Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 28, 2017

DUWA LA KUKU...23‘Haya tuambie ulisemaje wakati ulipompigia huyu mwenzetu simu .?’

‘Ndio nilimpigia mimi na nilimuambia kama nilivyoongea hapa kuwa majumbani kwenu kuna matatizo, yanahitajika kutolewa….’

‘Kwanini ulifanya hivyo, kwani alikuambia ana shida hiyo, anatafuta mganga,...eti uliwahi kuongea naye kuhusu hilo kabla...? akaumuuliza huyo mama mwenzake.

'Ajibu mwenyewe...'akasema huyo mama mwingine, na jamaa akakaa kimia

'Au labda ni katika namna yako ya kutafuta biashara au kuna jambo gani lilikuvuta mpaka ujue kuwa kwangu na kwa wenzangu kuna matatizo hayo..tuambie usiogope?’

Jamaa akatabasamu , lakini tabasamu la mashaka, akasema;

‘Ni kwa kupitia huyu binti, kama nilivyosema huyu binti nimemfahamu na nilijaribu kufuatilia wapi anapoishi, unajua sisi tukipitisha darubini zetu zinatuashiria kuwa hapa kuna matatizo, kuna ishara zinaonyesha, na ukiwa na nia njema na huyo mtu unaweza kumuambia, na kwenue nikaona hizo ishara, sasa kama mnahitajia msaada wangu, haya, tuongee, kama hamtaki siwezi kuwalazimsiha…’akasema.

‘Lakini wakati mnaongea na mwenzangu alikuuliza swali, ukamjibu, unakumbuka ni swali gani..?’ akaulizwa

‘Mhh, labda unikumbushe….’akasema.

‘Alikuambia wewe ni mchawi, kweli si kweli….’akaulizwa na hapo akainua kichwa akakutana na macho yangu akayakwepesha na kuangalia pembeni, ukumbuke sasa nilikuwa nimesimama karibu na mdada akitupa jicho mbele anatuangalia sisi.

‘Unajua kazi hizi zetu wakati mwingine unahitajia kumvuta mtu, kwa nia mbili, kwanza kumsaidia, na pili, na wewe unahitajia wateja, yote yote ni sawa, ni kweli huyo mama niliongea naye, na akaniuliza hivyo…sasa ili nimpate na kumuwelesha kama hivi, kuwa hayo sio ya kweli, ilibidi nikubali, na pili ndio niwaite…unaona eeh…’akasema.

‘Kwahiyo wewe ni mchawi au sio mchawi..?’ akaulizwa.

‘Nimeshawaambia hayo maneno ni ya uzushi, yanatoka kwenye vinywa vya maadui zangu….’akasema,

‘Lakini ulikubali ukasema zamani ulikuwa na tabia hiyo, lakini kwa hivi sasa umeamua kujirudi, na ili kuwaonyesha watu kuwa umbadilika, mojawapo ni hili kuwa umetuita,..au na unataka kusafisha madhambi yako, au sio, kama kuna sehemu uliweka mambo yako, sasa unataka kuyatoa si ndio hivyo…?’ akaulizwa

‘Hahaha, hapana..usiongeze maneno yako, sio hivyo kabisa,…mimi nimewaitata kwa vile kuna mambo ambayo nilishamuelezea huyu mdada, na yanahitaji kuondolewa, na mazindiko ya uchawi nimeyaona kwenye makazi yenu…’akasema

 ‘Kinachoshangaza kingine ni kuwa ni kwanini ni lazima tuje kwako, kwani hilo tatizo halitibiki sehemu nyingine..?’ akaulizwa.

‘Ndugu zanguni, bila kuwaficha nyie wote ..mpo kwenye matatizo makubwa, hata mkienda wapi, mimi nayafahamu hayo yote na mimi ndiye mtaalami ninayeaminika kule kijijini kwa matatizo kama hayo…,’akasema.

‘Tuambie sasa kuhusu hayo matatizo na tufanye nini, ili yaondoke ili tusikupotezee muda.?’ Akaulizwa na wakati jamaa anajibu hilo swali, mama yule aliyeitwa nje wakati huo akamnong’oneza kitu huyu mama anayeuliza swali, wakaongea kidogo kwa kunong’ona, mimi nilisikia akisema;

‘Wasifanye hivyo sasa hivi hatujamuweka sawa, kama kaja, asubiria kwanza, docta si katuruhusu au….?’akasema  hivyo na kuuliza, huyo mama mwingine akatoka nje, na baadae akarudi.

‘Tuendelee….’akasema

‘Ehee, mnataka niwaambie hayo matatizo ni nini…hayo matatizo ni mazindiko ya uchawi…kuna mtu kawategeshea, sasa kama mpo tayari, mimi nitawasaidia…niaminini mimi, siwezi kuwatapeli kabisa…mwenyewe mtaona tofauti….’akasema
‘Haya tuambie gharama zako, au tufanyeje…’akaambiwa.

‘Ni hivi,…nikiwaangalia kwa haraka hata bila kuwasiliana na watu wangu, nyie nyote mumeshaingiliwa na hilo tatizo, maana mazindiko ni kama kansa inayotembea, inakula kidogo kidogo…, inasambaza sumu, usipoiwahi maangamizi yake ni makubwa,..’akasema

‘Yalitokea wapi hayo mazindiko ya kichawi…?’ akaulizwa.

‘Yamkuja kwasabau ya …eeh, hawa mabinti wawili….’akasema sasa akiniangalia mimi na mwenzangu.

‘Kwavipi, na kwanini yahamie kwetu…?’ akaulizwa.

‘Kama nilivyosema matatizo hayo ni ya kuambukizana..kuna mambo walifanyiwa hawa mabinti, na mambo hayo popote watapokwenda, yanatua, sehemu hiyo na kujenga makazi, ..yaani hayo mazindiko,kwahiyo kila wanapokwenda wanaacha mizizi ya tatizo hilo, amblo kiasili ni wao walilogezewa…’akasema.

‘Una maana gani hapo kuwa sisi tulifanya makosa kuwachukua hawa mabinti, au makosa yao yanashinikiza kuwa kila mtu atakayewachukua aathirike ili wasisaidiwe ndio lengo lake au..?’akaulizwa

‘Maana sisi tuliwachukua kuwasaidia kwa nia njema kwanini tubebe mizigo yao, kwanini hayo mambo yahamie kwetu, ni ili tuwafukuze au…?’akaulizwa

‘Kuwachukua sio vibaya, mumefanya jambo jema kabisa… ndio maana hata huyoo mdada, maana matatizo yanvyoonekana yalianzia kwake, yeye alipoenda kwa huyo mtaalamu, aliambiwa nini, muulizeni…?’ akawa kama anauliza lakini hakusubiria kujibiwa akaendelea kuongea.

‘Yeye alitakiwa akifika mahali awe muwazi tu kwa muajiri wake,kwasabau bado alikuwa akitumia dawa,kuliondoa hilo tatizo,…sasa yeye alipofika huko kwa muajiri wake, akabakia kimia, hakusema lile tatizo likatua sehemu hiyo, likaanza kusambee, na kuwaambukiza wengine na …inaendelea hivyo hivyo kila anapokwenda mimi..sijui kama alimwambia bosi wake, au la, na mabosi zake, yaani nyie mumefanya nini,…muulizeni kama hakuwahi kuambiwa hivyo…’akasema.

‘Kuambiwa na nani sasa…?’ akaulizwa.

‘Na huyo mganga aliyekwenda kwake, maana mambo si yale yale, mimi nayafahamu yote, na najua tiba yake, na mengine ambayo hao wengine mimi nafahamu mengi zaidi yao, wengi wao, wakishindwa wanakuja kwangu….’akasema.

‘Kwahiyo una maana sisi sote hapa tupo kwenye matatizo, kwasababu hatukumsikiliza huyo binti si ndio hivyo….ukiwa na maana tumeshaambukizwa na hayo matatizo ya ..ya, sijui nini, zindiko au sio…kisa ni kutokana na hawa mabint, au kuna sababu nyingine ?’ akaulizwa.

‘Ndio hivyo,…hivyo hivyo… ndio maana nikawaita..kabla hamjachelewa, mkichelewa zaidi, waume zenu watakuwa hawashikiki, kutakuwa hakuna amani ndani ya nyumba, wanga watafanya majumba yenu sehemu ya kufanyia mambo yao, na zaidi, siri zenu za ndani zote zitakuwa zinajulikana, magonjwa, yatakuwa hayawaishi , mwishowe mtaanza kupagawa,….’akasema

‘Kupagawa kwa vipi..?’ akaulizwa.

‘Je hakujatokea lolote lisilo la kawaida kwenye majumba yenu, je waume wenu wapo sawa sawa, je hakuna migangano, kiasi kwamba waume zenu wanawaona wafanyakazi wa ndani ni bora kuliko nyie..eeh, ndio mambo kama hayo, manzindiko hayo ya uchawi, kazi yake kubwa ni hiyo, kuleta mifarakano, magonjwa na watu kuchanganyikiwa…

‘Kwahiyo ili wewe utuondolee hayo matatizo unataka sisi tufanye nini…?’ akaulizwa.

‘Sasa ndio tuingie kwenye mkataba wa matibabu,…nyie ndio mnapoteza muda, sijui kwanini mnaniuliza maswali mengi ambayo hayatawasaidia…shauri lenu…’akasema.

‘Ili tuingie kwenye huo mkataba na wewe tunahitajika kufanya nini, au kulipia nini..?’ akaulizwa.

‘Mhh, hapo kwanza, mnajua nipo sehemu ya watu hapa, ni mpaka niwasiliane na watu wangu, lakini kwanza mnaweza kutoa kianzio, ili niweze kuanza kufanya maombo yangu, unafikiri kwenu nyie ni pesa nyingi, muhimu ni afya zenu na amani kwenye majumba yenu, …’akasema.

‘Hicho kianzio kitatosha matibabu yako au sio…?’ akaulizwa

‘Hahaha, hapana, msinifikirie hivyo,…lakini ni sawa, ukifanya kazi , ukipata pesa zitafanya kazi vile vile,.. imetokea bahati hii, kuwa nikiwafanyia kazi nitapata pesa, na pesa itanisaidia na mimi….ila jamani msilipuuzie hili, ni tatizo kubwa…mtaangamia nyie na familai zenu, waume wenu wataanza kufanya mambo mabaya, watakuwa kama wehu, usiku wanakuwa sio wao tena, ..kama mna watoto halikadhalika, fanyeni juhudi mlimalize hili tatizo..mliondoe kabisa, mimi naiweza hiyo kazi…’akasema.

‘Tatizo lako, mpaka tunakutilia mashaka, ni kwanini unavutia kwako tu, na inavyoonekana wewe unacheza kote kote, kwenye uganga na uchawi, unaloga halafu unatibia, si ndio hivyo…’akasema

‘Kwanini…?’ akauliza sasa akishtuka.
‘Wewe kule kijijini wanakujua sana, kuwa wewe ni mganga lakini pia wewe ni mchawi, kweli si kweli, si ndio hayo unayoyaita kuwa ni maneno ya mitaani kweli si kweli..?’ akauliza hivyo

‘Mbona tunarudia kule kule, unajua nikuambie ukweli dunia hii hutapendwa na kila mtu, mimi nitaonekana mchawi kwa wabaya wangu , maana nitapambana nao kujilinda, wakinijaribu kwenye anga zangu, sasa nikiwashinda ndio wanaanza kupakaza mittani…’akasema.

‘Nikuulize inawezekanaje mtu akafika nyumbani kwako usiku kama mchawi usimuone, ilihali yeye anakuona..kwa utaalamu wako hebu tufahamishe hapo kidogo…?’ akaulizwa na hapo kidogo akashtuka, na akakohoa na kusema;

‘Hahaha, unajua hayo ndiyo mambo nayaagua mimi…huko ndio kwenyewe wengi hawayajui hayo.., ni kweli wachawi wanaweza kufika nyumbani kwa mtu usiku, wenye nyumba wasimuone..lakini kwa watu kama sisi tunaweza kuwaona, ..’akasema

‘Na kwa mfano wewe ndio mchawi, natoa mfano, eeh, upo umeoa, je ukiondoka nyumbani kwako usiku kama upo na mkeo, inakuwaje, au na yeye ni lazima mjuane, anakuaga, akijua unakwenda kufanya nini, au inakuwaje hapo…?’ akaulizwa.

‘Mhh..hapo, sasa kwa utaalamu wangu wa kuwatibia watu, ni hivi, ni vizuri, mke mjuane naye, ili ukiondoka akulinde ni sawa kabisa, vinginevyo, kama humuamini, au hutaki ajue,…au sio mtu mnzuri wa kutunza siri basi, inabid ufanye nguvu za ziada,unamfanyia kitu analala, mpaka ukirudi…’akasema

‘Sawa kabisa,..hapo sasa nimekuelewa,  na hicho ndicho, kilichokufanya wewe ukosane na mke wako au sio…,  kweli si kweli..?’ akaulizwa

‘Una maana gani kusema hivyo,…?’ akauliza halafu akacheka, baadae akasema

‘Sio kweli, kama unachukulia hivyo…tulikuwa na mambo mengi ya kutokuaminiana,..mimi nimeoa sio yeye aje na sheria zake, kama angelikuwepo hapa tungelimuuliza, maana sipendi kumsema mtu akiwa hayupo…yeye aliondoka kwa vile hakutaka kunitii mimi kama mume wake, ni hivyo kama nilivyowaambia awali nyie mnapoteza muda, mnafikiri mkiniuliza maswali hay ohayo kila mara mtanichanganya, hachangaywi mtu hapa,hahaha..’akasema na kucheka

‘Ok, sawa ni maswali ya kujiaminisha tu, maana familia ndiyo inayomfanya mtu aaminike, sasa kabla hatujakubaliana na wewe, ngoja nikuulize kitu nimekikukumbuka hivi wewe si ulioa, je hamkubahatika kuzaa mtoto, labda kama una mtoto maana hata binti yetu ana mashaka, asije kuolewa na mtu ana familia yake ikaja kumletea matatizo…?’ akaulizwa

‘Ndio tulibahatika kuzaa naye, …lakini ilikuwa ni bahati mbaya, kiukweli mpaka sasa sina mtoto hata wa kusingiziwa……’akasema na kujikesha.

‘Huyo alifariki akiwa na umri gani…?’ akaulizwa

‘Oh, unanikumbusha mbali sitaki hizo kumbukumbu, inaniuma sana…alikuwa mkubwa, alishaanza kuongea tu….’akasema

‘Na usijisikia vibaya ni kikuuliza haya, nataka tu kujirizisha, mtoto alipofariki, si mlimzika kama kawaida…’akaulizwa hapo akawa kama kashtuka, na kusema

‘Mbona maswali yako ya ajabu, kwani maiti inafanywaje…?’ akauliza

‘Nakuuliza wewe unijibu tu kawaida usiwe na wasiwasi, hujui nataka kuja kukuuliza nini ambacho kitanisaidia kwenye matatizo yangu, mimi nina matatizo, lakini siwezi kukuambia moja kwa moja, natolea mfano kwako …’akasema huyo mama.

‘Ndio tulimzika, kama kawaida, ehe, wewe una tatizo gani kuhusiana na watoto au sio, nieleze tu nitakusaidia…?’ akauliza

‘Unajua nikuambie kitu, ili tusiende mbali sana, pamoja na kukuuliza maswali yote hayo, mimi mola wangu kanijalia karama, ya kujua mambo na kuwajua watu, hata mimi nikikuangalia hivi naweza kukujua, umkweli au umuongo, umchawi au…unanielewa hapo...’akasema huyo mama, na jamaa akamuangalia huyo mama, halafu akasema;

‘Hahaha sio kweli…sio kweli kabisa, umesikia tu labda hiki na kile kunihusu mimi, na hayo wanayoongea watu huko kijijini, msiwasikilize kabisa, nyie ni wasomi, acheni kuskiliza umbea …’akasema

‘Unabisha…kuwa mimi nina karama, za kuweza kukutambua wewe ulivyo na ulichowahi kukifanya?’ akamuuliza

‘Sio maswala ya kubishana hapa, kama una karama sawa, lakini kwa uoni wangu nilijaliwa nao, nakuona huna, bali unabahatisha tu…’akasema

‘Nimeshajua ndio maana nikakuuliza yote hayo, nilijuaje kuwa ulikuwa na mtoto, huyo mtoto akafa, na tena alifariki kwenye mazingira ya utata, kweli si kweli…?’ akaulizwa hapo akatulia kwa muda, halafu akasema

‘Mimi sijui nani kakuambia yote hayo, yalishapita hayo…’akasema

‘Na zaidi kwenye kaburi lake lilikutwa limefukuliwa kweli si kweli..?’ aliposikia hivyo, akawa kama anataka kusimama, halafu akakunja uso na kumuangalia huyo mama muulizaji, lakini hakusema neno.

‘Na kuna watu waliona huyu mtu akilifukua, kweli si kweli….?’ Akaulizwa na hapo akainamisha kichwa hakujibu

‘Na zaidi ya hayo, wewe ndiye ulishutumiwa kuwa ndiye uliyelifukua hilo kaburi, kweli si kweli…?’akaulizwa na hapo akasema.

‘Ok yaonekana wewe umafuatilia mambo mengi yaliyotokea kipindi hicho, siwei kukubishia kwa hayo, yalitokea, lakini mengi yaliongezewa chumvi…’akasema

‘Kwahiyo unachotakiwa kujibu ni kweli au si kweli…?’ akaulizwa.

‘Hivi nikuulizeni mnataka msaada wangu au mnanihoji hayo yote ili yawasaidie nini…maana sasa mnaanza kunichanganya, ni kwa vile nauma, siwezi ...aah, je mpo tayari au la, niambieni ?’ akauliza.

‘Hatujamalizana na hili…tunataka ukweli ili tukuamini …je waliyoyasema kuwa wewe ndiye ulichimba hilo kaburi ni kweli au si kweli na ni kwanini walisema ni wewe,...ina maana walikuona,... na kama ni wewe ulikuwa unatafuta nini, kwanini usiseme ukweli, labda unaweza kujitetea kwa kukusaidia, ukasema  wewe ni mganga huenda ulikuwa unachimba kutafuta kitu, au kufanya uchunguzi kutafuta jinsi mwanao alivyokufa,.?’ Akaulizwa.

‘Hebu nikuulize ni nani kakuambia hayo yote..?’ akauliza sasa akibadili sauti kuwa nzito.

‘Nimekuambiaje, na mimi nina karama, lakini za kwangu sio za nguvu za giza, ni za mungu, ni sheria ni za ukweli, na ukweli una nguvu, za kwangu zinataka haki, na haki wakati wote ina nguvu zaidi ya nguvu za giza, …’akasema huyo mama sasa akimkazia macho huyo jamaa….na jamaa naye akatoa jicho la ukali, akasema;

‘Sikilizeni niwaambie mimi nilitaka kuwasaidia, na sasa naona mnaleta mambo mengine yakutaka kupambana na mimi, sijui hayo yamekujaje na tulikuwa tunakwenda vizuri, sasa nawauliza kwa mara ya mwisho, mnataka msada wangu au niyaache mpambane nayo wenyewe…’akasema.

‘Hatujamalizana baba, maswali yetu ya kukupima ili tukukubali kuwa kweli wewe ni mganga au ni mchawi, maswali bado bado yanaendelea,..au ushaanza kuogopa,  nakuuliza ni kwanini ulichimba kaburi la mtoto wako…?’ akaulizwa.

‘Hayo ya huko hayakuhusu yaache kama yalivyo, usije kujitakia matatizo, …’akasema

‘Kwahiyo ni kweli ulifanya hivyo…ili tuachane na hilo swali?’ akaulizwa.

‘Kama nilifanya au sikufanya hilo, kwanza hilo ni kaburi la mtoto wangu,..hivi niwaulize,kama nikikuona ukichimba kaburi la mtoto wako au jamaa yako nitakuuliza kwanini unafanya hivyo, ...unaweza ukawa na sababu zako..labda za kimila, za matambiko yako, nk..., sasa hayo ni mambo yangu binafsi, hayakuhusu….’akasema.

‘Sasa ndio uchimbe uchukue na mwili wake…?’ akaulizwa.

‘Nani aliniona nikifanya hivyo, haya mleteni, …’akasema kwa hasira.

‘Kama unataa ushahidi huo tutauleta, Upo tayari tufikie huko..au tuyamalize wenyewe kwa wenyewe humu ndani...lakini ukikubaliana na sisi hivyo, inabidi na wewe ukubali masharti yetu..upo tayari, ...?' akaulizwa

'Masharti gani...?' akauliza akiwa kanywea..

NB: Je itaishaje,..


WAZO LA LEO: Makosa, madhambi tunayotenda mbele ya mungu ni kitu kidogo sana kwake, tunaweza kuyaona ni makubwa sana..lakini ukiyakiri, na kutubu, kuwa umeyaacha na hutarudia tena, na akamuomba yeye akuongoze kuyaacha, n akujitahidi kuyaacha,..na huenda kwa kufanya hivyo ikawa ndio tiba ya maradhi au matatizo uliyo nayo, usingoje kesho, kuwa kesho nitatubu, au baada ya muda fulani ndio nitafanya hivyo, wewe unaijua kesho yako, hakuna anyeijua kesho yake,..muda wa kutubu ndio huu, tubu mja wa mungu, kabla mlango wa toba haujafungwa, ili uondokane na mzigo wa madhambi uliyo nayo ambayo mengine ni aibu mbele ya jamii….Tumuombe mola wetu atusaidie, atuongoze, atulinde..Aamin.

Ni mimi: emu-three

No comments :