Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, September 9, 2016

KISA CHA BINTI YATIMA-`KWANINI MIMI...'- 2


‘Mimi sipendagi kusimulia maisha yangu maana kila nikianza kusimulia ninaishia kulia tu, najikumbusha machungu mengi yaliyonisibu, maisha yangu yamekuwa ni kidonda kisichopona ambacho kila siku kinatoneshwa na watu…..’akasema huyu bint

Kisa kilianzia pale nilipomkuta binti mmoja akiuza mihogo, na mgongoni kabeba mtoto mdogo, na mtoto huyo akawa analia sana,..hali ya yule mtoto akiwa kabebwa mgongoni ilisikitisha, nguo alizovyaa, ...na hali ilikuwa nayo, na hali ya hewaa ilikuwa ni ya ubaridi..nikashikwa na huruma , nikamsogelea huyo binti, kujua zaidi, nia hasa ilikuwa kumshauri amuonee huruma huyo mtoto..lakini majibu niliyokutana nayo, yalinifanya niingiwe na hamasa zaidi ya kumfahamu huyo binti..

Wakati nikiwa kwenye hamasa hiyo mara linazuka jingine kubwa.....

Hiki ni kisa cha binti yatima, hebu tuenddee nacho...


***************  2***********‘Sasa utasaidiwaje, maana shida ni kila mtu anazo, na hakuna anayewez
a kusema mimi nimejitosheleza, nahitaji mtu wa kumsaidia, kila mtu hata tajiri anaona maisha kwa ke ni magumu, hajatosheka…sasa ili watu waweze kuvitika na matatizo yako ni wewe mwenye shida ujieleze…’nikasama na yeye akawa kainamisha kichwa chini akilia.

‘Haya…, ndio maisha yetu yalivyo, …, huruma haipo karibu kwenye nafsi zetu, ni mpaka ifukuliwe…unaonaeeh,. Na mwenye kukuhurumia zaidi ni yule aliyewahi kupatwa na shida, na shida zipo kwetu sisi watu wa chini,….sasa,… ukiongea watu wakakusikia wakaona shida zako wenye huruma za karibu wanaweza kukusaidia…au sio, masikini tunasaidia wenyewe kwa wenyewe…’nikasema.

‘Hakuna mwenye huruma dunia hii…nimeteseka sana, watu wananiona hivi hivi,….wanajua kabisa mimi sina baba wala mama, mimi ni yatima, au yatima anatakiwa aweje,….mimi ni yatima aliyepitiliza, sina baba wala mama, wala mjomba aau shaangazi, dunia imenitekeleza….’akasema

‘Katika maisha kama hayo ukiwa mdogo wa mwaka, ..utakuwaje,…ufe, au…..sasa aliyejitolea kunisaidia ndio huyo amefariki,….wangapi waliniona na zaidi ya msaada wao ulikuwa ni masimango na kunyanyapaliwa na hata kuzaliliswa…Namshukuru sana bibi yangu, bila yeye, labda ningelishakufa zamani… oh, na ndio huyo ameshafariki, na hata bila ya watu kumuelewa…binadamu, jamani binadam..’akasema

‘Mhh…pole sana…’

‘Na sasa ndio huyo amefariki bibi yangu masikini, nitakuwa mgeni wa nani…sina ndugu sina jamaa…na na.., kinachoniuma ni kuwa amefariki hata sijapata muda wa kulipa fadhila zake, alinilea nikiwa mdogo kwa shida…., akanitibu nikiumwa,..akiwa hana mbele wala nyuma,.. akataabika kwa ajili yangu, na…za zaidi nikamuongezea  ugumu wa maisha kwasababu ya tamaa zangu za kimwili….mungu wangu kwanini, kwanini…..’akawa analia.

‘Pole sana, yote maisha….’nikisema

‘Yote maisha ehe..mnasema tu….’akainua uso uliojaa chuki.

‘Maisha…hahaha, maisha…,  mengine yanauma….yanauma ukizingatiwa kuwa mengi ya madhila hayo waliosababisha ni wanadamu wenzetu…na ni ndugu kabisa, unajua ndugu...damu moja kabisa, tena wanaume, ….’akaninyoshea kidole, huku akisema

‘Wanaume kama wewe…., eti wanajita wanaume, hahaha, kama ni wanaume kweli ni kwanini wasihangaike kivyao, kwanini kama ni wanaume mbona wanadhulumu,..nawachukia sana wanaume... unajua kuchukia,…masikini bibi yangu…’akawa analia.

‘Kwani bibi yako kafariki lini…?’ nikamuuliza baada ya kupita kitambo kidogo.

‘Ndio nimepewa taarifa leo nikiwa nahangaika kuuza mihogo…lakini sijui kama kazikwa au la..maana hakuna mawasiliano huko kijijini,na huenda wamemtelekeza kwenye kibanda chake, baada ya kumfukuza kwenye nyumba yake ya urithi……na ndugu niliotegemea waniambie nini kinachoendelea ndio hao hao  aaah, bibi yangu masikini….’akawa analia.

‘Pole sana….’nikasema

‘Oh…bibi yangu masikini, hivi mzee kama yule kawakosea nini jamani, nyie walimwengu mna nini jamani, bibi, kizee, hakina nguvu kabisa, masikini , hohe hahe…wana..wana…ole wao, nasema ole wao..…nilijua tu... nilijua mwisho wa siku watamuua tu…’akasema

‘Ina maana wamemuua…?’ nikauliza

‘Kifo chake kitakuwa kimesababishwa na vipigo na mfadhaiko alioupata…sijui kwanini watu hawana huruma, hivi kama wana miguvu kwanini wasiende kupigana wakapata pesa, eti…yaani wanakwenda kumpiga kizee wa watu,…ni kwanini lakini…’akasema.

‘Kipigo…!, mfadhaiko..!…hebu anza hatua kwa hatua, kwanini bibi yako alipata kipigo..?’ nikamuuliza.

‘Eti wanasema bibi ni mchawi..’akasema na watu waliokuwa wasikiliza wakaguna,

‘Ndio wanavyosema na hilo lilimuumiza sana bibi…hakujua hata ajitetee vipi,akawa analia tu, akimuomba mungu amsaidia, hakuwa na jamaa wakumsaidia, ikabakia kila siku akilia, akimuomba mungu siku ifike aondoke hapa duniani, kuliko kupata adha hiyo…lakini aliomba kwanza anilee nifikie hatia fulani…..’akatulia

                         ***********

‘Mchawi,…..?’ watu wakaguna na kuuliza

‘Lakini wazee wengine vigagula….,. Yawezekana bibi yako kweli alikuwa mchawi kweli….’watu wakazidi kuongea..

‘Ndio zenu hizo,…..mna uhakika gani na hilo…kama na nyie sio wachawi…wanafiki wakubwa nyie…hakuna aliyemfahamu bibi, hakuna..zaidi ya uzushi huo….’akasema akiwaangalia watu kwa hasira na hapo kukazuka zogo, kila mtu akiongea lake

Kulizuka mabishano ya watu kila mmoja akisema lake, wengine walifikia kusema huenda kweli huyo bibi alikuwa ni mchawi, lakini huyo binti hakujua tu, au hata huyo bintu anajua lakini anamtetea tu bibi yake…..wengine wakasema ni imani haba tu….yaani kila mtu akawa anasema lake, …nilitaka hayo mabishano yaishe ili niweze kumsikiliza huyo binti…kwani atakeyeweza kuelezea ukweli wote ni huyo binti!

‘Hebu nikuulize kwanini walisema bibi yako ni mchawi , alikuwaje mpaka wakamuhisi hivyo, maana wewe ulikuwa unaishi naye au sio, kwahiyo unamfahamu alivyokuwa, unajua lolote kuhusu bibi yako…?’ nikauliza.

‘Hata sijui hayo ya bibi mchawi yalianzaje,…’akasema.

‘Ukituelezea maisha ya bibi yako, itakuwa rahisi kwetu kuyafahamu hayo….’nikasema
‘Mimi bibi yangu ndiye aliyenilea, baada ya wazazi wangu kufariki,..hata siwajui wazazi wangu wanafananaje,…maana hata picha hakuna,…wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo sana, bibi anasema nilikuwa na mwaka mmoja tu, unaona…sasa kama angelikuwa ni mchawi angenichukua mimi, angenilea mimi,…’akaanza kuelezea.

‘Si ili urithi uchawi wake…’akaropoka mtu mmoja.

‘Hujui unachokisema, kwasababu humfahamu bibi yangu…’akasema

‘Wazazi wako walikufa wote wawili kwa pamoja?’ nikauliza, nikitaka kudodosa ili kujua ukweli halisi wa binti huyo, kuliko kuchukulia juu, juu tu..

‘Alianza kufariki baba…..nilivyoambiwa na bibi, ..baba aliumwa sana, lakini chanzo cha ugonjwa wake ni kuwa alikuwa hajatulia, mlevi, mnzizi….ndio maana nasema siwapendi wanaume…kwasababu kutokana na tabia yake hiyo ya ulevi na umalaya, ndio alimuambukiza mama yangu, mama alikuwa mpole sana mcha mungu, lakini kutokana na baba, aah, nyie wanaume….’akasema akitikisa kichwa.

‘Oh…unasema baba yako ndiye alimuambukiza mama yako, una uhakika gani na hilo…?’akauliza jamaa mmoja.

‘Ndio nina uhakika..japokuwa sikuwepo, sikuwahi kuyaona maisha ya baba kwa macho yangu, lakini mengi niliyasikia kuhusu maisha yake, na sio mtu mmoja tu, wengi,….na hata waliowahi kutembea naye wamathibitisha hayo…wengi ni marehemu, waliopo hai walielezea kwenye…haya mambo ya ukimwi na matumaini…’akasema

‘Kwahiyo maisha ya baba yako unayafahamu kwa kupitia mazungumzo ya watu au sio…., je unaweza kutusimulia kidogo jinsi ulivyosikia kwa watu…, kwa faida ya watu wengine ili wajifunze, ..kama hutojali lakini…’nikasema

‘Siogopi kuyasimulia, …maana maisha yake yamekuwa ni funzo pale kijijini, kila mmoja amekuwa akitolea mfano kwake, hasa mzazi anapomuona mtoto wake anapotea, anakuwa mlevi, Malaya..ana uchu wa madaraka, hamtunzi mkewe….watu wamekuwa wakitoa mifano kwa kupitia maisha ya baba..kwahiyo hata nisipoongea mimi leo…, yameshaongelewa sana…mungu amsamehe tu baba yangu…’akasema

‘Kwani baba yako alikuwaje, maisha yake yalikuwaje ulivyosikia kwa watu...?’ nikamuuliza

NB: Haya haya…huyu baba mtu alikuwaje, kwani alikuwa kiongozi, mzazi…na mwenye uwezo kifedha, je hayo yalikuwaje mtihani kwake, na kwa jamii…, ni sehemu muhimu yenye mafunzo itafuata baadaye

WAZO LA LEO: Wazazi tunatakiwa tuwe kiyoo cha familia zetu, matendo yetu, tabia zetu huwa zinaaksi maisha ya watoto wetu, kwahiyo tuweni makini sana. Sisi wazazi ndio chanzo cha misingi mema ya watoto wetu,..huwezi ukamfunza mtoto adabu wakati wewe mwenyewe ni mtomvu wa nidhamu, unapigana na mkeo, mnazozana mbele ya watoto…hutunzi vyema familia yako..haya na mengine mengi huathiri sana maisha ya baadaye ya mtoto wetu. Na kama unatenda madhambi kwa watoto wa wenzako ujue na wewe madhambi hayo yatahamia kwa watoto wako. Uone jinsi gani mzazi ulivyo na dhamana kwa familia yako.

Tumuombe mungu tuwe wazazi wema, tutimize wajibu wetu, hata kama maisha ni magumu lakini hivyo hivyo tu, kwa matendo yetu mema, tabia njema… tunaweza kuwafanya watoto wetu wakawa nguzo imara ya vizazi vyetu.
Ni mimi: emu-three

No comments :