‘Nahisi labda rafiki yangu yupo matatani, au hata kama hayupo
matatani lakini naweza kukutana naye akaniambia ukweli kuhusu hiyo DNA, Je
matokeo yanasemaje..nitamuomba sana..ili nafsi yangu itulia…hata kama…
‘Na ni lazima nifanye lolote,kuonyesha utu, hata kama mtu
kakufanyia ubaya, lakini keshaniambia yupo matatani, hayo mawazo yaliuteka
ubongo wangu na sikuwa na sababu nyingine ya kuacha kwenda huko uwanja wa ndege....
Endelea na kisa chetu.....
********
Usiku una mitihani yake, japokuwa nilikuwa na nia ya kumsaidia
rafiki yangu, lakini moyoni, nilikuwa na mashaka ya usalama wangu, kiukweli
mimi sio mtu wa kuogopa ovyo, lakini wakati mwingine unahitajika kuwa na
tahadhari, kwani huwezi kujua wenzetu wamejiandaa vipi, ....
Wakati mwingine nikafika kujilaumu, kwanini sikumsikiliza docta,
rafiki wa mume wangu pale aliponisihi nisije nikaenda huko uwanja wa ndege, nahisi
kuna kitu wameona ambacho sio kizuri, kuna hatari, lakini hatari gani.Japokuwa
sikutaka kumwambia naenda wapi, lakini ingelikuwa vyema akajua,...
‘Nakufahamu sana unataka
kwenda huko uwanja wa ndege, ...usije ukafanya hayo makosa, mimi kama mtu
ninayekujali, nakukataza kabisa usiende huko....’akasema.
Kawaida yangu na huyu mtu, tunakutana, inakuwa hivyo, huwa
hatukubaliani kirahisi, yeye ananifahamu hivyo, na mimi namfahamu sana tabia
yake, mimi na yeye ni kama mafahali wawili, ...na sikupenda anione mimi sijui
ni nini ninchokifanya hata hivyo, nilishamfahamu kuwa mengine anayafanya ili
nimuone kuwa ananijali, au anafanya kuwarizisha wazazi wangu..sikupenda
kufanyiwa hivyo.
‘Hivi kwanini rafiki yangu alipofanyiwa hivyo, hakuwapigia simu
polis, lakini yeye ni mpiganaji anafahamu lipi jema, siwezi kumlaumu hasa
inapofikia kwenye familia yako…’nikasema kimoyo
‘Hao watu sio mchezo, ikibidi kufanya unyama wanafanya, wakijua
wana watu wa kuwalinda, kwahiyo uwe makini sana nao…’hiyo ilikuwa moja ya kauli
za docta akinitahadharisha.
‘Mimi sijaona uhatari wao…’nikasema na nilisema hivyo, kutokana na
kauli ya docta, yeye kaona kuwa watu hao wanafanya hivyo huenda kwa vile wana watu
ambao wanaweza kucheza na vifungu vya sheria na kufanya wapendavyo, na pia labda
ni kwa vile wana mtu mkubwa wanayemtegemea..’nilijikuta naongea peke yangu
kwenye gari.
Safari ya kwenda uwanja wa ndege inaweza ikakufanya hivyo,
ukaongea peke yako, ukawaza mengi, na kama huna mtu, utawaza na kuwazua peke
yako, na vinginevyo, ukutane na madereva wa daladala, mtukanane,…yaani ukifika
sehemu unayokwenda, kama umefika salama ushukuru mungu, ni mtihani kwa kweli.
‘Je kama nikutana na hao watu , na wana silaha, nitawezaje kujihami,
kama sina silaha..’nikajiuliza, hivi kwanini sikuchukua bastola yangu kwa ajili
ya kujihami, ili wakinitishia na silaha na mimi nawaonyesha kuwa nina silaha na
pia naweza kuitumia…oh, sasa nifanye nini, nirudi, hapana siwezi kuwahi, …hapana,
siwezi kurudi…’ nikawa naongea huku gari linakwenda
.
Niliona kuwa kama nitakwenda nyumbani kuifuata hiyo silaha yangu,
nitakuwa nimechelewa sana. Haitakuwa na maana tena, …
‘Hamna shida ngoja niende huko huko, sio lazima nipambane nao kwa
silaha, hata hivyo sizani kama kutakuwa na haja ya kutumia silaha, ikibidi,
nitatafuta njia nyingine...pale kuna kituo cha jeshi, nitafanya lolote wajue
kuwa nipo kwenye hatari, ila tatizo ni usiku…hata sijui, mungu nisaidie tu....’nikasema
Nilipokaribia uwanja wa ndege, nikampiga simu ya rafiki yangu,
tena na tena lakini simu yake ilikuwa haipatikani.
Labda atakuwa keshaingia uwanja
wa ndege, au …labda watu hao bado wamemshikilia,..lakini kwanini waendelee
kumshikilia, kuna ni nini hajawatimizia,…mmh, ngoja niwapigie watu wangu kujua
kinachoendelea..’nikasema na kuwapigia watu wangu.
‘Hatujampata mpaka sasa hivi, hata uwanja wa ndege hayupo,
hajaingia kabisa …’wakasema
‘Muna uhakia, basi Ina maana labda bado wamemshikilia sehemu..?’
nikauliza
‘Yawezekana, maana kwa mara ya mwisho kuna kitu walikuwa
hawajaelewana, kukatokea kitu kama vurugu, baada ya hapo mdada akatoweka, na
wale watu aliokuwa nao, wakawa wanamtafuta…hadi sasa huyo mdada hajaonekana yeye
au mtoto wake, na wale watu bado wanamtafuta…’wakasema
‘Basi yupo kwenye wakati mgumu angalau angelinipigia, nikajua
nimsaidie vipi au ndio keshanizarau……sijui nitampataje sasa..’nikasema
‘Madam, tuachie hilo, tutampata tu…’watu wangu wakasema na mimi
hadi hapo nilikuwa sijawajulisha kuwa nipo njiani nakuja huko huko, nilitaka
hilo lisijulikane mpaka nifike maeneo ya hapo.
‘Mtoto wangu aliibiwa…,
wakati nipo bafuni naoga, walifika watu nisiowafahamu, wakamchukua mtoto
wangu..nilichanganyikiwa…,lakini baadaye wakanipigia simu, kuwa kama namtaka
mtoto wangu, akiwa hai basi nifanye wanavyotaka wao, nikawaulize nifanye
nini...’
Nilikuwa najaribu kuyakariri maneno
yake kuona kama kuna uwalakini wa udanganyifu, lakini niliona huenda ni kweli…..
*********
Nilishafika maeneo ya uwanja wa ndege sasa, nikawa najiuliza
niingie ndani moja kwa moja au…nikaona niwapigia watu wangu tena kuhakiki bado
wakaendelea kusema kuwa hawajamuona, hajaonekan ndani ya uwanja wa ndege, na muda
wa watu kuingia kwa ajili ya ndege anayoondoka nayo umeshafika..na bado
haonekani.
‘Inawezekana kaahirisha safari yake…?’ nikauliza
‘Hapana, tumelichunguza hilo, hajaahirisha bado…’wakasema
Nikawa sasa nimefika sehemu niamua kuingia ndani ya uwanja wa
ndege au …kwa mbele nikaliona lile jengo nililoambiwa kuwa Makabrasha ana ofisi
zake humo ndani,..kumbe unaweza kuliona bila kupata shida.
Baada ya kuliona hilo jengo
tu, akili yangu ikanituma nifike kwanza kwenye HILO jengo, kwani huko ndani ya
uwanja wa ndege wapo watu wangu wanafuatilia, aanglionekana kama alikuwa
keshaingia huko, basi bado atakuwa kashikiliwa sehemu na sehemu ninayoishuku
mimi ni kwenye hilo jengo.
‘Au watakuwa sehemu gani nyingine…hawa watu wangu kama wamemtafuta
kila mahali hajapatikana, basi…hapana ngoja nikahakikishe mwenyewe..’nikasema
Nikawa sasa nimefika eneo la hilo jengo, ni jengo kubwa la ghorofa
tatu…na ukiliangalia kwa mbali ni kama halijamalizika kujengwa, lakini nilipofika
sehemu yenyewe nilikuta shughuli zinaendelea kama kawaida,
Sehemu kubwa ya chini
imechukuliwa na waendesha biashara za vinywaji, kwahiyo kwa wakati huo watu
walikuwa wamekaa kwenye viti vilivyopangwa kwenye miti iliyopandwa kwenye
bustani ya eno hilo, wakinywa, na mziki ulikuwa ukipigwa....
Mimi nilipoingia eneo hilo na gari langu, wakaja wapokezi,
wakinikaribisha kwa bashasha, huku wakinielekeza sehemu ya kuegesha gari langu,
nami nikafanya hivyo, na kutoka nje ya gari, na wale wahudumu, wakaendelea
kuonyesha ukarimu wao, inaonekana walisomea hiyo kazi, kwani walijua jinsi gani
ya kumkaribisha mgeni, mpaka unavutiwa ..
‘Unakaribishwa mgeni, hapa kuna huduma mbalimbali, kuna vinywaji,
kuna chakula, au kama unahitaji kumpumzika kuna sehemu ya kupumzika, vipo
vyumba, na huduma nyingine ...’nikashangaa, maana sikujua kuwa jengo hilo lina
mambo yote hayo. Kiukweli lilikuwa limekamilia kama jengo la ofisi, burdani na
vyumba vya wageni.
‘Kwani hapa kuna vyumba vya ofisi na hata vyumba vya kulala
wageni?’ nikauliza
‘Ndio vipo vingi tu, vyumba vya wageni vipo juu na chini, ni wewe
tu, unahitaji chumba, kwa muda gani je upo peke yako?’ wakaniuliza.
‘Hapana sihitaji chumba, mimi nataka kumuona mtu fulani…sijui kama
ninaweza kumpata humu mmh, sasa ni saa mmh…?’ nikauliza nikijifanya kujibaragua
hivyo, kwani sikuwa na uhakika nisemeje, maana nilitakiwa niwe na tahadhari.
Hizi kazi za watu, hizi zilimfaa rafiki yangu, sio mimi mtu wa ofisini.
‘Ni mtu gani huyo je ana ofisi hapa, au mteja wa mara kwa mara
hapa, tunaweza kukusaidia kumpata…?’ akaniuliza
‘Ndio anaitwa Makabrasha...’nikasema
‘Oh,…kumbe ni muheshimiwa,…mhh, ulikuwa na ahadi naye..?’
akaniuliza
‘Ndio…’nikadanganya hivyo.
‘Basi itabidi uingie sehemu ya ndani, sehemu ya mapokezi, huko
ndani watakuelekeza, sisi huku tunashughulika na wateja wan je, na ofisi za
chini, karibu sana…’akasema
‘Ahsante,….’nikasema
‘Lakini naona ajabu, muda kama huu, mara nyingi, anakuwa huku
chini, anapenda sana kujichanganya na
watu, sasa sijui kwanini hajateremka, na leo siku nzima sijamuona huwa ni
rafiki yangu akija hapa lazima tuongee na kutaniana…’akasema
‘Oh kumbe, kwahiyo labda ana wageni, ni mwanamke na mtoto au…?’
nikauliza
‘Yeye kila mara ni mtu wa wageni..ofisini kwake kama huna miadi
naye sio rahisi kumpata analindwa utafikiri muheshimiwa gani vile, sikumbuki
kumuona huyo mtu mwanamke na mtoto, hata..labda maana sio muda wote ninakuwa
hapa, mimi nimeingia jioni hii …’akasema
‘Ok…ngoja nikaonane naye tu nitajua huko mbele kwa mbele…’nikasema
‘Sawa…;lakini sio kawaida yake..kutokuonekana huku chini…, nahisi
ana kazi nyingi....ingia ndani watakuelekeza ofisini kwake, karibu
sana...’akasema huyo mpokeaji wageni.
‘Nashukuru hamna shida, na gari langu naweza kuacha hapa… , hapa
kuna usalama....?’nikauliza
‘Aah , ndio hakuna shaka, ila kama unahitaji ulinzi binafsi
inabidi ulipie pale, kwa yule mlinzi, vinginevyo, liache hapo hapo, ..’akaniambia
Na mimi kwa vile sikujua nitakaa huko ndani kwa muda gani, nikaona
ni bora nipate hiyo huduma ya ulinzi binafsi, nikaenda kwa yule mlinzi,
nikaandikisha, na kulipia. Baada ya hapo nikaingia ndani..
Sikutegemea sehemu ya ndani imejengwa kiofisi kweli, kuna sehemu
nzuri za kusubiria wageni, runinga, na vyumba vya huduma za vinywaji…na kulikuwa
na wahudumu kutegemeana na ofisi unayokwenda.
Haraka nikaenda kwa muhudumu nikamuelezea shida yangu, na
nilipomtaja huyo Makabrasha, akanielekeza kwa askari mmoja…
‘Yule ndiye mtu wake…’akaniambia
Nikamsogelea huyo askari, alikuwa kakaa na mbele yake kuna meza, na
kitabu kikubwa, alikuwa anasinzia, na aliponiona akasimama na kunikaribisha,
nikamuelezea shida yangu.
‘Oh, kwa muda kama huu, mara nyingi huwa hataki wageni, ....lakini
mmh, ngoja, maana alisema hataki
usumbufu, …alikuwa na wageni muhimu…mmh, sijawaona wakitoka,…eeh, ok,…unasema
una miadi na yeye, jina lako,..maana natakiwa kumpigia simu kuhakiki...’akachukua
simu yake na kupiga, ikawa inaita tu, akaniangalia, na kusema;
‘Unaona hataki hata kupokea simu, tafadhali hebu wewe nenda,….si
umesema una miadi naye au sio…basi nenda, maana muda umekwenda, ukifika rosheni
ya pili, upande wa kushito utaona ofisi yake, na maandishi ya ofisi yake sio
sehemu yenye utata,…lakini samahani, natakiwa nikukague kama huna silaha yoyote
ni kawaida usijali..’akasema akinipitishia mashine ya kukagua, na aliporizika
akasema
‘Ok, sasa unaweza kwenda...’akasema hata bila ya kunipa muda wa
kumuuliza nilichotaka kumuuliza, …
na mimi hapo nikawa huru, hata kama nitachukua muda mrefu huko
ninapokwenda, kwani yaonyesha kuna utaratibu mnzuri wa usalama, kuanzia nje
hadi ndani…
Nikaelekea kwenye ngazi za kupanda, juu, ..jengo halikuwa na lifti…ni
mwendo wa zoezi, sikujali hilo, maana
hata mimi ni mtu wa mazoezi.
Nilipoanza kupanda ngazi ya kwanza simu yangu ikaita, nikaangalia
ni nani mpigaji, nikaona ni docta rafiki wa mume wangu, sikutaka kuipokea simu
yake kwa muda huo, nikaikata, na kuanza safari ya kwenda juu, huku nikiwa na
mawazo mengi mengi kichwani.
‘Hivi haya aliyoniambia docta rafiki wa mume wangu kuwa wakili
huyu ni jasusi fulani inaweza kuwa ni kweli..na kwanini mume wangu akamchukua
mtu kama huyu, nataka nikikutana naye nimuulize kuhusu huo mkataba na mume
wangu, mimi kama mke wa mteja wake nina haki ya kufahamu hilo.
‘Hata hivyo muhimu wangu ni kuhakikisha kama rafiki yangu hayupo
naye huko, …’nikasema huku nikiangalia saa, na kwa muda huo kama ni wasafiri wa
kuondoka, watakuwa wameshaingia ndani, ..sijui kama huyu rafiki yangu ataweza
kusafiri leo..au …yupo matatani.’nikawa naongea kimoyo moyo.
Wakati natembea sasa kupandisha
ngazi ya mwisho ili nifike eneo la ghrofa iliyopo hiyo ofisi …ya makabrasha,
mara akatokea mtu akiwa na haraka, karibu anipige kikumbo kwa jinsi alivyokuwa
na haraka, ni kama anakimbia, alikuwa kavaa kofia kubwa, kiasi kwamba huwezi
kuona sura yake, mpaka, ainue kichwa kidogo.
Yule mtu aliponiona, kwanza aliinua kichwa ili aweze kuniangalia
usoni, ni kama kashtuka kuniona na alitaka kuhakiki, akainua kichwa kuniangalia
vyema…akataka kuongea jambo… akasita, kama anataka kuniongelesha, lakini akasita,
na kunipita kwa haraka na kukimbilia chini, mimi sikumjali nikaendelea na
safari yangu ya kwenda juu.
‘Huyu mtu ni nani, mbona anakuwa kama ana mashaka…’ nikajiuliza na
hapo nikaanza kuingiwa na mimi na wasiwasi, kiujumla kulikuwa kumetulia maana
muda huo ofisi nyingi zilikuwa zimefungwa.
‘Huyu wakili yaonekana sio mtu wa kawaida mpaka anaweka walinzi wa
kukagua watu, lakini labda ni mlinzi wa ofisi zote za huku juu..na ofisi nyingi
zimefungwa yeye bado yupo kazini…’nikasema
‘Ni lazima nikaongee naye, nitapambana naye uso kwa uso,
atashangaaa kuniona muda kama huu..’nikasema kimoyo moyo. Na nilijipa matumaini
kuwa hawezi kunifanya lolote, kwa jinsi walivyoweka taratibu zao, mtu
anayeingia anajulikana na akitoka
halikadhalika
Hata hivyo kutokana na familia yangu watu wengi wakisikia kuwa
mimi ni mtoto wa , basi kuna kuogopwa au kuheshimiwa kwa namna fulani, baba
yangu alikuwa na umaarufu fulani hivi…kwahiyo sihitajiki kuwa na mashaka..hata
hivyo moyo wa mashaka bado nilikuwa nao..
Sasa kiusalama nikaamua niwapigia watu wangu niwaambia kuwa nipo
sehemu hizo wakaribia hapo kama lolote likitokea,..nilishangaa kuona simu yangu
haina mawasilinai mtandao haushiki…, hii ni kuashiria kuwa eneo hilo, wameweka
vitu vya kuzuia mawasiliano, sasa wao wakitaka kupiga simu nje inakuwaje.
Nikaona haina shaka nisipoteze muda, nikatembe akwa haraka haraka , maana sasa
nilikuwa kwenye korido,.. sehemu ile ya kutembea ili uitafuta ofisi ya huyo
muheshimiwa,..hapo nikajiwa na mawazo, nikimuwazia mume wangu, jinsi gani alivyotekwa
kimawazo na huyu mtu hadi akukubali kuwa huyu jamaa awe ni wakili wake.
‘Hii inaashiria kuwa mume wangu kafanya makosa, na sasa anajihami,
sasa kafanya hivyo ili kujitetea, kwa vile anafahamu fika kosa alilolifanya
litamfanya akose kila kitu, na kiukweli mimi sitaweza kukubali, ni lazima
sheria ifanye kazi yake.
‘Lakini kafanya kosa gani, ..la uzinzi au….kavunja miiko ya ndoa,
hahaha, kama hilo sitaweza kumsamehe kamwe..anafahamu hilo kabisa, sasa kama
alifahamu hivyo kwanini akafanya hivyo…na kinachotakiwa ni ushahidi, na ushahidi
mnzuri ni huo wa mtoto, kumbe ndio maana,….
‘Na baya zaidi kama wanavyodai watu , kama ni kweli kuwa katembea
na rafiki yangu…mbona nitaumia sana, …hapana..hili
sitawasamehe kabisa, ni lazima nifanye jambo, ni lazima nimuonyeshe baba yangu
kuwa ninaweza kushika hatamu zake…’nikasema
‘Kwa vyovyote iwavyo, …mume wangu ana makosa, na kama alitembea na
rafiki yangu, basi wote wamenisaliti,..na bahati nimkute …kwanza nitamuokoa na
hao watu, lakini la pili ni lazima akapambane na adhabu ambayo hataweza kuishau
maishani, hataamini kuwa mimi ndio yule rafiki yake..’nikasema
Nilikumbuka kuwa mikataba imebadilishwa, kwahiyo sitaweza kuchuku
hatua yoyote kwa sasa, hasa kwa mume wangu maana ndio maana pale kwenye ule mkataba
waliandika kuwa:
`....mume ndiye atakuwa na mamlaka ya mali yote, na maamuzi
yote.....’ thubutu, mali yangu mwenyewe, mtu aje aniamulie..hilo halikubaliki,
tutapambana hadi tone la mwisho, na ikibidi, nitachukua hatua ambayo watu
hawataamini kuwa ndio mimi, mtoto wa muheshimiwa baba.
‘Na huyu rafiki yangu nitamfanya nini..maana nsipomfanya kitu kwa
hivi sasa hataniheshimu kamwe, ooh, lazima kila nilichopanga na yeye kimkute,
haijaslishi yeye ni ni rafiki yangu...’nikasita hapo kidogo nikiwazia adhabu
yake.
‘Lakini....’hapo nikatulia kidogo..
‘Ushaidi upo…mtoto anafanana na nani…na mume wangu, kwahiyo…lakini
cha muhimu ni hicho kipimo, cha DNA, nikikipata tu, basi…na lazima watakuwa
wamempatia huyo wakili kama wameamua kuandikishana kisheria…
‘Na kuna ushahidi wa DNA,
unaonyesha kuwa huyo mtoto sio wa mume wako ni wa mtu mwingine ambaye
hajatambulikana…’ nikakumbuka maneno ya docta
Kwa vyovyote iwavyo, mume
wangu kanisaliti,..kawahi kutembea na rafiki yangu vinginevyo asingelikuwa na
mashaka hayo, hata kama sio mtoto wake, ..kwanini akawa najihami, hapo hata
iwavyo, bado anastahiki adhabu kubwa, …
‘Na huyu rafiki yangu kama kweli hajaondoka, kaahirisha safari,
basi…nitamuonyesha kuwa mimi ni nani…kuja kwake atakujutia, ni lazima apambane
na kile nilichokiahidi…
Nilipowaza hivyo nikachukua simu yangu ..nikaanza kuipiga huku
natembea mwendo wa kawaida, simu hazitoki, basi nikaona niandike ujumbe wa
maneno;
‘Mimi ni yule dada niliyekuambia unitafutie wale mabaunsa wa ile
kazi, ...nitakuarifu pindi, ..ndio, kuna dada mmoja, kama nikithibitisha
kafanya hivyo, nataka tumfunze adabu, ...kabisa kabisa, waweke tayari tayari,
nitakuambia yupo wapi, wewe subiria simu yangu.....’nikaandika hivyo na kuutuma
huo ujumbe.
Mara nikasikia king’ora cha polisi kikisikika kwa mbali sana…
‘King’ora cha polisi, kuna nini
tena usiku huu, oh na muda umekwenda, huyu rafiki yangu sio muendaji
tena, ngoja, nitamuokoa, lakini usiku huu huu atakipata cha moto…’nikasema
King’ora cha polis kikanikumbusha yule mtu niliyekutana naye akikimbia.
‘Nahisi kuna hatari, kwanini nisirudi tu huko nilipotoka..mbona
moyo wangu unakuwa na mashaka…’nikajiuliza lakini sikutaka kushindwa, sikurudi nyuma,
nikajikakamua, na kuendelea kutembea
Na kwa muda huo king’ora kilikuwa wazi ni cha polisi, nikasimama
kidogo kusikilizia, kuhakiki, kama king’ora hicho kilikuwa kikitokea mjini, au
njia ya kutokea Gongolamboto, sikuweza kukisia vyema, maana kulikuwa na sauti
kubwa ya mziki. Nikajipa moyo kuwa huenda hawo askari watakuwa na safari
zao,...
Nikawa nimeshafika eneo nililoeleekezwa,na nilipotupa macho
kushoto, nikaona kwenye mlango, maandishi, `WAKILI WA KUJITEGEMEA, MH.
MAKABRASHA..
‘Mr. Mkabrasha...’nikasema kwa sauti ndogo, huku nikitabasamu.
Nikatulia kidogo, maana sasa huenda naingia kwenye matatizo, na
nisipokuwa muangalifu ninaweza kuhatarisha maisha yangu, japokuwa watu wengi walioniona
na watakuwa mashahidi wangu, kama likitokea lolote, lakini kama wataniua je,
itasaidia nini hapo
Hata hivyo siwezi kujiaminisha sana, kuwa kuna watu wameniona
nikipanda juu, kwani watu wote hawo wanaweza kuwa watu wake...wakamtetea yeye.Kwahiyo
sasa nifanye nini, na mimi nimeshafika hapo…
Kwanza nikavaa soksi za mikononi, maana ukiwa unakwenda sehemu
zenye mashaka, ni vyema ujenga tabia ya kujihami, na mimi tabia hiyo nimekuwa
nayo mara nyingi, hasa unapokwenda sehemu unazohisi kuwa zinaweza kuwa na
hatari ni vyema pia ukajihami na alama za mikononi, lolote linaweza kutokea.
Kwa haraka, ..nikazitoa soksi za kinga za mikono nilikuwa nazo kwenye
mkoba wangu, Mara nayingi nakuwa na hizi soksi kwenye mkoba wangu.
Na nilipohakikisha nimezivaa , ni kitendo cha haraka hapo,
japokuwa moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio.
Nikauendea huo mlango, ulioandikwa jina la huyo muheshimiwa,
nikajaribu kusikiliza kama kuna sauti yoyote inatokea ndani, lakini kulikuwa
kimiya, kimiya kabisa,unachoweza kusikilia kwa mbali ni hizo sauti za ving’ora
na mziki toka chini,....nikaona nispoteze muda, nikaugonga huo mlango mara
tatu...kimiya, mara nyingine tatu kimiya
Mwili ukaanza kujenga hisia nyingine, nywele zikaanza
kunisisimuka, nikawa nahisi uwoga fulani,....nikakumbuka wale watu chini,
waliniambia kuwa huyo muheshimiwa yupo juu, kwenye ofisi yake, kwanini nagonga
mlango wake mara nyingi, bila ya yeye kutokea au hata mtu mwingine kuja
kunifungulia mlango, nikagonga tena na tena kimiya..
Nikaona isiwe taabu nikashika kitasa cha mlango nikakizungusha
taratibu, nikaona mlango unafunguka...nikausukuma polepole, ukafunguka kiasi
cha mimi kupita, nikaona hapana, nikausukuma, ukafunguka kwa mapana, kiasi cha
kuona ndani, nikaona kwe mbele sehemu ya mapokezi, ..kumbe ni ofisi kubwa tu,
nikaangalia nje kama kuna mtu anakuja ...hakuna, nikaingia ndani.
Na wakati huo vile ving’ora vya polisi, vilikuwa vimeshafika eneo
karibu na hilo jengo ni kama vile wanakuja eneo hili, nikaona afadhali, kama
rafiki yangu yupo matatani, nitapata wasaidizi, nikapata nguvu, nikaingia
ndani, na kuangalia huku na kule nikaona mlango mmoja umeandikwa:
OFISI YA WAKILI..., nikaangalia saa yangu ilikuwa saa mbili na
nusu, nikausogelea ule mlango, nikagonga,...kimya nikagonga tena,
kimiya....mara simu yangu ikaita, nikaizima bila kuangalia mpigaji, nikashika
kitasa na kufungua mlango, mlango ukafunguka....
Kwanza nilisimama huku nikiangaza macho kukagua hicho chumba na
kama kuna usalama,, ilikuwa ni ofisi nzuri tu, ikiwa na kila kitu kinchoweza
kupatikana kwenye ofisi za mawakili,na macho yangu yakaenda moja kwa moja
kwenye meza, niliona mtu kakaa huku kalala kwenye meza.
‘Mhh, huyu jamaa kalewa mpaka kalala kwenye meza..ni kawaida yake
nini..’nikajisema hivyo.
Alikuwa kalala kichwa kakiweka mezani, lakini ulalaji ule sio wa
kawaida, ni kama mtu kalazimishwa, na macho yangu yakatua pembeni yake, nikaona
nakala za mikataba, na mmoja kati ya hizo nakala za ni ule mikataba wangu ...
nahisi ni ule waliyotengeneza wao,
lakini jamaa anaonekana hajitambui, labda kalewa sana, au ni usingizi gani
huo..
Hasira zikanipanda, nilitaka nifike kwa huyu mtu nimuinue nimsuke
suke, nikifahamu kuwa kalewa, hatakuwa na ubavu wa kupambana na mimi,...na hapo
inaonekana kanywa hadi kapitiliza maana pembeni kwake kulikuwa na chupa kubwa
ya kinywaji cha pombe kali, na gilasi mbili,....kuonyesha kuwa hakuwa peke
yake, nikaachia mlango, na kusogea kuingia ndani, huku king’ora cha polisi
kikisikika kwa nguvu, kuashiria kuwa sasa askari wapo chini ya hili jengo.
Hata hivyo, akilini mwangu nilikuwa na mashaka, nikijiuliza hawo
maaskari wamefuata nini hapo...kusije kuwa kuna matatizo.....nikaona nimalizane
na kilichonileta, kwanza nikasogea hadi pale kwenye meza, kwa haraka nikauchuku
aule mkataba na kuukagua…ni nakala ya mkataba wangu, ..
‘Nahisi walikuwa wakiufanyia kazi…’nikasema kimoyo moyo
‘Sasa walikuwa na nani, …?’ Pale mezani kuna gilasi mbili, na zote
zipo nusu… kuashiria hawa watu walikuwa wanaongea, alikuwa na mtu mwingine,.
Nikaone nisipoteze muda, nikaona nimuamushe huyu mtu nimuulize
rafiki yangu yupo wapi, na kwanini, kaingilia maswala ya familia yangu kwa
kuharibu mkataba wangu na mume wangu,...nilipofikia hapo kimawazo sikujali mambo
ya polisi, nikasogea upande ule aliokaa huyo jamaa ili kukabiliana naye....
Ni wakati huo huo, nasogea na mara macho yangu yakatua pale
alipolala huyo jamaa, nikaona kitu kilichonishitua, nikaganda, nikarudi kinyume
nyume na kugonga ukuta, nikafanya vitu vilivyokuwa nyuma kwenye kimeza kidogo
kudondoka,..ule mlio wa kudondoka hivyo vitu ukanishtua
Kwa haraka , nikashika mdomo,...kujizuia,..lakini haikuwezekana,
nikajikuta nimepiga yowe, unafahamu yowe, sijawahi kupiga yowe kama hilo....na
mara nikasikia mlango wa hiyo ofisi ukifunguliwa, .....
Tuendelee kidogo, mmh, kidole kinauma......wikiendi njema
NB: Kwa leo,..hapa hapa
WAO LA LEO:Kila
kazi ina utaalamu na utendaji wake, na pia kuna taratibu zake, ndio maana watu
wanakwenda kuzisomea hizo kazi, tusijifanye kuwa tunafahamu kila kitu, eti kwa
vile ulipitia pitia shuleni, kuna vitabu umesomasoma , hiyo peke yake haitoshi
...
Ndio maana kuna taaluma tofautitofauti, na kila taaluma, ina
mabingwa wake, ina wataalamu wake, ina watu wanapewa madaraja na nyazifa
mbalimbali, kuonyesha kuwa hizo ni fani zinazojitegemea, tusipende kujiingiza
kwenye kazi za watu ambazo huenda ni za kitaalamu zaidi, na kujifanya
tunaufahamu nazo, ilihali hatujazisomea, tujue kuwa kuongea na kutenda ni
vitu viwili tofauti,..tuweni makini na fani za watu jamani.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment