Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, March 29, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-29


Na mara mlangoni akaingia mdada mmoja, na wote wakageukia kuangalia huko mlango , na huyo mdada alipona hiyo hali, watu wote wanamuangalia yeye, akasita kuingia, baadae akawa anaingia kwe mwendo wa taratibu….

Wa kwanza kuongea alikuwa ni dereva, ambaye alionekana mwenye mshangao mkubwa mdomoni, na kusema;

‘Mke angu umekuja, mbona hukunipa taarifa…?’ akauliza dereva.

‘Nimeamua kuja tu, ….na nilipokuwa hapo mlangoni nimesikia mama akiongea neno, Mama, mbona unasema hivyo, mwanao hana matatizo yoyote ya uzazi, mimi hapa nina mimba,...nina mimba ya dereva, mimba ya mume wangu dereva…’akasema.

'Haiwezekani...'akasema dereva kwa mshangao.

‘Kwanini haiwezekani, huo ndio ukweli..nimeshapima na nimethibitisha hilo…’akasema

'Haya, kama ulijifanya huzai, ukatembea na binti wa watu, sasa huna cha kujitetea tena, sasa una watoto wawili…wa kwanza ndio huyo unamkataa na wa pili bado kuzaliwa…’akasema akimuangalia yule mdada aliyejifunika usoni, na huyo mdada alionekana kama kuchanganyikwia fulani, akawa kama anataka kuongea jambo.

Mke wa Dereva akasita aliposikia kauli ile kutoka kwa Soldier akauliza kwa mshangao

‘Watoto wawili…?’ akauliza mke wa dereva.

‘Ndio muulize atakuambia vyema….’akasema Soldier

‘Muongo huyu, usimsikilize kabisa, bro kwanini unafanya hivyo…’akasema Dereva akimuangalia Soldier…

‘Nataka ukweli ujulikane…’akasema Soldier

Tuendelee na kisa chetu…

**********************


‘Unasema ‘Muongo huyu’…ni nani muongo..?’ akauliza mke wa Dereva akiwa kashika kiuno huku akimuangalia mumewe. Na dereva akasema kwa harakaharaka.

‘Huyu anayedai eti mimi nina watoto wawili,…huyo mwingine katoka wapi, mimi najua huyo aliyepo tumboni mwako,…. hawa watu wanataka kuniharibia ndoa yangu, kama ni mtoto wangu ningelimuambia mke wangu, kwanini nimkatae…’akasema akimuonyeshea kidole dereva.

‘Unasema kama mtoto ni wako ungelimkubali, kumbe ndio tabia yako, kumbe una vimada nje,..sasa nimekuelewa, uliniona mimi sizai au sio, yaani kuhangaika kote huko kumbe mwenzangu unaniendea kinyume, haya sema ukweli kama ni mtoto wako au sio, ..na nikija kugundua kuwa ni mtoto wako, itakuwa mwisho wangu mimi na wewe, na ’Lisemwalo lipo…’akasema mkewe

‘Mke wanu hayo yametoka wapi..haya ni maongezi tu, wanajaribu kutafuta baba wa mtoto aliyeokotwa huko kambi ya wakimbizi nchi jirani…na mimi nilikuwa kiongozi kwenye kundi la kuwasaidia wakimbizi, wakaniletea huyo mtoto..sasa kuangaika kwangu kote kumtafuta mzazi wa huyo mtoto, ndio imekuwa kosa…’akasema.

‘Najua..unafikiri sikujui, nawafahamu sana nyie wanaume, haya hii hapa ni mimba yako, kama una mtoto mwingine ni shauri lako, nimeshakuambia hivyo….nimewaacha wanaume wengi wa maana kwa ajili yako, …’akasema akigeuka kutaka kuondoka.

‘Mke wangu hebu subiri, kwanza nimefurahi sana kusikia una mimba, siamini, unajua, nilishakata tamaa,…sasa sina wasiwasi tena, kuwa huenda hatuwezi kupata mtoto tena, mama alishaanza kusema ooh, urithi, oor baba yako, hapana mama hiyo ni bahati mbaya tu….’akasema na kumgeukia baba yake pale kitandani, akasema;

‘Baba mungu akipenda utapata mjukuu wako, …ni furaha iliyoje, mjukuu wako wa kwanza, umeona eeh …’akasema akionyesha furaha, na hapo hapo Soldier akasema;

‘Sasa kwanini unasema mjukuu wako wa kwanza, huyu aliyewahi kuzaliwa je, mbona humtaji, au umeshamkataa kabisa, utapata dhambi wewe, kazi kupora visivyo vyako, haya mungu kakujalia mtoto unamkataa, kisa una ajenda yako ya siri, au unaogopa kuwa shemeji atakuacha,....’Soldier akasema akimuangalia shemeji yake, ukumbuke huyo mdada ndiye awali kabisa alitakiwa kuolewa na Soldier, lakini akaja huyo ndugu yake akamzidi kete.

‘Bro, usiniharibie furaha yangu, huyo mtoto ni wa kwako, na kwa vile hamjajaliwa mtoto atawafaa sana, na hajatambulikana kama mjukuu wa baba, maana …’ akasita kidogo, na halafu akaendelea kusema;

‘Mke wangu naona tuondoke hapa, naona hakuna cha maana cha kuongea, wewe mdada huyo mtoto ni wa kwako, kama umeshindwa kuthibitisha kuwa baba yake ni nani, basi nenda kaishi naye na ukiwa na shida yoyote usisite kutuambia, kwani nahisi ana damu ya mzee …’akasema akimgeukia mkewe na mama yake alikuwa bado kaduwaa, akimkagua mkwewe, kama haamini alichokisikia.

‘Haondoki mtu kwanza hapa, unasikia dereva nilikuambiaje, sasa usitake niongee tena nikazidi kukuharibia, subiri tuyamalize haya, na tukitoka hapa sote tunakwenda huko nilipowaambia.., sasa ukitoka huko ndio mtakwenda kujipongeza….na shemeji…’akasema Soldier.

Mara yule mdada aliyekuwa kajifunika uso, ambaye kwa muda huo walisogea pembeni kidogo wakiteta, na shemeji mtu akasogea karibu na pale walipokuwepo wengine, naona bado walikuwa hawajaelewana na shemeji wa Soldier, kwani huyo shemeji alikuwa kama anamzuia, lakini ikawa haiwezekani tena, huyo mdada akasogea kwenye kundi, na kusema;

‘Jamani pamoja na hayo, nimeona niondoke na mtoto wangu, ila nahisi nina deni kwenu, ni lazima niuseme ukweli, japokuwa jamaa yangu mfadhili wangu ananionya kuwa nikisema huo ukweli huenda ikawa ni matatizo ya kiafamilia, na…huenda na mimi nikaingia matatizoni, lakini mimi sioni tatizo hilo ….’akageuka kumuangalia shemeji mtu.

‘Nimeshakuambia ukisema huo ukweli na mimi nitajitahidi ukafungwe, maana ulitoroka huko kwenu, na bado mumetoroka kambini, wewe na ndugu yako,..nyie ni wakimbizi..’akasema shemeji mtu kwa hasira, na huyo mdada akawa kainama chini, halafu akainua kichwa na kusema;

‘Kwani nikiusema ukweli wewe utakuathiri nini…sitaongelea mambo yako, naongea kisa changu na mtoto,…na hicho kisa kinastahiki kijulikane na hawa watu ili kuondoa dhana mbaya, na ili mwisho wa siku wasije kunilaumu ,..maana ni lazima niondoke na mtoto wangu…’akasema

‘Kama ni lazima kuondoka na mtoto ina haja gani ya kuwasimulia hayo yote…unataka hawa watu wakuhurumie,  hawa watu hawana huruma kamwe…hasa huyu, ..huyu ni tapeli wanamfahamu sana huko mjini, na huyu anayejiingiza kwenye kazi zisizo muhusu, nenda ukapigane vita huko …’akasema akimuelekezea kidole dereva huku akimuangalia Soldier

‘Shemeji, usinikashifu, sina utani na wewe….’dereva akasema kwa hasira.

‘Huo sio utani, Dereva huo ni ukweli, na sitaogopa kusema ukweli kwako na kwa huyu ndugu yenu…na hata kwa baba yenu, ndio maana nimemshauri huyo dada, kama nilivyomshauri dada ndugu yangu, kuwa hii familia haifai, asiache mtoto wake hapa…hanielewi, ok, fanya upendavyo…’akasema

********
Yule mdada akawa katulia kidogo, halafu akasema; akimuonyeshea shemeji kwa mkono,

‘Huyu jamaa namshukuru sana, kwani kama asingelikuwa yeye, huenda sasa hivi ningelikuwa maiti, yeye ndiye aliyeniokota nikiwa sijiwezi,….nikiwa ufwekeni mwa mto, na huo mto una mamba, hata sijui ilikuwaje, hao mamba wasinitafune…’akasema.

Basi kwa neema zake mungu akanichukua hadi kwenye hospitali ya karibu na hapo nilitibiwa, ma hali yangu ilikuwa mbaya sana, sijitambui na nilikaa hapo hospitalini mpaka wanataka kunifukuza, na muda huo mimba ikawa anakua,.

‘Na baadae alikuja akanichukua hadi kwenye nyumba za marafiki zake,na kipindi hicho bado afya yangu ilikuwa mbaya, na ilikaribia muda wa kujifungua, hata hivyo nilionekama mdhaifu, sina damu…taabu moja kwa moja, vidonda,…ooh, siwezi hata kuelezea..na niliposhikwa uchungu nikapelekwa hospitalini, hizo za serikali, unajua kulivyo, na hali niliyokuwa nayo,.. lakini nashukuru, walijitahidi sana…nakumbuka wakati napelekwa kufanyiwa upasuaji, maana ilibidi nizae kwa njia hiyo, docta alisema; ‘hapa ni moja,mama au mtoto…’akatulia.

Nashukuru sana, madocta wakafanya juhudi na bahati nzuri, mtoto akatoka salama, lakini mimi nilikuwa kwenye hali mbaya, sana, ikawa kama mtu wa kusubiriwa tu, masaa yangu yafike, niage dunia..’akasema.

‘Lakini ya mungu mengi, mungu anajua viumbe vyake , siku ya kwanza ya pili hali yangu ikaanza kurudia vizuri, lakini bado sikuwa mtu wa kutumainiwa, nilikaa pale hospitalini kama wiki mbili hivi, baadae matumaini yakaja, na afya yangu ikarejea, lakini nilikuwa kama sio mtu, nimekonda, makovu ..vidonda,…na hata mtoto alikuwa hapati maziwa, mtoto alianza kunyonya maziwa ya chupa akiwa bado mchanga.

Namshukuru jamaa huyu, ndiye aliyekuwa msaada wangu mkubwa, kunitafutia madawa, vyakula ..na sehemu ya kuishi,..na kweli baadae nilitoroka sehemu niliyokuwa naishia, lakini nilifanya hivyo kwasababu ya msingi.

‘Sema ukweli uligundua kuwa huyo jamaa anafanya biashara garamu…’akasema Soldier

‘Mimi sijui mambo yake, na sikuwa na muda wa kufuatilia mambo yake,….’akasema

**********

‘Siku moja nikiwa hapo alikuja jamaa mmoja anayenifahamu, na jamaa huyo anafahamika, mimi namfahamu kwasababu niliwahi kumuona huko, ni wale watu wanaocheza na sura mbili, anachukua habari za serikali anawapelekea waasi, …na kuniona mimi, ilikuwa ni hatari kwake, kwahiyo nilijua tu, atawasiliana na waasi, ili niuwawe. Aliponiona alijifanya hajaniona, akawa ananifuatilia, lakini nami nikamuwahi.. tukakutana uso kwa uso..

‘Wewe upo hai bado…?’ akaniuliza
‘Mungu mkubwa nipo hai, umetumwa kuja kuniua..?’ nikamuuliza

‘Nitatumwaje kuja kuua maiti, unajulikana wewe ni maiti…’akasema

‘Kwahiyo umekuja kufanya nini huku?’ nikamuuliza

‘Hiyo sio kazi yako,…ila kwa vile nimekuona na unataka watu wasikujue inabidi uwajibike,…’akasema

‘Unataka shilingi ngapi…?’ nikamuuliza na akataja pesa nyingi sana, nikamwambia nitazitafuta, nilimwambia tu ilimradi niachane naye…

Basi nikaona dawa ni kutoroka sehemu hiyo na kwenda sehemu nyingine, na huko nako kulikuwa na msako wa wageni haramu.., nikaona jambo jema ni kwenda kambi ya wakimbizi, na huko kambini nikajibadili, nikawa navaa hivi hadi leo.

‘Kwahiyo mfadhili wangu sikufanya hayo makusudi, na naheshimu sana msaada wako, sina cha kukulipa lakini ipo siku nitazilipa fadhila zako…’akasema akimuangalia shemeji mtu.

‘Sihitaji malipo yoyote, nimesaidia watu wengi sana…’akasema huyo shemeji kama kujinadi hivi, na Soldier, akamuangalia kwa makini halafu akamuuliza shemeji yake;

‘Wewe wakati unamsaidia ulikuwa wapi, au ulitokea wapi…?’ akauliza Soldier

‘Nilijua tu utauliza maswali hayo..jibu lake ni kuwa hayakuhusu maisha yangu, kwani wewe ni polisi, au.’ Akasema shemeji yake.

‘Najua maeneo hayo ni ya mpakani, na maeneo hayo ni sehemu wanapopitia wauza magendo, na madaa ya kulevya, na wewe ni moja ya kazi yako…’akasema Soldier

‘Nilijua hilo ndilo unalonitafutia, lakini kumbuka, polisi wameshanishuku hivyo mara nyingi, tukaongea nao, nikwaambia wanionyeshe ushahidi hakuna, wakanichunguza wee hawakuona kitu..unajua niwaambie nyie watu, msifanye kazi kwa wivu…hilo ndio kosa lenu, mimi nahangaika kivyangu, napiga dili zangu , kutafuta maisha yangu, hayo yanawahusu nini…’akasema

‘Tatizo lako wewe hufuati sheria,…na biashara zako sio halali, kama ni halali kwanini unapita njia za magendo, kwanini huna lesoni iliyotambulikana kisheria…ina maana kuna biashara zako sio halali…’akasema Soldier.

‘Unajua wewe unajifanya sio mbongo, haya maisha ukiamua kufuata sheria, utafanikiwa kweli, kuipata leseni ni mlolongo mrefu, na hapo nia yao ni kukukata kodi nyingi tu, utapata faida kweli..ni maisha yetu ya kawaida, uhangaike kwanza ukijiweka vyema utakata hiyo leseni yao,..lakini pesa hizi za kubangaiza, biashara yenyewe ya msimu, ..je ukiwa huna pesa utalipia nini hiyo kodi..usijifanye hujui maisha yetu….’akasema.

‘Hayo unaweza ukaongea na wahusika wakakuelewa, sidani kama hilo ni tatizo, nikuulize wewe unafanya biashara gani rasmi…?’ akauliza

‘Hayo maswali ya polisi, sitaki, na usitake kunichefua, mimi naweza kuwaambia polisi tabia yako ilivyo…’akasema.

‘Sawa kama unataka ukayajibie polisi hakuna shida, ni lazima utafika huko, …’akasema Soldier.

‘Na wewe mdada mlikutana wapi na huyo mtu…?’ akauliza Soldier.

‘Aliniokotea mpakani…nikiwa sijijui, ni mpakani mwa nchi hiyo yenye vita na ncho hiyo inayofadhili wakimbizi…’akasema

‘Sawa kabisa nilijua ni kwanini hataki wewe useme ukweli, huko huko ndio nia ya wauza madawa ya kulevya na biashara haramu, huwezi kulikwepa hilo…’akasema Soldier.

‘Hahaha, hamna shida, tutapambana, hujui ni kiasi gani nakufahamu wewe,…nina mambo yako mengi, na nikifika huko nayataja yote, sijali kuwa wewe uliwahi kumuoa mdogo wangu, kwanza ndoa yenye haipo…’akasema akimuangalia dada yake.

Dada yake alionekana hana raha, yaonekana kuna kitu kilikuwa kinamkera, na alipoona watu wanamuangalia, akasema;

‘Mimi naona tunapoteza muda kwa maswala mengine, sijui lengo lenu ni nini, hapa tuna jambo la awali, kutaka kujua, baba wa huyo mtoto ni nani, dada kwanini humtaji mara moja tukajua moja, hayo mengine hayatuhusu sisi…’akasema mke wa Soldier.

‘Ndio nilikuwa naanza kuelekezea ilivyo kuwa, maana kiukweli hadi nafika hapa bado nilikuwa sijaelewa, lakini nikielezea wapi nilipotoka, basi mwenyewe atajielewa…sitaki kumshinikiza mtu, sitaki mtoto wangu abakai huku, nitaondoka naye..’akasema.

‘Ok, elezea wewe umetokea wapi..ilikuwaje, mpaka ukapata hayo makovu, na hayo makovu yanaonekana uliiungua uliungua na nini?’ akauliza baba akiwa kitandani.

‘Haya makovu ni athari za mabomu…nilikanyaga bomu, wakati natoroka kutoka kambo ya wakimbizi…’akasema

‘What!.....Ukanyage bomu upone, haiwezekani…’akasema Soldier.

‘Ndivyo ilivyokuwa ndio maana wengi walijua mimi nimeshakufa,….hadi wiki iliyopita ndio niliweza kuongea na wazazi wangu, huko walishamaliza matanga yangu, kwasababu waliambiwa hivyo…’akasema

‘Oh, yaonekana una hadithi ya kuvutia ya maisha yako, au mlipanga hiyo hadithi wewe na dereva, maana inaonekana na wewe u mjanja-mjanja, hebu tuhadithia hiyo hadithi vizuri….. ilikuwaje, mpaka ukatoroka huko porini, tena kwa waasi, ilikuwaje ukafika kwa waasi, na mnashirikiana nini na hawa watu, nataka ukweli vinginevyo nitakukabidhi kwa poliai…?’akauliza Soldier, na huyo mdada, akaduwaa…na kutikisa kichwa, na kusema;

‘Ina maana huamini hayo ninayokuambia, kwahiyo sasa unahitajia ukweli, sawa mimi nitausema ukweli wote, ,…najua ni kwanini huaniamini, sasa mimi sitaki kuficha kitu tena,..nitauelezea ukweli wote hata kama utawaumiza watu…’akasema huku akimuangalia dereva halafu shemeji mtu.

‘Shauri lako…’akasema shemeji mtu

‘Asikutishe huyu…huyu kwanza yupo chini ya ulinzi…’akasema Soldier

‘Hahaha…soldier soldier, ungelijua,…hahaha,eti nipo chini ya ulinzi, usngelijua kuwa mimi kuna mambo nakuhifadhia tu,kwa vile umemuoa dada yangu, pamoja na uadui wetu lakini bado najali, lakini ipo siku, dada akinielewa tu utaliona vumbi langu …’akacheka huyo shemeji mtu, halafu akageuka kumuangalia dada yake, na kusema;

‘Jiandae, tuondoke…ukweli anaotaka kuongea huyo mdada, utakuumiza, …na nisingelipenda uusikie…’akasema na dada yake akawa kama anawaza jambo, halafu akasema;

‘Mimi naomba kwanza tuongea mimi na huyu mdada pembeni, nina wazo kwake, na ….sioni kwanini upoteze muda wako hapa, wewe sema neno moja huyu mtoto ni wa dereva, au Soldier, mimi nimeshajua huyu mtoto ni wa nani, nina ushahidi,…lakini kauli njema ni ya mzazi au sio..sasa sema ni nani baba wa mtoto, basi inatosha…’akasema

‘Dada kiukweli, hata mimi nimechanganyikiwa, ….kwa hivi sasa hata sielewi, lakini nina imani kuwa mwenye atajijua, nikianza kuelezea ilivyokuwa…, lakini kwanini nisielezee nilivyopata hiyo mimba, ..sikupenda, …sikutarajia, naona ilikuwa ni mapenzi ya mungu…’akatulia.

 Wakati anaongea hivyo Soldier akachukua simu yake na kupiga namba, akasogea pembeni kidogo halafu aakarudi na kusema;

‘Haya elezea…tusipoteze muda, nimeshapiga simu polisi, wakati wowote wanaweza kufika hapa…’akasema Soldier

‘Polisi wa nini, Soldier sasa unataka kuharibu…?’ akauliza shemeji sasa akiangalia mlangoni

‘Waache waje….’akasema huyo mdada na kuanza kuelezea kisa cha maisha yake ambacho ndio chanzo cha kupata mtoto ….

‘Mimi nimezaliwa hapa hapa Tanzania, ila mama ni mzaliwa wa nchi hiyo yenye machafuko, wasi wanapiga na serikali… na baba ni Mtanzania….wazazi wangu walihamia kwenye hiyo ncho katika kutafuta maisha, walihamia huko kabla ya machafuko na sisi tukiwa wadogo sana….’ Mdada huyo akaanza kuelezea….


NB: Tuvute subira tusikie kisa cha huyu mdada, na ndani ya kisa hiki ndio utapata ukweli halisi wa mtoto, alipatikanaje.


WAZO LA LEO: Kujenga chuki, na kutafuta sababu ya chuko, badala ya kujenga urafiki na kutafuta njia za kuwa marafiki, ni dalili kuwa sisi hatuna imani thabidi na muumba wetu ambaye katuagiza tupendane tuhurumiane. Watu kila mara hutafuta sababu za kuchukiana, utakuta umimi, sisi…nk ndiyo mazungumzo yetu
Ni mimi: emu-three

No comments :