Jana nilikuwa nawapa kuku wangu chakula, kuna kuku wawili
wanatembea pamoja, japokuwa mmoja ni mkubwa kuliko mwingine, huwa mmoja
akimkosa mwenzake utaona akilia huku na huku akimtafuta mwenzake wakiamuka
asubuhi mbio mbio kwenye kuchakarua majalalani... Lakini cha ajabu
nilipowatupia mchele, wa kutosha tu yule mkubwa akawa anamdonoa mwenzake,
badala ya kula akawa anafanya kazi ya kumfukuza mwenzake , nikajiuliza ‘hivi
ule urafiki umekwenda wapi, mbona nimewatupia mchele mwingi tu…
‘Na huyu kuku anayemfukuza mwanzake si yule kuku kama mwenzake hayupo anakuwa akilia huku na kule akimtafuta mwenzake,....' nikajikuta nikiongea mwenyewe, ... mhh, nikakumbuka ule usemi usemao ukitaka kujua tabia ya
mtu ngoja apate…
Wakati naliwaza hili mawazo yangu yakarejea kwenye ile
zawadi au bashishi iliyotokana na pesa ya RADA, nahisi wengi wameshaanza
kuisahau , ila kwa kukumbushia tu ni kuwa kuna fungu lilitolewa kutokana na ile
pesa iliyotolewa kwenye kadhia ile ya RADA, kutokana na hiyo pesa serikali
iliona iitumie hilo fungu kwa manufaa ya watu wake, ikalipeleka hilo fungu
wazarani na wizara kwa nia yake njema ikapanga kuwa pesa hiyo inunulie vitabu
vya shule kwa ajili ya shule za msingi, na kweli nia njema hiyo ikafanyika, na
mapesa yakagawanywa kwa wachapishaji wa vitabu ambao walikuwa na vitabu vingi
kwenye maghala yao. soma hapa:
http://www.pesptz.org/index.php/home?lang=swahili
Nakumbuka kwenye kasheshe hiyo kuna makampuni makubwa
yaliyokuwa na kesi mbali mbali yalikataliwa kupewa hilo fungu, ..Mimi niliandika
nakala moja kulalamika kuhusu hilo kuwa huenda katika kufanya hivyo itakuwa
haijatendea haki makampuni hayo, nikayaita makala hayo, `
mnyonge
mnyongeni lakini haki yake mpeni…’ niliandika nikijua katika kufanya hivyo,
sio tu hayo makampuni yatapata hasara, lakini pia hatukuwa tumewatendea haki
watu wengine wasiohusika, tunawapa adhabu hata wale wasiostahiki , yaani
wafanyakazi na familia zao, watungaji wa vitabu nk.
Nakumbuka wengi wa wafanyakazi wa hizo kampuni walikesha kwa
kuomba, wakafunga ,huku wakimlilia mola wao kuwa je hiyo ni haki, kwanini na
wao wasifikiriwe kwani wameteseka vya kutosha, wameishi katika mazingira magumu, kwani mishahara yao ni
midogo sana, na ilikuwa hata hiyo mishara yenyewe inalipwa kwa shida, maana
biashara za vitabu hakuna, sasa tangazo hilo kuwa pesa ya RADA italipwa kwenye
hayo makampuni, ikawa ni neema, lakini tena wanaambiwa nyie hamtapata kwasababu
mna kesi.. mmmh!
Wavuja jasho hawa hawakukata tamaa, wakazidi kukesha na
kuomba huku sheria zikifuatiliwa, na Mungu akasikia kilio chao, na baadhi ya
kampuni zikaonekana hazina hatia, serikali kwa nia safi ikasema hapana wote
wanaostahiki watapata hilo fungu ili waweze kuvitoa hivyo vitabu
vinavyoharibika maghalani, mabilioni yakatumwa kwa hizo kampuni.
Wavuja jasho, wanamaombi, waomba dua, wafanyakazi,
walalahoi, waliokuwa wakikesha kwa kuomba, wakasikia taarifa hiyo, ikawa ni
shangwe na vigelegele, kupongezana na kujikweza kwa wakubwa ili kuwapa mikono
ya ushindi, mungu hapo akasahaulika,…ndivyo wanadamu tulivyo tukipata hatusemi
ahsante mungu tunakimbilia kumuona mwanadamu mwenzetu ndiye mtoaji wa hiyo
riziki.
‘Mhh, sasa ni mwendo wa mkao wa kula..’ mmoja wa wafanyakazi
wa siku nyingi akasema, na wengine wakionyesha mfano wa mapaja ya kuku kuwa
sasa yapo mezani, akasema
‘Mapaja ya kuku sasa yapo mezani…..’ walisema hivyo wakiwazia
hayo mabilioni kuwa ni sawa na mapaja ya kuku na ya kuwa angalau… muajiri kwa
kuwaonea huruma atawawezesha na wao wafanyakazi waondokane na dimbwi la
umasikini kwa uvumilivu na kuvuja jasho kwao huku wakipokea mishahara midogo
sana kwa siku nyingi.
Lakini pia waliwazia mbali kuwa kutokana na pesa hizo ajira
itakuwa bora zaidi, watawekeza kwa kuzalisha vitabu bora zaidi, na hata
kugundua njia bora zaidi na matokea yake ni kuwaboreshea kipato chao, ikiwa na
maana mishahara itapanda ili kuondokana na dimbwi la umasikini.
Haikutosha hapo serikali kwa nia njema tena ikasema fungu bado lipo nitatoa zaidi, chapisheni
vitabu zaidi, visambazwe mashulani (BAE tender)…na ikafanyika hivyo kwa haraka
sana, maana makapuni haya yana utaalamu wa muda mrefu, mmmh mungu awape nini
wafanyakazi wakajua sasa hakuna shaka tena, kampuni itawafikiria hasa katika
mishahara maana pesa ipo mtaji upo, na wakitumia utaalamu wao waataboresha
kampuni yao na kuwa bora zaidi.
Nilipofikia hapa kuwaza hilo nikawaangalia wale kuku wangu,
nikawarushia tena mchele fungu la pili kubwa zaidi, kazi ikawa ile ile kuku
wakawa wanapigana na kukimbizana, mkubwa
anamuonea mdogo, mdogo hana haki, japokuwa fungu limetolewa kwa wote,
lakini mkubwa anasema `changu, changu …’ akitafuta kila mbinu za kuhakikisha
mwenzake hapati,…mmh,
Nikiacha kuwawazia wale kuku akili yangu ikarejea kwenye
hili tukio maana najiuliza hivi kweli hilo fungu la kwanza na hilo fungu la
pili, hivi kampuni itatetereka tana, hivi kwa pesa hizo waajiri hawataweza
kuwafikiria wavuja jasho, hawa waliokuwa
wakiomba na kukesha, wakiishi kwa shida na mshahara mdogo, wakiombea kuwa ipo
siku mungu atajalia neema iwashukie, ..ni kweli neema imeshuka, lakini je
wamepata nini…mmmh ukitaka kumjua mtu tabia yake ache apate..
Mara boooom….
Serikali ikasema kuwa sasa hivi itakuwa ikichapisha vitabu
vyake wenyewe, …kauli hii ikawa ndio
kisingizio, mapaja ya kuku, yaliyokuwa
sahanini, yaliyokuwa yakiwatoa mate walioandaliwa, mwenye nacho akataka zaidi,
na yule asiye nacho akawa ananyosha mkono, sasa kauli ya hiyo ya serikali,
ikawafanya mawazo yageuke..wasiwasi, ukawaingia wawekezaji, na ilivyo mwenye nacho atakuwa ka
neemeka, na muwekezaji kwa kauli hiyo,
japokuwa ana mapaja mezani,lakini kwa tabia na hulika, atageuka huku na kule,
akiwaangalia wenzake ambao wanaendana naye, hapo tena hataki jasho, wale wavuja
jasho, wananuka, hawafai tena keshapata kisingizio…mmh badala ya kumshukuru
mungu moyo unakengeuka, ubinafsi unatawala zaidi, akili inakuwa sio ile tena…
‘Jamanieeh mumesikia, serikali yenu ilivyosema…..kazi
hakuna, na siwezi kuendeleaa kuishi nanyi, najua mumeteseka sana, mumevumilia
sana, lakini nitawalisha nini…nimewapa kidogo, kinatosha,..kwahiyo naona mwisho
wa mwezi huu niwape haki zenu kisheria muende mkapumzike majumbani kama
kukitokea kazi nitawaita…’ ni kauli ya mshitukao, ni kauli ambayo
haikutarajiwa.. kila mtu alipigwa na
butwaa, huku mate yakiwa bado hayajakauka mdomoni, mate yakitamani yale mapaja
ambayo yanayeyuka sasa, ina maana hatupati tena kitu hapa, ina maana hata mifupa
hakuna…ukumbuke mishahara yao haijaboreshwa, na kisheria haki zao zinalipwa
kutokana na mishahara yao,…mwezi mmoja wa notice, na mwezi mmoja wa bye bye,
kafe na umasikini wako.
Ni ukweli usiopingika kuwa kwa muajiri akiambiwa kazi
inayokuzalishia haitakuwepo tena, inamvunja nguvu, anakuwa hana jinsi
akifikiria gharama za uzalishaji na mara nyingi anachokimbilia kuangalia ni
gharama za rasilimali watu, wengi hawaangalii gharama za uendeshaji kama mafuta
magari nk, maana magari na mafuta ni kwao wao wenyewe wakubwa, yeye anachoangalia
ni rasilimali watu, kile anachowalipa wafanyakazi ni mzigo kwake, sasa je
serikali kwa kutangaza hivyo haioni kuwa inawatelekeza watu wake, wale
waliokuwa wameajiriwa na haya makampuni je watakwenda wapi, au wana jinsi gani
ya kuwabeba hawa watu. Basi wawachukue kwenye hayo makampuni yao waliyopanga
kuwa yatazalisha vitabu .
Mabilioni yale yatakuwa hayana maana kwa wafanyakazi hao na
familia zao, ina maana watoto wao hawataweza kusoma tena…maana elimu sasa
inahitaji pesa, kama huna pesa mtoto wako hatakwenda na wakati,…kama
wafanyakazi hawa watakosa ajira, basi hata kule walipokuwa wamewapeleka watoto
wao kusoma inabidi wawaondoe, wakawasomeshe kwenye shule za kawaida…huyu mtoto
alishazoea huko alipokuwa sasa anarudishwa sehemu nyingine, kwa mtoto kuelewa
ni kugumu…yote ni kwa vile mzazi wake sasa hana ajira yote haya ni kutokana
changamoto ya hilo fungu la rada, badala ya neema kwa wengi limekwenda kuwa
neema kwa wachache.
Kilio cha wavuja jasho ni kuwa serikali iangalie upya hili
zoezi, la kuondo a uchapishaji wa vitabu kutoka kwa makapuni binafsi, kwani
inaua makampuni ya uchapishaji makampuni makongwe yenye kujua vyema vitabu
vyenye manufaa kwa wanafunzi, na pia mkumbuke kuwa mkiyaua haya makampuni mnawakosesha
ajira watu wenu, je wao watakwenda wapi,…watoto wao watasoma wapi..
Ndio mtachapisha vitabu vyenyewe, lakini mkumbuke serikali
imeshashindwa kuendesha shughuli zake wenyewe nyingi tu ikawapa watu binafsi,
na hawa wamekuwa wakizifanya hizo kazi kwa ubora zaidi. Tuangalie hili kwa mapana
zaidi, kwa nia njema ya kuwawezesha watanzania wajiingize kwenya ajira hii ya
uchapaji wa vitabu kwa manufaa ya taifa, na vitabu view vingie vyenye mawazo
tofauti.
Cha msingi ni kuangalia ubora na hili litawezekana kama
kutakuwa na idara maalumu ya wataalamu waliobobea wa mitaala , na ubora wavitabu
hivyo, wao wavipitie na kuona kama kweli vinastahiki, na utofauti wa vitabu
ndio chachu ya kuwezesha mtoto kufikiria zaidi, kwani yeye anapata mawazo
kutoka vichwa tofauti, na unamjenga huyo mtoto kupenda kusoma vitabu tofauti
tofauti, lakini kama tutakuwa na mawazo ya kichwa kimoja tu, aina moja ya
kitabu tu, bado tutafika mahali tutakuja kuona kuwa kumbe mawazo hayo yana
walakini…..tuangalie haya kwa mapana zaidi kuliko kuangalia yale mapaja yaliyoandaliwa mezani.
Mhh ama kweli ukitaka kujua tabia ya mtu, ..msubirie akipata….
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment