Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, May 27, 2017

MPENZI WA FACEBOOK-37


Ilikuwa ni siku nyingine ya kesi hii, kesi hii imepitia milolongo mingi ya kuahirishwa ahirishwa..., ikianzia kwenye kusomwa hatua ya kwanza,…. na kwa vile wengine hawakuwepo, ikaahirishwa tena na tena..., ikaja kusomwa tena, kukatokea udhuru mwingine, ikaja tena na tena…mimi awali nilijikongoja nikawa ninafika mahakamani, lakini siku nyingine nikashindwa kabisa kutokana na afya yangu

Basi siku moja nilipoona sijambo kidogo, siku ya kesi hiyo, ndio nikaamua niende nijue hiyo kesi imefikia wapi, maana docta naye alishindwa kuja kuniona mara kwa mara kwa vile alitingwa sana na kesi hiyo na mambo yake mengine.

Siku hiyo nilipofika mahakamani, …nilijua labda kuna tatizo, maana watu walihudhuria wengi , wengi kupita kiasi…mpaka mimi nikashindwa kupata nafasi ya kuingia ndani, nikaamua kumpigia docta, na docta ambaye alikuwa kama star wa kesi hiyo, akampata askari mmoja, ambaye alikuja kunichukua ndio nikapata nafsi ya kuingia ndani.

 Kiukweli, sitaweza kuisahau siku hiyo, japokuwa bado nilikuwa na matatizo yangu ya kiafya, lakini siku hiyo ilikuwa siku iliyonifunua akili yangu na kujua ukweli , na undani wa tukio hilo kwa ujumla,..mengine japokuwa aliwahi kunielezea docta, lakini mengine ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuyasikia,…

Nilijaribu kuwaangalia watu waliojaa hapo, na kila nikiwapita niliskia kila mmoja akisema lake,….na kil alikuja hapo na sababu zake, ..wapo lake, waliosikia kuhus kesi hiyo, wakaamua kuja tu, ili wajionee, wapo waliosikia vituko vya eneo hilo lililojulikana kama makaburini, wakata kujua je ni kweli, watu kama hao wapo..lakini pia wapo waliwahi kushuhudia maajabu hayo,

Na wapo waliosikia uvumi kuhusu mpenzi wa facebook, wakataka kuja kuona, kama kweli yupo au ni maneno ya kufikirika, kwahiyo kila mtu alikuja kwa hamasa zake, lakini kwa ujumla kwa wale waliofuatilia walikuwa kwenye sintofahamu ya kujua, je kweli kuna sheria inaweza, ikaingiza mambo hayo ya kiimani, shiriki, na kuweza kupata vielelezo halisi vya kumuweka mshitakiwa au washitakiwa kama wakosaji…na je kuhusu mtandao, ni kweli umevamiwa na mashetani,..ikawa ni kazi kubwa kwa walinzi.

Nikakumbuka mtangazi wa asubuhi, kwenye runinga ambaye alinifanya nihamanike kuwa lazima leo nifike mahakamani...mtangazi huyu alisema;

‘Hii kesi ya aina yake, ndani yake kuna mauaji, imani za kishirikina, na kila aina ya dhuluma zinazoendeshwa hapa dunia, ndani ya kesi hii mtaona jinsi gani wasomi wetu, kizazi tulichokitegemea, kuja kuleta maendelea chanya,..lakini kimekwenda kusoma hadi huko nje, ..na waliporudi wakaanza kuchanganya utaalamu wao wa shule na mambo ya mizimu, na kuzalisha mambo hasi yenye madhara kwa jamii, jeee…ni nini matokeo yake…

‘Huruma ya binadamu imepotea,..watu wakajali mali, yale yaliyotakiwa kuwa ya siri, wao wakayafanya yawe dhahiri, yale yaliyoambiwa yasifanywe, wao wameyafanya, yale waliyoambiwa wasichungulie wao wamtizama kabisa..na baya zaidi vyote vile Vitu vya siri na dhahiri ambavyo ni vibaya, vimekuja sasa kuwekwa mitandaoni. Kwenye mitandao hakuna mipaka, mtoto, mkubwa wanaweza kuviangalia,na kufanya wafanyavyo, hadi kutengeza taswira kinyuma na uhalisia wake,....ni ni hatima yake…

Wakatokea wajanja, wakaona humo kuna namna ya kuwekeza, kama kuna mambo ya siri , kama kuna mambo ya giza, kama kuna mambo ya imani ambayo binadamu akiyaona anaweza kughilibika, na zaidi akaweza kutishika,au kuhamasika,… kwanini yasitumiwe mambo hayo kama mtaji, …wasomi hao wakabuni hivyo.

Wasomi hao waligundua kuwa watu wengi sana wanapenda kutizama, na kudadisi kwa macho, sasa kama ni hivyo kumbe huo utakua mtaji, basi watu watizame lakini kwa gharama..

Na kwa gharama zipi na kwa vipi…ili wajanja hao wafaidikie,..watu wakabuni mbinu, isiwe kutizama tu, bali pia wakufanye uwe mtumwa wao wa kudumu (edicted),.. mtandao ukatumiwa kama mtego, kitega uchumi, watu watimize tamaa zao, lakini kumbe watumbukizwe kwenye ushetani, akili zao zitekwe na kuwa watumwa wa shetani, hili watu hawalioni..kesi hii imegubikwa na mambo mengi sana…

Huyu alikuwa mtangazaji, akisheheneza kuhusu kesi hii, na maelezo yake yalizidisha hamasa za watu kuja kwa wingi zaidi

Hata mimi ambaye sikuweza kuwepo muda wote, niliposikia maelezo yote hayo, kwanza nijilaumu kwanini sikuweza hata kujikongoja tu…lakini sasa nimefika nitawezake kuingia huko ndani…

‘Tuliwahi kuonana na docta, ambaye ndiye alifichua siri kubwa ya kundi hili tukajaribu kumuhoji, yeye alikataa kabisa akisema kwa vile kesi hii ipo mahakamani tayari, hawezi kusema zaidi,…na zaidi ya hayo kesi hiyo ina mambo mengi ya kutisha sio vyema kuyazungumza hadharani, yanaweza kuleta mtafuruku na uelewaji mbaya kwenye jamii…

‘Je washitakiwa wote wameshapatikana..tulisikia kuwa mshitakiwa mkubwa katoweka,au hajapatikana ..ni kweli..?’ akaulizwa.

‘Waulizeni polisi kuhusu hilo, mimi siwezi kuliongelea hilo hapa kabisa…’akasema docta.

‘Wewe ulisimamishwa kama shahidi, na unatajiwa kuwa muongeaji mkubwa kwenye hii kesi, lakini inayonyesha hii kesi inachukua muda mrafu ni kwanini..., je huoni kuwa haki itapotea tena,,na je umejiandaa vipi kwa siku hii ya leo,, maana kila ukisimamishwa mwakili watetezi wanakujijia juu na kukuandama na maswali mengi.,,unatarajia kusema nini zaidi hii leo.., maana watu mitaani wanatishika wengine wamesema hawataki kabisa kutumia mitandao, je wewe unasemaje kuhusu hilo..?’ akaulizwa

‘Nasikia hivyo…, nimeshapewa katarasi kuwa nitasimamishwa tena leo, na sijui nitaulizwa nini,lakini kuna taarifa nyingine kuwa mama, ndiye anaweza kuzungumza leo,..sijajua kama kujitetea, au kama shahidi…la mimi kuwa nitasema nini,  mtalisikia huko huko mahakamani, na kuhusu ushauri wangu, ni vyema tukawa makini sana, kwenye mitandao, maana kama hawa watu wamegundulikana na kweli wanafanya mambo hayo mabaya,..kuna haja ya sisi watumiaji kuwa makini sana..’akasema docta

‘Makini kwa vipi docta, ili tuweze kujihami…?’ akaulizwa

‘Mimi naon tukizidi kufuatilia hii kesi vyema mtagundua mambo ambayo wengi tunayafanya, bila kujua, na ni mbinu zao, …wanajua taaluma hii ni ngeni kwetu, wanajua hatari za mambo yaliyomo, lakini kwa malengo yao, wametuletea,..na sis tunapenda…lakini hwakutaka kutupa tahdhari hizo..kesi hii itawafungua macho..kwa mwenye kuelewa…’akasema docta

‘Tunasikia kwenye kesi hiyo kuna …mpenzi wa facebook, unaweza kutugusia kidogo kuhusu huyo mpenzi je ni nani, je yupo kweli, je ni shetani kweli...?’ akaulizwa

‘Kama nilivyowaambia hayo ni mambo ya mahakama, nikianza kutaja hapa, ninaweza kuikosea sheria, ila kiukweli, huyo mpenzi wa facebook yupo, …’ aliposema hivyo watu wakagwaya…wengine wakaguna.

‘Ndio yupo na wengi mnakutana naye mkiwa humo ndani ya facebook, na wengine mtakutana naye huko huko kwenye facebook…haina haja ya kumtaka kuwa ni nani huyo….maana hapo katumika kwa ujumla,.., ila anayehusikana na hii kesi tutamsikia huko mahakamani, sina zaidi ya maelezo yake kwa sasa…’akasema na kutaka kuanza kuondoka.

‘Ni kweli kuwa huyo mpenzi wa facebook, sio binadamu ni shetani, …?’ akaulizwa huku akitafuta nafasi ya kuondoka, maana waandishi wa habari walikuwa wamemzonga sana.

‘Mimi sijui…kama sio binadamu ni nani basi…’akasema docta

‘Lakini wewe uliwahi kusikiwa ukisema hivyo..’akaambiwa

‘Kuwa…’akasema hivyo.

‘Ulisema huyo mpenzi sio binadamu ni shetani…kweli si kweli…?’ akaulizwa

‘Jibu la haraka mimi sijui…kwa ufafanuzi zaidi fikeni mahakamani…siwezi kusema kitu ambacho kitakuja kunieletea matatizo baadae..’akasema docta sasa akisukuma watu ili aweze kupita na kuondoka.

‘Lakini iweje mwanadamu tunamuona halafu awe ni shetani, kwa vipi, au anawezaje kuingia kwenye mtandao…?’ akaulizwa

‘Kwani kuna makosa gani…ni namna ya kuelewa tu, shetani ni nini, ni kitu au matendo au …kama kitu, kipoje , kama mtu yupoje kama ni mtendo…eeh, yapoje, jiulize hayo na mukipata majibu mtagundua kuwa kumbe hata wanadamu wanaweza kuwa ni mashetani,..na hao wanadamu si tunao , tunaish nao,…au?... lakini wao wana miili tu ya kibinadmu, au sio… lakini ndani yake, eeh, na matendo yake,……sio-ya-ki bin-adamu…mumenielewa…?’akasema

‘Kama sio binadamu ni nani basi,…. maana sisi tujuavyo mashetani hawaonekana kirahisi..?’ akaulizwa

‘Hahaha..hapo sasa mnataka niwe mwalimu, na muda umeshapita, nahitajika mahakamani…majibu sahihi mtayapata huko mahakamani, na mnaweza kupata bahati ya kuliona hilo ..kwa macho yenu wenyewe, ……’akasema

‘Kuona nini docta, kuliona nini, docta.. …una maana tutamuona huyo shetani, au nani…docta, tupe jibu la hilo swali kwanza, kabla hujaondoka, tafadhali…’watu wakabakia na maswali yao..docta akawa keshaondoka.

‘Oh…hii sasa ni hatari..’kijana mmoja akasema, na kauli kama hizi zikafanya mahakama izidiwe kwa wingi wa watu..

***********

KESI:

Mlolongo wa kesi hii, kama ilivyokuwa kesi nyingine, ulikuwa mrefu…lakini kama alivyoahidi hakimu, alitaka kesi hiyo iwe fupi kwa kadri iwezekanavyo, kwa vile muendesha mashitaka alisema kila kitu, ikiwemo ushahidi vipo tayari, tatizo likawa kwa upande wa utetezi, na baadhi ya washitakiwa kutokuonekana,...


Mimi kutokana na afya yangu,  sikuwahi kuhudhuria siku zote, ila siku nilipohudhuria ndio siku mke wa mzee alikuwa akitoa maelezo, …na niliona jinsi gani mama huyo alivyoamua kujitolea kwa kuelezea kila kitu bila kuogopa,


Mimi nahisi aliamua kufanya hivyo , japokuwa alikuwa mmoja wa washitakiwa, aliamua kutoa maelezo hayo baada y akuona kesi hiyo ikipigwa dana dana, leo kesho na mwezi ukawa unakwisha,….


‘Ndugu muheshimiwa hakimu, pamoja ya kuwa mimi ni mshitakiwa, lakini naomba kwa ruhusa yako niweze kutoa maelezo ynayoweza kuisaidia mahakama yako hiii ikaweza kutoa hukumu kihalali,….kwa hili nimepingana na wakili wetu wa utetezi, najua vyovyote iwavyo, inayoumia zaidi ni familia yangu…’akasema huyo mama, na wakiliw a utetezi, alitaka kupinga lakini akaona anyamaze kwanza.


‘Najua wengi wamefikia kuniona labda mimi nilipenda kujiingiza huko, kwasababu za masilahi,..kiukweli, sio sahihi, kwasababu haya yote yametokea hata nikiwa sijui kama mimi ni muhusika wa mambo yaliyosababisha yote haya..

Ndugu muheshimiwa hakimu, mimi ninashukuru kwa maelezo mazuri aliyowahi kuyatoa shahidi upande wa mashitaki, docta..huyu kaweza kunirahishia ukweli wa haya mambo, kuwa chanzo hasa ni migogoro inayotokana na mambo ya kurithi, lakini zaidi ni kutokana na tamaa za watu ubinafsi, katika kutaka utajiri, bila kujali uhalali wake…

‘Mimi sikujua kwamba ni mrithi halali wa kiti cha ufalme wa enzi hizo, sikujua kuwa nilikuwa natakiwa kuvipata hivyo vitu vilivyoibiwa…, na sikujua umuhimu na ubaya wa hivyo vitu, na zaidi sina ujuzi wowote wa mambo hayo ya kishirikina, lakini naambiwa ni asili navyo, na kuna chanzo cha mgogoro wa kizalia, ..mimi sijui…..’akatulia.


‘Kwa maelezo hayo mafupi, utaona kuwa mimi sina lolote la kushitakiwa zaidi ya kutumbukizwa kwenye mambo ambayo hata sijui yalivyoanzia…ni kweli huyo kaka yangu…ni mtoto wa ndugu wa baba,  alikuja baadae kunishauri kuwa kuna kitu kama hicho, na alikuja kipindi ambacho matatizo yameshaanza kuikabili familia yangu…’akatulia.

‘Alikuja kama kunisaidia,…sikujua kama ana ajenda nyingine…mimi namfahamu,..na nimekuwa msiri wake, ..najua mengi kumuhusu yeye, na anapojitokea, najua kabisa kuna tatizo litatokea, lakini ni ndugu yangu sikupenda kumsema,…’wakili utetezi ukaingilia kuwa anamzungumzia mtu mwengina wakati yey hayupo.

‘Ndugu muheshimia hakimu, kwa mtizamo huo, mimi kama mzazi nilitakiwa kuchuku hatua ya kuhakikisha familia yangu ipo salama….’akatulia akiangalia upande ule alipokuwa muendesha mashitaka, nahisi alikuwa na wasiwasi fulani.


‘Na kama alivyosema muendesha mashitaka kuwa nilipopewa taarifa hizo, kuwa kuna vitu kama hivyo, vyenye mlengo mbaya kwanini sikuchukua hatua ya kulipeleka swala hilo mbele ya mahakama,..akishinikiza kuwa na mimi nitakwua muhusika ndio maana nilikaa kimia,… swali hapo, ningeanzia vipi, na ilihali mambo yote yamesimamia kwenye shiriki, kwenye imani za kufikirika zaidi…na niende kwa nani…’akageuka kumuangalia wakili aliyetaka kusimama.

‘Na je ni nani ningemuamini ambaye angelinihakikishia kuwa hayo atayasimamia kwa masilahi ya familia yangu, na ambaye asingeliweza kunisaliti, maana kama mnavyoona wengi wa washitakwa waliotajwa,..wana madaraka, wana wadhifa na wengine wapo kwenye idara za usalama,…’akamuangalia muendesha mshitaka.

‘Sasa je ni nani angeliweza kuwa mdhamini wangu na kuweza kulibeba hilo bila kuja kuwaambia washika dau…ni mkuu wa kituo, ni….hahaha, jamani dunia hii sasa ni hatari…mnavyoona sivyo ilivyo…’akasema huyo mama.

‘Washika dau…’hakimu akawa kama anauliza.

‘Washika dau hapa, ni hao waliounda kundi hilo haramu, na kuniingiza mimi bila kujua undani wake na hatima yake….’akatulia.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, najua …kisheria vyovyote nitakavyosema mwisho wa siku itarudia kwenye swali, kwanini…kwanini…lakini narejea tena ni nani wa kumuamini kwenye kadhia kama hii…hakuna,…labda ingelikuwa sehemu nyingine na huyo mtu awe hajakutana na hawa watu, ..maana kiukweli...hawa watu ni hatari, na uhatari wake ni kuwa , wao wamewekeza watu wao kila sehemu nyeti…’akatulia.

‘Ina maana huniamini hata mimi hakimu..?’ hakimu akauliza lakini huyo mama hakulijibu hilo swali akaendelea na maelezo yake.

‘Najua …kwa kuanza kutoa maelezo haya najiweka kwenye hatari zaidi, kwani haya mambo yamewekezwa kwenye kiapo, kuwa atakayetoa siri za hilo kundi, adhabu yake ni ku-uwawa,… lakini…’akasema sasa kigeuka huku na kule kama anaogopa.

‘Hata hivyo… kwa hivi sasa nina thamani gani,..nina nini tena, kama familia yangu ipo hatarini, siwezi tena kuvumilia ndio maana nimeamua kusema kila kitu ninachokijua kuhusiana na kundi hili…waje waniue tu lakini sitaogopa kusema ukweli wote ninao-ufahamu mimi….’akasema huyo mama, na kwa ghafala watu waliopo humo ndani na nje wakashangilia.

Hakimu ikabidi aingilie kati na kutoa onyo, kuwa hali kama hiyo ikarudia tena hakuna mtu atakayeruhusiwa kufika tena mahakamani, kesi hiyo itaendeshwa na washitakiwa na washitaki basi…

 Alipoendelea kutoa maelezo, ikafika mahali mawakili upande wa utetezi wakaona waingilie kati..na moja ya hoja yao ni kuwa mama huyo anatoa maelezo yenye mlengo wa kujitetea mwenyewe na kuwaweka wenzake hatarini, na wakati huo wenzake hawajaweza kufika mahakamani, hapo huyo mama akaja juu na kusema..

‘Kwanza niwaulize washitakiwa wengine wapo wapi, kama kweli nyie mnasimamia uadilifu..wao wamehindwaje kufikishwa hapa mahakamani..sote tulikuwa wagonjwa ..mbona tumajikongoja na kufika hapa…

‘Ni wagonjwa kukuzidi wewe,…ndio maana , hawapo hapa..’akaambiwa na hao mawakili.

‘Kama ni wagonjwa kwanini nyie mnasimamia upande wao, ..wenyewe hawapo, nyie mnadai kuwa mimi naongelea kuhusu wao wakati wao hawapo,na nyie mnafanya nini,…?’ akauliza na hakutaka jibu akaendelea kusema;

‘Na hapa kwa vile mimi nipo mwenyewe, nimeamua kujitetea mwenyewe na wao wakija watapata nafasi hiyo y akujitetea wao , ili haki iweze kutendeka na hakimu ndiye ataamua ..’akasema huyo mama na kukawa na mabishano ya kisheria, mwishowe hakimu akasema;

‘Mama tunaelewa kuwa huenda una mawazo maelezo mazuri kwa vile na wewe unahusika kwa namna moja au nyingine,..na huenda unajua ukweli wa kundi hili kiundani zaidi…, je maelezo yako yanalenga nini,kuhusu wewe kama mwanachama au kuhusu kundi kwa ujumla, au lengo lako ni kujitetea wewe kwa ajili ya familia yako kama ulivyosema kuwa familia yako ipo matatani?’ akaulizwa

‘Mheshimiwa hakimu, maelezo yangu yatanihusu mimi,..lakini mimi ni miongoni mwa kundi hilo, niliyeingizwa bila kujijua, sasa jinsi gani nitakavyojielezea mimi kama mwanakundi hilo ambalo kiukweli mimi silijui sana chanzo chake,… ila najua ukweli kuhusu mimi na jinsi gani walivyoniingiza kwa nguvu zao, na jinsi nitajitetea mimi bila kuligusa kundi au wanakundi, nashindwa, …’akasema.

‘Ina maana kwa maelezo yako, ulilazimishwa kujiunga na hilo kundi..?’ akaulizwa

‘Ndio …’akasema

‘Ni nani aliyefanya kazi hiyo ya kukulazimisha..?’ akaulizwa na wakili mtetezi akaingilia, lakini hakimu akasema ajibu swali hilo

‘Ni kaka yangu, ..’akasema

‘Kaka yako yupi huyo, ni miongoni mwa hao washitakiwa au sio..?’ akaulizwa.

‘Ndio,… lakini ni miongoni mwa hao washitakiwa ambao wanadaiwa wanaumwa, na hawawezi kufika hapa…’akasema mama.

‘Kuna picha zao hapa….ni yupi kati ya hawa hapa…?’ akaulizwa akionyeshwa hizo picha.

‘Katika hizi picha hapa hayupo…’akasema na hakimu akashtuka kidogo, na kuuliza swali;

‘Je…mbona mama hueleweki,…umesema kuwa kaka yako huyo ni miongoni mwa washitakiwa, ..’akaambiwa hivyo.

‘Ndio..’akasema kwa sauti kubwa.

‘Washitakiwa wote wapo kwenye hizi picha hapa, tumatumia hizi picha kwa vile washitakiwa wengine hawakuweza kufika hapa…, nakuuliza ni yupo kwenye hizo picha, ni yupo ni kaka yako kwenye hizo picha..maana hao washitakiwa picha zao hizi hapa, je ni yupo kati ya hizi picha,…’akaulizwa

‘Nimesema kwenye hizi picha hapa, hayupo..kwenye hizo picha hapa, simuoni, ..sio yeye, kwasababu sura zilizopo hapa sio zenyewe kwa baadhi ya wahusika,…’akasema na watu wakaguna .

‘Kwa vipi…?’ akauliza hakimu.

‘Kwasababu watu hawa wamejiwekeza kama vinyonga, wanajibadili kila wakati, ..lakini mimi najua sura zao za asili, na sura zao za asili sio hizi hapa,..na huu ni ujanja umefanyika ili mwisho wa siku wahusika wenyewe wasipatikane…’akasema na mawakili wakaingilia kati.

‘Lakini hawa ndio wamekamatwa..na askari,na waendesha mashitaka wamethibitisha hili, kuwa hao hapo ndio washitakiwa halali…’akasema hakimu.

‘Ndugu hakimu,…kama kweli mnataka haki na ukweli vitendeke, mimi naomba kwa ruhusa yako watu hao wafikishwe hapa , mbele ya mahakama yako tukufu…na nitaweza kuwatambua kwa sura zao kama kweli ndio wao au sio,..wakiwa hapa mahakamani..nitaweza kuwabainisha,, lakini sio kwa hizo picha, …..’akasema huyo mama.

Kukawa na kujibishana kwa mawakili na hakimu akaingilia kati tena na kusema
‘Mama, yaonekana wewe huna uhakika , maana kwenye mahakama yangu nimeletewa hao watu, kuwa ndio washitakiwa, lakini wewe unakuja na hoja nyingine kuwa hao wtu sio wenyewe, hebu tuambie, wewe hao washitakiwa wako ni akina nani…

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, washitakiwa ni hao hao..ila kwa asili yao, yaani, watu wenyewe halisi kwa sura zao,  ninaowajua mimi, sivyo,kama wanavyoonekana kwenye hizp picha,.. ..na huu ni ujanja wao,…sasa sijui …’kabla muheshimiwa hajamuuliza tena maswali, docta akajitokeza, kwa muda fulani docta alikuwa katoka kidogo, akifuatilia jambo fulani.

‘Ndugu muheshimia hakimu..huyo mama anazungumza ukweli kabisa, mimi ni docta, na ni miongoni mwa watu waliofuatilia hii kesi, kwa undani wake , na hatua iliyofikia, tukichelewa zaidi washitakiwa husika watapotea..kama ilivyotokea huko nyuma,…

‘Nimewaomba watu wa usalama watu hao wafikishwe mahamakani hii leo kama walivyo,hata kama ikibidi na vitanda vyao…na ukweli utabainika hapa hapa, kama kweli anayozungumza huyu mama ni sahihi au ni uwongo…’akasema na watetezi wakapinga na hakimu akatulai kwa muda, halafu akateta na wenzake, …baadae hakimu akasema;

‘Hatuwezi kuwaburuza wagonjwa mahakamani, …kwa hali ilivyo, basi inabidi tuahirishe hii kesi…

‘Muheshimiwa hakimu..isipowezekana leo, basi haitawezekana tena,na kama haiwezekani leo, basi sisi hatuna uaminifu tena na mahakama hii….’akasema docta na muendesha mashitaka akamsogelea docta, kukawa na kuelezana kwa muda, na muendesha mashitaka akamsogelea hakimu kuteta naye…lakini ikaonekana hakimu hajakubaliana nao…

‘Kesi imeahirishwa…’akasema hakimu akisimama akuondoka na mara mlangoni kule akatokea binti…akikimbia kuelekea mbele ya mahakama,na kukatokea ghasia za kumzuia…

NB: Ni nini kitaendelea, ni nani huyo?

WAZO LA LEO: Ni mwezi mtukufu wa Ramadhani, waislamu wote wanajiunga na wengine duniani kutimiza ibada hii muhimu sana kwao,…hata waumini wa imani nyingine, wanawasaidia wenzao hawa, kwa namna moja au nyingine,..

Wanasaidia kwa vipi!  Wanaweza kusaidia kwa kuhakikisha kuwa matendo yako, shughuli zao, haziwezi kuwakwanza wenzao na kuwavurugia ibada yao hii muhimu. Waajiri tuwe waadilifu kwa kuhakikisha waislamu wanaweza kutimiza ibada hii muhimu kwao, kwa kuwapa muda wa kuswali, na kutoka mapema kuwahi kufuturu..ni mwezii mmoja tu,…


Huu ndio utu wema huu ndio ubinadamu wa kweli.. na huu ndio upendo na mashirikiano mema katika jamii zetu Mtandao wenu wa ‘Diary yangu’, unawatakia waislamu wote MFUNGO MWEMA WA RAMADHANI, TUKISEMA RAMADHANI KARIIMU.
Ni mimi: emu-three

No comments :