Hali yangu ilikuwa yenye utata, maana
ilifikia hatua naweza kufika sehemu na kujisikia vibaya, na hapo hapo
nikapandisha, na kuwa mtu tofauti kabisa, na kitakachotokea hapo siwezi
kukijua, nakuja kuhadithiwa baadaye, kuwa nimefanya maajabu,…sikumbuki, na hata sielewi jinsi nilivyoweza kufanya hayo ninayokuja kuhaditihiwa baadaye kuwa eti ni mimi nimeyafanya’
Akaendelea
kuhadithia kisa hiki, msimuliaji wetu mkuu, Maua binti Maua.
**********
‘Haya uliyo nayo ni mashetani, inabidi tukahangaike, …na
nashukuru sana pamoja na hayo uliyomtendea yule tajiri, bado amekubali kukusaidia,
hali yake kwa sasa inaendelea vyema,…’akasema mama mdogo.
‘Lakini yote haya namtupia lawama yeye, huenda
yasingelitokea kama isingelikuwa ni yeye,…..mbona mwanzoni nilikuwa sina
matatizo kama haya’akasema Maua.
‘Huenda ulikuwa nayo, ila yalikuwa hayajachokozwa…au ndio
umekumbana nayo, au kuna mtu kakutupia, ….binadamu hawana wema, kijicho na
husuda kwa binadamu ni kawaida..., ‘akasema mama mdogo.
‘Wanionee kijicho kwanini, kwani mimi nina nini cha kuonewa
kijicho, wanataka umasikini wangu, au wanataka nini…mimi siamini hayo, nahisi
yote yamesababishwa na huyo Tajiri wenu..’akalalamika Maua.
‘Tatizo lako huangalii mbele, unachoangalia na nyuma, hayo
aliyokutendea yamepita, ….na alifanya hivyo kwasababu,…’akatulia
‘Kwasababu gani?’ akauliza Maua.
‘Hayo ni siri kubwa, sisitahili kuyasema, ila yanafungamana
na utajiri wake’akasema mama mdogo huku akiangalia huku na kule , kama
kuogopa,watu wasije wakamsikia.
‘Huoni, ina maana utajiri wake, ni wa kishirikiana, na
kwahiyo hatasita kunifanyia lolote baya, ilimradi afanikiwe zaidi’akasema Maua.
‘Afanye nini baya…kama ni yeye, basi usingelimdhuru
yeye…’akasema mama mdogo huku akikimbuka kashkashi la siku ile………….
******
Mama mdogo, wakati
anamsubiri Maua ,akijua Maua yupo ndani na bosi, na huenda mambo yakawa mazuri,
siku hiyo wanaweza kuondoka na mshiko wa nguvu, akaona walinzi wa Tajiri,
wakikimbilia ndani, na yeye kwa umbea akajitosa, …
‘Na wewe unataka kwenda wapi?’ akauliza na mmoja wa walinzi
‘Mwanangu yupo huko ndani, lazima nijue kuna nini
kimetokea….’akasema huku akisukumana na yule mlinzi.
‘Mwacheni aingie, huenda akatusaidia, maana sisi huku ndani
tumechemsha, …na bosi kasema tusimua’akasema mmoja wa walinzi.
Mama mdogo aliposikia hivyo, `tusimuue…, ‘akahisi kuna
tatizo kubwa limetokea, akaruhusiwa na kuingia ndani, na pembeni akaona Tajiri
akiwa kalala kwenye sofa, na kitambaa kikiwa kimelowana damu, alikuwa
akilalamika maumivu..
‘Docta keshafika…’akasikia mmoja akisema.
‘Kwanini tusimkimbize hospitali..’mwingine akasema
‘Bosi kasema hataki kupelekwa hospitalini, anahitaji
kutibiwa hapohapo….’akasema huyo mlinzi.
Mama mdogo, akageuka huku na kule akimtafuta mwanae, na
pembeni kabisa, akamuona Maua kalala chini, na alionekana kabisa hana
fahamu….akamsogelea, na mmoja wa walinzi, akasema;
‘We mama we unataka kufa, wenzako wote waliomsogelea sasa hivi
ni majeruhi, mwanao kageuka kuwa simba, ananguruma kama simba….’akasema mmoja
wa hawo walinzi. Na mama mdogo aliposikia hivyo,akasimama na akakumbuka kile
kichupa, ambacho, walishapewa na mmoja wa mtaalmu ambaye siku moja walikwenda
kwake kupata tiba.
Akatoa kile kichupa, na kumsogelea Maua, akachukua kisogo na
kuyatupia mwilini kwa Maua. Na mara Maua akainuka, kama anataka kusimama,
halafu akarudi chini na kulala, akatulia kimiya….
‘Kumbe unayo dawa…’akasema mmoja wa walinzi.
‘Sikujua kuwa kumetokea matatizo, ningelijua
ningelimuwahi’akasema mama mdogo.
‘Kwani binti yako ana matatizo gani?’ akauliza mmoja wa watu
wa karibu wa huyo mlinzi.
‘Sijui, tunahisi kakumbwa na mashetani’akasema mama mdogo.
‘Basi muhangaikieni…..hali aliyo nayo sio ya kuicha
hivyo….hilo ni tatizo kubwa, na nawashauri ili atibiwe vyema, rudini huko
alipotokea, kijijini kwenu, ….mara nyingi mambo hayo chimbuko lake ni huko
kijijini, na mara chache inakuwa ni kukubwa na hayo mashetani ….lakini
ukichunguza sana chanzo chake ni huko alipotokea….kama mna imani kweli, nendeni
kwenye dini zenu akaombewe,…..’akasema huyo mtu wa karibu wa Tajiri.
‘Tumeshaanza matibabu, …’akasema huku akitulia pale
alipomuona Maua akiinuka na kukaa vyema, na alionekana kama kushangaa, akawa
anaangalia mikono yake, ikiwa na damu.
‘Kwani kumetokea nini?’ akauliza
‘Ulitaka kumuua bosi wetu…’akasema mmoja wa walinzi.
‘Kwanini nimuue bosi wenu,….?’ Akauliza Maua huku akimwangalia
yule tajiri kwa wasiwasi, na kujaribu kukumbuka ni nini kilitokea, lakini akili
ilikuwa haikumbuki…ilikuwa kama mtu aliyekuwa kwenye usingizi mnzito…hata akili
zilipotulia alichokumbuka ni ila hali ya kujisikia vibaya, na kichwa kuuma, na
kusikia sauti zikimuamrisha kufanya jambo, na baada ya hapo hakukumbuka
jingine…..
‘Mimi sikumbuki kitu…’akasema Maua huku akishjika kichwa, na
kushangaa jinsi nywele zake zilivyovurugika, tofauti na zilivyokuwa mwanzoni.
‘Huyo binti keshazindukana, ….hakikisheni kuwa yupo sawa, ….?’
Akauliza mmoja wa walinzi
‘Ndio keshainuka, naona yupo shwari kwa sasa….’akasema
mlinzi mwingine
‘Basi bosi anahitaji aletwe mbele yake…’akasema yule mlinzi
wa mwanzoni
Walinzi kama kawaida yao ni kutii amri, na kwa haraka
wakamsogelea Maua, japo kwa tahadhari, wakikumbuka kile kilichotokea kwa
wenzao, wakamshika Maua mikono huku na huku, wakimuongoza kwenda kwa tajiri yao.
‘Msinishike hivyo, kwani mimi siwezi kutembea
mwenyewe..’akalalamika Maua pale alipoona wanakuwa kama wanambeba kama anavyobebwa
mgonjwa, na walipoona Maua akilalamika, wakamuachia, atembee mwenyewe hadi pale
alipolala Tajiri yao,.
Tajiri, aliinua kichwa, na kumwangalia Maua kwa muda, halafu
akajiinua na kukaa vyema, akakohoa, na kusema;
‘Natumai sasa nafsi yako imesharizika,….lengo lako lilikuwa ni
kuniua au sio ndio maana ukabeba kisu…’akageuza kichwa kumwangalia mama mdogo, wakati
huo mama mdogo alikuwa mbali , hakuweza kusikia vyema wanachoongea, ila
alionekena kushika mdomo, kuonyesha kushangaa jambo, huenda wale walinzi
walikuwa wakimsimulia yaliyotokea.
‘Maua,….kubeba kwako kisu inaonyesha ulidhamiria,….aaaah,
lakini tutaona,…, bahati nzuri, hukuweza kutimiza lengo lako,…sijafa, sasa una
nafasi ya kufanya hivyo tena, lakini safari hii sitaweza kukupa muda huo,…..itakuwa
zamu yako…huwezi kunitoa damu yangu hivi hivi nikuachie…’ akasema kwa ukali.
‘Mimi sielewei unaasema nini…kwani ni mimi nimekufanya
hivyo?’ akauliza Maua huku akionyesha mshangao.
Tajiri akamwangalia Maua kwa muda, halafu akageuka kuangalia
kule alipo mama yake mdogo, akaonyesha ishara huyo mama aletwe mbele yake, na yule
mama alipofika hapo mbele yake akaulizwa;
‘Binti yako ana matatizo gani?’ akauliza kwa sauti ya ukali
‘Nahisi kakumbwa na mashetani’akasema huyo mama
‘Kwanini hujamshughulikia, huoni kuwa hii ni hatari,
angeliweza kunitoa roho, …sikuamini binti mrembo kama huyu anaweza kugeuka kuwa
simba, na kunishinda mimi…mimi mwenyewe nina yangu yana nguvu, lakini ya huyu
binti yalizidi….ilikuwa ni balaa…ananguruma kama simba….anakuwa kama jamaa
mmoja, sijui ni wapi,….nilihadithiwa kuwa ana tabia kama hiyo’akasema huku
akitabasamu.
‘Bosi na wewe una mashetani?’ akaulia mmoja wa watu wake.
‘Ya kwangu sio mashetani bwana, huwezi kuyaita hivyo,…ni
mambo ya kimila….hata hivyo, mimi siwezi kudhibitiwa, kama wanavyodhibitiwa
watu wa mashetani, mimi nayadhabiti ya kwangu, ….nayapa amri,…na napata kile
ninachokitaka, sio kama haya, …..’akatulia na kumwangalia huyo binti.
‘Mimi sina mashetani….siamini mambo hayo…’akasema Maua, na
Tajiri akamwangalia kwa muda, halafu akageuka kumwangalia mama mdogo
‘Sasa kama anahitaji msaada wangu ninaweza kumsaidia, nina
mtu mmoja ninayemfahamu, anaweza kuyaondoa hayo madude, kabisa…..’akageuza kichwa
na kumwangalia huyo binti.
‘Mimi sihitaji msaada wako, ninachohitaji ni kuilea hii
mimba’akasema Maua.
‘Hilo tumeshamaliza binti,…’akamwangalia yule binti na huku
akiwa kama anataka kuinuka, akaendeela kuongea kwa kusema;
‘Mbona nilishakuandikia ushahidi, unataka nini tena….au unataka
hayo aliyoagiza huyo shetani wako, maana kaamrisha kuwa twende huko kijijini
kwa mama yako,…huko nitapata maagizo mengine, eti kuondoa ….sijui alitumia neno
gani, hata sikumbuki vyema,…eti….nisipofanya hivyo, akinijia tena, atahakikisha
kuwa anaichukua roho yangu…hahaha…mimi sio mtu wa kutishika, kirahisi, lakini….’akasita
pale alipomuona Maua kama anatetemeka.
‘Aaah, mwangalieni, aisije akapandisha tena….’akasema huyo
Tajiri.
‘Atapandisha tena, kama usipotii hayo maagizo yake’akasema
mama mdogo huku akitoa kile kichupa na kumnynyuzia huyo binti mafuta.
‘Huwezi kunilazimisha kwa njia hiyo, ila mimi sina shida,
tutapanga hayo, ….na nilikuwa na mazungumzo nyeti na nyie wawili,….’akatulia na
kuwaangalia wale akina mama wawili kwa zamu, na baadaye akawageukiwa walinzi
wake na kusema ‘Naomba mniache na hawa watu wawili, msiwe na shaka hawezi
kupandisha tena…’aaksema Tajiri.
Baada ya wao kubakia wawili, akainuka na kukaa vyema,
aliangalia sehemu ile aliyoumizwa, akawa anapitisha kidole juu kuiweka vyema
ile bandeji, na baadaye akamwangalia Maua, na mama yake mdogo, akasema;
‘Nimejifunza jambo moja…..pamoja na mambo mengine yote, mimi
nimetokea kumpenda binti yako,…’ akainuka na kusimama.
‘Vinginevyo, asingelitoka hapa hai,….ningeliweza kufanya
lolote, na bila kufanywa lolote, ….mtu kaja kwangu na kisu….ushahidi
ungelionekena…..na wewe huenda unajua, atachukuaje kisu aweke kwenye mkoba wake
wewe usijue?’ akamuuliza mama mdogo, ambaye alibakiwa kushangaa, alikuwa hajui
kabisa kuwa binti yake alikuja hapo na kisu.
‘Nasema kwa moyo wangu wote,…kuwa pamoja na haya, mimi
nimemsamehe, sina kinyongo na yeye, ….lakini kama anataka haya yaishe kwa
usalama, atahitajika na yeye kutimiza wajibu wake....hata hivyo siwezi
kumlazimisha, ila kiukweli, moyo wangu utauma sana, kama atachukuliwa na mtu
mwingine…’akatulia na kumwangalia huyo binti.
‘Kwahiyo unataka kumuoa?’ akauliza mama mdogo.
‘Huko unakwenda mbali saana…umekimbilia hatua ya juu, hayo
yatakuja baadaye, kama mambo yatakwenda vyema, tutafanya hivyo…ni kweli
nahitaji mke, kwani maisha haya ya kuishi leo huyu, kesho huyu nimechoka
nayo,….sasa nahitaji kutulia na mke mmoja ninayempenda, ….na nakiri huyu binti ananifaa’akatulia
kidogo.
Yule mama akatabasamu huku akimwangalia binti yake,
akamshika begani, na kusema kwa sauti ya kunong’ona..’Unaona, bahati hiyo….’
‘Hayo hayana haraka, cha muhimu…na kwanini unataka mambo
hayo kwa haraka…?’ Yule Tajiri akamgeukia mama mdogo safari hii akionyesha uso
wa tabasamu.
‘Sasa mara nimekwenda kwa haraka,..wakati wewe mwenyewe umeshazimia kwa binti yangu, na kwa ujumla unahitaji
mke, ungenipenda mimi, mzee mwenzako….’akasema kwa utani, na yule Tajiri
akaceka hadi jino la mwisho.
‘Mimi sioni kama kuna kizuizi, maana umeshampa uja uzito,
haina haja ya kuruka huku na kule, wewe toa mahari….ndoa haina umuhimu sana
maana umeshaifunga kwa nguvu’akasema mama mdogo.
‘Tatizo lako wewe mama una tamaa, tamaa ya pesa, pesa ni
ibilisi mkubwa, ….’akatoa pesa mfukoni na kuzishika hewani, na wakati huo yule
mama akawa anaziangalia kwa hamasa, na yule tajiri alivyoona jinsi yule mama anavyoziangalia
zile pesa kwa tamaa akamtupia usoni.
Yule mama bila aibu akaziokota na kuzifutika kifuani,…..Maua
akamwangalia mama yake kwa uso wa hasira, alitamani kumwambia azirudishe kwa
mwenyewe lakini akaona ajinyamazie, tu, na wakati huo huo yule jamaa alikuwa
akiongea utafikiri hilo tendo alilofanya halikuwa na maana kwake, akaendelea
kusema;
‘Wewe mama kwa tamaa yako ya pesa …..utafika kubaya,….na nahisi
kabisa kuwa wewe, ndiye umemchuuza huyu binti wa watu, sikupenda kabisa haya
yamtokee huyu binti, wakati mwingine najuta sana,…..huyu sio mtu wa kutendewa
hivi, huyu binti sio watu wa aina yako,….lakini imeshatokea hakuna jinsi, na
mimi naahidi kuwa nitamsaidia kwa nguvu zangu zote, lakini kama yupo tayari kwa
hilo….’akasemaTajiri huku akimwangalia huyo binti.
‘Mimi kama ulivyosema, ….kuwa umeambiwa twende huko
kijijini, kwa mama yangu, hilo wazo naliunga mkono,…twende huko huko kwa mama
ili akuone wewe ….uliyeniharibia usichana wangu, ….’akawa anatoa machozi.
‘Unalia nini sasa….’mama yake akasema kwa ukali huku
akimminya begani, na akawa kama anamnong’oneza….`sasa usiniangushe hapa ndipo
pa kucheza karata vyema…’.
‘Naona tumemalizana, nyie kajiandaeni, nikiwa tayari,
nitawaambia, safari ni lini, …na mumesema kwenu ni wapi vile?’ akauliza.
‘Singida,..mpakani….’akasema mama Mdogo.
‘Aaah,, basi haina shida, maana huko ndiko njia yangu nikiwa
na mambo yangu,….hata hivyo nilikuwa na safari ya huko, ….ni siku nyingi
sijafika, …’akawa katulia akiwaza jambo,….akamwangalia Maua, kwa makini,
baadaye akajikuta akiuliza;
‘Kwani wewe mama yako huko kijijini anaitwa nani?’ akauliza
‘Maua….’akasema Maua.
‘Kwani huko Singida unakujua?’akauliza mama mdogo, na yule
Tajiri hakujibu kitu, alikuwa anamwangalia Maua, pale alipoulizwa jina la mama
yake, akataja `Maua’, alihisi kuwa huenda huyo binti akili yake haijakaa sawa.
‘Wewe binti nakuuliza swali la msingi, huwezi ukaitwa Maua
na mama yako akaitwa Maua..’akasema yule Tajiri na Maua akabakia kimiya huku
akiangalia chini.
‘Haina shida…’akasema huyo Tajiri….huku akiwa kama anawaza
jambo, akamgeukia mama mdogo na kusema;
‘Kwani kiutaratibu, huko kwenu inatakiwaje, kwanza natakiwa
kwenda mwenyewe kujitambulisha au natuma mtu, maana mimi nataka nianze
kufuatilia taratibu zote, sitaki utani, nataka kuyabadili maisha yangu…’na
kabla hajamaliza simu yake ikaita. Akaipokea bila kuangalia nani aliyempigia.
‘Oh, ….nisamehe…mpenzi….’akasema pale aliposikia huyo
anayepiga simu ni nani, akageuka kumwangalia Maua, na baadaye akainuka na
kuelekea chumbani kwake,..
Binti akawa anaangalia kule alipoelekea huyo Tajiri na huku
akisema;
‘Unaona…..nilikuambia huyu mtu ana mke wake, na mimi anataka
kunifanya mke wa pili…’akalalamika Maua.
‘Hana mke huyu….’akasema jamaa ya huyo Tajiri
‘Sasa huyu anayeongea naye ni nani?’ akauliza.
‘Ni dada mmoja mtata,,,,,malikia wa Mererani….sijui mtaivana
kama akisikia wewe unatakiwa uolewe na huyu bosi, maana, mwanamke huyo ana
wivu, lakini hataki kuolewa,…..’akakatisha pale Tajiri aliporudi.
‘Natumai tumemalizana,…Maua upo tayari kuolewa na mimi?’
akauliza
‘Kama utamuacha huyo hawara wako,….’akasema Maua.
‘Hawara gani?’ akauliza Tajiri akishangaa.
‘Huyo anayeitwa Malikia wa Mererani’akasema na yule tajiri,
akabakia akishangaa, akawageukia watu wake akiwa kakunja uso,…..akasema kwa
hasira;
‘Ni nani katoa siri zangu za ndani….’akatoa sauti ya hasira,
na yule eliyeoongea akapiga magoti akiomba msamaha,….
‘Mkuu, sikuwa na nia mbaya ….niliongea hivyo ili kuongeza
wivu, ….wivu unasaidia kwenye mapenzi…..’akasema .
‘Toha humu ndani haraka,…na hutakuwa kwenye kikosi changu
tena, na adhabu nyingine zitafuata baadaye, ….sitaki msaliti kwenye kundi
langu…’alaipomaliza kuongea tu, wale walinzi wakambeba yule jamaa juujuu, huku
yule jamaa akilia na kuoba msamaha…
‘Kama maisha yenyewe ndio haya,….mimi siolewi na
wewe’akasema Maua na kutoka nje…
NB: JE tumalize ….?
WAZO LA LEO: Ni kweli tunahitaji pesa kwa ajili ya maisha yetu, lakini kupenda pesa huko kusivuke mipaka, na kujikuta tunasahau ubinadamu, pesa ni mtaji, lakini pia pesa ni kishawishi kibaya, zinaweza kutupeleka kubaya..Tuwe makini na hilo.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Oh my God! Maua katembea na babaake mzazi! nimeshahisi huyo tajiri ni Adam ambaye ndio alimpa mimba Maua kijijini akakimbia!
Hi there evегу onе, hегe every
peгson іs sharіng ѕuсh κnow-how, therеfore
іt's nice to read this weblog, and I used to go to see this webpage daily.
My page :: loans for bad credit
Tusubiri hatima yake, na kisa hiki kipo wazi tuone ni nini kitatokea. Swali kubwa la kujiuliza, kama wewe ni mzazi yamekufika hayo ungelifanya nini?
Post a Comment