Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, February 10, 2012

Ndoa ni kupendana sio kuumizana



‘Baba nimepata njiwa jike, nitamtunza kwenye kijumba nilichomjengea….lakini nahitaji wawe njiwa wengi, kwahiyo namtafuta njiwa jike…’ akasema mtoto wangu huku akiwa kamshikilia njiwa wake mkononi, sikutaka kumuuliza wapi alipompatia huyo njiwa, kwani nilishaambiwa na mama yake kuwa alimpa pesa baada ya kuomba kwa muda mrefu kwa ajili ya kununua njiwa.

‘Kwani utakuwa unamfungia ndani siku zote, wewe muachie awe anaruka mwishowe atakutana na dume …atataga mayai, na njiwa watakuwa wengi….’nikamwambia kimzaha.

‘Hapana baba, itakuwa sio sahihi, ukiwa na njiwa jike ni lazima uwe na njiwa dume pia,, huyu njiwa jike akikaa peke yake atakuwa mpweke na anaweza akatoroka…’akasema mwanangu.

‘Haya kamtafute huko ulikompatia huyu, kwani huyu ulimpataje, …?’ nikamuuliza.

‘Nimemnunua kwa rafiki yangu yeye ana njiwa wengi …lakini sina pesa nyingine za kumnunulia njiwa dume, kwahiyo naomba ..’akakatiza maneno yake kwani njiwa yule alitaka kumponyoka mkononi.

‘Nitakuapa hizo pesa, lakini kwa masharti kuwa safari hii uwe wa kwanza kwenye mtihani wako…’akakubali kwa msharti hayo, na kweli njiwa dume akapatikana.

Siku zilivyokwenda njiwa wakawa wanaongezeka kukawa na burudani ya aina yake, na siku moja akanitembelea rafiki yangu, tukawa tumekaa karibu na banda la njiwa, na rafiki yangu akavutiwa sana na wale njiwa akawa anawatizama kwa bashasha, nikamuuliza;

‘Vipi rafiki yangu inaonekana kuwa unapenda sana hawa njiwa, nakuona umevutiwa nao sana…?’ nikamuuliza.

‘Mhh, unajua rafiki yangu, viumbe wa mungu ni mifano tosha ya maisha yetu sisi wanadamu, unaweza ukawaaangalia kama wanyama, au kama ndege tu, lakini ukiwachunguza kwenye matendo yao, yanatupa mafunzo mengi, lakini ni kwa wenye kutafakari…’akasema na kuwasogelea wale njiwa na kwa mbele kulikuwa na njiwa wawili walikuwa wanatembea pamoja karibu karibu, na mmoja akawa kama anamtengeneza mwenzake mabawa yake kwa mdomo wake.

‘Angalia wale njiwa wawili pale, waleinavyoonyesha ni jike na dume, na inavyoonekana na wapenzi ni mke na mume, wanaonyesha ishara ya upendo, angalia mmoja anavyomjali mwenzake, na angalia na mwenzake anafanya hivyo hivyo…ule ndio upendo wa dhati…upendo wa asili tunaonyeshwa ishara na viumbe hawa wa mungu, …lakini sisi wanadamu hatupendani…tumejijengea mipaka ya chuki, na kuziita mila….’akawasogelea wale njiwa na kuwarushia mtama.

Mimi kwasababu nawaangalai sana wale njiwa, na vitu kama hivyoo nimeviona sana, sikujali mazunguzmo yake , nilishagundua hali kama ile na mimi niliwaza meni yanayohusiana na upendo wa viumbe hawa, kuwa ndege hawa njiwa ukiwachunguza kwa makini wanaonyesha ishara nzuri ya kupendana, jinsi gani wanavyokaa pale na ukiwalisha na jinsi gani wanavyokaa wawiliwawili, lakini kauli ya mwisho ya rafiki yangu ilinishitua kidogo ikabidi nimuulize ;

‘Kwanini unasema sisi wanadamu hatupendani…?’ nikamdadisi.

‘Ndugu yangu mimi nasema haya kwa mfano, maana nikikuhadithia maisha yangu utapata fundisho kubwa sana, na nilipowaona hawa njiwa machozi yalikuwa yakinilenga lenga, nikawa najisema moyoni, huenda ningelikufa huku sina radhi, na baraka za ndoa zilikuwa zimepukutika hutaamini hayo…’akasema yule rafiki yangu na akarudi kukaa kwenye kiti, nami nikawa na subira ili niweze kuyasikia maisha ya huyo jamaa ambayo kwa mtizamo wake anadai yana mafundisho ndani yake.

Wapenzi wa blog hii. Kisa hiki nimekitoa mapema kabla hatujamalizia kisa chetu kilichopo hewani, kisa hicho bado kinaendelea, na kwa vile ghala la kuhifadhia hivi visa ni shida, nikaona nikitoe hiki mapema, kwani ni kifupi tu, huku tukiendelea na kisa chetu, hili ni kwa maombi ya mama wawili,

‘Nimekua nikiishi kwenye ndoa huku sina raha, hivi kweli mapenzi ya ndoa ndio hivyo, hivi mapenzi nikuumizana, …hivi kweli mapenzi ni utumwa….’ Kauli kama hizi zililipa uchungu nikaona kuna haja ya kuweka hiki kisa, sio kuwa kanileta yeye hiki kisa, ila nimegundua kuwa kisa hiki kinaweza kikasaidia katika kuelimisha, na kama mtakifuatilia kwa makini, mtagundua kuwa kuna siri kubwa ndani ya `upendo wa dhati’ kati ya mke na mume. Badilika kama un atabia hiyo upime maisha yako kabla na baadaya yatakuwaje, ..ni siri kubwa, munu katujalia lakini wapi, tunajiona wababe ndani ya ndoa, wababe makazini, wababe wa dunia.

Hebu tuendelee kumsikiliza huyu rafiki yetu.

*****
‘Mimi natokea huko nyanda za ziwa, na kama unavyojua huko kwetu, kupiga mke au kupigana na mke ni sehemu ya mapenzi yetu…’akasema huku atatabasamu, kwani mimi sikuishia kutabasamu bali nilicheka maana haiji akilini, niliona kama mzaha, kuwa kupiga, iwe ni sehemu ya mapenzi, hata mabondia wakipigana ulingoni , sizani wanapigana kwa mapenzi, huwa kila mmoja anakuwa na chuki na mwenzake, ingawaje mwisho wa siku wanakumbatiana kama sehemu ya mchezo.

‘Hiyo ni imani imejijenga tu, lakini kihalisia sio kweli, watu wanaumia , watu wanateseka, katika maisha kama hayo, lakini imekuwa kama mfungwa ambaye kafungwa bila kosa, kila siku anasononeka moyoni na kila mara mfungwa huyo anajaribu kumuomba mungu wake kuwa lini atamsaidia aondokane na mazila hayo…na wengi wanaoteseka na mazila hayo ni wanawake , kwasasababu wao wameolewa….’akasema rafiki yangu.

‘Mimi nimekulia kijijini nikasoma huko huko hadi sekondari, kwahiyo maisha hayo nayajua na sio kuyajua tu, bali hata mimi nilikuwa na imani hiyo…na hata nilipooa, ilibidi niwe nafuta desturi hizo, nikijua bila kufanya hivyo mke atanidharau, jamii itanidharau, kwahiyo nilikuwa kama simba aliyejeruhiwa…’akasema kwa ujasiri, lakini huku usoni akionyesha machungu fulani.

‘Mke wanu alikuwa naye kalelewa kinyumbani hasa, alijua hayo ni sehemu ya maisha, kwahiyo kipigo kwake alikipokea kama sehemu ya mapenzi, ingawaje kwaweli alikuwa akilia kwa uchungu nakuomba msamaha pale inapotokea hivyo….’akasema rafiki yangu huyo, nami nikaona nimuulize swali haraka kabla hajaendelea kunipa utamu, lakini ilionekana rafiki yangu hakupenda kuulizwaulizwa maswali wakati anaongea, nikajua ni hulka yake…ubinafsi, umimi..

‘Kwani kipigo hicho kinatokea tu, bila kosa, yaani ni starehe ili ….?’ Nikauliza lakini jamaa hakuwa akinisikiliza akawa anaongea tu kama vile hakutaka niulize swali.

’Tuliishi na mke wanu hivyo hivyo hadi tukapata watoto wawili, na hali hiyo ya kupiga hakuishia kwa mke tu hata kwa watoto nilifanya hivyo hivyo, hutaamini huwa nikirudi nyumbani inakuwa kama simba karudi, watoto walikuwa na raha wakicheza lakini waliponiona walisinyaa, mke alikuwa akiongea na watoto wake, nikionekana watoto wanatafuta sehemu ya kujificha…mke naye anajiandaa akihisi kuwa atapigwa…’akasema rafiki yangu huyo.

‘Kosa dogo lilikuwa chanzo cha kutembeza kipigo, na kipigo chetu, sio kugusa, ni kipigo hadi mtu anavimba, au hata kutoa damu, hutaona ajabu asubuhi unamkuta mke kavimba jicho, na wakati mwingine naye ananirudishia, kwahiyo na mimi mara chache unaweza kunikuta nimevimba jicho…’akasema huku akicheka kwa mzaha lakini uso wake ulijaa uchungu fulani.

‘Maisha ya ajabu kweli hayo’ nikasema huku nikicheka…

‘Sio maisha ya ajabu, ni maisha ya dhuluma, mateso na…sio haki kabisa, mimi niliishi maisha hayo miaka kumi na tano nikiwa simba, nikiwa mbabe ndani ya familia, watoto mke, wanaona raha nikiwa sipo nyumbani, ila inabidi niwepo kwasababu wanahitaji pesa za matumizi, wanahitajii ada, …, wanahitaji sehemu ya kukaa, kwani nilikuwa naishi nyumba ya kupanga….kwahiyo kwa mtizamo huo, nilikuwa mtu muhimu sana, baba wa nyumba….unafanya mchezo, baba wa nyumba…’ akasema na kuyarudi hayo maneno kwa msisitizo.

‘Siku ambayo sitoisahau ni pale mke wangu alipokuwa mja mzito, nilirudi nyumbani, nikiwa nina hasira za kazini, bosi wetu mpya toka huko Uhindini, alinikasirisha sana, mimi kama mwanaume nanyanyaswa ndani ya nchi yangu, inafikia hatua mtu ananidharau na kuniambia, nipoo legelege kama mke…wewe ananizarau kiasi hicho, lege lege kama mke…’ akasema na kuinuka nikijua anataka kunivamia mimi, lakini akakaa tena.

‘Unajua hasira mbaya sana, …hata hivyo huyu mtu sitamsahau, nina uchungu naye, tuyaache hayo, …lakini kwanini,… wakati nimekuwa hapo kazini miaka kumi, nimepewa ufanyakazi bora mara nyingi, napiga kazi kama katapila, leo huyu jamaa kaja kakuta matunda mema ya kampuni, anaanza kutuandama na kutunyayasa kama watumwa ndani ya nchi yetu….siku hiyo nilikuwa na hasira za kuua mtu….kama angeyarudia hayo maneno tena mbele yangu, ningeliwekwa ndani …’akasema huku akinyiosha kidole juu.

Siku hiyo nilipofika nyumbani nikamkuta mke wangu kalala kwenye kochi, vyombo vichafu, chakula hakuna, nikamuuliza kwanini hali kama hiyo, mke wanu akasema anajisikia kuumwa,…na hana hela ya kwenda hospitali, …. nikamwangalia kwa hasira nikamsogelea na zile hasira za kazini nikazitolea kwake, sikujali kuwa ni mja mzito au vipi, nilichosikia ni kauli ya `nakufaaa..’

‘Ulimfanyaje shemeji …unyama gani huo…’nilijikuta nikisema kwa hasira.

‘Nilishituka na nilipomtizama mke wangu, alikuwa katulia kimiya chini sakafuni, kazirai…hapo hapo nikaanza kuchanganyikiwa, ukumbuke huko kazini hakuna cha pesa yoyote ya zaida , mwisho wa mwezi mpaka mwisho wa mwezi, na ikifikia katikati ya mwezi huna kitu, huyo muhindi kaondoa matibabu kwa familia, ina maana ujitibie mwenyewe, hapo nilikuwa mimi na….’akatamka neno ambalo sikulipenda kuliweka hapa.

Nilitoka mbio nje, nikitafuta usafiri, hapo sina hata senti mfukoni, nikapata taksi, yule dereva akaniambia shilingi elifu kumi hadi hospitalini, sikujali nikaingia ndani na kumkuta mke akiwa kalala vile vile, hapo nikashiwa nguvu, nikamuomba yule dereva aje anisadie kumbeba, maana hata majirani walikuwa hawataki kunisaidia kwasababu ya tabia yangu, huwa nikitembeza kipigo, atakayekuja kuamua naye anapambana na mimi, kwahiyo nilikuwa kama nimetengwa..

Yule dereva alikuja tukasaidiana kumbeba mke wangu hadi kwenye gari, na mara watoto ambao walikuwa wamejificha wakati natembeza kipigo, wakajitokeza na walipomuona mama yao katika ile hali wakaanza kulia kimiya kimiya wakijua mama keshakufa….hutaamini niliwageukiwa wale watoto na mimi nikajikuta machozi yakinitoka…

NB
Ndugu wepenzi kisa hiki kifupi kina mafundisho fulani , naomba mkifuatilie sehemu yake ya pili, lakini inabidi niishie hapa maana muda umekwisha, nitahitajika kupata elifu moja nyingine kukimalizia,lakini sio kwa leo, kwani hata hivyo nataka kuendelea kumalizia kisa chetu cha `Akufaaye,…’

Fundishho mpaka hapa ni kuwa : Unapofanya jambo kwa mwenzako hebu jaribu kujifikia mwenyewe, je kama ningelifanyiwa hivyo ningelifurahi, maana mkuki usiwe kwa nguruwe tu.

Ubabe, ukali kupita kiasi, kujiona wewe unaogopwa sio sifa, na hili tunaliona hata makazini watu mwisho wa siku wanakuwa na nidhamu ya uwoga, wanafanyakazi tu pale bosi huyo akija, …sio sahihi, jengeni utaratibu wa kushirikiana kwa upendo, elekezaneni kwa busara, kwa vitendo…ili mtu afanye kazi ile kama yake, aipende na mwisho wa siku ni mafanikio yenye baraka,…

Ni hayo kwa leo Ijumaa njema,





Ni mimi: emu-three

4 comments :

Anonymous said...

Huwa sijui kwanini, maana kuna kitu nakipendaga katika uandishi wako, lakini tuyaache hayo.
Mimi bado nasema kuwa mila na desturi tuzifuate kama zina faida kwetu, lakini kama zinatukwaza, kwanini tuzifuate?
Ama kwa hiki kisa, huyo jamaa alitawaliwa na hasira zake, na hasira ni mbaya, inaumiza na kujenga chuki, anachukuliaje makuzi ya hao watoto, watakuwa wanamchukia badala ya kumpenda,na wao huenda wakarithi hiyo tabia.
Tunasubiri sehemu iliyopita, nami nitazungumza yangu ya moyoni, maana msiseme tu wanaume ndio wabaya, kuna mengina hata wanawake wanakuwa chanzo...ngoja amalizie nitawaambia ni kitu gani
Mpenda amani

Yasinta Ngonyani said...

Nimesoma kisa hiki na nikasahau kusema kitu samahani. Nimekuwa najiuliza kwanini kama mikono yake inawasha asinunue ngoma au achukue jembe na kulima. Hapo waumiao ni watoto kwani nao watakapokuwa wakubwa watafanya hivyo . Maisha haya jamani taabu kweli. Ngoja niendelee kusoma sehemu ifuatayo....

emuthree said...

Nashukuru wapendwa `mpenda amani' na dada Yasinta kwa kuwa pamoja nami, Tupo pamoja

Rachel Siwa said...

Tehtehtheteh da'Yasinta kama mwaume kweli akaanzishe ugomvi uko nje kwa wanaume wenzie aone kama yeye anaubavu!!!!!watoto wakiona hivi hata upendo na baba kama huyo hawatakuwa nao.Ahsante sana ndugu wa mimi,Pamoja sana!!!