Simu ndiyo iliyomshitua Maua toka katika mawazo mazito, akaipokea haraka na kuanza kusikiliza, na sauti iliyojaa ndani ya sikilio ilikuwa sauti ya bosi wake mpya. Tangu bosi wake afike hapo amejikuta katika mtihani mgumu, amejaribu kuishinda hiyo mitihani na hata kuomba ushauri kwa rafiki yake wa karibu lakini badala ya kupata msaada alioutegemea alijikuta akishinikizwa kuwa asiichie hiyo bahati.
‘Hivi wewe una nini, Maneno kakupa nini, mtu mwenyewe yule mshamba wa kutupwa, hivi anajua hata mapenzi yule, sikiliza Maua, sisi wenzako tunaitafuta hiyo bahati tunaikosa, mimi huyu bosi mpya, nimemwekea mtego, ipo siku atanasa, kwasababu nimejaribu kile mbinu, lakini anajifanya kuwa hanioni, sasa nimejua kuwa kazimia kwako, na bahati mbaya kazimia kwa mtu asiyejua bahati..sikiliza Maua, mimi nakupa miezi miwili kama hujafanikiwa kuwa naye, namchukua..na nahakikisha akiingia kwenye anga zangu, habanduki…’ akasema rafiki yake .
‘Wewe Rose, hivi mume wako akisikia maneno hayo, siatakuua..ndoa yako siitakuwa mashakani, ina maana huogopi?’ akamuuliza Maua kwa mshangao.
‘Maua katika maisha ya mwanamke, kuna mapenzi ya aina mbili, mapenzi ya ndoa, kwa mume wako, off-course, unatakiwa uilinde ndoa yako,…unajua tena umuhimu wa ndooa…na ndoa ni kama sukari ndani ya chai….lakini lazima uwe na mapenzi ya kujiiba, haya ni kama kulamba asali,…asali sio kama sukari ambayo unaweza ukajaliwa kuwa nayo wakati wote, asali unaipata kwa nadra, siunajua utamu wa asali…! ‘ Akaonyesha kidole na kukilamba. Maua alimuwaza sana rafiki yake, na kumuonea wivu, kwa jinsi gani anavyojiamini , na kufanya mambo yake vile atakavyo, na haimpi shida, lakini yeye kila akiwaza anajiona ni kuitakia matatizo ambayo mwisho wa siku ni majuto.
Akamuwaza huyo bosi ambaye tangu afike hapo amekuwa gumzo kwa kila mwanamke hapo ofisini, umbo, sura na ameonekana kuwa ana kitu ambacho akina dada wanakitamani…sijui ni kitu gani hicho…. Yeye ingawaje alivutika pia, lakini alikuwa akiilinda ndoa yake na pia hakupenda kabisa kujiingiza katika kashifa yoyote , kwani ameshapitia katika mazingira ya utata, mazingira ambayo bado ana kitendawili kichwani, …kama mama angelikuwepo huenda hicho kitendawili kingeshateguliwa,… lakini ndio hivyo tena mama keshaondoka!
Akainuka haraka kuitikia muito wa bosi na kuelekea kwenye chumba kile kilichoandikwa `Mhasibu mkuu’ alipofika mlangoni akasita kidogo, akajikagua na kujiweka vizuri, halafu akafungua mlango, na na kuingia ndani, na mbele yake akakutana na macho ya bosi wake, ambaye alikuwa akimtizama moja kwa moja usoni utafikiri alikuwa akisubiri atokee pale mlango amwangalie, …
Maua hakujali akaingia moja kwa moja na kusimama mbele ya meza ya bosi wake na kusubiri kuambiwa alichoitiwa, lakini bosi wake alikuwa bado kamtizama machoni, na hali hii ikamfanya Maua ashikwe na kigugumizi, na kuangalia chini akisubiri. ‘huyu bosi vipi, mbona…’ akawaza moyoni!
Akiwa kainama akakumbuka mara ya kwanza alipokutana na huyu bosi mwenye mvuto `handsome’, lakini kabla ya kumbukumbu hiyo haijamjia sauti fulani kichwani ikatanda ubongoni ikisema…
`Sitaki kashifa…sitaki kashifa kabisa katika hii familia, makosa aliyofanya mama yako singependa yairudie kabisa katika familia hii…unasikia Maua, sipendi wewe uige kashifa za mama yako, nakupenda sana mwanangu, ila ukivunja miiko ya ndoa, sitakuwa na uvumilivu…sitajali kuwa wewe ni mwanangu na binti yangu mpendwa, a…
Akainua kichwa na kumtizama bosi wake, ambaye alikuwa bado kamtizama machoni, akatamani kufunua kinywa chake, lakini akasita, akasema kuanza kuongea ni kujitafuta mazungumzo ya kumtia kwenye mitihani, akasema `nitanyamaza kinya mapaka yeye aniambie nini alichoniitia’
Alitabasamu kimoyomoyo huku mawazo yake yakimkumbuka bosi huyu siku alipotambulishwa kwa mara ya kwanza.
‘Maua umtambue bosi wenu mpya wa hii kampuni, yeye ndiye meneja wa idara ya fedha, naomba mshirikiane naye…’ ulikuwa utambuslisho kutoka kwa meneja utawala kwa meneja huyu mpya. Na Maua akamtupia jicho la haraka, akahisi kitu fulani kikimvuta amwangalie tena, akatupa jicho jingine, akatamani kuendele kumwangalia na kila mara bosi huyo alipokuwa akiangalia upande wake, akawa anainama haraka,…mpaka bosi akahisi kitu.
‘Wewe ndio Maua, mtunza fedha na mhasibu wetu, nahisi tutakuwa karibu sana….’ Akasema na kumshika Maua mkono. Maua akaupokea mkono wa maneja wake huyo mpya, na hisia fulani zikawa zimemwingia mwilini, na kujiuliza kwanini hisia hizi zimjie, wakati hataki kabisa hisia kama hizi…akasema labda ni ibilisi tu.
Toka siku hiyo akawa na mazoea ya kukutana na bosi wake huyo mpya kwasababu wapo idara moja na kwa vile kazi yake ilihitaji awe karibu sana nay eye, na hili likazidi kumchochea na hatimaye hisia zikajifichua.
‘Hivi Maua unampenda sana mume wako?’ akauliza bosi.
‘Swali gani tena hilo, …kama unavyompenda mkeo ndivyo ninavyompenda mume wangu, kwanini umeniuliza hivyo…’ akamtizama bosi wake kwa macho ya yenye kurembeka.
‘Hata , …ila nimekuwa nikiwaza sana, kuwa kumbe unaweza ukaoa na bado ukakutana na mtu akakuvutia sana, na hata kumsahau mkeo, au mumeo, hivi kweli inawezekana hivyo…’ bosi akajifanya kama vile hatilii manani hayo mazungumzo, kwani aliwaza mbali sana. Alimkumbuka mkewe ambaye kumuoa kwake ilikuwa ni kwa bahati tu, na zaidi ilikuwa sababu ya uwezo na umaarufu wa binti huyo. Kwani mkewe alitokea kwenye familia ya watu wakubwa, wa heshima na kuogopewa.
Maua akaipokea mafaili ambayo bosi wake amempa huku akiwaza maneno ya bosi wake kwa mtizamo wa shauku, kuwa hivi kweli inawezekana, uwe umeolewa na mume uliyempenda tangu utotoni, na ghafla ukakutana na mwanaume mwingine, ukamtamani….hapana, hiyo haitatokea kwangu kabisa, nampenda sana Maneno, hata kama …..kataka kusema kitu, kikapotelea kichwani, huku akigeuka kutaka kuondoka, na bosi wake akamwiita jina lake, na akasimama kusikiliza bila kugeuka.
‘Maua, Maua, naona nimeingiwa na ….nataka uwe rafiki yangu…urafiki wa kweli, nahisi nimekupenda….’ Akasikia hayo maneno na kuhisi kama kitu kimekandamizwa ndani ya moyo wake, asiweze kusikia zaidi ila kukawa na maneno yanayojirudia rudia akilini mwake ambayo huwa yanasikika sana pale anapokuwa kwenye janga au kitu cha kumtia katika majaribu maneno hayo yanakuwa kama kinga yake , maneno hayo yakamjia akilini yakisema….
`Sitaki kashifa…sitaki kashifa kabisa katika hii familia,…..’ akafungua malango wa ofisi haraka na bila kutizama nyuma akaurudishia ule mlango nyuma yake na kurudi mezani mwake akiwaza.
*****
BOSI WA FEDHA, akiwa ofisini kwake akili ilikuwa haipo kwenye kazi, alimuwaza sana Maua, akawa anaiuliza kwanini anatamani sana huyu binti ndiye angelikuwa mke wake, kila alivyomuangalia aliona anaendana sana na yeye, ana kila sifa anayoitaka yeye, …lakini kila alivyowaza saa akajikuta anaogopa kuwa huko anakokwenda kutamtia matatani, akakumbuka kabisa kuwa yeye ni mume wa mtu na anachokitamani sio sahihi, keshaoa na anatakiwa kuridhika na mke wake…Akayakumbuka maneno na mikwala aliyowekewa siku ya harusi yake, hasa kutoka kwa kaka mtu…!
Mhh kaka mtu…alipomfikiria huyu mtu akasikia mwili mzima ukisisimka kwa woga!
Aliikumbuka vyema ile siku ya harusi yao ambayo walivweza kuhudhuria viongozi wakubwa na watu wa heshima zao, nahii ndio ndoto yake …umashuhuri, ..anapenda sana kuwa mtu wa matawi ya juu, ingawaje yeye anatokea kwa walalahoi. Hakuamini kuwa ndoto yake imetimia, nay a kuwa sasa yeye ni miongoni mwa mtu…ingawaje ki hali halisi hakutaraji kabisa kuwa ipo siku atakuwa miongoni mwa watu wakutizamwa na watu mashuhuri kama hawo.
Wakati anawaza haya ndipo akamkumbuka kaka mtu, siku ile ya harusi, …wakati anapongezwa na watu mbalimbali, mara akaja jamaa , mkakamavu, na macho yake yalikuwa mepesi ajabu, na hata kutembea kwake, kulikuwa kwa kikakamvu, ….akaja mbele yake na kujitambulisha mwenyewe kuwa yeye ni kaka mtu, yupo kwenye mambo ya usalama…hakumalizia usalama wa nini, lakini akilini mwa Bosi alijua ni nani. Ila kilichomtia shaka ni jinsi jamaa huyo alivyokuwa akimtizama, kwani macho ya huyu jamaa yalikuwa yakikuangalia, utahisi anauchungulia moyo wako na kujua kila kitu kilichojifichika ndani ya nafsi yako.
‘Bwa-shemeji, natumai hatujakutana, kwasababu zisizozuilika, usijali sana, ila mimi ni kaka kipenzi wa huyo mkeo…kwa kifupi mimi nampenda sana dada yangu, na wewe umeamua kumchukua awe katika himaya yako,….nimefurahi sana, ila tu nakuomba sana, usije ukamuuzi dada yangu. Sio kwamba naingilia ndoa yako, hapana, kuna kusigishana hapa na pale, hiyo ni kawaida, ila kuna kuvuka mpaka. Unajua bwashemeji, kuna watu hawajui nini maana ya ndoa, wao wanafikiri wameoa mfanyakazi au mtumwa fulani….wanafikia hadi kuwapiga wake zao hadi kuwaumiza…mmmh, huko ni kuvuka mpaka, na sidhani kuwa wewe utafikia huko. Jingine ni swala la tamaa, wewe umeoa, bado unataka nan je…hapo bwana nikisikia…
‘Unajua bwanashemeji nilipokuangalia tu mara ya kwanza kuingia hapa, nilihisi kitu fulani, nahisi umemuoa tu kwasababu…siunajua tena …, sasa jifunze kuishi naye, naomba sana uzingatie hilo, najua yote ni maisha, nahisi hivyo, huenda sivyo…usinielewe vibaya …cha muhimu ni jitihada za ukweli, ficha hiyo hisia ninayoihisi ….kwani ukiidhirisha…`hiyo hisia’, sizani kama utahimili gereza moja baya sana hapa nchini…’akamshika Bosi fedha begani na kutabasamu kama vile anafanya mzaha, …Bosi fedha, alihisi kama vile kashikwa na spana, iliyogusa hadi mfupa wa ndani, na maumivu aliyoyapata pale, anayahisi hadi leo…na toka siku hiyo alianza kumuogopa sana shemai yake, hata akimtembelea anatamani ajifiche amwambie mkewe hayupo, lakinii ni kaka mtu atafanyaje!.
Aliwaza sana yale maneno ya kaka mtu kiundani, kuwa imekuwaje jamaa huyu akagundua siri yake ya moyoni, kiukweli alimuoa mke wake …ndio anampenda , lakinii sio kihivyo sana, wapo aliowapenda zaidi yake, lakini hawana `mvuto wa kimaisha…pesa, utajiri!. Akamuwaza sana mke wake, kuwa ingawaje hisia za ukweli za upendo hazipo sana lakini ni msichana mrembo, na nia yake ikawa kujitahidi kumpenda, ili aweze kufanikiwa kimaisha. Na kweli walipo-oana, akajikuta akipanda ngazi moja baada ya nyingine, kimaisha, na hata kupata wadhifa mkubwa katika kampuni kubwa. Akashukuru sana, ila mabadiliko ya mke wake, yakawa hayampi raha, mkewe amekuwa akijiachia, na mwili umehumuka sana, hili lilikuwa likimpa shida…!
Siku moja alitoka naye, katika maswala ya sherehe, na wakati anamtambulishamkewe kwa marafiki zake, wasichana wa umri wake wakawa wanamzihaki kuwa mkewe sikuu hizi kaamua kuwa muinua vyuma.Na kweli mkewe licha ya kuonekana mnene, lakini ana nguvu za ajabu, unene wake sio ule wa kujaziana kimafutafuta, ni ule unene wenye nguvu. Anakumbuka siku moja walipokorofishana na mkewe baada ya tukio lile, ambalo hatalisahau maishani, aliinuliwa mzima mzima akalazwa juu ya meza, na kilichofuta siku hiyo hakuamini, alionyeshwa yale macheche ….na ya kuwa kama hatosheki , basi siku ile aliambiwa ale mpaka ashibe…akatabasamu huku akili yake ikiwaza tukio lile, ambalo hatalisahau maishani, …
Mhh, halafu ndio nataka nifanye makosa haya tena…’ akashika kichwa akiwaza,`lakini kwa binti kama huyu nipo tayari kufanya…, na nahisi tutaivana, na kufichiana siri…ngoja nimuweke sawa kwanza.
Akakumbuka tukio ambalo lilimtokea na kuwa kama onyo, na alipolikumbuka moyo wake ulijawa na hisia ya uwoga, lilikuwa tukio ambalo lingemrudisha katika ulalahoi ambao alishauaga, na huenda lingempelekea kuswekwa kwenye gereza baya kuliko yote…akasisimuka na mwili alipokumbuka jinsi ilivyokuwa;
Katika ofisi ile alikuwepo dada mmoja, dada huyo alikuwa `mcheshi ‘ kupindukia, kiasi kwamba bosi alianza kujenga urafiki naye, …kwani dada yule hakuwa mcheshi tu, bali alijaliwa urembo wa aina yake, siku moja utani ukaingiza ukweli, wakajipanga na huyo binti kuvunja amri ya ndoa,…na mbaya zaidi wakapanga kufisidi ndoa zao ndani ya ofisi baada ya saa za kazi….moyoni aliogopa, lakini tamaa za kimwili zikamzidi kimo. Ilipofika jioni akampigia simu mke wake kuwa atachelewa, basi wakabakia na dada huyo ambaye alikuwa na malengo yake …
Wakiwa wanajiandaa na wameanza kusarurana nguo, na kwa uzembe wao hawakukumbuka kufunga mlango , kwani wana uhakika kuwa kwa muda kama huo hakuna mtu anayekuja, saa za kazi zimekwisha. Wakawa wamezama kwenye makucha ya shetani, na dunia ya Ibilisi ikawa inawashangilia. Wakiwa katika pilika pilika mara binti yule akasikia haja, akamwaga mwenzake kwanza, kabla hawajaanza kile walichokuwa wakikiandaa, akamuacha jamaa akiwa hajitambui…
Bosi akawa kabakia huku akihema juu kwa juu, na ghafla akasikia sauti ya mlango ukifunguliwa, akashituka, na mwanzoni alizania kuwa huenda ni mlinzi anakagua mlango, akasogea karibu na mlango, ilikuwa kusogea kwa kuruka ruka, kwani nguo zilishashushwa nusu….aka…lakini ikashngaa ..kwanini kwani mlinzi hawezi kukagua mlango kama anajua kuna mtu ndani, akasikia mchanyato wa viatu ukija kuelekea ofisini kwake,…huo mwendo ni wa kike…akasema moyoni mwake, …. akaruka haraka huku akivaa vyema,…kwani ilionyesha dhahiri kuwa huyo anayekuja anakuja kuelekea kwenye ofisi yake..akaamua kuuwahi mlango na kuufunga, hawezi kuacha kile alichokianza…akajisema moyoni, basi katika ule mwendo wa kuruka, kuvuta suruwali juu, maana ilishaanza kuvuliwa na…akajikuta kala muereka na kulala kudondokea pua. Alipoinuka na kujigeuza kuangalia juu…macho yalimtoka kwa woga, …kila kitu mwilinii kilinywea, ….
Hebu fikiria mwenyewe bosi alifikwa na masahbu gani na alifanya nini…kumbuka familia hiyo sio ya mchezo…..
Ni mimi: emu-three
6 comments :
akaamua kurudi pale alipowaacha baba na mama yake, alipofika,…aliona kimya, watu hawapo…alijikuta akidondoka chini!).....
m3 kidogo nimepitikiwa ilikuwaje kutoka hapo sehemu ya 5 nahii ya 6 inavoelezea nieleweshe pls
Kweli familia hiyo sio mchezo!
Mie nasubiria muendelezo na kama ni limbwata basi KILIMBWATA nimedakwa na limbwata ya stori hii!:-(
Samira hiyoo itakuja katika muendelezo wake, ni mtindo wa ina hiyo, na hauendi moja kwa moja kimtiririko, nashukuru sana kwa kuwa upo nami , na hili linanionyesha kuwa `kweli unasoma' stori zangu.
Wakati mwingine navunjika nguvu, najua watu wanasoma, lakini kukiwa kimya bila neno, nashindwa kujua kuwa watu `wameipokeaje, je kuna sehemu nimeruka au vipi, kwasababu mwenyewe naiandika katika `msongo; mzito, kwa kujiiba ofisinii na kama ni internet cafe unakimbizana na muda.
Leo nimekwama tena kuandika, kwani nina vimeo vya kiofisi...Tukijaliwa weekend nitaiweka safi...NASHUKURU KUWA TUPO PAMOJA HATA KWA KIMYAKIMYA!
Mkuu Simon unasema Limbwata...hahaha...nashukuru kama limekupata. TUPO PAMOJA.
Habari yako m3 ni matumaini yangu u buheri wa afya, pongezi nyingi kwako, nimekuwa mfuasi mzuri wa blog yako hasa upande wa hadith, ile ya dawa ya moto ni moto yani nakupongeza sana kwa utunzi wko ambao unaelimisha yani hongera sana, m3 mie nipo pamoja na wewe sana tuu usikate tamaa zidi kutupa utamu, na kutujuza kuhusu hali ya maisha jinsi inavyokwenda hapa kwetu, uwezi amini mie nikiwa nasoma hiyo hadithi sitaki kabisa mtu anisemeshe jinsi ilivyokuwa tamu napenda nikianza kuisoma yani mwanzo mwisho ndio uu napumua, kweli nadhani sio mimi tuu ni wengi wanavutiwa na utunzi wako, wewe mkareeeee kwa kweli najifunza mengi toka kwako na kila navyozidi kukusoma nazidi kuelimika zaidi na kujua mengi toka kwako sio hadithi tuu na mengine yaliyomo mule kwenye blog yako nakushukuru sana tena sana, pia napenda nimshukuru rafiki yangu mpenzi ambaye amenipa hii blog yako nakili sikuwahi kuyafahamu kwamba haya mambo ya blog kuwa yanaelimisha kiasi hiki yani elimu bila ada, japo nilishawahi kusikia watu wanablog hapo nyuma ila sikuwa nafatilia, kwa upendo wake huyo rafiki wa mimi ambaye amenijuza na kunifundisha mengi sana sijui yeye mwenyewe kama anatambua kuwa amenifungua macho na kunitoa tongotongo nyingi sana, kwakweli sikuwahi kukutana na rafiki mwenye upendo wa kweli mvumilivu na mwenye sifa zote za kuitwa binadamu kama yeye, maana watu tupo wengi ila binadamu ni wachache mnoo, nampenda sana toka ndani ya moyo wangu namshukuru yeye pia
Sina mengi zaidi ya kukusifu na kukushukuru wewe sana kwa moyo wako wa kujitoa kuielimisha na kuijuza jamii yetu ambyo wengi bado tupo gizani hasa ktka uwelewa wa mambo yaani tupo utumwani kiakili
UBARIKIWE SANA
M.U.H
Nashukuru sana M.U.H , umenipa moyo sana, na kama kweli nimeweza kufanya hayo uliyosema kwako, napata faraja ya hali juu. Wewekweli umwema, na ubarikiwe sana.
Nami nitajitahidi sana nisiwavunje moyo, kwani najua mkiwa nje, nakala , hadithi na visa vya kiswahili mnavihitaji kwa wingi.
Tuendelee kuwa pamoja, na nashukuru pia kuwa umejisajili kama mpenzi wa kweli wa blog hii. Shukurani na namshukuru huyo aliyekuelekeza kuja ndanii ya blog hii, mpe shukuranii za dhati kuwa yeye ni rafiki wa kweli.
emu3 umekatisha patamu na pabaya nasubiri muendeleza. Ama kweli TAMAA ni mbaya kweli una mkeo nyumbani lakini bado una penda wengine.... ha ha ha haaaa nimecheka kweli hapa kaka Simon aliposema nanukuu "Mie nasubiria muendelezo na kama ni limbwata basi KILIMBWATA nimedakwa na limbwata ya stori hii!:-(" mwisho wa nukuu. kaaazi ipo...
Post a Comment