio yanayoleta utajiri…..nikamuuliza je ni
kweli yaliweza kuleta huo utajiri, akajibu huenda yanaleta, lakini yeye haamini
sana kuwa ndivyo, na hawezi kunipa jibu la moja kwa moja kuwa yanaweza kuleta
au la,….
‘Mpwa wangu, lakini masharti yake ni mabaya,….unajua mambo
haya ya kishirikina yalivyo, najuta kwanini niliamua kuyakubali…’akasema
mjomba.
‘Lakini mjomba huoni ulivyotajirika,….inaonekana kweli
yanafanya kazi yake…’nikamwambia na yeye alisema utajiri wake, ni wa
kuhangaika, pamoja na kupata bahati ya kuyapata hayo madini, na hana uhakika na
hiyo imani, ila kweli alifuata alivyotaka mkewe na maelezo ya huyo mganag wa
kienyeji, kwa hivi sasa hayataki na hayaamini, kama mimi nayahitaji nichukue, ….kama
sitaki basi yeey atachoma moto…
Nikamuuliza kama hayaamini, mbona wengi wanaamini kuwa hayo
ndiyo yaliyomletea utajiri, hata mke wake anasema hivyo, akasema kweli kila
walipokwama mkewe alimchukua hadi huko kwa huyo mtu aliyekuwa akiwasiliana na
mkewe, na kuna mambo wakiyafanya, wanajikuta wakifanikiwa….lakini yeye hakuyapenda,
…..na wakati mwingine aliona ni kama siku hiyo waliamuka na bahati ndio
wakafanikiwa .
‘Kama hukupenda kwanini ulikwenda huko?’ nikamuuliza,
akasema yeye kwa kipindi kile alikuwa akimpenda sana mkewe, na mkewe alipenda
sana mambo ya starehe, utajiri,… na hakupenda kumuuzi, na kwa vile walikuwa
wanafikia muda wanakuwa hawana kitu, na mkewe anakuwa hana raha, basi inabidi
afuate anavyotaka mkewe….na akajikuta anashiriki kwenye shiriki ambayo
hakupenda, na kwasasa kaamua kuachana nayo kabisa….
‘Mimi nilishasikia kuwa utajiri wa madini haupatikana bila
mambo hayo….nikamwambia mjomba, na mjomba akapinga vikali sana kauli yangu
hiyo, akidai, kuwa kuna muda mwingine alikuwa akifanikiwa hata bila kutumia
mambo hayo, ila kazi hiyo inahitajia kusubiri, kujituma na kutokukata tamaa…. .
‘Mjomba tangu nifike hapa Mererani, nimejituma sana,
nimesubiri sana, lakini sikuweza kufanikiwa, nakuomba, nipe mimi kama hutaki
hayo mambo,…mjomba akaniasa sana….kuwa hataki kwenya familia yao mambo kama
hayo, na katika mambo ambayo alifikia hadi kukosana na mkewe ni pamoja na hilo,…na
mengine ambayo ilibidi yafanyike ili ushirikina huo ufanikiwe…’akasema.
‘Mjomba nipe , mimi nilikuwa nayatafuta sana mambo haya na
nimesikia kuwa unayo…nipe, na usijali, nitajitahidi kuangalia jinsi gani
nitayafanya bila ya w ewe kuhusika….’nikamwambia, na mjomba akasema yeye hataki
kushirikishwa kwa hilo tena, ila kama nitakuwa tayari kufanya biashara na yeye
, yeye yupo tayari…Mimi nikang’ang’ania anipe kwanza hayo mambo
‘Mimi nitakuapa, japokuwa sikupenda iwe hivyo….lakini
sitaweza kukuelekeza lolote lile..’akasema
‘Wewe nipe tu nitajua mwenyewe…’nikamwambia, nikijua kuwa
nitakwenda kwa mkewe atanielekeza, kwani nilishaongea naye, na mkewe ndiye
aliyenituma nikaongee na mumewe, ….nimbembeleze hadi avitoe kama bado anavyo.
‘Mimi siwezi kwenda kumuona mume wangu, kwani hatuelewani
tena, na hata sina uhakika kama hivyo vitu anavyo au keshavichoma moto….na huyo
mtaalamu aliyetupa hizo dawa, na mazindikio yake hayupo tena, hajulikani wapi
kapotelea…wengi wanasema keshakufa..’akaniambia mke wake, siku aliponifunulia
siri ya utajiri wa mumewe.
Basi kweli mjomba akavitafuta kule alipokuwa kaviweka mkewe,
akavikkuta na kunikabidhi, na yeye akaondoka zake,…hakutaka hata kuniangalia
usoni, kwani anasema kuwa siku ndugu zake wakigundua kuwa ndio yeye kafanya
hivyo, sijui ataupeleka wapi uso wake…
‘Unajua ndugu zangu nimekosana nao kwasababu ya huyu mke
wangu,…hawakutaka kabisa nimuoe, kutokana na hsitoria ya familia yake, lakini
tulitokea kupendana sana….mwanzoni,…..na walipoona kuwa nafanya kila anachotaka
yeye, ndugu zangu wakadai kuwa nimeshategewa amdawa,…na wakajaribu kunikanya na
ndipo nikaanza kukosana na wao, kwa vile niliona wananiingilia kwenye ndoa
yangu, basi wakanitenga, wakidai kuwa sote ni washirikina, ….’akaniambia
mjomba.
‘Na sasa wewe umekuja huku kwangu, watasema nimekuvuta kwa
nguvu za giza, ili uje tushirikiane, kwa vile watoto wangu wamenikimbia kwa
sababu mimi na mke wangu ni wachawi, …...’akaniambia mjomba.
‘Mjomba wewe usijali, siku nikiibuka tajiri, wao wenyewe
watakuwa wakija kunipigia magoti, na kuniita bosi…’nikamwambia mjomba, lakini
ilionyesha kuwa mjomba hakuwa na raha, na maamuzi yangu hayo
‘Na kweli toka siku hiyo mjomba akawa hana raha,…na cha
ajabu, jina lake likawa linatumika vibaya,..na najisikia vibaya kusema kuwa
mimi nilikuwa mmojawapo ambaye nilitumia jina lake vibaya, na kila nilichofanya
mimi, nilifanya kwa kusema nimeelekezwa na huyo mzee…’akatulia na ilionekana
kama hataongea tena, halafu baadaye akasema.
‘Nikuambie ukweli, mimi ilifika hapo Merarani sina mbele wa
nyuma, na aliyeniingiza mjini, na kunielekeza mambo mengi, …na hata
kunishawishi niwe karibu na mjomba,….mjomba ambaye ndugu zake ikiwemo mimi,
tulikuwa tunamchukia kuwa hapendi ndugu, …ni mchawi,….lakini nilipokuja kukaa na
yeye, niligundua kuwa sio kweli…mjomba ni mtu mwema sana, kama ukimjulia….na
haamini mambo hayo ya kishirikina.
‘Mimi nikamjulia,nikawa karibu naye tukaivana…na aliponipa
hayo mambo, nikawa nayafanyia kazi kwa maelekezo ya mkewe, na washirika wake, ambao,
mjomba hakujua kuwa nipo nao ….nikaanza kuchuma mali. ….Kidogo kidogo, nikaanza
kuzoea, kwani mwanzoni, nilikuwa nikiogopa, …kuna mambo machafu yalitakiwa
kuyafanyika, …hata kuua…, kumwaga damu za watu, ….sasa ni jambo ambalo
linahitajia moyo wa kinyama…
Wenzangu hawakuogoap kabisa, na kila niliposhindwa jambo,
wao walilifanya bila kuogopa, na kwa vile tulikuwa na mtu ambaye ni mtaalamu wa
kufikia mashimo…na kufuta nyayo za machafu tuliyoyafanya, hatukuweza kukamatwa
kabisa….nikuambie ukweli…kama isngelikuwa hawa watu washirika, nisingelifikia
hapo nilipofikia, najuta sana, na wenyewe wameshanigeuka, na wamefikia hatua
hii ya kuniua, eti kwasababu nitataja siri zai, na pili, sitaki kuwapa huo
mkoba…
‘Siwezi kuwapa na wala hawataupata kamwe….kwani hata kama
ningeliwapa wangeliniua tu, kwanii walishanichoka, kwa kile wanachokisema kuwa
mimi ni kigeugeu, na nimwasaliti,na katika makubaliano yetu ni kuwa
atakayewasaliti wenzake, adhabu yake ni kifo….na hii ndio adhabu yangu, sijutii
kwa hili,,…naona nastahili kufanyiwa hivi kwa dhambi nilizozifanya…ila
nasikitika kuwa wadhambi wenzangu wataendelea kuwa hai….’akakohoa na kutulia.
‘Maua…nikuambie ukweli, mimi bila hawo wenzangu,
nisingeliweza kufanya lolote,…Malikia alikuwa kichwa changu, yeye ndiye
aliyekuwa akinielekeza nini nifanye, na nini nisifanye, na utakuta kuwa mambo
mengi alikuwa akinielekeza yeye….na nilikuwa nayafanya lakini sipendi, ila
inabidi, na ilifikia hatua waliamua kutafuta mambo ambayo yatanishinikiza
nifanye yale wanayotaka niyafanye, nisipofanya wananitishia, kuwa wataniumbua…
Nilitamani kwa muda mrefu niondakane na huyu mtu anayeitwa
Malikia, lakini haikuwa rahisi kiasi hicho,…kwani alionekana kama ndiye msemaji
na muongozaji, …na pale nilipopata huo mkoba na kupata maelekezo kutoka kwa mke
mjomba, … hutaamini , malikia alimgeuka shangazi, .., alikosana kabisa na mke
wa mjomba, na mke wa mjomba akatishiwa, kwani walichukua mapicha yake mabaya,
waliyomtegea, na kuambiwa kama asipohama huu mji, watamuumbua, ikabidi mama wa
watu ahame kabisa, ….maana zilikuwa picha chafu sana, na huo ndio uliokuwa mtindo
wao, kama hawataki kukuua,….
Kwahiyo kwenye kundi, kama viongozi, walibakia mimi, kama
mtu muhimu, ambaye, nilihitajika kwa ajili ya mali za mjomba,….pamoja na ujanja
wao wote,lakini mjomba alikuwa akiogopewa, hakuna aliyeweza kwenda karibu
yake,kumfanyia loloye, na wakawa wananitumia mimi…mwishowe, Malikia, akawa
anashinikiza nimuoa yeye, ili aweze kuingia ndani ya himaya ya huyo mzee…nia na
lengo lake kumuondoa huyo mzee…
Uchumba wa nguvu ukafanyika, na malikia akaanza kuzoeana na
huyo mzee, na ….nikuambia ukweli, malikia ni mjanja sana,..anaweza kuigiza hali
yoyote, na ukaamini ni kweli…..alipofika kwa huyo mzee, alijifanya binti mwema
sana…..adabu nyingi,….na alifanya hivyo kwa muda, hadi mzee wa watu akalainika,….na
sijui kama ni kweli, kwani wengine hata mimi, nilihisi hivyo, kuwa huenda malikia
aliwahi hata kutembea na huyo mzee, sina uhakika na hilo..
Malikia alikuwa akipanga mambo, na alikuwa kiongozi wa wazi,
na wengi wanajua kuwa yeye ndio kiongozii mkuu, lakini sio kweli…na wengi wanajua
kuwa mimi huenda ndiye kiongozi muhimu kwenye kundi, lakini sio kweli, kuna
watu, ambao tuwaite ni majembe….hawa ndio waliobuni kila kitu…tangu mwanzo ,
hata kabla mimi sijakanyaga Mererani.
Hawo walipanga mambo hayo siku nyingi, wakachukua kumbukumbu
za matajiri wote wa hapa Mererani na kuwaweka kwenye mitandao,…na walikuwa wakijua
kila kitu wanachokifanya hawo matajiri, na walichotaka ni kuwapata watu kama
sisi tusioona mbali na kututumia, lakini mwisho wa siku watu hawa walikuwa
wakineemeka bila jasho, …ni matajiri, lakini hawavumi……
Pamoja na ujanja wa malikia, lakini kwa watu hawo malikia
alikuwa akiwanyenyekea, kwani wao walikuwa sio tu na siri za kila mmoja wetu,
lakini kisheria walikuwa wanajua jinsi gani ya kujitetea, walikuwa ni wasomi.
Na hata kijamii, walikuwa wakionekana ni watu wema,…lakini kiukweli, walikuwa ni
chui, waliovaa ngozi ya kondoo,….wabaya na washirikina japo ni wasomi…usiwaone
hivyo, usomi wao, na mambo yao ya siri ni tofauti kabisa….
Nikuambie ukweli, watu hawo ndio walikuja kumshawishi mke wa
mjomba, hadi akawa anashirikiana nao,..hadi wakafanya hayo waliyoyafanya…na walifanikiwa
kwa vile walishajua uzaifu wa huyo mwanamama,….na mjomba hakuwa kugundua kamwe
kuwa wabaya wake, ndio marafiki wake wa karibu…..ilifikia hatua mjomba alitaka
kumuacha mkewe mapema, lakini kwa mambo jinsi yalivyowekwa,
ilishindikana,..maana kama nilivyokuambia kila wanalolifanya wana njia ya
kujikinga,….ukitaka kwenda kushitaki, wanakuwahi na machafu waliyoyahifadhi
dhidi yako….unajikuta unashindwa kufanya lolote, bali nikuwafuata watakavyo…
Mzee wa watu akawa anaishi maisha kama hayo….na hakujua kuwa
wanaomzunguka ni marafiki wake wakubwa, marafiki ambao alikuwa akiwaambia kila
kitu,….na cha ajabu zaidi ni watu walisoma naye shule ya msingi, na walitoka
kijiji kimoja, marafiki wa utotoni, lakini kumbe wenzake walishajua uadhaifu
wake, na wakautumia, kumuangamiza….na sasa mtoto wa dada yake, kashirikishwa….unaona
ilivyokuwa..’akasema huku akijaribu kujizuia, alionekana kusikia maumivu.
Mjomba alifanya la maana sana kuwapeleka watoto wake shule,.
…na shule ikawafungua macho, wakajua kuwa baba yao, na familia yao kwa ujumla
ipo kwenye utumwa fulani japokuwa ni matajiri, walichofanya wao ni kujitenga….huku
wakifuatilia kwa mbali…hadi walipoona ni jinis gani wataingia,…na kumuokoa baba
yao…..na sasa wamekuja wakiwa wamejiandaa…
Akatulia kwa muda, bila kusema jambo, mpaka Maua akahisi
huyo mtu keshapoteza fahamu, lakini mashine ilionekana kufanya kazi, na Maua
akasogeza mkono kutaka kumshika mkononi, lakini alipoufikisha mkono wake, ….
‘Najua mwisho wa siku wote waliokuwepo watanifuata …..kutokana
na tabia zao….Maua ngoja nikuambie nilichokuitia hapa kabla sijachelewa, kwani
naona nguvu inaniishia, ……’akasema na akawa kama anatetemeshwa,…na baadaye
akatulia, ikachukua muda tena, na baadaye akasema;
Maua,…pamoja na mengine mengi,…niliyokuetendea, lakini
nakuambia ukweli, moyo wangu, ulikuwa kila mara unasita kufanya baya lolote
kwako..na hutaaminii nikikuambia siku ile, sikuweza kufanya lolote baya kwako,
kama inavyoonekana…..’akatulia na Maua akaanza kuhisi vibaya, na kila mara
akiongea na huyo jamaa kuhusu siku hiyo, kuna halia anaisikia akatulia na
kujaribu kutoiwazia.
‘Maua kuna mambo yalifanyika siku ile,..na aliyekuwa nyuma
ya yote ni Malikia, na washirika wake,…sikuweza kufanya lolote kwako, sikuweza
kabisa….nilishindwa, ….na ikaidi nitoke nikanywe pombe, ….nilijisikia vibaya
sana..nikalewa, na niliporudi nikiwa sijitambui, nikashikwa na usingizi mnzito
ajabu….’akatulia.
‘Nina uhakika moja kwa moja kuwa mimba hiyo siyo ya kwangu….’akasema
na Maua akashituka na kusema;
‘Mwongo mkubwa wewe usitake kukataa …..’baadaye akakumbuka
maneno ya mama yake mdogo.
‘Maua ukitaka kuhakikisha siku ya kujifungua, kapime, na
chukua damu yangu mapema, ili uhakikishe, mimi nakuelezea ukweli…..kuna mambo
alinifanyia Malikia kila nikijaribu kukutana na mwanamke mwingine ….sifanyi
kazi, ila kwake tu…na ndivyo ilivyokuwa siku hiyo…hilo nakluhakikishia,…
‘Sasa ni nani aliyenipa huu uja uzito?’ akauliza Maua kwa
sauti ya kinyonge.
‘Nitakuambia Maua, aomba niendelee kuishi, maana naona mwili
unaishia nguvu,….nitakuambi ni nani….’mara akaanza kukoroma, na Docta akaingia
na kumwambia Maua mgonjwa anatakiwa kupumzika.
NB: Je ni nani, aliyempa Maua uja uzito?
WAZO LA LEO:Thamini
sana rikizi, kipato cha jasho lako, kwani jasho lako hilo, hata kama linawakera
wengine, lina thamani kubwa sana mbele ya muumba wako, kuliko kukaa kwenye
viyoyozi, na kusubiri kupata kutoka kwa wavuja jasho, Tukumbuke kuwa jasho la mtu
haliliwi hivi hivi, lazima utakuja kulilipa.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Waliosema haitawezekana leo, mbona imewezekana, hata mimi mwenyewe sikujua kuwa ninaweza kufanikisha sehemu hii, maana nimeiandika kwa kujiiba
Thanx God kwamba hiyo mimba ya Maua siyo ya Tajiri ambaye ni babaake mzazi! i was so worried yaani. Halafu mkuu jitahidi basi kupunguza maongezi marefu yaani yanakuwa yanajirudia rudia sana, tukio moja linaongelewa muda mrefu sana hadi inachosha kusoma. Samahani kama nimekukwaza ila huwa najikuta naskip sehemu kubwa ya stori pale inapojirudiarudia sana.
Hongera sana.
Post a Comment