Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, November 7, 2012

Mnyonge Mnyongeni Lakini Haki yake MpeniKila ukipita kwenye barabara zetu kubwa utaona mabadiliko makubwa, upo ujenzi unaendelea, na kwa kiasi kikubwa inaleta faraja, tukijua kuwa huenda lile donda ndugu la foleni za barabarani zitapungua,ili kuleta maendeleo, kwani miundo mbinu hasa ya barabara ni muhimu sana, katika maendeleo ya nchi, na wananchi wake.Tunaipongeza serikali kwa hilo.

Lakini kwa mtizamo wa haraharaka, tunahisi kuwa huenda tungeliangalia pia barabara hizi za mitaani, ambazo zinaweza kupunguza tatizo hili la foleni za barabarani, kwa mfano kuna barabara za mitaani, za mkato, zinaweza kufika sehemu nyingine bila kuzunguka hadi mjini, posta au Kariakoo, kwa mfano kuwa barabara zinazotokea Gongolamboto hadi Mbagala, au Gongolamboto hadi Ubungo, na nyinginezo, hizi zingeboreshwa, zingesaidia sana.

Tatizo kubwa, barabara kuu zote zilielekezwa mjini posta na Kariakoo,kwasababu enzi hizo huko ndio kulikuwa mjini na huduma zote,za kiserikali, masoko, bandari, nk, zilikuwa maeneo hayo, sasa mji umepanuka, mjini ni kila mahali. Hatuhitajiki tena kuelekeza hizo barabara kwenda Posta , au Kariakoo tu, tunatakiwa kuzielekeza sehemu nyingine ambapo kuna huduma kama hizo, au huduma hizo ziondolewe huko Posta na Kariakoo zipelekwe nje ya hapo.

Hakuna atakayepinga kuwa sehemu kubwa ya muda wetu tunaipoteza kwenye foleni za barabarani, na baya zaidi hata ukiingia kwenye maofisi yetu ya serikali utakutana na tatizo la foleni kama hizo, huenda watendaji wapo mabarambarani wakiwa kwenye foleni, hata kuna mzungu mmoja akasema, hii nchi kila kitu ni kusubiri, kila kitu ni kwa foleni, ikanikumbusha enzi ile ya sukari, unga na hata sabuni ilikuwa kwa foleni!

Lakini kilichokuwa kimesababisha hayo enzi hizo hakipo tena, kwanini bado tuna tatizo hilo.

Na katika hali halisi kunapokuwepo na kusubiri kwingi, mengi yatatokea, kuna ambao watatafuta njia za mbadala, hata kama sio halali, ili wawahi, ili wahudumiwe, ili wagonjwa wao wapate huduma, ili wawahi kwenye mambo mengine, na utakuta wengi wao ni wale wenye uwezo wao. Wanyonge watabakia kusubiri, wanazidi kuumia…..

Lakini yote haya yanabadilika kidogokidogo,kwasababu ya ushindani wa biashara, kunapokuwepo na ushindani wa kibishara,lazima huduma, na utendaji unabadilika, kila mmoja akitafuta njia bora zaidi, lakini kama ni mtu mmoja, au kampuni moja, inayotoa huduma hiyo pekee, tusitegemee mabadiliko ya harakaharaka.

Wakati hayo yakiendelea akatokea Mzee mmoja akaulizia wapi anaweza kupata vitabu, na alipoulizwa vitabu gani na vya nani, akasema vitabu vya shule, yeye alikuwa mwalimu wa siku nyingi, sasa kaombwa kujitolea kufundisha huko kijijini kwao, lakini tatizo vitabu havipatikani tena na yeye angelipenda vitabu vilichapishwa na Macmillan au Oxford, kwasababu wao ni wakongwe katika kazi hii ya uchapishaji.

‘Makampuni haya nayafahamu toka enzi na enzi..’akasema.

‘Hayo makampuni nimesikia yamefungiwa?’ mmoja akasema.

‘Ohh, hapana,kwanini wanafanya hivyo, hawajui kuwa wanadumaza soko la elimu, hawa watu walishaweza kufika hadi huko kijijini kwetu, sehemu ambayo ni ngumu kufika,na waliweza hata kufikia shule za ndani ndani, na kutoa huduma za vitabu, kama wamewafungia basi wanataka kuua elimu’akasema mzee huyo kwa masikitiko.

`Ni kweli ni nani kwa wazee wetu asiyejua makapuni haya, ubora wa vitabu vyao, na huduma zao katika elimu ya nchi hii. Makampuni haya yalikuwa mchapishaji na msambazaji mkubwa wa vitabu, kila kona ya nchi, kwasababu ya ushindani wao, walikuwa wakiboresha huduma zao siku hadi siku. Leo tunasikia kuwa huenda yamefungiwa!’ akasema mama mmoja mzee.

‘Yanafungiwa kwa kosa gani?’ yule mzee akauliza.

Mjadala ulikuwa mrefu kila mtu akisema lake, na wengi walikuwa hawana uhakika ni kwasababu gani yamefungiwa, lakini yule mzee akasema;

‘Vyovyote iwavyo, hiyo ni sawa na ile kesi ya yule mwanamke malaya aliyetakiwa kupigwa mawe, na wakaambiwa watu, aliye msafi ampige yule mwanamke mawe, ….tatizo sio hayo makapuni ya uchapishaji, tatizo ni hawo wanatoa hizo zabuni…’akasema huyo mzee.

‘Kwa vipi mzee?’ akaulizwa.

‘Kama wewe unahitaji huduma, ukafika, ukaambiwa njoo kesho, na hizo njoo kesho zikawa nyingi, unafikiri ni nini kinachotakwia hapo?’ akauliza huyo mzee na watu wakacheka.

‘Tatizo la nchi yetu ni hii kusumba ya `kusubiri’, tatizo la foleni, kila kitu kwa foleni, na haya yanafanywa kwa maana maalumu, wewe usiye na haraka utasubiri, lakini muda ni mali, kuna yule ambaye ana haraka, akichelewa ni ni hasara kwake, akichelewa mgonjwa wake atakuwa taabani, unafikiri atafanya nini, na akifanya hivyo aliyesababisha hayo yote ni nani, na nawauliza kosa hilo lilifanyika wapi?

Watu walisema kosa hilo halikufanyika hapa Tanzania…

‘Kama halikufanyika hapa kwanini tunayafungia haya makampuni, ambayo huenda yanaendeshwa kwa sasa na wazawa. Jamani mbona tunakimbilia kuangalia tatizo kwenye matawi, wakati tatizo limeanzia kwenye mashina,hatutafika, tutaishia kuyaua hayo makampuni ambayo yalikuwa yakisadia watoto wetu wapate vitabu kwa muda muafaka, na kwa ubora, kwasababu hapo kinachoonekana ni kukimbilia maslahi binafsi.

‘Kwasababu najiuliza kwaninni hayo yaonekane sasa hivi, sizani kuwa ni uboreshaji na uwajibikaji, nafikiri kuna jambo limetokea, kama sikosei ni hiyo pesa ya rada’akasema huyo mzee.

Wote tukacheka.

`Msicheke jamani, …hili ni tatizo, kunapokuwepo na masilahi, hata ndugu watauana, ..bila kujali udugu wao, bila kujali ni nani wataumia, sisi mawazo na macho yetu yote yatakuwa kwenye hayo maslahi. Tukumbuke kuwa kwenye taaluma hii ya vitabu, na elimu, kuna watungaji, kuna wafanyakazi na familia zao, hawa hawaangaliwi kwa sasa, wanachoangalia watu hawo kwa sasa ni kuhakikisha yule aliye mbele anaondoka ili mimi nishike nafasi yake.

`Huyu mtungaji wa vitabu ambaye alijitoa kwa hali na  mali hadi akafanikisha kutoa kitabu, na kitabu hicho kikapitishwa na hawo wanaoizinisha, na hata kutoa ithibati, amefikiriwaje? Sisi tunachokimbilia ni kuyafungia haya makampuni, je gharama za hawa watungaji, na muda wao, ni nani atawalipa? Kila siku tunalalamika kuwa hatuna watungaji wa vitabu, je hatuoni kuwa huku ni kuwavunja nguvu hawa watungaji wa vitabu hapa nchini,…

‘Tujiulize kosa limefanyika wapi na kwa nani, …na kwanini tuangalie upande mmoja wa shilingi tu, kwani huyo mchapishaji wa vitabu asingelifikia kufanya hilo kosa kama kusingelikuwa na huo mwanya uliosababisha hayo yote. Sasa ni nani anakomolewa hapo…?’ akauliza huyo mzee.

‘Hapo, atakayeumia sana, ni watoto wetu, watakosa elimu bora kwa wakati, watakosa vitabu, kwani vitabu vilivyokuwa vimechapishwa kwa ajili yao vipo kwenye magodauni, vimelundikana kwenye hayo makampuni …sasa macho na hamasa zetu zote ni kwenye hiyo pesa ya rada.

Kuna huyu mtungaji, alitarajia kupata chochote kutokana na kipaji chake hicho, leo akifika kwenye hayo makampuni aliyoingia nayo mkataba, anaonyweshwa maboksi yaliyojaa vitabu, anaambiwa kampuni imefungiwa, hatuwezi kuuza tena hivyo vitabu…hawa wanaadhibiwa kwa kosa gani?

‘Kuna wafanyakazi, na familia zao, ambao wamekuwa wakifanya kazi kwenye hayo makumpuni usiku na mchana, na wao wanafikishwa kubebeshwa huo mzigo, huenda kazi hawana tena, na tujiulize na wao watakwenda wapi,na je kwanini na wao wanaadhibiwa kwa kosa hilo, ambalo halikutendeka hapa nchini…hakuna anayejali hilo, hamasa zetu zote ni kwenye hiyo pesa , pesa ya rada.

‘Kila mmoja anataka apate, mwenzake aondoke, yeye apate zaidi, basi kama ni kwa ajili ya elimu ya watanzania, na maendeleo ya nchi, lililo jema na hekima kwa maslahi ya taifa, ni kuzitoa hizo pesa kwa makapuni yetu yote ili yaweze kufanya kazi, na baada ya hapo tunatoa `onyo kali’ kuwa kuanzia sasa, hatutakuwa na msamaha kwa kampuni yoyote itakayotenda kosa, lakini kwanza tuanzie na sisi wenyewe tunaotangaza hizo zabuni kuwa tutaboresha utaratibu wetu, ili tusijenge mianya …

‘Mimi nawapongeza sana hawa waliojitahidi hadi kuweza kufikisha vitabu kule kusipowezekana, makapuni haya makongwe, Macmillan na Oxford walifanya kazi kubwa sana hapa nchini, basi tu,…mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’akasema yule mzee kwa huzuni.

4 comments :

Anonymous said...

Kweli nchi hii ina mambo ukiona hivyo, mgawo haujafika kwa waheshimiwa

Anonymous said...

Umenena kweli mkuu, hoja hii itume bungeni

Anonymous said...

Wakati mwingine taasisi zetu zinatoa adhabu kwa kujipendekeza bila kujali utaifa wetu. Hapa watakaoumia ni watoto wetu

Anonymous said...

Kweli hii inahitajika ifike Dodoma kwa waheshimiwa