Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 6, 2015

NANI KAMA MAMA-72


‘Ina maana shemeji ulikuwa ukimfahamu huyo mama kabla…na huenda unajua kwanini aliharibika huo uso, kuacha hilo la kukatwa katwa na mapanga, au wewe ulivyomuona huo uso uliharibiwaje…’ akauliza docta.

‘Aliharibikaje huo uso hahaha, waniuliza hilo swali hiyo ndio adhabu ya msaliti, na jinsi gani alivyoharibiwa mimi sijui,  nitajuaje mimi yake…aliharibiwaje, haaa, acheni nyie…!’ akawa anarudia rudia hilo swali.

‘Kwasababu inavyoonyesha mnafahamiana au sio, na labda mlikuwa mnawasiliana…’akasema docta na nesi akawa anachungulia mlango aliolala dada yake kwa mashaka.

‘Mimi kuharibika kwake huo uso hakunihusu na kwanini nimuulize,na kwanini niwasiliane naye wakati alishanisaliti…?’ akawaangalia nesi docta na mlinzi kwa zamu.

‘Kwahiyo mlikuwa mnajuana kabla ya kukusaliti, mlikuwa mnajuana vipi…?’ akauliza docta

 ‘Ndio tulikuwa tunafahamiana sana…, namjua sana kipindi akiwa msichana, namjua toka utotoni, namfahamu mpaka ndani ya moyo wangu ….hadi siku ile aliponisaliti, ndio ukawa mwisho wetu wa kufahamiana, ….’akasema

‘Alikuwa mke wako, au mpenzi wako..?’ akauliza docta

‘Alikuwa mchumba wangu…’ alapotamka hapo kila mtu aliguna, nesi aliyekuwa anashangaa, akataka kusimama

Tuendelee na kisa chetu


*************

‘Ndio alikuwa mchumba wangu…’akasema shemeji mtu, na nesi akataka kusimama, lakini akasita, akasema;
‘Shemeji dada analifahamu hilo, maana….’akasita kuendelea kuongea na shemeji yake akatabsamu kidogo halafu akarudisha uso wake kwenye ile hali ya huzuni, chuki….na kusema;

‘Nimeshamsimulia dada yako, usiwe na wasiwasi, dada yako ..analifahamu hilo..’shemeji yake akasema na hapo nesi akapata amani

‘Hebu tuambie japo kwa ufupi mlijuanaje na huyo mwanamke na ikatokea hivyo, kama ulivyosema kusalitiana…na mwisho wake ukawa hivyo, mwenzako kuharibiwa sura…kiukweli mimi mwenyewe sijamuona hiyo sura, aliyewahi kuiona hiyo sura ni docta mwenzangu na yeye hakutaka kuniambia zaidi…’akasema docta.

‘Sikutaka kuyaongea haya mambo maana yalishapita, na nilishasahau  ..japokuwa mwenye kovu usione kapoa…linaweza likawa na maumivu ndani kwa ndani…..sikutegemea ..baada ya hilo tukio kuwa tutakuja kukutana tena na huyu mwanamke..sikutegemea kabisa, kwangu alishakuwa mfu….’akasema akitikisa kichwa

‘Oh, …’akaguna nesi

‘Huyo mwanamke alikuwa mchumba wangu, urafiki kutokea mbali kabisa na kila mtu pale kijijini alijua hivyo,…oh, sitaki kuayakumbuka hayo,….maana kama angelitunza ahadi yetu ya toka utotoni,…fikiria kutoka utoto, tupo mimi na yeye, hatuji ni nini maana ya mapenzi, ..’akatulia

‘Tulikuwa tunajuana tu kama marafiki, kaka na dada..unaona..tukakuua na kuanza kujua ni nini maana ya rafiki, ..tukaja kujua ni nini maana ya mapenzi….tunajitahidi kutunza sheria, na mila..kuwa mpaka tuoane, au sio….inafikia sehemu tonge lipo mdomoni,…haaaa,….unajua nawaza mbali kuwa kama angelitunza kiapo chetu, basi muda kama huu tungelikuwa hapa pamoja,..mke na mume…’akatulia

‘Lakini yote ni heri, nisije kukufuru, maana kama isingelikuwa hivyo nisingelimpata mke anayenipenda kwa moyo wake..asiyejali hali yangu…’akatulia

‘Umeona eeh…shemeji yangu,….mimi nakupenda zaidi ya huyo mwanamke wako, unaumia nini..’akamtania nesi

‘Mhh..kweli nimeona..na kweli natakiwa nikubali kuwa yote hupangwa na mungu, kwani kwa kunisaliti kwake nilikuja kumpata mke wangu huyu ninayeishi naye sasa. Na pendo analonipa mke wangu huyu sasa, sijui kama huyo mwanamke angeliweza ….sijui. …’ akasema huku akitikisa kichwa na usoni kulionekana ukungu wa huzuni.

‘Kwahiyo basi haitakiwi kumchukia huyo mama, ..inatakiwa umshukuru au sio…umsamehe, kwani kutokana na hilo tukio umempata chagua lako …au sio?’ akauliza docta.

‘Jamani niwaulize swali,…. kati yenu kuna mtu aliwahi kuachwa solemba siku ya ndoa yake, siku ambayo unasubiri, mfungishwe ndoa, halafu mwenzako hakutokea…?’ akawa kama anauliza na wote wakawa wanaangaliana bila kusema kitu.

‘Kama hakuna aliyewahi kufanyiwa dhuluma hiyo, basi hamuwezi kujua uchungu gani niliupata siku hiyo, hata niwasimulie vipi hamtanielewaa…’akatulia kidogo

‘Unajua katika maisha yangu sikutegemea kabis akuwa na mimi itakuja kunifikia hivyo, niliwahi kuwacheka wale wanaofikia hadi kujiua..lakini iliponifika mimi, huenda kama isingelikuwa mawaidha ya watu ningelishajiua…’akahema kama vile anatua mzigo mkubwa moyoni mwake.

‘Ujiue…kwanini, na wanawake wapo kibao..hahaha mimi siwezi ….’akasema mlinzi akionyesha kushangaa, na shemeji hakujali hayo maneno akaendelea kuongea;

‘Na kama nisingekutana na huyu mke wangu, sidhani kama ningekuwa nimeoa tena, kwani nilishawachukia wanawake wote, nikaona wanawake wote ni wasaliti, sikutaka tena kitu kinachoitwa mapenzi,..’akatikisa kichwa kama kukubali

‘Mhh….lakini ya mungu mengi, namshukuru mungu, kumbe yote ni kwa mapenzi yake, na unaweza ukachukia saana jambo, kwa shari zake, kwa dhuluma zake, lakini kumbe kwenye hiyo shari, kwenye hiyo dhuluma ndiko kwenye njia ya kupata heri….sasa nimeamini hilo kwa ushahidi..nsmshukuru sana mungu.’ akanyosha mikono juu, kama mtu anayeomba.

‘Ina maana baada ya kukusaliti hamkuwahi kukutana tena na huyo mama…?’ akauliza docta

‘Hatukuwahi kukutana tena…wewe ningekutana na mke wa tajiri, haaah, wewe ..sijitakii mema…mke wa tajiri analindwa, ana walinzi….hahaha…ungewahi kuwepo enzi za huyo tajiri ungelijua nasema nini….tajiri wa ng’ombe..’akatulia

‘Kwahiyo hukuhangaika kumuulizia ..kujua sababu yake ni nini..?’ akauliza docta

‘Sikumuuliza ilitokeaje , nitaka kufanya hivyo, lakini sikupewa nafasi,…nilisubiri kuwa atatokea kuja kuniambia sababu ni nini, lakini hakuna..nilichopata ni barua yake na ujumbe kuwa yeye sasa ni mke wa mtu..’akatulia na mchoni kulionekana kama kunataka kutoa machozi.

‘Lakini….’nesi akataka kusema neno, lakini shemeji yake akamkatiza na kusema;

‘Mke wa tajiri, hahaha…mke wa tajiri, aje kuolewa na mimi masikini khaaa, sasa kipo wapi….’akawa kama anajiangalia.

‘Na….alipokuja akakutambua, mkatambuana…ndio akakupigia magoti na kukuomba msamaha…..au sio..?’ akauliza mlinzi , na shemeji akamuangalia huyo mlinzi kwa muda bila kusema neno, halafu akasema;

‘Yah…ndio… alipotokea muda huu, eti ndio ananipigia magoti , kuniomba msahamaha, eti ananiambia yeye hakufika siku ile ya ndoa yetu kwasababu ya wazazi wake, eti wazazi wake walikuwa wakidaiwa na huyo mume aliyemuoa..’akasema

‘Lakini si kweli..?’ akaulizwa

‘Mawasiliano bhana..kwanini hakuja au kutafuta namna ya kuniambia....na tulishapanga jinsi gani ya kutoroka,..na ingeliwezekana , tungelifunga ndoa na hayo anayodai kuwa yneglitokea, yasingelitokea,….huyo tajiri pamoja na ubabe wake, asingelwieweza kushindana na sheria…huyo mwanamke alikusudia bhana…wewe unawajua hawa watu wewe…’akasema akimuonyeshea kidole nesi, na nesi akacheka

‘Lakini  huwezi kujua kwanini yeye alifanya hivyo, unajua….’akasema nesi

‘Hahahaha…wewe ngoja siku ikutokee utajua kwanini nasema hivyo…’akasema na nesi kabla hajasema neno yeye akasema;

‘Eti ilikuwa aolewe au wazazi wake wawe watumwa wa huyo jamaa. Yaani wamtumikie huyo jamaa kwa kazi zake mpaka atakapokubali kuwa deni limekwisha na pia wanyang’anywe eneo lote ikiwemo kibanda walichokuwa wakiishi wazazi wake….ndivyo alivyoniambia hivyo, sijui kama ni kweli , na hata kama ni kweli,..hivi kweli mtu angelifikia kuwafanyia hivyo wazee wale…hapana sikubali..’akasema

‘Shemeji yawezekana, unajua watu walivyo hasa wakiwa na utajiri, wanajiamini kupita kiasi, wanakula na wakubwa, wanaogopa nini, wengine hufikia kujiona wapo juu ya sheria…wapo…hasa huko kijijini….’akasema nesi.

‘Lakini alikuwa wapi muda wote ule niliosubiria, nilioteseka hadi kutaka kujiua…alipoanza kunisimulia ..sikutaka kusikia kauli yake, lakini aliniambia kwa haraka haraka,..na nikaona nimpe neno lake, nikamwambia hivi kuwa hilo lilitokea kama tishio tu kumpima imani yake kupima upendo wake kwangu…’akatulia

‘Ila hakutaka kujisumbua ili ampate mume tajiri, ili wazazi wake waneemeke na huo utajiri…, nilipomwambia hivyo akaanza kulia na kuomba msamaha, lakini sikuwa na muda huo tena,  sikutaka hata kumsikiliza msamaha wake…una maana gani kwangu, ili iweje, kwa vile keshaharibiwa sura, anajua kuwa hana thamani tena au….’.akasema

‘Inabidi umsamehe tu shemeji yangu….yeye lengo lake ni msamaha, sio vinginevyo, anajua kweli alikukosea,..japokuwa hukuwahi kufuatilia kujua undani wake, nay eye kakuambia kilichomsibu, yeye ni mtoto wa kike, yupo mikononi mwa wazazi wake,….angelifanya nini…’akasema nesi

‘Kwani kuna nini tena, mbona mimi nilishamsamehe..siku nilipofunga ndoa na dada yako nikawa nimeshamsamehe, na kumshukuru mungu…ila kwanini bado anifuate fuate….’akasema

‘Kwani sasa kaenda wapi..?’ akauliza mlinzi

‘Alipoona simsikilizi akawa mbogo na kuanza kudai mtoto wake, na hapo kwa hasira ndipo nilipokivuta kile kitambaa alichokuwa kajifunga usoni, ili nione anaficha nini cha zaidi,..sikujali hivyo vitisho vyake tena..khaaa, kumbe, kumbe alikuwa akificha aibu yake, adhabu aliyoipta na sio kama tulivyokuwa tukifikiria kuwa huenda ni kutokana na imani yake..hahaha’akasema akicheka kwa dharau lakini usoni kulionekana kuwa hacheki kwa furaha.

‘Hujulai vitisho vyake, vitisho gani..?’ akauliza mlinzi, na shemeji mtu hakujibu hilo swali akaendelea kuongea.

‘Ingawaje nilishamuona kabla, siku ile alipotaka kuungua, lakini sikumuona kwa uwazi zaidi, …na sikuwa na uhakika kuwa kweli ndio yeye,ila sasa, nilipomuona sasa, nikamtambua na yeye akanikumbuka....oh, huyo uliyemfanyia hivyo hapana alizidi mpaka….’akatulia akionyesha uso wa huzuni.

‘Ina maana hayo majeraha sio ya mapanga tu  , kulikuwa na majeraha mengine…?’ akaulizwa

‘Kwakweli nilivyomuona kwa uwazi zaidi hata mimi niliishiwa nguvu. Huruma iliniingia, nikabaki nimeduwaa, ….kwakweli kama ndio huyo mwanaume wake alimfanyia hivyo, basi huyo mwanaume ni mnyama, …kuna michiri mingi ya kabla…kama mtu alikuwa na waya wa sng’eng’enga akamkwaruza….vibaya vibaya….’akatulia

‘Mhh...ndipo hapo mke naye akamuona, na sikuweza kumuangalia zaidi, kwani mke wangu alidondoka, na ikatokea kama nilivyowaambia, kwahiyo, jamani mtoto huyo mpelekeni kwa mwenyewe, mtoto huyo mpelekeni kwa mama yake ni haki yake,….’ Akasema kwa msisitizo huku akionyeshea mlangoni.

‘Lakini shemeji kuna uhakika gani kuwa huyu mtoto ni wake?’ akauliza nesi

‘Kuna uhakika gani…!?’ akauliza shemeji mtu kwa kauli kama ya dhihaka na wote wakamuangalia kwa mshangao.

‘Mlishawahi kumchunguza huyo mtoto vyema..?’ akauliza akiwaangalia kila mmoja kwa zamu

‘Si ndio huyu tumekuja naye…tumchunguze kwa vipi tena….’akasema nesi

‘Oh, kama mumemchunguza vyema,… japokuwa …sijui kwanini, muda wote niliowahi kuishi na huyo mtoto, sikuwahi kujiwa nahilo wazo,..kabisa..lakini huyo mtoto na mama yake wanafanana, hubahatishi….’akasema

‘Hata akiwa kalala, sura ya huyo mtoto na wazazi wake haifichiki, macho ya huyo mtoto ni kama ya mama yake…’ akasema na hapo akasimama

‘Macho?’ akauliza nesi huku akifikiria kitu.

‘Macho…, ndio macho yake, …kama kuna kitu nilichokuwa nikimempendea zaidi huyo mwanamke ilikuwa ni macho yake..’akasema na kutabasamu.

‘Mhh, kumbe….’akasema nesi akikumbuka kitu.

‘Mwanamke huyo alijaliwa urembo, enzi za usiachana wake weeeeh,  na macho yake yalikuwa na mvuto,ni yale macho ya buluu, ya kipekee kama ya mzungu,  sijui nikuelezeje, kama mumemkagua huyo mtoto wake mtajua macho yake yalikuwaje.., sasa yake yalikuwa na urembo wa kike, si unajua wanawake macho yao yalivyo..eehe’akatulia kidogo kama anaonyeshea ili watu wamuelewe.

‘Lakini sasa nayaona kama ya shetani…mchawi….hahaha, ndio maana hata watu wakakimbilia kumuita mchawi, je wangeliona hayo macho yake sijui inaglikuwaje, hahaha…..’ akasema na kukatiza kauli yake ghafla na kugeuza kichwa upande wa mlango wa chumbani.

Alikatiza kauli yake, kwani mlango wa chumbani ulifungulia, na aliyejitokeza pale mlangoni alikuwa mke wake akiwa kajifunga khanga mbili, akionyesha kuchoka…. Nesi naye akageuka kumuangalia dada yake, huku akiandaa kusimama, lakini akashikwa na butwaa,  na kabla hawajasema kitu, mke mtu huyo akawa wa kwanza kuongea , akasema;.

‘Mume wangu kwanini unamtusi mama wa watu, ulisikia kabisa kuwa sio kosa lake, hebu jiweke wewe kwenye nafasi yake, ungelifanyaje, uchague mume uwatelekeze wazazi wako,unaweza kweli kufanya hivyo?’ akauliza mke wake, na mume wake akabakia kimia.

‘Fikiria sana, hali ya kule kijijini kwenu ilivyo, na huyo mwanaume, ambaye umekiri mwenyewe kuwa huyo mwanaume alikuwa akiogopewa,  watu wa huko kijijini kwenu walikuwa wakimuogopa sana.., ulisema mwenyewe kuwa alikuwa tishio, ulitaka wazazi wa watu wawe watumwa…hapana, hata ingelikuwa mimi nahisi ningelifanya hivyohivyo…’ akasema mkewe

‘Najua wanawake mnachojali ni mali, najua kabisa ungelifanya hivyo hivyo au sio, ili upate mali, au sio, mbona upo na mimi…ndio najua kwenu wanawake wanajali sana mali , mali kwao ni bora kuliko mapenzi au sio mke wangu…, sawa, lakini tafadhali …tafadhali, nimekuambia ulale,…..kalale usije kuniletea balaa jingine, kwani huku umefuta nini?’ akasema huku anamfuata mkewe  pale aliposimama.

Nesi ambaye alikuwa kashikwa na butwaa, akimwangalia dada yake, akawa kama kagandishwa, nusu kukaa na nusu kusimama, akawa sasa anainuka taratibu huku haamini nini anachokiona. …haamini macho yake…

NB: Twende kidogo kidogo kidogo tutafika tu, tunakimbizana na salio.


WAZO LA LEO: Ni kweli kutendewa ubaya kunauma sana, hasa kusalitiwa, ni kweli kudhulumia, kunyimwa haki yako, kunauma na kunatesa sana, lakini tukumbuke kuwa mpaji ni mungu, mtoa riziki ni mungu, na hayo anayafahamu vyema kuliko utashi wa nafsi zetu. Muhimu, yakitotokea hayo, mitihani ya maisha kudhulimiwa kusalitiwa, tukajitahidi kadri ya uwezo wetu kudai haki,..kusubiria na juhudi za kila namna, ni lazima tufanye juhudi sio kukaa tu na kulia…na bado ikashindikana, iliyobaki nini…tumkabidhi mungu,yeye anajua nini la kufanya….wangapi wangapi walifanya hivyo na sasa wapo wapi…

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hi there! This is my first comment here so I just wanted to give a quick shout out and say I genuinely enjoy reading your articles.
Can you suggest any other blogs/websites/forums that deal with the same subjects?
Thank you so much!

Also visit my site - Android 3D Puzzle Game