‘Mume wangu
leo nina mazungumzo na wewe..’ akasema mke wakati huo mumewe alikuwa kakaa
kwenye kiti cha nje, akiwa kakunja
nne,kando yake ipo chupa ya kinywaji, utafikiri hana shida, kumbe kichwani
alikuwa kama kachanganyikiwa, leo aliamua kununua kinywaji kuja kunywea
nyumbani, bar hakuendeki tena.
‘Una
mazungumzo gani tena mke wangu, tafadhali nakuomba nipumzike...sipo sa-sa-sawa...mwenyewe
siunaona....’akaongea kwa sauti ya kilevi.
‘Haupo sawa
kwa vipi unaumwa, na leo kwanini umeamua kuhamishia ulevi wako hapa nyumbani,
si nilishakuambia mimi sipendi mambo ya pombe pombe hapa nyumani, kama unataka
kunywa kanywee huko huko, na wanawake wako....’akasema kwa hasira
‘Mhhh,....sitaki
tena kwenda bar, na hao wanawake sio wanawake wangu, wewe ndiye mke wangu,
unasikia, hao, siwataki, na sitaki kwenda huko tena...nitakuwa nakunywa hapa
hapa....’akasema
‘Sawa...sawa,
kweli naona leo haupo sawa,...tutaongea
kesho,na hakikisha kuwa hiyo kesho hulewi, kwani hayo ninayotaka kuongea na
wewe yanahitajika uwe na akili timamu..’,mke akasema na kugeuka kuondoka
‘Sasa
unakwenda wapi....’akasema
‘Umesema
haupo sawa, na jinsi ulivyo kweli haupo sawa, siwezi kuongea na wewe ukiwa
hivyo tutakosana, na haya niliyokuwa nayo yatasubiria ukiwa mzima, ni muhimu
sana.
‘Poa....unafikiri
najali,...sijali, hata wakichukua zote, sijali....hata na
wewe...kamaumenichoka, sijali...nikiona vipi, nakunywa weee,mpaka napitiliza,
si mtazika tu.....’akawa anamumunya maneno
Mkewe
akaondoka kuendelea na shughuli zake, hakusikiliza nini mumewe anaongea maana
maneno yalikuwa kama ya kulalamika, basi siku hiyo ikapita na kesho yake sasa...
Tuendelee na
kisa chetu
*****
Aliyeamuka
mapema alikuwa ni mume, akatoka alifajiri sana,.. na kwa vile ilikuwa siku ya mapumziko, yeye akatoka nje
na kupitia pitia bustanini, nia ni kukwepa kuongea na mkewe, alihisii jana
atakuwa kamkorofisha, ila anakumbuka kuwa mkewe alisema ana jambo la kuongea,
akilini akawa anajiuliza ni kitu gani.
Akilini
alikuwa katulia, lakini kuna kitu alitakiwa kukifuatilia, na alishaambiwa ili
akipate, anahitajika kupeleka salio lililobakia.
‘Kwa vile
pesa hii haitoshi, hatuwezi kukupa zile picha,....na kanda ya video, ujue hizo
picha zimechukulia kwenye video,...’akaambiwa
‘Kilichfanyika
mpaka sasa ni kuiondoa hilo tukio kwenye mitambo ya kwenye ile bar, hukohawawezi
kulioa hilo tukio tena, sasa hilotukio lipo mikononi mwa watu, ambao
wamejitolea kufuta huo uchafu wako....sasa utaka huo uchafu wote uwe mikononi
mwako,kamilisha hiyo pesa iliyobakia....’akaambiwa
‘Lakini
nimewaambia siwezi kutoa pesa banki....’akasema
‘Hizo
nyaraka ni kitu kidogo sana, ukipeleka sasa hivi watakamilisha na wewe utaweza
kuchukua pesa yako, sisi tunajua yote hayo, ukitoka hapa peleka hizo
nyaraka,baada ya masaa 24, akaunti yako itakuwa huru..sasa ukizid kuchelewesha
ndio unajiweka kubaya...’akaambiwa
‘Nina
uhakika gani kuwa mtanipa hiyo video,je kama mumetoa kopi ili mje baadaye
kunisumbua tena...’akasema
‘Sisi tuna
uaminifu,...na sijui kwanini usituamini, kama tumeweza kufuta kila kitu kwenye
mitambo ya ile hoteli na bar, kwanini tukufanyie hivyo tena.....’akaambiwa
‘Nakuapia,
kama mtanifanyia ubaya, mkanisaliti,..hamjui nilivyo...nitawatafuta hata chini
ya ardhi nitawapata..na nikiwapata hamtaamii nitakachowafanya....’akasema
‘Hahaha,haina
haja ya kutoa vitisho,tumeshakufahamu ulivyo...lakini huwa hata siku moja mtu
hatishiwi nyau..wewe shukuru kuwa tumekusaidia, je kama tungeacha huo uchafu
ukaonekana na utawala,...wakaufichua kwa wadaku, hizo ndio shukurani zako,kweli
shukurani ya punda ni mateke....’akaambiwa
‘Niwashukuru
kwa lipi, walamlungula nyie, blackmailer wabaya
kabisa,najua kabisa hili mumelipanga, hizi ni njama,najua kabisa,... mimi sio
mtoto mdogo,nyie ni shetani,mnaishi kuwa dhuluma,mfanye hivyo ili mpata pesa ya
wizi....’akasema
‘Kwahiyo
unasemaje, kama vipi ngoja tupeleke nakala moja ya picha kwa mkeo, aone huo
uchafu wako achilia mbali mkweo...’akasema
‘Mkwe wangu
anawahusu nini...’akasema
‘Hahaha,
ndugu, wewe umesema unafahamu sana,...hilo ni swali lakuuliza, ujue hawa
unaopambana nao sio watu wa huko kwenu,ni wataalamu...sitaki nikuambie mengi,
....’akaambiwa
‘Siwaogopi
kabisa, nitapambana na nyie, ngojeni,mumeniwahi,nakubali, lakini lipizo lake
hamtaamini...’akasema
‘Kwahiyo
unataka tupeleke nakala kwa mkweo.....unasemaje ili uone kuwa hawa watu
hawaogopi...’akaambiwa, na hapo akahema tu.
‘Ndugu,ukumbuke
mkweo alivyo, hakupendi, hawakutaka kabisa wewe uolewe na mkeo, nasema
uolewe,maana hata mahari ya kulipa ulikuwa huna mkeo ndiye aliyekulipia mahari,
kweli si kweli...’akaambiwa na akaa kimia akihema kwa hasira.
‘Kwahiyo mke
wako anakupenda sana, hivi unataka upendwe vipi, ..nyie watu hamna
shukurani, ujue ni mkeo tu ndiye anayekupenda,...sasa
na yeye akikuchukia utakuwa mgeni wa nani...utarudia umasikini wako,najua huko
ulikuwa genge la vibaka, najua ulijiunga na kundi la kubaka, mkawa na mnaweka
vifaa vya kuchukua video kwenye majumba ya watu mnawatishia na kuwadai pesa
nyingi, hiyo ilikuwa kazi yako kabla hujakutana na huyu binti, ‘akaambiwa na
aliposikia hivyo akajikuta mwili ukinywea
‘Mambo yako
yote yaajulikana na mengi hayafahamu mke wako, wakitaka wanaweza kuyaweka wazi
yote, lakini kwa vile upo tayari kutoa ushirikiano, basi, wameyasahau, ukilipa
hiyo pesa,wanakukabidhi kila kitu, unakuwa huru, ila uache hiyo tabia....’akaambiwa
‘Mtaona....’akasema
‘Ndugu, hiyo
tabia yako, uliyokuwa nayo huko ni cha
mtoto...ni sawa na mtoto kuchezea kigari
cha mwanasesere na kujiita dereva,...hapa kuna wajuuaji,wanajua ni nini
wanachokifanya, mimi sitaki kukutisha saana, sasa kama wewe unabisha jaribu....’akaambiwa
‘Sawa nyie
si mnahitajia pesa,...nyie si wajanja,pesa mtapata,mnasiki pesa mtapata, lakini
mkumbuke hizo ni pesa chafu zitawaandama...’akasema
‘Kwetu sisi,
kwao hao watu maana mimi ni mjumbe tu, kazi yangu ni kupeleka taarifa,....hatutofautishi
pesa chafu na safi ilimradi inalipa...unasikia, fanya unavyoambiwa,
vinginevyo,mimi nitawaambia umeshindwa, kutoa ushirikiano, ukiiona hii
video,ndio utajua wewe hufai kabisa kuishi na huyo mwanamke...weweni mbakaji,
mzinzi, mlevi.....hahaha....’akasema na kucheka
‘Nakuapia
nitawapata tu....ni lazima mtalipa...’akasema
‘Hahaha,
..kumbe muda wote huo ulikuwa unateseka,unatamani
mabinti wa kwenye bar, au mkeo anakubania nini, hahaha, mzee mzima huna
aibu...wewe, shukuru sana, maana video hii ikiingizwa sokoni,mbona inalipa
sana, ina kichwa cha habari, mzee
kazidiwa na kugeuka kuwa mbakaji....hahaha...’akasema
‘You devil...nitahakikisha ninawapata
mmoja baada ya mwingine,mtaona....hamunijui mimi...’akasema na kubamiza simu
kwenye sofa....
‘Halloh ...unasikia....’akasikia
jamaa akiita kwenye simu, akaitizama, baadaye akaiendea na kuchukua akaiweka
sikioni kwa hasira akasema;
‘Kumbukeni
hilo,...mimi siomjinga kama mnavyofikiria,...hayo maisha nilishawahi kuyapitia,
hamjui ninapotokea,....mtaona...’akasema
‘Unachelewa
mzee,...saa hivi ni saa ngapi....hujui ni nini mkeo kakipanga,....shauri lako...’akaambiwa na
alipotajiwa mkewe ndio akakurupuka haraka akaenda kuziwakilisha hizo nyaraka
benki, akambiwa asubirie masaa 24
‘Oh,...’akasema
akiwa hana ujanja
Kichwani
alikuwa na hasira, lakini hata hivyo, aliogopa hayo mapicha yasije kufika kwa
mkewe, lakini akawaanajiuliza je kama wanamchezea, atatoa pesa na itakuwa ndio
mchezo wakumtoa pesa.
‘Mhh,hawa
wanaonekana hawawezi kunitapeli...lakini lazima nipambane nao..’akajikuta
akisema/
‘Halafu
wamesema wanaweza kufikisha huo uchafu kwa mkwe wangu,hivi hawa watu
wamenijuaje,na wamemjuaje mkwe wangu yaonekana ni watu wabaya sana,natakiwa
kuwa makini nao..hata hivyo sikubali, nitapambana nao...’akasema
*******
Basi siku
hiyo kazini alijifanya mgonjwa,akaruhusiwa kuondoka mapema, na alipotoka hapo
kazini, akapitia bar , lakini sio ile ya kawaida, akanunua vinywaji akaenda navyo nyumbani,
akanywa huku anawaza jinsi gani ya kufanya
‘Ningelikuwa
kwetu ningeliwatafuta wahuni wangu, ....nawafahamu wanajua kufuatilia haya
mambo,..lakini huku simfahamu yoyote...ooh, nitamtafute nani sasa...?’ akawa
anajiuliza baadaye akakumbuka jambo, akachukua simu akampigia rafiki yake mmoja
‘Ndugu yangu
nipo Ulaya, na wameniingiza mjini, nataka unisaidie, ulisema huku kuna watu
wako ehee...nataka unitafutie mpelelezi, binafsi...ehee, nataka anifanyia kazi
yangu kuna watu wanajifanya wajanja...ehee, nitakurushia gharama zako, usijali,
...ndio nimekuelewa, ndio nimekunywa kidogo,...ndio nakuelewa, sijalewa sana
nipo makini,..fanya hivyo...ni muhimu...’akasema na kurudi kwenye ulevi wake.
‘Lazima
nipambane nao..na ole wao,nikimfahamu mmoja tu...atakuwa ni mfano,...’akasema
na akakumbuka kitu, akasimama na kuingia ndani, alipofika akafungua kabati,
sehemu ya chini, akavuta droo, na humo akakiona anachokitafuta,...
‘Mhh,..wewe
hujatumika...miaka mingi hujatumika,....’akachukua kitambaa akakizungushia
mkononi, halafu akatoa kitu, na kuanza kukiangalia, akaikagua...
‘Rafiki
yangu upo eeh...’akasema, halafu akachukua boksi, , akatoa risasi, na
kuzihesabu, halafu akazirudisha kwenye boksi,
‘Hizi
zinatosha, mapambano yakianza, sijali....’akasema huku akichukua kitambaa
kingine maalumu akafuta futa kile kitu na kuirudisha mahali pake...
‘Wewe ni
rafiki yangu huwezi kuniangusha ...ukumbuke kunisaidia muda ukifika,umelala
sana...najua,najua..upo ulaya hutaki shida, lakini, watu wananichezea,
wananichokonoa,...’akawa anaongea utafikiri kuna mtu humo ndani...
‘Hivi ni
kwanini, pesa zangu mwenyewe, wanazichukua,....kisa malaya....hahaha....hahaha’akawa
anacheka kama kichaa, halafu akasikia sauti, akageuka kuangalia nyuma, alikuwa
na uhakika ni sauti ya kitu, na ni lazima atakuwa ni mtu
Kwa haraka
akafunga kabati, na kuhakikisha kila kitu kipo sawa, kama ilivyokuwa awali,
halafu akatoka nje, ...
Alipofika
sehemu ya maongezi, akahisi mlango upo wazi, lakini alikumbuka kuufunga, nywele
zikamsisimuka, akaanza kunyemelea, ....kuelekea sehemu ya jikoni, huko alisikia
kama sauti ya maji.
Alitembea
hivyo kwa kunyemelea hadi akaingia jikoni,
akamuona mkewe akiwa kainama kwenye sehemu ya vyombo akiwa anapanga
panga vitu, taratibu akageuka na kwa mwendo wa kunyata akarudi sehemu
alipokuwepo awali na kuendelea kunywa, kunywa kwa hasira
‘Huyu mtu karudi
saa ngapi, leo mbona kawahi hivyo....ni tatizo jingine hili , sina uhuru,
sina...aah,...’akawa anaongea kwa sauti ndogo.
‘Nikwanini
mke wangu mwenyewe, nikimuona mwili wote unazizima kwa woga, wasiwasi,....sijui
nifanye nini.....ni kutokana na hao watu....’akasema huku akitupa jicho ya
kujiiba kwa mkewe...
‘Aaah,
aishie zake,leo,simtaki, nataka kinywaji tu...siwataki wote,hata yule
malaya...aliyenifanyizia..’akasema akimimina kinywaji kwenye gilasi
‘Kama
ningekuwa sehemu kazi hii angeifanya yule malaya...’akawa anaongea peke yaka.
‘Na yule
malaya...siku nikikutana naye tena,...sijui,....nitajikumbushia ule uovu wangu
wote wa zamani, ....hawanijui hawa watu...ngoja...’akawa anazidi kuongea peke
yake
‘Hawa watu
hawanijui, wananiona mimi lofaaa.., hawawezi kuniadhiri kiasi hichi,haijaahi
kutokea, kiongozi wa genge haramu kuwekwa uchi...hawanijui hawa, hawanijui...’akasema
na mara akahisi kama kuna mtu anamkaribia,akahisi mwili ukiingiwa na woga
Kwa hali ile
alijua ni nani... ndio hapo akasikia...
‘Mume wangu leo nina mazungumzo na
wewe..
‘Una mazungumzo gani tena mke wangu,
tafadhali nakuomba nipumzike...sipo sa-sa-sawa...mwenyewe siunaona....
NB:Leo
nakupa hiyo sehemu ndogo, kufichua
fichua kujua ilikuwaje,....tutaendelea na mazungumzo ya wawili hawa sehemu
ijayo,mazungumzo yao ni muhimu
sana,..kwani kutokana na wao,tutaweza kuona jinsi gani mlungula ulivyo mbaya,
unavyoweza kuharibu ndoa za watu,na hata kufikia watu kuuana...
WAZO LA LEO: Pombe ni kilevi kinachoathiri
ubongo, japokuwa twaona ni kitu cha kustarehesha ubongo,lakini madhara yake ni
makubwa, kiafya na pia ni kishawishi kibaya cha maasi. Ewe ndugu mpendwa,
jiepushe na ulevi
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment