Mlango wa geti la nje uligongwa ndio,…!
Sio mlango wa nyumba yenyewe, maana hiyo nyumba imezungukwa na
geti, , nina uhakika ni geti hili la nyumba anayoishi rafiki yangu…nikamtupia jicho rafiki yangu
huyo,….nikamuona, akitoa macho kuangalia kuelekea kule mlangoni…
Ni kweli atakuwa huyo mgeni wa rafiki yangu, maana nilisikia sauti
ya mlango wa geti ukilia,…geti linafunguliwa, sasa kuashiria kuwa huyo mtu
kaamua kulifungua hilo geti yeye mwenyewe hapo ina maana gani, kuw huyo mtu
kazoea kufika hapo, anapajua vyema.
Hapo ikawa kama kamchokoza rafiki yangu huyo, nahisi rafiki yangu hakutaka kabisa huyo
shemeji tuonane naye mimi, kwa jinsi nilivyomuona akihangaika, na kwa jinsi
alivyobadilika sura, usoni alionekana kutahayari…, mpaka nikamuonea huruma,…lakini
nikawa sijali, kwanini …mimi sina nia mbaya, hanielewi tu…
‘Kwanini unapata shida hivyo, mkaribishe mgeni…’nikasema lakini
rafiki yangu alibakia akiwa kashika kichwa, akiniangalia kwa macho yenye
huruma, au…kama anataka kulia…
‘Hapana, sio leo jamani..sijajiandaa kwa hili, nahisi imekuwa ni
haraka sana, …nahisi hatari…unasikia, rafiki yangu, wewe pitia mlango wa nyuma
uondoke, sitaki matatizo hapa nyumbani kwangu, najua kabisa itakuwa hivyo….’akasema
akishika kichwa.
‘Kwanini…mbona sikuelewi…’nikasema nikimuangalia kwa macho ya
kujiuliza na yeye akawa ananikwepa kabisa kuniangalia machoni.
‘Tafadhali fanya hivyo….nitakuja kukuambia ni kwanini…lakini kwa
hivi sasa ili kuepusha shari..ili , nisivunje uaminifu..unajua aliniomba tena
sana nisije kumsema kwa watu, hadi muda muafaka ufike,…na nikifanya hivyo, ..na
yeye…unanielewa hapo, haya nenda pitia mlango huo wa nyuma…’akasema
‘Mimi siendi mahali, lao nataka hili jambo lifikie mahali na mimi,
niwe na amani , nahisi kuna …sijui nisemeje, unanifanya nianza , kama
nilivyokuambia nitunge kitabu, sasa ni kwanini, maana matendo yako, kauli, zako
zinanihamasisha nifenye hivyo, kifupi nahisi kuna kitu unaficha, ambacho ni
zaidi ya hilo tulilokubaliana, sasa ningeliomba umkaribishe huyo mgeni, najua
tutayamaliza,….’nikasema
‘Hapana, nielewe nina maana yangu kubwa sana, najua itafika muda
hili itabidi liwe hivyo, lakini sio kwa leo, sio kwasasa…nakuomba mimi ni rafiki
yako, niamini ninalokuambia…yanayotokea, na kauli zako…hapana, na iwe hivyo
tu..ila nitakuja kukuelezea kila kitu..unajua, nitaumia sana ikifikia mahali pabaya….’akasema
na mimi nikataka kusimama
‘Unataka kufanya nini sasa ?’ akaniuliza
Mimi nikamtizama kwa macho ya kujiuliza, akilini nilishadhamiria
kitu, lakini sina uhakika nacho, na alipoona kweli nataka kuchukua hatua
akasema
‘Rafiki yangu, ndugu yangu sivyo kama unavyofikiria wewe, tulia
kwanza unataka kwenda wapi…nielewe maana hata mimi nilivyokuwa nikitegemea,
imekuwa sivyo kabisa, nahisi nahitajia muda zaidi wa kulitafakari hili nisije
kuleta hatari…..!’ akasema akiwa kasimama mbele yangu kama kutaka kunizuia
Mimi pale nilishikwa na butwaa, sikumuelewa kabia, ni kwanini
anafanya hivyo,..nikabakia kumuangalia, uso ukiwa na maulizo mengi, kujiuliza
kwingi, ..baadae nikasema
‘Mhh..hatari…hatari gani….mbona unanichanganya, au hatupo sawa tena,nieleze
rafiki yangu kama kuna kitu kibaya kimetendeka nielewe mapema, hivi unanitesa
kabisa, wewe hujui tu,…hapana mimi bado nakuamini, mimi bado nipo na wewe, usiwe
na wasiwasi bwana…achana na mafikira potofu,…nikuambie ukweli, mimi nina hamu
sana ya kumuona huyo shemeji yangu..’nikasema
‘Utamuona…kwanza ushamuona sana..ila kwa sasa naomba nipo chini ya
miguu yako tafadhali…’akasema akiashiria kutaka kupiga magoti.
‘Unajua sijakuelewa, kwanini..…kila siku ni …shemeji, shemeji, nataka
nimuone huyo shemeji, hata kama yupoje, labda unahisi hadhi yake haiendani na
wewe labda, kama kweli sio huyo ninayefikiria mimi,… labda umekuja kutembea na
mtu, asiyekustahili labda hivyo..mim hilo sijali kabisa , ilimradi kakupa kile
ulichokitaka na mimi ndiye msiri wako…’nikasema
‘Hapana, sio hivyo…ninasababu nyingine kabisa, ya nia njema,
…nielewe hivyo tu…’akasema
‘Mhh..mimi hapo sitakuelewa kabisa.., leo…eeh, hakuna jinsi,
lazima nimuone huyo mtu, kama kaja yupo huko nje, mwambia aingie ndani,
tuyamaliza hapa hapa…’nikasema na yeye akabakia kimia
‘Sasa unaogopa nini, mtu yupo huko nje, anasubiria, unajua naanza
kuingiwa na wasiwasi, kitu ambacho sikuwa nacho dhidi yako, na hizi eeh…kauli
zako zinanipa mashaka, ..kwanza najiuliza kuna hatari gani, kuwa itakuwaje,
kuwa nitatoa hii siri nikimfahamu au..hahaha, mimi nimeshamfahamu, muite tuyamalize
leo hii, ili na mimi niwe na amani..’ nikasema
‘Siwezi kufanya hivyo, for
the sake of our friendship….kwa minajili kwa kuwa hata yeye mwenyewe hataki,
na kama angelijua nipo na mtu asingelifika kabisa,…alishaniomba na akafikia
kunitisha, kuwa ni..iwe siri yetu,…’akasema
‘Kukutisha kwa vipi….?’ Nikamuuliza
‘Bwana wewe liache kama lilivyo… na sijui kwanini unang’ang’ania
hivyo, wakati hata wewe mwenyewe ulitaka
iwe hivyo…hapana, acha tu, iwe hivyo hivyo.., nakuhakikishia muda utafika kila
kitu kitakuwa bayana, ikibidi….’akasema na mimi nikatikisa kichwa kukataa.
Hapo akageuka kuangali mlangoni, …uzuri mlango ulifungwa..kuna
namna ukifunga mtu wa nje hawezi kufungua, mpaka mtu wa ndani labda uwe na
ufungua…sasa sikujua kama aliuegesha tu,…
Nikawa naangalia kule mlangoni nikitamani huyo jamaa aingie,
lakini nahisi alikuwa kasimama, anasubiria mwenye atoke, au kahisi kuna …na
mara nikasikia sauti ya viatu vya mtu kukaribia mlangoni …ka-ka-ka-ka..huyo mtu
kavaa viatu vinavyotoa sauti,
Nakumbuka kuwa hata leo mume wangu wakati anaondoka kwenda kazini
alikuwa kavaa viatu vinavyotoa sauti ukitembea, nikamwambia hivyo viatu
vinavyotoa sauti sio vya kisasa, abadilishe, lakini hakutaka, siku ya leo
alisema alivitamani kuvivaa viatu vyake maana vinamkumbusha mbali.
‘Bebii…upoooh…’nikasikia sauti ikasema kutoka nje…..
‘Bebii…..’nikajikuta
nikisema hivyo, akili ikanipeleka mbali kabisa, hivyo ndivyo mume wangu alizoea
kuniita, kipindi hicho, mambo hayajawa mambo, na sikumbuki tena kuniita hivyo,…na,
mbona hata sauti ni kama …hapana…mmh,
Unajua nilihis moyo ukinienda mbio nikishindana na nafsi yangu,
sikupenda kamwe nafsi inishinde, ..lakini hata hivyo, hata huyo mdogo wa mume
wangu ana sauti kama hiyo, isipokuwa ya kwake inakwaruza-kwaruza hivi, hiyo
imetoka sawa sawa naya mume wangu.
Na hata kufikiria hivyo,
sio kwamba nilihisi kuwa ni mume wangu yupo huko nje, hapana siwezi kudanganya,
akili yangu ilinizidi kunipa tashwishwi ya kumuona huyo mtu anayefanana mambo
mengi na mume wangu.
‘Mume wangu yupo ofisini sio…’nikajikuta nasema hivyo kwa sauti
ndogo.
Rafiki yangu akanitupia jicho aliposikia nikiweweseka hayo maneno,
na ni kweli..nilikuwa na uhakika kuwa mume wangu yupo ofisini kwao, ana kikao
muhimu sana, asingeliweza kuja huku,…ndio maana alizima hata simu yake kuchelea
kusumbuliwa.
Sasa kwanini moyo wangu ukashtuka hivyo, niliposikia sauti hiyo,
inayofanana nay a mume wangu, na kwanini kauli hiyo neno hilo, liwe sawa sawa
na neno alilopenda kulitumia mume wangu enzi mapenzi yamepamba moto....hapo
nikagwaya...
Lakini atakuwa ni shemeji tu huyo….
**************
‘Kumbuka ahadi yetu, kumbuka kuwa wewe ndio uliyenishauri hivyo,
na naomba iwe hivyo ...nataka tukubaliane, ili lisije kuleta shida baadaye…’.
Nikiwa nasubiria rafiki
yangu amkaribishe mgeni wake, nikahisi maneno hayo yakijirudia rudia kichwani
mwangu kama onyo…na mara mtoto akaanza kulia,…na muda huo rafiki yangu yupo
mlangoni, anataka kufungua mlango,
Mtoto alipolia akageuka kumuangalia, na akaniona mimi nasimama
kwenda kumuhudumia, akawa na amani akashikilia kitasa kunyonga mlango ufunguke
Mimi mtoto alipolia kwa
haraka nikasimama na kuelekea pale alipolazwa huyo mtoto, alikuwa kwenye
kitanda chake chandarua , nikamkagua na nikaona kakojoa, kwa haraka nikaanza
kumbadilisha, na kuwa muda huo akili ikawa kwa mtoto sikuwa na muda tena wa
kuangalia kule mlangoni, ila nilisikia sauti kwa mbali ikisema;
‘Upo peke yako, …sijakuelewa, nauliza upo peke yako…mbona
hunikaribishi ndani..?’ sauti hiyo niliisikia kwa kuunga unga, sikuweza
kubahatisha vyema, maana kulikuwa na kelele za tv,na kulikuwa na kitu kama upepo
nje, ulikuwa unapita, sikuweza kusema hiyo sauti inafanana nanni, sio ..kama
ile ya awali alipotamka neno bebii, …na mara kukawa kimia.
Mtoto akawa kalala , basi mimi nikasimama sasa, sasa namuangalia
rafiki yangu, sisikii wanachoongea kama wanaongea itakuwa ni sauti ya chini
sana,…hapo nikatamani nisikie wanachoongea, nikatembea taratibu kuelekea huko
mlangoni
Nikasogea taratibu, hadi nikakaribia mlango, na nilipofika ,
kwanza nilikuwa na nia ya kuwaingilia, na kumkaribisha huyo mgeni, lakini
nilipofika hapo nafsi ikataka kusikia wanachokiongea,..na kwa muda huo rafiki
yangu alikuwa kazama kwenye mazungumzo na huyo mtu, na nilichoweza kusikia kwa
muda ni haya maneno, yalikuwa ya kuwewesa zaidi kiasi kwamba huwezi kuyasikia
vyema, alisema ;
‘Kama upo peke yako unaogopa nini…’ni sautiya chini sana….kiasi
kwamba sikusikia alichoongea zaidi
‘Wewe nenda, siku ya leo sio nzuri, muhimu unielewe, …ondoka
haraka sana,..mimi hapa nipo peke yangu, lakini muda wowote anaweza kufika mtu,
nielewe hivyo, kwaheri…oh..’akasema rafiki yangu na kutaka kuufunga mlango, na sasa
akageuka, na kunikuta nipo nyuma yake, alishtuka, ..na kunitolea macho yenye
dalili ya uwoga fulani hivi
‘Oh, ulikuwa unani…sikiliza…?’ akauliza kwa mashaka
‘Vipi, mbona haingii…’nikasema, na akiniashiria nikae kimia, kwa vidole,
akisema,
Sshiii…huku akitikisa kichwa, na mkono mmoja bado umeshikilia
mlango ina maana hataki huyo mtu huko nje ajue kuwa kuna mtu ndani…lakini mimi
nikajifanya sijamsikia, nikasogea karibu sasa nikitaka kufungua huo mlango.
‘Haya baadae nitakuja,…’sauti huko nje ikasema, hiyo sauti
nikaisikia, sauti hiyo iliyonifanya nishtuke kidogo, lakini sio saana, maana
haiwezi ikanihakikishia nilichokifikiria kwa muda, nikajikuta nikisema;
‘Mhh..ni nani huyo anaongea sauti kama ya mume wangu..?’ nikauliza
‘Ni shemeji…’akasema rafiki yangu akionekana kuwa na wasiwasi, na
sasa akawa kasimama kati kati ya mlango kunizuia nisiweze kufungua mlango na kutoka
nje.., huku akiniangalia machoni kwa yale macho ya mtu aliyetoka usingizini, au
alikuwa analia, …au mashaka…hivyo!
Mimi nilimuangalia kwa
mashaka, ...na sasa kitu kama hasira zilianza kujijenga, ni kwanini rafiki
yangu mwenyewe ana nifanyia hivyo, kwa vyovyote iwavyo rafiki yangu hataki
nimuone huyo mtu, ni kwanini… na inawezekana ikawa sio huyo shemeji…, na kama
sio shemeji atakuwa ni nani..au anaweza akawa ndio yeye, lakini hataki tuonane
naye uso kwa uso..ni kwanini…, labda kutokana na jinsi walivyoelewana. Hata
hivyo, ..
Kwanza nilitaka nirudi, niyaache kama yalivyo, lakini nafsi
ikasema, kwanini ..kwanini niyaache , hapana, ni lazima nihakikishe huyo ndiye
kama ninavyofikiria, na kwanini nisimuone, ni kwanini nisimuone tukaongea naye, haya mambo niyaweke
sawa yaishe tu, nina imani nikionana naye nikaongea naye, yataisha tu..nataka
nimuone huyo, she-she…shemeji….
Hapo sikuwa na simile, nikasogea na kuubandua mkono wa rafiki
yangu pale mlangoni, na kumpiga kikumbi cha kumsukumiza pembeni…, ili asogee,
na hakulitazamii hilo, akapepesuka na kutaka kudonoka chini, mimi hilo sikujali,
nikavuta mlango, ukafunguka…
Nje…hakuna mtu…lakini hisia zinanifanya nihisi kuna mtu, ila
simuoni..yupo wapi..!nikageuka huku na huku , sioni mtu…
‘Mhh…haya..’nikasema hivyo tu
**********
‘Mbona hivi rafiki yangu, imekuwa ugomvi…’akasema sasa yeye akiwa kasimama
mlangoni, akinitizama kwa mashaka,..
Muda huo ndio naangaza huku na kule kumtafuta huyo mtu kwa macho
lakini huyo mtu haonekani,…haiwezekani huyo mtu ayeyuke hivi hivi, haiwezekani
kwa muda huo mfupi awe keshafika getini na kutoka nje,..hapo nikataka
kuhakikisha, nikatembea hatua chache kuelekea getini, lakini sikuona mtu.
‘Amekwenda wapi huyo mtu uliyekuwa ukiongea naye…?’ nikauliza
‘Nani, …keshaondoka bwana…?’ akaniuliza na kusema hivyo, sasa akionyesha uso wa kunishangaa
mimi. Nikamtizamaa weeh, na kutikisa kichwa.
‘Hahaha, haiwezekani, …huyo mtu anapaa au….yupo wapi huyo
shemeji….nataka nionane naye…kakimbije
haraka hivyo na kutoka nje, haiwezekani, yupo wapi…’nikasema na nikaona kama
uso wa rafiki yangu ukinawiri, ni kama vile alitarajia nitaongea kitu kingine
kibaya, lakini akakuta nimeongea kitu ambacho hakikumkwaza, akasema;
‘Utamuona tu ndugu yangu..subira huvuta heri, njoo ndani tuongee ,
tumalizane, maana leo sina amani, natamani niondoke leo hii hii nikakae huko
Zanzibar, mpaka siku yangu ya kuondoka kusoma ifike.., lakini haiwezekani, mambo
ya visa bado hayajakamlika…lakini sikufukuzi, njoo ndani tafadhali…’akasema
‘Kweli ni bora niondoke zangu, huna maana wewe kabisa…yaani leo,
sijui hasira zangu zimekwenda wapi..haya bwana fanya utakavyo, naona …aah,
sijui kwanini,…mimi ninavyokujali na kukupenda malipo yake ndio haya, baya
bwana…lakini…hiyo lakini iweke moyoni, ipo siku nitaimalizia,..’nikasema sasa
nikitaka kuondoka
Nikakakumbuka kuwa nimeacha mkoba wangu ndani,…uone mambo ya
mweneyzimunu yalivyo,..nikarudi ndani kwa haraka, muda huo nishakasirika nataka
niondoke tu hapo.
Mimi kwa haraka nikarudi kuelekea ndani, ila haraka, uso
umeshakasirika, hata nampita rafiki yangu anaonekana kuogopa labda nitafanya
kitu..yeye kasimama kwa tahadhari,, akionekana hana amani…mimi sikutaka hata
kumuangalia machoni.
Nilipofika ndani, mtoto
alikuwa kaamuka, nikamuona anavyochezesha-chezesha vimkono vyake pale
alipolazwa, nikavutika kumuangalia…unajua tena ukiwa na hulka ya kupenda watoto…,
keshaamuka macho yake yamefunguka,
ananitizama, kama vile ananiona na hapo hapo taswira za watoto wangu wakiwa
wadogo zikanijia akilini.
Kila ninapomuangalia huyu mtoto , nawaza mengine ambayo siyataki,
nahisi kama ni mtoto wangu, nahisi..kufanana…na… lakini hainijii akilini, na
naishia kuhitimsha kuwa baba wa huyu mtoto atakuwa mdogo wa mume wangu…hivyo tu
na kujiaminisha kwa msimamo wangu huo. Mungu mwenyewe ndiye anajua..
Nilisimama pale kwa dakiki kadhaa nikimkagua huyo mtoto kwa macho,
kabla sijageuka kuondoka, na mara huko nje nikasikia sauti ya viatu kama mtu
anakimbia, tatatatata…sauti ya viatu…ni sauti ile ile…atakuwa ni huyo jamaa
kumbe alikuwa hajaondoka, atakuwa alijificha sehemu kwanini sikuwa makini
kukagua upande wa nyuma wa hiyo nyumba,
Hapo, hapo…nikamuangalia rafiki yangu kwa macho yaliyojaa hasira,
na kwa haraka nikawa nimeshauweka mkoba wangu mkononi, na sasa najiandaa kuelekea
mlangoni, ili niweze kumuwahi huyo mtu, na rafiki yangu alikuwa hajaondoka pale
mlangoni, malngo upo nusu wazi, lakini kaushikilia, na aliponiona akajua nataka
kufany anini, akaufunga mlango na kuendelea kuushikilia…, kasimama kati kati ya
mlango.
Nikamsogelea nikiwa na haraka nataka kutoka lakini safari hii
alikuwa kajizatiti, akawa hasogei, hata baada ya kumsukuma anipishe nipite..na
huko nje nilisikia mlango wa geti ukifunguliwa na najua atakuwa keshaondoka,
kiukweli kitendo hicho kilinikwanza
kweli……sasa ikawa kama shari, tunasukumana, na bado hataki mimi nitoke…baadae
nikafanikiwa nikamtoa pale mlangoni, nikafungua mlango na kutoka
nje,…nilishachelewa.
‘Kwanini unanifanyia hivi lakini, kwanini, ..?’ nikamuuliza sasa
akiwa kasimama pale mlango akiniangalia tu kwa mashaka..baadae akasema
‘Ni bora nusu shari kuliko shari kamili, ni bora tu, iwe hivi, ili
nisije kuharibu…najua utakuja kunielewa baadae, ..samahani sana rafiki yangu,
nakuomba unielewe hivyo, sina nia mbaya kabisa, natimiza masharti yetu
tuliyowekeana, na ahadi niliyoweka na huyo mtu, haitapendeza kabisa, nikifanya
kinyume chake, nielewe hivyo tu, samahani sana rafiki yangu…’akasema
‘Kwahiyo kumbe ni kweli…eeh,’nikasema huku nikitikisa kichwa
changu
‘Kweli kuhusu nini..nimeshakuambia huyo ni shemeji, hutaki
kunielewa,sasa bora iwe hivyo hivyo tu…., na ukweli ndio huo, nimetimiza kile
tulichokipanga, ni wewe sasa unayetaka kuharibu, sijui kwanini unataka
kujisaliti mwenyewe…’akasema
‘Shemeji ..shemeji,…,
hata mimi ninao wengi tu… haya kaaga na huyo shemeji yako na sitaki tena
kumuona, ila ole wako, litokee tatizo, unasikia, ole wako…si unanifahamu
nilivyo, na usifikiri nimekata tamaa, …nitamfahamu tu, huwa sishindwi jambo …haya kwaheri…’nikasema na kuanza kuondoka..
Nikageuka nyuma, nikamkuta rafiki yangu kasimama mlangoni mwa
nyumba anapoishi,..bado ananiangalia kwa mashaka, ..mimi nikatikisa kichwa kama
mtu anayesikitika, sikusema kitu zaidi…nikaanza kutembea kuelekea kwenye geti
na hapo simu yangu ikaita.
Nilipoangalia mpigaji, nikagundua ni namba ya docta , huyu ni
jirani yangu, sikutaka kuipokea kwa muda ule.., sijui kwanini. Docta ni mtu ninayejuana
naye sana, na mara nyingi hunipigia simu tunaongea naye sana, huyo kwa viwango
naweza kumweka kwenye nafasi ya marafiki zangu ninaoaminiana naye sana.
Kwa muda ule sikutaka kuipokea simu yake maana mara nyingi
akinipigia tunaishia kuongea mengi sana yaliyopita, kutaniana…kwahiyo nikadharau,
kwa vile akili yangu haikuwa sawa, nikakata simu
Baadae alipopiga tena, nikajua kuna jambo, nikapokea
‘Upo wapi zilipendwa…’ akasema kiutani, najuana naye kiukweli
‘Acha utani wako, nipo kwenye …jambo muhimu, tutaongea baadae,
naelekea nyumbani…’nikasema, yeye akasema niende kwake.
‘Nije kwako kuna nini…?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Pitia hapa ni muhimu tuonane…kama unaelekea nyumbani…’akasema
‘Sawa…’nikasema , lakini sikuwa na shauku , na moyoni nilipanga
nisipitie kabisa, namfahamu , tumezoeana kihivyo …nitakuelezea baadae ni
kwanini nimezoeana naye hivyo
Nilielekea pale nilipoweka gari langu na kumlipa huyo kijana
ambaye ninamuamini sana, nikaingia kwenye gari, na wakati nataka kuondoka, yule
kijana akasema
‘Shemeji naye alileta gari lake, nilisafishe … , lakini
hakusubiria nimalizie kusafisha, anaonekana ana haraka sana, ameondoa gari kwa
haraka sana, sio kawaida yake….’akasema
‘Shemeji gani…?’ nikamuuliza na mara honi ikapigwa nyuma ya gari langu,
kulikuwa na gari lilikuwa linataka kuingia, basi,…sikuweza kuongea na huyo
kijana, ikabidi nisogeze gari langu mbele kwanza, na nilipomaliza, nikafungua
kiyoo cha gari, kutizama nje, kumtafuta huyo kijana, nikamuoana anaongea
nawateja wake, nikaona isiwe taabu…nikapandisha kiyoo changu kuanza kutoka nje
ya eneo lile.
Nikabakia kwenye kitendawili,..ni nani shemeji, ..ni kwanini
rafiki yangu ananificha, kuna nini hapa….akili ilikuwa bado imefungwa
kabisa….huwezi amini, ilikuwa hivyo…
Wakati nakaribia nyumbani, nikaona nipitie supermarket, ninunue
vitu fulani,…lakini nilihisi moyo wangu ukiwa hauna amani, sijui kwanini,..hata
hivyo nikasema labda ni hayo mawazo, ya rafiki yangu…nikasimamisha gari…,lakini
akili ikawa haitulii…
‘Huyu kijana kasemaje, ‘shemeji
naye alileta gari..’ naye shemeji, rafiki yangu shemeji..shemeji, shemeji….si
alisema shemeji, au sikumsikia vyema, huyu shemeji atkuwa ni nani, ni mume
wangu, hapana, mume wangu yupo kazini,…ana kikao muhimu sana, hawezi kutoka,
aliniambia, hatatoka kazini mapema..
Nikataka kumpigia simu mume wangu, ili nihakikishe,…lakini nikaona
nitamsumbua tu, sasa hivi atakuwa kati kati ya mikutano yake…nikaachana na wazo
hilo, nikaingie hapo, sokoni-duka, na kununua vitu nilivyovitaka.
‘Oh, nimekumbuka , huyo atakuwa ni shemeji… mdogo wa mume wangu ..’nikasema
kwa suti, niliwazia hivyo kwasababu huyo kijana kipindi fulani nilifika akawa
analisafisha gari langu na mara mdogo wa mume wangu akafika, na aliponiona
akasema
‘Shemeji kumbe umeniwahi, basi ngoja amalize, na mimi nitafutia,
vipi shemeji hatuonani…’akasema na tukawa tunaongea, na huyo kijana alipomaliz
kusafisha, akafika na kusema
‘Shemji zamu yako…’alipotamka hivyo sisi tukacheka,…basi akawa
kila akionana na huyo shemeji yangu anamuita hivyo shemeji…sasa sijui kuwa
alikuwa na maana ya huyo shemeji au la…mmh, shemeji, shemeji..hapa kuna kitu,
kimejificha, nah ii itakuwa ufungua wa kuupata ukweli.
Sikuwa na tabia ya kumdhania mtu vibaya,… hasa mume wangu, au huyo
rafiki yangu, niliwaamini sana, kutokana na jinsi tulivyoishi,…mume wangu ni
mwaminifu sana, na namuamini kwa hilo,sikuwa na shaka naye hata kidogo, licha
ya tabia hiyo ya kulewa, ambayo ilianza baadae tu…hata sijui ni kwanini, lakini binadamu bwana….
Kiukweli hadi hapo sikutaka kuingia na dhana mbaya dhidi ya mume
wangu, wala rafiki yangu…ndivyo nilivyokuwa, utaniona ni mtu ajabu lakini ,
sijui nisemeje, na ilinisaidia sana kuwa na tabia hiyo kipindi , hadi
lilipotokea hili tukio.
Mimi mwenyewe ili kulimaliza hilo akilini, ili nisije kuingiwa na
shetani mbaya wa dhana chafu, nikahitimisha kichwani kwangu kuwa, huyo
aliyefika pale nyumbani kwa rafiki yangu atakuwa ni mdogo wa mume wangu, na kwa
kujiridhisha tu, nitarudi kwa huyo kijana tena kumuulizia vyema au nitakwenda
kwa shemeji, yaani mdogo wa mume wangu. Hilo nikalimaliza hivyo kichwani.
Lakini bado nikasema;
‘Huyu rafiki yangu kuna kitu ananificha..na hicho kitu ni zaidi ya
tulivyokubaliana, na nafsi yangu haitatulia mpaka nikigundue, nitakigundua tu,..’
Wakati huo naendesha gari
kulekea nyumbani….mara simu yangu ikaita, na kuangalia nikakuta ni mmoja wa
wateja wangu , nikaipokea simu, muda huo ndio nataka kuingia kwenye gari,
‘Unasemaje,…nini, ajali, …wewe una….hapana, sijasikia,…ndio
naelekea huko, wapi lakini…’ nikahisi kitu kama kikigonga kichwani, kizungu
zungu,…sikujitambua, baadae nafungua macho najikuta nipo nimelala chini, watu
wamenizunguka.
‘Ajali….!!!’ Nikajikuta nimesema hivyo, kwa haraka nikainuka
kutaka kuingia kwenye gari langu.
WAZO LA LEO: Ni kweli tunahitajia kitu, ni kweli
tunataka kupata lakini je ni sahihi kupitia njia ambayo sio sahihi, kwa vile
tu, muda umekwenda, kwa vile upo kwenye shida, kwa vile tu…je unauhakika
utakipata na kuishi muda wa kukifaidi hicho kitu…..tuwe makini na mambo
tunayotenda huku tukiangalia uwepo wetu hapa . Tumuombe mungu atupe hekima ya
kutafakari mambo kabla ya kuyafanya Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment