Ni kituo cha
polisi, ofisa mpelelezi alifika kwa mkuu wake akiwa na makabrasha ya kazi zake,
na wakati wanamsubiria muendesha mashitaka, ikawa ni kazi ya ofisa huyu
kumuelezea mkuu wake kazi ilivyokwishafanyika, akijua kuwa kuna mambo ambayo yanaweza kuja kuleta utata...
'Ehe endelea na maelezo yako,...kuna mauji,...kwanini imefikia huko..?' akauliza mkuu
'Ni kweli mtu mmoja kauwawa, ....na ....'akawa anaendelea kuelezea
‘Kwahiyo sasa ni kesi ya mauaji, sipendi hivi kabisa,....’akasema mkuu akisoma moja ya makabrasha.
‘Ndio
mkuu....’akasema mpelelezi.
‘Na kwahiyo
sasa imefikia hatua mbaya,...siwezi kukupa tena muda,...sasa nataka kujua wapi
ulipofikia,...tulimalize hili jambo, huko juu nalaumiwa sana...’akasema
‘Mkuu,
..hata hivyo sihitajii muda tena kwani kazi niliyokuwa nikifuatilia
imeshakamilika,...’akasema
‘Ok, kwahiyo
kumbe leo umakuja na kila kitu, nasema
hivyo, kwa vile, hata mimi nakabiliwa na shinikizo kutoka juu kwa wakubwa,..na
tatizo hili, sasa limeinua hisia kubwa,
hasa kwenye vyombo vya habari, kwa wananchi...sasa nambie kila kitu,...'akasema na mpelelezi akawa anatoa makabrasha yake kwenye mkoba wake.
'Si umesema upo tayari,...?’
akaulizwa na mkuu wake.
‘Ndio mkuu nipo tayari,...maana kama ujuavyo, walikamatwa hata watu wa habari,waendesha mitandao
ya kijamii ambao hawaendani na maadili na ,nia na lengo ni kujaribu kuzuia hili
jambo lisije kupotoshwa zaidi...hawa waliokamatwa kwa sasa wanatumiwa,ndio maana kumekuwa na sintofahamu nyingi....’akasema
‘Ukisema
hili jambo, una maana gani, ni hili la hii kesi.?’ akaulizwa
‘Ndio, ....ni
kuhusu hii kesi, mkuu...’akasema
‘Ok,
endelea....’akasema
‘Katika hii
kesi, kuna watuhumiwa wawili, kuna huyu ambaye tumeshamkamata tayari ni raia wa nchi za nje..., yeye ni wakala
wa milungula, na kuna mwingine ambaye hatujamkamata, ni raia wetu....yeye anatumia sana watu
wanamitandao, na kueneza propaganda za kuonyesha au kujenga chuki, katika jamii.....’akasema
‘Mhh.....hebu
niambie zaidi kuhusu huyo mtu anayetumia watu wa mitandao, je kuna mahusiano ya
hayo mauaji na huyu mtu, na je alikuwa
akishirikiana na huyo mshukuwa wa haya mauji?’ akaulizwa.
‘Mwanzoni
tuligundua kuwa hawana mahusiano, kutokana na uchunguzi wa mwanzo, lakini
tulipofanya uchunguzi wa kina tumekuja kugundua kuwa watu hawa wawili walikuwa
wanafanya kazi pamoja,....’akasema.
‘Ok, swali
langu muhimu kabla hautajaendelea je kundi hili lina mahusiano na yale makundi
haramu yaliyokuwepo kipindi kile cha nyuma?....
‘Hapana...’akasema
na kabla hajafafanua mkuu wake akasema
‘Unakumbuka yale
makundi ya nyuma yalivyoharibu huu mji, na watu, hasa vyombo vya habari,
wamefikia kusema kuwa haya ni mabaki ya yale
makundi haramu....na wanafikia kusema sisi watu wa usalama tulidanganya kuwa
tumelimaliza hilo kundi,sasa iweje wimbi hili la mlungula, mauaji limeibuka
tena....?’ akauliza mkuu.
‘Hili sio
kundi kubwa...kama wanavyovumisha watu wa habari,na tutalimaliza haraka
iwezekanavyo...na halihusiania kwa vyovyote
vile na makundi yaliyopita...ni kwa vile mbinu au kazi wanayoifanya
inafanana fanana tu, na yale makundi ya zamani.....hawa ni vijana chipikizi
kabisa.....’alikuwa ofisa mpelelezi akitoa taarifa kwa mkuu huyu ambaye alikuwa
kasafiri, na aliporudi akataka kusikia wapi kazi hiyo imefikia.
‘Mbona
dalili zake,...na harakati zake zinafanana sana na makundi yale yaliyopita...yawezekana
hilo hamlikuliona?’ akaulizwa mpelelezi.
‘Hili kundi
limejitokeza tu hivi karibu, ni chanzo chake ni athari za vijana kukosa ajira
za uhakika, wamesoma, na utaalamu wanao, lakini hakuna ajira za uhakika..na wengi
walisoma wakiwa na mategemeo ya kuajiriwa...’akasema
‘Hilo ni
kweli....’akasema mkuu wake akitikisa kichwa kwani ana kijana wake msomi, kasomea
mambo ya komputa, na ana uwezo mkubwa, lakini bado hajapata kazi, na katika
kuhangaika, ...kijana wake akasema kagundua kuwa kuna mtu anaweza kumsaidia,
yeye ni mtaalamu wa hali ya juu kwa mambo hayo...
Alikumbuka
siku moja alipokuwa na kijana wake wakiongea, na alitaka ikiwezekana amuingize
kijana wake kwenye kazi za uaskari, kama yeye, lakini kijana wake alikuwa
hapendeleo kazi hizo,kijana wake alijikita zaidi kwenye mitandao na komputa.
‘Baba usiwe
na wasiwasi,...nimehangaika na sasa nimempata mtu wa kunisaidia, kwani
anasaidia watu wengi sana...’akasema
‘Yeye..ni
nani, ni mtu, wa namna gani na atakusaidia kwa vipi, ana kampuni au anafanya
nini huyo mtu...?’ alimuuliza kijana wake
‘Ndio yeye ana
kampuni yake mwenyewe, na sio kampuni moja tu..japokuwa wengi wanahisi hivyo
kuwa ana kampuni moja,...ni mtu ana ujuzu wake mkubwa, na kaamua kuutumia ujuzi
wake, sio kwake tu, pia kwa wengine...’akasema
‘Hivyo ndio
inatakiwa,..elimu yako iwe na manufaa kwa watu wengine pia, ukiwa na ujuzi au
utaalamu uwe ni sababu ya kusaidia na wenzako, na kuleta maendeleo, tunahitaji
watu wa namna hiyo...’akasema baba mtu.
‘Kampuni yake
inajihusisha na nini zaidi,....?’ akauliza
‘Yeye zaidi
kampuni zake zote, japokuwa anajitanua zaidi kwa mambo mengine ili kuendana na
wakati, lakini hasa, kwa kisaisi kikubwa anajishughulisha na mitandao, na
biashara za komputa na vifaa vyake, anauza vifaa vyote vya kisasa vya komputa,kuweka
mitandao majumbanina fani kama hizo....’akasema
‘Umeshaongea
naye au nikaongee naye mimi mmwenyewe..?’ akamuuliza
‘Nimeshaongea
naye na nimeshaanza kazi kabisa, nimepata ujuzi mkubwa kutoka kwake,....nilianza
muda, sema sikutaka kuwaambia kwanza mpaka nihakikishe nina uhakika na ajira
hiyo...’akasema
‘Vizuri
sana, nataka hivyo, uwe unajisumbua mwenyewe, ila uwe makini,sio makampuni yote
yanaweza kukusaidia kwa maisha yako ya baadaye....mengine yanakutumia
wakifanikiwa wanakutupa.....nina uzoefu sana wa mambo ya ajira....’akasema
‘Ndio baba
usiwe nashaka, kwa hilo....najua ni kitu gani ninakifanya, muhimu kwa sasa
napata mahitajio yangu yote bila kukutegemeeni, na nikijaliwa na mimi
nitaanzisha shughuli zangu binafsi...’akasema
‘Hiyo
kampuni inamilikiwa na nani...?’ akaulizwa
‘Mhh,...huyu
mtu, .... yeye anajulikana zaidi kwa jina moja tu, la Mtaalamu...japokuwa ana
majina yake mengine..’akasema
‘Mtaalamu...mtaalamu....mmh,
kwa kumbukumbu zangu huyu mtu, kama namfahamu.....’akasema
‘Ndio
anafahamika sana, anasaidia sana watu,....anasaidia sana taifa kwenye maendeleo
yake.....’akasema
‘Ok,.....sina
uhakika kama ni huyo ninayemfahamu mimi,...unajua kijana wangu kulikuwa na
jamaa mmoja alijulikana kwa jina hilo, ...Mtaalamu mtundu, akawa na kampuni
kubwa sana,..tulikuja kumgundua kuwa alikuwa na biashara haramu ndani
yake,.....’akasema
‘Baba, sio
huyo....’akasema kijana akiangalia saa yake.
‘Najua sio
huyo, nakuambia tu, kulikuwa na mtu kama huyo tukamgundua na tukaja kumfunga na
kampuni zake, zimeshakufa....sasa uwe makini sana....’akasema
‘Huyu ana
ujanja ujanja wa komputa, mitandao...au yupoje, maana wengine huamua kuutumia
utaalamu wako,nia kubwa sio hasa kupata lakini kwa kisai kikubwa sio kwa njia
za halali, wanatumia utaalamu wao kuiba, kuibia serikali....yeye kampuni yake
ipoje...?’ akaulizwa
‘Baba, huyo
sio mjanja mjanja ....ni mtu na fani yake, ni mtaalamu kweli, na ujuzi alio
nao, sio wa kubahatisha...kausomea hadi ngazi za juu,...na aliona kuwa
kuajiriwa hakumlipi, na ndio maana akaja kuanzisha kampuni yake mwenyewe,......na
kampuni hiyo ikawa inajitanua....mimi napenda sana juhudu zake......’akasema
‘Ok....’akasema
baba yake akimuangalia kijana wake kwa makini, anampenda sana kijana wake, na
hataki aje kujiingiza kwenye matatizo....kilichomshangaza ni jinsi gani kijana
wake akapata kazi, na akakaa kimia bila kumuarifu yeye mwenyewe,lakini hakuwa
na shaka.
‘Dad, huyu
mtu kawasaidia, vijana wengi walikuwa wakihangaika na ajira, ...si unamsiki
anavyotoa msaada, ...sasa hivi kaanzisha kampuni ndogo ndogo nyingi, na
kuwaajiri watu wengi....huyu anafaa hata kuwa kiongozi wa nchi, maana ni msaada
mkubwa kwa taifa...’akasema
‘Mhh, kama
ni hivyo, ....hata mimi nimeliona hilo, anaweza kuwa kiongozi mnzuri kwa
maendeleo ya taifa, ...nitamtembelea ofisi kwake nione tutakavyoweza
kumsaidia,...anafanya kazi nzuri....vizuri sana kijana wangu.....’akasema sasa baba
mtu akifurahia kuwa sasa angalau mtoto wake atakuwa kwenye ajira yenye faida
kwake na baadaye ataweza kuwekeza zaidi.
*******
Wakati
anawaza hili,....mwenzake alikuwa akiendelea kumuelezea tatizo hili la ajira
linavyowakabili vijana..
‘Kwahiyo
kama unavyoona mkuu,...taifa na sio taifa hili sasa ni tatizo la dunia nzima,
kuna tatizo la ajira.... ajira hakuna japo kweli vijana wapo wengi wanajiobidisha
kusoma, elimu zinazotolewa ni za misingi ya kuajiriwa, sasa vijana wanaomaliza
shule, vyuo, ni wengi, hebu niambia watakwenda wapi,.’akasema
Mkuu wake
alitaka kumwambia kuwa kijana wake keshapata ajira ya uhakika, lakini akaona haina
haja kumuelezea hilo kwa sasa...akawa anasikiliza tu.
‘Mkuu,na
hata wale walioajiriwa wamejikuta wengine wakiachishwa kazi, kwani makampuni
waliokuwa wakifanyia yameshindwa
kupambana na ushindani wa kibiashara,....hili ni tatizo jingine....’akatulia
‘Kampuni
zinapokuwa nyingi, kama uonavyo wengi nao waliamua kujiajiri, wakaanzisha
kampuni zao, kampuni zinaongezeka, kuongezeka kwa kampuni ni tatizo kwani
kunatokea ushindani wa kutafuta masoko,....utaalamu unakuwa, na sehemu yenye
watu wengi, wanahitajika watu wachache, wengi wanaondolewa....
Ina maana
gani hapo,... makampuni mengi sasa yanaamua kupunguzwa wafanyakazi, kwa
visingizio mbali mbali, wengine wakidai wanabana matumizi..... kwahiyo
tunajikuta tuna wataalamu, na wasomi ...wengi tu,wasiokuwa na ajira wapo mitaani,hawana
kazi, ogopa kuwa na wasomi wengi, na wasiwe na ajira, wasiwe na malengo yoyote,
kama huko Nigeria....’akasema
‘Sasa wale
waliopunguzwa,wanakuja mitaani, wana utaalamu wao,wameshaonja pesa...wakifika
mitaani, wanakutana na upinzani mnzito, kuna wenzao walishajiajiri
tayari,....
'Na ukumbuke pia kujiajiri nako kuna changamoto zake, maisha ni magumu,
hawa walitoka maofisini, hawana maandalizi yoyote, na ukumbuke huko walipokuwa
wameajiriwa kipato kilikuwa kidogo,sasa hawajui waanze vipi maisha mapya ya
kujiajiri...tatizo linaanzia hapo’akatulia
Wengine
wanafanikiwa, lakini ndio wanajikuta katika kunyang’anyana wateje...tatizo juu
ya tatizo...unaliona hapo mkuu....’akasema na mkuu wake akatikisa kichwa
kukubali, huku kwa mbali akimuwazia kijana wake.
‘Kwa hali
kama hiyo,...mwisho wake ndio hapo wanabuni njia mbadala ya kujipatia kipato,
kwa kutumia migongo ya utaalamu wao,.njia zenye muelekeo hasi ili kupata kipato,..na hizo njia
nyingi,ni njia zisizo sahihi,na ndio chanzo cha haya makundi ya sasa...’akasema
‘Mhh,
nimekuelewa, kweli,...hii kweli ni shida,maana mzazi umejitahidi umetumia
gharama nyingi ukitegemea mafanikio kwa mtoto wako, lakini inafikia hatua
unasema sasa mtoto kamaliza shule, anakwenda kupata ajira...lakini kazi hakuna,
ajira sahihi hakuna, au mbinu za kujiajiri hakuna..kwakweli hilo ni
tatizo....’akasema mkuu,
‘Ndio hivyo
mkuu,...’akasema
‘Natumai
utakuwa na ushahidi wa hayo yote kwani itafika wakati tutatakiwa kukutana na
wana siasa,....’akasema akizama kwenye mawazo mazito
‘Hilo
tutaliona huko baadaye....’akasema
‘Sasa swali
hapo ni je ushahidi tulio nao watatuelewa, je utaweza kuwa..kamata hawa watu,
au tutafute njia za kuwasadia, maana kama unavyoona watu hawa ni msaada mkubwa
kwa vijana wetu na taifa kwa ujumla....’akasema
‘Mkuu, huu sasa sio msaada kwa taifa, ni
mnzigo....kama watu wanaamua kutumia mbinu chafu, hilo sio tegemeo, hilo ni
kututengenezea janga, sijui umenielewa mkuu..’akasema
‘Nimekuelewa,
sana, sana...ila nataka hili walione hawa viongozi wetu, na tusije kujenga
uhasama..badala ya kusaidia jambo,..na pia wasije kukimbilia kutulamu sisi,
kuwa watu wa usalama ni chanzo cha
vurugu......ni kazi kubwa sana kazi yetu ikihusisha na watu wa siasa, si
umeliona hili, sasa mimi kama kiongozi natakiwa kuwa na hekima ya kila jambo...’akasema
‘Kwa
ushahidi tulio nao watatuelewa, kwani athari zake zinawagusa hata wao wenyewe, wana
vijana wao hawana kazi pia nalielewa hilo, kama tulivyo sisi... na wengine walioguswa
na watu hawa, kwenye shughuli zao kabisa,kwani mambo yao ya chini kwa chini
yaligunduliwa na hawa watu,..yakawa ni mtaji kwa hawa watuhumiwa...’akasema.
‘Ni
kweli...’akasema na kutabasamu
‘Japokuwa
wengine wakiingia kwenye mitego ya hawa watu hawataki kuja kwetu moja
kwamoja,wanasubiria mpaka balaa litokee .....lakini wapo kwenye shida, hawana
amani....na chanzo ni hawa watu wanaondesha hizi biashara haramu...’akasema
mpelelezi
‘Kwahiyo kwa
namna fulani,...hizi shughuli za hawa watu, zliwabana hawa watendaji waovu,
wenye mambo ya chini kwa chini, ambao wanatumia siasa za mdomoni, kuwahadaa
wananchi kumbe chini kwa chini wana mambo yao mabaya....?’ akauliza
‘Ukiweka
kihivyo, unaweza kusema imesaidia, lakini kwa njia isiyo halali,....hawa wataalamu,
waliwasoma hawa watendaji,....ni kweli, wakagundua kuwa uzaifu wao pia unaweza
kuwa ni soko kwao, ...ndio maana mlungula umeshika hatamu sana, biashara ya
udaku, umeshamiri....’akasema
‘Mkuu,..blackmail.. sasa ni hatari,kwani
wanaofanyiwa hivyo nao wanajaribu kujihami kwa njia yoyote, hata ikibidi kuua,
maana mtu anajiona anavuliwa nguohadharani, anajua atafirisiwa, ...hebu fikiria
mtu kahangaika kupata pesa zake,leo anakuja mtu anamtaka azitoe .... ‘akasema
‘Lakini ni
kwauzembe wao,kwanini wanaogopa kuja kutoa taarifa polisi..’akasemamkuu wake
‘Ni kutokana
na vitisho, ama watoe pesa au
wayatangaze hayo machafu yao hadharani...ni njia isiyo halali,...lakini pia wao
wanaogopa kujiabisha, wakija polisi, ina maana hayo machafu yao, hayana siri
tena....una ona hapo....’akasema
‘Naelewa
hilo,ika kitu ninachochelewa, hawa watu wana washabiki wao, hasa wana siasa...au
sio,..., na huku kwenye hawa wahalifu wanaotumia mitandao, nao wana wapenzi
wao, ...’ akatulia
‘Jambo kama
hili, tunahitajika kuwa na ushahidi wa kutosha, hasa tukifika mahakamani, tuhakikishe
tunashida,vinginevyo, tutaharibu kazi zetu....’akasema
‘Hilo mkuu
usiwe na shaka,....’akasema
‘Shaka ni
kuwa, hawa watu wana pesa watawatumia mawakili wajanja,...watatumia vyombo vya
habari, watawashawishi watu ...kwahiyo tunahitajia ushahidi wa kutosha
kuhakikisha tunalimaliza hili tatizo,....’akasema mkuu.
‘Ndio maana,
tumechukua, muda....watu watafikiri tumeanza baada ya haya mauaji,..hapana
mkuu,ulipo nipa hii kazi, niliamua kuifanya kwa undani zaidi, ndio maana kila
mara nilikuwa nakuambia, bado,nipo muda....’akasema
‘Sawa kabisa...ndio
maana hata mimi sikutaka kukulazimisha, kukuhimiza, ili tatizo liishe kabisa,
lisije kujirudia tena..je hilo mumelifanyia kazi...?’ akaulizwa mkuu akionyesha
kufurahiwa na kazi nzuri ya mpelelezi wake.
‘Ndio tunao ushahidi
wakutosha, hatuna shaka na hilo mkuu, ...hilo tumelifanyia kazi, na kuna jambo
jingine mkuu, nitaliongezea kwenye ushahidi wetu....’akasema
‘Jambo
gani....maana nataka tumalizane na hili tatizo kwanza, je hilo linahusiana nah
ii kesi yetu? akauliza kwa mshangao
‘Japokuwa
hatutaeleweka kwa hilo,.... lakini sasa hili limekuwa ni tatizo, ni kuhusu hawa
wahamiaji...hawa wahamiaji wamekuwa ni tatizo, kwani wanakuja na tabia zao, wengine
ni wakorofi huko walipotoka,..na wengine walikuja wakitarajia maisha mazuri,
....lakini wamejikuta kwenye maisha magumu...ndio hapo wanaamua kujiunga kwenye
haya makundi machafu, wanatumiwa...’akasema
‘Sasa hilo
tutaongea na wenzetu wa uhamiaji...wahakikishe wanaoingia wana sababu muhimu, wakague
uhalali wa hawa watu,..hilo lina uzito wake, lakini tutaona jinsi gani ya
kufanya ni kikutana na wenzangu....’akasema mkuu
‘Ndio maana
sikuliweka kwenye ushahidi wetu, ni jambo la kujitegemea....’akasema
‘Sasa, ..
kwahiyo inahitajika wote wanaohusika
wakamatwe...’ akasema akishika simu akawa anaongeajambo na mkuu wake huku
akikagua makabrasha yake.
‘Ndio hivyo
mkuu....’akasema
‘Ok, kibali
kimeshatoka, kwahiyo watuhumiwa wote wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mbele
ya mahakama.., au wameshakamatwa,,?’ akauliza mkuu
‘Leo
sijaonana na msaidizi wangu,nilimwambia ukiwa tayari, kama sijarudi afanye
kinachowezekana....je hili zoezi lakuwakamata wahusikawote limeshafanyika?’
akaulizwa
‘Limefanyika
mkuu, lakini sio wote tuliowakamata..., kuna ambao hawajakamatwa, ikisubiriwa
kibali chako,....’akasema
‘Kwanini,
maka kibali changu...?’ akauliza kwa mshangao
‘Kwa mfano
kuna huyu mmoja ambaye tulikuwa tunamshuku siku nyingi,....ni mfanyabiashara
mkubwa wa mitandao, na msaidizi wako alisema hatuwezi kumkamata mpakatupate
kibali chako, na tulichofanya ni kumtumia, kwa hivi sasa yupo na watu wetu, nia
ni kutaka kuhakikisha kila alichokifanya kinajulikana....’akasema
‘Ni nani
huyo....?’ akauliza akikunja uso kwa mashaka
‘Huyu mfanyabiashara
unamfahamu sana,ni muwekezaji mnzuri, ..’akasema akifungua makabrasha
‘Ndio ni
yupi huyo, ...?’ akaulizwa mkuu akiinama kuangalia lile kabrasha.
‘Ni jamaa
mmoja ....eeh, huyu hapa,...’ akawa anaonyesha picha yake, na kuendelea kusema
‘Yeye anajulikana sana kwa jina moja la Mtaalamu...’akasema
‘Mtaalamu!..mtaalamu!,...una
maana...haiwezekani, ina maana ni huyu, huyu mwenye kampuni kubwa ya
mitandao...anayesaidia watu wasio na ajira...huwa anajitahidi sana kuwaajiri
vijana wasio na kazi,,...haiwezekani?’ akauliza huku akonyesha usio kukubaliana
na hilo.
‘Ndio huyo
huyo mkuu ndio maana tukasubiria kibali chako, ikizingatiwa kuwa katika safari
zako ulisema unakwenda kuangalia jinsi gani watu kama watakavyoweza kusaidiwa
na serikali,kwa vile wanasaidia vijana, lakini kwa ushahidi ni mmoja wa
mafisadi, waendesha biashara ya mlungula....’akaambiwa na
mpelelezi,mpelelezi alishangaa kumuona
mkuu wake akikuna kichwa mara nyingi....
‘Haiwezekani....’mkuu
akasema huku akisimama, na mara mlango ukafunguliwa na muendesha mashitaka
akaingia.
WAZO LA LEO: Taifa likianza kujenga matabaka la
wasio kuwa nacho na wenye nacho, elimu ikatolewa kwa misingi hiyo hiyo, wenye
nacho wanapata elimu nzuri, na wasio nacho hawapati elimu sawa na wasio nacho,
na kwahiyo hata ajira zikawa zinaelekea kwa misingi hiyo hiyo,...na kwahiyo
hata viongozi wakawa wanagawana madaraka kwa misingi hiyo hiyo, siasa
ikaingiliwa na wenye nacho hapo unategemea nini....rejea misingi ya ubepari.
Mimi najaribu
kutafakari kwa maono, umma wa walio
wengi ambao ndio wasio kuwa nacho watafanya nini, ...nahisi amani itakuwa ni
kitendawili, au , huoni kuwa umma wa waliowengi utakuwa na kinyongo, hasira na
visasi vitajaa moyoni, na ikitokea kuwepo na sababu kidogo tu, inaweza kuwa ni chanzo
cha machafuko yasiyo na kikomo, hivi sisi ni tofauti na huko kunaotokea vurugu,
wananchi ni sugu kiasi hicho....tumuombe
sana mungu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment