Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, August 15, 2017

DUWA LA KUKU....36



‘Kiukweli inabidi nielezee, ila nakuomba sana mke wangu uniongoze, najua wewe unaweza kuniuliza maswali ya kuniongoza….’nikamwambia mke wangu, na yeye akabakia kimia.

‘Wewe ongea bwana, wewe si mwanaume,….’akasema mke wake kwa hasira.

‘Sawa, nitaelezea tu, ila hamuwezi kuamini, inaniuma sana ikizingatiwa kuwa mimi nilishawishika kijinga na kuyafanya hayo yote, lakini kama ungelinifunua moyo wangu ukauona ulivyo ungeniamini haya ninayowaambia, hii ni familia yangu, na nilitaka kufanya hivyo nikijua…’akawa anataka kuongea zaidi, lakini mke wake, akamkatiza kwa kusema

‘Wewe ongea hayo ya muhimu, hayo ya kujidai kuwa unaijali fanulia yako yataonekana kwenye maelezo yako…’ akaambiwa

‘Inabidi nijitetee kwa hili kuwa nilifanya hadi hapo, licha ya kuwa nilishaona kuna madhara, ila kwa hatua niliofikia hadi hapo sikuweza kuacha, kwa masharti hayo, kuwa nikiacha kuendelea kuyafanya kama yalivyotakiwa ili yawezekane, basi kafara lake ni mmoja wa ninaowapenda afe…awawe kama kafara la hiyo mizimu.

‘Sawa hapo tumekuelewa na imani zenu za kishirikina,…..endelea ….’akasema mke wake naona alishakubalia kumuongoza kwa maswali.

‘Basi, baada ya tendo lile la kuhamisha nguvu za uwezo wangu kama mume wa familia, …na kuhamishiwa kwa kijana wangu,…,ikawa mimi kazi yangu ni kuwa msindikizaji tu, ila kila anachofanya kijana nilitakiwa niwepo, na niwe nimemshika mkono, inakuwa nguvu zetu zipo pamoja,….hayo yanafanyika mimi sijijui..na hata kijana wetu hajijui..’akasema

‘Kwahiyo kila mkienda kwenye hizo shughuli za usiku, ilikuwa ni lazima kijana wako, apitie kwa mama yake afanye yale uliyotakiwa wewe uyafanye kwa mama yake..?’ akaulizwa sasa na mama Ntilie.

‘Nahisi ndio hivyo, ili dawa hizo zifanye kazi, …’akasema

‘Kwahiyo unahisi huna uhakika….hakuwahi kukuambia kuwa ndivyo ilivyokuwa inafanyika...?’ akaulizwa na mke wake.

‘Aliniambia, ndio kawaida ….kila safari ikifanyika huniambia kilichofanyika, ila mimi nilimuomba hayo ya kijana wangu asiwe ananiambia, lakini akasisitiza kuwa ni lazima nijue kila kinachotendela kabla ya kutenda na baada ya kutenda ndivyo masharti yalivyo hivyo, ….’akasema.

‘Kwahiyo hiyo safari ya kijana wako kuchukua nafasi yako na kufany akila ulichokuwa ukikifanya wewe kama mume wa familia, ni zaidi ya mara moja…’akaulizwa.

‘Ndio..mimi siwezi kuwa na uhakika ilikuwa mara ngapi, lakini ni zaidi ya mara moja, na baadae huyo mtu akasema tayari nguvu zimeshahamia kwa kijana na nyota imeshaanza kuonyesha uhai, iliyobakia ni matendo mengine sasa ya kuihamisha kutoka kwa kijana kuja kwangu, lakini hiyo si lazima kwa sasa, ilimradi nyota sasa ipo ndani ya familia yetu….’akasema.

‘Kwahiyo utajiri ulianza kuonekana ..au?’ akulizwa

‘Kijana alianza kubadilika, ..ghafla akanunua gari la kifahari tu… nakumbuka tuliulizana na mke wangu kijana kapatia wapi pesa kiasi hicho cha kuweza kununua gari la gharama hivyo, mimi akilini najua ni kitu gani, mke wangu akawa hajui, kwahiyo yeye akataka tumuulize kijana, na mimi nikamwambia ni juhudi za kijana wetu tusipende kumuingilia maisha yake…’akatulia akisubiria kuulizwa maswali.

‘Ehe, endelea sio lazima nikuulize maswali wewe si unaendelea kuelezea tu…..’akasema mke wake.

‘Kijana akaanza kubadilika, akawa hata nyumbani haonekani mara kwa mara , kitu ambacho sio kawaida yake, ukimpigia simu anakuambia, nipo kwenye mishe mishe zangu, ninalala hotelini, na anaongezea kwa kusema, sasa atanunua nyumba yake ili tusiwe tunamuulizia ulizia, kuwa yupo wapi…’

‘Kununua nyumba  au kupanga nyumba?’ akaulizwa

‘Yeye alisema anataka kununua nyumba ..tukamuuliza pesa kapatia wapi, yeye alisema kwenye dili zake za hapa na pale, ikabidi mama yake amuwekee watu wakufuatilia nyendo zake, na akagundua kuwa pamoja na mengine kijana, alikuwa akicheza kamari, na alikuwa akipata pesa nyingi sana, na ndio hizo anazichezea hivyo…mimi nilijua ni hiyo nyota sasa inafanya kazi,…lakini sikuwa na raha na hali iliyokuwa ikiendelea maana sio mimi naonekana mwenye utajiri, na mimi nilitaka nionekane mimi ni tajiri kwa ajili ya kumuonyesha baba mkwe.

Mama yake hakuwa na raha na mabadiliko hayo ya kijana wake, akashangaa kuniona mimi namtetea, sitaki kumfuatilia, …na akataka tumuite huyo kijana kwenye kikao, na kijana alipokuja akawa anatujibu kijeuri, kuwa kama ni pesa anazitafuta kwa akili zake, kwahiyo tusimfuate fuate…ilikuwa kwa mara ya  kwanza kijana wetu anatujibu hivyo, hakuwa na tabia hiyo kabisa,…’akatulia.

‘Unaona kijana wako alivyobadilika, wewe unakaa kimia tu…sasa mke wangu akaanza kuniandama mimi, mimi sikupenda kubishana na mke wangu maana nilijua ni nini kinachoendelea..

Na mara nyingine namjibu, hivi;
‘Atatulia tu, nina imani akioa, mambo yatakuwa safi…ndio maana nafurahi akiwaleta mabinti ili niweze kuwachunguza ni nani anafaa…’nikamwambia mke wangu.

Katika mambo yake aliyokuwa akifanya, zaidi ilikuwa ulevi, kubadilishana mabinti, na siku nyingine anakuja na mabinti wa watu zaidi ya watano, kustarehe nao, kwangu nilijua ni kwasababu gani, na ni mimi nilimshauri afanye  hivyo awali, na nilimuambi ahakikishe anachagua wazuri…hakujua usiku hao mabinti wanachukuliwa kufanyiwa mambo na hao wachawi…

‘Basi ikawa sasa ni kero hata mimi nikawa sina raha, maana mama yake alikuwa haachi kunisemesha kuhusu mtoto, na hata ndugu zake achilia mbali wazazi wake,…nikaona sasa ni bora nitafuta njia ya kulituliza hili, nikawasaliana na huyo mtaalamu, ndio akaniambia japokuwa yupo kwenye matatizo na huyo mpinzani wake, lakini yeye anatarajia kuja huku hivi karibuni, na akija huku atahakikisha analimaliza hilo tatizo…

Kweli haikupita muda, akafika huku Dar, tukaongea naye, akaniambia ni nini cha kufanya…na hapo nikazidi kuingia matatani…lakini sikuwa na jinsi…’akasema

‘Uliambiwa ufanye nini…?’ akaulizwa

‘Ili tulimalize hilo, inabidi turejeshe hizo nguvu alizo nazo kijana kwangu mimi, kwani hizi sasa inawezekana kufanya hivyo, awali ilikuwa haiwezekani, ilitakiwa muda fulani upite…na muda huo ulishapita…’akasema.

‘Ina maana ukizirejesha hizo nguvu kwangu, hali yangu itakuwa kama awali, na kijana atakuwaje..?’ nikamuuliza

‘Ndio, hali yako itakuwa bora, kama kijana wako… ila kijana wako yeye, anaweza akawa kama wewe…’akaniambia hivyo..na kunifanya nishtuke.

‘Kwa vipi…awe kama mimi?’ nikamuuliza.

‘Ujue hizo nguvu utakazozipata sio zile za kwako za asili, hizo ni nguvu za kupandikizwa, lakini zinafanya kazi kama kawaida,, ….’akaniambia

‘Ina maana mimi sitaweza kuwa na nguvu zangu za asaili…?’ nikamuuliza

‘Hilo hatujui, maana mizimu ndio inayokumiliki, na hatuwezi kuilazimisha,…kwahiyo kwa hivi sasa tunatakiwa kufanya yale wanayotaka wao kwanza, …ila ukiona umechoka na hizo nguvu, kwa kipindi fulani mtakwua mkibadilishana na kijana wako, ukitaka lakini…’akasema.

‘Lakini yeye bado kijana anazihitajia sana kuliko mimi…’nikamwambia

‘Sasa ni wewe mwenyewe kuchagua, kama unataka kijana wako aendelee kuwa hivyo, na hatari yake ni kama mnavyoona, yeye ni kjana hajui kujizuia, hana busara, atawaletea keshi humu ndani, bora umnyamazishe kwa hivyo kwanza, na baadae akirejeshewa atajirudi…’akanishauri hivyo.

Basi nikaongea na mama yake nikamwambia kuna dawa natakiwa nimfanyia kijana ili atulie, aachane na mambo hayo.

‘Dawa, kwanini dawa, kwani huwezi kumshauri tu hivi hivi akatulia…?’ akaniuliza.

‘Tumemuita mara ngapi, mke wangu….na tumemkanya mara ngapi…, umeona majibu yake, sasa uamue mwenyewe , tumueche hivyo hivyo au tumtafutie hizo dawa, maana ni wewe unanisumbua kuhusu yeye…’nikasema na mke wangu akasema;

‘Hizo dawa unazitafutia wapi…?’ akaniuliza kwa mashaka.

‘Wewe niruhusu tu, nitazipata, kuna mtu kaniambia zipo dawa za kumdhibiti mtu wa namna hiyo, vinginevyo atazidi kuharibika na hata kuchanganyikiwa, wewe huoni imekuwa ni tatizo sasa…uso wetu tutauweka wapi….au wewe unasemaje mke wangu…’nikamwambia mke wangu nikiwa kama muungwa anayetaka kushirikiana mambo na mke wake, lakini hakujua kuwa mimi ni ndumila kuwili…’akasema akitabasamu ile ya kuumia.

‘Basi sawa ilimradi zisiwe za kishirikina..’mke wangu akasema hivyo
Mimi nikawasiliana na huyo mtaalamu, na kuwa muda huo bado yupo hapa Dar, akiwa na shughuli zake, akaniambia tujiandae usiku, atakuja na watu wake….

‘Na ujue zoezi lilivyo, ni kama lile la siku ile,…sasa sijui mke wako kajiandaaje, lakini tumeshamjulia madhaifu yake hawezi kutushinda,..ila kuna kazi ya ziada, kuna mambo yatakiwa kufanyika kuzimuni…’akaniambia hivyo.

‘Kuzimu ndio wapi..?’ nikamuuliza

‘Makaburini, na huko wewe unatakiwa kuona, utachukuliwa hujijui, ila ukifika huko utarejeshewa fahamu zako, na  utaona yatakayofanyika, ila kijana wako atanyamazishwa…kama ilivyo kawaida yake….’nikaambiwa

‘Kwani ni lazima niyaone hayo mambo yenu ya kichawi…?’ nikamuuliza

‘Ndio kwasababu hayo ni dhidi yako na kijana wako, …inakuwa ni wewe unamfanyia kijana wako..’nikaambiwa

‘Na mama yake je…?’ nikauliza

‘Kawaida njiayetu nikupitia kwa mama yake, atafanya yote kama kawaida, na tukishamaliza mambo ya huko kuzumuni ukirudi wewe ndio utashika usukani, na ukitoka kwa mkeo, ni lazima kuwe na mabinti kama kawaida, hao mabinti ni wa kuwafurahisha vijana wangu,…unanielewa…’nikaambiwa.

 ‘Na itakuwaje kwa mtoto wangu baada ya hapo…?’ nikauliza

‘Itakuwaje kwa vipi, si unataka mtoto wako atulie, atatulia kama awali…’akasema

‘Sawa…’mimi nikakubalia, nikijua kwua kijana wangu atakuwa kama zamani, sikujua kuwa kuna jambo linguine litamtokea….’akasema.

‘Basi usiku hiyo ikafanyika hivyo, nakumbuka kijana sijui ilikuwaje, wakati tupo huko makaburini, ghafla akazindukana na kuanza kukimbia, …na ikawa kazi ya kumtafuta, …lakini alipatikana na kazi ikafanyika kama kawaida…’akasema…

 ‘Asubuhi yake ikawaje…?’ akaulizwa

‘Kijana akawa mgonjwa hatoki kitandani, hatoki nje yeye na ndani tu, …sasa ikawa kuhangaika mimi na mama yake, maana inabid nifanye hivyo, ili mama yake asijuei kinachoendelea,…kijana akawa habadiliki, mpaka mama yake akaanza kukata tamaa..

‘Hivi kijana wangu kawaje tena…?’ akaniuliza

‘Mimi sijui labda ni hizo dawa ndio zimemfanya hivyo…’nikasema

‘Dawa gani ulimpa mtoto wangu…?’ akaniuliza kwa ukali

‘Ni dawa za kumzuia mtu mlevi, aache pombe, na huyo mganga alisema, hali hiyo itatokea lakini itakwisha taratibu taratibu, kwahiyo tusubiria tu mke wangu…’nikasema.

‘Na kama umemfanyia mtoto wangu mambo ya kishirikina hatutaelewana, sizani kama nitaweza kukusamehe kwa hilo, maana wewe mtu sasa sikuelewi elewi…’akaniambia hivyo, na ninachoshukuru ni kuwa mke wangu alikuwa haamini mambo hayo zaidi ya kuhimiza tumpeleke mtoto wetu hospitalini, lakini mimi nikawa nazuia kinamna.

‘Kwanini hukutaka apelekwe hospitalini…?’ nikaulizwa

‘Haikutakiwa kupelekwa hospitalini, vinginevyo angeliharibika kabisa….ndivyo nilivyoambiwa na huyo mtaalamu…’akasema

‘Basi sina hili na lile siku moja nilikuwa nimetoka maana kuna mambo mengine ilibiaidi nisafiri kama alivyotaka huyo mtaalamu, nikawa nimesafiri kufuatilia vifaa fulani, niliporudi, mke wangu akasema alimpeleka kijana hospitalini.

‘Eti nini…kwanini umefanya hivyo, si nilikuambia dawa hizo alizopewa, hazitakiwi kuchanganya na madawa ya hospitalini, sasa utakuwa umemuharibu mtoto..’nikasena nikiwa nahaha sasa…

Na kiukweli, hali ya kijana sasa ikazidi kuwa mbaya zaidi ya hapo, akawa kama kachanganyikiwa kila mara anapiga makelele, wakati mwingine anakimbia na kupotea, tunamtafuta anarudi, akawa sasa ni mtu wa kufunga kamba ndani…anatoa ulimi nje kama mbwa anavyofanya, mtoto akawa sio mtoto bali ni kama dalili za mnyama anavyokuwa…’hapo akatulia.

‘Je hamkuwasiliana na huyo mtaalamu wako ili muone jinsi gani ya kumsaidia…?’ akaulizwa.

‘Tulifanya hivyo yeye,alisema hiyo hali itakwenda na itakuja kutulia baadae, ila sisi tumeharibu kwa kumpeleka mtoto huyo hospitalini,…

Basi muda ukafika akatulia, na wakati huo yale matendo ya kuhamisha zile nguvu kutoka kwake, zikawa zimafanyika na mimi nikawa na nguvu …nguvu za ajabu, ikawa ni shida sasa, yale aliyokuwa akiyafanya kijana yakahamia kwangu, japokuwa mimi nilikuwa nikiyafanya ki utu uzima zaidi.

‘Ukawa unacheza kamari..?’ akaulizwa

‘Ndio, unajua pesa za kishetani hupatikana kwenye njia za kishetani pia, kwenye kamari ndio ilikuwa sehemu ya kukusanya mali, na kila ukicheza hukosi, na hiyo hali ya kupata pesa inakuvutia kucheza zaidi na zaidi, na huko ulevi, umalaya ndio sterehe yenyewe,…na kiukweli kwa mapesa hayo, ni lazima ufanye mambo ya kujionyesha,  ndio nikaanza kujenga majumba, unakumbuka mke wangu alilalamika kuwa nina nyumba mahali,..ndio hizo pesa, lakini utajiri wake haudumu, unajenga nyumba nzuri  ikiisha unauza, au unahonga kwa wanawake…ni utajiri wa shida tu, na muda huo hujitambui, akili inakuwa na kumuhe muhe cha kufanya machafu, starehe, ‘akasema

‘Kwahiyo hata wewe ulikuwa ukiwachukua mabinti wadogo…?’ akaulizwa

‘Ndio..maana ndio makafara ya hao watu wa mtaalamu, ni lazima hayo yafanyike kila akiwahitajia, na mimi usiku kama wamekuja ni lazima nishirikie, kuwepo,, …’akasema.

‘Kwahiyo kumbe ndio wewe ulimpa ujauzito huyo mdada aliyetoa mimba…?’ akaulizwa

‘Hapana, sio mimi, pamoja na mengine pamoja na hata kumtamani huyo binti, kufanya hivyo, sikuweza kwasababu ukumbuke huyo binti ni msichana aliyekuwa akitakiwa na huyo mtaalamu, ni mtu wake, ila alitaka kumfundisha adabu, na akatumia watu wake wengine kumzalilisha…’akasema.

‘Wakina nani hao…?’ akaulizwa

‘Mimi siwajui, ila anasema ana vijana wake, ana watu wake ambao hutembea naye usiku na hao ndio wanatumiwa kushiriki na hao mabinti wakichukua makafara yao…’akasema.

‘Kwahiyo tuseme kuwa kwa upande wako hao mabinti wa usiku ulikuwa huhusikani nao, hao ni kwa ajili ya hao wachawi ….?’ Akaulizwa

‘Ndio….’akasema

‘Je si hayo mambo ya kutuma mabinti na kuhamisha nyota yalishakamilika kwanini sasa muendelee kuwazalilisha watoto wa watu usiku ..?’ akaulizwa.

‘Hayo mambo ya muda wake kila mara kuna namna ya kuyaweka yawe yanafanya kazi, kwa hiyo mara kwa mara wao walikuwa wakija, na kunichukua ili kuwezesha nguvu ziendelee kuwemo, kwahiyo vitendo hivyo vilikuwepo lakini sio kama awali, ni mara moja labda kwa mwezi, au mara mbili hivi…’akasema.

‘Wewe hayo yakitokea ni lazima ujue..?’ akaulizwa
‘Wakitaka kuja wananiarifu kuwa watakuja, ..kama wanakuja kwa kushitukizia ujue wamekuja kwa mambo yao mengine..ambayo mimi sihusiki…’akasema

‘Kijana wako ikawaje..?’ akaulizwa

‘Kijana japokuwa alikuwa kapona kinamna…, lakini hakuwa na nguvu zake, …na hali hiyo ikaanza kumtesa kimawazo, si unajua tena…ikabidi hata aniambia mimi kuwa na hali fulani inamkera…akaniambia ukweli alivyo, na ikabidi sasa nimshauri twende hospitalini.

‘Si uliambiw usiende huko hospitalini…?’ akaulizwa

‘Hio ilikuwa ni awali, kwasasa haikuwa na shida, mimi najua ni kwanini, ila kwa kumuaminisha kijana ikabidi nimshauri hivyo,..twende akapimwe,..na kupimwa ndio ikagundulikana ana magonjwa kama yangu, kisukari ..na shinikizo la damu..yaani yale yale niliyokuwa naumwa mimi ndio sasa anaumwa mtoto wangu, nikajua ni hizo nguvu ndio zimesababisha hayo…

‘Oh, kwahiyo wewe ukawa radhi na hali hiyo ya kijana wako ateseke wewe, uwe kijogoo..au sio…?’ akaulizwa

‘Kiukweli, kwa muda huo sikujali kabisa, niliona ni sawa tu, atulie nyumbani, ilimradi nafahamu ni kwanini, na utajiri ukipatikana itakuwa kwa manufaa ya familia, sio kama ilivyokuwa yeye, utajiri ulikuwa kwa ajili yake tu, na hakutaka kuulizwa…’akasema.
.
‘Kwahiyo kumbe ni kweli, kuwa ukifanya hayo mambo unapata utajiri, japokuwa ni wa kichawi..?’ akaulizwa

‘Ukweli ndio huo kuwa unapata utajiri, lakin kwa kupitia njia za kishetani..unafanya mambo mabaya sana..mengine siwezi hata kusimulia, na mbaya zaidi huwezi kufaidi huo utajiri maana unaumiza wengine, unaumiza hata familia yako, na wakati wote huna amani, kila muda una mawazo kuwa huenda nikajulikana huenda watu wananiona huenda…halafu shughuli unazozofanya kwa jamii, ni za kukuzaraulisha tu japokuwa mwenyewe unajifanya hujali…’akasema

‘ Sasa ikawaje kwa kijana wako….?’ Akaulizwa.
.
‘Nilianza kukaa naye kumshauri, na nilimuahidi kuwa kila anachotaka nitampa, lakini hakuwa na raha kabisa,..unajua tena hali ya kibindamu ilivyo, ulikuwa hivi, mwanume sasa unajiona tofauti, huna kazi, alizoea kubadili mabinti sasa akiwaleta anaishia kuabika tu…, na taarifa zikawa zinazagaa kuwa kijana hana nguvu tena..ikawa ni aibu na ikawa inamtesa sana kisaikolojia…’akasema

‘Mungu wangu ikawaje sasa…?’ akaulizwa

‘Ndio hapo akaanza kutumia pombe zaidi kupitiliza,…, na hakutosheka na hilo, akaanza kutumia madawa ya kulevya

‘Mungu wangu, kwanini, na wewe ulijua hilo…?’ akaulizwa

‘Mimi nilijua, ila mama yake alikuwa hajui kuwa kijana wake kaanza kutumia madawa ya kulevya, nikawa namtetea na kuificha hiyo hali, na nikawa najaribu kumshauri kijana wangu aachane na madawa kwani ni mabaya zaidi…

‘Sasa kwanini uifiche wakati unajua kijana anaharibika kwasababu yako…?’ akaulizwa

‘Mtaalamu aliniambia nisimzuie kwa yale anayoyafanya , maana yatakuja kuisha kwa muda muafaka,… ni mambo ya muda tu, lakini hayo hayakuwa kweli..nikaona kama huyu mtu hamtakii mema kijana wangu…’akasema

‘Kwanini sio kweli..?’ akaulizwa

‘Kwasababu kipindi kile kijana wangu akiwa kijogoo, yule binti wa awali alishafika, huyu mtaalamu kume aligundua kuwa kijana wangu kampenda huyo binti, na akagundua kuwa wana mahusiano ya siri…’akasema

‘Kwa vipi sasa kijana nguvu zake ulishazichukua..au ilikuwa bado…hapo unatuchanganya?’akaambiwa

‘ Huyo binti alikuja muda, ..na muda aliofika niikuwa bado zitazichukua, hizo nguvu kutoka kwa kijana,..na nilikuja kugundua baadae kuwa kumbe huyo mtaalamu alifanya hivyo kumuadhibu kijana wangu, pamoja na mengine …’akasema.

‘Ikawaje sasa,….je huyo mtaalamu hakutaka kumsamehe huyo kijana wako…?’ akaulizwa

 Ghafla ndio huyo mtaalamu akaanza kuzidiwa zaidi,…tatizo lake likazidi kuwa kubwa zaidi, awali sikujua ni tatizo gani, hadi alipofika kuniambia kuwa kagundulika ana ugonjwa mbaya, ila anahisi kuwa mbaya wake ndiye kamfanyia hivyo.

‘Lakini wewe si ulikuwa na pesa kwanini sasa alikimbilia kuomba kwa akina mama, au kipndi hicho alichokuja kuomba pesa ilikuwa bado,…?’ akaulizwa

‘Kipindi hicho, ilikuwa bado, kipindi anakuja kuomba pesa, ni kipindi hali imebadilika hata kwangu….’akasema

‘Ehee, endelea…..’akaambiwa

‘Kukawa kunakuja taarifa kuwa kwa wakwe zangu hali yao ni mbaya, kiuchumi,

 ‘Kwahiyo kumbe kweli nyota iliondoka kule kwao na kuja huko kwenu au sio…?’ akaulizwa

‘Hapo mimi sijui, ila kiukweli, wazazi wa mke wangu walikuwa na hali mbaya, na mimi nikitaka kuwasaidia lakini wao walikataa kabisa, waliniambi wazi wazi kuwa wao hawataki pesa za kishetani….

‘Oh, ina maana wao walishajua kuwa pesa zako ni za kishetani…?’ akaulizwa

‘Wao waliniambia hivyo, na sikuwa na muda wa kuwafuatilia kwa nini wanasema hivyo, ila walikuja kumuita mke wangu wakamkanya kunihusu mimi, na kipindi hicho ndio mke wangu akaanza kunifuatilia kwa karibu, …’akatulia.

‘Haya sasa tuambie kuhusu yaliyotokea kwa hao mabinti wawili….maana naona umefikia kipindi chao, ilikuwaje maana mama alisema kuna mambo mabaya mliwafanyia wao..?’ Akaulizwa

 ‘Kama nilivyosema binti wa mwanzo nisingeliweza kumgusa, japokuwa nilifanya juhudi hizo mara kwa mara, na wakati mwingine naamua kwenda kwake usiku,lakini kila nilipojaribu nilijikuta nikikutana na huyo mtaalamu.

‘Unakutana naye kwa vipi, yeye si anakuja humuoni,…?’ akaulizwa

‘Simuoni ila ananifanyia mambo yanayo-onyesha kuwa yupo….’akasema

‘Sasa yeye anajuaje kuwa wewe unakuja kwa huyo binti…?’ akaulizwa
.
‘Sijui anajuaje, sio kila siku, ila siku ambazo, navutika kwenda kwa huyo binti, ndio siku nakutana naye, na yeye, ananiuliza nimefuta nini kwa mke wake…na hata kesho yake lazima atanipigia simu kuniuliza na kunikanya, kuwa nisipoacha hiyo tabia atanifanya kitu kibaya sana….’akasema.

‘Mke wake!!!..kwanini anamuita mke wake…?’ akaulizwa

‘Yeye anadai alishamuoa kimzimu, kwahiyo ni mke wake kihivyo…’akasema.

‘Kwahiyo yawezekana mimba iliyotolewa ya huyo binti ni ya huyo mzee..au sio…?’ akaulizwa.

‘Hapo mimi sijui….maana siku ilipotolewa, huyo mjamaa alikasirika sana kuwa huyo binti kamfanyia kitu kibaya, na zaidi kajiunga na adui yake kummaliza yeye, na kwahiyo anafanya kila njia kuhakikisha huyo binti anamrejea yeye.

‘Oh, sasa ikawaje…?’ akaulizwa

‘Muda huo ndio vita ikapamba moto, kati ya hao watu wawli....mimi muda huo sina hili wala lile kumbe wajamaa wanapambana usiku na mchana, na ndio ikaja huyo binti mpya…huyu hapa…’akasema

‘Je hayo ya kumleta huyu binti mpya ilitokea kwa amri ya huyo mjamaa, kuwa huyo binti aondoke hapo, mlete mwingine au ni wewe na mke wako mlipanga hivyo…?’ akaulizwa

‘Ni amri ya huyo jamaa aliniambia hapo nyumbani kwangu mambo yanaanza kuwa mabaya, tumeingiliwa, kwahiyo tutafuta makao mapya ya kufanyia shughuli zetu, na huyo binti aliyepo humo aondolewe, tutafuta binti mwingine, na ndipo nikamshauri mke wangu atafute binti mwingine, na alipokwenda huko kijijini ndio akaja na huyo binti …’akasema.

‘Shughuli gani hizo zilihitajika kufanyika kwingine..?’akaulizwa

‘Si nimekuambia, hayo mambo yalihitajia kuyaongezea nguvu ili yaweze kufanyaa kazi, yana-expire, kwahiyo yanahitajia kuwa activiwa…labda niseme hivyo kwa kiingereza…’akasema.

‘Kwahiyo mkafanyaje…?’ akaulizwa

‘Huyo binti akaondoka pale, na kuhamia huko kwa rafiki wa mke wangu, na huko ndio hao wachawi wakaweka makao mapya,..lakini haikuwa rahisi kihivyo, …’akasema

‘Kwanini…?’ akaulizwa.

‘Huyo binti alishajiunga na huyo adui wa jamaa, akawa kapata namna ya kujilinda, na huko kwenye hiyo nyumba alipokwenda wenyeji wake ni wacha mungu, hawaingiliki ovyo…ndio akaja na hoja ile ya kuondoa makafara…nia yake ni kuweza kuweka mambo yake…lakini kama mlivyoona haikuwa kazi rahisi, na yeye hali yake kiafya ikazidi kuwa mbaya, akawa sasa analemewa na adui yake…’akasema

‘Kwahiyo na wewe ikawaje…?’ akulizwa

‘Sasa kwa vile hayo mambo hayafanyiki tena, madawa na zile nguvu za kishetani zikawa zinaisha nguvu, mimi nikawa naanza kuishiwa nguvu, mambo yakaanza kuwa mabaya, madeni,..kamari, ukicheza hushindi, unaishia kukopa, kulipa siwezi, nikaishia kunyang’anywa nyumba, magari…hali ikaanza kuwa mbaya sasa …’akasema

Na siku moja kijana wangu akanitaka tuongee, kipindi hicho naanza kuchanganyikiwa, jamaa mtaalamu hapatikani na akipatikana analalamika hali mbaya anahitajia pesa za matibabu, hana pesa, nimsaidie au nitaishia kubaya, na leo kijana wangu ananiita, sikutaka kabisa kuongea naye…

‘Mliongea naye, ..alikuambia nini…?’ akaulizwa

‘Baba nimegundua kuwa matatizo haya niliyo nayo sababu kubwa ni wewe, umenifanyia hivi ili nifirisike ili nisiwe tajiri, umenipa madawa ya kuniharibia nguvu zangu za kiume,… ili nisiwe natembea na wasichana warembo umenionea wivu na kunifanya..hivi sasa nakupa wiki moja tu, unirejeshee hali yangu la sivyo , nitamuambia mama haya yanayoendelea humu ndani….’akaniambia hivyo na kuondoka.

‘Sasa ilikuwaje….?’ Aakulizwa

‘Nikawasaliana na mtaalamu, na mtaalamu akasema dawa ipo hapo hapo nyumbani, …huyo binti mpya ndiye kafara, kwani ana sifa zote…nisiwe na wasiwsi atayamaliza hayo, ila mimi hali yangu itawa vigumu kuirejeshwa kwani mambo yameharibika, na kijana ili afanyiwe hivyo, kuna mambo makubwa yanatakiwa kufanyika, nitafute mbwa..…’akasema mzee sasa akiona aibu kuniangalia mimi machoni.

‘Mbwa wa nini…?’ akaulizwa

NB: Mbwa wa nini….tutakuja kusikia sehemu ijayo..


WAZO LA LEO: Utajiri wa kishetani hata kama utaupata lakini ukumbuke mwisho wake ni mbaya sana,..wengi waliofanya hivyo, wameishia kubaya sana, na kama itatokea ukafariki kabla hujatubu , kifo cha mtu kama huyo kinakuwa kibaya sana, wengine wanafikia kuoza wakiwa wazima, na mambo mengi mabaya hutokea kwa watu hawa hata kabla ya kukata roho, jamani tumuogope mola wetu, kwani hayo tunayoyataka ya utajiri ni vitu tu vya kupita, na mwisho wake tutarejea kwa yule aliyetuumba, je unajuaje kuwa utaupata huo utajiri na kuendelea kuutumia, hukumbuki kuwa siku ya kufa ni siri ya mola pekee…tutubie na tuache…
Ni mimi: emu-three

No comments :