Ilikuwa muda wa mchana wakili mwanadada akafika nyumbani kwa
wakili mkuu wa kitengo chao nyumbani kwa bosi wake, alikuwa na uhakika kuwa
bosi wake huyo hayupo nyumbani muda kama huo, akagonga mlango na kufungulia na
mfanyakazi wa nyumbani, na kwa vile walikuwa wakijuana baada ya kusalimiana
wakawa wanataniana.
‘Leo mimi ni mgeni wako, nataka unipigie ugali wa nguvu….siunajau
tena mimi ndio mume wako mtarajiwa….’akamwambia.
‘Ugali tu, …hapa umefika, nashangaa leo kuja hapa mchana
tena muda wa kazi, umekuja kunifumania nini…maana waume nasikia wanafanya
hivyo, ….eti mume mtarajiwa, ….’akasema huyo mfanyakazi huku akicheka.
‘Nani kakumabia hayo, ….umeshaanza kunikana, ….unajua lazima
nilinde mali yangu, wewe unafikiri huko nilikokutoa nilikutoa kwa mahari ndogo,
…mimi ni mumewako..’ Akawa anaigiza suti ya kiume na wote wawili wakawa
wanacheka huku wakitaniana, na hili lilimfanya huyo mfanyakazi wa nyumbani
amuzoee sana huyo dada wakili.
‘Sasa sikiliza mimi nimekuja hapa, nataka unisadie jambo
moja, lakini iwe siri yangu mimi na wewe, …ehe nimekumbuka, kwanza
hujanimalizia kile kisa ulichonisimulia,….siku ile hatukuweza kukimaliza,
kwanza naomba unisimulie kwa urefu ilivyokuwa halafu kama tutapata muda kuna
kitu nataka tukifanye, usijali mimi nipo kwa ajili yako,…’akasema mwanadada.
‘Mimii sipendi kuongea tena kuhusu maisha yangu, maana kila
nikiongea nazidi kujiongezea machungu, maana hata mama huyu mwenye nyumba, naona kafikia kuniona mimi
labda ndiye mbaya, anafikiri kuwa mimi ndiye nimefanya mume wake abadilike, na
juzi tu alikuwa akitaka kunifukuza nirudi kwetu kijijini, …..’akaanza kulia.
‘Sikiliza mpendwa, mimi nia na lengo langu ni kukusaidia
wewe, lakini sitaweza kuchukua hatua yoyote mpaka nijue kiini na ukweli ulivyo,
ujue yule ni bosi wangu kazini, na lolote nitakalofanya juu yake natakiwa niwe
na uhakika nalo, na ukizingatia kazi yangu ilivyo yeye anaweza akaweka
pingamizi ambalo litanifanya hata nisiweze kuanzisha ofisi yangu, kwahiyo
nahitajika kuwa muangalifu sana….’akasema wakili.
Kimiya kikatawala, na wakili akasema; Anzia pale huyu mama
alipokuja huko kijiji, akakuta ukiwa majalalani, ….’akasema huyo wakili na huyo
binti akaanza kuongea;
**********
‘Huyu mama wa hapa alinichukua kijijini,nikiwa mdogo,
sijavunja ungo, alinichukua kwasababu mama yangu alikuwa hana mbele wala nyuma,
ukumbuke kama nilivyokuambia awali kuwa mama yangu, alipata ujauzito,
akafukuzwa kwao na wazazi wake, ….na niliuambia kuwa ili aweze kuishi
alianzisha biashara ya pombe,….waanwake wengi kule kijijini wanafnya hiyo
biashara ya kuuza pombe,….
‘Huyu mama kukutana naye kwa mara ya kwanza, ni pale
alipopita akiwa na wenzake akaniona nikiwa majalalani,akanione huruma,
nilivyochafuka kuna baridi lakini nilikuw akifua wazi, na vinguo vilivyochakaa,kwa
muda huo, nilikuwa natafuta vyakula vilivyotupwa kwenye hiyo hoteli iliyopo
hapo karibu na hilo jalala, angalau siku hiyo ipite, akanionea huruma na
kuniuliza mama yangu yupo wapi…
‘Mama anaumwa, kashindwa kwenda kufanya biashara, hatujala
toka jana…’nikamwambia, huyo mama hakuniamini, akaniambai nimpeke huko nyumbani
akamuona mama yangu, nikamchukua hadi hapo tunapoishi, ni chumba kidogo tu cha
uani,akamkuta mama yupo hoi, anatapika na kuharisha. Kwasababu huyu mama ni
dakitari akamchuku hadi hospitali ya karibu ….’ Hapo akatulia ilionekana
alikuwa akimuwaza mama yake, na wakili akamwambia;.
‘Endela kuongea nataka kusikia kila kitu kutoka kwako, ili
nijue wapi pa kuanzia. Ikawaje?’ akauliza.
‘Basi mama akatibiwa kwa msaada wa huyu mama na kweli alipona
vizuri, baada ya siku tatu akarudi kwenye kazi yake ya kuuza pombe, na mimi nmara
nyingi huwa naachwa nyumbani, ….nilikuwa bado mdogo tu, wakati mwingina mama
anakuwa hana kitu, ananiacha bila hata kitu cha kula, naishia kwenda kuomba kwa
watu, au kuokota chakula majalalani,.
‘Huyu mama alipoondoka kumbe alishapanga kuja kunichukua,…lakini
kwa safari hiyo hakuja yeye, .siku hiyo alikuja mtu anaishi huko huko kijijini
, tunamfahamu, akanimbia kuwa yeye katumwa na huyo mama kuwa anichukue niende
nikaishii naye, lakini mama yangu kakataa. Mimi niliona kuwa hiyo ndiyo nafasi ya
kuondokana na dhiki tuliyokuwa nayo,, licha ya kuwa nilikuwa mdogo,lakini
nilishaona haya sio maisha ya kuishi. Nikamwambia huyo mtu nipo tayari
kutoroka.
‘Hapana nilivyoagizwa na huyo mama ni kuwa nikuchukue
mikononi mwa mama yako, siwezi kukutorosha wale watu wapo serikalini, hawawezi
kufanya jambo kama hilo, nandoka, kama huyo mama ana nia ya kweli atakuja yeye
mwenyewe. …maana mama yako mimi simuwezi…mwenyewe anauma, hawezi kukuhudumi
bado anakung’ang’ania,…eti mwanangi sitaki achukiliwe….’akasema yule mtu na
kuondoka.
‘Basi kweli siku hiyo ikashindikana, na baada ya mwezi hivi,
yule mama akaja kweli, na kukutana na mama yangu, alichofanya ni kumsaidia mama
pesa za msingi za biashara nyingine zaidi ya pombe, mama alipoona pesa,
akakubali na kesho yake nikaondoka na huyu mama kuja huku mjini.
Nilipofika huku mjini huyu mama alinifanya kama mtoto wake,
na akanifanyia taratibu zote za kusoma, na kuanza darasa la kwanza, nilisoma
nikiwa kwakke hadi darasa la saba,na muda owte huo akinilea kama mtoto wake.
‘Tatizo lilianza nilipofika darasa la saba,…mwili wangu
ulikuwa haraka, na kuonekana msicha mkubwa, kuliko umri wangu,… baba akaanza
kuniangalai kwa jicho la kuniogopesha,…’akasema na kutizama chini.
‘Jicho gani hilola kuogopesha…?’ akauliza wakili.
‘Jicho la …..yaani sijui nisemeje,…anakuwa mara kwa mara
anaiangalia hasa nikitembea au nikiwa nimekaa , naona kama ananichunguza
chunguza sana, na siku moja nikamwambia mama , mbona baba ananitizam hivyo,
akaniambia, niwe mwangalifu,..na kama nitafanya uchafu atanifukuzilia mbali.
‘Uchafu gani huo mama, mimi sina maana yoyote mbaya ni kwa
vile naona baba anavyonitizama sio kama ilivyokuwa zamani…anakuwa kama
ananichunguza mwili wangu kwa macho….’nikamwambia mama nikiwa sijui lolote,
akili yangu ilikuwa haina maana nyingine yoyote.
‘Nitalifuatilia hilo, ila jaribu kutokuwa karibu naye hasa
nikiwa sipo,..unanusikia,….’akanionya.
Dada wakili akauliza haraka kabla huyo binti hajaendelea,
‘Kwanza nikuulize baba na mama yako hapa wana maelewano
mazuri, nakumuka siku moja uliniambaii huwa wanapigana, bado mambo yao yapo
hivyo hivyo…?’ wakili akamuuliza huyo binti.
‘Kwaweli mara nyingi wanazozana, sijawahi kuwaona wakiwa na
furaha, naona kila mmoja ana lake, wanaweza hata kupigana kwa jambo dogo tu, na
huwa nikisia hivyo nakimbilia nje, sitaki hata kusikia wanavyozoazana, maana
mama mkali na baba mkali siuombe, wakianza kuzozana mmoja anaweza akaokota chochote
na kimpiga mwenzake…’akasema huyo binti.
‘Je hukuwahi kusikia maswal ya kufumaniana, yaani mama
kumsema baba au baba kumsema mama…kuhusu maswala hayo?’akauliza wakili.
‘Na mara nyingi ugomvi wao unahusu hayo maswala, nakumbuka
kuna siku mama alimwambia baba kuwa anaushahidi kuwa baba anatembea na
machangudoa, na atamkomesha, kwa tabia hiyo….’akasema huyo binti na hapo wakili
akatulai kuwaza, halafu akamwambia huyo binti aendelee kuongea.
‘Siku moja mama alisafiri kikazi, akabakia baba na mimi,
ujue mama huyu hana mtoto, sijui kwanini, na hil pia limekuwa ni tatizo lao,
maana wakija wanandugu hapa wanamsema sana baba kuwa eti kaoa mke tasa,wanamshauri
aoe mke wa pili au amuache huyo mke wake, kwasababu hana maana yoyote, lakini
baba hakubali,…nahis huenda baba ndiye mwenye matatizo lakini hataki kukubali
ukweli yeye anadai mama ndiye mwenye matatizo…’akasema huyo binti.
‘Kwanini unasema huenda baba ndiye mwenye mtatizo?’ akauliza
wakili.
‘Kwasababbu mara kwa mara mama amekuwa akimwambia baba
waende wakapime, ili wajue tatizo lipo wapi, lakini baba hakubali, na wakinza
kuongelea hayo baba anaondoka kwa hasira na kwenda zake, akirudi amelewa. Hapo
hakukaliki, maana ni fujo, nyimbo, kupigana, muda kama huo nijifungia chumbani
maana yanayofanyoka hapo hayafai, baba huwa anamshika mama kwa nguvu, hajali
hata kama nipo karibu…’akasema.
‘Anamshika kwa nguvu kwanini, yaani kutaka kupigana au
anamshika kwa vipi, hebu nifafanulie hapo….?’ Akauliza wakili.
‘Anamshika kwa mambo yao ya kindoa, yaani baba anakuwa kama
kachanganyikiwa vile, mama ana taabu kweli kweli, ila huyu mama ni mvumilivu
ajabu, anamvumilia sana mume wake,….pamoja na hayo, baba akizidiwa ulevi,
anamchukua anampeleka kumalza chumbani kwake…’akasema huyo binti.
‘Ehe endelea ikawaje?’ akasema wakili.
‘Basi huyu baba akarudi kazini jioni, akanikuta napika
chakula,…nilikuwa nimetoka bafuni,kuoga,na sikutarajia kuwa baba atarudi mapema
hivyo, kwahiyo sikujali, nilijau nipo peke yangu ndani,….baba alipofika
akaniangalia kama kawaida yake, akanitizama mwili mzima, huku nikiwa naogopa,
…. akaniambia nije anataka kuongea na mimi, nikaacha kupika na kumfuata huku
naogopa, nikijua nimefnya kosa nisilolijua ….’akasema.
‘Kakuita umfuate wapi, yaani chumbani kwake au barazani au
wapi?’ akauliza.
‘Aliniitia akawa aoanongza chumbani kwangu, na nikajua kuna
kitu hakikuwa sahihi huko ndani, na kwa vile najua huwa anakagua kila mahali
kuwa kila kitu kipo sawa, nikajua labda
kuna kitu nimeweka vibaya,…’akasema
‘Je ina maana huwa mara kwa
mara anaingia chumbani kwako kukagua?’ akauliza wakili.
‘Ndio, huwa anasema anakagua usafi,…huyo baba mkoloni kweli,
akiona vitu vimekaa vibaya hakukaliki, anakagua kuhakiksha kila kitu kipo safi
na kimepangwa vizuri…hata mama haoni ndani kwa usafi wa huyo mzee….’akasema.
‘Ehee, ikawaje?’akassemawakili.
‘Yeye alitangulia chumbani kwangu, huku nyuma nawaza sijui
kupoje,maana sikuwa nimejua kuwa atarudi mapema,huwa muda wa kurudi nahakikisha
kila kitu kipo sahihi,…., nilipofika nikamkuta kakaa kwenyekitanda, nikashangaa
sio kawaida yake, kukalia kitanda change, akaniambia nije nikae naye karibu
nikaogopa, nikakumbuka alivyoniambia mama, nikakataa katakata, akasimama kwa
hasira. Na kusema;
‘Ina maana siku hizi umekuwa na kiburi, mimi nakuita hapa
hutaki, ngoja leo nitakiondoa hicho kiburi chako, akanivamia na kunishika kwa
nguvu….’akasema huyo binti.
‘Alikushikaje kwa nguvu, kwa vipi, hebu elezea hapo vizuri….?’akaulza
wakili.
‘Mimi kwa muda huo kama nilivyokuelezea, nilikuwa nimevaa
khangatu, kwasababu nilikuwa nimetoka kuoga, na nilipitia jikono kuangalia kuwa
vyakula haviungulii, na nikitoka hapo niende chumbani kwangu kuvaa , sikujua
kabisa kuwa huyo baba atarudi muda kama huo, kwahiyo aliposimama pale aliishika
ile khanga niliyovaa na kuivuta kwa nguvu, nikabakia uchi, akanivamia na
kilichofuata hapo siwezi hata kuelezea….’akaanza kulia.
Yule wakili mwanadada alimpa nafasi huyo binti alie,
hakutaka kumsemesha kwa muda, na alipoona katulia
akamuuliza swali jingine;
‘Mama alikaa huko alipokwenda kwa muda gani….?’akauliza
wakili.
‘Mama alirudi kesho yake, na nilijaribu kumkwepa ili asijue
ukweli,sikutka kumwambia, ingawaje alihis mabadiliko, maana huyo baba
aliniumiza kweli siku ile, hata kutembea ilikuwa natembea kwa shida. Lakini mama akanigundua na kuniuliza,;
‘Wewe una matatizo gani,ndio kutembea gani huko….?’
Akaniuliza na mimi nikasema ni miguu nilidondoka unaniuma, niliogopa mama
akijua atanifukuza na baba alishaniambia kuwa kama nitamwambia mama atahakikisha
kuwa naondoka hapo nyumbani….’akasema huyo binti.
‘Je mambo kama hayo yaliwahi kutokea teana, na kamailitokea
ilikuwaje..?’akauliza wakili.
‘Ilitokea tena....siku hiyo mama alikuwa kasafiri na siku hiyo nilipiga
makelele mpaka majirani wakaja, na hata walipofika huko nje, huyo baba
hakufungua mlango mpaka alipomaliza shida yake …yaani ungemuona siku hiyo,huwezi
kuamini kuwa ni mtu na heshima zake, alikuwa kama kichaa, …nilipigana lakini
yeye ana minguvu
akanishinda,…yaani siku hiyo nililia sana,…unajua hakujali
kuwa watu wapo nje, kwani alipotoka nje
kuonana na hawo majirani aliwadanganya kuwa, eti alikuwa akiniadhibu kwasababu
nimeharibu vitu, na kweli hawo majirani walimuamini, ....’akasema.
‘Mama alivyokuja hukumwambia , uliendelea kukaa
kimiya?’akauliza wakili.
‘Mama alikuja kupata taarifa toka kwa majirani, na hapo
akanijia juu na kuniambia kuwa nisiposema ukwelii ataniridisha kwetu, ikabidi
nimwambie ukweli...’akasema na kutulia.
‘Huyo mama alisemaje,….?’ Akauliza wakili.
‘Alichanganyikiwa, alisikia hayo aliinuka akachukua gilasi
ya maji aliyokuwa kashika na kutupa ukutani, nafikiri kama baba angekuwepo hapo
angempiga nayo,…na baba aliporudi nilijua leo kuna mambo, huenda ikawa siku
yangu ya mwishoo kuishi hapo.
Siku hiyo hakukalika, mama na baba walipigana vyombo
vikavunjika, vitu vikadondoshwa huku na
kule, hakuna jirani aliyejali, kwani walishawazoea, wakaumizana kweli damu
zinawatok, hawajli,…., baba akavimba jicho hakuweza kwenda kazini kesho yake,,…hata
mama hakwenda kzini siku hiyo, na baba alipopata mwanya akasema atahakikisha
ananifukuza hapo nyumbani…., na kumbe mama alisikia akaja na kusema haondoki mtuu
hapo nyumbani na atahakikisha kuwa huyo baba hanifanyo lolote tena.
‘Hawa watu wanatoka wapi,….mkoa gani…?’ akauliza wakili na
kabla huyo binti hajajibu akamuuliza swali
jingine kkwa haraka;
‘Ina maana baada ya yote hayo huyo mama hakuchukua hatua
yoyote?’ akauliza wakili.
‘Nakuambia huyo mama ni mvumilivu sana, alimsamehe mume
wake, lakin kwa masharti kuw akirudia tena
analipeleka hilo swala kazini kwa
baba, na unajua likifikishwa huko kazini kwa baba itakuwa vibaya…baba akaomba
msamaha ’akasema huyo binti.
‘Huo msamaha ulifanywaje, mlikaa kikao, au waliongea wenyewe
ukasikia…?’ akauliza wakili.
‘Tulikaa kikao, baba aliniita mimi na akamuita mkewe,
akaanza kuongea, kuwa anajua yeye ndiye mkosaji, na ibilisii alimpitia kwasabbu
ya pombe,….huwa anapenda kujitetea kwa njia hiyo kwa kusingizia kuwa anafanya yote hayo kwasababu ya pombe, na mama anamwambia kama ni pombe achane nayo, lakini baba anasema yeye hawezi kuacha pombe…kwasababu anakunywa kumuondolea mawazo....’akatulia
kuongea huyo binti.
'Mawazo gani hayo, ya kuja kuharibu .....'akasema mama kwa ahsira.
'Wewe mwanamke, huwezi kujua mawazo aliyo nayo mwanaume, tuna mambo mengi ya kufikiri....pombe ndiyo inasaidia kunituliza akili, kunipa maarifa, ....hujui wewe....'binti akawa akawa anaongea kuigiza sauti ya kilevi ya baba yake, na wakili atakatabasamu na kusema;
‘Nikuulize swali moja, unijibu kwa moyo wako ukiwa huru hebu
niambie ukweli, je hayo aliyokufanyia huyo baba uliyachukuliaje?’ akauliza.
‘Kiukweli huyo baba namuona kama baba yangu mzazi ingawaje
simjui baba yangu yupoje, yeye nilimuona
ndiye baba yangu….kwamba nieyachukuliaje,…sijui niseme nini…’akatulia kwa muda
halafu akasema;
‘Mimi,nimeyachukulia kuwa kanifanyia hivyo kwasababu
hanijali ananiona kama mtumwa fulani, au changudoa tu, mtu nisiye na thamani
kwake, kuwa anaweza kunifanya atakavyo kwasababu nakula kwake, ananilisha yeye,
nasema hivyo kwasababu, siku hiyo aliponibaka kwa mara ya kwanza aliniambia ni nini
atapata kutoka kwangu baada ya fadhila zote alizonifanyia mimi, akaniambia kuwa
mimi ni damu ya Malaya muuza pombe, changudoa….alitamka hilo akimaanisha kuwa
mama yangu ni Malaya, muuza pombe na anajiuza…kwahiyo hata mimi nipo kama yeye,…iliniuma
sana….’akasema na kuanza kulia.
‘Kwahiyo hujafurahia hilo tendo,…nina maana kuwa, kuna
baadhi ya wasichana niliowahoji, baada ya kufanyiwa hivyo, walisema kuwa
wanatamani wawe wake wa hawo wanume waliowafanyia hivyo na wengine kudiriki
kuzivunja ndoa za hawo wenye nyumba, kwa kudai kuwa kama baba mwenye nyumba
kampenda, kwanini ajivunge,…’wakili mwanadada akautulia na kumwangalii huyo
binti na alipoona yupo kimiya akasema.
‘Unajua kwanini nakuuliza hivyo, au hujanielewa,…..kwasababu
gani nasema hivyo, kwanini hukutafuta mpango wa kuondoka hapa, maana naona
hakuna amani…au ungelichukua hatua nyingine za juu, hata kuwaambia majirani
wakusaidie, lakini wewe ulikaa kimiya, je una hisia zozote na huyo mzee?’akasema
wakili.
‘Nitaenda wapi mimi,…. mama yangu huko kijijini anaumwa
sana, anahitaji pesa, na mimi lengo langu nikukusanya pesa nikamtibie,….ingawaje
huyo mama anajitahidi,alijaribu kumtibia lakini naye ana majukumu yake huko
kwao, anasomesha wadogo zake, na pesa hazimtoshi na mume wake, tangu
walipogombana kuhusu mimi, alisema yeye hatatoa pesa yoyote kunisaidia mimi
tena….’akasema huyo binti huku akilia.
‘Kwahiyo ina maana hata akiamua kukufanyia hivyo na
kukuahidi pesa utavumilia tu, ili upate pesa za kumsaidia mama yako?’ akauliza
wakili.
‘Baada ya kile kikao,mimi nilimuamini kuwa hataweza
kunifanyia hivyo tena ndio maana nikawa na amani, ili nilijiahidi kumkwepa ,
sikuwa karibu naye tena…’akasema huyo binti.
‘Hakuwahi kukufanyia hivyo tena…?’akauliza wakili.
‘Mama alijitahidi kuhakikisha kuwa mume wake akiwa nyumbani
na yeye yupo, ana watu wake kawaweka majirani, wakisikia baba kaja nyumbanai na
yeye huja haraka, kwahiyo baba amekuwa hapati mwanya huo tena, ila namuona kila
mara anatafuta mbinu nyingine …naskia mama akisema huyo baba kaamua kutembea na
machangudoa ili kumzalilishiai yeye , eti hamtoshelezi…’akasema huyo binti kwa
aibu.
Yule wakili alitaka kumuuliza swali jingine lakini akasita,
na kuangalia saa yake. Halafu akasema huku akiinuka kwenye kiti na
kujinyosha,ilikuuwa kama vile anataka kuondoka, akasema;
‘Nina mengi ya kuongea na wewe, …lakini nikuulize tena, haijawahi
kutokea tena kukufanyia hivyo, nauliza hilo swali mara nyingine nikiwa na maana
yangu, niambie kiukweli….?’ Akauliza huyo wakili alipoona kuwa huyo binti
anaficha baadhi yaukweli.
‘Kuna mara nyingi anakuja usiku chumbani kwangu, lakini mama
anamuwahi kabla hajafanya lolote…na hajaweza kufanikiwa kwa hilo….nashukuru kwa
hilo….’akasema huku akiwa na wasiwasi.
‘Kwa mfano, nikuulize swali kwa namna nyingine, kama huyo
baba akisema anataka akuoe wewe,…upo tayari?’akajikuta akimuuliza hilo swali
kimtego, lakini baada ya kufikiri sana, huku
akimwangalia machoni huyo binti, yule binti aligeuka pembeni akawa hamuangalii
moja kwa moja huyo wakili , kwanza alitulia na baadaye machozi yakaanza kumtoka
na kusema;.
‘Huyu baba kwangu namuona kama baba yangu, ….siwezi kabisa
kuolewa na yeye , nitakaaje naye, hata kufikiria hivyo sifikirii, kitendo
alichonifanyia sitaweza kukisahau maishani kwangu….naona kama ni hivyo ,kama
ndivyo mateso yalivyo ….machungu niliyoyapata, naona ni heri nsiolewe, sitaweza
kuvumilia tena …..’akatulia huku akiangalia chini.
‘Una maana gani kusema hivyo…?’ akauliza wakili.
‘Natumai hapo umenielewa dada, ni maumivu unayoyapata, sijui
nikuambieje, ….kama kuna watu wanasema hivyoo kuwa wanatamani kuolewa na baba
zao, sio mimi…sitaki hata huko kuolewa kwenyewe, kuna raha gani kama ni hayao
mateso….’akasema na na wakili akamuelewa na kutabasamu.
‘Siku itafika utaolewa na mume anayekupenda utayasahau hayo
yote….’akasema wakili mwanadada na yule binti akasema kwa uchungu.
‘Mimi hapa nipo kwa vile sina pa kwenda,sina kazi sina mbele
walal nyuma,…nitafanyaje mimi,mimi mtoto wa masikini, mimi naitwa mtoto wa
Malaya muuza pombe,…matatizo ya mama, na mimi nabebeshwa huo mzigo, labda kama
wanavyosema mtoto wa nyoka ni nyoka, lakini mimi sifikirii kuwa kama mama, na
mama alifanya hivyo ili kujisaidia katika maisha, sizani kama alipenda hayo
maisha,….mmh, mimi sijui la kufanya kama huyo baba ataendelea kunifanyia tena
tendo kama hilo, naona kama nikunizalilisha tu…’akawa analia.
‘Nimekuuliza hivi kama atasema anakupenda wewe, uwe mke
wake, …nijibu tu unavyofikiria moyoni, ungalimjibu vipi kama kakujia na hoja
kama hiyo, na mke wake akakubali, kwasababu labda ya kutaka kupata watoto au tu
huyo baa kakupenda, natoa kama mfano,?’ akauliza huyo wakili.
‘Nikuambie ukweli dada, mimi hapa natamani dunia ipasuke
nizame, na kila nikimuona huyo baba, natamani sijui nifanye nini, simpendi
kabisa, lakini, mimi kama nani,… maana imefikia mahali sioni raha ya kuishi
hapa duniani, siku moja nilishaamua kunywa sumu, ….lakini bahati huyu mama
akanifuma, na aligombeza sana akajaribu kunipa ushaurii nasaha, nikamuelewa,….
ndio maama bado nipo tu, lakini kama huyo baba ataendelea tena kunifanyia hivyo,
kwakweli, sijui nitachukua hatua gani….’akasema huku akionyesha chuki ya wazi
usoni.
‘Sikiliza katu usije ukafanya ujinga huo,…nina maana ujinga
wa kutaka kujiua, ili iweje,…. maana wewe utajiumiza mara mbili,….umezalilishwa
wewe na bado ukimbilie kujiua, umemkomoa nani kama sio kujikomoa mwenyewe, huko ni sawa na kujiumiza mara mbili, na je
ukijiua huko kwa mungu utasemaje,….!’akasema na kumwangalia machoni.
‘Lakini mungu anaona nini ninachofanyiwa, ….hebu jiweke katika
nafasi yangu, uone, machungu yake, mtu anakubaka, tena sawa na baba
yangu,….hajali , anakubaka huku anakusimanga, kuwa wewe ni Malaya tu kama mama
yako kama nini sijui….mimi nimeujuaje huo umalaya, wakati yeye ndiye mtu wa kwanza
kuniharibu, kunifanyia huo uchafu….hebu niambie dada yangu….mungu anayaona yote
haya, sio kwamba nimepnda, anaiona nafsi yangu,….’, akasema huku akiwa analia
kwa uchungu.
‘Sikiliza ushauri wangu ni hivi,mababa kama hawa wanatakiwa
kuchukuliwa hatua za kisheria, ili iwe ni fundisho,…ndio maana mimi nataka
tushirikiane na wewe kwa hilo,…sasa leo nataka tuanze kwa kufanya jambo moja
muhimu, naona muda umekwenda …’akatulia huku akiangalia saa yake, halafu
akasema;
‘Najua leo mama harudi mapema na mzee mwenyewe nimemuacha
kwenye kesi, kwahiyo tuna muda kidogo umebakia naweza kufanya jambo ambalo
litatusaidia, ili tuweze kukusanya ushahidi….nitapambana na huyo baba….na
utakuwa huru, …lakini sitaweza kufanikiwa hili kama utakuwa unanificha jambo….’akasema
na kumwangali yule binti.
‘Unataka tufanye nini maana ninavyomuogopa yule mzee, sijui
kwanini….sikujakuficha kitu, ndivyo ilivyokuwa hivyo….’akasema.
‘Kuanzia sasa usimuogope, wewe mpe heshima yake tu kama baba
yako, na kama atataka kukufanyia hivyo hakikisha unapigana naye, piga ukulele,
nitakupa simu uifiche kabisa, akitokea kukufanyia
hivyo, nipigie haraka, hata hivyo kuna
kitu nataka nikifanye humu ndani ingawaje ni hatari kidogo…..lakini sina
jinsi,…’akasema huku akiwa kashikilia kitufe kidogo mkononi.
‘Ni nini hiyo….?’ Akauliza huyo binti.
‘Wewe usitake kujue mengi, yatakutia wasiwasi bure, hayo
niachie mimi, wewe nifungulie huo mlango wa chumba cha makitaba cha mzee, najua
bado una ufunguo wake,au sio….?’ Akauliza.
‘Ndio upo kule juu ya kabati, huwa nautumia tu anapokuwepo,
ngoja nikauangalie….’akasema na kuingia ndani kwenye chumba kikubwa cha weney
nyumba. Baadaye akaja na kusema tayari.
‘Sasa wewe kakae nje mlangoni, hakikisha kuwa ukiona dalili yam zee au mama kuja nipe
ishara….’akasema.
‘Lakini mimi naogopa dada…’akaanza kulalamika
‘Ukiwa na mimi usiogope, wewe fanya nilivyokuambia sawa…hili
nalifanya kwa jaili yako, ….mengine tutajua mbele kwa mbele, sasa hivi nabeba dhamana
hiyo usijali….’akasema wakili mwanadada, na kuingia huko ndani.
*******
Sehemu inayofuata itakuwa hivi.....
Huko kwenye mahakama alipo wakili mkuu wa kitengo cha sheria kesi aliyokuwa akiisimamia ikaahirishwa, na wakili mkuu wa kitengo cha
sheria, akakumbuka kitu, alikumbuka kuwa alipoondoka nyumbani hakufunga kabati
lake ambapo huweka vitu vyake vya siri, na anavyojua yule binti wao wa kazi anaweza akingia kufanya usafi, licha ya kuwa
alishamwambia kuwa awe anaingia humo akiwepo tu, lakini moyo ulikuwa ukishauri arudi nyumbani akalifunge hilo kabati kwanza....
‘Kwanza najua mke wango hayupo ana semina mapaka usiku, ngoja nifike nyumbani,kabla sijafika huko nipate chupa moja tu ya kunichangamsha,..’akasema na kupitia sehemu akapata chupa moja, na ikawa sio moja tena, mbili, tatu, na baadaye akajiona yupo tayarai kuondoka.
'Sasa nipo tayari, ...nikifika nyumbani nitajua nini cha kufanya,....aah, mimi mwanaume bwana,naogopa nini,eti, atanishitaki kazini,.....na ashitaki.nikifukuzwa kazii na yeye atapata nini....tutaona huko mbele kwambele...…na kabla wazo hilo halijajiweka sawa kichwani;
mara simu yake ikaita.
Aliipokea ile simu huku akikunja uso alipoona ni moja ya watu wake waliopo huko hospitalini, na aliyempigia ni nesi
rafiki yake, akasikiliza kwa makini na kumwambia;
‘Kwahiyo keshazindukana,..na anaweza kuongea?’ akauliza na
alipojibiwa akaongeza gari mwendo na kumwambia huyo nesi
‘Hakikisha haongee na mtu yoyote kabla yangu…nafika nyumbani
mara moja, nitakuja huko..’akasema kwa hasira.
NB: Mambo yanaanza kujikoroga, hapa hata mimi nachanganyikiwa
nilimuangalia huyu msimuliaji na kutaka kumuuliza mbona hicho ni kisa kingine
kipya,…na yeye akahisi hivyo nakusema, ‘
‘Hicho sio kisa kingine ila ni mnyumbulIko ambao utakuja kufichua
siri kubwa katika mfululizo wa matatizo yaliyomkuta’
Haya ….tuzidi kuwepo, kama mumechoka semeni, tuanze kisa
kingine kipya, au mambo mengine …
WAZO LA LEO: Ukiwa na uwezo hebu jaribu kuwakumbuka hawa
watoto wanaoitwa watoto wa mitaani, najiuliza, hivi kweli hakuna matajiri wenye uwezo
wa kuwasaidia hawa watoto, …najua wapo lakini hatujali hilo, kinachonishangaza ni kuwa wapo hawo matajiri wanafika hata kwenye yumba za ibada na kusikia wakiambiwa wawasaidie mayatima, masikini…lakini akitoka hapo keshasahau.
Jamani kusaidia mayatima, au msikini, au wale wasiojiweza ni amri ya mungu, kwasababu wao hawakupenda iwe hivyo.....tukumbuke kuwa ... HUJAFA
HUJAUMBIKA.
Ni mimi:
emu-three
4 comments :
Tuchoke? Yaani mahali anbapo panakolea utamu wewe unasema tumechoka au hutupendi siku hizi?
Natamani hata jumamosi na jumapili uendelee kuandika.
Jamani haya mambo kweli yapo, usifikiri huyo mtoto kafanyiwa kwa sababu mama yake ni hohehahe muuza pombe malaya; yaani wanaume wanawafanyia watoto wa ndugu na jamaa zao wanaowalea majumbani mwao. Kisa tu wao wana uwezo na wana pesa. Mimi mwenyewe nimenusurika kwenye mdomo wa mamba, yaani hata huwezi kuamini nikianza kusimulia hapa utatunga kitabu kingine. Ila uzuri huyo mlezi wangu yeye alikuwa harape wala halazimishi anatumia ushawishi wa pesa, yaani anamwambia mtoto nitakufungulia account, nitakununulia hiki nitakupa kile. Wapo waliokubali na wakawa na kiburi cha ajabu, kina sie ndio tukaishia kula mihogo mikavu na maji au chakula cha shule. Wakati mwingine anakunyima mpaka nauli ya shule yaani maisha ya ajabu kabisa. Mara nyingi huwa najiuliza hivi watanzania huwa wanaabudu nini? Wanaabudu Mungu kweli au kuna vitu vingine wanaabudu? Maana haingii akilini mtu anayejua uwepo wa Mungu na uwepo wa siku ya hukumu anafanya madudu ambayo huamini mwanadamu anaweza kuyafanya.
Usikatize hiki kisa malizia mpaka mwisho na hata ukiandika kitabu pia bado kisa kitakuwa hakijaisha utamu.
Subira uliadimika kidogo nashukuru umebeki, ulisafiri nini?
Nashukuru kwa kisa chako,ukipata nafasi niandikie ilivyokua ili tukinyumbulise na kuwa kisa.
Sijaadimika humu huwa sikosi kuingia kama sala, yaani kama hivi leo nishasoma hiki kisa tayari lakini nimeshaingia 3 times kabla hujapost.
Nashukuru sana Subira, maana ni kama majirani, akiwa kazoea akipita kwako ni lazima akusalimie,siku akipita kimiya kimiya na hukumuona,utajiuliza vipi leo jirani yangu yupo wapi.
Mungu akuzidishie kila lakheri
Post a Comment