Kila ukipita kwenye barabara zetu kubwa utaona mabadiliko
makubwa, upo ujenzi unaendelea, na kwa kiasi kikubwa inaleta faraja, tukijua
kuwa huenda lile donda ndugu la foleni za barabarani zitapungua,ili kuleta
maendeleo, kwani miundo mbinu hasa ya barabara ni muhimu sana, katika maendeleo
ya nchi, na wananchi wake.Tunaipongeza serikali kwa hilo.
Lakini kwa mtizamo wa haraharaka, tunahisi kuwa huenda
tungeliangalia pia barabara hizi za mitaani, ambazo zinaweza kupunguza tatizo
hili la foleni za barabarani, kwa mfano kuna barabara za mitaani, za mkato,
zinaweza kufika sehemu nyingine bila kuzunguka hadi mjini, posta au Kariakoo,
kwa mfano kuwa barabara zinazotokea Gongolamboto hadi Mbagala, au Gongolamboto
hadi Ubungo, na nyinginezo, hizi zingeboreshwa, zingesaidia sana.
Tatizo kubwa, barabara kuu zote zilielekezwa mjini posta na
Kariakoo,kwasababu enzi hizo huko ndio kulikuwa mjini na huduma zote,za
kiserikali, masoko, bandari, nk, zilikuwa maeneo hayo, sasa mji umepanuka,
mjini ni kila mahali. Hatuhitajiki tena kuelekeza hizo barabara kwenda Posta ,
au Kariakoo tu, tunatakiwa kuzielekeza sehemu nyingine ambapo kuna huduma kama
hizo, au huduma hizo ziondolewe huko Posta na Kariakoo zipelekwe nje ya hapo.
Hakuna atakayepinga kuwa sehemu kubwa ya muda wetu
tunaipoteza kwenye foleni za barabarani, na baya zaidi hata ukiingia kwenye
maofisi yetu ya serikali utakutana na tatizo la foleni kama hizo, huenda
watendaji wapo mabarambarani wakiwa kwenye foleni, hata kuna mzungu mmoja akasema,
hii nchi kila kitu ni kusubiri, kila kitu ni kwa foleni, ikanikumbusha enzi ile
ya sukari, unga na hata sabuni ilikuwa kwa foleni!
Lakini kilichokuwa
kimesababisha hayo enzi hizo hakipo tena, kwanini bado tuna tatizo hilo.
Na katika hali halisi kunapokuwepo na kusubiri kwingi, mengi
yatatokea, kuna ambao watatafuta njia za mbadala, hata kama sio halali, ili
wawahi, ili wahudumiwe, ili wagonjwa wao wapate huduma, ili wawahi kwenye mambo
mengine, na utakuta wengi wao ni wale wenye uwezo wao. Wanyonge watabakia
kusubiri, wanazidi kuumia…..
Lakini yote haya yanabadilika kidogokidogo,kwasababu ya
ushindani wa biashara, kunapokuwepo na ushindani wa kibishara,lazima huduma, na
utendaji unabadilika, kila mmoja akitafuta njia bora zaidi, lakini kama ni mtu
mmoja, au kampuni moja, inayotoa huduma hiyo pekee, tusitegemee mabadiliko ya
harakaharaka.
Wakati hayo yakiendelea akatokea Mzee mmoja akaulizia wapi
anaweza kupata vitabu, na alipoulizwa vitabu gani na vya nani, akasema vitabu
vya shule, yeye alikuwa mwalimu wa siku nyingi, sasa kaombwa kujitolea
kufundisha huko kijijini kwao, lakini tatizo vitabu havipatikani tena na yeye angelipenda
vitabu vilichapishwa na Macmillan au Oxford, kwasababu wao ni wakongwe katika
kazi hii ya uchapishaji.
‘Makampuni haya nayafahamu toka enzi na enzi..’akasema.
‘Hayo makampuni nimesikia yamefungiwa?’ mmoja akasema.
‘Ohh, hapana,kwanini wanafanya hivyo, hawajui kuwa
wanadumaza soko la elimu, hawa watu walishaweza kufika hadi huko kijijini kwetu,
sehemu ambayo ni ngumu kufika,na waliweza hata kufikia shule za ndani ndani, na
kutoa huduma za vitabu, kama wamewafungia basi wanataka kuua elimu’akasema mzee
huyo kwa masikitiko.
`Ni kweli ni nani kwa wazee wetu asiyejua makapuni haya,
ubora wa vitabu vyao, na huduma zao katika elimu ya nchi hii. Makampuni haya
yalikuwa mchapishaji na msambazaji mkubwa wa vitabu, kila kona ya nchi,
kwasababu ya ushindani wao, walikuwa wakiboresha huduma zao siku hadi siku. Leo
tunasikia kuwa huenda yamefungiwa!’ akasema mama mmoja mzee.
‘Yanafungiwa kwa kosa gani?’ yule mzee akauliza.
Mjadala ulikuwa mrefu kila mtu akisema lake, na wengi
walikuwa hawana uhakika ni kwasababu gani yamefungiwa, lakini yule mzee
akasema;
‘Vyovyote iwavyo, hiyo ni sawa na ile kesi ya yule mwanamke
malaya aliyetakiwa kupigwa mawe, na wakaambiwa watu, aliye msafi ampige yule
mwanamke mawe, ….tatizo sio hayo makapuni ya uchapishaji, tatizo ni hawo
wanatoa hizo zabuni…’akasema huyo mzee.
‘Kwa vipi mzee?’ akaulizwa.
‘Kama wewe unahitaji huduma, ukafika, ukaambiwa njoo kesho,
na hizo njoo kesho zikawa nyingi, unafikiri ni nini kinachotakwia hapo?’
akauliza huyo mzee na watu wakacheka.
‘Tatizo la nchi yetu ni hii kusumba ya `kusubiri’, tatizo la
foleni, kila kitu kwa foleni, na haya yanafanywa kwa maana maalumu, wewe usiye
na haraka utasubiri, lakini muda ni mali, kuna yule ambaye ana haraka, akichelewa
ni ni hasara kwake, akichelewa mgonjwa wake atakuwa taabani, unafikiri atafanya
nini, na akifanya hivyo aliyesababisha hayo yote ni nani, na nawauliza kosa
hilo lilifanyika wapi?
Watu walisema kosa hilo halikufanyika hapa Tanzania…
‘Kama halikufanyika hapa kwanini tunayafungia haya makampuni, ambayo huenda yanaendeshwa kwa sasa na wazawa. Jamani mbona tunakimbilia kuangalia tatizo kwenye matawi,
wakati tatizo limeanzia kwenye mashina,hatutafika, tutaishia kuyaua hayo
makampuni ambayo yalikuwa yakisadia watoto wetu wapate vitabu kwa muda muafaka,
na kwa ubora, kwasababu hapo kinachoonekana ni kukimbilia maslahi binafsi.
‘Kwasababu najiuliza kwaninni hayo yaonekane sasa hivi,
sizani kuwa ni uboreshaji na uwajibikaji, nafikiri kuna jambo limetokea, kama
sikosei ni hiyo pesa ya rada’akasema huyo mzee.
Wote tukacheka.
`Msicheke jamani, …hili ni tatizo, kunapokuwepo na masilahi,
hata ndugu watauana, ..bila kujali udugu wao, bila kujali ni nani wataumia,
sisi mawazo na macho yetu yote yatakuwa kwenye hayo maslahi. Tukumbuke kuwa
kwenye taaluma hii ya vitabu, na elimu, kuna watungaji, kuna wafanyakazi na
familia zao, hawa hawaangaliwi kwa sasa, wanachoangalia watu hawo kwa sasa ni
kuhakikisha yule aliye mbele anaondoka ili mimi nishike nafasi yake.
`Huyu mtungaji wa vitabu ambaye alijitoa kwa hali na mali hadi akafanikisha kutoa kitabu, na
kitabu hicho kikapitishwa na hawo wanaoizinisha, na hata kutoa ithibati,
amefikiriwaje? Sisi tunachokimbilia ni kuyafungia haya makampuni, je gharama
za hawa watungaji, na muda wao, ni nani atawalipa? Kila siku tunalalamika kuwa hatuna
watungaji wa vitabu, je hatuoni kuwa huku ni kuwavunja nguvu hawa watungaji
wa vitabu hapa nchini,…
‘Tujiulize kosa limefanyika wapi na kwa nani, …na kwanini
tuangalie upande mmoja wa shilingi tu, kwani huyo mchapishaji wa vitabu asingelifikia
kufanya hilo kosa kama kusingelikuwa na huo mwanya uliosababisha hayo yote.
Sasa ni nani anakomolewa hapo…?’ akauliza huyo mzee.
‘Hapo, atakayeumia sana, ni watoto wetu, watakosa elimu bora
kwa wakati, watakosa vitabu, kwani vitabu vilivyokuwa vimechapishwa kwa ajili
yao vipo kwenye magodauni, vimelundikana kwenye hayo makampuni …sasa macho na
hamasa zetu zote ni kwenye hiyo pesa ya rada.
Kuna huyu mtungaji, alitarajia kupata chochote kutokana na
kipaji chake hicho, leo akifika kwenye hayo makampuni aliyoingia nayo mkataba,
anaonyweshwa maboksi yaliyojaa vitabu, anaambiwa kampuni imefungiwa, hatuwezi
kuuza tena hivyo vitabu…hawa wanaadhibiwa kwa kosa gani?
‘Kuna wafanyakazi, na familia zao, ambao wamekuwa wakifanya
kazi kwenye hayo makumpuni usiku na mchana, na wao wanafikishwa kubebeshwa huo
mzigo, huenda kazi hawana tena, na tujiulize na wao watakwenda wapi,na je
kwanini na wao wanaadhibiwa kwa kosa hilo, ambalo halikutendeka hapa nchini…hakuna
anayejali hilo, hamasa zetu zote ni kwenye hiyo pesa , pesa ya rada.
‘Kila mmoja anataka apate, mwenzake aondoke, yeye apate
zaidi, basi kama ni kwa ajili ya elimu ya watanzania, na maendeleo ya nchi, lililo
jema na hekima kwa maslahi ya taifa, ni kuzitoa hizo pesa kwa makapuni yetu yote
ili yaweze kufanya kazi, na baada ya hapo tunatoa `onyo kali’ kuwa kuanzia
sasa, hatutakuwa na msamaha kwa kampuni yoyote itakayotenda kosa, lakini kwanza
tuanzie na sisi wenyewe tunaotangaza hizo zabuni kuwa tutaboresha utaratibu
wetu, ili tusijenge mianya …
‘Mimi nawapongeza sana hawa waliojitahidi hadi kuweza kufikisha
vitabu kule kusipowezekana, makapuni haya makongwe, Macmillan na Oxford walifanya
kazi kubwa sana hapa nchini, basi tu,…mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’akasema
yule mzee kwa huzuni.
4 comments :
Kweli nchi hii ina mambo ukiona hivyo, mgawo haujafika kwa waheshimiwa
Umenena kweli mkuu, hoja hii itume bungeni
Wakati mwingine taasisi zetu zinatoa adhabu kwa kujipendekeza bila kujali utaifa wetu. Hapa watakaoumia ni watoto wetu
Kweli hii inahitajika ifike Dodoma kwa waheshimiwa
Post a Comment