Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, November 14, 2012

Uchungu mwa mwana aujuaye ni mzazi-22




  Mzee Adui aliinuka kwenye kiti chake cha enzi huku akiwaza kuhusu hiyo taarifa aliyopewa, akamwangalia yule askari aliyemletea hiyo taarifa kwa muda mrefu na macho yake makali, hadi yule askari akaingiwa na waiwasi. Yule mzee akilini mwake alikuwa akimuwazia huyu askari, ni kweli anamfahamu sana kama mmoja wa vijana wake anaowatumia kwa upelelezi, na mara nyingi akimletea taarifa zake huwa ni za ukweli, lakini kwa mtizamo wake wa harakaharaka, hilo jambo aliloambiwa haliwezekani,…akatabsamu na kusema;

‘Una uhakika kuwa kweli kuwa huyo kijana wao, kauwawa, …?’ akauliza tena swali hilo , hiyo ilikuwa ni mara ya tatu, anauliza swali kama hilo hilo, na yule askari akawa anatoa maelezo yale yale, aliyokwisha kumuelezea mwanzoni, kwa jinsi alivyosikia na jinsi alivyofuatilia na hata kuweza kuongea na maaskari wahasimu wao, ambao waliandamana kwenye huo msafara.

‘Mzee,mimi nimeongea mwenyewe na mmoja wa maaskari wao, ambaye aliongozana na huyo kijana, yeye ndiye alikuwa kiongozi, baada ya huyo kijana wao, wanayemuita jemedari wao. Kwahiyo taarifa yake tunaipa uhakika kuwa ni ya kweli…’akatulia yula askari kumpa nafasi mzee wake kuyaweka hayo maelezoakilini, halafu akaendelea kutoa maelezo;

‘Kama unavyomjua jamaa huyo, huwa hapendi kushindwa, na siku hiyo ya tukio walikuwa katika moja ya mafunzo yao, maana siku nzote siku hizi wana mafunzo magumu, wanatuiga. Walipofika pale kwenye mto, kwa maelezo ya huyo askari, wakidondosha moja ya mzigo wao, uliokuwa na vifaa vyao muhimu, na ilihitajika lazima mzigo, huo uokolewe.

Mwenzetu huyo akaamua kujitosa,…kama unavyojua mzee, kwenye ule mto kuna sehemu ambazo haziingiliki, hata kama ungelijua kuogole, kwasababu ya matope, unaweza ukaona maji juu, kumbe chini ni matope. Wenzake waliogopa,….walijaribu kumshauri kuwa ndani ya ule mto, huwezi kuingia kipindi kama hiki, kwani pia mamba wengi wana njaa, hakusikia…’akasema 

‘Aliingia kufuata huo mzigo tu, au kulikuwa na kitu gani kingine, maana lazima kuwe na jambo kubwa ,lililomsukuma kuingie humo ndani ya mto, huo mzigo ulikuwa na vitu gani ambazo vilimfanya huyo kijana ahatarishe maisha yake kiasi hicho, ikizingatia kuwa yeye ni jemedari wao, na walikuwepo majasiri wengine ambao wangeliweza kuifanay hiyo kazi, au alikuwa akitaka kumuokoa nani?’ akauliza yule mzee kwa mashaka.

‘Baada ya kupata hiyo taarifa hata mimi niliwaza sna hilo jambo, kuwa inawezeka, huenda alikuwa akitaka kumuokoa yule mwanamke aliyetakiwa kuuliwa kwasababu hakutakiwa hapa kwenye ardhi yetu, lakini sehemu hiyo ni mbali na kule alipotupwa huyo mwanamke, …au nikiwaza kuwa huenda alikuwa akitaka kuvuka kwa ujanja ili aje sehemu hiyo lakini akashindwa…kwa maana likuwa akikaidi amri ya wakuu’akasema huyo askari.

‘Kwahiyo huyo askari wao anasema alihakikisha akiliwa na hawo mamba,..mbona hiyo haiji akilini,?’ akauliza huyo mzee huku akitabasamu kwa dharau, na alisema hivyo akidhihaki kwani kwa imani yao watu wanaostahili kuwa ndani ya eneo takatifu hawawezi kuliwa na mamba, labda iwe kwa hukumu maalumu.

‘Wanasema alipiga mbizi , akijua kuwa kuna maji mengi, akazama moja kwa moja,hakuonekana akiibuka tena, …..kwani sehemu aliyoingia ilikuwa na matope, na wanahisi alipofika chini, alishindwa kutoka , tope litakuwa lilimzidi nguvu,….na wenzake walitafuta vifaaa vya kumuokoa, kwa kuingia na kamba, na wakajaribu kutafuta sehemu hiyo aliyoingilia, hawakuona kitu na wakati huo huo, mamba walishafika eneo hilo, hakuna angeliweza kufanya lolote…’akasema huyo aaskari.

‘Mamba hao hawakuonekana wakimla huyo kijana?’ akauliza mzee

‘Wanasema waliona mamba wakigombea kitu,….lakini hakuonekana moja kwa moja kuwa ni yeye, ila vipande vipande vya nguo yake vilionekana baadaye vikielea kwenye maji, na ndipo, wakawa na uhakika kuwa keshaliwa na mamba, na ikabidi watoe taarifa kwa wakuu wao…’akasema

‘Kama hiyo ni kweli, hilo ni jambo muhimu sana, na tutalitumia kuwaondoa hawa watu , na pia kama keshakufa, ina maana yule malikia anahitajika kuondolewa kwenye hiyo familia haraka, na anahitajika kuolewa na jemedari mwingine, ..’akasema kwa sauti na kwa kimoyomoyo akasema;

 `Na kijana wangu atakuwa na nafasi kubwa ya kumuoa,….malikia hastahili kuishi tena kwenye hiyo familia..labda asiwe huyo malikia tuliyebashiriwa.’akasema yule mzee, huku akiinuka  kwenye kiti chake na kuichukua fimbo yake, kuonyesha kuwa anataka kuondoka. Yule askari akawa anasubiri amri nyingine yoyote.

‘Ngoja nikawaone wenzangu, kwani hili ni jambo kubwa sana, lakini …..mbona sijasikia mlio wa msiba, sijasikia wapiga parapanda la msiba, hii  inaashiria kuwa bado kuna utata, hebu fuatilia kwa makini, nataka nipate taarifa zote toka ndani ya familia yao, ili tujue kuna nini kinachoendelea….’akasema huku akitembea kuelekea makao yao makuu. Na yule askari akaondoka, kutii hiyo amri.

Mzee alipofika alikutana na washauri wake na baadaye wakakubaliana kuitisha kikao cha dharura, na wazee mbali mbali walipofika, akaanza kuwaelezea nini kilichotokea;

‘Wazee wenzangu sijui kama mumeisikia hiyo taarifa kuwa kijana wa asimu wangu huenda kaliwa na  mamba…’akasema na wenzake wakashituka kwa taarifa hiyo, na wengi hawakukubaliana na hiyo taarifa, kwani kiimani zao, mtu analiwa na mamba kama ni mtu mbaya, au awe amehukumiwa. Wao wanaamini kuwa mamba hawo hawawezi kumla mtu ambaye anastahili kuwa miongoni mwa watu wa eneo takatifu.

‘Hii inaashiria kuwa huyo kijana hakustahili kuwa miongoni mwa watu wa sehemu yetu takatifu, toka lini mkasikia mtu wa nyumba hii takatifu akaliwa na mamba…hii nilishawaambia kuwa hawa watu hawastahili kuishi kwenye nyumba hii….wanatakiwa wafukuzwe haraka wasije wakatuletea mabalaa mengine…’akasema na wenzake wakawa wametulia.

‘Mimi bado sijamini …hiyo taarifa bado ina utata, kwani kama ingelikuwa ni kweli, tungesikia, hatujasikia baragumu la msiba, hatujaona wenzetu wakikutana kwa ishara ya msiba, na ikizingatiwa kuwa huyo jemedari, mbona vikosi havijawekwa kwenye tahadhari, msiba haufichiki, tumefanya upelelezi wa kutosha kuthibitisha hilo?’ akasema mmoja wa wazee.

‘Wewe unawajua hawa wenzetu, lengo lao ni kupoteza muda, ili wajipange vyema, hawawezi kuiweka hiyo taarifa hadharani mapema hivyo, lazima kwanza wawe wameshapanga mambo yao vyema, na huenda bado wanatapatapa kumtafuta, lakini mtu ukishaingie pale na kukutana na hawo mamba, unafikiri nini kitafuata. Mamba hana urafiki na binadamu, na ikizingatia kuwa kipindi hiki ni cha njaa sana kwa mamba. Na pia huenda wanajipanga, ili wamchague kijana mwingine kushika nafasi yake….’akasema huyo mzee.

‘Sasa tufanyeje, maana kama ni kweli tunatakiwa kujiandaa kwa hatua nyingine,….pia tujue kuwa malikia bado yupo kwenye miliki yao, kama tukio hilo limetokea, malikia anatakiwa atolewe na kuwa huru, kwa maamuzi mengine ambayo , yatatokana nay eye mwenyewe kumkubali mtu mwingine?’ Akauliza mzee mmoja.

‘Kwanza tunahitajika kuwa na ujumbe maalumu, ujumbe huo utakwenda kutoa rambi rambi, lakini tukiwa na lengo la kuchokonoa, ili hili swala lijulikana na kama walitaka kulificha wasipate nafasi hiyo tena. Tukifika tunafika kama watu walio na uhakika na taarifa hiyo, na kutoa rambi rambi zetu, na wito wa kumpata mrithi wa kijana wao, na hapo hapo tutahitaji huyo malikia atolewe kwenye hiyo familia haraka iwezekanavyo’akasema huyo mzee.

Baada ya mjadala huo ujumbe ukaundwa, ukiongozwa na mzee mwenyewe, na waliondoka hapo haraka kuelekea makao ya wahasimu wao, ili wakitoka hapo waelekee nyumbani kwa mzee hasimu wao, kumpa pole.

*******

Huku kwa mzee mwingine taarifa hizo zilikuwa zilikfanyiwa kazi, na moja ya makubaliano ni kuhakikisha kuwa taarifa hizo hazifiki kwa mahasimu wao. Kwahiyo mambo mengine yalikuwa yakiendelea kama kawaida, huku kikosi maalumu kikuwa kinafutailia ukweli wa jambo hilo.

‘Mimi nina uhakika kijana wetu bado yupo hai,ila kuna sehemu ka kwama. Najua vyema inavyokuwa pale hawo mamba wanapokula mtu, nimefuatilia kwa amkini, sikuona dalili yoyote’akasema mmoja wa wazee ambaye anaaminika sana, ni mtaalamu wa mamba na dawa za kutibiwa watu walijeruhiwa na mamba.

‘Kwa mtizamo wako, hata huyo mwanamke aliyetupwa siku ile, hakuwa ameliwa na hawo mamba?’ akaulizwa.

‘Ndilo jambo la kushangaza, maana hawo mamba wakila mtu , wanajulikana, na hali ya hapo mahali inakuwa na damu , kwa sababu mara nyingi wanakuwa wakigombea ile nyama yake….hakuna dalili kama hizo, hii ni kuashiria kuwa kijana anaweza kanasa mahali, au yupo mahali…’akasema huyo mzee.

Vijana alio kuwa nao kwa kazi maalumu tuliyowatuma, wamerudi, na wanasema mwenzao, jemedari wao, walimuona kabisa akizama,…hii inanipa amshaka kidogo,kwanini yeye aliamua kujitosa sehemu ambayo wengi tunaifahamu kuwa haifai kuingia…?’ akauliza mzee mmoja.

‘Ajali ikipangwa haina kinga,mimi naona  tufanye uchunguzi wa kina, …maana tunavyojua, wahasimuwetu wakipata hii taarifa, basi watakimbiliakuchukua hatua, na kama ujuavyo malikia, yupo mikononi mwetu, na ikitokea taarifa kama hii, anahitajika kuwa huru,….anatakiwa tumtoe, aiswe mikononi mwetu tena,…’akasema mmoja wa wazee wa sheria.

‘Lazima tuhakikishe taarifa hii haifiki kwao,na kama ikifika kwao tujue jinsi gani ya kujihami, ….tuhakikisha hakuna 
makundi,hakuna vikao, shughuli zote ziendelee kama kawaida…’akasema mzee mkuu wao, huku akiwa na huzuni moyoni.
Mzee huyo alipoletewa taarifa hiyo kwa mara ya kwanza , hakuamini, lakini siku zilivyozidi kwenda mbele, alihisi kuna jambo baya limetokea, na kama limetokea kweli, alishajua kuwa huenda mwisho wake wa kuishi kwenye sehemu takatifu umefika,lakini myoni alijipa moyo, akijua kuwa kijana wake ndiye stahili la eneo hilo, bila yeye sehemu hiyo itaendelea kuwa na uhasama.

‘Lazima lifanyike jambo…’akasema na akazamiria kusafiri hadi eneo lao walipotokea, ..mara nyingi huenda huko anapokwama,na kabla hajaondoka ikabidi aitishe hicho kikao kupata ushauri wa wenzake, na kikao kilipoisha, wakawa wanatwanyika, lakini kabla ahwajatawanyika waliona wajumbe wakiongozwa na mzee adui, wakija maeneo ya kwao.

‘Hawa wameshapata taarifa?’ mmoja wao akauliza na wazee wote wakaduwaa wakisubiri huo ujumbe umekuja na taarifa gani.

NB Haya hayo ni mambo ya wazee wetu, tunahitajika kuyakumbuka, huenda katika destruri na mila zao tunaweza kujifunza kitu.

WAZO LA LEO: Tuwaenzi wazee wetu, kwani bila wao, hali hii tuliyo nayo sasa isingelikuwepo , je kama nchi kuna utaratibu gani wa kuwaenzi kwa vitendo hawa wazee, …hasa katika kupatiwa huduma muhimu, za kiafya, makazi na haki zao. Ukiangalia maeneo mengi ya kijijini, wamebakia wazee, hawana mbele wala nyuma, hatuoni kuwa tunajilaani wenyewe? Tuwaenzini wazee wetu kwa vitendo,na sio kwa kauli za mdomoni tu.


Ni mimi: emu-three

No comments :