Alikuwa dada mrembo, ambaye alivuta hisa za kila mtu, na kila aliyekuwepo mahali pale aligeuza shingo kumwangalia, lakini cha ajabu hakuwa na mawazo na mtu mwingine yoyote ila mimi tu. Akanisogelea kwa mwendo wa madaha, kama ule wa tausi , na kila hatua ilikuwa kama inachukua masaa kabla ya kupatikana kwa hatua nyingine, ubongoni, nilikuwa kama nimewekewa kipunguza mwendo, aliponikaribia akageuka kidogo kwa pozi kama wale warembo wa mitindo, na halafu akawa anagonga meno yake na sehemu ya ile miwani kabla hajatamka kitu, akatabasamu, tabasamu lile ambalo muda wote nilikuwa naliota, …
‘Maneno ndio wewe, hata siamini macho yangu, kwanini unajitesa hivi, ilihali nilishakuambia kuwa tuonane, …kuna shughuli kibao za kuzalisha na nilishakupangia mipango mingi, lakini yote ilikuwa inaishia kichwani mwangu…, mbona nakupigia simu hupatikani…’ alianza kusema huyo binti, huku akinikaribia, nami nikawa narudi kinyumenyume, hadi nikafika ukutani mwa nyumba ambapo nisingeweza kurudi tena nyuma, nikasimama, nikajiangalia …nikatamani nikimbie, lakini…
‘Maua naona sio muda muafaka wakuongea na wewe, unaniona nilivyo, nitakuchafua, …hapa sio mahali pako, namimi bado sijaweza kuwa wa aina yako, nakuomba uondoke, kwani bado nipo nahangaika, ipo siku nitakutafuta…tutaonana siku nyingine..’ nikasema huku nageuka kumtoroka, lakini alinishika mkono. Ilikuwa kama mtu kashikwa na barafu yenye umeme! Mikono yale laini utafikiri sio ya binadamu, ilinisismua mwili mzima, nikashikwa na butwaa, nikamgeukia naye akaniangalia machoni. Naye akayatuliza macho yake yakiangalia mboni za macho yangu…kwa dakika chache halafu yeye akaanza kuongea
‘Sikiliza Maneno, mimi msimamo wa urafiki wangu upo pale pale, sijali kuwa wewe upoje,…nilikupenda wewe, kama ulivyo, sikukupenda kuwa upon a hali gani…sikiliza maneno kama nilivyokuahidi kuwa nikipata kazi, nitakusaidia kwa namna yoyote ile, ili mwisho wa siku tuishi sote kama mke na mume….’ Akasema hayo maneno ambayo sikuyaamini, ina maana kweli msichana kama huyu atakubali kuishi na mume kama mimi, nisiye na mbele wala nyuma…hapana, huyu ananijaribu.
Nikageuza shingo na kuchungulia lile gari lake na kujaribu kuwaza, hivi kweli ninaweza kuishi na msichana mwenye uwezo wa kumiliki gari la kifahari kama lile, sijui kanunuliwa na wazazi wake, au mwenyewe au rafiki yake wa kiume...nikaingiwa na kumuhemuhe cha kutaka kugundua mle ndani kuna mtu au hakuna , pengine kamuacha rafiki yake ndani ya lile gari, na lilivyo huwezi kuona ndani, kwasababu viyoo vimewekewa kizuizi cha kuona ndani, nikajaribi kumuwaza mtu ambaye anaweza kuendana naye….
‘Usinitanie Maua, ..’ nikasema nakugeukia upande mwingine kumkwepa asiniangalia machoni, halafu nikageukia lile gari tena, nikajaribu kuchungulia kwa ndani kama nitaona mtu mle ndani lakini haikuwa rahisi kwasababu limewekewa kiambata cha kuzua mtu kuona ndani.
‘Hebu ingia ndani ya gari tukaongea sehemu muafaka…’ akanivutia ndani ya gari lake, nilijaribu kujizuia lakini haikuwezewezekana ikawa kama mbwa anayemfuata chatu, kwani hatima yake nikajikuta naingia ndani ya gari kwa mashaka , nikidhania nitamkuta mtu humo ndani lakini kulikwa hakuna mtu mwingine Nilijiona mchafu na ningeliweza kulichafua gari la watu lililojaa harufu ya manukato ya uzuri. Na yeye bila kusema neno akaondosha gari kwa mwendo wa kasi, na kuingia barabarani. Aliendesha gari tukiwa kimya hadi kwenye nyumba moja nzuri ambapo aliniambia kuwa ndipo anapoishi akasema nyumba hiyo ni moja ya nyumba za wazazi wake, na yeye kakabidhiwa kuishi.
‘Kama hutojali nyumba hii utakuwa ukiishi mimi na wewe…na nilishawaelezea wazazi wangu kuhusu wewe, wakasema nikutafute, nikikupata wapo radhi kabisa…unajuwa wazazi wangu wanajali sana uhuru wangu wapo tayari kunisaidia kwa vyovyote vile ili wanione nina raha…siwezi kusema wananidekeza, kwasababu mimi ni mkubwa najua kipi kizuri na kibaya, kwahiyo siwezi kuwadai kile chenye madhara, wewe ni tulizo la moyo wangu…Maneno naomba uniamini hivyo…’ sauti nyororo ilikuwa ikiongea sikioni mwangu na kinifanya niishiwe nguvu…oh, Maua akawa maua wa moyo wangu!
Basi ikawa ndio mwanzo wa kuishi na msichana huyo, na maisha yakaanza kubadilika, kwani nilikuwa sina tatizo tena la pesa za matumizi na mtaji wa biashara na hatimaye nikaanza kusoma. Nilisomea VETA, na hata kufikia hatua nzuri, tatizo lilikuwa sina bahati ya ajira, kila nikiomba kazi naahidiwa lakini sipati kazi. Na Maua aliniambia nisiwe na wasiwasi, kwasababu yeye ana kazi na mshahara anaopata unatutosha mimi na yeye. Nikalemaa, mimi nikawa nabangaiza hapa na pale na muda mwingi nipo nyumbani.
Kwasabau nipo nyumbani, nikawa kazi zote za nyumbani nafanya mimi, kupika, kuosha vyombo , kufua nk, kwangu mimi mwanzoni sikuona ni tatizo, lakini siku zilivyozidi kwenda , nikajikuta nakwazika, nakuwa mnyonge,na hasa ninapokutana na marafiki zangu huishia kunisimanga na kuniita kuwa mimi nimeolewa na pia ni mume bwege. Sikujali nikawa napuuzia ingawaje moyoni naumia, nakujiuliza hivi mimi nina kasoro gani!. Na nikiongea na mke wangu, yeye huniambia nisijali kwani ipo siku nitakuwa mtu wa …kama wanavyotaka wao!
‘Naogopa nikikutafutia msichana wa kutusaidia kazi utanizunguka, na …lakini kama unahitaji nitakutafutia, ila…naomba sana….’ Akasema huku ananisogelea, nikacheka na kumwambia sihitaji msichana wa kazi, hakuna kazi ya kumtafuta msaidizi..
Siku moja tukawa tumetoka na ilikuwa siku ya kutalii ufukweni, nikawa nimevaa nguo za kuogelea, napenda sana kuogelea, basi tukaanza kuogelea na kukimbizana huku na kule…ilikuwa raha ya aina yake,…baadaye tukawa tumekaa kwenye viti maalumu vya kulipia, nilijisikia sipo Tanzania,…nilikuwa katika dunia nyingine kabisa, ingawaje wakati mwingine akiliilinisuta kuwa hivi nani alitakiwa amfanyie mwenzake hivyo, mimi kama mume ndio nilitakiwa kubeba gharama zote, lakini eti mimi ndio nafanyiwa, nalipiwa…aah, lakini nani ajali, …hii ni zamu yake, ipo siku itakuwa zamu yangu, nikajipa moyo.
`Surprise, mpenzi..’ Maua akaja na kusimama mbele yangu halafu akatoa kiboksi kidogo, ambacho najua mara nyingi huwekwa vito vya thamani, na kabla sijaua nini kinatakiwa kufanyika, mara kiboksi kikafunguliwa na pete mbele za thamani zikaonekana.
Nilimtizama Maua nikashikwa na kutahayari, kwani nilimuona sasa kavuka mpaka, hii sasa ni kujipa udume, na mimi kuwa jike…sikukubalina na hilo, lakini kama nilivyosema awali nilikuwa kama goigoi fulani wa mapenzi, nikatabasamu, huku akilini nikiwaza kuwa mimi ndio nilitakiwa siku moja nimpe pete ya uchumba, leo imebadilika na kuwa kinyume chake. Nikageuka pembeni kwa aibu.
‘Sikiliza Maneno, najua jinsi gani unavyojisikia, lakini ukumbuke hakuna sehemu inayosema mume ndiye pekee anatakiwa kumtaka mke uchumba, hayo yametokea kwasababau asilimi akubwa ya wanaume ndio walijaliwa kuwa na hali nzuri, lakini inawezekana wanawake wakawa na hali nzuri, nami sioni kwanini usikubali hili, kama kweli unanipenda naomba uipokee pete hii, chukua boksi hili, uchomoe pete unavalishe kama ishara ya uchumba…’ akasema na kunikabidhi lile boksi, nami nikafanya kama alivyotaka, basi ikawa furaha, na hapo tukaahidiana kuoana karibuni,…
‘Nataka harusi ndogo, sitaki waje wageni wengi wakuniumbua..’ nikampa masharti
‘Wewe tu, vyovyote upendavyo,…’ akasema na kweli ikafanyika harusi ndogo, na nikampata mke, kwani wazazi wa Maua hawakuwa na pingamizi lolote. Basi niliishi naye kwenye nyumba yao, lakini sina kazi , mimi ndio baba wa nyumbani na mke wangu mfanyakazi. Na huku masimango ya mume bwege, mume aliyeolewa yakipamba moto… hata hivyo sikuyajali, niliwaona wao ndio mabwege na watu wenye wivu!
‘Jamani kwani kuna tatizo gani, mimi napendana na mke wangu, yeye kajaliwa kuwa na kazi, mimi ndio hiyo bahatii sina, …mnataka iweje, nimuache nikaishi shimoni Kariakooo tena…najua mnanionea wivu tu, sijali..’ nikawaambia huku moyoni naumia. Siku zikaenda na maisha yakawa raha kila leo zinakuja mpya, nikamezwa na mapenzi ya kitajiri na kujiona miongoni mwa tajiri, asiyevuja jasho, zaidi ya kazi ndogondogo za nyumbani, na wakati mwingine napiga madili makubwa ya kupata pesa…
‘Siku hizi kuna kazi za usiku, kwahiyo nitakuwa narudi jioni kidogo, ili kuangalia nini unahitaji, halafu ikifika saa mbili usiku naondoka, na huko ninaweza kulala au kama nikirudi inaweza ikawa usiku mbaya, kwahiyo naogopa kiusalama naweza kudhurika…’ akaniambi mke wangu. Mimi baba wa nyumbani sina cha kupinga, nikamwambia mke wangu ni vyema kiusalama asirudi usiku kama kuna sehemu ya kukaa mpaka asubuhi sio mbaya.
‘Ila naomba ujilinde maana ukiumia sijui nitaishije…’ nikasema na yeye akanikalia mapajani na kusema, nisiwe na wasiwasi, kwani atahakikisha akiwa hai siumii hata dakika moja. Basi ikawa imetoka hiyo, mke wangu akawa karibu kila siku anakwenda kazi za usiku, hata sikujali kuulizia kazi gani hizo za usiku , kila mara…
Siku moja wakati wa jioni hivi, likaja gari, na akatokea jamaa akajitambulisha kuwa ni mfanyakazi anapofanya kazi mke wangu, akasema kaleta barua muhimu sana, inatakiwa mke wangu aipitie na kuiidhinisha.
‘Mbona mke wangu yupo huko kazini!’ nikamwambia
‘Hapana yeye huondoka saa kumi, na harudi tena mpaka kesho yake…’ akasema yule dereva.
‘Harudi tena, mbona ana zamu za usiku..na ni muda mrefu sasa’ nikamwambia
‘Zamu za usiku! Hapana, labda kama ana kazi mahali kwingine, lakini nimjuavyo hana sehemu nyingine, , na kazi zetu hazina shughuli za usiku…labda kama nilivyosema awali kuwa labda anaweza akawa na kazi sehemu nyingine…’ akasema yule dereva, akiondoka, kwani sikujua wapi nimuelekeze, kwani hata simu nilipopiga ikawa haipatikani.
Kesho yake nikamuuliza mke wangu kuhusiana na maelezo ya yulee dereva, naye akasema huyo dereva hajui kitu, kwani kazi yake ni kuendesha magari…
`Atajuaje kazi za ofisini, wakati yeye ni dereva tu…usiyasikilize kabisa maneno kama hayo, au huniamini?.’ akasema mke wangu akiinuka kuelekea ndani, ilionekana wazi hakupendezewa na hayo mazunguzo. Nikaona nimemuuzi, nikamfuata huko chumbani na kumuomba msamaha, na mwisho wa siku nilikubaliana na mke wangu kwani nilimpenda na sikupenda tugombane kwa kitu kama hicho.
Hali iliendelea hivyohivyo, mke wangu kila siku anakuwa na zamu za usiku, mpaka nikaingiwa na wasiwasi, ikabidi nifuatilie kuwa kweli mke wangu ana kazi za usiku kihivyo, nikatafiti mpaka nikajua wapi mke wangu anapofanyia kazi, na nikagundua kuwa kazi kama hizo za usiku kwenye kmapuni yake hazipo,! Je ina maana mke wangu anasehemu nyingine anafanyia kazi, mbona hajaniambia kuwa anafanya kazi sehemu zaidi ya moja? Na nilipomuulizia mara ya kwanza alisema wazi kuwa hana sehemu nyingine anayofanyia kazi zaidi ya kampuni yake, …kwahiyo kuna jambo, kuna kazi nyingine isiyojulikana, au wapi mke wangu anakwenda? Nikawa na wasiwasi….nikaamua kuchunguza wapi mke wangu anakwenda na kulala huko huko, huku anasingizia kuwa ana kazi za usiku.
Naona niishie hapa ili tutafakari kwa pamoja, je huyu mke ana kazi gani za usiku na kwanini amfiche mume wake, je mume wake atafanya nini, na kutatokea nini
Ni mimi: emu-three
6 comments :
hapo ndo wanawake huwa tunakosea ku2tumia uwezo kunyanyasa patna kihisia... too bad.
Mhhh! kazi za usiku, amekuwa korokoroni huyu naye alilewa sana mapenzi mpaka uwezo wa kufikiri ulikuwa mdogo!
Kama alipenda maisha ya kujirusha na wengi ni kwani ajifunge kwa kuvalishana pete. Nadhani watu hukimbilia kuvalishana pete bila kuelewa maana ya kuvulishwa pete. Au ni tamaa ya fisi au pengine jeuri ya kuwa nazo. Je huyu mume alikuwa na mapenzi ya dhati kwa msichana zaidi ya kutekwa kwa uwezo wa kifedha!
salama? wadau tupo tunazungukia zungukia kusubiri uhondo.
M3 umenikumbusha mbali sana tena sana. Mi niseme nimeshakutwa na jambo kama hili lakini ilikuwa tofauti kidogo. Mi nilimpenda bwana mmoja sana na pia mafundisho ya alikutoa bikira ndo huyo huyo yalichangia sana mimi kunyanyaswa na huyu mheshimiwa. Mi ni mwalimu wa shule ya msingi nikampenda jamaa darasa la saba anafanya kazi ya kuuza vitu fulani kwa bosi mmoja hivi, kwavile yeye alikuwa ndo mwanaume wangu wa kwanza na sikutaka kuhangaika nikasema hamna neno kidogo tupatacho atasoma. Akaenda VETA akapata leseni tena class C. Mi hapo nyumbani ndo baba ndo mama, mzee anasoma... kumbe jamaa ameshapachika mimba mwanamke mwingine huko nje, hela anajifanya shule kinatakiwa hiki na kile. Bahati mbaya au nzuri nikaend ongeza ujuzi kidogo (diploma) huku nyuma yule mwanamke akahamishiwa kwangu, kumbuka hapo nimeenda diploma mshahara nimemuacha yeye. Shule imeisha yule binti akaondolewa, mshahara si nikachukua mwenyewe,matunzo tena hakuna, yule dada akaja kubagwa mtoto hapo, niko ndani nasikia mtoto analia nje kutoka hata sikuuliza, maana ni kopy right na binti yangu ambaye anafanana na baba ake mno... Niakchukua mtoto hawezi hata kutembea nikaingia nae ndani nikampa maziwa akalala. Baba ake anarudi anashangaa kuna kitoto kitandani, huyu nani, nikamwambia mfunue... kumuona alikaa chini, mi hata sikumfatilia nikaendelea na shughuli zangu, baada ya saa kama 5 hivi yule dada akarudi, analia anataka mtoto wake, unajua nilivyotoka nje kidogo nilie, huyo binti aliezaa nae nadhani atakuwa ndio amemaliza darasa la saba, mdogo, mwembamba, maziwa yamemvimba.... jamani, machozi yalinitoka. Kafukuzwa kwao arudi kumfuata mtoto. Eti mwanaume kwa kibesi kabisa anamwambia sikupi mtoot, mke wangu atamlea, wewe nenda tu..... Nikamwambia mpe mtoto kwa mama ake unataka tumlee sisi nenda kwa wazazi wake ukamchukue kwa utaratibu na kifupi mi sitamlea mpeleke kwa mama yako.
Hiki ni kisa kimoja kati ya vingi, mwisho akapata leseni yake akapata kazi, LOOOOH, nilikoma.... akiarudi nyumbani ni mara 3 kwa wiki na hapo ni kuanzia saa 9 usiku na kuendelea, siku nyingine anakuja kubadili nguo na kurudi kazini. Mpya alokuja kunipa ni pale sasa siku moja aliporudi nyumbani saa 6 mchana, hee hata mtoto alimuuliza baba unaumwa? Akashinda, akalala, tukaamka asubuhi...... yupo hana mpango wa kutoka... mmh machale yakanicheza, baba fulani vipi leo, aaa napumzika. Ok, ila ajabu ikogongwa hodi anakimbilia chumbani, mmmh? maswali yakawa mengi kichwani bila majibu........ kesho yake akaomba nimpe nauli aende kwao kusalimia, nikamwambai sina akasema tafuta, kopa iba ila lazima unipe hiyo hela. Nikamwambia kama hunambii ukweli sikupi hata shilingi, nikaenda ofisini kurudi majirani wanambia polisi walikuja kumtafua mume wangu, walipomkosa wakataka kujua nafanya kazi wapi waje waniulize maswali niseme mume wangu alipo........ Nikashtuka, nikabeba mwanangu mgongoni mpaka nyumbani kwetu, kufika nikahadithia mwanzo mwisho, kaka angu akaenda ofsisini kuuliza, jamaa kumbe kaiba hela nyingi kwa wakati huo haalfu ndo hivyo katoroka anatafutwa na polisi azirudishwe, asipopatiakna eti mimi niisaidie polisi kupatikana kwake. Hapo ndo nilipofunga virago, nikaihama hiyo nyumba mpaka hivi tunayoongea ni mwaka wa 8 sijamtia machoni huyo mwanaume. Mwanangu yupo form 1 sasa na haijatokea siku ameuliza baba yuko wapi. Ila ajabu nikikutana na rafiki zake anasema. Mwanamke ameninyanyasa sana yule kisa msomi.................! Poleni kwa gazeti lakini leo nimeona nitue huu mzigo. BEDANK
Nashukuruni wapenzi wa blog hii, kisa kinaendelea, lakini kuna shida ya mtandao tanguasubuhi kila nikijaribu kukiendeleza hiki kisa naishia kuambiwa `network haifanyi kazi...basi, lakini nitaweka sehemu ambayo ipo tayari.
Nakushukuru sana BEDANK,
HIVI NDIVYO NATAKA, WATU KUTOA ushuhuda, kwani tunayoandika hayatoki hewani, ni visa asilia, nakushukuru sana na pole sana, hata hivyo wewe ni jasiri sana, na mungu atakusaidia kwa uvumilivu na ujasiri wako!
Post a Comment