Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, July 14, 2015

RADHI YA WAZAZI-19


Ilikuwa ni kipindi cha chai ya asubuhi, wanandoa wawili hawa walikuwa mezani, aliyekuwa wa kwanza kufika mezani alikuwa mke, alipofika mezani mume alikuwa nje akijibaragua,  baadaye kidogo akaingia ndani, na kumkuta mkewe tayari akiwa kaandaa kila kitu, akafika na kuanza kunywa chai, mwanzoni, kukatanda ukimia fulani, kila mtu akimtegea mwenzake kuanza neno, na mke akawa wa kwanza kuongea;

‘Mume wangu kama nilivyokuambia jana, nina mazungumzo muhimu leo mimi na wewe...’akaanza kuongea mke huku akimkagua mumewe kama yupo sawa, au alizidamkia za asubuhi, kupoteza malengo.

‘Sawa mke wangu, hakuna shida, ...tuongee tu nipo safi, ila samahani kwa jana, niliamua kunywa kuondoa stress, unajua hizi kazi zetu za wavuja jasho, kiujumla unapokua kwenye ngazi ya kutumwa, wewe sio bosi, tunaseka sana, unajituma sana kazini, lakini watu hawaoni unachokifanya, kila ukifanyacho chenue faida,bosi ndiye anayeonekana wewe mchumia juani,  huthaminiki,...’akasema

‘Mhh ni kawaida...’akasema mke mtu akitafuta jinsi ya kuanza yale yake, hakutaka kumuharakisha, kwani ni muhimu kuhakikisha anaupata ukweli wote.

‘Angalia kwa mfano, kinaharibika kitu kazini, hapo habebi lawama sio za bosi, lawama ni kwako wewe mtendaji, lakini kukiwa na mafanikio, wewe mtendaji umafanya jambo likaleta mafanikio wewe tena huonekani, wewe uliyevuja jasho, hadi ukafanikisha hilo, huonekani, anayeonekana ni bosi, ....faidia na ziada yote, anapewa bosi..., wewe utaambulia tu ahsate na sifa nyingi za maneno...’akaendelea kuongea kupoteza muda

‘Ndivyo ilivyo, sio kwenu tu, haki na ukweli huwa haupewi nafasi, hata majumbani, unaonaeeh....’akasema mkewe

‘Na hali hiyo,inamfanya mfanyakazi wa kawaida kuwa kama mchumia tumbo tu, angalia, ...mshahara mdogo haukidhi haja muhimu, ni wa kula nusu tumbo, hauwezi kukuletea maendelea hata siku moja,...lakini huyu mnyonyaji anayeitwa bosi yeye anapewa gari, mshahara mkubwa na marupurupu yote,...na bado hatosheki...’akatikisa kichwa

‘Ila  wewe uneyeumia mshahara mdogo,...huna hata angalau kitu cha kujikumu, kuwekeza, ...huna kabisa, ni kunyonywa kwa kwenda mbele....sasa ukiwazia hayo unaona bora kunywa , nimekunywa pombe wee kupoteza mawazo, lakini mhh, napo sijapoteza mawazo, zaidi ya kuyapumzisha tu...ni taabu, ni majeraha...’akasema

‘Umeonaeeh,taabu na majeraha, ...’akasema mkewe akiongeza chai

‘Ni taabu kweli mke wangu, na ni kujipa majeraha, hebu angalia, sasa nina madeni, na sio madeni ya maendeleo, madeni ya kubambikiwa,...ukiona mimi sina kosa, ni ajali za kazini, hayo habebeshi bosi, hayo unayabeba wewe mwenyewe, kwa anuani ya uzembe..,’akashika kichwa

‘Sasa mke wangu usione nakunywa, usione nipo hivyo, ni maisha, tu...’akasema

‘Ndio maana nawazia, ikiwezekana nitafute sehemu nyingine ya kazi...nibadili sehemu ya kupata riziki, maana riziki ni popote, au sio mke wangu....’akasema sasa akimtupia mkewe macho ya kujiiba

‘Pole sana mume wangu ndio mitihani ya kazi hiyo, wengi wa binadamu wapo hivyo, na watu kama hao wanajiona wanachofanya ni sahihi, kwa vile umimi, ubinafsi na roho mbaya imeshatanda kwenye mioyo yao...wao kuishi kiujanja ujanja ni ufahari, ...na wanaweza hata kujinadi, sasa tuyaache hayo ,...’akasema mkewe na kuona anapotezewa muda, kulisema alilolitaka.

‘Eeeh, ni kweli kabisa mke wangu kwahiyo naomba unisamehe sana, ....sasa ulikuwa unasemaje,  umesema ulikuwa unataka tuongee, haya tunaongea au sio, maisha yetu, tufanyeje, tukianzia na hilo la mimi kutafuta kazi sehemu nyingine au unasemaje...?’ akauliza sasa akiona kuwa hakuna tatizo.

‘Mume wangu pamoja na hayo, kuna mambo naona kwanza tuyaweke sawa, nimeona hayo tusipoyamaliza, yatakuja kuleta ufa mbaya kwenye ndoa yetu,...na ni muhimu sana katika mipangilio yetu ya kimaisha humu ndani, na nimeona nikikaa kimia sijui kama tutafika..’akasema na mume akataka kukatiza na mke akanyosha mkono na kusema

‘Naomba kwanza unisikilize kwa makini...ili tuelewane’akasema mkewe, kwani alioa akimuachia mumewe kuongea muda utakwisha nay ale aliyopanga yaje kufanyika hayatapata muda.

‘Aaa ok, ok,nakusikiliza, sina neno, leo nipo nyumbani nataka tukae mimi na wewe,...si unajua mke wangu, sitaki watu watusumbue, leo mimi na wewe, unajua nakupenda sana mke wangu...wewe hujui tu...nimewaza sana nikaona hakuna haja ya mimi kwenda kulewa huko, na kumuacha mke ndani...kwanza natafuta nini,....’akasema akijichekesha

‘Nashukuru kusikia hivyo, na hiyo kauli ya kuwa unanipenda naisikia kwa mara ya kwanza tangu tufike huku ulaya, na inaonyesha kuna shinikizo fulani,...lakini usijali, hata mimi nakupenda sana mume wangu, ndio maana nataka tuyaongee haya...tuelewane ...’akasema mke sasa akiwa kakunja nne.

‘Mhh, kweli mke wangu,najua kabisa sisi tunapendana sana, tangu nifike hapa watu wanatuonea wivu,...japokuwa ulaya ni ulaya, kila mtu na hamsini zake, ...eeh, hebu sema hilo la  moyoni mke wangu,...nakusikiliza mke wangu mrembo...’akasema huku akicheka cheka

‘Kwanza tuanzie kule, katika swala la kuaminiana, na kuambizana ukweli, hili lilikuwa ombi langu toka mwanzo...unakumbuka nilipokubali kuwa tufunge ndoa mimi na wewe,...nilikuambia hilo, kuwa tuwe tunaaminiana, kila kitu chetu kiwe wazi,changu kiwe chako na chako kiwe changu,tuwe hatufichani mambo....’akasema mke

‘Ni sawa kabisa mke wangu....nakumbuka sana hilo, na kwa ujumla hilo tumelifanya, na tumefanikiwa au sio, kila kitu changu kipo wazi kabisa kwako,...sijui kama kuna kitu nimekuficha,...hakuna, nina nini cha kukuficha, si unanijua nilivyo , unanifahamu kuwa sikuwa na kitu zaidi na hivi tulivyochuma sote....na nisingelipenda kurejesha historia nyuma, au sio mkewangu...sasa tusonge mbele....au unasemaje...?’akasema

‘Una uhakika kuwa umekuwa mkweli kwangu,kuwa kila kitu chako umekiweka wazi kama tulivyokubaliana,..huna kitu ambacho umekiacha kama chako na sio chetu...labda una sababu za msingi, kama zipo niambie nisikie,.., ?’ akauliza

‘Kila kitu changu nimeshakiweka wazi, sina changu, vyote ni vyetu...sina shaka na hilo mke wangu,na mungu ni shahidi,..kwanza mimi nina nini cha kukuficha, siwezi kukuficha kitu mke wangu,wewe na watoto wetu ni kitu hiki...kimoja...mengine labda yawe ni majungu..’akasema

‘Mume wangu kwanza nikuambie kitu, wewe unavyofanya sio sahihi, mfano huko kwenda kuelewa, kwenda kushika shikwa kwenye bar, wakati k e.mke nyumbani unajivunjia heshima yako....hivi nikuulize hao wanawake huko wana nini zaidi ya mke wako nyumbani..?.’akasema na mume wake akasimama kujinyosha.

‘Mke wangu wewe una tofauti kabisa na hao, wewe ni mke wangu,mrembo, huwezi kujilinganisha na hao..na nakupenda sana....’akamwendea na kukaa karibu yake, kwanza alitaka kupitisha mikono nyumba ya shingo ya mkewe kama kumkumbatia, lakini akasita

‘Sikiliza, haina haja ya kujibaragua kwa haya, maana mimi sio mtoto mdogo, tuna miaka mingi ya ndoa mimi na wewe,nakufahamu zaidi ya unavyojifahamu wewe, kwahiyoo kujiigiza kinafiki hapa hakusaidii kitu....’akasema kwa sauti ya juu kidogo

‘Mke wangu, kwanini...mimi nataka tuwe pamoja, na hata kama siku mbili tatu, nimekuwa mbali na wewe, sasa nataka tuwe kama ilivyokuwa awali, kama ndio tunaoana,...’akasema

‘Tusipoteze lengo, nilianza kwa kauli ya kuaminiana, na kuelekezana ukweli, nikakuuliza kama kweli una uhakika kuwa chako, ni chetu, na hakuna chako ambacho hujakiweka wazi, na kama kipo huenda una sababuu ya msingi,....sasa mimi, nataka kujua ukweli..ukiniambia ukweli hapo nitajua kweli unanipenda, ’akasema

‘Mhh, ukweli upi tena mke wangu...?’ akauliza

‘Je una uhakika kuwa kweli chako ni changu na changu ni chako,una uhakika kuwa kweli huna jambo au mambo unayonificha, ambayo unayafanya kibinafsi kinyume na makubaliano yetu, je una uhakika kuwa huna mahusiano nje....’akasema na hapo mume akanywea

‘Mke wangu, siwezi hata siku mja kuwa jambo kinyume na makubaliano yetu,....hebu toa mfano,na kwanini tuzunguke niambie kitu gani ambacho sijawahi kukuambia, au....eeh ni kuhusu ile akaunti ..nilishakuambai ukweli wote...au sio...’akasita

‘Wewe ulidai kuwa hiyo akaunti yako, haitumiki, na ulikuja kuitumia wakati unapokea malipo ya kazini tu, na haijawahi kuingiza pesa zako binafsi, au sio, huo ndio ukweli wako au sio....?’ akauliza na mume mtu kwanza alitulia halafu akasema

‘Ndio hivyo...kwani kuna tatizo gani hapo, kama kungekuwa na kitu kingine ningekuambia, achana na hiyo akaunti haina lolote muhimu, na pesa iliyopo humo ni ya watu, nitaitoa ibakia kama ilivyokuwa....’akasema

‘Una uhakika na unachokisema....?’ akauliza

‘Kwanini unanitilia mashaka ka hilo,...,sikuelewi mke wangu hicho ni kitu kidogo tu, hakina maana mbele ya ndoa yetu, au sio....’akasema

‘Mume wangu, hapo hapo umeshanitilia mashaka,kama unanificha ukweli kwa hilo najua kuna mengi unayafanya, na,huenda yamekwisha kukufika kubaya, ndio maana unalewa tu, na hayo ya kazini kwako ni kisingizio tu, na ndio maana leo umeamua kujifanya upo karibu na mimi....niambie ukweli’akasema

‘Sio kweli, kama ni hilo la akaunti hiyo...ili uwe na uhakika twende pamoja benki,mimi nitaitoa hiyo pesa yote ya watu, halafu uone kama kutabakia kitu...’akatulia

‘Mume wangu,...nilikuonyesha barua ya kutoka benki, ukasema ni barua ya kutaka kujua kama hiyo akaunti unaihitajia au waifunge, kweli si kweli...?’ akauliza

‘Hapana, ...nilikuambia kuwa akaunti hiyo mwanzoni ilikuwa haitumiki, na benki wakaniuliza hivyo, basi ili kuifanya iendelee nikawa naweka pesa za malipo ya watu, ili iweze kufanya kazi, sasa benki wakawa wanataka baadhi ya nyaraka ndio wakaniletea hiyo barua...’akasema

‘Na hiyo akaunti yako haijawahi kuingiza pesa zako binafsi, .....?’ akauliza

‘Pesa zangu binafsi kama zipi, maana pesa zangu ni zako...’akasema

‘Je mshahara wako huwa unapitia benki, uliniambia awali kuwa kwa vile mshahara wako ni mdogo, hauitii benki, unakumbuka hilo, au umesahau...?’ akamuuliza

‘Aaah, kumbe ni hilo, ndio, kuna wakati napitishia huko, si unajua, kuwavunga watu wa kazini wasijue kuwa mshahara wangu upoje, leo naweka hapa kesho hapa....hilo lisikupe shida...ni kitukidogo tu...’akasema

‘Na je mshahara ulionitajia awali ndio huo huo unaingia benki au ...?’ akauliza hapo mume akashituka akasema

‘Mshahara, ...ooh, kwani ...mmh, mke wangu, kuna tatizo kuhusu mshahara wangu, kila mwezi naleta pesa yote tunapigiana mahesabu, kama unvyofanya wewe...kuna tatizo gani kuhusu mshahara wangu...?’akasema na kuuliza

‘Naomba unipe salary slip yako....’akasema mkewe

‘Ya nini, una maana leo huniamini mke wangu, ....kwanza hiyo nyaraka ya nini, mimi sichukuagi, haina maana kwangu...’akasema

‘Kwasasa siwezi kukuamini,kiukweli maswali machache hayo niliyokuuliza yamenifanya nisikuamini kabisa, .....na kwa vile unataka twende kihivyo hamna shida....’akasema mke mtu

‘Kwanini mke wangu, nimeshakuambia kama unataka twende pamoja benki,uone kama hiyo akaunti ina chochote..na pili hiyo salary slip nitakueleta kesho, kama unaihitaji, si huniamini mke wangu, mbona vitu vidogo sana hivyo mke wangu....’akasema

‘Yah...,najua yote hayo umeshajipanga, huko benki huenda umeshazichukua hizo pesa, ukazihamisha au unataka kufanya hivyo, ...na hiyo salary slip unaweza kwenda kuibadili ukaweka unavyotaka wewe ,...’akasema

‘Kwanini nifanye hivyo,mbona unajibebesha mzigo ambao haujatua kichwani mwako,....mke wangu niamini, mimi nipo wazi kwako,...siwezi kukuficha hata mara moja....’akasema

‘Je hizo pesa ulizotoa leo ulizipeleka wapi....?’ akaulizwa

‘Pesa gani,...ok,hizo nilikwenda kulipia lile deni la kazini, na nyingine nitakwenda kulipia watu wengine niliowakopa ili kulipa hilo deni la kazini ....hata hivyo umenikumbusha,..hapa nilitaka kutoka,...nikawakilishe hizo pesa za watu ...hivi sasa ni saa eeh, ngoja,....’akasimama kama anafikiri jambo.

‘Ulisema leo upo nyumbani mimi na wewe au sio,sasa hiyo safari inatoka wapi?’ akaulizwa

‘Nilisahau,..kuna pesa natakiwa kuzipeleka mahali,...’akasema

‘Mume wangu tulia, naona tusipotezane muda, kiukweli hiyo akaunti yako inatumika,na umekuwa ukiitumia tangu tufike hapa ulaya, umekuwa ukipitishia mshahara wako,na nusu ya huo mshahara ndio unaleta hapa nyumbani ukidai ndio mshahara wako wote, ...’akasema

‘Na karibuni ukatoa pesa benki kiasi kikubwa tu, sijui ulikuwa unazipeleka wapi, sasa mimi ninachotaka ni kujua ukweli hizo pesa ulikuwa unapeleka wapi, ukinijibu ukweli, mimi sina tatizo,...’akaambiwa

‘Hizo pesa nilikuwa napeleka kulipia hilo deni,na kuna mtu mwingine nilimkopa, ndio maana nikakumbuka,unajua mambo mengi kichwani, umenikumbusha kitu cha muhimu sana ...’akaangalia saa

‘Mume wangu hizo pesa za deni la kazini unampelekea nani hasa mhasibu au unamlipa nani...?’ akauliza

‘Kuna mfanyakazi mmoja nilimkopesha, yeye anatoa pesa kwa riba...’akasema

‘Je kazini una deni kiasi gani, ...?’ akamuuliza

‘Deni gani, ohoo, lile la uharibifu wa vifaa,...sikumbuki ni kiasi gani mpaka sasa,maana wenzangu waliniunga mkono, hilo mpaka nikamuulize muhasibu..’akasema

‘Mume wangu, sikuamini tena na sitaweza kukuamini tena, wewe ni muwongo,na unachofanya hapa ni kujidanganya mwenyewe...hayo niliyokuuliza yote nimeshayafahamu ukweli wake, nilikuwa nakupima tu...’akasema

‘Kwanini usiniamini....?’ akauliza

‘Ninachotaka kujua kwasasa ni kuhusu hizo pesa nyingi ulizitoa ulizipeleka wapi..?’ akamuuliza

‘Nimeshakuambia ukweli wote mke wangu,...labda kama una lako jambo, naona unataka kuniumbua tu, kwa vile...labda umenichoka,...’akasema

‘Hahaha eti nimekuchoka,...’ akasema mke wake

‘Mke wangu nilishakuambia, hii ni akaunti nilikuwa nayo tu, haikuwa na pesa awali,...,na nikaja kutumia kwa dharura, na pesa humo sio zangu, na kama ni mshahara unapitia tu,, naweka  baadaye nazitoa, kuzikabidhi kwa walengwa au kama ni mshahara naleta hapa nyumbani, tatizo lipo wapi...’akasema kwa sauti ya ukali

‘Nimeshakuambia kuwa yote niliyokuuliza hapa nimeshayafanyia kazi,na ukweli wote nimeshaupata, na nilitaka kuhakiki kutoka kwako, ili nione kama umejirudi, maana binadamu hukosea na baadaye anatambua kuwa kakosea na hujirudi, sasa nataka kujua pesa uliyotoa uliipeleka wapi....?’ akaulizwa

‘Nimeshakuambia nilitoa na kuzipeleka kwa wadai wangu....hunielewi..’akasema

‘Hii hapa nyaraka ya benki inayonyesha pesa uliyotoa....sasa ili tuelewane niambie ukweli wote...’ akasema mke wake akimkabidhi mumewe ile nyaraka ya benki, na mume akaipokea akionyesha kushangaa

‘Nimeshakuambia kuwa sehemu yake  ni pesa ya kazini, ilipitia kwangu nikawa nimechelewa kuipeleka, na walikuwa wakiihitaji...tatizo likawa ni  benki waliniambia akaunti yangu haijafanyiwa uhakiki, ila wakakubali nitoe kiasi tu...’akasema.

‘Mume wangu ,mimi nakufahamu sana kuliko unavyofikiria wewe, nakufahamu ukibadilika, nafahamu ukiwa na matatizo...tulipofika hapa ukawa unachelewa chelewa kurudi nyumbani,, nikajua labda unajiburudisha kujichanganya na wenzako ili uzoee, lakini uhuru huo umepita mipaka...’akasema mkewe

‘Mke wangu niamini, hakuna tatizo kabisa , kama ni hayo tu naona tuyamalaze kwa leo, nataka kuwahi mahali,huyu mtu atakuwa kanisubiria sana....’akasema

‘Hatujamalizana mume wangu...kwa vile akaunti zangu zote zipo kwenye makubaliano, na wewe akaunti yako hiyo haipo kwenye makabaliano, leo wakili anakuja turekebishe makubaliano yetu..hutaweza kuchukua pesa bila sahihi ya wawili, yangu na yako 
’akasema mkewe

‘Lakini hiyo dhamana naitumia kwa malipo ya kazini, huoni kuwa italeta usumbufu kila mara nikikuomba tukae kujadili....’akasema

‘Mimi sioni usumbufu, kama kweli ni jambo sahihi, kwanini nione usumbufu, muhimu kuwe na nyaraka sitahiki, sizani mtu atalipa tu bila nyaraka, au kama ni kazi umefanya binafsi basi hilo ni swala la kifamilia nahitajia na mimi kulifahamu...’akasema

‘Kama ni hilo hakuna shida....ngoja niende nikirudi tutakaaa....’akasema

‘Wakili anakuja nilimuambia apitie benk kuzuia malipo yote , ....’akasema

‘Eti nini....sasa nitachukuaje hizo pesa zawatu....na benki hawawezi kuruhusu kitukama hicho mpaka mwenyewe niwepo, ...’akasema akionyesha kukasirika

‘Ndio maana nataka tukae tuongee, tuweke mambo sawa, kuwa kuanzia sasa hiyo akaunti iwe kama tulivyokubaliana, ....na hilo ni kuanzia sasa,...’akasema mke

‘Tunapoteza muda bure, acha nimalizane na hao watu kwanza, halafu hayo mambo mengine baadaye....’akasema

‘Tunaanzia sasa hivi, wakili anakuja hawezi kufika hapa halafu akusubirie,...’akasema


‘Hapana mke wangu,..hilo haliwezekani, subiri kwanza nichukue pesa ya watu ndio tuingie kwenye makubaliano hayo...’akasema

‘Pamoja na hilo kuna mengine nataka yaingie kwenye makubaliano yetu, nataka tuingize kila kitu, maana sasa hakuna kuaminiana tena...’akasemamkewe

‘Mengine yapi, kuna nini kwani, unataka kusema nini...?’ akauliza mumewe akionyesha wasiwasi na kama kukerwa

 ‘Nyendo zako zinanitia mashaka, ...sikuamini tena mume wangu...’akasema

‘Kwanini..?’ akauliza mume akiwa kakunja uso ,lakini moyoni akihisi wasiwasi fulani, akikumbuka kauli ya wale watu;

‘Kama unabisha ngoja tumuonyeshe mke wako picha ya uchafu wako..’

NB: Naona tuishie hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Wanandoa, tujitahidini sana kuwa waaminifu, kuna mambo mnaweza kuyafanya nje kwa kificho yakaja kuathiri familia, lakini kama mngeshauriana mkawa kitu kimoja hilo lisingelitokea.
Ni mimi: emu-three

No comments :