‘Ina maana shemeji ulikuwa ukimfahamu huyo
mama kabla…na huenda unajua kwanini aliharibika huo uso, kuacha hilo la kukatwa
katwa na mapanga, au wewe ulivyomuona huo uso uliharibiwaje…’ akauliza docta.
‘Aliharibikaje huo uso hahaha, waniuliza
hilo swali hiyo ndio adhabu ya msaliti, na jinsi gani alivyoharibiwa mimi
sijui, nitajuaje mimi yake…aliharibiwaje,
haaa, acheni nyie…!’ akawa anarudia rudia hilo swali.
‘Kwasababu inavyoonyesha mnafahamiana au
sio, na labda mlikuwa mnawasiliana…’akasema docta na nesi akawa anachungulia
mlango aliolala dada yake kwa mashaka.
‘Mimi kuharibika kwake huo uso hakunihusu
na kwanini nimuulize,na kwanini niwasiliane naye wakati alishanisaliti…?’ akawaangalia
nesi docta na mlinzi kwa zamu.
‘Kwahiyo mlikuwa mnajuana kabla ya
kukusaliti, mlikuwa mnajuana vipi…?’ akauliza docta
‘Ndio tulikuwa tunafahamiana sana…, namjua
sana kipindi akiwa msichana, namjua toka utotoni, namfahamu mpaka ndani ya moyo
wangu ….hadi siku ile aliponisaliti, ndio ukawa mwisho wetu wa kufahamiana, ….’akasema
‘Alikuwa mke wako, au mpenzi wako..?’
akauliza docta
‘Alikuwa mchumba wangu…’ alapotamka hapo
kila mtu aliguna, nesi aliyekuwa anashangaa, akataka kusimama
Tuendelee na kisa chetu
*************
‘Ndio alikuwa mchumba wangu…’akasema shemeji mtu, na nesi akataka
kusimama, lakini akasita, akasema;
‘Shemeji dada analifahamu hilo, maana….’akasita kuendelea kuongea
na shemeji yake akatabsamu kidogo halafu akarudisha uso wake kwenye ile hali ya
huzuni, chuki….na kusema;
‘Nimeshamsimulia dada yako, usiwe na wasiwasi, dada yako ..analifahamu
hilo..’shemeji yake akasema na hapo nesi akapata amani
‘Hebu tuambie japo kwa ufupi mlijuanaje na huyo mwanamke na
ikatokea hivyo, kama ulivyosema kusalitiana…na mwisho wake ukawa hivyo, mwenzako
kuharibiwa sura…kiukweli mimi mwenyewe sijamuona hiyo sura, aliyewahi kuiona
hiyo sura ni docta mwenzangu na yeye hakutaka kuniambia zaidi…’akasema docta.
‘Sikutaka kuyaongea haya mambo maana yalishapita, na
nilishasahau ..japokuwa mwenye kovu
usione kapoa…linaweza likawa na maumivu ndani kwa ndani…..sikutegemea ..baada
ya hilo tukio kuwa tutakuja kukutana tena na huyu mwanamke..sikutegemea kabisa,
kwangu alishakuwa mfu….’akasema akitikisa kichwa
‘Oh, …’akaguna nesi
‘Huyo mwanamke alikuwa mchumba wangu, urafiki kutokea mbali kabisa
na kila mtu pale kijijini alijua hivyo,…oh, sitaki kuayakumbuka hayo,….maana kama
angelitunza ahadi yetu ya toka utotoni,…fikiria kutoka utoto, tupo mimi na
yeye, hatuji ni nini maana ya mapenzi, ..’akatulia
‘Tulikuwa tunajuana tu kama marafiki, kaka na dada..unaona..tukakuua
na kuanza kujua ni nini maana ya rafiki, ..tukaja kujua ni nini maana ya
mapenzi….tunajitahidi kutunza sheria, na mila..kuwa mpaka tuoane, au sio….inafikia
sehemu tonge lipo mdomoni,…haaaa,….unajua nawaza mbali kuwa kama angelitunza
kiapo chetu, basi muda kama huu tungelikuwa hapa pamoja,..mke na mume…’akatulia
‘Lakini yote ni heri, nisije kukufuru, maana kama isingelikuwa
hivyo nisingelimpata mke anayenipenda kwa moyo wake..asiyejali hali yangu…’akatulia
‘Umeona eeh…shemeji yangu,….mimi nakupenda zaidi ya huyo mwanamke
wako, unaumia nini..’akamtania nesi
‘Mhh..kweli nimeona..na kweli natakiwa nikubali kuwa yote hupangwa
na mungu, kwani kwa kunisaliti kwake nilikuja kumpata mke wangu huyu ninayeishi
naye sasa. Na pendo analonipa mke wangu huyu sasa, sijui kama huyo mwanamke
angeliweza ….sijui. …’ akasema huku akitikisa kichwa na usoni kulionekana
ukungu wa huzuni.
‘Kwahiyo basi haitakiwi kumchukia huyo mama, ..inatakiwa umshukuru
au sio…umsamehe, kwani kutokana na hilo tukio umempata chagua lako …au sio?’
akauliza docta.
‘Jamani niwaulize swali,…. kati yenu kuna mtu aliwahi kuachwa
solemba siku ya ndoa yake, siku ambayo unasubiri, mfungishwe ndoa, halafu
mwenzako hakutokea…?’ akawa kama anauliza na wote wakawa wanaangaliana bila
kusema kitu.
‘Kama hakuna aliyewahi kufanyiwa dhuluma hiyo, basi hamuwezi kujua
uchungu gani niliupata siku hiyo, hata niwasimulie vipi hamtanielewaa…’akatulia
kidogo
‘Unajua katika maisha yangu sikutegemea kabis akuwa na mimi
itakuja kunifikia hivyo, niliwahi kuwacheka wale wanaofikia hadi kujiua..lakini
iliponifika mimi, huenda kama isingelikuwa mawaidha ya watu ningelishajiua…’akahema
kama vile anatua mzigo mkubwa moyoni mwake.
‘Ujiue…kwanini, na wanawake wapo kibao..hahaha mimi siwezi ….’akasema
mlinzi akionyesha kushangaa, na shemeji hakujali hayo maneno akaendelea
kuongea;
‘Na kama nisingekutana na huyu mke wangu, sidhani kama ningekuwa
nimeoa tena, kwani nilishawachukia wanawake wote, nikaona wanawake wote ni
wasaliti, sikutaka tena kitu kinachoitwa mapenzi,..’akatikisa kichwa kama
kukubali
‘Mhh….lakini ya mungu mengi, namshukuru mungu, kumbe yote ni kwa
mapenzi yake, na unaweza ukachukia saana jambo, kwa shari zake, kwa dhuluma zake,
lakini kumbe kwenye hiyo shari, kwenye hiyo dhuluma ndiko kwenye njia ya kupata
heri….sasa nimeamini hilo kwa ushahidi..nsmshukuru sana mungu.’ akanyosha
mikono juu, kama mtu anayeomba.
‘Ina maana baada ya kukusaliti hamkuwahi kukutana tena na huyo
mama…?’ akauliza docta
‘Hatukuwahi kukutana tena…wewe ningekutana na mke wa tajiri, haaah,
wewe ..sijitakii mema…mke wa tajiri analindwa, ana walinzi….hahaha…ungewahi
kuwepo enzi za huyo tajiri ungelijua nasema nini….tajiri wa ng’ombe..’akatulia
‘Kwahiyo hukuhangaika kumuulizia ..kujua sababu yake ni nini..?’
akauliza docta
‘Sikumuuliza ilitokeaje , nitaka kufanya hivyo, lakini sikupewa
nafasi,…nilisubiri kuwa atatokea kuja kuniambia sababu ni nini, lakini
hakuna..nilichopata ni barua yake na ujumbe kuwa yeye sasa ni mke wa mtu..’akatulia
na mchoni kulionekana kama kunataka kutoa machozi.
‘Lakini….’nesi akataka kusema neno, lakini shemeji yake akamkatiza
na kusema;
‘Mke wa tajiri, hahaha…mke wa tajiri, aje kuolewa na mimi masikini
khaaa, sasa kipo wapi….’akawa kama anajiangalia.
‘Na….alipokuja akakutambua, mkatambuana…ndio akakupigia magoti na
kukuomba msamaha…..au sio..?’ akauliza mlinzi , na shemeji akamuangalia huyo
mlinzi kwa muda bila kusema neno, halafu akasema;
‘Yah…ndio… alipotokea muda huu, eti ndio ananipigia magoti ,
kuniomba msahamaha, eti ananiambia yeye hakufika siku ile ya ndoa yetu
kwasababu ya wazazi wake, eti wazazi wake walikuwa wakidaiwa na huyo mume
aliyemuoa..’akasema
‘Lakini si kweli..?’ akaulizwa
‘Mawasiliano bhana..kwanini hakuja au kutafuta namna ya
kuniambia....na tulishapanga jinsi gani ya kutoroka,..na ingeliwezekana ,
tungelifunga ndoa na hayo anayodai kuwa yneglitokea, yasingelitokea,….huyo
tajiri pamoja na ubabe wake, asingelwieweza kushindana na sheria…huyo mwanamke alikusudia
bhana…wewe unawajua hawa watu wewe…’akasema akimuonyeshea kidole nesi, na nesi
akacheka
‘Lakini huwezi kujua
kwanini yeye alifanya hivyo, unajua….’akasema nesi
‘Hahahaha…wewe ngoja siku ikutokee utajua kwanini nasema hivyo…’akasema
na nesi kabla hajasema neno yeye akasema;
‘Eti ilikuwa aolewe au wazazi wake wawe watumwa wa huyo jamaa.
Yaani wamtumikie huyo jamaa kwa kazi zake mpaka atakapokubali kuwa deni
limekwisha na pia wanyang’anywe eneo lote ikiwemo kibanda walichokuwa wakiishi
wazazi wake….ndivyo alivyoniambia hivyo, sijui kama ni kweli , na hata kama ni
kweli,..hivi kweli mtu angelifikia kuwafanyia hivyo wazee wale…hapana sikubali..’akasema
‘Shemeji yawezekana, unajua watu walivyo hasa wakiwa na utajiri,
wanajiamini kupita kiasi, wanakula na wakubwa, wanaogopa nini, wengine hufikia
kujiona wapo juu ya sheria…wapo…hasa huko kijijini….’akasema nesi.
‘Lakini alikuwa wapi muda wote ule niliosubiria, nilioteseka hadi kutaka
kujiua…alipoanza kunisimulia ..sikutaka kusikia kauli yake, lakini aliniambia
kwa haraka haraka,..na nikaona nimpe neno lake, nikamwambia hivi kuwa hilo
lilitokea kama tishio tu kumpima imani yake kupima upendo wake kwangu…’akatulia
‘Ila hakutaka kujisumbua ili ampate mume tajiri, ili wazazi wake
waneemeke na huo utajiri…, nilipomwambia hivyo akaanza kulia na kuomba msamaha,
lakini sikuwa na muda huo tena, sikutaka
hata kumsikiliza msamaha wake…una maana gani kwangu, ili iweje, kwa vile
keshaharibiwa sura, anajua kuwa hana thamani tena au….’.akasema
‘Inabidi umsamehe tu shemeji yangu….yeye lengo lake ni msamaha,
sio vinginevyo, anajua kweli alikukosea,..japokuwa hukuwahi kufuatilia kujua
undani wake, nay eye kakuambia kilichomsibu, yeye ni mtoto wa kike, yupo
mikononi mwa wazazi wake,….angelifanya nini…’akasema nesi
‘Kwani kuna nini tena, mbona mimi nilishamsamehe..siku nilipofunga
ndoa na dada yako nikawa nimeshamsamehe, na kumshukuru mungu…ila kwanini bado
anifuate fuate….’akasema
‘Kwani sasa kaenda wapi..?’ akauliza mlinzi
‘Alipoona simsikilizi akawa mbogo na kuanza kudai mtoto wake, na
hapo kwa hasira ndipo nilipokivuta kile kitambaa alichokuwa kajifunga usoni,
ili nione anaficha nini cha zaidi,..sikujali hivyo vitisho vyake tena..khaaa,
kumbe, kumbe alikuwa akificha aibu yake, adhabu aliyoipta na sio kama
tulivyokuwa tukifikiria kuwa huenda ni kutokana na imani yake..hahaha’akasema
akicheka kwa dharau lakini usoni kulionekana kuwa hacheki kwa furaha.
‘Hujulai vitisho vyake, vitisho gani..?’ akauliza mlinzi, na
shemeji mtu hakujibu hilo swali akaendelea kuongea.
‘Ingawaje nilishamuona kabla, siku ile alipotaka kuungua, lakini
sikumuona kwa uwazi zaidi, …na sikuwa na uhakika kuwa kweli ndio yeye,ila sasa,
nilipomuona sasa, nikamtambua na yeye akanikumbuka....oh, huyo uliyemfanyia
hivyo hapana alizidi mpaka….’akatulia akionyesha uso wa huzuni.
‘Ina maana hayo majeraha sio ya mapanga tu , kulikuwa na majeraha mengine…?’ akaulizwa
‘Kwakweli nilivyomuona kwa uwazi zaidi hata mimi niliishiwa nguvu.
Huruma iliniingia, nikabaki nimeduwaa, ….kwakweli kama ndio huyo mwanaume wake
alimfanyia hivyo, basi huyo mwanaume ni mnyama, …kuna michiri mingi ya kabla…kama
mtu alikuwa na waya wa sng’eng’enga akamkwaruza….vibaya vibaya….’akatulia
‘Mhh...ndipo hapo mke naye akamuona, na sikuweza kumuangalia
zaidi, kwani mke wangu alidondoka, na ikatokea kama nilivyowaambia, kwahiyo,
jamani mtoto huyo mpelekeni kwa mwenyewe, mtoto huyo mpelekeni kwa mama yake ni
haki yake,….’ Akasema kwa msisitizo huku akionyeshea mlangoni.
‘Lakini shemeji kuna uhakika gani kuwa huyu mtoto ni wake?’ akauliza
nesi
‘Kuna uhakika gani…!?’ akauliza shemeji mtu kwa kauli kama ya dhihaka
na wote wakamuangalia kwa mshangao.
‘Mlishawahi kumchunguza huyo mtoto vyema..?’ akauliza akiwaangalia
kila mmoja kwa zamu
‘Si ndio huyu tumekuja naye…tumchunguze kwa vipi tena….’akasema
nesi
‘Oh, kama mumemchunguza vyema,… japokuwa …sijui kwanini, muda wote
niliowahi kuishi na huyo mtoto, sikuwahi kujiwa nahilo wazo,..kabisa..lakini
huyo mtoto na mama yake wanafanana, hubahatishi….’akasema
‘Hata akiwa kalala, sura ya huyo mtoto na wazazi wake haifichiki,
macho ya huyo mtoto ni kama ya mama yake…’ akasema na hapo akasimama
‘Macho?’ akauliza nesi huku akifikiria kitu.
‘Macho…, ndio macho yake, …kama kuna kitu nilichokuwa nikimempendea
zaidi huyo mwanamke ilikuwa ni macho yake..’akasema na kutabasamu.
‘Mhh, kumbe….’akasema nesi akikumbuka kitu.
‘Mwanamke huyo alijaliwa urembo, enzi za usiachana wake weeeeh, na macho yake yalikuwa na mvuto,ni yale macho
ya buluu, ya kipekee kama ya mzungu, sijui
nikuelezeje, kama mumemkagua huyo mtoto wake mtajua macho yake yalikuwaje..,
sasa yake yalikuwa na urembo wa kike, si unajua wanawake macho yao
yalivyo..eehe’akatulia kidogo kama anaonyeshea ili watu wamuelewe.
‘Lakini sasa nayaona kama ya shetani…mchawi….hahaha, ndio maana
hata watu wakakimbilia kumuita mchawi, je wangeliona hayo macho yake sijui
inaglikuwaje, hahaha…..’ akasema na kukatiza kauli yake ghafla na kugeuza
kichwa upande wa mlango wa chumbani.
Alikatiza kauli yake, kwani mlango wa chumbani ulifungulia, na
aliyejitokeza pale mlangoni alikuwa mke wake akiwa kajifunga khanga mbili,
akionyesha kuchoka…. Nesi naye akageuka kumuangalia dada yake, huku akiandaa
kusimama, lakini akashikwa na butwaa, na
kabla hawajasema kitu, mke mtu huyo akawa wa kwanza kuongea , akasema;.
‘Mume wangu kwanini unamtusi mama wa watu, ulisikia kabisa kuwa
sio kosa lake, hebu jiweke wewe kwenye nafasi yake, ungelifanyaje, uchague mume
uwatelekeze wazazi wako,unaweza kweli kufanya hivyo?’ akauliza mke wake, na
mume wake akabakia kimia.
‘Fikiria sana, hali ya kule kijijini kwenu ilivyo, na huyo
mwanaume, ambaye umekiri mwenyewe kuwa huyo mwanaume alikuwa akiogopewa, watu wa huko kijijini kwenu walikuwa
wakimuogopa sana.., ulisema mwenyewe kuwa alikuwa tishio, ulitaka wazazi wa
watu wawe watumwa…hapana, hata ingelikuwa mimi nahisi ningelifanya hivyohivyo…’
akasema mkewe
‘Najua wanawake mnachojali ni mali, najua kabisa ungelifanya hivyo
hivyo au sio, ili upate mali, au sio, mbona upo na mimi…ndio najua kwenu
wanawake wanajali sana mali , mali kwao ni bora kuliko mapenzi au sio mke
wangu…, sawa, lakini tafadhali …tafadhali, nimekuambia ulale,…..kalale usije
kuniletea balaa jingine, kwani huku umefuta nini?’ akasema huku anamfuata mkewe
pale aliposimama.
Nesi ambaye alikuwa kashikwa na butwaa, akimwangalia dada yake,
akawa kama kagandishwa, nusu kukaa na nusu kusimama, akawa sasa anainuka
taratibu huku haamini nini anachokiona. …haamini macho yake…
NB: Twende kidogo kidogo kidogo tutafika tu, tunakimbizana na
salio.
WAZO LA LEO: Ni kweli kutendewa ubaya kunauma sana,
hasa kusalitiwa, ni kweli kudhulumia, kunyimwa haki yako, kunauma na kunatesa
sana, lakini tukumbuke kuwa mpaji ni mungu, mtoa riziki ni mungu, na hayo
anayafahamu vyema kuliko utashi wa nafsi zetu. Muhimu, yakitotokea hayo,
mitihani ya maisha kudhulimiwa kusalitiwa, tukajitahidi kadri ya uwezo wetu
kudai haki,..kusubiria na juhudi za kila namna, ni lazima tufanye juhudi sio
kukaa tu na kulia…na bado ikashindikana, iliyobaki nini…tumkabidhi mungu,yeye
anajua nini la kufanya….wangapi wangapi walifanya hivyo na sasa wapo wapi…
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hi there! This is my first comment here so I just wanted to give a quick shout out and say I genuinely enjoy reading your articles.
Can you suggest any other blogs/websites/forums that deal with the same subjects?
Thank you so much!
Also visit my site - Android 3D Puzzle Game
Post a Comment