Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, December 23, 2014

NANI KAMA MAMA-12

       

Jamaa kuona hivyo, akaona humo hakukaliki, yeye alikuja kwa taarifa nzuri kuwa kaona ng’ombe mweusi kwa jamaa yao mmoja, na hilo linaweza kumfurahisha rafiki yake, lakini anachokikuta hapo ni tofauti, ..

‘Ina maana mimi nimeacha shughuli zangu kwa ajili ya kujali urafiki wetu, nimefanya makosa, ndio haya yamekuwa hivi, kama ni hivyo,mimi naona hapa hakuna amani, ngoja nijiondokee zangu tu , samahani naomba nitoke....’akasema akigeuka kuondoka, ikawa kosa.

Ilikuwa ni Bahati tu,kwani aliinama kufungua kitasa cha mlango, na ndicho kilichomsadia, kwani rungu lilikuwa lipasue kichwa likagonga kwenye bega upande wa nyuma.


‘Khaa, rafiki yangu vipi...’akasema na kabla hajageuka vyema, alishitukia teke, na rungu la pili likimkosa kosa tena, kwani kwa muda huo alishageuka kiaina  kujihami, akaona sasa hana hiari ni mapambano tu, kwani mwenzake inavyoonekana kadhamiria kumuua!

Ilipita dikika kumi, ngumi zikurushwa, mateke, rungu, viti, ..na kila mmoja akijaribu kutumia ubavu wake, na kuhakikisha anamjeruhi mwenzake, ubinadamu ukatoka, ukabakia unyama, urafiki ukatoka ukabakia uadui...damu ikaanza kumwagika....

Tuendelee na kisa chetu...

 Majirani walisikia ghasia na baadhi wakafika hapo kuangalia kuna nini, wakasukuma mlango uliokuwa umeufungwa kwa ndani, ukawa haufunguki, lakini watu wakiguna kuonyesha kuna mapigano luliwaanya waamue kuuvunja huo mlango, walipoingia wakakuta jamaa wawili wakiwa wanapambana mtu na rafiki yake. Damu zinawavuja

Hali waliyokutwa nayo ilikuwa mbaya, wanaume walikuwa wakivuja damu, huku wakiwa hoi wamechoka, na bado vita ilikuwa ikiendelea. Ilibidi vijana wenye nguvu waitwe kuwakamata na walipokuja ilichukua muda sana kuwatenganisha.

Walishangaa kmuona mama mwenye nyumba akiwa kalala sakafuni, walipomchunguza wakagundua hana fahamu, ikabidi atolewe nje kwenye upepo na huduma ya kwanza ifanyike kwa haraka.

Mpaka muda huo hakuna aliyeweza kugundua chanzo cha ugomvi huo ni nini,…wakati wengine wanahangaika kumfanyia mke mtu huduma ya kwanza, wengine bado walikuwa na kibarua cha kuwasuluhusha hao mafaili wawili,kwani japo wamechoka, wameumia, lakini kila mmoja alikuwa na mori wa kupambana na mwenzake, kila mara walikuwa wakikurupuka kutaka kupigana, ikaonekana dawa na kumuondoa kabisa huyo aliyekuja kwenye nyumba ya mwenzake na kumpeleka mbali kabisa, ilikuwa mshike mshike hadi anaondolewa hapo.

‘Niacheni huyu mtu hawezi kuniumiza hivi bila kosa, nimemfanyia nini mimi , mangapi tunasaidia, leo hii ananifania hivi sikubali…..’akawa anasema rafiki wa baba yako, na baba mtu akisema;

‘Ni lazima ulipe, na bado nitakuumiza sana, mpaka nihakikishe na wewe upo kama mimi, hamuwezi kunifanyia hivi mimi na huu mzogo wako uuchukue…’wakawa wanajibishana kwa  kauli za kukata hakuna aliyeweza kugundua chanzo cha mapigano hayo ni nini kutokana na kauli hizi zisizokamlika….

Wazazi na mjumbe wakaitwa ili kusuluhisha hayo mapigano, na hao mafaili wawili wakaitwa mbele ya mjumbe na wazee wa kijiji, wakaanza kuulizwa,  chanzo cha ugomvi wao, ikawa kila aliyeulizwa anapandisha hasira, anataka kwenda kupambana na mwenzake hakuna aliyekuwa na lakusema, ila kutizamana kwa hasira mbele ya mjumbe na wazee wa heshima.

Kule kwa mama aliyepoteza fahamu, juhudi zilikuwa zinaendelea, Ilichukua muda mama  kuzindukana, na alipozindukana, na kuonekana kuwa anaweza kuongea, ikabidi aulizwe chano cha mapigani hayo nay eye kupoteza ahamu ni nini, ikawa hakuna jinsi akaelezea ilivyokuwa.

‘Ukweli ukadhihiri, na mafahali wawili wakaambiwa wajieleze, kila mmoja akaanza kujitetea kivyake, na wazee wakasema;

‘Hili ni kosa na ni tatizo kubwa, hatuwezi kuliacha hivi hivi kwani linaweza kuleta maafa baadaye, inabidi  kuitisha kesi ya kimila, ili kujua ukweli na kama kuna ushahidi wowote wa hiyo shutuma unahitajika mbele ya baraza la wazee…’ikatolewa hiyo taarifa.

Kesho yake, watu wakakusanyika kwa mjumbe, wakiwemo wazee wa kimila ambao wanajua mambo hayo na usuluhishi, ikabidi sasa kila mmoja apewe muda wa kujieleza na kutoa ushahidi wake. Baba yako, akatoa taarifa yake kuwa alisikia tetesi za watu, na akaamua kuuatilia akagundua kuwa kweli raiki yake ana mahusiano na mke wake.

‘Hizi taarifa au tetesi ulipewa na nani?’ akaulizwa
‘Na marafiki zangu wa kijiweni, na pia mke wangu mdogo ambaye hayupo mbali na nyumba ya mke wangu mkubwa…’akasema

Ili kujua ukweli, Ikabidi marafiki hao waitwe kuhojiwa, na wao wakasema walikuwa wakimona rafiki huyo akifika mara kwa mara wakati mume wa familia hayupo.

‘Je kabla ya hapo huyu rafiki alikuwa hafiki, kabla ya kuhisi hivyo, kuwa huenda wana mahusiano?’ wakaulizwa

‘Alikuwa anafika, lakini hali iliyoendelea baadaye ilitutia mashaka ndio maana tukaona tumueleze rafiki yetu achunguze mwenyewe…’wakasema.

‘Yeye ni rafiki yake, yeye ndiye aliyesimamia harusi na mara nyingi mtu ambaye kakusimamia kwenye harusi na ndoa yako anakuwa ndugu yako, kufika kwake hapo nyumbani ni jambo la kawaida kuna ushahidi gani mwingine wa kuonyesha kuwa huyu mama alikuwa na mahusiano ya karibu na huyo mke wa mtu?’ wakaulizwa

‘Hakuna…’wakasema.

‘Kuna mtu alifika kwake akaona ushahidi wa kuonyesha kuwa hao watu wanamhusiano ya kimapenzi?’ wakaulizwa.

‘Hakuna aliyefika, ndio maana tulimuambia achunguze kuhakikisha, hatukumwambia kuwa tuna ushahidi, …’wakajitetea.

‘Kwahiyo nyie mlihisi tu, mkajenga fitina na umbea…’wakaambiwa, na baadaye akaitwa mke mdogo na kauli yake ilikuwa hiyo hiyo kuwa huyu jamaa alikuwa akifika mara kwa mara na mara nyingi mume wake anakuwa hayupo.

‘Wewe ni mke mwenza, je uliwahi kufika ukashuhudia wakiwa na mahusiano kama hayo mnayodai, kuna dalili gani zilizokuonyesha kuwa wana urafiki wa karibu?’ akaulizwa

‘Jinsi walivyokuwa wakiongea na huyu mtu akifika hukaa sana ndani, akitoka anasindikizwa…’akasema

‘Ina maana wewe hajawahi kufika mgeni kwako wa kiume, akakaa halafu alipotoka ukamsindikiza?’ akaulizwa
‘Wanakuwepo , lakini kwa mwenzangu ilikuwa imezidi, ni huyo huyo tuu, inatia mashaka..’akasema.

‘Je uliwahi kufika ukawafuma wakiwa katika hali ya mahusiano, maana wewe upo karibu, hukufanya utafiti huo?’ akaulizwa.

‘Kwanini nisumbue kwenda kuangalia wakati hali inajionyesha, sikutaka kupoteza muda wangu mimi nilimwambia mume wangu ajaribu kuchunuza maana mimi nina wasiwasi na huyo rafiki yake….’akasema.

‘Hivi kweli nyie mpo majirani ulishindwaje kufanya utafiti, lakini ukaweza kwenda kutangaza mitaani kuwa mwenzako ana mahusiano na huyo rafiki wa mume wako…huoni kuwa huo ni uchonganishi, na wewe ndiye umesababisha yote hayo….’akaambiwa.

‘Kama hamuamini basi, ila mimi nilitimiza wajibu wangu kusema kile nilichokiona, na nilimuambia mume wangu achunguze, sasa yeye akachukulia hasira…’akasema mke mdogo.

‘Lakini hukuwahi kuthibitisha hilo kuwa kweli watu hao wana mahusiano, umeona wakiongea, umeona huyo mtu akiingia na kutoka , na ni kawaida yake kuja hapo, hata kabla yaw ewe hujaolewa, hata akiwemo mume wake, kama alivyijieleza, je sio kweli kuwa anafika hapo hata akiwemo mume wenu?’ akaulizwa.

‘Ni kweli huwa anafika, lakini mara nyingia anafika mume wetu akiwa hayupo..ndio maana mimi nikatilia mashaka’akasema.

‘Hebu tumuulize muhusika ni kwanini ulikuwa ukifika wakati mume wa nyumba hayupo?’ akaulizwa.

‘Mimi kazi zangu ni za uvuvi, pamoja na uchungaji, nyumba ya rafiki yangu ipo njiani, napita hapo nikiwa nimetokea kwenye kazi zangu, siwezi kupita tu bila kusalimia wakati huyo ni rafiki yangu, na urafiki wetu ni kama udugu,kwa ukaribu tulio nao…’akasema.

‘Hebu tuambie siku ya tukio ilikuwaje?’ akaulizwa.

‘Siki ya tukio mimmi nilifika kutoa taarifa kwa rafiki yangu ambaye alikuwa akitafuta ng’ombe mweusi kuwa nimempata huyo ng’ombe, nilipofika nikakuta mke wa rafiki yangu kalala sakafuni, na kabla sijajua ni kitu gani kilichotokea rafki yangu akaanza kuniandama kuwa kasikia kuwa mimi nina mahusiano na mke wake…ilikuwa ni mshangao kwangu maana mimi na yeye tunaurafiki wa karibu, kama ndugu haingeliwezekana mtu kama mimi kufanya uchafu wa namna hiyo…’akasema

‘Na kumpa lifti ya baiskeli sio mara ya kwanza, kama nilimuona yupo sokoni na mimi naelekea njia hiyo kuna ubaya ganni kumpa lifti, anafahamu sana, sema katekwa na ibilisi…’akasema.

‘Ibilisi umenipa wewe….acha kujikweza hapa…..’akasema baba yako akanyamazishwa na wazee kuwa hajapewa nafasi ya kuongea.

‘Lakini kwanini iwe kila siku unafika nyumbani kwa mwenzako wakati hayupo, hilo ndilo linakuwa swali kwa wengi, imeonakana kufika kwako kwa rafiki yako kumezidi sana,….’akaulizwa.

‘Kama nilivyosema mimi nikitoka kwenye shughuli zangu napitia hapo, na muda huo rafiki yangu anakuwa hayupo, je ingelikuwa ni busara mimi kupita bila kusalimia,..hivi kweli kwa mila zetu inakubalika hivyo, je mimi hapo nimefanya kosa gani,mbona yeye akienda kijiweni au kilabuni anapitia kwangu na kumsalimia mke wangu …’akasema.

‘Haya baba mwenye nyumba tuje kwako, kuna ushahidi gani mwingine wa kuthibitisha hiyo kauli yako kuwa rafiki yako anakuibia mke wako?’ akaulizwa

‘Mke wangu ni mja mnzito…’akasema na watu wakacheka na wengine wakampa hongera.

‘Msicheke, huenda kauli yake hiyo ina maana kwake, hebu tuambie mke wako kuwa mja mnzito inahusikanaje na rafiki yako, maana huyo ni mke wako na kuwa na mimba ni jambo la kawaida..?’ akaulizwa na hapo ikabidi aelezee alivyoambiwa na mganga wa kienyeji.

‘Ndugu yetu, huyo mganga yupo wapi, maana hilo linatushangaza sana,yeye anajuaje kuwa wewe hutazaa, ana vipimo gani, vya kukuthibistishia hilo, au je uliwahi kwenda hospitalini ukaambiwa kuwa hutazaa?’ akaulizwa.

‘Niende hospitali, ….nyie wazee vipi, hivi hili nalo ni la kuwenda hospitalini kujitangaza, hapana, mimi najua kuwa dawa za kienyeji na mambo ya wazee wetu yana uhalisia zaidi…’akasema
‘Kwahiyo wewe hivi sasa ni tasa, unaamini kuwa hutazaa tena?’ akaulizwa

‘Nani tasa….sasa mnataka kunitukana…’akasema na watu wakacheka.

‘Si ndivyo alivyokuelezea mganga wako kuwa ukikiuka mashartii basi hutazaa tena, utakuwa tasa, si ndivyo ulivyosema,je wewe unaamini hivyo. Kuwa wewe sasa ni tasa…ili wake waondoke, maana sheria zinawaruhusu au?’ akaulizwa

‘Siiii-amini…kuwa mimi ni tasa, mimi rijali bwana….kama itakuwa hivyo, hapana mimi sio tasa, nitahangaika mpaka nilimalize hili tatizo na huyo rafiki yangu nitahakikisha na yeye anakuwa kama mimi….’akasema akimuangalia rafiki yake kwa hasira.

‘Anakuwa kama wewe kivipi…? kama wewe tasa au kama wewe nani?’ akaulizwa

‘Kama wameamua kuniharibia yeye na mke wangu, basi na mimi nitawaharibia wao, nitahakikisha hakieleweki, nitawafanya wao kama mimi…’akasema.

‘Kwahiyo wewe unaamini kuwa sasa hivi umeshakuwa tasa?’ akaulizwa.

‘Nani kawaambia mimi ni tasa bwana nyie wazee vipi, mimi tasa mimi tasa, mnafanya tangazo, je nikizaa mtasemaje,….mabona hatuelewani…’akasema kwa jaziba.

‘Masharti ya tambiko, au kama alivyokuagiza mganga wako yamevunjwa, mke kaenda kupimwa hospitalini na ili apimwe damu inabidi achomwe sindano, je hajavunja hayo masharti…’akaambiwa kama anaulizwa kabala hajasema neno mjumbe akasema;

‘Haya kwa kauli yako na uvumi uliopewa wewe unaamini kuwa mke wako katembea na rafiki yako je hajavunja hayo masharti, na kwa kauli ya mganga masharti ya kivunjwa wewe hutazaa tena, umekuwa taa-saa, si ndio hivyo jamani alivyosema,…tunakuuliza tena je wewe unaamini kuwa sasa hivi umeshakuwa tasa…?’ akaulizwa.

‘Siamini…nitahangaika, japokuwa mganga kasema hivyo, lakini wanazidiana nitakwenda kwa mganga mwingine atanitengeneza, na ole wao,nawaambia mbele yenu ole wao…’akasema.
‘Acha vitisho, kijana, wewe bado mdogo sana, hujui maisha yalivyo, sikiliza tukuelemishe….’akaambiwa na akatulia akiwa kainama chini.

 ‘Lengo letu la kukuhoji hivyo nikutaka kukuonyesha kuwa hayo uliyoambiwa na mganga wako sio kweli,…mwenyewe unakiri hapo kuwa huamini kuwa wewe ni tasa, kama ungelikuwa unamuamini basi ungelikubali kuwa wewe ni tasa,au unaamini hivyo tukusaidie ..?’ akaulizwa tena akawa kimia.

‘Jamani nyie vijana, nyie watu, tusipende kuamini mambo hayo bila kuwa na vipimo halisia, na vipimo halisia ni kwenda hospitalini je hawa waganga wana vipimo gani vya kukuonyesha kuwa wewe hutazaa au utazaa, ni Bahati nasibu tu wanacheza, nikuulize tena wewe bondia,  je wewe uliwahi kwenda hospitalini ukaambiwa huwezi kuzaa?’ akaulizwa.

‘Mimi siamini vipimo vyao hivyo vya hospitalini huwa siendagi huko, wanaweza kukupiga sindani wakakumaliza kabisa ukawa huzai kabisa, wajanja sana wazungu wanataka sisi waafrika tusiwe na watoto wengi…’akasema na watu wakacheka.

‘Msicheke nyie hamjui tu…mimi ni kichwa najua mengi, hayo madawa ya uzazi wa mipango, yote hiyo ni ujanja wao, mara sindano za kinga, sijui madawa ya ….aaah, yote hayo ni mbinu zao za kutaka kumaliza kizazi cha kiafrika, sasa mimi hawanipati ng’oooo,’akasema na watu wakacheka.

‘Ndugu yetu kwa kauli zako hizo inaonyesha jisni gani ulivyo nyuma ki-utalamu na elimu yako ina walakini,…inabidi uende ukasome zaidi , ukaelemishwe vyema…fanya utafiti wewe bado mdogo, jielimishe ndugu yetu….huoni watu wanakucheka, utajiri wako utakuwa hauna maana kama huna elimu…’akaambiwa.

‘Ni kuambi ukweli, na huyo mganga wako unayemuamini ni kwanini akuagize ng’ombe,…si unajua wewe ni tajiri wa ng’ombe,  kwani awe anaagiza nyama, tena zilizonana, huoni kuwa ni mbinu yake ya kupata kitoweo…je huyo ng’ombe akichinjwa nyama unarudi nazo..?’ akaulizwa

‘Hapana zinatolewa kafara…’akasema kwa kujiamini

‘Kafara, kafara kafara…haya wewe unalijua vyea hilo kafara,  wazee happ hapa watanisaidia nisije kukiuka utamaduni, ina maana hizo nyama anapelekewa nani ili liwe kafara, ndi nataka kujua hapo au zinazikwa, au zinapelekwa wapi?’ akaulizwa
‘Mimi sijui hiyo ni kazi ya mganga aliyeniagiza….’akasema.

‘Hahaha, ndugu , kijana, umeliwa…’akasema huyo mjumbe na watu wakacheka.

‘Jamani ndugu zanguni, hatutaki kuzalilisha utamaduni wetu, tiba mbadala zipo, waganga wa kienyeji wapo, kafara zipo na zinajulikana kuwa kama ni nyama zinapelekewa masiki wasiojiweza, na nyingine tunagawana majirani hilo ndio kafara….’akasema

‘Lakini waganga wetu hawa, wajanja, mafisadi, nia na malengo yao ni kuwahadaa wananchi, wanachotaka ni kujali matumbo yao kwa udanganyifu wa ramli, hii inayoitwa ramli ni viini macho, ujanja wa kukuhadaa wewe,kama wanaweza waniloge mimi, mimi siogopi kwasababu hawawezi …’akasema

‘Hata kwenye vitabu vitakatifu ramli ni haramu,…au nadanganya wataalmu wa dini, ramli ni haramu , ni haramu….huyo anayepiga ramli hamuamini mungu,maana mwenyezimungu kakataza yeye anafanya, ni nani anayempinga mungu, ni rafiki wa shetani, na kama ni rafiki wa shetani nay eye ni nani ….ni shetani, msiogope kusema waganga hao si lolote, wezi wakubwa, hao wanapingana maandiko ….vijana, hata wazee hebu someni dini zenu vyema someni elimu zote muijue duni ilivyo.

‘Pia hebu waangalieni maisha ya hao wanaoitwa waganga, japokuwa siku hizi kuna ambao,wamekiuka miiko, wanajijenga siku hizi, lakini swali ni hili, kama wao wanaweza kuleta utajiri, watoto nk, mbona maisha ya ndio zaidi ya wewe unayekwenda kuomba msaada huo

‘Hahahaha,wengine hata wake hawana, kama hana mke wewe unakuadanganya kuwa atakupa uzazi, kama yeye anaweza kuleta utajiri kwanini wanadai muache pesa, muwalipe viingilio, mtoe ..mpaka wanatumia neno zuri ambalo hawastahili kulitumia, eti mtoe sadaka, sadaka ni kitu kitakatifu hakistahiki kutumiwa na hawa watu, ….hebu jiulizeni hizo pesa wanataka za nini kama wana uwezo wa kukupa wewe utajiri….msidanganyike, chunguzeni kwanza…’akasema mjumbe.

‘Wanawadai pesa, wanawadai eti sadaka, kwa vile wanajua kidogo kidogo, wewe umeika yula kaja, ikifika jioni ana pesa,…ndio maana wengine wajanja sasa ni matajiri…kwa sababu ya ujinga wenu…mimi hawanipati ng’oooo’ akasema mjumbe na watu wakacheka.

‘Sasa wewe uliyeamu kuchukua sheria mikononi mwako una makosa, kwanza kusikiliza umbea, mwanaume kama wewe hustahili,…unatuabisha, pili, kupiga, na kujeruhi, …halafu wewe mwanaume unapigana na akina mama, kama una miguvu kajiunge na ngumi za kulipwa, utatajirika, usipoteze nguvu zako bure kwa akina mama, hao akina mama, hawatakiwi kutumia nguvu, eeh, au hujapitia jando wewe, kwakweli umetutia aibu....’akaambiwa na wazee, na jamaa akainama chini.

‘Una makosa…kwahiyo kama  sheria za kimila zilivyo, unastahiki kutoa faini, faini kwa mke wako, na faini kwa rafiki yako, kwanza umuombe mke wako msamaha, pili unatakiwa umlipe ng’ombe mzima, na hilo pia ulianye kwa rafiki yako,umuombe msamaha, na pia umlipe ngombe mzima…’akaambiwa

‘Nini, mimi niwaombe msahamaha, nani mimi, labda sio mimi, eti nimpig make magoti nimuombe msamaha wakati, wao ndio wana makosa, hapana wazee mimi hilo sikubali…’akatulia alipoona wazee wanamkodolea macho.

‘Sisi kama wazee wako, tumeliangalia hilo kwa makini tumelichunguza, na sio kwamba tunasema tu,tulishawahi kusikia tetesi kama hizo, tukachunguza, kiukweli, hakuna kitu kama hicho, umedanganywa, na kama  ulitaka kupeleka ng’ombe kwa huyo mganga, acha, utaliwa ng’ombe wako bure..huyo mganga ametafutwa hajapatikana…kashakimbia kajua keshasababisha mapigano…’akaambiwa.

‘Sisi tunaona mbali, tunatumia busara, hekima zetu zinaonyesha kuwa mkeo ana uja uzito wako,…unatakiwa ufurahie, ndio maana unatakiwa upigia magoti, ili moyo wake ufurahi…’akaambiwa akainua kichwa kuangalia upande ule aliokaa mke wake, kwa macho ya hasira.

‘Hivi mnanifanya mimi mtoto mdogo au…?’ akauliza

‘Kwahiyo sisi tunaokuambia haya ni watoto wadogo, hatuna akili, unatuzarau?’ akaulizwa

Baba yako hakuwa na kufanya, akakubali shingo upande kwani wazee wa kimila wanaheshimiwa sana, na hata hivyo akasema anasubiri mtoto akizaliwa kama ana sura ya huyo jamaa atahakikisha anamletea huyo raiki yake kiwiliwili kisicho na kichwa na mke atakuwa kiwete. Na rafiki yake akajibu;

`Na hata akizaliwa sura kama yako, namchukua huyo mtoto kwangu, kwani hustahili kuwa na baba kama wewe anayepinga uhalali wako, hivi utapata wapi mke kama huyo anayejiheshimu, na kwanini mimi nitembee na mke wako, wakati mke wangu unamtambua kwa uzuri wake...’akasema

‘Kama angekuwa mzuri ungekuja kuzini na mke wangu….ipo siku nitakusana, na akizaliwa ushahidi utabainika…’akasema

‘Kwa kauli yako sitaki urafiki na mtu kama wewe, ole wako, ukanyage kwangu, na huyo mtoto akizaliwa sio halali yako hata kama mnafanana naye, na kama atakusaidia, hatafanikiwa, maana hustahili msaada wake, kwani umeshamkana…huyo ni mtoto wa mama,na hakuna mama anayeweza kumkana mtoto wake, hakuna mzazi anayekana mtoto wake, wewe umemkana, hata kabla hajazaliwa..…’ rafiki yake akasema.

`Tatizo lako unafikiri mimi ninatania, we subiri uone, labda kama sio mimi…wewe unanionaje mimi, mimi siwezi kulea mimba za watu, azaliwe mwanaharamu, utakuja kuchukua kinyago chako, kikusaidie wewe…’ baba yako akasema na kuondoka hapo kwenye kikao.

NB: Mnaona eeh, weke akili ni hapo

WAZO LA LEO: Chungeni sana kauli zenu, kauli nyingine ni hatari zinaweza kusababisha maafa, na kauli nyingine huumba,..na kwa wazazi msipende kuwaita watoto wenu majina mabaya,….majina hayo na matamshi yenu yanaweza kuwaathiri watoto kisaikolojia, na watoto wakawa hivyo hivyo….tuwe makini, maana ulezi ni ualimu, na elimu ya mtoto huanzia kwa wazazi wake.



Ni mimi: emu-three

No comments :