Maneno alijaribu kupiga simu tena na tena mpaka kidole kikauma kwa kubonyeza,… lakini cha ajabu kila alipopiga zile namba, sauti ilisikika ikisema, tafadhali simu inatumika! Alijikuta katika mshango, kwani kama kweli inatumika, ina maana hayo maongezi ni zaidi ya masaa matatu, haiwezekani, ina maana muda wote mke wake anaongea kwenye simu, haiwezekani. Akafika mahali akakata tamaa kabisa, hasa baada ya kuangalia saa ya ukutani na kuona inaingia saa sita za usiku, akainuka pale kwenye kochi na kuelekea chumbani, alipofika kwenye mlango wa chumba, akasimama kidogo, na kutafakari kitu, akaishika simu yake tena mkononi, na kupiga tena ile namba ya mkewe, ikatoa maneno yale yale kuwa simu anayopiga inatumika kwa sasa.
Tangu waoane na mkewe haijawahi kutokea hivyo, huwa inatokea mara chache mkewe anachelewa kidogo, lakini hajawahi kuzidi saa mbili za usiku. Ingawaje kweli mke wake alishampa taarifa kuwa watachelewa, kwasababu wana maandalizi ya kiuhasibu kwa ajili ya wakaguzi wa mahesabu, lakini hakumbuki mkewe kumwambia kuwa watakesha huko huko. `Lazima kuna sabababu nyingine’, akasema kwa sauti, huku akikuna kichwa.
Akajiuliza huku anakuna kichwa, `au kuna ajali imetokea nini…? Hapana…wazo baya hili’ akasema kwa sauti. Akaingiwa na wasiwasi pale wazo hilo la ajali lilipoingia ubongoni, ‘Lakini kama kuna ajali, sikuona tangazo lolote kwenye luninga likisema kuna ajali imetokea hapa Dar’, akasema kimoyomoyo, akiogopa kuyatamka yale maneno kwa nguvu, huku akijipa moyo kuwa hilo halipo, lazima kuna sababu nyingine,…`sababu gani sasa?’ akapiga ngumi kwenye mlango, huku akikunja uso kwa hasira akasema kimoyomoyo `Labda mkewe wangu kaanza mahusiano mabaya, haiwezekani, haiwezekani, hayo ni maneno ya watu wenye nia mbaya na ndoa yangu, ninavyomjua Maua hawezi kufanya hivyo, kwani tunapendana kikweli’ akasema kwa sauti na kuingia chumbani hadi kitandani na kujitupa mzimamzima..
Baadaye sijui akawaza nini, akaichukua simu yake, na kukaa vizuri, akaitafuta simu ya baba Mkwe wake, akataka kupiga, lakini akasita, akaona hiyo sio vyema, kwani itakuwa kama anamshitakia mkewe, kama kuna jambo linaendelea nay eye alitakiwa kuchunguza kwanza, lakini kama kuna tatizo lazima awafahamishe ndugu za mke, lakini nani kamwambia kuna tatizo…
Saa saba ikaingia, akajaribu simu , sasa inasema simu unayopiga haipatikani, basi akajirusha kitandani na kujaribu kupata usingizi, usingizi ukawa haupatikani, kachukua komputa ndogo na kuingia kwenya mtandao , labda kama bado wapo kazini, anaweza kuwasiliana naye, lakini mtandao ukawa haupatikani, akasonya na kuifunga ile komputa, akajifunika uso gubigubi, na katika kuhangaika akajikuta kashikwa na kausingizi ka kujiiba.
Walikuwa wakiogelea na maji yalikuwa mengi, yakiwa na mawingu, kwa mbali akaona mamba, cha ajabu mamba huyo alikuwa na kichwa cha mtu, akawa anamsogelea Maua, …Maneno akamwita Maua kuwa aogelee kutoka nje ya maji kwani kuna Mamba anakuja lakini Maua akamzarau akisema yule sio mamba, toka lini mamba akwa na kichwa cha mtu, Maneno akaingiwa na wasiwasi, akawa anaogela kwa haraka ili kwenda kumzuia Maua asielekee kule alipo yule Mamba.
Maneno alijua mbinu za mamba, anajifanya kafa , au anajifanya vyovyote iwavyo, hata kujifanya ana sura ya mtu huku akificha domo lake baya, aligundua hizo mbinu, lakini Maua hakuwa anajua hizo mbinu za mamba, akawa anavutika kutaka kujua ni mamba gani yule mwenye kichwa cha mtu., ..alikuwa kaduwaa, bila kujua kuwa yule mamba anamsogela taratibu…
Maneno akapiga mbizi ya kwanza, alipoibuka, akakuta bado yupo mbali na alipo Maua, akapiga mbizi ya pili na ya tatu, lakini kila akiibuka anajikuta yupo mbali na Maua, na Mamba alikuwa anakaribia sana na alipokuwa Maua, na Maua hasogei kabaki anashangaa, na wala hataki hata kugeuka nyuma ili apate kumsikia mume wake anavyomshauri.
Maneno akapiga mbizi za mfululizo, alipoibuka,akakuta kweupe, si Maua wala Mamba anayeonekana, Maneno akaanza kupiga kelele ya kuita Maua, Maua, huku anaangalia huku na kule, na mara maji yakaanza kugeuka rangi, …rangi nyekundu…hii iliashiria nini,, kuwa Maua kaliwa na Mamba..,.Maneno akawa kama kapagawa anapiga kelele za kuita,Maua maua, kwanini hukunisikia, Maua , maua…
‘Wewe vipi mume wangu, mbona unapiga kelele Maua, Maua, unaniota nini…nimerudi sasa…lakini najisikia vibaya mume wangu kanitafutie dawa na maji, kichwa kinaniuma kwelikweli..’ sauti ya mkewe ilijaa chumbani, na kumfanya Maneno ainuke haraka kitandani huku akihema, kutokana na ile ndoto mbaya ya kutisha. Alimwangali Maua mara mbili tatu, hakuamini kuwa ile ilikuwa ndoto, na ukweli upo wazi, Maua yupo salama.
‘Siamini…siamini mke wangu..upo salama kweli…’ akasema Maneno
‘Huamini nini wewe, niletee dawa, usiseme unaamini ndoto…kichwa changu kinauma Maneno, nilitee dawa..’ Maua alisema huku kashikilia kichwa. Ni kweli kichwa kilikuwa kikimuuma, tangu alipoamuka, kule….na hata alipopewa kile kinywaji eti cha kuzimua , bado mauimvu ya kichwa yalikuwa yakimwandama, na kila alipojaribu kuwaza nini kilitokea ule usiku ndivyo alivyozidisha maumivu ya kichwa.
Alikumbuka jinsi alivyotaka kudondoka pale aliposikia sauti ikimuita nyuma, pale alipotoka hotelini, akiwa kamuona baba yake, alikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa, na nia yake ni kuondoka pale hoteli haraka iwezekanavyo, ikiwa anakwepa kabisa asikutane na baba yake, kwani angesema nini, pale atakapoulizwa alikuwa wapi asubuhi kama ile, …ndio walikuwa kwenye mktano wa kampuni, lakini hadi asubuhi…kuwa walikuwa na kazi na mkutano, uliomfanya alale hapo hotelini, asingeleweka, na hili baba yake alimshauri sana, kuwa hata iweje, asije akalala nje na kumuacha mume wake, …labda iwe ni safari.
‘Mwanangu, kazi hizi za maofisini zina vishawishi sana, kama ingekuwa uwezo wangu ningekuambia usifanye kazi, lakini umesoma ili iweje, …uelemike tu, hapana, lazima ufanye kazi kwa maendeelo yenu na familia yako, …sasa itumie elimu yako kujua vishawishi vibaya, usidanganyike na vikao vya mahotelini, vya kurudi usiku, au kulala huko, huko…wengine wanalenga vikao kama hivyo kwa mabaya..chunga sana mwanangu, …chunga sana kwani inaweza ikawa mwanzo wa kashifa katika familia, nami sitavumili hilo, ni bora nijue sina mtoto…kuliko kashifa kama hizo…’ akayasikia yale maneno ya baba yake yakipenya ubongoni!
Wakati anawaza maneno haya ya baba yake ndipo akasikia sauti inamuita,…alishituka kiasi kwamba aliukosa mlango aliokuwa kaushikilia akahisi kizunguzungu,…na akajua huyo anayemuita nyuma ni baba yake, atamwambia nini, …mungu wangu, namjua baba hana simile, ataanza kunichamba hapa hapa mbele za watu na sijui itaishiaje…oh, nimeshaleta kashifa kwenye familia…
‘Maua kwanini unachukua taxi, nitakupeleka mwenyewe…’ kumbe ilikuwa sauti ya bosi wake! Akasonya na kugeuza kichwa kidogo kuhakikisha kuwa sio baba yake. Kwa muda ule,hakutaka kabisa kumsikia bosi wake, hakutaka kabisa aijulikane kuwa alikuwa na yeye usiku huo, mbona huyu mtu haelewei au ndio ulikuwa mpango wake wa kumzalilisha…akageuka kwa hasira akitaka kutamka maneno mabaya, lakini akasita, akafungua mlango wa taxi haraka na kumwamrisha dereva aondoe gari haraka. Na wakati wanaondoka akamuona baba yake akitoka mlangoni mwa ile hoteli, ina maana watakutana na bosi wake, sijui wataongea nini, na asije akaharibu kwa kusema walikuwa pamoja.
Akatamani kumpigia simu bosi wake kuwa asimtaje kuwa walikuwa pamoja, lakini akaghairi kwani kichwa kilikuwa kikimgonga isivyo kawaida, akaona ajilaze nyuma ya kiti…akitafakari kwa upole jinsi gani atamwabia mume wake, ilikuwaje mpaka alale huko huko, na alishangaa, kwanini mume wake hakumpigia, sio kawaida yake, kwani akichelewa kidogo anapigiwa simu…na hata hivyo akajilaumu mwenyewe kuwa yeye ndiye alitakiwa kumpigia mwenzake kuwa kachelewa kwasababu gani. Akataka kupapasa begi ili aangalie kuhakikisha kuwa huenda Maneno alipiga simu na yeye hakuisikia, akashika begi mara mbili kuipapasa simu,…akawa hajaiona, akasema kimoyomoyo, ataiangalia akifika nyumbani, kwani muda ule alikuwa kachokoza kichwa, kichwa kinauma …
Alipofika nyumbani kwake, ilikuwa bado ni alifajiri, akashangaa taa za ndani bado zinawaka, inaonyesha mume wake bado alikuwa macho anamsubiri, akagonga mlango lakini kulikuwa kimya, akagonga tena na tena, alipoona kimya akachukua ufunguo wake wa akiba na kufungua mlango, akafulululiza chumbani, akiwa na lengo la kwenda kitandani na kujifunika gubi gubi, hakutaka kuongea na mtu kwa wakati huo, …
`Maua maua…’ akashangaa kumusikia mume wake akimuita huku akiwa usingizini, na alionekana kuhangaika ndani ya ndoto…moyo wa huruma ukamshika, na machozi yakambubujika, alikumbuka kuwa mume wake wanapendana , nay eye kafikia kuisaliti ndoa yake, akawaza sana huku anabibujikwa na mchozi, akamsogelea mume wake pale alipolala nakujaribu kumuita…lakini kichwa kikawa hakimpi nafasi, kichwa kinauma kufuatana na mapigo ya moyo.
‘Maua ulikuwa wapi usiku kucha ina maana ndio mkutano umekufanya ulale huko huko…’akauliza Maneno baada ya kumpa mkewe dawa ya kutuliza maumivu ya kichwa, na kumuacha kiasi cha nusu saa.
‘Tutaongea baadaye mume wangu, ni hadithi ndefu, na isitoshe hali yangu sio nzuri kwa sasa , tafadhali naomba nilale kidogo…’ akasema, Maua, na kabla hajajilaza vizuri, mara simu ya Maneno ikaita, Maneno akaipokea aliposkiliza akamwangalia mke wake, mke wake alikuwa kajifunika gubi gubi…
‘Kalala anaumwa…mpigie baadaye’ akasema Maneno. Simu ikamwambia kuwa ni muhimu amwambie ni kuhusu simu yake. Maneno alivyosikia hivyo akachukua mkoba wa mke wake na katafuta simu ya Maua kwenye begi lake akakuta haipo.
`Maua simu yako ipo wapi , kuna mtu kapiga simu kasema `ni kuhusu simu yako’..akasema Maneno.
‘Nimekuambia nataka nipate usingizi kidogo, simu yangu ipo ndani ya mkoba wangu, huyo aliyepiga mwambia nimelala…’ akasema Maua, na Maneno akambia kwa msisitizo kuwa simu yake haipo kwenye mkoba. Maua akainuka kitandani huku kakunja uso akachukua begi lake na kuitafuta simu yake , akakuta kweli haipo, akashangaa, kwani hakumbuki kuitoa ndani ya begi.
Maua alipohakikisha kweli simu yake haipo, akamuomba Maneno simu yake na ili aipiga ile simu iliyoita, akakuta ni namba yake, akamwangalia mume wake,… lakini hakutaka kusema kitu . Akaipiga ile namba, na mara ikapokelewa na badala ya mtu kuongea simu akaanza kutoa sauti za mziki laini, halafu sauti ya kike ikasikika ikisema maneno ya ajabu ajabu…`nakutaka, nakupenda, twende chumbani…..’ yalikuwa maneno ambayo ukiyasikia unajua huyo ni mwanamke Malaya akimbembeleza mwanaume kimapenzi…! Maua alijikuta mkono ukiishiwa na nguvu, na simu ikamponyoka mkononi na bahati nzuri ilidondokea kitandani alijikuta nguvu zikiisha, na yeye mwenye akadondokea kitandani akazirai….
Tuendeleee.....oooh, muda umeisha tuzidi kuwepo, kwani sasa mambo yanaanza kuiva
Ni mimi: emu-three
3 comments :
m3 mambo hayo
nangoja kwa hamu nijuwe what is next
na nakushukuru kwa kuwa nasisi katika kutuendeleza mkasa huu mzuri
mungu akubariki
M3 NASHUKURU LEO NIMEKUPATA KWY MTANDAO NILIKUWA NA MIS STORY. NIMESOMA YOTE LEO, AMA KWELI IBILISI WA MTU NI MTU.
KAZI NZURI M3 UBARIKIWE.
BN
Siku 2 mtandao wa blog ulikuwa na matatizo.tukutane j3 mungu akipenda
Post a Comment