Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 27, 2017

KITANDA HAKIZAI HARAMU-28



‘…. Sasa kwanini usiwe na amani, wakati mtoto keshafikishwa kwa wenyewe…?’ akauliza mama, akimuuliza huyo mdada aliyekuwa kajifunika usoni.

‘Mama, hivi kweli kuna mzazi anaweza kumuacha mtoto wake kwa watu baki..sawa tunaweza kusema labda, mtoto kafikiswa kwa watu ambao unajua ni damu yao,…labda,  lakini je mtoto mchanga kama huyo anawezaje kukaa  mbali namama yake..?’ akawa kama anauliza na mama akamuelewa na kusema;

‘Kiukweli hakuna, lakini mbona hatukuelewi, wewe ulimuokota ukatimiza wajibu wako au sio….?’akauliza mama

‘Mama mimi…’akasema hivyo halafu akamgeukia ndugu yake, halafu kwa mashaka akataka kumuangalia dereva, halafu, akatizama chini, akawa kama anawaza, halafu akainua kichwa na kumuangalia shemeji wa mtu…kwa haraka akarudisha uso kwa mama, na kusema;

‘Mimi mwenyewe ndiye mama mzazi wa huyo mtoto…’akasema

‘Nini, mbona hatukuelewi..ina maana wewe ndiye uliyemzaa huyo mtoto, sasa ilikuwaje uje kumuokota jalalani…?’ akauliza

‘Ni hadithi ndefu sana,…ila nimekaa na kufikiria sana, na kufikia uamuzi kuwa nimfuate mtoto wangu,…nije nimchukue mtoto wangu, siwezi tena kuendelea na mpango huo…’akasema

‘Mpango huo, mpango wako na nani…?’ mama akamuuliza huku akimtupia jicho dereva, na dereva alionekana kuwa na wasiwasi!

‘Kiukweli nimeamua kuja kufichua siri yote ili moyo wangu uwe na amani,…mama mimi ndiye mama halisi wa mtoto huyo, na nimekuja kumchukua mwanangu….’akasema na mara akawa anajifunua uso wake, kubakia wazi, na wote humo ndani wakawa wameshikwa na butwaa..

Tuendelee n kisa chetu

******************.

‘Wewe….’aliyesema hivyo alikuwa dereva

‘Haiwezekani…’akasema Soldier

‘Unafanya nini sasa…’alisema Shemeji

‘Dada….mbona unaharibu tena…’akasema Yaya akimuangalia dada yake, lakini dada yake akawa anatizama chini, kuonyesha aibu au fadhaa,….na aliacha muda kidogo ili watu wajirizishe na wanachokiona , na baadaye akafunika, na kusema;

‘Nimefanya hivi ili watu wajirizishe, na yule ambaye ananifahamu ajue kuwa mimi ndiye yeye, …na hasa huyo baba mwenye mtoto,..najua huenda asinitambue tena kutokana na makovu haya, lakini sura inaonekana wazi, au sio…?’ akamuuliza dada yake.

‘Dada usingelifanya hivyo jamani…’akasema mdogo wake.


‘ Nimeshindwa kuvumilia mdogo wangu, unisamehe kwa hilo, na najua kwa njia hii tunaweza kufanya hicho kitakachowezekana, mungu atakuwa nasi daima..’akasema.

‘Dada…’mdogo wake akazidi kulalamika.

‘Unajua mdogo wangu huwezi kujua mapenzi ya mama kwa mtoto mpaka upitie uzazi, upitie miezi tisa, tena ile ya mateso, unaumwa, unajiuguza huku mateso ya mimba yanakuandama huku hujui hatima yako ni nini, na bado uzae kwa shida…....hapana, mimi siwezi kuachana na mtoto wangu kamwe…’akasema.

'Dada, unajua maisha ya familia yetu yalivyo, wewe ndio twakuhitajia ukafanye kazi ili uweze kwenda kuwasaidia wazazi wetu.., je utafanyaje kazi ukiwa na mtoto, na wakati baba yake yupo, …’akasema mdogo wake.

‘Baba yake…baba yake gani umesikia kauli zao, hakuna anayekubali kuwa huyu ni mtoto wao, nimepata taabu muda wote huo namtafuta ….haya mtoto huyu hapa, baba yake hamkubali…’akasema sasa akimuangalia dereva..

‘Lakini mimi sio baba yake….’akasema dereva, akatahayari.

‘Dada ni vyema kama wanamkataa huyo mtoto tufuate sheria, ili haki ya mtoto ipatikane, na ….’akasema na dada yake akasema;

‘Sitafanya hivyo kamwe…wangapi wanafanyakazi na watoto wao...nimeamua hivyo,  nitaondoka na mtoto wangu, nitaishi naye kwa vyovyote iwavyo,..’ akasema na mama akasema akimuangalia huyo mdada;

‘Lakini wewe binti, hujatuweka wazi ni nani baba wa mtoto, mimi ni bibi wa mtoto nipo tayari kumlea mjukuu wangu, lakini tupe uhakika, je baba wa mtoto huyo ni mwanangu au ni dereva, na hata huyo dereva kwa mujibu wa baba yake, huyo sasa naye ni mwanangu…’akasema mama.

‘Ni kweli mama..kama angelikuwa ni mtoto wangu , kwanini nimkatae…’akasema dereva, na aliposema hivyo, Shemeji wa mtu akamsogelea huyo binti na kumshika mkono, huku akisema;

'Sikiliza...kamchukue mtoto wako uondoke naye, na usionekane tena maeneo haya...'alisema shemeji na kitendo kile kilimfanya Soldier amuangalie kwa mashaka, ni kwanini huyu mtu anafanya hivyo,…lakini hakusema kitu.

'Nitafanya hivyo lakini ni lazima kwanza niuseme ukweli, ni vyema baba wa mtoto aufahamu huo ukweli,..na sijui kwanini, lakini…sawa nitawaambi ilivyokuwa,  ili hata nikiondoka hapa nisije kulaumiwa….’akasema.
 
'Ukweli gani unaoutaka wewe…wameshamuona huyo mtoto au sio, sasa wataka kusema nini tena, ..unataka kuharibu,… sikiliza kwanza nikuambie,.., unakumbuka nilivyokuambia,…sitaki turudie kule tena,…kwanza ukumbuke, nilivyokuhangaikia,… sasa kwanini unafanya hivyo…’akasema shemeji akikatiza katiza maneno kuficha jambo fulani.
Soldier akawa anamuangalia shemeji yake huku akiwaza;

‘Nahisi huyo mtu kuna jambo na huyu mdada, kwanza huyu mdada ni mkimbizi, amekujaje huku…ok, naanza kuelewa, inawezakana wana biashara za pamoja, itabidi niwasiliane na watu wa usalama wa mpakani, ….kwanini unamshurutisha huyo mwanamke aondoke…’akataka kuingilia kati na kusema;

‘Hebu kidogo hapo.., kuna kitu gani kip kati yako na huyo dada, nahisi unataka kumuondoa hapa ili asiuseme ukweli, na huo ukweli huenda unakuhusu, au utakuweka matatani…?’ akauliza Soldier.

‘Haya hayakuhusu wewe,..haya ni yangu na huyu mdada, unasikia, usitake kuingilia mambo,…hujui katokea wapi huyu…na kwanza nyie mumeletewa mtoto , damu yenu mnamkutaa, tunapoteza muda hapa bure,…sasa sikiliza huyu dada anaondoka, na hakuna kudai mtoto tena...si mumemkataa….kila mtu kasikia, baba, watoto, haya mnataka nini tena…’akasema na kumgeukia huyo mdada.

‘Umeshawaona walivyo hawa watu, hawa watu sio waungwana…usitegemee huruma hapa..nashangaa kwanini umewaletea huyu mtoto wako, nilikuambia mimi naweza kumlea, umeona sasa…, hapa hakuna baba wa huyo mtoto, au nadanganya…umewasikia wenyewe wakikataa, kuwa huyo mtoto sio wa kwao,...umeonaeeeh, wanachoshindwa kusema ni hivi; huyo mtoto ni mtoto wa haramu..' akasema.

‘Eti nini….?’ Akauliza kwa hasira,…’Sijasikia mtu akitamka maneno hayo, na hakuna mtu anayeweza kumkataa mtoto wake, mtoto atakuwaje wa haramu, sitaki kusikia kauli hiyo, na atakayesem hivyo, nitakosana naye, mnasikia,…’akasema akiwaangalia Dereva na Soldier.
‘Hayo ni yak wake, bwana….’akasema dereva, Soldier yeye alikaa kimia, akili yake ilikuwa mbali ikijiuliza maswali mengi, na hapo alikuwa akijaribu kufahamu uhusiano wa Shemeji yake na huyo mdada, alishawawekea alama ya kuuliza.

‘Hivi mnajua jinsi gani huyo mtoto alipatikana..hakuna anayejua hilo..hata …sitaki kusikia jamani,…naona niondoke hapa tu…haramu haramu…acha hizo kauli mbaya,…hata kama kamzaa nje ya ndoa, lakini sio kwa…hata mimi nataka kuondoka..'akasema.

‘Lakini dada ukiondoka hujaweza kulitatua hili jambo, mwisho wa siki utaumua mwenyewe..na wazazi wetu je…’akasema mdogo wake, na Shemeji mtu naye akadakia na kusema;
 
 'Ina maana hukusikia walivyosema, japokuwa sura ya mtoto na wao huwezi kusingizia, lakini bado wanamktaa…muhimu ni kuamua moja, …hebu twende, mimi nitakusindikiza…huyo mtoto yupo wapi,..,'akasema shemeji mtu.

'Ngoja kwanza, je mpo tayari niondoke na huyu mtoto bila kuujua ukweli, je hakuna baba wa huyu mtoto hapa ndani…?’ akauliza.
‘Baba wa mtoto halisi anayemfahamu ni mama, wewe ndio utuambie huo ukweli…’akasema mama.
 
'Kama ingelikuwa mimi, ndio wewe ningeshaondoka na huyo mtoto, na baba yake asingelimuona tena...'akasema shemeji.

'Kaka kwanini unamsisitiza huyu mdada afanye hivyo, mimi sioni sababu ya yeye kufanya hivyo...kwanza ni lazima auseme ukweli, unakumbuka nilivyokuambia, ukweli ndio utanifanya na mimi niweze kuchukua hatua hatua stahiki....

'Dada hatua hiyo haina mjadala, familia hii haikufai, umesikia baba alichokifanya, kazaa, na mke wa rafiki yake, unakumbuka alichokufanyia,anakwenda kunywa kwa ajili ya kutaka kuingili mke wa mwanae… tabia ni hiyo hiyo, utaolewa hapa lakini kumbuka maneno yangu, kamwe hutakuwa na amani..'akasema.

'Dada hebu tuambie ukweli ulivyo, nakuonea sana huruma, nahisi umepitia maisha magumu sana, je majeraha hayo yalisababishwa na huyo mwanaume,...je ni huyu mume alikutenda hivyo...?'akauliza akimnyoshea kidole Soldier.

'Hapana....'akasema huyo mdada kwanza akimuangalia Dereva halafu Soldier.

'Sasa kwanini husemi huo ukweli, ni nani hasa baba wa ukweli wa huyo mtoto...'akasema mke wa Soldier. Na huyo mdada akamuangalia kwanza Dereva halafu Soldier, halafu akainama, na machozi yakaanza kumtoka.

‘Sikiliza binti, mimi nawafahamu sana wanaume, ni kweli hawa wanangu wote wawili wana wake zao, huenda kila mmoja anaogopa akiusema ukweli kuwa huyo ni mtoto wangu mkewe atakosana naye..lakini hata iweje, ukweli ni lazima ujulikane, baada ya hapo tutakaa na kuona tutalitatuaje hilo..au sio…?’ akasema mama akimuangalia mke wa Soldier.

‘Mama mimi, naona tusizunguke zunguke, bro,.. hebu kubali yaishe…huyo mtoto ni wa kwako bro…unaona jinsi gani mnavyofanana….’akasema dereva akimuangalia Soldier.

'Kwanini unasema hivyo dereva, kama kweli angelikuwa ni mtoto wangu kwanini mimi nimkatae, wakati hata mke wangu keshampenda, kwanini niwe na roho mbaya kiasi hicho..mimi nahisi huyo mtoto, ni wako, kwanini umkatae, najua ni kwanini unafanya hivyo, ni kutokana na tabia zako chafu, za utapeli,..hili sio swala la kutapeli tena, na nakuahidi tabia yako hiyo nitaimalize,sasa kama hutaki kusema ukweli, ok, sawa mke wangu na mimi tutamchukua huyo mtoto, tusaidiane na huyo mdada, hadi hapo ukweli utakapojulikana, na tutaujua tu, ngoje ufike polisi…'akasema akimuangalia mkewe.

Mkewe akaishia kucheka, akacheka sana, halafu akasema:

'Sijawahi kuona hii, hivi kwanini mnaogopa kusema ukweli, kuwa mtawakosa wake zenu wa ndoa....mume wangu, niliishakuambia, awali, ukweli wako ndio utakaonipa matumaini kuwa kweli, ulichofanya hukukusudia, lakini mpaka hatua hii, yaonyesha wazi kuwa ulikusudia,na kwahiyo, mimi naondoka, ila nataka tuongee na dada hapa,yeye ni nesi, na mimi ni mfanyabiashara, nimeamua kujiajiri, kwahiyo hatutashindwa kumlea huyo mtoto….’akasema mke wa Soldier.
‘Lakini mimi sihitajii tena msaada wa mtu, nimesema naondoka na mtoto wangu, niwaombe msamaha kwa haya yote, ….sawa jamani…’akasema huyo mdada aliyekuwa kajifunika.

‘Hapana huwezi kuondoka,…’ilikuwa kauli ya baba kitandani.
‘Kwanini baba…?’ akauliza huyo binti, na kabla hajajibu, mara mlangoni akaingia mama mmoja, alikuwa ni mama mjane, akionyesha ana wasiwasi sana. Kwanza akasimama pale mlangoni kwa muda kabla hajaingia ndani.

'Mama ingia umsalimie mgonjwa, keshapona, kaweza hata kukaa mwenyewe kitandani…'akasema dereva. Na mama akaingia na kuanza kusalimiana na mgonjwa, baadae akageuka kutaka kuondoka, huku akisema;

'Samahani, naona mpo kwenye maongezi,…lakini nataka kuongea na wewe...'akasema akimuangalia mtoto wake dereva

'Kuhusu nini tena mama, ngoja nimalizane na hawa ndugu zangu.

'Nimeshakuambia,…namtaka huyo mjukuu wangu, hakikisha unamchukua leo hii, yule ni mtoto wako, nimemuangalia kwa makini, ile ni damu yako,…unasikia sitaki hiyo tabia yako tena..kubadilisha badilisha mambo, unataka kupata nini kwa ajili ya hilo…, hebu wewe fikiria mwaka sasa unatarajia kupata mtoto, hujampata, haya umempata huyo ..hata kama sio kwa njia halali, lakini ndio damu yako,..’akasema mama yake.

‘Mama huyo sio mtoto wangu, nakuhakikishia mama, docta alishanipima, bado muda wangu wa kupata mtoto, kuna mapngufu mwilini, lakini yataisha tu…’akasema dereva.

‘Mimi ni mama yako, huwezi kunificha kitu… nafahamu mengi kabla yako, usifanye makosa hayo ya kukataa damu yako..’akasema mama yake.

‘Lakini umejuaje kuwa ni mtoto wa mwanao…’akauliza mama yake Soldier.

‘Nimejua tu…’akasema mama yake dereva na kumgeukia mwanae

‘Mama…’akasema kutaka kujitetea

‘Sitaki kusikia zaidi…kama ni mke wako nitaongea naye, hakuna shida…wewe umerithi uzazi wa baba yako, unasikia, kumpata mtoto mwingine inaweza isipatikane, mkeo naye hajulikani, huenda ana matatizo, sasa kwanini uikatae hii bahati…’akasema mama yake.
Na mara mlangoni tena akaonekana mdada mmoja akiingia, na wote wakageukia mlango , na huyo mdada alipona hiyo hali akasita kuingia, baadae akajongea taratibu, akionyesha mashaka mashaka.

‘Mke angu umekuja, mbona hukunipa taarifa…?’ akauliza dereva.

‘Nimeamua kuja tu, ….na nilipokuwa hapo mlangoni nimesikia mama akiongea neno, Mama, mbona unasema hivyo, mwanao hana matatizo yoyote ya uzazi, mimi hapa nina mimba,...mimba ya dereva…’akasema.

'Haiwezekani...'akasema dereva.

'Haya, kama ulijifanya huzai, ukatembea na binti wa watu, sasa huna cha kujitetea tena, sasa una watoto wawili…’akasema Soldier.

‘Watoto wawili…?’ akauliza mke wa dereva.

‘Muongo huyu…’akasema Dereva.


WAZO LA LEO: Kuna kauli nyingine zinaweza kutamkwa kwenye jamii, na zikitamkwa kumuhusu mlengwa, labda ana mapungufu fulani, au kakosea jambo, au mgonjwa..kauli hizo zinaweza kumvunja nguvu yule mtu, na kumkatisha tamaa, au kama ni tatizo, huyo mtu anaweza kujisikia vibaya na kujiona kazalilishwa, na ikaishia kuumia ndani kwa ndani, na kauli nyingine hazifai kuongea mbele ya mgonjwa, kauli hizi zinaweza zikamuongezea mgonjwa tatizo badala ya kumsaidia, tuweni makini sana kwenye ndimi zetu... 
Ni mimi: emu-three

No comments :