Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, April 30, 2012

Hujafa hujaumbika-29



Nikiwa chumba cha wageni kwenye gereza la wanawake, niliangaza huku na kule, nikikumbuka kuwa na mimi niliwahi kufungwa kwenye geerza kama hili inakaribia mwaka mmoja sasa, na nilikuwa nimeapa kuwa sitafika tena hapo, lakini huwezi amini kuwa leo nipo hapa, lakini safari hii kama mgeni wa mfungwa, …mfungwa ambaye sijamjua ni nani,na ilikuwa kazi kweli kukubali kufika hapa, kwani  wito haukataliwi, ….

‘Leo nimekuja kukuchukua,tunakwenda gerezani,…..’akasema yule wakili mwanadada. Nikashituka na kumwangalia kwa mashaka.

‘Gerezani,una maana huko wanakufungwa watu, au maeneo ya gerezani….?’ Nikauliza
‘Gerezani, kweney gereza la wanawake….’akasema huku akiniangalia kwa uso wenye tabasamu, …sioule uso wa kwenye ulingo wa mahakamani.

‘Hapana,mimi nilishaapa kuwa huko sitafika tena,…hapana, nakuomba tafadhali…..huko siendi labda nije nikamatwe na polis kwa kosa,lakini sio kwa utashi wangu….’nikasemanikigeuka pembeni, sikutaka kumwangalia huyu dada machoni.

‘Huendi huko kwa nia mbaya na sio nakupeleka tu ….kwa kujifurahisha, ujue mimi ni wakili, na nafanya hili sio kama wakili wa mtu, bali naitikia wito, na nafanya hili kwa kujitolea kuwasaidia, wewe nap engine na huyo aliyekuhitaji uende ukaonenane naye..... ,kuna mtu mmoja kakamatwa huko, anahitaji muonane na yeye, …..’akasema huyo mwanadada.

‘Mtu gani huyo….mimi sina…..hapana huko siendi, naogopa isije ikatokea la kutokea nikafungwa huko huko tena…..yaani kunipeleka huko, labda iwe kwa kushikwa tena na kosa…na nimeapa kuwa nitajitahidi niwezavyo, nisifike huko tena……’nikasema.

‘Utaenda tu, maana huyo anayekuita inawezekana kuwa ni mtu muhimu sana kwako….na ni bora kuitikia wito….’akasema huyo mwanadada.

‘Ni nani huyo,mbona huniambii kuwa ni nani….lakini hata hivyo ,siendi kabisa…hata akiwa nani…?.’nikasema huku nikiangalia pembeni.

Yule mwanadada alitulia akiniangalia na mimi nilipona kuna kimiya, nikageza shingo, nikamuangalia machoni, na yeye alikuwa bado kanikazia macho yale ya kimahakamani, na polepole, akayalegeza na lile tabasamu lake la akiba likatanda usoni, akaangalia chini kama vile wanawake wanavyofanya wanapokutanisha macho yao na wanaume, ……akasema, huku akiwa kaangalia chini.

‘Kabla sijakuambi lolote, hebu kwanza nikuulize kuhusu historia yako ya ndoa,….nina mengi nataka kujua kutoka kwako,licha ya kuwa mimi ni wakili mwanamama, lakini pia nimekuwa nikifanya utafiti juu ya hali halisi ya maisha ya wanandoa……kwasababu imegundua kuwa chanzo kingine kikubwa cha matatizo ya akina mama kinatokana na matatizo ndani ya ndoa…..’akasema na kuinua kichwa kuniangalia, alinitizama kwa amkini
.
‘Kabla sijakujibu hilo swali naomba nikuulize kitu….maana tangu siku iletulipooachana nimekuwa nijiuliza…kichwani, na leo tena umazidi kunichanganya…..’nikasema huku nikimwangalia mkononi.

‘Mhhh…..’akahema halafu akasema; `Sasa tutakuwa tunacheza,na muda unakwenda, sawa utaniuliza hilo swali lako, au maswali yako…kwanza tumalizane na mimi unaonaje, ili tusipoteze wakati,najua una mengi ya kuniuliza, na sio wewe peke yako tu, lakini wanaume wengi wamekuwa na tafsiri au muwasho au tuseme dukuduku la kutaka kunjiua ,sasa sijui ndivyona wewe unavyowaza,lakini hata hivyo,muda utafika dukuduku lako litaisha….’akasema,

‘Hivi wewe umeolewa…..?’ nikamuuliza,licha ya kuwa hakutaka nimuulize swali kwa muda huo, akaniangalia akionyesha kama kukereka,lakini akaondoa hiyo hali haraka usoni mwake na kunikazia macho.

‘Kwanini unanuliza hilo swali….’akainua mkono wake ambao mara nyingi ulikuwa na pete,kidoleni  kushiria kuwa yeye ni mke wamtu,kwa sasa haukuwa na pete, lakini nakumbuka nikiwa na uhakika kuwa siku za nyuma nimeshawahi kumuona akiwa na pete kidoleni. Akatabasamu, na hakusema kitu, akaniangalia ,halafu akasema;

‘Najua unaniuliza hilo swala maana kipindi cha nyuma uliniona nikiwa nimevaa pete, …huwa mara zote ninaivaa, leo tu nimeisahau, maana nilikurupuka kuja kwako baada ya kupkea huo ujumbe kwenye simu,nilipokea simu ya haraka …..’akasema na kabla hajamaliza nikamdaika kwa swali.

‘Simu gani hiyo….?’ Nikauliza swali haraka.

‘Unajua wewe una pupa,kabla sijakujibu swali uliloniuliza mwanzoni, umeshakimbilia swali jingine, na kwa mtindo huo hatutafika mahali,na mimi kama wakili nimezoea kuuliza maswali, sio kuulizwa maswali, na hata kama ni kuulizwa mswali, naulizwa kwa mpangilio….’akasema na kuangalia saa yake.

‘Kwahiyo tuanzie wapi….?’nikasema na safari hiii nikamuangalia usoni, na yeye akaniangalia, halafu kwa mara ya kwanza nikamuona akinionea aibu na kuangalia pembeni…

‘Unajua ….tangu nikufahamu, sijawahi kukuona ukiwa na aibu, huwa ukimwangalia mtu machoni hupepesi macho…ilifikia mahali nikawa nakuogopa, maana ukimwangalia mtu unakuwa kama vile unamsoma ndani ya moyo wake…’nikasema huku nikitabasamu, nay eye akatabasamu na kuniangalia kwa uso ule ule wa aibu aibu…

‘Mimi kama mwanamke,siwezi kuikana hulka yetu, hata hivyo huo ni wasiwasi wako kwa vile tumekutana ndani ya ulingo wa kisheria, na unapokuwa ndani ya mahakama, huwa unachoona mbele yako ni mistari ya sheria…huwa mimi simuoni mtu, nakuwa kama nasoma sheria huku nikikusoma wewe uliye mbele yangu,….ni sitaweza kufanya hilo bila ya kukuangalia kwa makini…’akasema.

‘Sasa katika hali ya kawaida ya maisha yako upo hivyo hivyo….?’ Nikamuuliza,alibetua mdomo akaniangalia usoni,na hapo kukawa namchanganyiko ,unashindwa kuelezea kuwa ni ule uso wa mahakama au ni uso ule wahali ya kawaida.

‘Nashukuru mungu kuwa najaribu sana kujiweka mizania,yaani nikiwa kazini ni tofauti na nikiwa uraiani, vinginevyo nitakuwa nakosana na watu, maana unaweza ukaongea,ukajikuta unauliza kimahakama, au ukauliza kitu mtu akakujibu utumbo…anajibu tofauti na swali….kwa mtu kama mimi niliyezoea kupata jibu la namna ya kisheria, …mmh…naona tuyaache hayo, tuingie kwenye hoja yangu, maana tutapoteza muda hapa…’akasema na kunigeukia.

‘Kwanini umeingia kwenye ulingo huo wa kisheria….?’ Nikauliza licha ya kuwa kanikanya kuwa napoteza muda wa maswali mengi. Akatulia na kugeuka, nilijua anataka kuondoka, lakini alifanya kama vile yupo mahakamani, anatembe ahatua mbili pembeni halafu anageuka kukuangalia.

‘Mimi kama mwanamama, nawapenda sana wakina mama wenzangu, na kila ninapowaangalia na walinganisha na marehemu mama yangu kwa vile nimekulia katika maisha ambayo ninaweza kusema, ni ya kulelewa na mama bila baba, …maisha ya shida, …unaamuka hujui leo mtakula nini, unaamuka asubuhi,mkitamani kuche haraka mkimbilie hospitalini, lakini kunapokucha, manjikuta mnapambana na maisha, uone jinsi ilivyo….’akatulia na kidogo, akagonga gonga kisigino cha kiatu sakafuni.

‘Ugonjwa unaonekana sio kitu, ….mbeleya masiha mengine yaliyopo mbele yako, mtu anajitolea kufa kwa ajili ya familia yake…hajali kuwa anaumwa,anachojali ni kuangalia maisha ya mtoto wake….nikiyakumbuka hayo ninasononeka sana, lakini sijawahi kukata tamaa katika maisha yangu,….’akasema na niliona kitu katika macho yake,….unashindwa kukielezea, …. ujasiri na hekima, ndivyo ninavyoweza kuelezea kwa kifupi.

‘Mbona unanipa hamu ya kutaka kujua kuhusu wewe kabla hatujaongea kuhusu hilo lililokuleta,lakini kama ni la kwenda huko gerezani, sitaenda katu…..naomba tu unisimulie maisha yako usije ukaniitia askari wakanipeelka huko gerezani kwa nguvu kabla sijasikia nini kuhusu maisha yako…’nikasema,nay eye akacheka, na nikashangaa, maana alitafuta sehemu aka…kaaa,na kuniangalia kwa muda,akasema;

‘Haina shida, ….nitakusimulia maana nia na lengo langu ni kukusaidia wewe, na najau kabisa nikikusaidia wewe nitakuwa nimewasaidia akina mama wanaokuzunguka, na nitakuwa nimejifunza kitu ambacho nitaweza kukiandika katika utafiti wangu kuhusu ndoa na matatizo ya ndoa …’akasema na kuniangalia nami nilikuwa nimeinama nikiwaza jambo.

Tulitulia kwa muda, mimi nikimsubiri aanze kunisimulia kuhusu yeye, lakini kwa wakati huo nilikuwa pia nawaza lengo la huyu mwana dada ni nini, ni kuja nipeleka huko gerezani au ndio huo utafiti anaoufanya, au kuna kesi ipo mbele yake na anataaka kukusanya vielelezo….nikasema kimoyomoyo, muda utasema…..

‘Unajijua kuwa wewe naweza kukuita baba wa wake watatu, ….’akasema na kuniangalia sasa akiwa na yale macho ya mahakamani, na alipogundua hilo akajibadilisha na kutabasamu, ….sijui nisema nini, kuna kitu ambacho nimejifunza toka kwa huyu mwanadada, nashindwa hata kukuielezea,ila kwa ufupi, nabakia kusema kuwa mwanadada huyu kajaliwa na sifa nyingine ya huruma na upendo wa kuwajali wengine. Na kama akina mama wangelitulia na kujijua basi hii ndio hulka yao.

‘Wewe una huruma , akili,na hekima…’nikasema.

‘Kwanini unasema hivyo…?’ akaniuliza.

‘Kwasababu naiona kwenye macho yako,..unavyofikiria wenzako, na kujibadili ili mwenzako asiiumie, na pale unapojigundua kuwa umefanya jambo la kumuumiza mwenzako, kinyume na matarajio ya mwenzako unajibadili haraka, na kuleta jambo litakalomfanya mwenzako aingiwe na faraja….hilo wengi hawana, …kumfikiria mwenzako….atajihisije,ni nadra sana kwa mtu kuliwazia…., na kama ingelikwua hivyo, natumai upendo na amani vingelitawala dunia….’nikajikuta nikisema.

‘Ni kweli, nami nataka iwe hivyo,nataka kusaidia  bila kuumiza mtu , ….na kama ikibidi ni bora mimi niumie kwa ajili ya mwenzangu,lakini mwisho wa siku afanikiwe katika wema, sio katika ubaya…’ akatulia na kuniangalia na kuyarudia hayo maneno kwa upole.

Mwisho wa siku afanikiwe kwa wema,na sio kwa ubaya, maaa nisije nikaumia halafu wewe ninayekusaidia ukaangamia, hapana, sio lengo langu…..’akaangalia saa yake kw amuda kama vile anaakdria muda ,halafu akaningalia na kusema,

‘Mimi nimekulia kwenye matatizo na kutokana na matatizo hayo imekuwa kama shule kwangu,….matatizo hayo yamenivuta nijue nini wenzangu wanahisi pale waanpokuwa na matatizo kamahayo,kwasababu huwezi kuijua njaa,kama hujawahi kukukaa na njaa,….huwezi wewe umekulia nyumba ya geti kali,ukajua adha za wale wanaoishi kajamba nani….huwezi…..’akatizama chini, halafu alipoinua kichwa alisema.

‘Nataka kutokana na matatizo yaliyonikuta iwe fundisho la kuwasaidia wengine….’akasema na hapo akanipa hamu ya kutaka kusikia historia ya maisha yake, nikatulia kimiya nisimbughudhi tena,lakini kimiya kilitanda, hadi nikaona kuwa huenda hataki kusimulia kuhusu maisha yake, na alipoinua kichwa, nikaona macho yake yakiwa na kiza za machozi….

‘Ohh, kama nakutia uchungu,naomba unisamehe,lakini moyo wangu hautatulia kama sitaweza kusikia kisa cha maisha yako,  tafadahli nakuomba unisimulie angalau kidogo kuhusu wewe na ulipotokea…’nikamuuliza na bila hiyana ndio akanipa kisa cha maisha yake,….

************

‘Wewe ni mja mzito…?’ akasema mama wa mama yangu, yaani bibi yangu. Mama anasema mama yake alibadilika ghafala siku hiyo, maana ingawaje alikuwa keshaanza kuhisi lakini hakuwa na uhakika wa moja kwa moja, na alipoelezewa chanzo cha mimba hiyo, ndio akazidiwa kabisa,…akawa kshikwa shinikizo la damu na kutafuta hewa dirishani..

Siku hiyo bibi alipoona dalili zote za mimba anazo binti yake, akaamua kumbana kwa maswali, na mama alipouliza alikimbilia kulia na kusema;

‘Mama mimi sijui….na…’mama akaanza kulia na kabla hajajiweka sawa ndio akaingia baba, baba yake mama alikuwa mkali kama mbogo, ….huwa akiingia ndani wote wanajikunyata, na kuombe mungu kusiwe na tatizo….ila uzuri wake, kama kila kitu kipo shwari anageuka kuwa mcheshi na kuwachekesha,ila kama kuna kasoro, kuna tatizo huwa anatembeza kipigo kama anaua nyoka.

Mama anasema siku siku hiyo ilikuwa ni ya mvua,na kumbe baba yake alikuwa kafika muda mrefu , alikuwa hapo dirishani, na kwasababu kulikuwa kunanyesha mvua,….waao walikuwa ndani wakifanya shughuli za ndani, baba alipofika hapo hakuingia ndani na wao walikuwa hawajui kuwa keshafika.

`Baba yeye alikuwa akitengeneza mifereji ili maji yasituame, na baadae akawa anakandika sehemu kwenye nyumba ambapo aliona kuna uwazi. Kwasababa ya mvua, mama na bibi hawakujua kuwa kuna mtu dirishani, wao wanaongea tu kwa sauti hawana wasiwasi.

Huko nje babu alivutika na mazungumzo akawa katega sikio dirishani ,hakutaka kuingia moja kwa moja,na aliyoyasikia humo, yalimpandisha ile hasira aliyokuwa kaivundika kwa muda mrefu, maana siku kadhaa nyuma ,aliwahi kumpiga mke wake karibu ya kumuua, alikuja baadaye kujijutia na akatulia.Hakutaka kabisa kupiga,na likitokea jambo la kumtia hasira anaondoka kabisa humo ndani mpaka hasira iishe….

 Sasa hayo aliyoyasikia humo ndani yakamzindua na ile hasira ikamrejea, hasa aliposikia hilo swali la mkewe akimuuliza mama yangu, na pale kulipotanda kimiya na mama kutotoa jibu la haraka, akajua kweli binti yake ni mja mzito, na yale maelezo yaliyofuta baadaye ndiyo yaliyomuumiza na hakuweza kabisa kuvumilia,

Binti yake ana mimba, na isitoshe, waliompa mimba hawajulikani….kitu ambacho hakutaka kabisa kukusikia , na alikuwa mara kwa mara akilikemea hilo, na kutoa ilani kuwa ikitokea hivyo, basi huyo binti hatapata msamaha wake,na  kitakachotokea asije akalaumiwa.

‘Siku nikisiki kuwa una mimba, ama zako ama zangu ,nitatangulia mimi,au wewe..kablahicho kiumbe hakijazaliwa….’alisema hivyo siku moja, na mkewe akamkanya kuhsu huo usemi wake, na hapo akageukwa yeye, na kuambiwa….

‘Na wewe utakuwa wa kwanza kuondoka hapa duniani siku hiyo…kama utatetea huo upuuzi…’babu alisema 
na kuondoka.

Kwa ukweli mama yangu hakujijua kuwa ni mja mzito,kwani tendo alilofanyiwa lilitokea bila ridhaa yake, hakutarajia kuwa hivyo, …na alificha kabisa,..na wiki ilipopita, akasahau na kumshukuru mungu,ingawaje,ilibakia donda moyoni, lakini angelifanya nini,na wavulana waliomfanyia hilo walishahama hapo kijijini, kwa kuogopa kukamatwa.

Mwezi ulipokatika, akawa anajihisi vinginevyo,…mwezi wapili, hali ikazidi kuwa tete,…masikini ya mungu akajikuta katika wakati mgumu, hakujua kuna attizo gani, hakuwa na ufahamu huo,kuwa yale aliyofanyiwa yamezua jambo, na akashngaa kila akilakitu,anajisikia kichafuchefu, mwili unachoka, anajisikia kulalala ovyo…na alijaribu kujizuia, akijua ni hali ya muda tu,….

Lakini kumbe mama yake alikuwa akimchunguza, ila hakuwahi kupata muda wa kumuuliza, kwani walikuwa na kilimo,na wote walikuwa shamba muda mwingi, na baba yupo karibu, na siku moja mama alipokula kitu na kuanza kujisikia kichefu chefu, akakimbilia pemeni namama akamuona na aliporudi hapo walipo mama akambana na kumwambia…

‘Mwanangu vipi unaumwa….?’.

‘Mama najisikia vibaya , kichefu chefu…tu,sijui kwanini….’akamwambia mama yake siku  hiyo wakiwa shambani,mama akageuka kumwangali mumewe alipo, na alipoona yupo karibu akamwambia binti yake.

‘Labda unaumwa, chukua zile dawa alizokuja nazo kaka yako,za mseto, …maana kwenda hospitali kupimwa nako ni gharama, hatuna pesa kabisa ndani, na nikimgusia baba yako, atakimbilia kukutafutia miti shamba….’akasema bibi.

‘Wewe huamini tiba ya miti shamba wakati ndiyo inayokutibu kila siku….’akasema mumewe, na siku hiyo hiyo ikaisha salama, na walipofika nyumbani kwa vilebinti hakujijua alichofanya ni kuzitafuta hizo dawa alizoambiwa.

Basi mama akachukua dawa na kuzitumia, na mama alisema huwa hakuwa na kawaida ya kumwaumwa ovyo, na akiumwa, akila dawa kidogo tu, keshapona, hahitaji kukamilisha dozi, lakini alipokunywa hizo dawa hazikusaidia kitu, …

‘Mwanangu mbona unanitia wasiwasi….’akasema mama.

‘Mama hata mimi sijui kwanini….

‘Una mimba …..na nimekuchunguza kwa makini naona dalili zote za ujauzito unazo...mungu wangu tutaishije humu ndani, habu niambia ni ya nani hiyo mimba….?’ Akasema mama.

‘Mama,kwanini unasema hivyo….hapana, sina mimba…’akajitetea mama.

‘Sikiliza mwanangu,huna haja ya kuficha ni bora ijulikane mapema, ili hata baba yako akijua tujue huo mzigo ni wa nani,maana utakipata kipigo usichokitarajia…unakumbuka nini kila siku baba yako anasema, unamjua alivyo mkali….sasa sema mapema, ni uja uzito wa nani..?’ akasema mama kwa ukali.

‘Mama mimi sijui…mama naomba unisadie mimi sijui kuwa nina mimba, na wala sijui ime….sijui…kwasababu sikupenda iwe hivyo…walinibaka…..walinibaka, siku ile ya sherehe ya kumaliza darasa la saba…..na sikumbuki vyema ni akina nani, maana nilipoteza fahamu…’akasema.

‘Mwanangu una mimba….sijui itakuwaje…mungu wangu tulinde na hili…….’akasema huku akiona hakukaliki, moyo ukawa unmwenda mbio, hewa ilionekana ndogo, akaona akapate hewa dirishani

Mama akainuka pale alipokuwa kakaa na kueleekea dirishani , akasogeza pazia na kutizama nje kwa kupitia dirishani, ili pate hewa na akawa hapo akajikuta anatizamana uso kwa uso na mumewe, hakujua kuwa mumewake yupo hapo dirishani akisiriba dirisha, na alijua kabisa kayasiki hayo waliyokuwa wakiongea,  Alishituka akashikwa na kizunguzungu ,na hata pale alipojaribu kujizuia aisidondoke, ikashindikana na kujikuta akidondoka chini, lakini alijitahidi asipoteze fahamu,…

‘Mama..mama…’alikuwa mama yangu akimkimbia mama yake aliyekuwa kadondoka chini. Na mama yake akamsukuma akimwashiria kuwa aondoke hapo haraka, lakini mama haukuelewa, yeye mawazo yake ni kumasaidia mama yake ,… na mama yake alizidi kumwambia aondoke hapo haraka, ndipo mama akajua kuna jambo,na kabla hajajiweka sawa, mara mlango ukafunguliwa kwa kishindo, mama alipogeuka akakutana na bakora ikitua usoni,hajajiweka sawa,  nyingine ikatua kichwani….

‘Baba Nanihii utaua mbona unapiga binti yako kama unaua nyoka….’Bibi akasimama huku akipepesuka kumzuia baba, na baba hakujali anapiga nani, ikawa fimbo zote zinaishia kwa mkewe,na nyingi zilitua kichwani,na mama alipoona fimbo zitamuua mama yake naye akaingilia kati, hapo alipata mateke mangumi…akadondoka chini na kupoteza fahamu.
Alipozindukana alikuwa watu wamejaa, na yeye yupo kitandani,na mtu wa kwanza kumuona alikuwa mjomba wake,….macho yamjomba  yalikuwa mekundu yakionyesha kuwa alikuwa akilia.Mjomba alimpenda sana dada yake, kwani katika familia yao walizaliwa wawili, kwahiyo walipendana kama mapacha. Mama alipomuona mjomba yake yupo hivyo akamuuliza.

‘Mama yangu yupo wapi…’akauliza mama.

‘Hatunaye tena duniani ….dada yangu  kaondoka,mimi sina ndugu tena….’akasema mjomba huku akilia,mama hakuamini, akainuka pale kitandani na kwenda paletukio lilipotokea, hakuona mtu, bali watu wamejaa, akajua kweli…, ina maana huo ujauzito ambao hakupenda ndio umemuondoa mama yake duniani, anasema alichoweza kusema ni hayo maneno;

‘Heri na mimi nife….’halafu akadondoka na kupoteza fahamu.

Mama alipoteza fahamu kwa siku mbili, na alipozindukana, alijikuta yupo nje kwenye majani,na pembeni yake wapo watu wamejaa, na kila mmoja hana habari na yeye,…na hapo kumbukumbu ikamjia kuwa ndio siku ile ilipotokea msiba wa mama yake, hakujua kuwa kuna jingine tena,akainuka na kukaa vyema.

Mara akasiki sauti ikisema ; ’Nilishawaambia kuwa huyu mtoto ni nuksi katika hii familia,mnakumbuka yule mganga alivyosema…’akasema baba mkubwa.

‘Tuliwaambia hawakutusikia na akizidi kukaa hapa atazidi kutumaliza….tutakufa mmoja baada ya mwingine….heri asizindukane afe moja kwa moja…’akasema mke wa baba mkubwa.

`Nikiwa nawaza nini kimtokea tena, nikageuka huku na kule,nikaona watu wameinama kwa masikitiko’, mama alisema lakini yeye kwa mtizamo wake alijua ni maombolezo ya mama yake, kwahiyo aliinama na kuanza kulia, na baadaye akaja mjomba wake na kumuuliza anajisikiaje sasa.

‘Aheri ningekufa tu kama alivyokufa mama…mjomba nataka nikamuone mama, kawekwa wapi?’ akauliza mama na mjomba akasema kwa sauti ndogo ya huzuni.

‘Mbona mama yako kashazikwa siku mbili zilizopita, wewe ulikuwa umepoteza fahamu hata wakazania na wewe umeshakufa kama walivyokufa wazazi wako……’akasema mjomba.

‘Kama walivyokufa wazazi wangu …..,mbona mjomba sikuelewi…..’akauliza mama kwa mshangao.

‘Wanadai chanzo ni wewe kwasababu wewe una damu ya mkosi, hata ulipozaliwa ulitabiriwa hivyo na mganga wa kienyeji, na pale ulipoanza kuota meno sehemu ambayo sio kunapohitajika kwani  mara nyingi watoto wanaanziakuota meno sehemu inayotambulika lakini wewe ilikuwa kinyume  chake,  ikawa eti ni moja ya dalili alizosema huyo mganga,alisema na huyo mganga alidai kuwa ipo siku utaanza kuua wazazi wakommoja baada ya mwingine,na sasa imetokea hivyo,mama hayupo na sasa kafuta baba yako…..

 Mama anasema hakuamini, alibakia mdomo wazi…mama anasema hakuamini hizo imani zao, lakini matukio ambayo yalisemwa na yakatokea, akaona kweli huenda yeye ana nuksi na dawana kujiua mapema,….na bahati akasikia kuwa imepangwa mpango wa yeye kuuliwa kwa sumu , …akaona afadhali ngoja asubiri hiyo sumu…

Lakini alikuja mjomba na kumpa ushauri,kuwa hayo yote yaliyoongewa ni uongo, hakuna kitu kama hicho, na alichofanya ni kumchukuamama usiku usiku na kumpeleka  kijiji cha mbali,….’akanisimulia mama ,kipindi hicho na mama yupo kitandani akiumwa.

Ilivyotokea ni kuwa, baba alipogundua kuwa kamuua mke wake, akawa kama kachanganyikiwa, akawa anajipiga piga na kujiangusha chini, watu walijaribu kumshika lakini haikusaidia ,….kuna muda alitulia baada ya kufungwa kamba, kwani alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa kabisa.

Baada ya mazishi ya mama walirudi nyumbani,na baba akiwa kafungwa kamba,maana ilibidi wampeleke mazikoni akiwa kafungwa kamba hivyo hivyo, ili ahudhirie mazishi ya mkewe. Na baada ya mazishi ikapita siku ya pili yake , na wakizani kuwa baba katulia wakamfungua zile kamba,  hapo haijulikanai ilikuwaje, maana baba yake mama alijirusha juu na kudondokea kichwa na walipokuja kumuangali alikuwa marehemu.

Ulikuwa msiba mkubwa sana hapo nyumbani na kutokana na hizo imani ambazo zilienezwa kwa haraka,watu wakamchukia sana mama kuwa yeye ndiye chanzo cha vifo vya wazazi wake,na huko alipopelekwa akawa anaishi kwa shida,maana ni sehemu ngeni na walichokuta huko ni kijumba ambacho kilikuwa kimeachwa siku nyingi…..

Mama aliishi huko ufichoni, akiganga njaa,mpaka mimba ikakua na baadaye ndio akanizaa mimi….nikalelewa na mama yangu huyo kwa shida,simjui baba yangu , siwajui ndugu , ila majirani , …ksuikitisha ni kuwa mimi simjui baba yangu, hata mama mwenyewe hamjui kwani mimba hiyo aliipata kwa kubakwa….

Mama hakukata tamaa kunilea,lakini kuna tatizo ambalo lilijitokeza,kumbe kile kipigo cha mateke na mangumi,kiliacha athari katika mbavu zake, ikawa ni tatizo,….lakini haukuchoka kunilea, hakutulia, huku anapata maumivu huku anadamka asubuhi kutafuta mboga mboga, anakwenda kuziuza anapata vijisenti,tunaishi….hakujali afya yake…alinijali mimi

Mama aliomba usiku na mchana kuwa asife hadi hapo nitakapoweza kujishika mwenyewe,na mungu alisikia kilio chake,ingawaje aliniacha nikiwa bado nasoma,lakini sio sehemu mbaya,…..alinilea,akahangaika, nikamalzia darasa la saba, kwa shida na taabu,alihakikisha halali mpaka nimepata chakula….

Kitu kilichompa mama faraja ni akili yangu ya ajabu darasani, hata walimu walinishangaa, ikabidi nivushwe madarasa mawili mbele,kwahiyo mimi nilimaliza shule mapema kuliko umri wangu,….nikafaulu kwenda kidato cha kwanza,na kuchaguliwa shule ya vipaji maalumu….huko nikapata mfadhili wakunisomesha.

‘Mama namuoma mungu nipate kazi nije nikutibie….’siku moja nikamwambia mama, pale nilipogundua kuwa anaumwa, licha ya kunificha kwa muda mrefu,  mama akacheka kidogo nakusema;

‘Nashukuru sana mwanangu kuwa mungu kasikia kilio changu,maana aliona nitakufa kabla hujafikia sehemu 
nzuri,….nimevumilia sana mateso ya maumivu,na hapa nilipofikia sina uwezo tena wa kuyavumilia,….’akasema mama kumbe muda wote alikuwa akiteseka na jereha lililokuwa ndani kwa ndani ambaloo liligeuka kuwa donda ndugu,…kansa ikawa inamtafuna ndani kwa ndani.

‘Mama siuliniambia kuwa unakaribia kupona,naaahidi kuwa nikipata kazi tu nitafanya kila njia ukatibiwe upone kabisa.

‘Mwanangu alilopanga mungu halikwepeki, ninachoshukuru ni kuwa dua niliyoiomba imekubalika, ndio maana akafanikisha wewe kuvuka madarasa mawili mbele, ili muda wangu ukifika uwe umeshafikia sehemu nzuri….kwasababu muda aliopangiwa wa mwanadamu kuishi ukifika, huna ujanja....sasa hapo ulipofikia ni sehemu ambayo  unaweza ukajikongoja mwenywe…ngoja na mimi nikapumzike walipo wazazi wangu..

‘Mama unaongea nini, mbona unanitisha…mbona bado sijapata kazi,sina ndugu, sina wa kumtegemea….mama usije ukafa ukaniacha peke yangu, ni bora kama ni kufa tufe pamoja….’nikalalamika.

`Mwanangu, wa kumtegemea ni mungu….hapa nasubiri matokea yako ya mitihani,najua utakwenda kidato cha sita….huko hutashindwa maisha…na nakushauri mwanagu, usikate tamaa katika maisha,fanya juhudi ukijua kuwa huna ndugu, ndugu yako ni elimu yako….soma sana, na ushauri wangu nakupa….’mama alipofika hapo alaikohoa sana,na kwa mara ya kwanza, nikagundua kuwa kweli mama anaumwa,na anateseka sana kwa maumivu, alikuwa akinificha kwa muda wote huo lakini hapo hakuweza tena.

‘Mama ngoja nikamuite rafiki yako aje tusaidiane tukupeleke hospitali…’aliniambia mama kuwa alisema hayo huku mwili hauna nguvu kabisa,anatetemeka mwili mzima,huku akijizuia kulia, lakini mama yake akamuwahi kumshika mkono kabla hajaondoka karibu yake na kumwambia;,

‘Mwanangu usijali, nimemuomba mungu, kuwa nisikuache mpaka hapo nitakaposikia matokea yako ya kidato cha sita,…najua mungu yupo pamoja na waja wake, amesema tumombe naye atasikiliza maombi yetu, nitasubiri hadi matokeo yako yatoke,na hapo yakitoka ujue sitakuwa nawe tena kimwili,lakini kiroho nitakwua nawe daima,…nakushauri sana,elimu na kipato utakachopata kitumie kuwasadia wasiojiweza, ….kwa kufanya hivyo utakuwa umenisadia mimi mama yako,….’akasema huku akilalamika kwa maumivu

‘Ndio mama nitakusaidia nitakupeleka kwa wataalamu bingwa, utapona tu mama…siuliniambi akuwa kila ugonjwa una dawa …utapona tu mama…’nikamwambia yangu huku nikianza kulia.

‘Ni kweli kila uginjwa una dawa yake, isipokuwa kifo na uzee, hivyo havina dawa,….unajua mwanangu nikumabie kitu, ili unisaidie mimi hakikisha unawasadia akina mama, msaidie   mwanamke yoyote anayehitaji msaada,ukiwasaidia wasiojiweza, utakuwa umenisaidia na mimi huko nitakapokuwa…na nitafurahi sana, huo ndio ushauri wangumuhimu….’akakohoa na kukunja uso kwa maumivu, mama anasema kwa jinsi alivyomuona mama yake, aliyahisi na y eye yale maumvu.

‘Ujue mwanangu, mwanamke yoyote hapa dunia mwenye shida, ni sawa na mimi ukimsaidia utakuwa umenisadia mimi ,na pepo yangu itakuwa ya raha….na hapa nilipo naiona ipo mbele yangu…jingine ni kuwa, usikate tamaa,usisononeke,na usiishi kwa matarajio ya kumtegemea mtu, ujue kuwa kila mtu anatafuta kwa maslahi yake,…’alisema mama huku akikunja uso kwa maumivu.

`Mwananguna ni nadra kumpata mtu atakeyekusaidia kwa maslahi yako,….hilo sahau,ukiona mtu anakusaidia ujue anatarajia kitu fulani kwako, ….ila mzazi kwa mwanae, ila mama kwa mtoto wake, na wewe kama mwanamke unatakiwa ujichunge sana, uwe makini na mtu kama huyo anayekusaidia, atakuwa na ajenda fulani ya siri, kuwa makini kwa hilo….’akatulia kiasi kwamba nilidhania keshakufa,lakini kumbe alikuwa akijaribu kuvumilia maumivu, na baadaye akahema na kusema;

‘Matajiri wote pamoja na utajiri wao,wanasadia…wapo wanasaidia, lakini ukiwaona wanatoa misaada, ni sehemu ya kujitangaza,ili waonekane na wenye nchi, kwa ajili ya kulinda maslahi yao,….tajiri mwema, utamuona anatoa misaada kimiya kimiya na hata hataki ajulikane kuwa kasaidia,…uliwahi kuwaona matajiri wa namna hiyo….?’ Nikataka kumjibu,lakini alikuwa kafumba macho, nikamshika usoni, naikaoana anakunja sura,ina maana kila umapomgusa anahisi maumivu.

‘Mwanangu jua katika dunia hii kila mtu yupo kivyake,  kila mtu ana nafsi yake hasa inapofikia kitu maslahi,….kila mtu akiona maslahi anajiwazia yeye,…hata kama hajakifanyia kazi, atakitamani, atataka apate yeye, na hata ya aidi ya yule aliyevuja jasho…..’akatulia kwa muda, halafu aksema;

‘Mwanangu tegemea sana jasho lako, ogopa sana jasho la watu wengine, …..na kila chumo lako, ujue kuna sehemu ambayo sio yako, mwenyezimungu kakutunuku, ili iwe mtihani tu, humo kwenye chumo kuna chumo la masikini,kuna chumo la wazazi wako….na mzazi wako sio lazima niwe mimi niliyekuzaa tu, kila mwenye makamo kama mimi, mwenye familia ni mzazi wako,…na ni vyema ukakumbuka pia kutoa sadaka katika chumo lako….’akatulia hapo kwa muda mrefu sana.

Baadaye akafumbua macho na kuniangalia ,halafu akatabasamu, na kusema;

‘Safari imewadia mwanangu, nawaona wazazi wangu , wakinipokea baba na mama yangu,....tafadhali nakuomba usilie, ukajipiga piga na kulaani, kwanini umezaliwa aktika hali kama hiyo…yote ni mapenzi ya mungu, mshukuru yeye, na atakujali badala…ila tu ukumbuke mungu atanijali hadi hapo nitakapoyasikia matokeao yako ya mtihani, utafaulu,…na hiyo iwe ni mwanzo wa maisha yako, soma,…soma….soma….’akawa anayarudia hayo mpaka akatulia tuliii….’hapo nikashindwa kuvumilia nikamwendea rafiki yake mkubwa.

Rafiki yake huyo ndiye aliyemkaribisha hapo, akamsaidia na vyombo vya kupikia, wakawa wameshibana utafikiri ni ndugu wa tumbo moja,yeye ndiye aliyekuwa akijua siri ya mama,na matatizo yake, alikuja baadaye baadaye kuniamia kuwa walikuwa wakihangaika huku na kule kutafuta madawa na matibabu hadi pale mama alipopimwa na kugundulika kuwa ana huo ugonjwa na alikuwa kachelewa kutibiwa…..na kwahiyo hakuna la kufanya…

‘Sasa  kwanini alichelewa kutibiwa,….?’ Nikauliza huku nikijizuia kulia.

‘Shida…., huna pesa,huna elimu, huna ndugu,….alikuwa akijua ni maumivu ya kawaida tu yataisha, lakini kila siku maumivu hayo yalikuwa yakikua, ina maana hapo alipopigwa, kulivilia damu ndani kwa ndani, na matokeo yake ni kutengeneza ugonjwa mwingine,na hata hivyo hakutaka kukuonyesha kuwa anaumwa, aliniomba kabisa nisje kukuambai kuwa mama yako anaumwa…’akasema huyo rafiki yake.

Alipofika na kumuona mama hali yake ilivyo, akasema ni vyema tusaidiane tumpeleke hospitali, tukapata mkokoteni, tukamlaza humo na kuukokota hadi hospitali, na bahati nzuri tulikutana na dakitari ambaye alishawahi kumtibia awali,akamtizama na kumpima, ….

Yule dakitari alipomaliza kumpima mama alihema, na kutuangalia,akaniomba mimi nitoke nje,…sikukubali, nikasema nataka kusikia kila kitu,maana mimi ni mtoto wake,basi ndio akatumabia kuwa hali ya mama hapo alipo, ni bora angejifia tu, maana maumuvu anayopata sio ya kuelezea,..kila sehemu ya mwili ina maumivu.

Alimchoma sindani ya kutuliza maumivu na kumpa dawa nyingine za kumeza,na akatuambia kuwa hakuna zaidi , hata kama tutakwenda wapi,maana mimi niliomba kama inawezekana twende haospitali za juu, lakini alitushauri kuwa ni vyema tukamrudiha nyumbani tu,kuliko kumsumbua zaidi…

Basi tukawa hatuna jinsi tukarudi nyumbani. Kwa maiujiza ya mungu,ile sindano ikampa unafuu,akafumbua macho …lakini hakuwa akiongea tena, zaidi ya kujaribu kutikisa kichwa kila unapumuuliza kitu,kauli ikawa imekatika,……hata kula ikawa kwa shida…

Matokea ya mtihani yakatoka, na siku hiyo niliondoka nyumbani kwenda kuyaaangali hayo matokea nikamuacha mama akiwa na rafiki yake. Nilipofika hapo nikakuta jina langu likiwa ni miongoni mwa wanafunzi waliofaulu kwa maksi za juu, na bahati nzuri alikuwepo mfadhili wangu ambaye alikuwa, akisaidia wale wasio na uwezo wa kifedha,…alikuwa keshanijua kwasababu ya akili ya ya darasani.

‘Umefaulu vizuri sana, na ukiendelea hivi hivi utafika hadi chuo kikuu na mimi ninakuahidi kuwa niakusaidia hadi chuo kikuu,maana maksi zangu ni juu sana,….’akaniambia na mimi nikawa na matumaini kuwa sasa nina mu ambaye ni sawa na mzazi wangu.

Siku hiyo nilisahau kabisa kuwa mama yupo nyumbani mgonjwa, na nilisahau kuwa mama alishaniamabia kuwa akisikia matokeoa yangu tu ndio itakuwa mwisho wa kuishi kwake hapa duniani,…kwa ile furaja, sikutaka kupoteza muda, nikakimbilia nyumbani huku nikishangilia kuwa nimefauli vizuri.

‘Mama nimefaulu….kwa maksi za hali ya juu…’nikasema huku nikiingia chumba anacholala mama,nilimkuta akiwa kalala vile vile, maana ilishafika hatua kuwa kila kitu ni hapo hapo kitandani, na mtu wa kumsaidia ni mimi au huyo rafiki yake, na aliposikia sauti yangu akafungua macho, aliniangalia kwa muda, nikaona akitabasamu….tabasamu lile lilikaa muda  mrefu usoni, na baadaye akafumba macho, ….hakuyafumbua tena…ikawa ndio kwaheri……

Alikuja rafiki yake , akanikuta nimesimama namwangalia mama , akainama na kumgusa, akamshika shingoni,halafu akanigeukia na kusema;

‘Mama yako keshaondoka…sasa keshapumzika, ….kumbuka alichokuambia mama yako,usilia…..,jipe moyo,na hiyo ni heri kwake, kama ulivyoona, na kama alivyosema dakitari kuwa alikuwa akiumia kwa maumivu makali, lakini alisubiri mpaka ayasikie matokea yako,keshayasikia na karizika nayo ,na kwahiyo sasa mungu kamchukua akajipumzikie, …’akaniambia rafiki yake aknikumbatia akasema;

‘Pole sana, ….ndio kidunia, kaza moyo, na tutakuwa pamoja,wewe ni mwanangu, hadi hapo na mimi nitakapoondoka dunia ….’akasema huyo rafiki wa mama yangu, lakini sikuweza kuvumilia….sikuweza kujizua kulia, nikalia hadi nikazirai…..

Alipofika tena hapo huyu mwanadada alishindwa kuvumilia machozi yakamtoka,na  harakaharaka akajifuta na kujifanya anafuta jasho, na kugeukia upande mwingine kwa muda, akaniambia anatoka kidogo kunawa uso, na aliporudi akaniangalai na akatabasamu, nami nikatabasamu,na kusema;

‘Pole sana, unajua wewe ni mwanamke wa peke yake, ambaye ninaweza kusema ni adimu katika hii dunia,…kwanza ile kukubali ukweli, ukaamua kuwa sasa mimi nipo pake yangu, na njia peke yake ni elimu, ….hukujilemeza na kusema mimi basi,…na hukujiunga na mambo machafu,kama  walivyofanya mke wangu, kweli wewe umebarikiwa na huko mama yako alipo atakuwa na furaha sana….lakini…’nikataka kusema kitu lakini yeye akanikatiza na kusema;

‘Kweli mama yangu yupo kwenye furaha maana siku za mwanzo nilikuwa nikimuota, nakutana naye kweney njozi, na hata wakati mwingine namuona kama taswira, hasa ninapokuwa kwenye shida fukani, na hunielekeza nini la kufanya….unajau kwenye kupambana na maisha kuna majaribu mengi, na mimi kama binadamu yalikuwa yakinikuta, inafikia mahali unatafuta mtu w akukusaidia hakuna, huna ndugu huna wazazi, basi hapo hapo taswira ya mama hunitokea na kuniambi nipo pampoja na yeye,fanya hivi na vile utafanikiwa.

‘Anakutokea unamuona hivi kwa macho yako….?’ Nikkamuuliza.

‘Unaweza ukasema hivyo kwa moyo wa harakaharaka, lakini ni kitu kama hisia,ila kuna taswira kabisa unaiona mbele yako inaongea, na hata kama nipo mahakamani namuona akiwa kama mshauri wangu, …..ni miujiza ya mungu,….na hata jana alinitokea akanishauri nikusaidie wewe kwa ajili ya wanawake..’akasema

‘Unisaidi kwa ajili ya wanawake! ….Sijakuelewa wanawake gani hao….?’ Nikamuuliza.

‘Ndio maana nataka kukuulizia kuhusu maisha yako ya ndoa, nataka kujua jinsi ilivyokuwa wewe na hawo wanawake uliwahi kuishi nao, ili nijue wapi pa kuanzia, na ikizingatia kuwa kuna huyo anayekuhitaji huko gerezani,aliyekamatwa ,….’akasema na kuangalia saa yake.

‘Kiukweli nimepewa taarifa tu kuwa kuna mwanamama kakamatwa, na huenda akawa mke wako, mimi sijaonana naye, na wala sijamjua ni nani ….  lakini kabla hatujafika huko, naomba sasa nikuulize maswali kuhusu maisha yako ya ndoa zako ,na naomba unijibu,….umekuwa kila nikikuuliza swali na weweunaniuliza swali, kwa mtindo huo tutakesha hapa na mimi nina majukumu mwengi sana….’akasema.

‘Sawa nimukuelewa,niulize nami nitakujibu,kadrii ya uwezo wangu…ila kuna swali ambalo ulilikwepa kulijibu, nilipokuuliza awali, je wewe umeolewa……?’
Akaniangalia na kutabasamu…..

NB.Nawaomba kwa leo tuishie hapa,sijui kama nawachosha au tupo pamoja....vyovyote iwavyo nawapenda sana.

WAZO LA LEO: Tuwapende na kuwasaidia wazazi wetu, ujue kila chumo unalochuma kuna sehemu ya wazazi wako, pia kila chumo unalopata, kuna sehemu ya wasiojiweza,….hata kama kipato unachopata ni kidogo sana, toa kutokana na udogo wake, kwani kwa kutoa hivyo ndivyo unaongeza Baraka ya riziki yako, kumbuka kuwa kutoa sio utajiri, kutoa moyo….


Ni mimi: emu-three

No comments :