Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, August 14, 2017

DUWA LA KUKU....35


Nilipokuja kuambiwa haya yote, kweli nikaikumbuka hiyo siku, nakumbuka sana siku ile nilikimbilia kulala bila kufanya ibada yoyote, nilikuwa nimechoka sana, nilikwenda kwenye sughuli za harusi za jamaa zetu, kwahiyo niliporudi nyumbani, nikajibwaga kitandani.., bila hata kumuomba mola anilinde, maana usiku ni safari ya nusu kifo.

Ni muhimu jaman kabla ya kulala, kufanya ibada, kumuomba mola wetu atulinde, maana usiku una masaa mengi ambayo huoni kinachoendelea mbele yako, usiku kama huo, wengine wamelala, wengine kwao ni masaa ya kazi, kuna viumbe vingine usiku ndio vinafanya shughuli zao, kwa wema na kwa ubaya, kwao ndio kumekucha, yanayotokea ukiwa usingizini mola ndiye mlinzi wetu, sasa kwanini tunalala bila kumuomba…

Siku hiyo nilipitiwa…..

Nilikuja kuikumbuka sana siku ile, kwani ilikuwa siku ambayo nilipata mateso sana, zaidi ya siku nyingine. Kiukweli siku nyingine mambo kama hayo yalikuwa yakitokea, sawa ila siku hiyo yalizidi,…unajua hata hawa mabint walipokuwa wakilalamika kuwa wanaota ndoto za majinamizi, mimi niliwahi kuwaambia hata mimi naotaga lakini kwangu mimi nilichukulia kuwa ni ndoto tu, ila moyoni nilishaanza kuingiwa na wasisi, …..ni kwanini itokee hivyo karibu kila siku…

Ndio maana niliamua kufanya uchunguzi wa kisayansi wa kuweka vyombo vya kunasa matukio, baada ya kusikia kuwa kuna mtu wa namna hiyo ambaye ana uwezo wa kuyagundua mambo yaliyofichika kwa kutumia, picha, au video,…na siku akielezea niliona ni kama uwongo wa kutafuta pesa, ila baada ya kufikia sehemu akaelezea kuwa kuna watu wanaingia majumbani usiku hatuwaoni, ukiweka video, ukapiga matukio ya usiku, yeye anaweza kusafisha vile video ukawaona hao watu wanakuja kwako usiku.

'Hiyo ni kweli,…yawezekana kweli, mmh… je kweli uliona hivyo…?’ akauliza mama Ntilia na kabla huyo mama hajajibu na mimi nikauliza hapo kwa hapo…

‘Kwani huko kwa huyo mtu aliyekuambia anaweza kuona hivyo vitu kwa kusafisha picha hukuweza kumpata tena?

‘Kwa bahati mbaya sikuweza kumpata…hayupo tena hapa nchini, kasafiri nchi za nje….’akasema
‘Kwahiyo ilikuwaje maana tuna hamu ya kuusikia usiku huo ulivyokuwa….’akasema huyo mama Ntilie.

'Tukirudi kwenye huo usiku, kiukweli nilipambana sana,….ukiwa na imani ya dini, inasaidia sana, lakini kwa kujisahu kwangu kufanya ibada siku ile, na kuomba, …mmh, yakanikuta makubwa, japokuwa nilijitahidi sana…na mengine hutokea ili iwe mitihani kwetu, naweza kusema hivyo tu… nakumbuka hata nilipoamuka, mwili mnzima ulikuwa unauma, na kiukweli, ndani ya ndoto, niliwaona watu ninao wafahamu,…’akatulia

‘Nani hao…?’ nikajikuta nimeuliza

‘Mume wangu na kijana wangu,…’akasema na sisi tukageuka kumuangalia huyo mzee.

‘Mume wangu alionekana akiwa anamlazimisha kitu kijana watu, huku kijana wangu analia hataki,… lakini mume wangu akishirikiana na watu wengine wakawa wanamlazimisha, na kitendo hicho kilionekana ni kibaya kwangu, na sikuweza kukitambua hicho kitendo,…maana niliona mambo mengi ya kutisha, huku nimekabwa, nahangaika huku na kule, yaliyotokea usiku huo itaweza kuyasahau na mengine siwezi kuyahadithia…’akasema

‘Hao watu wengine ni akina nani, hukuweza kuwakumbuka…?’ akaulizwa

‘ Nakumbuka siku nilipomuona yule marehemu pale hosp, tulipokwenda kumuona, nikajiuliza huyu mtu niliwahi kumuona wapi,…akili yangu ilikuwa ikinituma kuwa niliwahi kumuona mahali,.. baada ya kupata huu ukweli, ndio nikakumbuka, nilimuona kwenye ile ndoto mbaya….’akasema

'Naona unazunguka mama, je waliweza kufanikiwa kukufanyia kama walivyotaka…?’ akauliza mama Ntilie.

'Mimi sijui,…kama nilivyosema mengine yatabakia moyoni mwangu, siwezi kuyahadithia, lakini kwa ufupi kwa hicho walichotaka kukifanikisha walikifanikisha, maana bila kupitia kwangu, kama walivyoelekezwa na huyo mchawi, wasingeliweza kufanya mambo mengine…na hayo mambo mengine yalikuwa ni muhimu kwao…’akasema huyo mama kwa huzuni, akitamani kulia.

'Lakini wewe si uliwauliza …ulimuuliza huyo aliyekuhadithia kuwa walifanya hivyo, au ilikuwaje…?’ akauliza mama Ntilie.

'Kuwauliza akina nani sasa…, haya ninayoongea aliyenisimulia ni huyu mume wangu, sasa aseme ukweli, je haya ninayoyaongea ni uwongo, na je siku ile akinihadithia aliongea tu , akiwa kachanganyikiwa. Hayana ukweli ndani yake…’akasema huyo mama akimuangalia mumewe.

Basi sisi tukamgeukia huyo mzee tusikilize jibu lake, naye kwanza alitulia kama anawaza jambo, aliopnekana kuchoka, hana raha, hata uso wake ulikuwa umesawajika…., baadae akasema;

'Hata nikidanganya kua sio kweli, namdanganya nani,..hata niki…unajua naona kama ndoto ya kulazimishwa, sijui ilikuwaje mpaka nikaghilibiwa kiasi hicho,…hapana isiwe ni…naombea iwe ni ndito tu….’akasema akishika kichwa.

‘Swali je ni kweli au si kweli..hata mimi natamani isiwe ni kweli, sema ukweli wako…?’ akauliza mke wake.

‘Yote ni kweli, siwezi kuwaficha hayo, na hata mimi usiku ule nilipata shida sana, maana nilijipanga kukataa, nilimuomba mungu sana ili aniepushie na hao watu, wakija isifanikiwe, kwa namna yoyote ile, kwahiyo hata walipokuja nilijaribu kuonyesha kukataa, lakini nilijikuta kama kawaida mwili wote unaisha unaisha nguvu, na unazama kwenye giza ambalo hajui kinachoendelea…’akasema

‘Kwahiyo kumbe wakija usiku wewe unaowaona…?’ akaulizwa

‘Siwaoni, ila inakuja hali fulani, unahisi mabadiliko...kitu kama njozi fulani hivi, na mwili unalegea kabisa, unakuwa huna nguvu kabisa,..ni kama njozi,…njozi ambayo huwezi kukumbuka ulichokifanya, ila unahisi kuna kitu ulikifanya, na ukiamuka asubuhi, kuna hali unaihsi kuwa kuna kitu umekifanya , lakini hukumbuki ni kitu gani,...'akasema

'Wakija, unahisi, unalegea au sio..una kabwa...kama sisi au sio...?' nikamuuliza

'Hukabwi,..nyie mnaotendewa hivyo ndio mnafanyiwa hivyo,...mnajiona mnakabwa, hasa mkileta kiburi...ila kwa upande wangu nilikua nahisi wamefika, sasa …na hapo sasa unakwua sio mtu wa kawaida,...na kinachoendelea huko mbele mimi huwa sikijui, mpaka narudi kulala….’akasema

‘Kwahiyo kume wewe unaamuka kiukweli, kimwili na kiroho…?’ akaulizwa

‘Ndio hivyo, utatendaje bila mwili…’akasema

'Sasa kwanini wao wakija hawaonekani, lakini nyie mnaonekana mkifanya hayo mambo, kwasababu wewe ulionekana ukitoka chumbani kwako na mkeo....au sio...?' nikauliza

'Wao ni wachawi, lakini sisi sio wachawi, sisi tuanatumika tu...kwahiyo, wao wa namna ya kujificha wasionekane , namna ambayo hawawezi kutufanyia sisi...mpaka na sisi tuwe wachawi kama wao...'akasema

‘Sasa unasema ulipambana nao kwa vipi sasa…?’ akaulizwa

‘Nilikuwa sitaki, siku nyingine nakuwa huru, kukubali, lakini siku hiyo , nikijua ni kitu gani kinakwenda kufanyika sikuweza kukubali kwa haraka, ila wao wanajua jinsi gani ya kunifanya nikubali tu,….’akatulia.

'Kwahiyo kwa uoni wako, au ulivyokuja kuambiwa, …Je hilo tendo lilifanyika la kumkabidhi mtoto wako hayo mambo yako…?’ akaulizwa

'Ndio lilifanyika…jamaa kesho yake alinipigia simu, akanielezea lilivyofanyika akaniambia walifanikiwa lakini ni kwa shida sana, na ilibakia kipindi kifupi…mke wangu alikuw amgumu sana, lakini mwisho wake walimshinda, kwahiyo nikiona mke wangu hayupo vyema leo, nijua kuwa ni hayo mapambano, ila makafara ya kimizimu yameshakamilika, na sasa kazi itakuwa mikononi mwa kijana wangu…’akasema

‘Mungu wangu ina maana wewe ulikubali kijana wako awe ….mume, awe ..hapana, una akili wewe….’nikasema nikimuangalia huyo mzee bila kum-maliza.

‘Ningefanyaje muda kama huo, muda huo shetani alishaniteka, nikijua kama nisipokubali mke wangu, au kijana wangu wanakuwa marehemu ili kuzima hasira za mizimu hiyo…ndio badili yake, je hapo ningelifanyaje…’akasema

‘Kwani wao ni mungu anajua kumuua mtu, na kujua ….?’ Nikauliza na kushindwa kumalizia.

‘Binti, hayo mambo yasikie hivi hivi, kwenye kujiingiza kwenye mambo hayo nilijifunza mambo mengi, usiku una maajabu, usiku una vitisho…kuna kipindi huyo mtu alimua kunionyesha mambo wanayoyafanya…wanavyokwenda makaburini, wanavyokula nyama za wafu…inatisha, kuua kwao ni kutu rahisi tu….’akasema

‘Kwahiyo na nyie mliwahi kula nyama za wafu…?’ akaulizwa

‘Kipindi cha awali ili kuja kuanza huo mchakato, tuliambiwa ni lazima tule nyama za wafu..tunywe damu za watu…kesho yake nilipoyakumbuka hayo nilitapika sana, nikawa sitaki kula nyama, hata mke wangu alishangaa sana, maana mimi nilikuwa mpenzi wa nyama,…lakini kila nikiona nyama nakumbukia hizo nyama za wafu…’akasema

'Sasa j mlifanikiwa….?’ akaulizwa

'Kwa lipi sasa hapo…?’ akaulizwa

'Hilo la nyota ya utajir kuhamia kwako…?’ akaulizwa

'Halikuwezekana, kwasababu mbali mbali…, kulikuwa na vita kati ya huyo mtaalamu wangu na mwenzake, ikawa wanapambana wao wenyewe kwa wenyewe mwenzako akitaka yeye ndio alifanikishe hilo…kutokana na kuwa yeye ndiye aliyekuwa na huo mkoba wa uganga…na kuna mambo mengine makubwa tu….’akasema

'Mambo gani hayo, hatuwezi kuyafahamu…?’ akaulizwa

'Kuna mambo yao mengine ya kugombea maeneo yao, ardhi….huko kwao ugomvi wa ardhi ni mkubwa sana, na wengi wanauana kwasababu ya ardhi….’akasema

‘Kwahiyo hilo la kuwa alitaka kumuoa binti akamkatalai sio kweli…?’ akaulizwa

‘Hilo pia ni moja wapo,…lilijitokeza katika mapambano yao, ..na huyo binti alikuwa na kitu wanachokitaka, wana..mambo yao ya kuamini nyota ya bahati…huyo binti alikuwa nayo…na hata hivyo huyu mtaalamu akatokea kumpenda huyo binti, baada ya kuachana na mke wake, na alisema angelimpata mambo yake mengi yangelifanikiwa…’akasema

‘Sasa ilikuwaje…?’ akaulizwa

‘Kumbe huyo binti ni mtoto wa nje wa adui yake, adui yake akaligundua hilo, kukawa na vita vya kupambana, na kilichotokea ni kuwa huyo binti akaenda kwa mganga, kumbe huyo mganga ni kati ya wafuasi wa huyo adui wa huyo mtaalamu, kwahiyo ikajengwa hoja, ya kuhakikisha huyo mtaalamu hawezi kumuoa huyo binti….’akasema.

‘Je huyo binti anayafahamu hayo, kuwa baba yake alikuwa huyo adui wa huyo mtaalamu wenu…?’ akaulizwa

‘Hafahamu….maana huyo mama yake aliyepewa huo ujauzito alifukuzwa kwa wazazi wake akahamia mbali na hicho kijiji, na huku yalitokea mengi hadi huyo mtoto wake akachukuliwa huku mjini, na …akapotea kwenye mazingira ya ajabu, amekuja kuonekana akiwa mkubwa tu….ila hao wazee walikuja kumtambua kuwa ndio yeye…’akasema

'Kwahiyo ikawaje sasa…?’ akaulizwa

'Ikawa jamaa haji tena mara kwa mara…, anatuma watu wake, …na mambo mengi yakawa hayakamiliki, maana watu wake wakija wanashindwa kumuingia mke wangu, wanaishia kukimbia,….na ghafla nikasikia jamaa anaumwa, alidondoka kwenye safari zao akaumia, na anadai chanzo ni huyo rafiki yake, katupiwa mzinga,…kwahiyo vita vyao vikawa ni kipaumbele…’akasema

'Kwahiyo hukuweza kufanikiwa….?’ Akaulizwa

‘Kwa jinsi ilivyotakiwa haikufanikiwa, lakini jamaa alisema anakuja mwenyewe kumalizia sehemu iliyobakia, ila alidai nyota tayari ipo nyumbani kwetu, sasa imehamia kwa mtoto….’akasema

‘Kwahiyo mtoto wenu akaanza kuwa tajiri…?’ akaulizwa

‘Utajiriri...hahaha, alianza ...lakini, ooh, yakaanza kutokea matatizo kwa mtoto, akaanza kupatwa na maradhi kama yangu….na...na....’akasema na kushindwa kuendelea kuongea zaidi.

‘Maradhi gani….?’ Akaulizwa na hapo akainamisha kichwa chini, na mke akasema

‘Ulisema tuhadithie yote, sasa elezea kila kitu…..mtoto alipatwa na maradhi gani, kama yako….?’ Mkewe akamuliza kwa hasira, na jamaa akashikwa kichwa, na kuanza kulia….

‘Kulia hakutasaidia kitu,..., si umesema ili upone matatizo yako watakiwa kufunguka, kuyaelezea yote kwa uliowakosea, unakumbuka,…?' akaulizwa

'Nakumbuka sana mke wangu....'akasema kwa unyonge.

'Na mpaka nafika hapa na wewe uliniomba sana, ukasema kutokana na hayo, kujitolea kutubu, kuanza kuongea yote kwa watu uliowakosea umeshaanza kupona ni kweli si kweli...?' akaulizwa

'Ni kweli mke wangu....'akasema

'Sasa ni kipi kinakufanya ushindwe kuongea mwenyewe,ili na mimi haya yaishe vyema moyoni mwangu, na sijui yataishaje..'akasema huyo mama

'Yatakwisha tu mke wangu mimi nina uhakika na hilo....'akasema

'Kama una uhakika na hilo,...basi ongea, ulivyofanya,....'akaambiwa

'Sio mimi niliyefanya, alifanya huyo mtu kwa kunitumia mimi....'akasema

'Ehee....hapo hapo, alikutumiaje, maana usione mimi naongea hivi ukahisi kuwa mimi nina moyo wa jiwe, je na huyu binti ambaye anahitajia maelezo yako jinsi gani ilitokea kwake, au umesahau kuwa kisa cha kuja hapa ni kuelezea yaliyotokea kwake, ili akusamehe vyema kiukweli kutoka moyoni,
isije akaja kuyasikia kwa mtu mwingine akaumia, na kusema kwanini hukuyasema hayo…..’akaambiwa.

‘Lakini mke wangu unanifahamu nilivyo, kwenye kuongea wewe upo bora zaidi, mimi siwezi kuyaelezea kama utakavyoelezea wewe, hapa nilipo…naumia sana…tafadhali nakuomba elezea nimekuruhusu , elezea kila kitu usiogope...’akasema

‘Wewe leo unaumia eeh., wakati unautafuta utajiri, hukuliona hilo au sio...?' akaulizwa

'Mke wangu, hayo yameshapita,...'akasema

'Kama yamepita na kweli unataka yapite, sasa ongea, au unanionaje mimi, .., je mimi ambaye pamoja na hayo mliniumiza, mlinifanyia mambo ambayo hayatakiwa kufanyika kwenye ustaarabu wa kibinadamu, na mbaya zaidi kwa mtoto wangu mwenyewe, halafu naambiwa nikusamehe, labda sio mimi …'akataka kulia.

'Lakini mke wangu, ina maana hutaki mtoto wetu apone, ....'akasema

'Ndio unanitega kwa hilo....'akasema mkewe

'Wewe mwenyewe umeota ndoto kuwa usiposamehe haya mtoto wetu hatapona, je tuyaache hivi hivi, sawa, mimi nitaenda mitaani, au nitaenda kujinyonga, ...maana kiukweli usiponisamehe wewe, sina haja ya kuishi tena...'akasema

'Unanitishia, jiue tu..kwani ukijua unaniongezea au kunipunguzia nini, wangapo wajane wapo na wanaishi....'akasema mke wake

'Sio sababu hiyo, ni sababu ya mtoto wetu,...mimi nina imani kuwa ukiyasameeh haya, tukawa kitu kimoja na mimi nimeshatubu, mtoto wetu atapona, na...wote waliohusika hapa, akiwemo huyu binti, mambo yake yatakuwa sawa, atajifungua salama..si ndio hivyo,...?' akauliza

Mkewe akabakia kimia akiwa kashi

'Mke wangu....'jamaa akalalamika.

'Kwani mama, hayo anayosema baba kuwa ukimsamehe, ndio itakuwa sababu ya matatizo haya kuisha ni nani kayaongea, au yametokea wapi....?' akaulizwa

'Yalitokea kwangu usiku, niliota ndoto ya namna hiyo, ndio ikabidi nimtafute huyu mwanaume ili tuje tuyamalize hapa, ..ni ndoto, lakini ndoto zangu za namna hiyo mara nyingi huwa ni kweli....lakini siwezi...'akasema

'Mama mbona hata mimi naamini hivyo, haya yote yatakwisha, lakin kuisha kwake ni wewe na bab msameheane, kwangu mimi haina shida, nimeshawasamehe....'akasema

'Hujasikia yaliyotokea kwako bado...'akasema huyo mama

'Yapi hayo,..mimi naona umeshayaelezea, na yalitokea kwa muongozo wa huyo marahemu au sio...?' akaulizwa

'Mengine ni kutokana na huyo marehemu lakini mengine ni kutokana na yeye mwenyewe...'akasema

'Kwa vipi wakati yeye umesema alikuwa anaumwa, na hakuwa na uwezi tena...?' nikauliza

'Unajua mengine nikiongea mimi watu wataona kama natilia chumvi, hata huyu mwanaume kuna muda nikiongea unanikatiza...sasa kwa vile yeye mwenyewe yupo na ndiye alikuwa mtendaji, basi aelezee kila kitu....'akasema na kumgeukia mumewe

'Haya…tuambie sisi sote, mimi nimefikia pale mliponifanyia uchafu wenu, mkahamisha uwezo wako kwa kijana wetu....ilikuwaje sasa kwake,...na kwa vipi akaanza kubadilika, na ni kwa vipi akaanza kuumwa kama wewe, ..na aliumwa nini, ambacho unasema ni kama wewe, na je mlifanikiwa kwenye mipango yenu hiyo, …hayo ni maswali yanahitaji majibu kutoka kwako?’ akaulizwa.

'Sawa....'akasema na kuanza sasa kuelezea yeye mwenyewe.

NB: Inasikitisha,….je mpo tayari tuelezee yaliyotokea kwa mtoto hadi akafikia hapo alipo,…au tumalizie kisa chetu..?

WAZO LA LEO: Matatizo mengine ya watu yanayotokea ukubwani yameanzia utotoni,, kumbe yalianzia kutoka kwa wazazi au walezi, kuna watoto wamekuja kuathirika na maradhi mbali mbali, au kuja kuiga tabia fulani, au kuja kuwa kasoro fulani, kisa ni kutokana na wazazi au walezi waliowalea.

Wazazi jamani tuweni makini sana kwa watoto wetu, na hasa pale wanapokuja wageni, mnawalaza na watoto je mnawafahamu hao watu tabia zao. Tujenge tabia ya kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na vyumba vyao ambavyo, wageni hawaruhusiwi kulala nao...

Nayasema haya sio kwa kukataa wageni, lakini kua mengi yametokea ya kuharibu watoto, na matokea yake wanakuja kuharibika ukubwani, kisa ni mgeni, tena ndugu wa akribu tu, kisa ni mlezi, kisa ni wafanyakazi wa ndani, au kisa ni hata mzazi wenyewe. Tumuombe mungu atulindie vizazi vyetu, na atuepueshie na mitihani mingine ambayo sio dhamira yetu…Aamin.

No comments :