Kama ulivyoona sehemu iliyopita rafiki yangu ilifikia muda alishindwa kuendelea kunihadithia kisa chake,...kina machungu mengi, ... na akaondoka, niliwasiliana naye baadaye akapanga kuja na tulikutana sehemu ile ile..nikiwa na maswali mengi kichwani, kwani kuna sehemu kubwa kama kaicha, ni kwanini..tutakuja kufahamu huko mbele, ..na je ni kwanini alishinwa kuendelea kuhadithia kisa akawa kama analia, hebu tuone sehemu hii ndogo ambayo inamtoa machozi...
*****
‘Maisha yangu na mama
yakawa ni ya kuomba omba, kuzunguka majalalani, tutakachopata ndio riziki
yetu….mama aliniambia tutanatafutwa na polisi kwahiyo hatuwezi kukaa sehemu
moja, tukawa tunabadilisha maeneo leo hapa kesho kule.., na usiku ukifika
tunatafuta sehemu salama tunalala. Kuna matukio mengi tulikutana nayo, siwezi
kuwaelezea kila kitu, ila nitawahadithia baadhi yake…’ alianza kusimulia rafiki
yangu siku alipofika tena eneo hilo.
‘Siku moja wakati tupo majalalani tukiokota makombo na masalio ya
vyakula waliyotupa matajiri, mara ghafla tukazungukwa na mgambo wa jiji. Unajua
mgombo wa jiji wapo kila mkoa, mimi kwa vile nilishazoea hizo hangarihangari
kwa kipindi hicho nikatimua mbio, na tulijua wapi pa kukutana na mama yangu
zikitokea vurugu kama hizo.
Mama yeye mara nyingi alikuwa mbishi na aliweza kupambana na watu
kama hawo, au vibaka. Ujue hata sisi tulikuwa tukipambana na vibaka,..vibaka
hao walikuwa wakija kwenye maficho yetu na kutunyan’ganya hata kile kidogo
tulichobahatika kukipata. Ndio maisha yalivyo…
Mama yangu alikuwa mlezi wa watoto watano kama mimi, kwani
hutoamini eneo hilo tuliwakuta watoto wengine wadogo , ingawaje walikuwa na
umri mkubwa kidogo ukilinganisha na mimi, lakini walikuwa watoto wadogo , na
hawakustahili kuwa mbali na wazazi wao hasa mama!
Basi mama kwa upendo wa
watoto akawa ndio mlezi wao, atakachopata kidogo tunagawana, ingawaje mama
alihakikisha kuwa mimi kwasababu ni mdogo kuliko wenzangu Napata kipa-umbele.
Ilikuwa tukiamuka asubuhi, wengine wanakwenda mabarabarani kuomba,
wengine wanazunguka kwenye majalala na mama anahakikisha usalama wetu kwa kuwa
karibu nasi na kidogo tulichopata tunakaa pamoja tunakula, kama ni pesa, mama
anapanga nini tununue. Na watoto wakawa wamemheshimu mama na kumtii kila
analosema. Mama alikuwa mkali kwa watoto watukutu, na kwahiyo adabu ilifuatwa.
Ilibidi ikifika jioni lazima maji ya kuoga, na kuhakikisha nguo
zetu zipo safi, na usafi wa jalalani unaujua, zitafuliwa na maji machafu
angalau sizipate chawa, wakati mwingine ilikuwa ni matambara tu yakusitiri
aibu, na mama ikifika jioni anayashona-shona, ili kesho tusiadhirike.
Usiku wakati mwingine unakuwa wakati wa kupigia stori, kila mmoja
anaelezea maisha yake, wapi alipotoka kitu gani alipambana nacho, hutaamini,
watoto hawa wanakumbuka walipotoka, mmoja alisema alikimbia mteso ya mama wa
kambo, baada ya mama yake kuachika, akawa anaishi na mama huyo wa kufikia.
Mwingine akasema alikimbia mateso ya baba yake mkubwa aliywakuwa
akimlea, wazazi wake walifariki akiwa mdogo akawa analelewa na baba yake
mkubwa, baba yake huyo alikuwa mkali kupita kiasi basi akaamua kukimbia…mwingine
alipotea, wakiwa safarini na wazazi wake, ilikuwa kituoni gari limesimama, yeye
akatoka nje, akajisahau, alipogeuka pale basi lilipokuwa limesimama akakuta
halipo, akawatafuta wazazi wake mpaka leo hajawaona…ilikuwa ni visa vya
kusikitisha tu. Mimi sikuwa na cha kusimulia.
Tulibahatika kupata eneo nzuri la kulala, na tulifanya hivyo baada
ya kufukuzwa maeneo ya mjini, Kwani ingawaje sikumbuki vizuri, maisha ya mjini,
ila kumbukumbu zinanijia kuwa tulikuwa tukiishi mjini kwa mara ya kwanza,
lakini maeneo ya mjini yalikuwa ya mateso, na wahuni , watu wazima omba omba
kaam sisi walikuwa wengi , kwahiyo mchana mnahangaika, lakini usiku ulikuwa
mbaya sana,kwani usiku hupambani tu na wezi bali wauza unga, wabakaji …balaa
mtindo mmoja.
Basi siku hiyo naikumbuka sana, kuliko siku zote ndio siku
tulipovamiwa na mgambo, ….nilikimbia hadi juu kidogo ambapo niliweza kuona nini
kinatokea kule chini, nikawaona wale mgombo wakitembeza kichapo, hutaamini kuwa
binadamu wale hawakuwaonea huruma binadamu wenzao, badala ya kupambana na
vibaka na wezi mitaani walikuja pale kupambana na masikini wanaotegemea makombo
na masalia ya vyakula vilivyotupwa na matajiri.
Tuliwahi kuambiwa kuwa eneo hilo linahitajika kuchukuliwa na
muwekezaji kutoka nje, kwahiyo lilitakiwa kusafishwa, kwahiyo ilitakiwa akija
hapo asione hiyo aibu ya watu kama sisi…tukaanza kufukuzwa kwa njia hiyo.
Wakazi wengi wa eneo hilo hawakukubaliana na hilo, kwani wengine
walikuwa wamejenga biashara zao pembezoni mwa barabara na wao pia walitakiwa
kuondoka, sisi tulikuwa chini kwa bondeni ambapo taka taka hutupwa bila
mpangilio, halikuwa jalala maalumu, ila watu wa maeneo hayo walikosa sehemu ya
kutupa taka wakawa wanakuja kutupa hapo.
Kumbe eneo hilo sasa linahitajika kumilikiwa …
Nikiwa sehemu ya juu, nilimuona mama kwa mbali akipambana na
mgambo mmoja, na baadaye yule mgambo alipomshindwa akawaita wenzake, wakaanza
kumpiga mama kwa kushirikiana, utafikiri wanapiga mwizi, na baadaye nikasikia
kwa mbali, wakisema kuwa mama yangu anaonekana ni mwizi kwasababu sura yake
ambayo alikuwa akiificha ilikuwa imeharibikwa kwa kupigwa kama kibaka.
‘Huyu mama kumbe anaficha sura yake iliyoharibiwa..kumbe..anaogopa
kutambulikana, ..ni kibaka huyu..piga…’nikasikia wakisema.
Wakaanza kumpiga,niliona kiatu cha mgambo kikitua kichwani kwa
mama, baada ay kupigwa mtama na kudondoka chini..kwakweli niliumia, ..nikashindwa
kuvumilia, …nikatafuta jiwe, nilikuwa na manati yangu ya kuwindia ndege
shingoni, nikaitoa,..nikatafuta sehemu yenye nafasi,..nikachukua manati yangu
nikaweka jiwe,..nikamlenga yule mgambo aliyekuwa akimkanyaga mama kwa
buti..mimi nina shabaha sana, simukosea, nilisikia kilio tu, akawa kashika
kichwa kinatoa damu.
Wenzake wakawa wanamuuliza kafanya nini, akawa kashikilia kichwa
damu zinavuja.., akawaambia kpigwa na jiwe,..sasa wakawa wanahangaika kutafuta
wapi jiwe lilipotokea, mimi nilikuwa mjanja nilishahama hapo na kuelekea sehemu
nyingine ambapo hawanioni….nikakaa hapo kwa muda, halafu nikasimama kuangalia
kinachoendelea., nilimuona mama akiwa chini, nahisi alikuwa kapoteza fahamu.
Nilipomuona kwenye ile hali, nikakumbuka kipindi tulipowasili maeneo
ya hapo kutoka mjini, … nikiwa bado bado sijazoea hangari hangar hizo za
kukimbizana na mgambo, au vibaaka…nilikuwa mchanga wa tabia hiyo…unajua eneo
hilo tulikaa kama mwaka hivi.
Ilikuwa ni usiku ambao sitaweza kuusahau kwenye akili
yangu..tulikuwa tumejibanza sehemu ambayo tunalala, kwenye chumba cha pembeni
kabisa kwenye jengo ambalo halijakamilak kujengwa, mara mlinzi wa nyumba ile ambayo ilikuwa ndio
inajengwa akaja na vijana wanne, akasema;
‘Ndio hawa…’akasema na kuondoka, hatujua ana maana gani, mara wale
mijaa wakatavumaia , mama akaanza kupambana nao. Mama alikuwa na nguvu, …
Lakini ile mijitu nayo ilikuwa na nguvu sana, walipigana na mama,
sikujua nini wanataka kutoka kwa mama, kwani kwa walivyoonekana waliweza
kutafuta mahitaji yao bila kuja kutuuibia, kwani vijisenti mama alivyopata siku
hiyo vilikuwa vya kuuza mchicha na mboga mboga. Mboga mboga hizo zilitoka
kwenye bustani mama aliyotengeneza kipindi cha mwanzoni mwa utoto wangu kabla
hatujafukuzwa hapo.
Mama mwanzoni alimua kujituma kwa kulima bustani, kabla
hajajiingiza kwenye kuomba omba..mama akawa analima na tunamwagilia mboga kwa pamoja, lakini mavuno yanachukua muda,
tunahitajika kula..kwahiyo ilibidi kufanya kazi nyingine, ..mama akawa anaomba
vijikazi vya hapa na pale..ndivyo alivyokuwa akifanya mama mwanzoni kabla
hatujafukuza kwenye hilo bonde eti lina mtu na huyo mtu analihitaji kwa kilimo
cha kisasa….na pia tulikimbia hapo baada ya tukio baya ambalo sipendi
kulihadithia…’akasema
‘Tukio gani,..tuhadithie tu bwana..’jamaaa mmoja akasema
‘Unajua maisha niliyopitia ni mabaya ..yana taabu, huzini na
matukio mengine yanaumiza sana..sikupenda kumuhadithia mtu,..nitawahadithia
hili moja tu…’akasema
‘ Basi kipindi hicho tulizoea hiyo kazi, mama analima mboga,. Kama
mchicha ukikua, tunauza mitaani tunapata
hela ya kula , na kuipikia kidogo, baadaye tunakuja kulala kwenye hilo
jumba.Jumba hilo lilikuwa na mlinzi, kilichotakiwa kufanywa ni kumlipa huyo
mlinzi kiasi fulani kwa siku ili tupate kijisitiri hapo, na kama huna kitu
huruhusiwi kulala hapo. Kwasababu nilikuwa mdogo, ikifika usiku mimi nalala
fofo, na wala sijui kinachoendelea, mama ndiye mlinzi wangu, hakiwezi kupita
kitu asiwepo macho…ole wako uniguse….
Siku moja, nilikuwa naumwa,mama akahangaika ili apate pesa ya kuniitibia,
alihangaika huko alipohangaika,….mchicha ulikuwa umekwisha na kipindi hicho
ndio tumepigwa marufuku ya kulima hilo bonde….mama akapata pesa kidogo,
akanipeleka hospitalini, nikapata dawa, tukarudi mapema kwenye lile jengo na
mlinzi yule muda kama huo haruhusu watu kama sisi kuwepo, kwani atagombezwa na
muajiri wake, na usiku anafanya kama msaada tu, kwa posho kidogo tunayompa….
Kwa siku ile kwa vile nilikuwa naumwa, hali yangu ilihitaji kutulizwa
mahali, basii mama akaongea na yule mlizi kuwa atalipa hela ya ziada mimi
nipate shemu nilale…yule mlinzi akakubali kwa ahdi ya kulipwa pesa zaidi…,
kumbe yule mlinzi alikuwa na lengo lake
kutukomoa. Hakupenda sisi tuendelee kukaa hapo.
Basi mimi nikalala pale na kwa vile nilikuwa naumwa nilishikwa na
usingizi nilipoamuka nikakuta mama amesharudi, anahangaika kutengeneza malazi ya
usiku. Na akanilisha chakula alichokuwa nacho akanipa dawa tukalala…
Ilikuwa usiku sasa, ndio hiyo mijamaa ikafika na mlinzi akasema
`ndio hawa..’ akaondoka zake, na wale mijamaa ikatuvamia…nikajua wanataka hivyo
vijisenti vya mama, nikatamani kumwambia mama awape tu, wasije wakamuua.
Wakamshika mama kwa nguvu, wakampiga, na mmoja akamkaba mama shingo nikajua
mama sasa anakufa na , mwingine akamshika miguu….’akatulia kidogo
Unajua kama nitaweza kukutana na watu wale, nikiwa na bastola
sizani kama nitaweza kuvumilia, nita….oh…’akatulia kidogo
Wale mibaba, hawakujali kuwa mama kazimia..maana walihakikisha
wamempiga, hadi kupoteza fahamu…na baadaye wakafanya walichokitaka huku
nashuhudia kwa macho yangu, na baadaye wakachukua vile vijisenti vya mama
wakaondoka navyo, na wakati wanaondoka wakaniona nimekaa pembeni nalia,
waliponiona nalia hivyo wakanizaba kibao cha nguvu nikapoteza fahamu.
Tulihama eneo hilo usiku ule ule….
************
‘Ukumbuke kumbukumbu hizo zilinijia wakati nipo pale kilimani walipofika
mgambo,….wakati nachungulia, nikihakikisha mgambo hawanioni, nia ni kuona kama
mama yupo salama…nilimuona mama akiwa kalala chini, na wakati huo mgambo
wanafukuzana na watu wengine.
Nilijua mama atakuwa kaumia sana, maana alikuwa kalala na
hatikisiki..mara nikamuona mgambo mwingine sio yule ya kwanza niliyempiga jiwe,
yule sikimuona maeneo hayo tena, huenda alikuwa kaondoka kujitibia jeraha..huyu
sasa alikuwa mgambo mwingine .
Nikawa cha kufanya kama atampiga mama…nikawa nasubiria, sikujua
nichukue hatua gani kumsaidia mama, ..yule mgambo akawa anamsogelea mama, pale
alipolala, akamkanga mama mgongoni, maana mama alilala kifudi fudi..alipoona
mama hainuki, akawa anamvuta mama juu akiwa kashikilia nguo za mama…nguo za
mama zilikuwa ni kuuu kuu..zikawa zinachanika.
Mama akawa kabakia wazi mgoni, ..yule mgambao akainama na kumgeuza
mama, nahisi alijua kafariki, …akawa anazidi kuzivta nguo za mama…mama akawa
sasa karibu nusu uchi…wakati ule watu wengi walikuwa upande mwingine. Nikasikia
akimuita mgambo mwenzake.
Yule mgamabo..akawa anamkokota mama sehemu ya chini kidogo,
asipoonekana, nikajua ni yale yale ya wale mibaba..sikuvumilia, haraka
nikatafuta kigogo…, nikashuka mbio nikiwa nimeshika kigogo, kwasababu nilikuwa
mtoto, mgambo wengine hawakuweza kunijali, wakijua nakimbia tu huku na kule…
Nikafika karibu na pale aliposimama mgambo, yule mgambo bado
alikuwa akihangaiak na mama, … akimburuza mama kama mzoga, na nikajua huenda mama
ameshafariki,…alipofika ufichoni nikaona akimvuta mama nguo zilizobakia,
sikuweza kuvumilia, mimi nilitumia nguvu zangu zote nikakirusha kile kigogo
nilichokuwa nacho…, nilitumia nguvu zangu
zote, na kweli kilikwenda na kutua kwenye kichwa cha yule mgambo.
Kwa wakati ule gari la jiji la kuwasomba wote waliokamatwa pale
lilishawasili kwahiyo ilie vuruguvurugu na watu kupambana na mgambo, huyu
mgambo hakuona hicho kigogo kimetoka wapi. Kilimgonga yule mgambo bara bara
kichwani, na kweli kilifanya kazi yake, yule mgambo akadondoka chini..nahisi
alipoteza fahamu, kwani lidondoka chini akawa kimia..mimi nikakimbia hadi pale
alipolala mama, nikamtiskisa
‘Mama amuka tukimbie…mama..mama…’nikaona mama yupo kimia,
nikakumbuka kitu nikageuka huku na kule nikaona chupa yenye maji, sikujali ni
chupa ya nini, nikasogea hadi pale alipo mama nikamwagia yale maji kichwani na
mara maam akazindukana
Mama alipofumbua macho tu na kuniona mimi, na alipogeuka na kuona
yule mgambo kalala chini nay eye yupo kwenye ile hali, haraka akanishika mkono
tukaanza kukimbia..tulikimbia, hadi pumzi zikatuishia, tukawa tupo mbali kabisa
na eneo hilo, na mama akasema tupumzike….
Ikabidi tuhame eneo hilo mama tulipata taarifa kuwa polisi na
mgambo wanatutafuta kwa kuwaumiza walinzi …
NB: Haya tumeona tukio hilo
kidogo, tutaona tukio jingine kabla ya kuhitimisha kisa chetu, au mnasemaje..?
WAZO LA LEO: Binadamu ana stara yake hata kama
hajitambui tunahitajika kuiheshimu stara hiyo, kuna watu wana majukumu ya
kikazi kama vile walinzi, mgambo hata polisi, ni kweli tunapowajibika
hatutakiwi kuangalai huyu ni nani, amri ikitolewa ni amri moja…piga ua, kama
tunavyoona. Lakini sio lazima kufanya hivyo wakati wote, tukipewa amri
tunatakiwa pia tujue jinsi gani ya kuitekeleza, tuheshimu sheria, kwani sisi
ndio walinzi wa sheria, kuna walinzi hawajui hilo, na wanafanya kazi hizo kama
kukomoa, au kwa matakwa na utashi wao,…huu sio uungwana kabisa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment