‘Rafiki yangu kabla hatuajendelea huko sisi tuna hamu sana ya
kusikia jinsi gani uliyochukuliwa na mama yako, na ile familia iliyokulea
ilikuwaje, ..nesi yupo wapi, hukuwahi kuonana naye tena…na yule mume mwenye
nyumba na mama yako mlezi, hamkuwarudia kuomba msaada…?’ nikamuuliza
`Ukumbuke kuwa mama ndiye aliyekuwa akinisimulia hiki kisa, na
mama alikuwa akinisimulia huku akiwa kalala kwenye kochi, kwani mwanzoni
nilikuwa nimekaa naye na kichwa chake kilikuwa kwenye mapaja yangu, lakini
baadaye nilipokwenda kumchukulia maji na dawa ya kutuliza maumivu, akawa kalala
kwenye kochi…
Mnakumbuka sehemu hiyo mama
aliposema;
‘Mwanangu nitafutie nauli niondoke…sitaki niwakosanishe wewe na
mke wako, lakni kabla sijaondoka, nataka nikuhadithia maisha yangu yaliyopita,
ambayo hujawahi kuyasikia,….’ Akasema na mimi nilimuambiaje;
‘Mama nilishakuambia huwezi kuondoka hapa nyumbani, ..huwezi
kuniacha..’nikasema na mama akasema hivi
‘Hapa ilivyo mke wako keshatoa tamko, ama mimi ama yeye…je unahisi
hapo utafanya nini, …huwezi kumuacha mkeo kwasababu yangu mimi, hilo
silikubali, mke wako ni muhimu sana,….’akasema mama
‘Mnakumbuka sehemu hiyo…?’ akatuuliza
‘Ndio…kwani ilikuwaje kwa mama mpaka ashindwe kuendelea kuongea..?’
nikamuuliza
‘Sikujua kuwa japokuwa mama alikuwa kiongea kumbe kichwa kilikuwa
bado kinmuuma, ila alitaka kuhakikisha nafahamu wapi nilipotokea, kwahiyo akawa
anajikaza tu..huku anaumia ndani kwa ndani..na jinsi muda ulivyokwenda hali
yake ilikuwa inajionyesha sasa, hali yake ilikuwa sio nzuri…, ‘akasema
‘Oh ina maana mama yako,…alikuja kufa…?’ jamaa mmoja akauliza
‘Mama hali yake kwa muda ule ilikuwa mbaya,…mimi nikawa nimekaa
pembeni yakenikimsikiliza, akili ikiwa imetekwa na hayo matukio ya nyuma…nikawa
nikimsikiliza tu anavyohadithia hayo yote niliyowaelezea... Lakini baadaye
nikaja kugundua…, kuwa kila muda ulivyokuwa ukienda sauti ya mama ilikuwa
ikibadilika, ilikuwa inakuwa ndogo, yaani sauti ilikuwa kama inafifia…’akasema
‘Nikawa mara kwa mara najaribu kumchungulia, nikajua ni kiu, kwa
vile kaongea sana, basi nikainuka na kumpa maji, akanywa kidogo tu na kuendelea
kusimulia kisa hicho kama nilivyowahadithia huko nyuma…’akatulia
‘Lakini jinsi muda ulivyokwenda , na ndivyo sauti ya mama ilivyozidi
kufifia ikawa nasikia kwa shida…nikaingiwa na wasiwasi nikijua kuwa mama hali
yake sio nzuri. Na lipofika ile sehemu ambayo nesi alikuwa akifurahia kumuona
dada yake ni mja mzito, wakiwa kule kijijini, hapo nikajua mama sasa sio tatizo
la sauti, …kwani ghafla mama akanyamaza
kimya.
‘Mama vipi mbona unaonekana hupo sawa sawa…?’ nikamuuliza
Mama akatikisa kichwa, akainua mkono na kushika kichwa, alikuwa
kama kapitiwa nausingizi wa ghafla, akasema kama vile yupo usingizini,
‘Mwanangu…mwanangu..nashindwa kuongea
zaidi…nguvu inanishia, ila mwanangu usikate tamaa ya maisha..utafanikiwa tu,
nimeridhika kuwa wewe huna kosa, japokuwa ulaghai wa wake unaweza kumteka mume
asijue thamani ya mama yake, siwezi kukulaumu kwa hilo, kwani huyo mke ni
dhamana yako, umekabidhiwa na wazazi wako,…lakini mama ni mama tu…’akasema
‘Mama mimi nakupenda, …’nikasema
‘Mwanangu nafahamu kuwa kweli unanipenda sana mama yako na kweli
huna kinyongo na mimi kama mkeo anavyodai kuwa eti mimi nimewaloga…mimi niloge
damu yangu anajua wapi ulipotokea, kwanini nisingelikuua huko…kwanini
nikahangaika nilivyohangika ukiwa huna mbele wala nyuma hujui dunia ni
nini..kwanini nije kufanya hivyo sasa hivi….kwa lipi nitpata….’sauti ikawa inatoka
kwa shida
‘Mama ngoja nikupeleke hospitali…naona kama hali sio nzuri….’nikamwambia
‘Mwanangu nisikilize kwanza, maisha bila mama hakuna,…. ni nani
aliyezaliwa hewani, ndio baba yupo, aliweka mbegu kwa mama…, sasa yupo wapi,..hebu
niambie sasa hivi baba yako yupo wapi..najua akikuona sasa hivi umekuwa dume …atakukimbilia,
atakutaka ….lakini anajua wapi ulipotokea…’akawa kama anauliza
‘Mama achana na huyo baba, wala simjui na sina haja ya kumjua..’nikasema
‘Hapana..ili maisha yako yakamlike, ili upate radhi za mungu ,
jitahidi umtafute baba yako,..yule ni mzazi wako na mzizi wa mzazi haukatiki
hadi hapo atakapoingia kaburini..bado una dhamana naye..’akasema mama
‘Mama kwa hayo uliyonihadithia, hata siku moja sitaweza kupoteza
muda wangu kumtafuta, maana nikikutana naye, sijui kama nitaweza kuvumilia…tutakosana
kabisa na huenda akaniachia laana..’akasema
‘Hapana,….nikuambie kitu, baba ni baba..hata kama ananuka, …hata
kama hana kitu, kama ni baba yako umpe thamani yake kama baba…jitahidi sana
umtafute, kama yupo hai, basi jitambulishe kwake, na umpe salamu zangu..’akasema
‘Mama ina maana katika akili yako bado unamuwaza baba , mtu
aliyekufanyia hivyo…’nikasema
‘Namuwaza kwa hayo yaliyotokea..lakini nikikuangalia wewe namuona
baba yako, kwanini nisimuwaze, bila yeye labda ningekuwa na sura nyingine,
kuwepo kwako ni fahari kwangu, kama wewe umetokana na yeye, ni lazima nimuwaze,
nimshukuru mungu kuwa wewe umepatikana kupitia yeye…’akasema
‘Mama…..achana na baba…’nikasema nikionyesha kukereka na huyo baba
‘Mwanangu hilo sio ombi, ni amri, …mtafute baba yako ili baraka za
mungu zishuke kwako, utaona mabadiliko yake, ..utakuja kunikumbuka kama utafanya hivyo…’akasema na sauti ikawa kama inakata.
‘Mama ngoja nikatita usafiri, hali yako sio nzuri…’nikasema
‘Pili hakikisha unaishi na mkeo vyema, mpe mawaidaha mema ,
mwambie kuwa hata siku moja mama hawezi kumloga mwanae, tena mtoto wa tumbo lake …hizo ni dhana potofu za
kishirikina tu, kwanini mama amloge mtoto wake, ina maana analoga tumbo lako….’akasema
‘Mama hayo yamepita niachie mwenyewe …nitajua la kufanya..’nikasema
‘Mwanangu mimi nilikutafuta nikiwa sijiwezi, sijijui, sina
kumbukumbu, kumbukumbu iliyokuwa imebakia ilikuwa ni ya kwako, ya kuku-kumbuka
wewe,hebu jiulize kwanini mungu hakuiondoa hiyo kumbukumbu, sababu kubwa ni
uchungu wa uzazi…’akatulia
‘Uchungu huo anayeufahamu ni mama peke yake…unafikia kwenye kuzaa,
mtoto hutoki, unapasuliwa sehemu zako ili wewe mtoto uweze kutoka, wakati mwingine bila ganzi, unashonwa nyuzi bila
ganzi..lakini hayo maumivu ya kushonwa, huyasikii, unachosikia ni ule uchungu
wa uzazi, hebu fikiria huo utamu wake, kama ni utamu kweli….’akasema mama
‘Mwanangu sijui kwanini mkeo ananishutumu kwa uchawi….nimewaza
saan hilonakosa majibu, kama asingelikuwa amezaa ningelisema hajui uchungu wa
uzazi,lakini amezaa, labda alizaa bila shida…hata hivyo kama mke, angelijua
thamani ya mama kwa mtoto wake…
‘Hapana..mkeo anahitajia ushauri, na mawaidha makubwa, aachane na
hizo dhana potofu za kishirikina, ukiwa na dhana hizo, kamwe hutaendelea , kamwe hutakuwa na amani,..na kamwe hautakuwa na maisha mema…kiukweli…imeniuma
sana kunidhania mambo kama hayo…lakini nimemsamehe, najua hajui alitendalo….’akatulia
‘Mama basi subiri nikachukue usafiri..naona hali yako sio nzuri….’nikasema nikiwa najiuliza nitapatia wapi usafiri , maana hapo sina kitu mfukoni....lakini mama hakuniachia mkono wangu akasema
‘Ngoja niongee hayo nitakayoweza kuyaongea,…sijui kama nitaweza
kuyaongea tena, mungu mwenyewe ndiye anajua…oh, mwanangu, kweli nguvu
zimekwisha, naona muda umefika…sasa nashindwa kukusimulia mengi yaliyonikuta..nguvu
sina tena mwanangu, jitahidi, jitahidi…..’akawa anahema kwa nguvu
‘Mama usiniache mama..mama, mamaaaa..’nikajikuta nimemuinamia
mama, akainua mkono wake mwingine kwa shida akanishika kichwa
‘Mwanangu ujikaze kwa lolote litakalotokea, mimi nimeshaishi sana
inatosha, wewe bado unahitaji , maisha bado yapo mbele yako, …pambana na maisha…ukumbuke kuwa maisha ni
magumu..maisha sasa yametapeliwa na wachache, lakini usikate tamaa, fanya kila
ufanyalo ukimuweka mungu wako mbele,….mimi niliyoyafanya kwa ajili yako yanatosha…’akatulia
ma mkono uliokuwa kichwani ukadondoka.
‘Mama…’nikaita na kuushika ule mkono, ulikuwa umelegea lakini
sauti bado ilikuwa inatoka kwa shida.
‘Mwanangu sasa hivi umekuwa mkubwa, na unaweza kusimama kwa miguu
yako mwenyewe, huumwi tena.., kama mkono wangu umeweza kukishika kichwa chako
kwa wakati huu wa mwisho wa maisha yangu, basi ujue utapona, na utaneemeka,…najua
sasa hata nikiondoka leo sitajutia…ila kumbuka kitu, hakuna
kama mama, hakuna kama mama ……mwa-na-ngu…’ akanyamza kimya.
‘Mama…’nikaita,…mama akawa kimia,hatikisiki kabisa, nikajaribu
kumwangalia mapigo ya moyo, nikaona kama yamesimama…mungu wangu ina maana mama
oh haiwezekani,…hapana haiwezekani, itakuwa kazimia tu…’nikasema
‘Ukumbuke muda huo mimi mwili umekwisha mabega yamepanda juu,..naonekana kama mtoto kimwili, ila uso umekomaa, na kukunjamana kama mzee ... na
wengi walijua naumwa ugonjwa huo wa ukimwi..sina nguvu kabisa…sasa na hali kama
hiyo mama, hajiwezi, mimi mwenyewe, hata kutembea siwezi, lakini nifanyeje..
‘Nilikurupuka pale nikatoka nje, nia nimwangalie mke wangu ili
tusaidiane tumpeleke mama hospitalini, nilikuwa napepesuka, ..miguu inagongana
nilikuwa nimekonda rafiki yangu siunakumbuka ulivyoniona pale Lugalo…hapo nina mawazo
nina njaa, lakina havina maana kwa muda huo…kwahiyoo kwa hali niliyokuwa nayo hata
kumuinua mama peke yangu nisingeweza.
Nilipotoka nje nikashangaa kupo kimyaa…, hakuna cha mke wangu wala
mtoto. Nikaingia chumbani nikakutana na mshangao, …chumba kina mlango wa nyuma,
mlango huop ulikuwa wazi, mara nyingi tulikuwa hatuutumii…chumba kilikua kama
hema, hakuna kitu hata kimoja…
‘Hebu jaribu kufikiria chumba kilikuwa kina vitu vingi, kitanda,
redio yangu ambayo niliipenda sana, kabati la vyombo, kwani ilibidi tuhamishie
vitu karibu vyote kwenye chumba hicho, ili kuwepo an nafasi ya kulala mama,
…vyote vilikuwa vimebebwa.
Sikuamini kuwa tukio hilo limefanyika hapa kwangu, kwani na
umasikini wangu wote bado watu wanachukua hata kile kidogo nilicho kuwa nacho, ..sikufikiria
kuwa aliyefanya hivyo ni mke wangu…akili hapo ilikuwa haijakaa sawa,…na hata
hivyo hao watu waliwezaje kuingia humo chumbani kama sio mke wangu,…hapo sasa
nikahisi, nikajua aliyefanya hivyo bas atakuwa kashirikiana na mke wangu, sasa
mke wangu yupo wapi…sikuwa na muda huo tena..
Mimi nikawa nahangaika kutafuta mtu wa kunisaidia, kunisaidia mama
afike hospitalini, hayo mengine ni mamb ya kupita tu…hata hivyo nikawa
najiuliza hao watu a gari walifika saa ngapi, na gari lililochukua hivyo vifaa
vyangu lilikuja saa ngapi, mbona sikulisikia hata mngurumo!. Nikatoka haraka
hadi nyumba ya jirani kuulizia kama nitapata msaada, jirani yangu huyo ana
baiskeli...
‘Jamani mumesikia gari likiingia hapo kwangu ..nimeibiwa..’nikasema
huku nikishika kichwa
‘Sisi tulijua kuwa mnahama, maana kuna gari lilikuja na kusimama
mbali kidogo na hapo kwenu, na watu wakawa wanachukua vifaa hapo kwako
wanavihamshia kwenye hilo gari, huku mke wako akiwa anawasimamia …’ akaniambia
jirani yangu.
‘Oh, huyu mke wangu kama kafanya hivyo basi sio mtu ni..shetani,
lakini sasa jirani yangu, nina shida kubwa sana, naomba msaada, maana mama hali
yake sio nzuri, je mume wako yupo aniazime baiskeli?’ nikamuuliza huku nikijizuia
machozi kunitoka.
‘Mume wangu aliondoka kitambo na baiskeli yake, lakini alisema
hatakawia kurudi…ina maana mama kazidiwa sana…?’ akasema akishika simu yake
akitaka kumpigia mume wake simu na kabla hajafanya hivyo tukasikia kengele ya
baiskeli, …
‘Huyo amekuja…’ akasema yule jirani yangu mwanamama, na hapo
nikamuona mume wake akija na baiskeli, nikashukuru sana.
Alipokuja yule rafiki yangu sikupoteza muda nikamwambia hali ya
mama ni mbaya sana anisaidie baiskeli ili tumpeleke mama hospitali…Yeye bila
ubishi akaingia ndani kwake halafu akatoka na kunifuata nyumbani kwangu, na mle
ndani tulimkuta mama kalala vilevile, ina maana kazimia…sijui, au ndio
keshakufa sijui mungu wangu…!
Kwa hali kama ile, nikawa nimechanganyikiwa nahaha huku na kule…mfukoni
sina kitu, hata kama tutamfikisha hospitalini , tutaambiwa kuchangia pesa nitapatia
wapi pesa, na tutakula nini maana hata kama kulikuwa na akiba ya chochote huyo
mwanamke kasomba kila kitu….. Isingekuwa huyo rafiki yangu, sijui ingekuwaje.
Yeye alimbeba mama na kumtoa nje, na akachukua simu yake na
kumpigia jamaa mmoja mwenye bajaji, na huyu jamaa akaja haraka wakasaidiana
kumbeba mama hadi kwenye hiyo bajaji, na sisi tukaingia na kuelekea
hospitalini.
Hebu tuishia hapa kwa leo…maaana inasikitisha
WAZO LA LEO: Wazazi ni muhimu sana kwetu mama na baba,
tusiwatelekeze mama kama mama hana mfano wake, muheshimu na mtimizie mahitaji
yake yote kwa kadri ulivyojaliwa na hata siku moja usimlinganishe mama yako na
mkeo, kwani hivyo ni vyeo viwili tofauti…kwanza mama kama mumejaliwa,… mkeo
mtajitajitahidi mtajua la kufanya kwani bado mna nguvu. Lakini pia usimsahau
baba yako, ..kwani ili upatikane baba alikuwa mshirika. Mtafute na mtambue kama
baba yako.
Usijali historia za wazazi wako, hata kama ilikuwa ni historia mbaya
ya wawili hao wewe kama mtoto timiza wajibu wako kwao , muheshimu baba yako na
mpe stahiki yake.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment