Ilikuwa ndani ya ofisi moja , ikiwa na wafanyakazi wengi, lakini vyumba vidogovidogo viligawa maidara , na kila mmoja alionekana kainamia au kuchungulia komputa yake, na mojawapo ya chumba kimoja kilichoandika ‘Mhasibu ‘ alionekana dada mmoja mzuri, akiwa kashika shavu, na kuangalia juu, kama vile anahesabu vitu vilivyopo juu, na baadaye akainama kama vile anataka kuandika kitu. Akageuza kichwa kuangalia chumba kilichopo mbele yake, kikiwa na maandishi makubwa yaliyoandikwa `Mhasibu Mkuu’.
Mhasibu mkuu tangu aje amenibadili maisha yangu kabisaa…raha kwa kwenda mbele, hayo ndiyo maisha, lakini…akawaza kwa makini akijuta moyoni, akikumbuka maneno ya baba yake, alivyokutana naye karibuni;
‘Mwanangu nimekuita hapa leo, unajua tena mimi ni mzazi wako, na nisingependa kuishii kiajabu-ajabu, lazima niwe karibu sana na wanangu. Ulipoamua kuolewa na yule mume hakuna aliyekulazimisha, uliamua kwa hiari yako mwenyewe, ingawaje mama…mama yako mdogo, alipinga sana, unajua mama yako anakupenda sana, utafikiri alikuzaa, najua unajua hilo, ndio maana unadeka kwake. Sitaki mambo ya kudekezwa, …unasikia, wewe sasa ni msichana mkubwa, una akili, ya jambo baya na zuri, au sio mwanangu, yeye anadai kuwa nilikubali uolewe na huyo mume wako kwa kukukomoa, kwanini nikukomoe wakati wewe ni mwanangu…achana naye, ila ninachotaka kusema ni kuwa naomba muishi vyema sana na mume wako, ikibidi umsaidie mumeo, kama mnahitaji msaada sema usiwe na wasiwasi, mfanye mumeo awe mzalishaji, asiwe ana kaa tu, …ila naomba sana usimsaliti…kama unavyojua kazi zeti ni nyeti sana, hazihitaji kashifa…, ’ haya yalikuwa maneno ya baba kwa binti yake, ambayo Maua aliyatafakari kwa makini sana.
Wakati Anayatafakari hayo maneno, akawa anavuta hisia, na kuwaza kwanini baba yake akamwamba hayo maneno, amehisi nini kikubwa, au kagundua mahusiano yake na…akatikisa kichwa na kuangalia ena ule mlango uliandikwa Mhasibu mkuu, akayasoma kwa sauti `MHASIBU MKUU’, alipogundua kuwa kasoma kwa sauti akatizama pembeni kuwaangalia wafanyakazi wenzake wakiwa wanapilikapilika za kazi, akaguna, na kurejesha kumbukumbu zake, na sasa zilirejea kipindi ambacho aliitwa na baba yake na kuambiwa maneno yale, yale aliyoambiwa juzi,
Alimuita baada ya kuingia na kumuona anaongea na …oh, aliogopa kutanguliza neno la `marehemu’ akasema kwa sauti `Mama yangu mpenzi’, akashika shavu na kukumbuka ile siku ambayo menono aliyotamka baba yake siku ile, kayarudia tena walipokutana juzi, alimuita alivyomuona anaongea na mama yake akiwa katika hali ya kulia ndio akahisi kuna kitu. Licha ya kuwa karibu na baba yake bado alimuogopa sana, akiwa hana uhakika wa kikweli kuwa, huenda yeye sio mtoto halali wa baba huyu,ingawaje mama alimthibitishia kuwa hizo hisia sio za kweli,.. .
‘Kama sio kweli, mbona baba litamka maneno yale, maneno yale aliyasikia siku baba yake alipokuwa akizozana na mama yake, kama kawaida yao, na hata baba kutamka maneno makali kuwa mama sio mwaminifu na kamzalia binti wa `haramu’…alitamka wazi hilo neno..`haramu’, na katika familia hiyo binti pekee ni yeye, ina maana kweli ndio yeye analiyekuwa akizungumziwa. Siku hiyo mzozo ule ulifikia karibu mama afukuzwe,… lakini ndivyo ilivyo kwao, wakikutana neno dogo huzaa ugomvi, lakini mwisho wa siku wanakimbiana, kil mtu chumba chake, na nje kama ni lazima kuwa pamoja huwezi kugundua,…wanaogopa kashifa!
Siku aliposikia maneno hayo, hakuweza kulala, ina maana, aliwaza sana , ina maana huyu sio baba yangu wa kunizaa,…haiwezekani, baba ananipenda sana, mimi na ndugu zangu tunapendana sana, kaka zangu wananijali, …hili la mtoto wa haramu limetokea wapi, akajikuta akilia, …na hata kufikia kumlaani mama yake kuwa kama kweli ni hivyo, ….hapana kwanini aliamua kufanya hivyo, na hata kumzaa na kuitwa jina baya la `haramu’…ina maana kama ndugu zake wengine wanajua, na baba akaondoka duniani bila hati yoyote anaweza asipate lolote.
Hali ile ya mawazo, hakuivumilia, siku moja akaamua kumuulizia mama yake, kuwa ni kweli aliyoyasikia siku ile, kuwa baba huyo sio baba yake wa kumzaa. Mama yake alishituka sana kusikia hivyo, karibu odondoke kwa shinikizo la damu, alipotulia akamsihi sana mwanae kwa kupinga katakata hayo madai, na kusema kuwa baba yake alimshuku tu kuwa anatembea na mtunza bustani, hata akamfukuza kazi kijana wa watu ambaye kazi yake kubwa, pamoja na nyingine ni kutunza bustani, …
‘Sasa ilikuwaje, mpaka akushuku, sidhani kama baba atayatamka maneno makali kama hayo, bila kuwa na dhana yenye ushahidi…mama naomba uniambie ukweli, kwasababau nisipojua ukweli nitaishi maisha ya mawazo na huwezi jua ya mbeleni…mama ilikuwaje, niamabie tafadhali…’ Maua akakazania kuulizia hata mama yake alipokataa kata kata kuwa hakuna haja ya kuongelea kitu kisicho na ukweli, lakini baadaye akaamua kusimulia baadhi ya maisha yake, hadi dhana hiyo kutokea.
`Mwananguu baba yako ana wivu sana, mimi nina tabia ya kuwa karibu sana na wafanyakazi wangu, awe mtunza bustani au mpishi, nawafanya kama watoto wangu, na nawaonea huruma katika maisha yao,…ilitokea huyu kijana kuwa karibu sana, kwasababu ya kazi zake…na tabia yake ya kujitolea kufanya kila kazi hata kama sio kazi aliyoajiriwa nayo, na alinijali sana..kutokana na..tabia yangu ya kulewa…!
Hata hivyo ukilinganisha na wafanyakazi wengine huyo mtunza bustani alikuwa katokea katika mazingira magumu na maisha yake yalikuwa ni ya taabu sana, hana baba wala mama, na hakuwahi kuwajua…basi nikawa nimemweka karibu sana na mimi, na hata wakati mwingine akiwa mgonjwa, namtembelea anapoishi, sio kwa yeye tu kwa nafanya hivyo kwa wafanyakazi wangu wote wa hapa...baba yako sijui aliwaza nini, kwani alianza kunihisi vibaya na mfanyakazi huyu, kwanini asiniwaze kwa wengine..sijui, labda matukio yaliyotokea baadaye ndiyo yalimwingiza kwenye dhana hiyo…’ Mama akasita kuongea na kumwangalia binti yake
‘Matukio gani mama…niambie au nitamuulizia baba yangu mwenyewe?’ akasema Maua. Na mama yake akamwambia asijaribu kumuulizia baba yake maswala kama hayo, kwani baba yake ana hasira zisizo na maana ndio maana tangu waoane, maisha yao yamekuwa yakukwaruzana, na hasa alipozaliwa yeye..
Unajua mwanangu, dhana ya baba yako kwa mtunza bustani haina ukweli, …ni moja ya chuki za baba yako, mimi ndiye mama, mimi ndiye ninaweza kujua wewe, kweli sio mtoto wake, …hisia zake tu..kuwa karibu na huyo kijana ndiyo ilizaa yote hayo…sio kweli. Ujauzito wako niliupata kwenye mazingira ambayo baba yako alikuwa analewa sana kwasababu ya mimi kuwa tunagombana sana na yeye…na tulikuwa hatulali kitanda kimoja.
Sikumbuki vyema ilikuwaje mapaka ikafikia hapo, kwani hata mimi muda huo nilishaanza tabia ya kunywa,…sikuwa na tabia hiyo kabla…yeye ndiye chanzo chakunifanya mimi niwe mlevi… na hata kulewa sana, na nikirudi mara nyingi huyo mtunza bustani ndiye ananisaidia kuniingiza ndani, kwani nalewa kiasi cha kutokujitambua nakumbuka siku moja nilikunywa pombe nikiwa nje ya bustani, nikanywa kisawasawa, hadi nikawa chakari…’ akasema akiwa anaongea kilevi. Maua alishamzoea mama yake, kuwa akitaka aongee basi anywe, kama hajanywa haongei, mkimiya..
‘Mwanangu sio kwamba nilipenda kunywa, bali taabu za ndoa, maisha yasiyo na raha kati yangu na baba yako, huwezi amini kuwa tangu baba yako anioe, sijui shughuli gani anazifanya, hanishirikishi kabisa, ana ile imani kuwa mke hana haki yakujua nini mume anafanya..sina haki hata ya …sijui nisemje mwanangu, ila hayo yaache tu, nisikutie katika simanzi sizizo faa…nakunya ili kuondoa mawazo, na hata huko kwenda kunywa nilikuwa najiiba, baadaye nikaamua kufanya wazi, akasema wee, akanipiga wee…akaona hina haja, akaniachia niendelee na ulevi wangu…basi ikawa hivyo..’ akasema huku anatafuta chupa ya kunyoagi ilipo. Maua alitaka kumwambia aache, kunywa, lakini alijua akifanya hivyo hatapata ukweli wakile anachokitaka, akanyamaza kimya.
‘Mwanangu, baba yako ni tajiri, lakini sisi sio matajiri,..hatuna raha ya utajiri wake, huo utajiri una maana gani,kujihusisha na mambo ya hatari tupu…hatari mwanangu, sijui kwanini niligundua yale…lakini hayo mwanangu sitaki kukuambia..nakunywa tu , na inabidi kufanya hivyo, kwasababu utajiri upo, lakini hakuna mapenzi, ninafugwa kama mfungwa,hakuna kutembea, hakuna…basi mwanangu mawazo hunijia kichwani kwa yale niliyobahatika kuyaona na huku kutojaliwa na..nakunywa tu, ..’ akasema mama huku anakunywa kweli.
`Sikumbuki kabisa mwanangu ilitokeaje kipindi siku au kipndi kile…kwasababu ndio nilikuwa pombe inanitoa akili kabisa..nikilewa nakuwa kama sio mimi…, baba yako anadai kuwa alipokuja alinikuta nimelewa sijijui, anadai alinikuta nikiwa nazini na huyo mtunza bustani, lakini mimi sikumbuki kabisa kufanya hilo tendo, na akadai sio mara ya kwanza, aliwahi kunikuta, lakini hakuwa moja kwamoja kama sfari hiyo…mimi sijui kama ni kweli kwani nikilewa huwa nakuwa sijitambui…na siku hiyo anavyodai alinikuta moja kwa moja tukufanya hilo tendo…hivi mwanangu kweli inawezekana nikazini na kijana yule…humjui vyema yule kijana, ni mwanifu na anaigopa kama mama yake…!
`Basi baba yako akaahidi kuwa lazima atamuua huyo mtunza bustani,…hataki kumuona kwenye nyumba yake tena, alishatoa amri afukuzwe, nikawa namng’ang’ania mimi, nikaona kuepusha shari ni heri aondoke, kwakweli iliniuma sana kwani nilikuwa namuonea sana huruma kijana wa watu, na kama lilitokea la kutokea, kama anavyodai baba yako mimi sikuwa najua, na makosa huenda ni ya kwangu,…na hilo halipo, sio kweli..ingawaje nilikuwa sijitambui, lakini nilikuwa bado nalinda heshima yangu ya ndoa,… sijui na sina uhakika.
‘Mimi ninachojua mwangu, baba yako alimuone wivu yule kijana kwasababu ya ile hali ya yeye kuwa karibu na mimi, hasa nikiwa katika hali ya huzuni, na alikuwa anajua kuniliwaza, nikawa …sijui niite kupenda,…kwani yale aliyokuwa akijitolea yula kijana ndiyo baba yako alitakiwa kuyafanya…sio kama anavyodhania yeye, ya kuvuka mpaka, hapana ile hali ya mume kuwa karibu na mkewe, haikutokea, kamwe kati yangu na baba yako…mimi na yule kijana haikuwa hivyo anavyodhania na haikuwahi kuingia akilini mwangu kufanya hivyo, katu na kamwe……
Alivyoahidi kuwa atamuua huyo kijana wa watu sikulala kabisa, kwani baba yako ana hasira na akiamua kitu ni lazima atakifanya, alisema kwasababu kagundua moja kwa moja tendo likifanyika , ambalo mimi sijui kuwa ni kweli, mtunza bustani hastahili kuishi tena. Atahakikisha amemtoa roho yake…niliogopa, nikamwambia yule kijana apotee, atokomee kabisa hapa jijini, lakini yule kijana alisema haendi popote, kwani Dar ndipo nyumbani, aatakwenda wapi, kama ni kufa siku imefika, yeye atakuwa kama sababu, basi akaondoka, nikampa vijisenti kidogo nilivyokuwa navyo…huwezi amini, mimi sistahili hata kuwa na pesa, nikitaka kitu nanunuliwa, lakini sio mimi nikanunua…eti nitalewea, nitalewea, mbona hata kabla alikuwa ahanipi hela!
Muda ukapita nikaona kumepoa, mara nikaihisi nina ujauzito, na ingawaje tulikuwa tunalala chumba tofauti mimi na baba yako, lakini zipo siku moja moja tulikuwa tunakutana na baba yako, lakini kwa tahadhari, na kukutana kwetu, ndio hivyo basi, tukiwa na hasira za hata kupigana… huishia kwingineko..’ hapa mama akacheka cheko la dharau, akachupa chupa na kumimina kinywaji chote kilichokuwa akimebakia, na kuitupa ile chupa pembeni.
‘Hii ndio starehe iliyobakia…kunywa, kunywa kwa kwenda mbele…sio kwamba napenda, basi tu….baba yako anadai eti hiyo mimba sio yak wake, toka lini kitanda kikazaa haramu…wewe, wewe mwangu,..mimi sio mjinga, nisijue nani kanipa mimba, nani mwingine wakati yeye ni mume wangu, na angejuaje kuwa mimba haijaingia, wakati yeye ….’ Akacheka sana, hata kutoa machzoi, halafu akamwangalia Maua kwa makini, akatoa machozi ya huzuni, halafu akamshika mkono na kumvutia kwake, akamkumbatia mwanae.
‘Mwanangu, najua nakutesa, najua hupendi hii hali, lakini wa kulaumiwa ni baba yako, naomba ukiolewa upate mume mwema, mtulie na umpende, mpendane,kama atakuwa hakupendi ni bora akueleze, ni bora ujua, na …naomba sana usome, ili usiwe na wasiwasi wa maisha…unanielewa, …maana wakati mwingine wanaume, wengine ahwajali wake zao wanawaona kama kitu…kama kitu, sio mtu, hawajui dini kabisaa..kwa ujumla, nakuhakikishia mwanangu mimba hiyo ni yakwake, ….yeye anadai siyo ya kwake, kwasababu mara nyingi kila mmoja yupo kwake. Ili kuondoa huo utata, nikamwambia basi tukapime, kama sio yake, niaondoka kwetu, akasema hawezi kwenda kujizalilisha, kwani kazalilika vyakutosha, ndani, na hapendi na kashifa hiyo itoke nje, halafu tena akapime, atamwaminije dakitari kujua nini kilitokea na kwanini tupime…na je hataweza kutoa hiyo siri…. Basi nikawa naishi kwa mashaka, nikiwa na mawazo sana
`Mwanangu, siku moja nimepumzika ndani, akaniita mlinzi kuwa nina mgeni, sikuwa napenda wageni, nikamwambia amwambie huy mgeni sipo, sitaki kuonana na mtu…lakini huyo mlinzi aakasema haraka kuwa huyo mgeni ni kijana aliyekuwa mtunza bustani…nilishituka, nikampita yule mlinzi na kutoka nje, na kukutna na huyo kijana, alikuwa kakua, sio yule kijana niliyekuwa nikimjua, kajizia kifua kama mwiinua vyuma, nikamwambia moja kwa moja aondoke nyumbani kwangu haraka.
‘Leo mama unanifukuza, umesahau fadhila, …sawa, lakini ukumbuke, mimi sikuomba niwe hivyo…ninachodai ni haki yangu, ukumbuke nilijitolea kufanya kazi kwa ajili yako…kwa kukuonea huruma, sasa nimeishiwa, sina pesa, nadaiwa kodo, sina kitu mama, naomba angalau kodi ya nyumba…halafu mama mkumbuke mimi nilikuwa naishi hapa, najua mengi sana hasa anayofanya baba, nimemwambia kama asipo nipa hela nilizomtajia nitatoa siri ambayo itamwangamiza, mama sikuenda nifanye hili, najua yeye ana uwezo zaidi yangu, najua kwa kumwambia hivyo atakimbilia kuniua…lakini ajue atakuwa kuvunja tawi, shina bado lipo…
`Mama naomba umwambia hili ninalodai sasa ni jasho langu, hicho kingine natimiza wajibu wa hawo …sio mimi ila nia kubwa ni kumfichia siri yake, kwani hawo jamaa wamepania,…walijua kuwa niliwahi kufanya kazi humu, wakanitesa na kuniweka sawa, mwisho wa siku niliwapa walichokitaka…skuwa na jinsi, wakanifunza ukomandoo..mama nakwambia wewe kwasababu nakujali nakuheshimu…wewe ni sawa na mama yangu’ yule kijana akafikia kunipigia magoti, nikamuone huruma sana…lakini maneno mengine aliyoongezea yakanitia kichefuchefu, kwa kuondokana na mambo mengine yasiyo nihusu nikamwambia nitafikisha uumbe aondoke, nakumkanya kuwa kama kajiunga na vikundi vibaya aachane navyo kwani anachotaka kufanya atakuwa kajipalia mkaa.
Akasema kuwa yeye ni kiumbe tu,…na swala la usalama wake halimtii wasiwasi kwani yeye anajiona kama mfu, hana baba , hana mama, na watu alionao hawatanii, kama asingefanya walichomwambia wangeshamua, hata hivyo yeye akifa hana mtu wa kumlilia, …haogopi tena…. ! Maneno yake niliona kweli kabadilika, na kweli kapania na kile kifua, inaonekana kaamua kuwa mshari, au kalazimishwa. Nikamwambia kuwa anavyojua mimi siwi na hela, nitajitahidi kumwambia mume wangu akirudi kesho yake. Akaniambia nifanye juhudi ya kumwambia na…halafu akanyamaza, kageuka na kuondoka, baada ya kunielekeza anapoishi kama nitazipata hizo hela.
‘Wewe njoo kesho, kwani shilingi ngapi hizo atakupa tu…’ nikamwambia
‘Shilingi ngapi,. ..mama wewe mwambia anajua nini kaagizwa, nyingine ni za kwangu, nyingine anajua yeye mwenyewe…’ akavaa mawani meusi aliyokuwa kayaweka mfukoni na kwa mendo wa haraka akapotea. Niliogopa sana, kuwa yule kijana mbona kabadilika, au kuna nini kimemtokea, nilimuonea huruma, kwani kama wamefikia huko, maisha yake yapo hatarini. Nilimuwaza sana, nikasema kama nitakuatana naye nitajaribu sana kumrudisha kimawazo, kwani ni yatima, nab ado anataka kuitia kwenye balaa…hapana, lazima nionane naye tena!
'Ujumbe nikaufikisha kwa mume wangu pindi tu alipofika,..aliposikia jina la mtunza bustani alishituka karibu animeze, aliniangalia kwa hasira..akafikiri sana baadaye, akatoa bulungutu la hela, sijui shilingi ngapi,…lakini zilikuwa nyingi, akazitia kwenye bahasha akasema nimpe huyo kijana akija, `kama atakuja tena mpe hiyo hela, mwambie sitaki kusikia kafika tena hapo mpe hela yake na atokomee mbali, … na mwambie kajipalia mkaa…kama bado mna mahusiano, basi ujua hana muda wa kuishi hapoa duniani…ok, usijali wewe mpe, wao siwanataka hela, mpe…ila ama zake ama zangu… ama zake, zangu haziwezi’ akasema mume wangu, ilikuwa kama nimemtonesha donda lililokuwa limepona, kwani alibadilika na akatembea huku na kule kabla ya kunipa hizo hela.
'Nilizipokea zile pesa kwa mashaka ni kuwaza kwanini kaamua kumpa huyo kijana pesa nyingi kiasi hicho, na utafikiri ilikuwa imeshapangwa kuwa atakuja na atalipwa kiasi gani, …nikasema labda ni dhana zangu tu, nikazichukua nikijua kuwa huyo mtunza bustani atakuja, kesho yake,…lakini moyoni…na kesho yake ikafika lakini huyo kijana hakutokea, nikawaza sana nifanye nini, na unajua baba yako alishampiga marufuku kabisa kuja hapo nyumbani, na mimi niliambiwa siku nikikutwa naye, tutasindikizana kuzimu.
Mama aliendelea kumuhadithia Maua mkasa wake na mtunza bustani akisema; `Nikawa siku nzima nawaza,...lakini, mwishowe nikamua kufanya jambo la hatari, sijui ilikuwaje mimi kwa huruma zangu nikaamua kwenda kwake kumpelekea hizo hela, niliwaza nifanyeje bila kujulikana. Nikaona nitumie zilezile mbinu zangu za kwenda kununua pombe, nikajibadili , huwa nikijibadili huwezi kunijua kuwa ni mimi, mara nyingi nampita mlinzi asijue kuwa ni mimi, …niliona nichukuea taksi huku nimevaa mawigi kupoteza sura yangu.
Huyu kijana alishaniambia wapi kahamia , kwahiyo nikafuta maelekezo yake, hadi nikafika, siunajua tena mataksi dereva wanajua kila mahali. Nilipofika eneo anapoishi, lipo ndani ndani…nikawakuta watu wamekaa nje, wanegina wakifanya biashara wengine, wakicheza karata…basi nikauliza kuwa huyo kijana yupo wakaniambia kalala ndani chumba chake ni cha mwisho…nikaelekea kwenye chumba chake.
Nikabisha hodo kimya, hodi kimya . kulikuwa hakuna dalili yoyote ya mtu kuwemo ndani, hakuna sauti wala…nikasikia sauti ya redio kwa mbali, nikawaza huenda ni jirani, …nikabisha hodo tena , nilipoona kimya nikawauliza wale majirani zake kuwa mbona kimya, wakanijibu kwa nyodo kuwa mbona wengine walikuja wakaulizia, na walipofika hapo walifungua mlango wakaingia,na baadaye wakatoka kwanini na mimi nisifanye hivyo kama mimi ni demu wake wa kweli…
‘Kama mimi ni demu wake?’ nikajiuliza kichwani, na kutaka kuwaambia kuwa mimi sio demu wake ni bosi wake, lakini nikasema niachane nao, nikabisha hodi tena mara tatu, …nikageuka kuwaangalia wale watu waliokaa pale , lakini hawakuwa na haja na mimi na shida zangu, wao walikuwa wakiendelea na shughuli zao na walionakena hawana habarikabisa na mimi, …nilpoona kimya nikaamua kuufungua mlango…, na malango ulikuwa haujafungwa na fungua, ukafunguka.’ Mama alipofika hapo akaanza kutoa machozi, nikawaza kuna nini kimlize mama, nikasubiri amalize
‘Sikuamini macho yangu mwanagu, nilichokikuta mle ndani, masikini najua baba yako...’ mara mlango ukafunguliwa kwa kasi ya ajabu, mama akakatisha maongezi, na sote tukageuza uso kuangali anani kaingia mlangoni, tulikuwa sote tunahema kwa woga
Sehemu hii inaishia hapa, hebu tuangalie sehemu ijayo ilikuwaje
Ni mimi: emu-three
6 comments :
safi sana m3 big up
Naona "toleo" la leo limeshiba haswa! Nimesoma weeee mpaka nikasahau kama itakatizwa at some point hehehe! Haya M3 mimi nipo...nani kawatokea mama na mwana...je baba ndiye kweli? Kama kawa mtu wangu..
You are back on track, hongera sana, yaani unasoma hutamani kisa kiishe, na hapa inaonyesha ulikaa mahala pemye utulivu ukaandika, hii sehemu inatupa picha halisi ya hiyo familia ilivyo, yaani kama namuona huyo mama na pombe zake na mawigi yake mtaani.
Subira
Candy1 kadaka nilichotaka kusema! Nipo!
hongera sana ndugu yangu simulizi zimetulia big up
Jamani, jamani maisha haya!! Sasa kama huyu baba ana mashaka kwa nini asikubaliane na mkewe na kupima ili ajue kweli.?? na kama ni kweli kwa nini mama asimwambie Maua kwani ni lazima atajua yupi ni baba. Swali langu kubwa Je? penzo lao kweli lilikuwa la dhati???
Post a Comment