Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, July 31, 2017

DUWA LA KUKU...25Japokuwa, jamaa alionekana kuwa na hali mbaya, lakini akajitutumua, na lakini alionekana kuongea kwa shida, na wale akina mama wakaangaliana na wakawa wanatoleana ishara….Nilivyowaangalia mimi nikajua wanaonyeshana ishara kuwa jamaa anaigiza tu ili kukwepa maswali.

‘Vipi hali imekuwaje mtaalamu..mbona upo hivyo, au unataka kukimbia maswali yetu, usihofu nia ni kutaka kukusaidia tu wewe…kama tulivyokuambia awali..’akaambiwa.

‘Hapana, sio kwamba nataka kukwepa maswali yenu,..kiukweli kuna hali napamabana nayo, hamuwezi kuiona,.. najisikia vibaya tu, lakini tuendee tu, nipo sawa sasa nimeshinda….oh, kazi kweli kweli,..’akasema na kujinyosha halafu akasema;

‘Na hayo masharti mengine yanasemaje…?’ akasema kuuliza, huku akishika kichwa.

Kama hakuna matatizo, basi tuendelee maana docta alisema ukiwa hujisikii vyema tuachane na wewe, hata hivyo muda umekwisha, lakini ni muhimu tukakubaliana ili tukija tena tunakuja kuwekeana sahihi ya makubaliano, au sio, na kuendelea na mchakato mwingine, ila muhimu kuanzia sasa uanze kuyaondoa hayo mazindiko yako uliyoyaweka huko majumbani kwetu…tumekubaliana na hilo au sio..?’ akaulizwa

‘Mhh..sawa…huyu mtu bila kumuondoa, atanitesa….’akasema.

‘Unasemaje..mtu gani…?’ akaulizwa

‘Hapana, ni mambo yangu napambana nayo kichwani, tuendelee tu….’akasema.

‘Kwahiyo kwanza uifanye hiyo kazi, uyaondoe hayo mazindiko uliyosema yapo majumbani kwetu , ukifanya hilo tutaweza kuendelea na mengine, kama tutakavyokubaliana…’akaambiwa.

‘Nitayaondoaje hayo mazindiko…?’ akauliza.

‘Wewe si ndio umeyaweka, kwahiyo unajua jinsi gani ya kuyaondoa, au…?’ akaulizwa.

‘Mimi nipo hapa hospitalini, na kwanini mnasema ni mimi nimeyaweka, sijasema hivyo, kuwa mimi ndiyo nimeyaweka jamani,….’akasema.

‘Sasa ni nani,… ‘ wakasema wale mama  kwa pamoja.

Jamaa aliposikia hao akina mama wakisema kwa pamoja tena kwa hasira, akainu uso na kuwaangalia mmoja mmoja, kama anawahesabu, halafu akatulia kimia, hakujibu kitu, na mama muuliza maswali akasema

‘Tuambie ni nani, kwasabbu tokea awali ulishakubali kuwa ni wewe, unahusika na mauchafu hayo, tusipotezeane muda hapa, unajua hili ni kwa manufaa yako, ukumbuke nilivyokuambia awali, usipokubaliana nasi, basi tutachukua hatua nyingine, wapo mashahidi, na mmojawapo anakujua kuliko unavyofikiria, na kile kifaa pale kilishachukua mazungumzo yetu yote…’akaulizwa hivyo, huku huyo mama akimuonyesha kwa kidole kile chombo kilichopo.

‘Tatizo nyie watu hamnielewi, hebu jiuliizeni tu,…kwanini kama ni mimi nimeyaweka hayo mazindiko, kwanini tena niwe mimi wa kuja kuyatoa, yaani mimi niwe nacheza mchezo wa kuigiza, mimi sina tabia hiyo, tatizo ni kuwa hamjafahamu nilivyo,..ila nafahamu ni nani kayaweka,…, na kwanini kafanya hivyo, ndio maana nikajitolea kuja kuwaambia, katika namna ya kupambana naye, ni adui yangu mkubwa sana na ndiye …aah…’akashika kifuani kama kun akitu kimemchoma..

‘Vipi tena….?’ Akaulizwa, akabakia kimia akiwa anatoa jasho, baadae akasema;

‘Haya tuendelee, mimi nawasikiliza nyie.., nitafanya mtakavyo, ila munielewe hivyo….’akasema

‘Hapo sawa, sasa pamoja na masharti hayo, kwa vile nia yetu ni kukusaidia, ili uondokane na mauchafu hayo, sisi tutahitajia uharibu uchawi wako wote… maana ukishatubu, huhitajiki kuendelea na madhambi hayo tena, hilo ni ombi kwetu na sharti la mwisho…, na kama ukiendelea kitakachokupata tena usije kutulaumu…’akaambiwa

'Kwa vipi mtalihakikisha hilo, maana nyie hamjui uchawi ni nini, hamjui watu wameupataje, hamjui unavyofany akazi, je ni kikubali kuwa nimeharibu , hivi hivi na bado nikawa naendelea nao, mtajuaje,…niwaambie kitu sio wote wanao-ununua uganga, wengine ni urithi kwa mashinikizo makali sana, wakiuacha, waanishia kubaya…’akasema

'Kwa vipi,…eeh, unauliza kwa vipi,..unajua sisi tutakuamini, si kwa masilahi yako, kwani wewe unaweza kushidnana na mungu, kiapo chako kitawekezwa kwenye nguvu za mwenyezimungu, kama utaweza kushindana naye haya, hata hivyo, wapo watu wa kutusaidia, ambao ni zaidi yako…’akaambiwa

‘Mhh, nani hao, ambao ni zaidi yangu, nitafurahi kuwafahamu, ….’akasema

‘Unajua mzee, wapo wenzako tena wa karibu yako mnaoshirikiana nao, wanakufahamu uwezo wako wote, na wao wameshaamua kuachana na mambo hayo na wapo tayari kushirikiana na sisi,  wametubu na sasa wapo kwenye michakao ya kuharibu uchawi wao wote…’akaambiwa.

‘Hahaha, kweli nyie mnanichekesha, hivi mnafikiri hilo ni jambo rahisi kihivyo,…saa, mimi sijui, labda mniambia ni akina nani,..mkinitajia nitaweza kuwashauri kama kweli wamesema kweli au uwongo…?’ akauliza na kuto hayo maelezo.

‘Hao hao waliokuwa walimu wako,….’akaambiwa na hapo akatoa jicho la kushtuka, na kusema.

‘Walimu wangu…mmh, ajabu kabisa, ni  akina nani, …mimi sina mwalimu, mwalimu wangu wa uganga, ni nani huyo, maana mimi nimepitia sehemu mbali mbali hadi kufikia hapa,..na niwaambie ukweli, uganga wangu nimeurithi kutoka kwa mababu zangu, mengine ni ziada tu…’akasema

‘Tatizo lako bado hujaamua kusema ukweli..hujaamua kutubu, hujajua kuwa hapo ulipo umefikia kubaya, hebu tukuulize unajua mguu wako una tatizo gani..?’ akaulizwa na yeye akainama kuuangalia mguu wake, na kusema;

‘Najua, nimeshaongea na docta, wameniambia tatizo ni nini… lakini mimi nafahamu jinsi gani ya kujitibia, magonjwa kama haya nimekuwa nikiwatibia watu wengi, wamepona, ulizeni huko ninapotokea,..lakini hili la kwangu limekuwa la aina yake, nahisi ndio katika vita hivi na maadui zangu…’akatulia.

‘Kwahiyo una imani kuwa matatizo yako hayo yanatokana na maadui zako..?’ akaulizwa.

‘Mhh…naweza kusema hivyo, na mizimu nayo imenigeuka, lakini, sikuwa na jinsi,..hata hivyo, bado sijakata tamaa, na wao watu wangu wanajaribu kunipima, hawawezi kuniacha…’akasema hivyo.

‘Kwahiyo mpaka unafikia hapo kutaka msaada kwetu si ina maana mumeshindwa…?’ akaulizwa

‘Kushindwa, sio kwa maana sijui madawa yake,  ila kuna madawa mengi natakiwa kuyapata, yanatokea mbali, huko yana bei sana…hali yangu imekuwa ikizidi siku baada ya siku …sasa nikaona nije huku hospitalini, labda kuna njia rahisi, kumbe ndio nimejiweka kitanzi,..hakuna wanachokifanya hapa, nimeona nimekuja bure tu.. vipimo, vipimo..lakini eeh, sawa ngoje nivute subira tu…’akasema.

‘Je ukiambiwa mguu huo ukatwe utasemaje…?’ akaulizwa
‘Kwanini ukatwe, haaah, we mguu wangu ukatwe hapana, hilo sikubali, nilishawaambia, waliniambia hivyo, awali nikagoma, …baadae wakaenda huko na vipimo vyao, wakaja na shauri hilo kuwa , ili nipone natakiwa kwenda kutibiwa India,..hilo hata mizimu yangu umekubali..lakini kwenda huko sasa, ooh, gharama,  ndio nikaanza mchakato wa kutafuta pesa,..hata hivyo, ..aah, sijui kwanini..’akasema akitikisa kichwa.

‘Wewe unahisi kwa tiba zako utapona, sio umeshashindwa na je una uhakika gani kuwa utapata msaada wa kwenda kutibiwa huko India…?’ akaulizwa.

‘Kama nikipata hizo dawa zangu nitaweza kujitibia mwenyewe,..lakini sasa kwa hilo inaniwia vigumu, maana kuna mtu ananipiga vita, kila nifanyalo yupo nyuma yangu,…muda mfupi uliopita alinitembelea hapa, hamkumuona tu,…ndio mkaniona kimia, nilikuwa napambana naye, kakimbia, nilichomfanya hatakisahau, alijua nipi bure bure hapa..…’akasema.

‘Ni nani huyo..?’ akaulizwa.

‘Siwezi kuwatajia,…maana huenda ni mshirika wenu keshawahadaa, sasa anataka kunipata kwa kutumia mgongo wenu, haniwezi,..’akasema na kabla hajatulia mara akatoa jicho, kama kaona kitu mbele yake, akakunja uso, alionekana anahisi maumivu, ..jasho likawa linamtoka…akawa anaongea lugha ya aina yake huku anahangaika pale alipokaa,…baadae akatulia, akawa anahema kweli kweli…

‘Kama haupo sawa, basi tutakuja kesho…’akaambiwa.

‘Hapana ya kesho hayo mengine, …hamjui mwenzenu nipo vitani, natamani niondoke humu…nyie tuendelee tu maana nataka mkitoka hapa na mimi niwe na tumaini .. nawategemea nyie, lakini pia mkumbuke kuwa na nyie ndio mnanitegemea mimi ili niweze kuwasaidia, kwa hilo tatizo lenu….mna matatizo kwenye majumba yenu, hilo tatizo mimi nalifahamu jinsi gani ya kuwasaidia, lakini linahitajia haraka, mkinikosa mimi litawaumiza, na mtaishia kudanganywa tu…’akasema.

‘Mbona wenzako wamesema ni tatizo dogo tu…wewe naona ni zako za kutaka kutupata kirahisi,. Na hayo wamesema ni mazindiko ya watu wameyaweka, kututishia, na kutesa wengine, na wewe upo nyuma ya hilo, hawajasema ni wewe, ila upo nyuma ya hilo…’akaambiwa.

‘Umeona kama ni mimi wasingelisita kunitaja kwa vile ni maadui zangu, wanafahamu kuwa sio mimi, ila mimi ndiye naweza kuyaondoa kwa urahisi, wao, watakuwa wanabahatisha tu…na mniombee niendelee kuishi,la sivyo,..sijui, mimi siwatishi, lakini….’akatikisa kichwa.

‘Tukuambie ukweli, wenzako walikuwa kama wewe, tumeongea nao, na sasa wamekubali kutoa ushirikiano, wamekubali kuachana na mambo hayo, kwani wameona hayana faida kwao….kama ni uganga, basi wataendelea nao kwa nia njema kabisa tu, imebakia ni wewe, kwanini unakuwa mgumu hivyo,…’akaambiwa.

'Ni nani hao, wanaowadanganya hivyo, mmh, nyie hamjui tu…?’ akauliza tena.

'Huna haja ya kuwafahamu, ukikubalina nasi, basi utawafahamu, kwasababu mtakutana katika hali ya kubadilshana mawazo na mnatakiwa muungane ili muweze kubuni njia mbadala ya maisha mazuri, kuliko kutegemea maisha hayo ya kutesa wengine, ifike sehemu mjirudi, hivi hamumuogopi mungu…..’akaambiwa.

 'Mimi nina imani, nitapona, mimi nina imani sina matatizo kama hao wengine, tatizo langu limtokea kwa vile nimeamua kupambana nao, baada ya kutaka kunigeuka, na jingine kwa vile na mimi nimekengeuka kugoma kufuatilia mambo ya mizimu, wakati mwingine najuta kwanini nilikubali haya mambo, nakuwa sina uhuru wa maisha…’akasema.

 'Sasa unasemaje maana muda umekwisha, anza kazi, yako, haraka, kwa kuondoa hayo mazindiko yako, mengine tutaendelea hatua kwa hatu,au sio wenzangu..?’ huyo mama akasema na kuwageukia wenzake.

‘Sawa kabisa sisi tunamsikiliza yeye,….’wakasema hao akina mama wengine.

‘Kwa hilo lenu siwezi kulifanya nikiwa humu hospitalini, siwezi kuwadanganya, mimi sina tabia hiyo ya uwongo, hayo mambo yenu nitaweza kupambana nayo nikiwa majumbani kwenu, ana kwa ana, na kama kuna mtu kawaambia ataweza haya nendeni mkafanyiwe, lakini nina uhakika mtakuja kurudi hapa kwangu, na muombe mungu niwe bado sijaondoka,..…’akasema na ghafla, akashika kifuani tena na kukunja uso, kuashiria maumivu.

‘Kuondoka, kwenda wapi…?’ wakauliza

‘Huko kwenye mat-t-tibabu,..ooh, ole wako…’akasema kwa shida

‘Basi sisi tukuache kwanza, naona hauko vyema, au…, … tutaongea na docta tuone atakavyoweza kukusaidia, ili ikiwezekana utoke kwanza ukayaondoe hayo mazindiko yako, na huku michakato yako ya kutibiwa ikiendelea …’akaambiwa

'Tatizo, hamjui ubaya wa hayo mazindiko mliyowekewa, ,…nawaambia mkiondoka hapa, mnaweza kuanza kupagawa, na hebu fikiria mkibadilika akili mkawa hamjijui ni nani atawafuatilia, na labda mimi nitakuwa sipo, mtapata shida sana, nawaonea sana huruma…’akasema.

‘Sasa kwahiyo unasemaje ..?’ akaulizwa.

‘Kuna mtu kasema anaweza kuyafanyia kazi, kama wewe utagoma,..’akaambiwa
‘Tatizo la waganga wa kienyeji, wengi wao hawatki kusema ukweli, sawa watajaribu lakini watafikia sehemu watashidnwa, na muda huo mumeshaliwa pesa zenu na kiendacho kwa mganga hakirudi au sio….’akasema

‘Lakini yeye ni mwalimu wako, kakufundisha wewe, sasa kwanini yeye ashindwe….’akaambiwa

'Nani mwalimu wangu, yupo huyooo….?’ Akauliza akiwa kakunja uso, na akatikisa kichwa huku na kule halafu akasema
‘Oooh, ni huyo muhini, ....sasa nimewaelewa, nilikuwa najiuliza ni nani huyo aliyewadanganya, kumbe ni huyu, wewe…unanitafutia nini, nitakuumiza,sitajali kuwa wewe ni mwalimu wangu…’akasema sasa akiangalia mbele, ukumbuke sisi tulikuwa tumesimama mbele yake, kwahiyo ni kama alikuwa akituangalia sisi .
 Baadaye akatulia, akahema kama mtu aliyetua mzigo, akasema

‘Kumbe ni huyu muhuni, hahaha, hahaha hana kitu kwa sasa, sawa kiukweli alikuwa anajua madawa, lakini mambo makubwa kama hayo, hana uwezo nayo kwasasa, anachojua yeye,  kwasasa kwa vile keshanyang’anywa karibu kila kitu anachofanya ni kucheza mazingaumbwe…uwawekezea watu mazindiko, na hapo hapo anakuja kuyatoa, ni mazingaumwe tu aliyobakia nayo…’akasema.

‘Kwahiyo yeye, ni kweli alikuwa mwalimu wako…?’ akaulizwa.

‘Hilo nalikubali, ni kweli siku nilipokabidhiwa mikoba na mababu zangu, walinipeleka kwa mababu wa huyo mtu, na yeye alipewa mikoba kabla, na hao watu, nilipofikishwa kwa hao mababu nikaambiwa huyi atakuwa ndiye mwalimu wangu, na kweli alikuwa anajua sana…na hakujua kuwa na mimi nilikuwa mwepesi wa kujifunza haraka sana..hakuamini hilo…’akatulia.

‘Kwahiyo ukawa sawa na yeye..au ukamzidi..?’ akaulizwa.

‘Kuna mambo hakutaka kunifundisha, kama angelifundisha wakati huo ningelikuwa zaidi yake kwa kipindi hicho na iisngelikuwa na maana ya kukaa kuendelea kuwa mwanafunzi wake tena…lakini tatizo lake kubwa alikuwa mchoyo, na si mchoyo tu akawa anatutumia sisi kufanikisha malengo yake mabaya…’akasema.

‘Kwa vipi…?’ akaulizwa.

'Uganga, na hasa uchawi, umegubikwa na matambiko, na makafara, na tofauti kubwa ya mchawi na mganga unaweza kuuona kwenye hayo mambo mawili, matambiko, na makafara, ila waganga wengi wasiojihusisha na mambo hayo wanakuwa na utaalamu wa madawa tu, ukiona mganga kakuingizo kwenye hayo mambo mawili uwe makini sana, ….’akasema.

 'Wachawi wao wapo tayari kutoa makafara ya damu za watu, kuua kwao ni kitu rahisi tu…nia ni  ili wafanikiwe zaidi, na wanafanya hivyo kwa kuwatumia mashetani wenye nguvu, ambao wanahitajia damu za watu. Mashetani ndio watumishi wao, kwa ujira wa damu za watu..na maagano yao ni makali zaidi, wakokosea na wao wanadhurika,…sasa yeye katika kutufundisha hayo, akawa anatuelekeza hayo kwa kutupima…, tufanye hayo kwa vitendo, anatutuma kutafuta damu za watu…’akasema.

'Kwahiyo mkawa mnaua, ili mpate damu au…?’ akaulizwa

‘Unajua sisi tulikuwa wanafunzi, na wanafunzi, kama walivyo wanakuwa na uchu wa kujua, na wakati mwingine huwezi kuwa makini na unachokifanya, kwasabau hukijui, na kama unajua ni hivyo, bado, unamtegemea mwalimu wako kuwa ataweza kuzuia kwa namna nyingine, kama ni majaribio tu ya kawaidia..sijui mnanielewa,  maana mwalimu yeye ndio anafahamu matokea yake, sisi tulikuwa tunafanya kile tunachoagizwa, tukijua ni sehemu ya mafunzo…’akatulia.

'Sawa kwahiyo mkiagizwa kuua, mnaua si ndio hivyo,…, kwa maelekezo ya huyo mwalimu wenu, si ndio hivyo,….?’ Akaulizwa.

‘Lakini sisi hatukujua madhara yake, kwa upande huo, na tuliambiwa tusipofanya hivyo, sisi au familia zenu ndio zinatakiwa kukamilisha makafara hayo…’akajitetea.

‘Kuua si kuua, madhara ya kuua, ni nini hapo, kwa kifupi mlikuwa mnaua lakini kutokana na maelekzo ya mwalimu wenu au sio.?’ Akaulizwa.

‘Nina maana hivi, kwasababu sio unakwenda unamuua mtu hivi moja kwa moja, unaambia fanyeni hivi na vile, halafu mtaona kitakachotokea, eeh, sisi tunafanya, tunasubiria, mara  haipiti muda, huyo mtu anakutwa na mabalaa, ajali, au chochote, au wakati mwingine huyo mtu anapoteza maisha, baadae tunaambiwa twende kwake, tukafanye jambo…’akasema

‘Jambo kama lipi..?’ akaulizwa na hapo akasita kidogo , baadae akasema;

‘Kama ni ajali, tunawahi damu yake, kama…ni viungo vyake vinahitajika, tunaviwahi kabla hajafa…maana vinahitajika vikiwa na moto, na vitu kama hivyo…’akasema.

‘Oh…ina maana ajali nyingine sio ajali za kawaida…mnatengeneza nyie…?’ akaulizwa.

‘Sisi tulikuwa hatujui, unielewe hapo, mpaka tulipofikia hatua ya kujua, ndio tukagundua kumbe tulikuwa tunatumiwa, na wale walioamua kuachana naye, na kuwa watu safi wakafanya hivyo, ila wale waliozidiwa na mambo hayo wakaona ni mambo ya kawaida tu wameshagibikwa na ibilisi.., wakabobea huko kwenye uchawi….’akasema.

‘Wewe ulifanyaje, si uliendelea naye, usitudanganye hapo..?’ akaulizwa.

‘Kwa vile mimi nilikabidhiwa kwa huyo mtu, haikuwa kazi rahisi kwangu kuachana naye, nikaendelea kuwa naye lakini huku nikitafuta mwanya wa kumzidi nguvu, kwa kuyafahamu hayo anayoyajua ambayo ndio yanamfanya awe zaidi ya sisi, na nikawa nagoma kuyafanya yale ambayo najua yanamadhara kwa watu ndio hapo tukaanza kusigishana…’akasema.

‘Kwahiyo ukafanikiwa..au ilikuwaje?’ akaulizwa.

‘Haikuwa kazi rahisi, nilianza kukosana naye zaidi na hata kutengana naye, pale aliponiambia, nahitajika kuua mtoto wangu, ili niweze kukabidhiwa mikoba yangu…’akasema

‘Mikoba yako, kwa vipi, kwani ni yeye alitakiwa kukupa au …wewe si ulisema uganga wako ni kutokana na mababu zako,…?’ akaulizwa.

‘Mikoba yangu alipewa yeye, ili nikiiva, na kuwa tayari ndio anikabidhi, na nisipo kabidhiwa kuna madhara nitayapata mimi na familia yangu,…na hatua niliyofikia sikutakiwa kuikosa, hata niliposema, niachane naye, ikawa siwezi, kuachana naye, ningeharibikiwa kabisa, na mabaya yangeniandama…’akasema.

‘Kwahiyo ukafanya hivyo..?’ akaulizwa

‘Awali hakuniambia moja kwa moja nahitajika kumuua mtoto wangu, aliniambia, nahitajia, kupata nguvu, ili niweze kuyabeba hayo majukumu, na nguvu hizo zipo kwenye viumbe vizivyo na dhambi, ..’akasema.

‘Viumbe gani hivyo…?’ akaulizwa

‘Mfano watoto wadogo….’akasema.

'Mungu wangu, kumbe ni kweli...'akasema mdada akimuangalia huyo jamaa kwa macho yaliyojaa chuki.

'Kweli nini…kuwa mimi nilimuaa mtoto wangu mwenyewe , hapana wewe hujui tu, kwanini mnakimbilia kunishutumu kabla amjasikia ilivyokuwa,…’akauliza alipomuona mdada anamuangalia hivyo.

‘Si ndivyo ulivyofanya, uliua mtoto wako ili upate huo mkoba, ni kweli, usibishe, uliwahi kuniambia,….’akasema huyo mdada

‘Hebu subiri kwanza , …’akasema huyo mama akimzuia huyo mdada asiongee zaidi.

‘Kwahiyo huyo mwalimu wako, alikuambia kuwa ili akukabidhi hicho kijiti, au mkoba, ili ufuzu mafunzo yako, inahitajika damu ya viumbe visivyo na dhambi, ambavyo uliambiwa ni watoto wadogo, si ndio hivyo…?’ akaulizwa

‘Ndio hivyo….’akasema

‘Kwahiyo ukatakiwa utafute damu ya mtoto mdogo, ..?’ akaulizwa

‘Ndio, lakini hakusema hivyo kuwa damu kwa maana ya kuua, hapana alisema, tunahitajika damu ya  viumbe hivyo, vipatikane vifanyiwe kafara, na vitakuwa kama kinga yetu,…’akasema

‘Kwa vipi..kafara ni nini hapo, si ina maana kuua, ili damu itoke, au tueleweshe hapo zaidi..?’ akaulizwa
‘Ina maana ukitaka kupambana na adui, mtoto huyo anakuwa ngao yako, sio lazima kila siku, ndivyo alivyotuambia hivyo,…’akasema

‘Hapo naona unakwepa kutuambia ukweli….nikuulize hivi hilo kafara ni nini hasa…?’ akaulizwa

‘Kafara mara nyingi linafanyika kwa kutumia damu….’akasema.

‘Damu ya watu au wanyama..?’ akaulizwa.

‘Kwa mambo ya kichawi, mara nyingi ni damu za watu, mara chache ni damu za wanyama,..lakini kwa huyo mwalimu wetu yeye mara nyingi alikuwa akihitajia damu za watu….’akasema.

‘Kwahiyo nyie kila mara kwenye makafara yenu mkawa mnatafuta damu za watu, si ndio hivyo…?’ akaulizwa

‘Kwa mara chache tulikuwa tunafanya hivyo, hasa..kwa matambiko makubwa sana,…’akasema

‘Sawa hata kama ni machache, ila mliyafanya kwa kutumia  damu za watu…?’ akaulizwa.

‘Ndio…lakini hatukuwa tunajua hayo awali, kama nilivyosema tulikuwa ni wanafunzi tu….’akajitetea.

‘Na sasa ukaambiwa damu ya mtoto mdogo, si ndio hivyo..wakati huo unajua, sio mwanafunzi tena si ndio hivyo…?’ akaulizwa

‘Elewa nilivyokuambia awali, hapa huyu mtu alinitega, akisema anahitajia mtoto kama kinga, yaani ili nipate huo mkoba wangu, ni lazima nimpate mtoto kama kinga yangu…’akasema.

‘Umpate kwa vipi, si kwa kafara au sijui mnaita matambiko au sio…?’ akaulizwa.

‘Hakunifafanulia hivyo awali,..angelisema hivyo ningelijua na ningelichukua tahadhari, nisingelikubali kumchukua mtoto wangu…’akasema.

'Ungelimchukua mtoto wa nani...?' akaulizwa

'Ningelijua , ningejua jinsi gani ya kulikwepa hilo , mbona kuna mengi aliniambia nikakataa, kwanini hilo nisingelikataa,...mimi sio mjinga kiasi hicho....'akasema

‘Kwanini sasa, kwanini mtoto mdogo asiye na dhambi, …hapo tueleweshe kidogo…’akaulizwa.

‘Mhh…hapo alivyonieleza yeye, akinivunga..sijui kwanini nilifunikwa akili nisielewe...aliniambia sasa nimeiva, lakini sio kwamba nimeshafikia hatua ambayo ninaweza kujilinda mwenyewe, lakini kwa hatua niliyofikia, hatua kwa hatua, na kwa jinsi nitakavyopambana na majanga, mitihani nk, kwenye kutibia watu na kwenye kujilinda, ni lazima nitakutana na mitihani mbali mbali, kwahiyo kwa vile bado najifunza kwa vitendo, nahitajia kuwa na ngao…’akasema.

‘Ngao hiyo inatokana na kafara la damu ya mtoto au sio…?’ akaulizwa.

‘Subiri,... unielewe hapo…’akasema

‘Ehee elezea inakuwaje…?’ akaulizwa

‘Katika kuendelea na kazi hizo, nitakutana na mitihani, kutakuwepo na maadui, wengine wanaweza wakawa wametuzidi huwezi kujua, sasa ili uweze kupambana nao, unahitajika kuwa na, ngao ambayo nguvu yake hupatikana kwa watoto wadogo tu, ...…akatuambia hivyo maana tulikuwa watatu, wengine walishaondoka....'akasema.

‘Mkauliza ngao hiyo ni nini, mkaambiwa ni watoto au damu ya watoto wadogo au sio…?’ akaulizwa.

‘Hakufafanua hivyo…yeye alichoendelea kusema ni kuwa kila mmoja atatahiniwa kivyake,..’akasema

‘Uliambiwaje mpaka ukamchukua mtoto wako,..?’ akaulizwa

‘Ili nifanyiwe hilo nimchukue mtoto ambaye, ninaweza kuwa naye mara kwa mara na nitaonyeshwa hatua kwa hatua, jinsi gani inafanya kazi…’akasema

‘Kwahiyo wewe ukamchukua mtoto wako, kwa vile yeye mpo naye mara kwa mara au sio..?' akaulizwa

'Awali, nilimuuliza mtoto yoyote..akasema je unaweza kumchukua mtoto wa atu ukakaa naye muda wote...basi nikasubiria siku moja akasema mlete huyo mtoto…ili tufanye hicho kitendo...'akasema

'Alisema mlete huyo mtoto mfanye nini...?' akaulizwa

'Kafara la kumaliza na kuwa na ngao kwa ajili ya kupewa huo mkoba

'Hapo alitamka kafara si ndio...?' akaulizwa

'Kihivyo, lakini alishafafanua, ni vipi, kwahiyo mimi nilijua sio kafara kama lile....akili hapo ilinituma hivyo...'akasema

'Lakini awali ulisema kafara hufanywaje...'akaulizwa

'Hapo akili ilikuwa imefunikwa kiukweli,...nakumbuka kauli yake ya mwisho alitamka hivyo, kuwa mlete huyo mtoto tumalizie hicho kitendo, cha kafara la mwisho...'akasema

'Ok ikawaje..maana usitudanganye hapo maana kiulimu ulikuwa hatua ya juu, ulishaiva, na ulijua ni nini maana ya kafara, ulijua ni nini kitatendeka kama ni kafara, au sio?’ akaulizwa.

‘Mhh, unajua ni hivi, alisema anahitaji mtoto ambaye utakuwa naye karibu siku zote, na huwezi kumchukua mtoto wa mtu mwingine…hapo elewa, nitakuwa naye siku zote, hiyo ni kauli yake ya awali, …ina maana gani hapo, ni mtoto wako na , kwa vile hata hizo nguvu zitamsaidia na huyo mtoto wako....hayo aliyatamka hivyo..., kwahiyo ina maana nifanye nini...'akauliza

'Jibu wewe ambaye ulifanya....'akaambiwa

'Ni moja kwa moja alimtaka mtoto wangu...'akasema

'Lakini hakuwahi kusema mtoto wako, sema ukweli wako...?' akaulizwa

'Maelezo yake yalilimaanisha hivyo, asijitete bwana...'akasema

'Kwahiyo wewe kwa maelezo yako, na kwa vile ulikuwa na uchu wa kuupata huo mkoba, akili ikafunga, ukawa huna uchungu wa mtoto tena, ukamchukua mtoto kwenye mambo yenu ya kishirikina, sema ukweli na ukiri kosa, hapoo huwezi kuchomoa...'akaambiwa

'Usilazimishe maana haikuwa hivyo unavyofikiria wewe...sikuwa na uchu na huo mkoba,kama huyo mwalimu atasema ukweli ataweza kukuelezea jinsi gani nilivyokuwa nataka kuachana na mambo hayo na yeye ananiwekea mitihani migumu mpaka nakubali kurudi tena, muulizeni kama ataweza kusema ukweli...'akasema

'Kwahiyo wewe  ukamchukua mtoto wako, ili mpate faidi wote wawili ndio kauli yake iliyokufanya uvutike kumchukua mtoto wako au sio…’akasema.

'Ndio hivyo,lakini nikijua nitakuwa naye, kama ngao, katika kazi zangu za kila siku...'akasema

‘Kwahiyo ukamchukua mtoto wako…mkafanya nini hapo..?’ akaulizwa na hapo jamaa akainamisha kichwa chini na alipoinua akawa kajawa na machozi

‘Kiukweli mimi sikujua, ningelijua nisingelifanya hilo..alinihadaa…kwanini nimuue mtoto wangu, …’akalalamika.

‘Tuambie sasa mlifanyaje..mlifany atambiko la kumwaga damu au sio damu ya mtoto mdogo, asiye na dhambi, ili iweje,..uweze kuupata huo mkoba, na mkoba si umeshaupata, si ndio hivyo?’ akaulizwa.

‘Unajua ukiongea hivyo unalazimisha,...yeye hakusema moja kwa moja ni tambiko la kumwaga damu, hakusema hivyo, mwishoni wakati imeshafikia hatua ya mwisho ndio akatamka neno kafara la mwisho...muulizeni vizuri, kauli hiyo aliitamka mwishoni kabisa, na mimi sikuwa na ....utashi, maana nilishajenga hisia kuwa , atakuwa kinga yangu....'akajitetea

'Tuendelee, hapo, sijui.....tuendelee, inauma kwa kweli, ..mimi ni mama na kauli hiyo, inaanza kunifany anitake kulia, kwanini muwe na tamaa kiasi hicho...'akasema

'Najua hadi hapo hamtanielewa, ..lakini hamjui ni mateso gani nilipitia, maana hadi namchukua mtoto nilipitia mateso, niligoma awali, nikaanza kuteswa, silali, muulizeni hata mke wangu, kipindi hicho..'akasema

'Kwanini sasa..?' akaulizwa

'Kwa vile sikutaka familia yangu hata mmoja ije kujihusisha na mambo hayo, siyapendi kabisa...'akasema

'Kwanini..?' akaulizwa

'Ni mabaya...'akasema

'Kwa vipi..?' akaulizwa

'Oh, naona unataka kunitega...'akasema

'Kwasababu ni kazi ya uchawi, sema ukweli, na uchawi kama ulivyosema umegubikwa na makafara ya kuua watu, ili mpate damu zao, na wewe hukupenda mtoto wako apitie huko, kweli si kweli...?' akaulizwa na kukaa kimia

'Haya tuambie ikawaje, maana hapo hata mimi sitaki kusikia, lakini ni lazima useme ili ujikoshe au ujiweke sehemuu ambau sis tutakusamehe...'akaambiwa

'Ndio akaanza kuonyesha jinsi gani ya kujikinga, nikipambana na hao, walionizidi nguvu, akanitupia kombora, akasema, fanya hivi na vile nikafanya, …ooh…’hapo akatulia kimia.

‘Ikawaje,….?’ Akaulizwa jamaa akwa kimia…jamaa alikuwa kaduwaa, macho yamemtoka, hasemi kitu, katulia kama mfu…
Akina mama pale wakashtuka, mmoja akasema;

‘Tumuite docta, mwingine akasogea kutaka kumgusa jamaa,…na mara  mlango ukagongwa kwa nguvu, na mama mmoja, akaenda kuufungu akijua ni docta kaja kwa dharura,…alipotaka kuufungua, huyu mgonjwa akasema kwa sauti kubwa.

‘Usifungue…’ lakini huyo mama alikuwa keshafungua, mlango
 ..
NB: Mhh..hapo sasa


WAZO LA LEO: Usikusudie kutenda dhambi huku unajua, ukiitakidia kuwa utatubu, au hutarudia tena baada ya tendo hilo la dhambi, au unatenda ili upate, ukipata hicho unachotaka kukipata, japo ni kwa njia ya dhambi, utaacha, na kutubu dhambi hizo..SWALI. Je una uhakika gani baada ya kitendo hicho utaweza kutubia, au utafanikiwa kukipata hicho kitu,  au baada ya kufanikiwa utakuwa na utashi wa kutubia, au una uhakika gani, kuwa utaweza kuiona hiyo kesho yake…Dhambi ya kukusudia, ina dhamira ndani yake, ni kufuru..ni heri utende ukiwa hujui na ukijua utatubu, lakini sio kwa kukusudia, ili baadae utubu, tumuogope mola wetu. Tumuombe mola wetu atusaidie, tuweze kuyatenda yaliyo haki, na mabaya tuweze kuyaepuka Aamin.

Ni mimi: emu-three

No comments :