‘Wewe umekuja na nguo gani ofisini leo, hili sio vazi la ofisini…’ ilikuwa sauti ya meneja utawala. Nilijiangalia bila kuelewa ni kwanini niambiwe sio vazi la ofisini.
‘Kwani lina kosa gani, au sheria ipi imaesema nivae vazi gani, maana sio mara ya kwanza kuvaa hivi, na sio mimi tu mbona hawa mabosi wetu wa kizungu wanavaa hivihivi…’ nikajitetea.
‘Natumai barua ya kwanza ya kuvunja amri za ofisini utaituma kwa bosi wako huyo, unaona alivyovaa, kavunja amri zote zilizoko kichwani mwako, sasa hebu niambie kosa langu lipo wapi…?’
‘Wewe nishakuambia ofisi zina taratibu zake, na mimi ni meneja utawala, lazima uzitii, na niwajibu wangu kuhakikisha zinatimizwa `kwa walio chini yangu’ , umenielewa, sasa jilinganishe na hawo wazungu tuone siku nikikulima barua watakuja kukutetea…’ akaondoka.
Ni kipindi cha joto kwa kweli na watu wameshaanza kubadili mavazi na kuvaa nguo nyepesi , fulana na wengine vikaptula. Na hili maofisni linaanza kuijengeka, eti kwasababu wazungu wanavaa hivyo! Na hali kama hii inawapa shida mameneja utawala, na kuja juu, wanataka mtu ujikwide tai na suti , hapo hutasemwa. Lakini tai na suti kwa sisi tunaogombea daladala itakuwaje, ikizingatia kuwa ni kipindi cha joto? Nilijiuliza .
Haya ndio maisha yetu ya kiofisini, labda meneja wangu angeweza kunishinda kama mkurugenzi angekuja na vazi alilolitaka na angeishia kuwasifia wazungu kuwa wao wanajua utaratibu wa kiofisi, lakini kitu nilichokigundua katika ofisi yangu, wazungu hawana muda wa mavazi, labda itokee siku moja moja au kuna sherehe na wageni wakubwa waanakuja, …wao na kazi, vazi sio muhimu sana!
Katika wazo la siku ya leo ni kujaribu kuulizana, je kuna vazi rasimi la kiofisi, achilia mbali wale wenye sare kama kwenye majeshi na wale wanaotambulikana, na wale ambao kwa nia njema wameamua kuwa na sare za kikazi. Lakini wengineo sidhani kuwa kuna ulazima wa kuvaa kwa hicho kinachoitwa `vazi la kiofisi’ ambalo nashindwa kulijua kuwa ni lipi! Labda kampuni kama hii ingelitakiwa kuainisha katika mkataba wake kuwa vazi la kiofisi ni hili na lile, hapo tungekubaliana, na sheria hiyo ingewabana hata hawa wazungu, kwani tunawajua jinsi gani wanavyofuata sheria!
Lakini kwa kusema hivyo sina maana kuwa watu wavae kiajabu ajabu, na kujiamulia utakavyo, kwani mwisho wa siku watu watakuja na nguo za kulalia, wengine wanaweza hata kuja na nguo za ndani, kwani huo si uhuru wa mtu bwana! Hapana, nguo za ofisini kwangu mimi ni zile nguo za heshima, ambazo hazikiuki maadili mema, na inategeana kazi na wadhifa na mahali ulipo!
Au wenzangu mnasemaje ? Ni ipi nguo ya ofisini, je mumewahi kukutana na kisanga kama hiki au kusikia kuwa mtu kalimwaa barua kwa kuvaa nguo iliyoitwa `sio ya kiofisi’?
************
Nimewakilisha, na sasa twende kwenye kisa chetu cha usia wa mama!
mimi: emu-three
No comments :
Post a Comment