Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 30, 2016

YOTE NI KWA MAPENZI YA MUNGU-13‘Sawa tupo pamoja…mimi nipo tayari kwa lolote lile ilimradi hilo deni lilipwe….na kama mnasema sio deni la kaka,  niambieni ni la nani, unajua mimi ninawashangaa kwanini hamtaki kunionyesha huo ushahidi wenu ambao umewaonyesha kuwa hilo deni sio la marehemu kaka….nimeshawauliza mara nyingi kuhusu hilo, lakini hamjaweza kunitolea hata ushahidi mmoja…na uwe ushahidi wa kimaandishi, ambao tunaweza kusimama nao mahakamani…’akasema

 ‘Sawa wewe tuliza kichwa, natumai kesho tutaongea, na tutaulizana maswali yetu, tuone tutafikia wapi, uwe tayari kwa hilo…’akaambiwa

‘Maswali ,… maswali..hivi mnafikiria mimi mtaniweza kwa maswali…hahaha…haya karibuni sana…mnajidanganya kweli, …kiujumla nyie mnanipotezea muda wangu bure….’akasema akifunika shuka, kama vile anasikia baridi .

Jioni tulirudi tena kumjulia hali, alionekana yupo vizuri tu, na sijui kwanini docta hakutaka kumruhusu, lakini hatukutaka kulazimisha, sasa wakati tunatoka  na mama mjane nikaweza kumuuliza;

‘Huyu docta ana udugu wowote na familia ya mume wako….?’ nikamuuliza na mama mjane akasema;

‘Mhhh, hapana huyo docta nisikiavyo, ni kaka wa ……huyo mwanamke wake wa siri, hawa watu wana damu za nchi mbili….’akasema mama mjane akitizama nyuma kwa mashaka.

‘Mke wa siri…una maana waitavyo nyumba ndogo au…?’ nikamuuliza

‘Mhhh…mimi sijui hayo, ila ndivyo nisikiavyo…’akasema hivyo tu , na alionekana hakutaka kuliongelea hilo zaidi nikajua ni kwanini…

                               *********

Siku nyingine tulifika na Dalali, alikuwa sasa yupo katika hali nzuri tu, na ilivyoonekana alishajiandaa kuondoka, kwani alisharuhusiwa , alikuwa akisubiria kibali kutoka watu wa usalama, na aliyesubiriwa kufika ili aweze kukipata kibali hicho ni mpelelezi, ….

Mimi nilipofika tu…akasimama, na kuniangalia kwa jicho la dharau na kama kawaida yake akacheka huku akinyosha nyosha suti yake kwa majigambo  akasema;

‘Eheee, wewe mtu umefika, nakutafuta sana, ..yaani ungelijua ninavyoku-mind…nikuambie kitu  sasa hivi mimi nipo tayari kupambana na nyie watu, wewe na huyo mpelelezi….msifikiria baada ya haya yote mimi nimerudi nyuma, ..hapana, sasa ni hivi,….. mimi nikitoka hapa nakwenda kuonana na watu wa benk  nijue wamefikia wapi…kama msimamo wao ni huo huo wa kupiga hiyo nyumba mnada basi mimi sina budi kutii amri ya mahakama…’akatulia kama anawaza jambo halafu akainua kichwa na kuniangalia akasema;

‘Ehe, nambie…wewe ulifikia wapi…au hujaenda hata huko benki au huko mahakamani kuwauliza, maana sikuelewi, ..haya mambo huwezi kuyamaliza kwa kupoteza muda na mimi,…nakushauri wewe kama ndugu, au sio nenda benki, nenda mahakamani ujuaribu kuongea na wao, au umeshafanya hivyo…?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimia

‘Sasa ndio hayo mambo siyataki,… mimi siwezi kuumia tena, mimi nitakachofanya ni kutoa go a head… waendelee, unajua, mimi nimechoka, …hapa akili imechoka, mumenisumbua sana nyie watu, haijatokea hivi………’ alirudi kwenye kitanda akakaa huku  akionyesha shauku ya kuondoka.

‘Kwahiyo wewe hupendezewi na hizi juhudi zetu za kutaka hiyo nyumba isipigwe mnada kwa masilahi ya mjane na watoto wake….si ndio hivyo?’ Nikamuuliza na yeye akiwa ananionyeshea kwa mikono akasema;

‘Unielewe ndugu….sio kwamba sipendelei hilo, lakini je hilo deni litalipwa eeh, na litalipwaje,  na nini, na nani,…that’s is my point…sijui unanielewa,….’ Akaniangalia , halafu alipoona sisemi kitu akaendelea kuongea.

‘Au kama mumepata mfadhili mniambie,hahaha… sijui nani atakubali kubeba mnzigo wote huo,….maana deni kama deni lipo pale pale, vinginevyo…..mhh, labda benki  aweni shemeji zenu,…eti, …haiwezekani, kuna mkataba wa kukubaliana, au sio…kwamba  mumeshakubaliana nao kuwa hilo deni lifutwe, au…’akaniangalia huku akitabasamu kidharau

‘Unaona…hahaha, hamna jipya nyie…eti deni lifutwe hata kama ingelikuwa ni mimi ndio hao benki nisingelikubali hilo..pesa yote hiyo, hebu jaribuni kufikiria na nyie, anyaway, mimi sijui…unafikiri, hao watu hawawezi kukubali hilo, piga ua hilo  deni lipo na nyumba hiyo itapigwa mnada..wewe si utaona tu….unajua,  hata mimi sipendi lakini sasa tufanyeje…tufanyeje sasa, hebu niambie ndugu..?’akatikisa kichwa kama anasikitika huku akiniangalia akitaka niseme neon.

Mimi nilimtizama kwa makini, nikiwazia ….maana ukimwangalia jamaa unaweza kusema yupo sahihi, na anavyojua kuigiza, kiukweli huwezi kumfikiria lolote baya,…lakini akilini sikukubali, nilitaka kuthibitisha hofu yangu, yaweza asihusike moja kwa moja…hapo nikasema;…

‘Benki wana haki na taratibu zao, na ni wajibu wao kufanya hivyo, ..lakini kwanza ni lazima tutafute ukweli wa hilo deni, tujirizishe, …ni kweli kuwa bado benki wanataka mnada ufanyike, na hata sijui kama watavumilia zaidi. ..lakini  hata hivyo, na wao…’nikatulia, pale nilipoona mpelelezi  anaingia na askari mwingine, ….

‘Na wao wana…wana nini..?’ dalali akaniuliza lakini sikumjibu, nilitulia nikimwangalia mpelelezi aliyekuwa akiingia.

                                              **************

Mpelelezi aliingia huku moja kwa moja akimuangalia Dalali pale alipokaa,…kwanza hakusema neno, alionekana kama kuna jambo zito, kama sio tabia yake ya kukunja uso…nilimuona akijaribu kulazimisha kutabasamu, alipomwangalia Dalali, na mimi anatikisa kichwa tu kunisalimia, hakutamka neno, akasogea hadi pale alipokaa Dalali na kuanza kumuuliza hali yake…, na Dalali akawa anamjibu kwa mkato, mkato tu kuashiria ana donge au hasira na mtu huyo.

‘Sasa Dalali…sisi bado tuna maswali mengi dhidi yako, na kama ulivyoambiwa na docta unatakiwa uwe na afya ili uweze kupambana na misuko suko mingine,…na nia yetu ni njema kabisa, ni kutaka kumalizana na hili tatizo, kiufupi bado kuna utata mkubwa, ….’akaanza kusema mpelelezi, na Dalali aliposikia kauli hiyo akataka kumkatiza mpelelezi , lakini akaghairi na katulia , na mpelelezi akaendelea kuongea;

‘Utata upo kwenye huo mkopo wenyewe, kuna walakini nyingi …lakini huko kwenye huo mkopo, mimi sipo sana ,nashukuru yupo mwenzetu hapa kaamua kujitolea kuutafuta ukweli, nimemruhusu asaidiane na rasimi na sisi, kwahiyo keshapew kibali, mkuu sasa fanya kazi..’akaniambia akinyosha mkono kama kunisalimia.

‘Lakini pamoja na hayo…na, mimi nina yangu hatujamalizana na wewe,,nilishakuambia awali,..sijafunga jalada la kesi ya kifo cha kaka yako..ni ajali ndio..lakini hatujajirizisha …kuna utata pia…lakini hilo tutaulizana , muda ukifika…’akatulia mpelelezi

‘Unasema kuna utata, sasa kwanini msiulizane wenyewe, na  huyo aliyesema kuwa ilikuwa ni ajali..ina maana hamuaminiani…?’ Akauliza Dalali akimuangalia mpelelezi.

‘Nilitaka tu kukuambia hayo, kuwa hata report ya ajali ya kaka yako, sijaweza kuimalizia, faili lake bado lipo wazi, kuashiria kuwa kuna jambo linahitajia ufuatiliaji, kuna maulizo mengi, kifupi kuna utata, lakini hili litasubiria….’akasema mpelelezi  na  jamaa akainua kichwa na kumuangalia mpelelezi, akiwa kakunja uso na kusema;

‘Hayo ni yako,…mimi nijuavyo, tena sio mimi ni nyie wenyewe mlitoa ripoti kuwa kaka alikufa kwa ajali, au sio, sasa huo utata unaokuja sasa hivi, mimi sijui ni utata gani , niambie kuna utata gani….?’ Dalali akauliza kwa sauti yenye kukereka, huku akikwepa kuangaliana na mpelelezi.

                            *************

‘Nilitaka kwanza umalizane na mwenzangu, kuhusu hilo swala la deni, ili nione kama kuna kitu kinaweza kuingia kwenye upelelezi wangu, unajua kazi zetu hizi, kila jambo lina umuhimu wake,…sasa kama upo tayari tusipoteze muda,…tunachotaka kwako ni ushirikiano, ili tujirizishe,..na muhimu uwe huru, ujitahidi kutoa ushirikiano, ili mwisho wa siku tuachane nawe kwa amani…..’akasema mpelelezi.

‘Sawa haya niulize….unataka niseme nini, maana ukweli wote nimeshawaambia, labda sasa ni nyie mniambie mnataka niseme nini, niambieni, mnajua mimi nina familia inanitegemea, na kazi zangu nikiwa sipo zimesimama, mnionee huruma na mimi…’akasema kwa sauti ya kinyonge, akageuka kuniangalia  mimi;

‘Haya wewe, niambia unataka nini kwangu….’akasema akiniangalia mimi na mimi nikaanza kwa utani;

‘Unaonekana una haraka sana, kuna mishe mishe gani unaifuatilia…au ndio kuhusu huo mnada wa nyumba…maana nyie madalali kila kitu kina cha juu chenu, …usiniambie hata huo mnada una asilimia yako hapo…. , tuambie tujue na sis tuambulie,…’ nikasema na yeye akaniangalia kwa jicho moja …halafu akasema;

‘Ndugu, nikuambie kitu, ukiwa hai, unapumua,.. .ni lazima upambane na maisha,..huwezi ukakaa hivi hivi tu ukafikiria utapata…., kila mtu anahitajia maisha mazuri,sasa wewe ukilala, wengine wameamuka zamani wanachakarika, wanayafaidi maisha na mimi nikuambie kitu, …silali, kila siku nahangaika, natafua kwa njia yoyote…inayofaa…umenielewa,…..’akasema akitikisa kichwa kama kukubali jambo

‘Sasa bwana Dalali, mimi naona tusipotezeane muda, tukuulize swali, je upo tayari kutoa ushirikiano wote uujuawo wewe, ili tuweze kulimaliza hili, kwasababu sisi tulijua baada ya huo mtihani uliokutana nao, ungekuja na jambo jingine kabisa..’nikasema na yeye akabenua mdomo kutabasamu kizarau Fulani hivi.

‘Kawaida tu…..’akasema hivyo

‘Mimi nilijua mitihani yote hiyo ni jinsi ya kukumbushwa  jambo…..na sisi kiukweli tunahisi kuna jambo, kwenye hili tatizo, …..kuna kitu kimejicha, ishara na dalili zinaonyesha, kuachia mbali  ushahidi ,…nsjus ksms ulivyosema watu wanatakiwa kuhangaika, na kila nafasi unatakiwa uitumie kwa faida, lakini kuna muda tunatakiwa kujitolea, hasa ukiangalia wahanga, hapa tuna mama mjane, kuna watoto,…tufikie mahali tuingiwe na utu, ubinadamu….’nikasema

‘Unajua sijakuelewa….unataka kusema nini, unauhitajia ukweli upi kutoka kwangu, hebu niambieni jamani, hivi mnataka nisema nini….?’ Akauliza sasa akikunja sura

‘Kwahiyo ina maana mpaka sasa umeshikilia msimamo wako…?’ akauliza mpelelezi

‘Msimamo upi…?....kwanii mimi nilikuwa na msimamo gani…?’ akauliza

‘Msimamo kuwa hilo deni  kweli ni deni la kaka yako?’ akaulizwa

‘Kuhusu hilo,…’kwanza akatulia halafu akasema 

‘Kiukweli msimamo wangu ni ule ule..maana mimi nimesimamia kwenye ukweli, siwezi kusema uwongo mnielewe hivyo na nataka mjue hivyo kuwa mimi ninachotambua ni kile kile tulichoongea awali sasa kama nyie mna jipya, mna ushahidi nionyesheni..’akasema

‘Tunafahamu tabia yako kuwa ukitaka kitu mpaka ukipate…au sio..?’’nikasema na akaniangalia akitabasamu kwa dharau, akatikisa kichwa na kusema.

‘Wewe mjanja sana…sawa ndio hivyo, ….Ok, sasa niwaambie kitu, nipeni huo ushahidi kama bado mnasema deni hilo sio la kaka, ili tumalizane na hilo,na mimi nitashukuru sana, lakini hamuwezi kufanya hivyo maana hamna jipya, na kwanza,….’akakatiza pale akiangalia mlangoni

‘Aheri shemeji umekuja, utuambie madalali walifika wapi…maana hawa watu bado hawan jipya,…’akasema akiangalia mlangoni.

Shemeji yake alikuwa akiingia mlangoni…na baadaye ukapita muda wa kusalimiana, na Dalali akauliza swali lile lile

                                            ************

 

‘Haya shemeji tuambie hao watu wa kupiga mnada walikuja…maana nimekuwa nje ya dunia…?’ akauliza, na shemeji yake akasema;

‘Ni kweli walifika hao watu, kampuni gani sijui…. lakini walikuta karatasi mlangoni kuwa mnada hautafanyika mpaka kuwe na muafaka,…wakaondoka, lakini wao wakaweka kufuli lao pale mlangoni wakidai wao wanachofuata  ni amri ya mahakama, kwahiyo hakuna mtu kuingia humo….’akasema mjane

‘Sasa nyie mlilala wapi..?’ nikauliza

‘Kwenye mabanda ya uwani, kuna kitanda…’akasema mjane

‘Mhh, Dalali, umesikia hayo, familia iliyopo chini yako imelala nje, kwenye mabanda ya uwani wakati nyumba yao ipo….sasa ndio mwanzo huo, je nyumba ikichukuliwa, watakwenda kulala wapi?’ Nikauliza na jamaa akaniangalia kwa macho yenye hasira na kusema;

 'Hivi kwanini unasema hivyo!, …ina maana mimi ndio nimesababisha hayo yote..usinipakazie ubaya wewe ndugu…ni mimi au ni benki waliofanya hivyo? …wewe mtu una lako jambo…wao wamelala mabanda ya uwani na mimi nimelala wapi…? Na mimi si ndio nateseka  huku, ulitaka mimi nifanyeje, na kiukweli yote haya ni nyie, haya yangelikwisha isha tukajua moja…’akasema akinionyeshea kidole, na mpelelezi akaingilia kati na kusema;

 ‘Naona tuulizane hayo maswali tuone tutafikia wapi,….maana mimi nina kazi za kufuatilia, hili jambo linanipotezea muda…., lakini lazima leo tufikie muafaka,  ili hatua nyingine zifuatwe, hatuwezi kuvumilia tena, kama ukweli upo,basi sheria ichukue mkondo wake…’akasema mpelelezi, na Dalali kusikia hivyo akamtupia jicho la haraka mpelelezi, akataka kusema jambo lakini mimi nikamuwahi

                                                      ***************
‘Umesema wewe unataka ushahidi wangu kuwa ni kwanini mimi nasema kuwa hilo deni sio la kaka yako au sio…?mimi awali nishakuonyesha ni kwanini nimevutika kufanya hivyo na kuamini kuwa huo mkopo una walakini, ya kuwa huenda huo mkopo hakuuchukua kaka yako…sasa kama hakuuchukua kaka yako aliuchukua nani,….ndio hoja yetu hapo umeona eeh?.’nikasema hivyo kwa kumuuliza  na Dalali akasema kwa haraka;

 ‘Ndio…hiyo ndio hoja yako…, na mimi ndio maana ninasema ninataka ushahidi wa kuthibitisha hoja hiyo yako…tusiongee tu kama hadithi, je unao ushahidi kuthibitisha hoja yako….?’ Akaniuliza, na mimi sikumjibu mioja kwa moja, yeye akaendelea kuongea

‘Mimi wakati wote huwa  nasimamia kwenye  ukweli wa ushahidi wa vidhibiti, kumbukumbu na nyaraka,….na kwa hili, nimethibitisha hivyo kutokana na nyaraka za benki… ‘akatulia kama anataka mimi niongee jambo, na mimi nikaendelea kukaa kimia.

‘Sasa ndugu, kuliko kuniuliza maswali, maswali wee…hebu unionyeshe angalau ushahidi mmoja kuwa, ni kwanini hadi sasa unang’ang’ania kuwa hilo deni  sio la kaka wakati benki  walipeleka hadi wakili wao mahakamani kulithibitisha hilo…na pili ni kwanini wewe badala ya kuwauliza benkii unaniuliza mimi!’akasema , sasa kwa sauti ya ukali na nilimuona akimtupia jicho mpelelezi, nahisi kuna kitu kimemtia mashaka.

‘Sawa nilishakuambia kuwa ushahidi wangu wa kwanza ambao ulivuta  kulifuatilia hili ni wewe mwenyewe…’ nikasema na yeye akageuka kumuangalia mpelelezi akionyesha kwa mkono wa kuuliza, au kulalamika lakini hakutamka neno na mimi nikaendelea kusema;

‘Sasa kama ushahidi wangu wa kwanza ni  wewe mwenyewe siwezi kukuachia mpaka nijirizishe nawe, siwezi kuwakimbilia kwanza benki , wewe ndiye ninaweza kupata njia ya kuwaendea hao benki kuwa hilo deni sio la marehemu…umeona eeh, kwahiyo haop benki kwangu, watafuatia baadaye kwa muda muafaka,….’nikasemaa na yeye akatikisa kichwa kama kukataa.

‘Na ndugu Dalali  ukumbuke hapa tunaongea tu, hatupo mahakamani, nia ni kujirizisha….’nikasema na yeye hapo akacheka kweli, halafu akasema ;
‘Nilikuambia kuwa mimi nahimiza hivyo sio kwa kupenda, sio kwamba nililikubali hilo deni hivi hivi tu, uliza utaambiwa,….lakini hadi kufikia mimi kuamua hivyo, ujue nimeamini kuwa kweli hilo deni kaliacha kaka…’ akatulia.

 'Hebu niambie, kama nimethibitisha hilo, na …. mimi kama ndugu yake ulitaka nifanye nini, ….nikae tu, au kwa vile kafariki basi…hata mimi siwezi kukaa kimia, mali hizo, nyumba, mashamba yalikuwa ni yake, kwanini niache kaka ateseke huko alipo..na ni nani atamsaidia kama sio sisi tuliopo duniani...Pili, mimi ndiye nilipewa majukumu ya familia yake, hilo sawa, siwezi kuitupa, nitajitahidi kadri ya uwezo wngu kuhakikisha haizaliliki, lakini kwanza ni kuhusu marehemu…’akatulia akiniangalia kwa makini.

‘Sasa nakushangaa, na kushangaa kauli yako ukisema mimi ni ushahidi, ushahidi  kwa vipi…?.’akatulia na kumwangalia mpelelezi kama vile anahitajia msaada kwa hayo aliyoyaongea.

‘Kwanini unishangae…! Mimi si ninatoa ushahidi wangu bwana,..au wewe ushahidi unauelewaje, au wewe ulitaka nimuite mtu mwingine , ushahidi wangu wa kwanza ni wewe, sawa…’ nikasema.
‘Najua ni kwanini unasema hivyo, eti ni kwa vile wewe unaniona eti labda mimi nakomalia hilo deni, kwa masilahi yangu …labda,  nikuambie kitu kama unafikiria hivyo, unakosea kabisa…, na huo ushahidi kama huu,  eti ushahid wa kwanza ni mimi mwenyewe,  huo  hauna nguvu..toa ushahidi mwingine…,’akasema

 ‘Kwanza kabla hatujaenda mbali,  kuna kitu nataka shemeji yako anikumbushe kumuhusu marehemu mume wake, eeh,…..’nikasema na Dalali akawa kama kashtuka,halafu akatulia, halafu akageuka kumuangalia shemeji yake huku akisema;

‘Hapana hilo sikubaliani nalo…sitaki shemeji yangu umuhusishe na hili, hili ni kati yangu mimi na wewe…shemeji hawezi kuvumilia hii mikiki mikiki, ….mnafahamu afya  yake ilivyo, kama ni maswali niulizeni mimi….’akasema akipiga kifuani

‘Nafahamu hilo……, lakini ni hivi, wewe huwezi kufahamu kila kitu kumuhusu kaka yako zaidi ya mke wake…, au sio…?’nikauliza na yeye kwanza akamuangalia tena shemeji yake, na kabla hajajibu hilo swali wakili wake akafika, na kukawa na muda wa kusalimiana….

‘Ohh, muheshimiwa aheri umefika…, hawa jamaa wameniwahi , lakini usijali, mimi nitamalizana nao, wala usiiingilie, kaa hapo usikilize tu, haya niachie mimi,  huu ni mpira wangu,  hawa hawaniwezi , si unanifahamu nilivyo, mimi nilitakiwa niwe wakili ,lakini ndio hivyo…..’..akasema na kweli wakili  wake akakaa na kutulia, hakusema neno. Wakili wake hakutaka kuingilia maana tangia awali alishaambiwa hivyo kuwa yeye ni msikilizaji tu.
 
Mama mjane, akaamua kuingilia kati na kusema;

 ‘Jamani mimi samahanini sana…,mimi  nisingelipenda kuongea lolote maana mimi nilisha waambia tokea awali kuwa yote nimeshamuachia mungu, nikifanya lolote zaidi kwa sasa kulalamika, ku-ku-hapana, jamani mnionee huruma, nimechoka, mimi namuamini mungu wangu,…na  nasubiria mapenzi yake tu yatime….., basi….’akasema huyo mama mjane.

 naona…ahsante sana shemeji yangu….’akasema Dalali, akitikisa kichwa kama wafanyavyo wahindi wakikubali jambo

‘Dada,ni kweli, nimekuelewa sana, lakini kwa hili mimi nahitajia kauli yako ya ukweli , na hilo siwezi kulipata kwa mtu mwingine zaidi yako wewe. Mume wako hayupo hawezi kujitetea, lakini wapo waliokuwa wakimfahamu na kumjua vyema, na hakuna anayeweza kumfahamu vyema yeye zaidi yako wewe uliyekuwa mkewe…,na naitaka kauli yako ili kila mtu aisikie…’nikasema na jamaa akadakia akisema

 

‘Lakini ulimsikia mwenyewe shemeji alivyosema,  kasema  hapendi kuongea lolote kuhusiana na  hili…..,keshamuachia mungu, sasa kwanini unataka kumlazimisha…ina maana wewe una ubavu zaidi ya mungu…acha kuchezea imani ya shemeji yangu…’akasema Dalali, na shemeji yake ghafla akasema;

‘Kwani mlitaka kuniuliza kuhusu nini..?’ akauliza mama mjane na  kauli hiyo ilimfanya Dalali abakie mdomo wazi, akataka kusema neno lakini akasita, na mimi sikutaka kuchelewesha, nikamuuliza shemeji swali …
 
NB, Naona tuishie hapa ili kuwekana sawa, kujikumbushia kisa kilivyokuwa kikiendelea, swali hili linafungua mambo, je ni swali gani, na kwanini Dalali anakwepa shemeji yake asiulizwe….
 

WAZO LA LEO: Usiogope kuusema ukweli pale panapohitajika, usiogope kwa vile labda ukiusema huo ukweli, mtu Fulani au bosi wako, atakasirika,  au huenda ukapoteza kazi,…Ukweli huo utakulinda leo hadi mwisho,…kuliko kusema uwongo, kwa masilahi…!

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

raha kweli like a movie.