‘Kumpenda kwasababu hizo,…mhh…naomba uwe na stahimili…sitaki
nikujibu swali lako kihivyo…hilo la kupenda lipo wazi,…maana mengine yanaweza
kuja kuwa kuni,…lakini si wewe mwenyewe umetaka, na nataka nikisafiri niwe na
amani, au sio…sasa mimi nakuomba unisikilie kwa makini…nikuelezee ilivyotokea,
…tafadhali…’akasema
‘Sawa uonavyo wewe uwanja ni wako, au sio…..lakini mimi nimeshajua
kuwa ni nani unayemzungumzia, ni nani baba wa mtoto wako, hilo sina shaka,..na
hata mume wangu japokuwa hataki kuliongelea hilo, eti anadai hayo ni mambo yetu
hayamuhusu, lakini kwa namna fulani, anakubaliana na wazo langu….’nikasema.
‘Ina maana mlinijadili, ..si ulisema hutaongea naye sana kuhusu
siri zetu…?’ akaniuliza
‘Tuliongea, yale ya kawaida, si lazima mtu aulize baba wa mtoto
wako ni nani, na lazima wengi wataniuliza mimi, kwa vile mimi ni rafiki yako,
na nimeshajipanga jinsi gani ya kuwajibu,..lakini kwa mume wangu nilitaka
nichukue tahadhari, jinsi gani ya kumjibu, umenielewa hapo…’nikasema
‘Ok, sawa…’akasema
‘Kwani hajafika kukuona…alisema akipata muda atafika kwako,
hajafika…?’ nikamuuliza
‘Keshafika…’akasema
‘Mhh, alikuuliza….kuhusu mtoto…?’ nikamuuliza
‘Mhh…ndio…lakini …tuliongea, …’akasita
‘Najua, …mume wangu sio muongeaji, sana, hawezi kukudadisii
kivile, baba yake ni nani, una matarajio
gani, mengi anajua tumeshaonge, namfahamu sana..’nikasema
‘Sawa….utakuja kuelewa huko mbele ya maelezo yangu, kama utavuta
subira…’akasema
‘Aaah, kama leo umeamua kunisimulia ukweli, nipo tayari kuvumilia
mpaka umalize, nitafurahi sana…moyo wang utatulia,…’nikasema;
Tuendelee na kisa chetu…
***********
‘Basi siku ile, ya tukio la kwanza ilikuwa kama bahati mbaya, au
ndio niseme ilipangwa itokee hivyo, kwani siku ile kulikuwa na sherehe ya
kampuni yetu, huwa tunafanya hivyo mara kwa mara kwa namna ya kujitangaza, na
kuwapa pongezi wafanyakazi kwa kazi fulani iliyofanikiwa….’akasema
‘Na sherehe kama hizo, familia inawajali sana familia na
wafanyakazi, maana bila ya wao, wafanyakazi hawawezi kufanya kile walichofanya,
tuna msemo hapo kazini kwetu kuwa juhudi ya mtu huanzia, nyumbani kwake…waingereza
wanajua sana kuwale wafanyakazi wao…wajanja sana….’akasema
‘Ni kweli hata mimi najitahidi kuwafanyia hivyo wafanyakazi wangu….’nikasema
‘Basi kila mtu alipewa nafasi ya kuwaalika wanandoa wenza wao, na
kama huna mwanandoa mwenzako, basi uje na mpenzi wako anayetambulikana, sio
muhuni tu,…na wengi wanajulikana, hakuna siri hapo kazini kwetu,..au kama huna
hata mpenzi, basi tulipewa nafasi ya kuja na hata ndugu yako..ilimradi kuwe na
namna ya kupongezana kifamilia, na kijamii zaidi…’akasema.
‘Na wewe ukamualika nani, …hahaha, najua ulimualika yeye, au sio…?’ nikajikuta nimemuuliza hivyo…nitamani
asema ndio, ni yeye, lakini haikuwa hivyo….ila akilini mwangu nilishajua kuwa
ndio huyo ninayemfikiria mimi.
‘Sasa cha ajabu siku hiyo sikuwa na mtu wa kumualika,..unajua tena
wapenzi wangu walishaoa,..na nilikuwa kivyangu zaidi,…na siku
hiyo,..sikuhitajia mtu, nilikuwa na yangu kichwani…’akasema
‘Mhh..kweli hilo…’nikasema
‘Kabisa kabisa sikutaka kuwa na mtu, nilikuwa nimetingwa na mawazo
yangu maana siku zinakwenda, lile zoezi tulilolipanga halifanikiwi,…naona kama
wanaume wannikwepa, na ninaokuwa karibu nao, siwezi kufanya nao…yaani ikawa
shida, na sikutegemea kuwa itakuwa
vigumu hivyo.
‘Yah..kiu ukikidhamiria inakuwa hivyo…’nikasema
‘Ila kwa siku hiyo, kiukweli… nilitaka nisiwe na mtu karibu yangu
anayeweza kunigusa…kunipa mawazo..nilitaka niwe peke yangu …, nilitaka hata
kuwepo nisiwepo kwenye hiyo shughuli…, lakini ningeonekanaje na mimi ni mmoja
wa mabosi wa vitengo, hapo nilipoajiriwa,,
Kwahiyo siku hiyo nikaingia kwenye ukumbi kivyangu, sikuwa
muongeaji siku hiyo niliwaambia wenzangu kuwa sitaongea kabisa, ..niliwaambia
naumwa, …najisikia vibaya, na wenzangu walinielewa, wao wakaongea, walichoongea,
na akili haikuwa hapo kabisa....’akasema.
‘Wakati nimekaa naongea na wafanyakazi wenzangu, ..kikiwa ni
kipindi cha kula na kunywa,…wenzangu wakawa
wananitambulisha familia zao, na wale waliokuja na watoto wao wakawa
wananionyesha watoto wao,..basi hapo ndio nilikuwa sipataki…sio kwamba
siwapendi watoto, wewe mwenyewe unanielewa, ila hisi fulani ndani kwa ndani…’akatulia
‘Nakuelewa sana…’nikasema
‘Mtu akiwa ana familia, ..anaweza hata kujingiza kwenye shirki,
sio kwamba anataka,…maana inaumiza ndani kwa ndani, na huwezi kuelezea hilo
labda liwe limeshakufika…
Basi, wakawa wakinionyesha watoto wao, najitahidi kuwaonyesha ile
hali yangu ya kupenda watoto lakini moyoni naumia,…na mpaka ikafika muda…, najiuliza
ni kwanini, wote hapo tupo umri mmoja wana familia zao, na wengine nimewazidi, lakini
wameshabahatika kuwa na familia zao, kwanini mimi....kwakweli niliumia sana,
hadi nikajikuta machozi yananitoka,...na kabla sijaonekana nikainuka …
‘Nilikimbilia washroom, kunawa nikiwa na maana
nikitoka huko, sirudi tena kwenye sherehe, naondoka zangu kulala, na siku hiyo
sikutaka kabisa kugusa kilevi, nilishadhamiria kuacha kilevi kabisa, niwe huru,
niwe tofauti..…,
Sijui nilikaa muda gani, ila nililia sana,…sijui,..nilimlilia
mungu wangu..sana, na kama mtu angeliingia akanigusa,..sijui…nilikuwa sio mimi…
na nilipohakikisha machozi yamekwisha, nikatoka mle ndani,…, nikarudi pale
mezani kwangu kwa nia ya kuchukua mkoba
wangu, niondoke zangu…lakini haikuwezekana.
‘Kwanini…?’ nikamuuliza
*********
‘Wakati nimetoka chumb cha kunawa, niliona mtu mgeni mezani kwangu…’akasema
‘Mhh, hapo hapo,….’nikasema
‘Tulia basi…’akasema
‘Kwasababu alinipa mgongo sikuweza kumtambua kwa haraka, na
akilini mwangu sikutaka …kuongea na mtu, kwahiyo sikutilia maanani, nikawa
nakwenda mwendo wa haraka kwenda kuchukua mkoba wangu, na sikutaka kuaga…’akasema
‘Ok…’nikasema
‘Pale nilihisi machozi kama yanataka kunitoka tena,..nikajikaza
ki-kike…na..niliposogea nikashikwa na butwaa, sikutarajia kabisa,…’akasema
‘Una maana ni …huyo
bwana’ko...?’ nikajikuta nimemuuliza maana kwa muda ule nilikuwa nimetekwa na
hisia za huruma, kama nilivykuambia awali rafiki akiumizwa na jambo ni kama
mimi niliyeumizwa, kwahiyo hata mimi pale nilitamani kulia, lakini nikawa
namuuliza maswali ilikupotezea….
Kiukweli usichanani kwetu ilikuwa hivyo, ikitokea tatizo la
kuumia, kulia, kuhis jambo kwa mwenzangu na mimi nakuw ahivyo hivyo..sijui
ilikuwaje, kwa watu wasiotufahamu wakituona walihisi sisi ni mapacha…maana kama ni tukioa la kulia, tutalia sote…mmoja
akiwa na furaha, basi tunafurahi sote, …kwahiyo maneno yake hayo hapo
yalinifanya nitoe machozi na mimi….sasa uone kiasi gani tulivyokuwa tumeshibana.
Yeye hakujibu hilo swali mara moja…, muda huo alikuwa kimia
kidogo, nahisi alikuwa akiwazia mbali,..basi ili kumpa unafuu, nikauliza swali
la kumtoa hapo alipo
‘Si huyo bwanako mliozaa naye, au…?’ nikauliza hivyo kumchochea,
nafahamu hapendi kuambiwa hivyo, na kweli, akainua kichwa na kuniangalia huku
akisema kwa jaziba;
‘Huyo sio bwanangu bwana,…mume wa mtu atakuwaje bwana’ngu, …!’akasema
kwa sauti ya kukereka…!
‘Nauliza ni huyo aliyekupa huo ujauzito, au huyo unayefikiria kuwa ndiye aliyekupa
mimba…, maana awali umesema huna uhakika,…na mpaka sasa hujaelewa, nakushangaa,
ina maana ulipewa madawa ya kulevya au ilikuwaje …..hahaha mtu wewe, yaani wanificha hata mimi, haya ngoja tuone unataka nini ….?’
Nikamuuliza, hapo akatikisa kichwa tu.
‘Sio hivyo rafiki yangu, hujui nipo kwenye wakati gani sasa,
unajua ..nilijua baada ya kumpata huyu mtoto, akili yangu itatulia,…nilijua
kila kitu kitakwenda sawa,..lakini nashangaa sana,…nakuwa na wakati mgumu
kuliko…lakini yote haya ni sababu ya ….anataka mambo ambayo …we acha tu…’akasema
‘Una maana gani hapo…?’ nikamuuliza
‘Nitakuja kukuambia tu…., wewe si unataka nikuambie…u-ukweli,
subiria sasa, ila nakuomba tafadhali uwe na subira,…tafadhali sana, wewe ni
rafiki yangu na hili tulilipanga pamoja, au sio..’akasema
‘Kwanini unasema hivyo..?’ nikamuuliza nikimuangalia moja kwa moja
usoni, yeye akanikwepa na kuangalia pembeni.
‘Lakini si wewe umeamua tuvunje yale makubaliani yetu moja baada
ya jingine…ulisema iwe siri, sasa unataka nikuambie ukweli, haya, au niache…?’
akaniuliza akiniangalia kwa macho ya kutia huruma
‘Ndio, nataka uniambie kila kitu,…wewe ndiye ulianza kuharibu,
sasa endelea, nautaka sana huo ukweli,…, wewe ni rafiki yangu nilijua
utaniambia tu,…huwezi kunificha jambo hata siku moja, … au sio....ila kauli
yako inanipa mashaka, nahsi kuna jambo baya lilikutokea unaogopa kuniambia kuwa
labda na mimi nitaumia, usijali, wewe niambie tu..…haya endelea, mimi sina
wasiwasi na wewe, wewe ni ndugu yangu, kama kuna jambo limekutokea, siwezi
kukutupa kamwe, niambie tu ilikuwaje…’nikasema
‘Mhh, wewe wasema tu, kwa vile hujausikia huo ukweli…lakini sina
jinsi inabidi nikuambie tu…ila sitakuambia ni nani , ni wewe mwenyewe
utamfahamu…kutokana na maelezo …sasa utakaloamua, sina jinsi…’ akasema na
kugeuka pembeni.
Niliwaza huyu mtu ana maana gani, nikajikuta nasema
‘Wewe endelea bwana…acha kuniweka roho juu…’nikasema
‘Kumbe mjamaa alishafika muda, kwani nilimkuta anakula, sikujua
kuwa nilichelewa sana chomba cha kunawia mikono, ni kweli nilichelewa nikiwa
nimezama kwenye mawazo, mawazo ya mitihani niliyo nayo…ok, ndio hivyo….’akasema
‘Basi nikamkuta jamaa anakula...pembeni kilevi…nikajua ehee…kazi
ipo leo,..sijui ni nani alimualika, maana mimi sijafanya hivyo, …japokuwa wengi
pale ofisini walishaniona nikiwa naye, na wanajua ni nani kwangu, …na sijawahi
kusikia mtu akiniongelea vibaya dhidi yake, maana wanamuheshimu sana…na,
wanamfahamu kuwa ni mtu mstaraabu tu…’akasema
‘Yule..hahaha, mstaarabu, au maana ya ustaraabu hamuijui nyie,
acha bwana, hata wewe unamuita hivyo,…hahaha, ..labda , kwasabbu ulishapenda,
utasemaje, ukipenda chongo utaita kengeza au sio, hahaha, hata hivyo sikulaumu,…’nikasema
‘Ndio kupenda, nilipenda, kama nilivyowahi kukuambia awali lakini
nilishaweka mpaka, kwa vile ni mume wa mtu..nielewe hapo….’akasema
‘Nakuelewa sana, mimi ninachokataa ni kumuita eti mstaarabu,…hana
hiyo sifa kabisa,…labda, maana mtizamo wa watu, unatofautiana,…nikuambia kitu,
na nilishawahi kukuambia, unakumbuka nilikuwambia huyo jamaaa alifanya nini
kwangu…ananitongoza mimi, shemeji yake mke wa kaka yake, nilichomuambia
hajawahi kurudia tena…’nikasema.
‘Mhh…sawa nakuelewa, ulishaniambia
bwana, hayo tuyaache, …ngoja niendelee au…?’ akaniuliza
‘Sawa endelea, …lakini usimvike sifa hiyo ya ustaarabu, hamtoshi….’nikasema
‘Utakuja kuelewa tu kwanini nasema hivyo…’akasema
‘Sawa endelea….’nikasema
‘Kwanza, nilitaka nigeuze , niondoke, ..kabla hajaniona, lakini
macho ya watu, waliniona na yeye alipoona watu wanaangalia upande wangu,
akageuka akaniona..ikawa haina jinsi, …nikasalimiana naye, naye akanikaribisha
nikae utafikiri yeye ndio mwenyeji, mimi nikamwambia najisikia vibaya nataka
kuondoka.
‘Aaah,…mimi nipo nitakupa dawa…’akaanza utani wake, unajua kuna
kitu kimoja nilimpendea, anajua kumfariji mtu…na hata kama ulikuwa huna raha,
utatulia tu, mna bahati sana mlioolewa….’akasema
‘Hata mume wangu ana tabia hiyo, ila kuna muda, akiwa na mambo
yake, …hataki kusema, anaumia ndani kwa ndani, yeye akikuona upo huna raha,
atakudadisi mpaka basi, lakini yeye, akiwa hana raha, ngumu kujua labda awe
anataka kukuambia, anasema kuna mambo mengine ya kiume, sio lazima kumsumbua
mkewe, basi, mimi najionea sawa tu, ila kiukweli hatufichani, …ndio hivyo tena,
siku hizi, sijui uzee…’nikasema
‘Eti uzee, unanitisha mimi, una uzee gani….’akasema
‘Mkiishi sana na mwenzako, unajionea kawaida, hata ile …raha ya
usichana inakuwa haipo, utaolewa utajionea wewe mwenyewe…’nikasema
‘Basi mimi nikazidi kumsihi kuwa najisikia vibaya yeye aendelee
tu, …mimi naondoka kurudi nyumbani,…unajua alisema nini….’akawa kama anauliza
‘Yaani hiyo tabia gani,…mimi mgeni wako nimekuja, kwa ajili yako…,
mwenyeji wangu unataka kuondoka, haiwezekani, kaa angalau kidogo, nimalize
kinywaji, ..na hiki chakuka, ..au niaviache…?’ akauliza akiashiria kwa mkono
pale mezani, uzuri pale mezani hakukuwa na mtu mwingine, watu
walishajichanganya huku na kule,
‘Hapana wewe endelea tu wapo wengine mtaendelea nao, usiwe na
shaka jisikia upo nyumbani…’nikasema sasa nikidhamiria kweli kuondoka.
‘Mimi wengine siwajui, nimekuja kwa ajili yako…nimekuja
kukupongezeni, …na mimi ninayemfahamu hapa ni wewe…au nimekosea kuja, basi kama
unaondoka, nikuombe kitu kimoja, wewe si unaumwa, subiri nimalizie hiki
kinywaji nitakupeleka nyumbani kwako, vinginevyo ukae, au…?’ akaniuliza
Basi nikaona sio vizuri..nikaa kidogo, na yeye akaendelea
kunywa, nilishangaa kumuona shemeji
akinywa kwa pupa siku hiyo ,… sio kawaida yake, ni kama alikuwa na kitu kinamkera,…hata
sielewi… mpaka nikaingiwa na wasiwasi , kwanini anakunywa hivi.…’akasema
‘Lakini yule ni mlevi, anakunywa sana, hata kaka yake aliniambia,
labda akiwa kwako ndio anajivunga, haya
ikawaje, …?’ nikamuuliza
‘Nikamtahadharisha kuwa kunywa kwa namna ile mimi sikupendi,
anaweza akazidiwa ikawa shida kwangu, nikamwambia mimi naondoka,….akanizuia,
akisema hii moja basi, hii moja basi..basi moja baada ya nyingine…’akasema.
‘Hapana shemeji…mbona leo hivi….?’ nikamuuliza
‘Usijali, siku moja moja, nafanya hivi, ili akili yangu iwe
sawa,…nataka nikirudi nyumbani sisumbui kichwa changu tena, nalala tu, sitaki
shida,..na leo sijisikii kwenda nyumbani, sitaki, na..na mambo yangu ya kufanya
mengi ofisini, ikibidi nitenda kulala ofisini…’akasema
‘Shemeji mimi nakuhofia wewe, imetosha…’nikasema
‘Mhh, wanaume jamaani…., mimi sioni ajabu hata mume wangu kuna
kipindi ilikuwa hivyo, mpaka nikawa sielewani naye, hasemi tatizo ni nini,
anarudi kalewa, na ilikuwa sio kawaida yake, sijui, wakati mwingine najilaumu
maana hizi kazi zinanifanya nakuwa mbali na mume wangu, ndio hivyo…’nikasema
‘Mhh, yawezekana, ndio maana ilitokea hivyo...’akaguna na kusema
hivyo
‘Endelea na kisa chetu, nilitaka tu kukuambia kuwa hayo ya ulevi
ni kawaida ya wanaume, hasa waliopo kwenye ndoa ...usijali sana, na wala
usimwazie sana mtu kama huyo, kama kakupa ulichokitaka mpotezee, haya niambie
ikawaje baadae naona muda umekwenda sana, ..’ nikasema.
‘Basi, aliendelea kunywa, na mimi sijui ikatokeaje, akanishawishi,
nilianza na mimi kunywa kidogo, kidogo ooh… akawa ananiongelesha kunichkesha,
utani, nakunywa, nakunywa,..weeeh, akili ikabadilika, nikawa nami nazipupia, …japokuwa
kiukweli nilijitahidi kujizuia,…’akatulia
‘Mhh, kumbe…naanza kuipata picha….’nikasema
‘Basi bwana, ikafikia muda nikaanza kujisahau na mimi nikawa
nakunywa kupitiliza, ila nikabakiwa na akili kidogo ya kukumbuka, hapo
nikaingiwa na shaka..huyu mtu kalewa hivi atakwendaje nyumbani, sikujijali
mimi, maana najua nitapara msaada kwa wenzangu, huwa wanafanya hivyo wakiona
mmoja kazidiwa kwa kilevi,a pombe mbaya jamani...’akasema.
‘Nikatoka kidogo, kwenda `wash-room’ …nikampigia ndugu
yake mmoja, ili kama akizidiwa ahakikishe anamchukua na kumfikisha nyumbani
kwake…’akasema
‘Ok, namfahamu sana yule ndugu yake, wanasema eti ni mapacha, sio mapacha ila wamepishana kidogo sana, kama miezi
tisa hivi au pungufu ya hapo kidogo…, sijui ilitokeaje mama yao alishika mimba
mapema, ..ndio hivyo tena, bahati mbaya, kwahiyo wanakaribiana sana, sio
mapacha wale…’nikasema.
‘Nikampigia simu…kumbe alikuwa naye karibu tu, …akasema anatuona
nisiwe na wasiwasi...’akasema.
‘Mhh, hata mume wangu akilewa mara nyingi anamuita mdogo wake aje
amchukue...hilo ni kawaida kwa wanaume wengi, na wadogo zake kuna kipindi
wanakosana na kaka yao kuna kipindi wanaelewana, damu ni nzito bwana asikuambie
mtu ....’nikasema.
‘Ndio..naelewa hayo sana…’akasema
‘Ok, sasa ikawaje...?’ nikamuuliza.
‘Yaani baada ya kurudi mezani, akili hayo iliganda, sijui
nilikunywaje,..sijui ilitokeaje, mengi nimekuja kuhadithiwa,…maana
ninachokumbuka ni wewe kuwa kichwani mwangu na wazo lako hilo, kila mara
unanighasi, ukisemaa…sasa fanya lile jambo wakati ndio huu… usimwachie huyu
..mshawishi, ...ukishindwa hapo basi tena..’
‘Mimi nipo kichwani mwako….?’ Nikamuuliza kwa kushangaa
‘Nakuona mbele yangu, ….nakusikia kichwani mwangu,
unanishurutisha, nifanye kile tulichopanga nikifanye,…..akili ilikuwa sio
yangu,…pombe mbaya, jamani..sitaweza kulisahau hilo…na yaliyotokea hapo, hapana….’akashika
kichwa
‘Ikawaje sasa….?’ Nikauliza nikiangalia saa yangu
‘Nilijikuta nipo kitandani kwangu, nilivyofika, sijui…na wakati
nazindukana, mara mlango unagongwa,…nikasema nikiwa nimejichokea ‘nani wewe, fungua
mlango…mlango upo wazi,’
Mara mlango unafunguliwa taratibu, anayefungua anaonekana kama
anaogopa,..halafu kama ana uhakika, akafungua mlango kabisa,
Mtu niliyemuona pale mlangoni, alinifanya nipandwe na hasira,
sijui kwanini, nikasimama kwa hasira nikitaka kumfukuza, ..oh, najikuta nipo
kama nilivyozaliwa..
‘Nani sasa…yeye, kwanini umkasirikie, na …ina maana hukukumbuka
kilichotokea usiku….?’ Nikamuuliza
‘Sasa subiri kwanza, unajua ni kwanini nilikasirika, na huyo
aliyeingia unamfahamu ni nani…?’ akaniuliza
NB: Naishia hapa kwa leo, kili imechoka kidogo
WAZO LA LEO: Kiukweli pombe kwa wanyaji huwezi
kuwaambia kitu, lakini pombe ni sababu kubwa ya maasi,…imekuwa ni kichocheo cha
kuharibika maadili, kuharibu ndoa..na kuharibu afya za watu, …wengi wanasema
kuna faida ndani yake, lakini ukilinganisha faida na hasara , hasara ni nyingi
zaidi. Nawausia wenzangu na kujiusia mwenyewe tuachane na ulevi…ewe kijana ewe
mwanandoa, kulewa sio suluhisho la matatizo, bali ni kuahirisha tu tatizo kwa
muda, tusijidanganye kuwa pombe inaondoa mawazo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment