Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, December 19, 2014

NANI KAMA MAMA-10



‘Nia yangu ni kuhakikisha wote mnatibiwa, mnajua tatizo ni nini, au kuna matokeo gani,  kuna mambo ya kizamani na kimila tunataka kuyapiga vita kwa manufaa yenu, hasa hili la kuja kutibiwa mke peke yake au mume peke yake…ni vyema eeeh’akaangalia ile karatasi kama anataka kusoma majibu ila akasita na kusema

‘Unajua piaa kuna magonjwa yanahitajia muwepo wote wawili ili iwe rahisi kwetu kutoa maelekezo, na matibabu pia…ndio maana nataka na mume wako awepo ili mpate majibu yenu kwa pamoja, na matibabu na ushauri pia, na pia ndio utaratibu wetu wa hapa hospitali…’akasema dakitari.

‘Mungu wangu…’nikasema huku nikiwa nimeshika kichwa kwa mikono yangu miwili..

‘Kwani kuna tatizo gani..?’ akauliza dakitari

‘Dakitari nimeshakuambia kuja hapa nimefanya kujiiba…wewe hunielewi, mume wangu akisikia nimekuja huku kutibiwa ataniua, na hata hivyo kwani kuna tatizo gani kubwa mpaka yeye awepo…..ina maana nina ugaonjwa mbaya sana, au….oh, au nimeathirika, na hilo gonjwa la…ooh, docta niambie kama ninao nijue moja….?’nikasema kwa wasiwasi maana nilishasikia mengi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, nikajua labda kagundua kuwa ninao, ndio maana dakitari anaogopa kunipa majibu yangu. 

‘Ni utaratibu na kikao kilichpita cha wadau, walinishauri hivyo na mimi natekeleza tu…’akasema kama vile hospitali sio yake.

`Docta mimi sislwei maana ninayeumwa ni mimi, ni kwanini mpaka mume wangu awepo, naomba sana unipe hivyo vipimo na nisingependa mume wangu ajue kuwa nilikuja huku…’ nikasema, huku sasa nampigia magoti nilijua kama mume wangu atajua kuwa nilifika huku, cha moto nitakiona

Tuendee na kisa chetu….

               ************
  
Docta alishangaa na kumwangalia yule mama kwa makini, akainuka kwenye kiti na kwenda pale alipokuwa yule mama kwa muda huo alikuwa kapiga magoti akilia…alipomuinua akamuangalia moja kwa moja usoni, akatabasamu, na mama akashangaa kwanini huyu mtu anatabasamu.

Docta akasema;

‘Kwanini unanipigia magoti...aah, usifanye hivyo mama, inuka, unajua jamii zetu bado tuna mambo ya kizamani, mambo ya afya za akina mama au akina baba inakuwa vyema kama nyote mnakuwepo…akarudi kwenye kiti chake na kushika ile karatasi…

‘Kuna kitu tunakosea sana katika ndoa, ndoa inaunganisha mwili kuwa kitu mmoja, sasa naona ajabu sehemu ya mwili inauma, moja inakuja kutibiwa nyingina inabaki nyumbani, hivi kweli inawezekana, hebu niambie mpendwa kweli hilo linawezekana…’akawa kama anauliza

‘Doctaaaa, mbona unazidi kunichelewesha….’akasema mama

‘Hili ninalokuambia ni muhimu kuliko hayo majibu unayotaka, kwani ushauri wa mmoja mmoja hausaidii sana, nikikushauri wewe tu, ukifika nyumbani unaweza ukasahau, au ukaogopa kumwambia mwenzako…itakuwa imesaidia nini’ Docta akachukua kile cheti cha majibu mkononi, akakisoma halafu akamtizama yule mama.

`Hebu nikuulize swali moja, una watoto wangapi?…’ docta akatabasamu na kumwangalia mama kusubiri jibu

‘Docta mimi nataka majibu, watoto wanakujaje, hivi mna nini, ungelijua hali ninayopamabana nayo usingeiendelea kunipotezea muda, …kuniuliza kuhusu watoto…wakati …sina mtoto docta, na mimi ni….mgu-mba!’ mama akaangalia pembeni kwa huzuni.

‘Mgumba!? Hapana,….kwanza ni nani kakuambia kuwa wewe huzai, ..?’ akauliza docta.

‘Mhh, mimi sijui..mwaka unakimbilia wan ne, sijawahi kushika mimba, hapo utajitetea nini, hata hivyo hayo sio muhimu kwangu nimeshakubaliana na hiyo hali, ..mimi ninachotaka sasa hivi ni kujua kwanini naumwa….mimi siumwi umwi ovyo nimepata matatizo gani?’ akauliza mama

‘Unasikia mpendwa, wewe sio mgumba, na ujiandae kuwa mzazi, u-mjamzito, una mimba, na….’ Docta akawa anaongea, lakini hayo maneno yaliyokuwa yakiongea baada ya kutamka kuwa mama ana ujauzito yalikuwa hayaingii akilini mwa mama.

Mama alibakia mdomo wazi akimuangalia docta, alitaka docta arudie tena yale maneno, lakini hakuwa na nguvu za kutamka neno, akabakia ameduwaa na kujihisi yupo ndotoni…baadaye akatikisa kichwa kurudisha akili akamsikia docta anaendelea kuongea;

‘Umja-mzito mama, una mimba, ndio maana nilitaka baba watoto wako awepo ili niwape hongera na kuwapa jinsi gani ya kuishi , ili mtoto aje kuzaliwa akiwa na afya nzuri. Lakini yote utayapata ukija kwenye `clinic’ yako , mshauri sana mume wako aje pamoja na wewe …’ docta akasema na kuinuka, aliona hakuna haja ya kupoteza muda

Mama alibakia kaka kwenye kiti akiwa ameduwaa, akawaza kuwa hayo anayosema docta yanaukweli, au vipimo vimekosewa, akawa hainuki pale kwenye kiti, mpaka docta akashangaa, na kumuuliza swali;

‘Vipi, wewe mama, siumesema una mume, nakuona kama hujaupokea vyema huo uja-uzito au huamini kuwa una mimba, na nilitumai ungeinuka kwa furaha, au kuna tatizo jingine..’ akasema docta

‘Siamini docta, una uhakika na hivyo vipimo kweli, mimi nilishaambiwa kuwa ni mgumba, toka lini mgumba akazaa?’ yule mama akainuka huku kaangalia juu.

‘Ni nani alikuambia kuwa wewe ni mgumba, ulikuja kupima hapa hospitalini, au wapi…musiamini maneno ya mitaani, mama wewe una ujauzito na huenda imeshapita miezi miwili au mitatu,..niambie toka lini ulikoma kuona siku zako?’ akauliza docta.

‘Docta…sikumbuki, maana mimi naweza kupitiliza kwa muda mrefu tu mpaka nahisi nina mimba, baadaye zinafululiza siku zangu…kwahiyo hata sikumbuki, …akili yangu haipo sawa docta hata ukiniuliza kitu hapa sitaweza kukuambia, sikumbuki docta….’akasema mama.

‘Basi , ila hilo ni muhimu , jaribu kukumbuka, na kesho uje umuone dakitari wa akina mama wajawazito atakupima na kukupa taarifa ya afya yako na atakufungulia daftari la kliniki, kuna uchafu kidogo kwenye mkojo na hilo ni muhimu hata baba akapimwa, ili tuone kama na yeye hajaambukizwa..lakini sio tatizo kubwa sana…..unaweza kwenda’ Docta akasema na mama akasimama na kuanza kuondoka, docta akamsindikiza mama hadi nje.

********

Mama njiani alikuwa akiwaza mengi, anakumbuka siku mume wake alipokuja toka kwa huyo wanayemuita mtaalamu , akasema kuwa kaambiwa kuwa yeye ni mgumba, hazai na mume wake alitakiwa atafute mke mwingine! Siku hiyo alilia sana, na kumuomba mungu amsadie angalau apate hata mtoto mmoja.

Kutokana na muda mrefu kupita bila kushika mimba yeye alikubaliana na hilo kuwa yeye ni mgumba, kwahiyo hakuwa na kipingamizi cha mume wake kutafuta mke mwingine, japokuwa hakutamka moja kwa moja kuwa amekubali kuolewa mke mwingine.

‘Ningelikataa ili iweje, maana watoto ni sehemu ya familia, kama mimi ni mgumba, kwanini niinyime familia kizazi, moyoni nikakubaliana na hiyo hali na nikawa tayari kumpata mke mwenza, japokuwa taratibu za kumtafuta hadi kuolewa kwa huyo mke mwenza sikushirikishwa.

Basi alipoolewa mke mwenza, akawa naye hazai mumewe alienda kwa wataalamu akaambiwa hatazaa mpaka akatambike kwa mizimu, huko apelike ngo’mbe na vitu kibao, akitoka hapo atazaa na mke mdogo, kwani mke mdogo sio mgumba, ila mizimu imekasirika tu…

Sasa akahisi furaha ikimjia, akainua mikono ju kushuru, halafu bila kujitambua akaanza kucheza njiani, baadaye akagundua kuwa watu wanamtizama wanamuona yeye kachanganyikiwa akasimama huku kashika kiuno, alitaka kuwaambia kuwa yeye sio mgumba, kwa nguvu…

Lakini mara akakumbuka kuwa kuja kwake huku hospitalini ni kwa kujiiba, hapo kaanza kuharakisha. Furaha aliyo nayo akaona apitie sokoni anunua vitu vya kupika, na aliona siku hiyo ni ya furaha kwao kwahiyo anahitajika kupika kile chakula mumewe anachokipenda zaidi na ikizingatiwa kuwa leo ni zmu yake..

Kwahiyo akaptia sokoni  na huko akakutana na rafiki wa mume wake, na kwa vile alikuwa na baiskeli akasema atampa lifti huyu mama, na huyo mama akaona itakuwa vyema ili afike mapema. Basi aliponunua vitu wakaondoka pamoja na huyo rafiki wa mume wake hadi nyumbani kwao.

Huyu ni rafiki mkubwa wa mume wake na ndiye aliyekuwa mshirika mwenza wakati wa ndoa, na mara kwa mara huja nyumbani kwao kuongea, kwahiyo alimuona kama sehemu ya familia ya mume wake.

Wakati wanafika nyumbani, mume wake kumbe alishafika, alikuwa ndani, na mara akatoka, mama alipomuona mume wake akitokea mlangoni karibu aruke kwenye baiskeli, lakini hakuweza, hakutarajia kuwa mume wake angelikuwepo nyumbani muda kama huo , inaonekana alikuja nyumbani kwa dharura fulani, kwani sio kawaida yake kuonekana nyumbani muda kama huo.

‘Leo rafiki upo nyumbani …lakini mimi sikai nimemleta shemeji mara moja, tutaonana kijiweni…’akasema rafiki yake huyo na mume wake hakujibu kitu.

Kumbe mume wake aliwaona wakija na baiskeli kwa kupitia dirishani, aliwatizama kwa muda hadi walipokuwa wakifika na baiskeli toka mbali, wakafika na mama akashuka kwenye basikeli na mama kwa heshima akawa anamkaribisha huyo rafiki wa mume wake aingie ndani, lakini huyo rafiki wa mume wake akasema anataka kuwahi kwenye shughuli zake.

 Mumewe aliwaangalia kwa muda halafu bila kusema neno akaondoka zake. Mkewe moyoni akasema leo kutawaka moto, lakini alishazoea kupigwa,  akajionea kawaida tu, kwani ndivyo mumewe alivyo, akamshukuru yule jamaa, na kuondoka na baiskeli yake.

Mama yeye akaingia ndani kutayarisha chakula maalumu, akijua kuwa leo ni zamu yake, mumewe atakuwa kwake, na pia ni siku maalumu, ya kumpa mume wake taarifa muhimu ya furaha…!

Ilipofika jionii mumwe akarudi, kama kawaida yake alikuwa sio yule mume aliyekutana naye mchana, alikuwa akiyumba njia yote na watu wanaomfahamu wanakuwa mbali kabisa na yeye, na kama kawaida yake alikuwa akiimba nyimbo zote za utotoni, na wakati mwingine anasimama na kuanza kucheza, kama anacheza ngoma. Akafika nyumbani kwake, na kusimama mlangoni.

‘Wewe mwanamke fungua mlango au niingie naoooh’ akasema sauti ya kilevi, huku anatizama huku na kule

‘Au huyo mume mwenzangu bado yupo, maana haya maendeleo bwana, mkeee anataka awe sawa na mumeee, mume akiwa na wake watatu na mke naye anataka waume watatu…eeh, sasa huyo sijui kwako ni wangapi, wa pili eeh, au tayari wa tatu….’akawa anaongea.

‘Unasikia sana…sasa ruhusa, eeh, ruhusa, sio mimi nakuruhusu, hapana….nyie mnataka …mnataka…, sasa sijui kama mumefunga ndoa lini…nauliza lini hiyo ndoa imefungwa…naulizaaa, na nataka jibu leo hii…’akagonga gonga mlango kwa nguvu.

‘Mimi naona ajabu wewe ni mgumba, unataka waume wa nini, ili uhakikishe kuwa unazaa au huzai,…unajidanganya,  hata ukitembea nje nani atajua, eehe, hebu fungua mlango, nina washwa na mkono, natamani kupiga leo…, piga piga, piga mapaka damu itoke…’ akagonga mlango kwa nguvu, na kuupiga mateke, akakosa balansi na kudondoka chini.

Kila akijaribu kusimama anajikuta anadondoka chini, hadi mlango ulipofunguliwa na mkewe, na mkewe, akiwa na wasi wasi, akasalimia, na mumewe wakati huo anahangaika kuinuka juu, pale alipodondoka, na kila akiinuka anadondoka tena. Mkewe aliogopa kumsogelea kwani anamjua alivyo, anaweza akakushika mkadondoka wote na akaanza kukusindilia na migumi hapohapo chini.

‘Unaangalia nini we ma-layaa mkubwa…huyo mume mwenzangu yupo wapi…kaondoka au kalala ndani unaogopa kufungua haraka maana nimewafumania eeh,, na---ona mlikuwa mkipeana mapenzi….najua yule ni mtaalamu wa mapenzi…mmmh, ‘akasimama na akapepesuka na kudondoka chini.

‘Hii pombe ya leo kiboooko…hahaha, inaninyima starehe za kupiga,…najua …ngoja, ngoja,…umesema yupo ndani, eeh, mtaalmau wa mapenzi,…eeh,ngoja nikapambane naye, kama yeye ni mtaalamu basi mimi ni zaidi yake …’akasimama tena, akawa anayumba yumba.

‘Mhh,…ngoja nimkute atajua mimi ni mtaalamu wa nini…mimi anichukulie mke hivihivi…rafiki yangu mkubwa, toka ni toke, rafiki yangu mkubwa….kasimamia ndoa yangu, halafu leo, na mkweche wake, ana…ana kuja kunionyesha kuwa yeye ni kidume…aaah, yaani pombe ya leo waliweka nini…’ akajaribu kuinuka anadondoka!

Baadaye akasimama, na taratibu akaanza kutembea kuingia ndani, huku anapiga mruzi, akakagua kila eneo, nafikiri alikuwa akitarajia kumkukuta huyo anayemfikiria kuwa ni mgoni wake. Alipohakikisha kuwa hakuna mtu akajilaza sakafuni.

‘Mimi silali kitandani, najua hicho kitanda kimeshanajisiwa…nitalala hapa chini, na…na nasema sitaki usumbufu…umesikia wewe mwanamke..sitaki nini..u-su-mbu-fu…’ akaanza kukoroma.

Mama aliishiwa nguvu na kujiuliza sasa ataanza wapi, akaona asimwamshe aliyelala, akamtayarishia kile chakula mezani na akiingia chumbani kulala mpaka ilipofika asubuhi na mapema akijiremba vyema, akitaka kuitoa taarifa hiyo akiwa katika hali nzuri,akajiangalia kwenye kiyoo akaona sasa eeh, mume akiamuka akimuona hivyo na taarifa hiyo njema mbona itakuwa raha.

Kumbe mume pombe zilishamwishia na alikuwa kakaa nje akipigwa mswaki wa mti huku akiwa na mawazo yake mengi , hasira ...na alipanga akitoka hapo anamuendea huyo rafiki yake akampashe kuwa keshajua kuwa anatembea na mkewe...

Mke akamletea maji ya moto mume wake kwa tabasamu zuri mdomoni, mume wala hakuwa akimuangalia, akachukua maji na kunawa, bila kujali kusema neno, alipoamaliza akaingia ndani, alikaa kwenye kiti akisubiri chai, akatizama kile chakula mezani, akaguna na kusema.

‘Hiki chakula ulimpikia nani…’ akauliza huku kakunja uso

‘Mume wangu sinilikupikia wewe, jana umerudi umelewa, hukutaka kula wala kusemeshwa, basi nikaona nikifunike hapo mezani, lakinii nilikuwa na habari nzuri sana mume wangu…’akasema huku anajikalisha karibu na mumewe.

‘Habari nzuri eeh, najua umeanza, unataka kanga za harusi, sina hela za mchezo, na unasikia, marufuku kumuona yule mwanaume akikanyaga hapa tena, nimesikia taarifa zake, na ole wake, siku nikimuona humu, lake au langu na wewe utakuwa kitoweo cha mamba…unasikia wewe mwanamke..’ akasema huku anainuka kuondoka.

‘Lakini mbona kila siku anafika hapa na wewe ukiwemo na ndiye aliyesimamia ndoa  kwa upande wako, mimi nafahamu kuwa ni rafiki yako mkubwa, ndio maana sina wasiwasi na yeye akasema mama…’na mumewe akamuangalia kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Usitake nikaiharibu siku yangu,…hakuna urafiki kwa mke wa mtu, huyo huyo rafiki ndiye anayekuwa mbaya wako mkubwa, nimeshaambiwa habari zenu zote, ..anakuja hapa kwa kisingizia cha urafiki, na yeye keshajua huzai, basi anajimwaga tu,…hata ukitembea naye nitajua wapi, huzai,…wewe hujali,…nimeshaambiwa, na kama ungelizaa, najua mtoto angekuwa ni wa kwake..mimba itakuwa ni yake….’akageuka kutaka kuondoka

‘Mume wangu hayo ni maneno ya watu, nakuhakikishia mimi siwezi kusaliti ndoa yanu hata siku moja, sijui nani kakudanganya, ila nina habari nzuri nataka kukuambia, ….’akasema na mume wake wakageuka akiwa kakunja uso, akisubiri

Mkewe akaona asipoteze muda, akasema;

‘Mume wangu, nataka kukufahamisha kuwa mimi ni mja mzito, nina mimba mume wangu, hatimaye mungu katusikia duwa yetu nina mimba mume wangu……’akasema kwa furaha.


NB Haya, mume  ataupokeaje ujumbe huo.

WAZO LA LEO: Kwa wana ndoa na wachumba’z,  Kuweni makini na taarifa za watu ambazo hujazifanyia uchunguzi wa kina, `kuwa huenda mwenza wako anatabia chafu anafanya hiki na kile…’ hizo ni taarifa, inawezekana ikawa ni uzushi ili kuwaharibia, kwahiyo fanya subira na kama ni kweli utakuja kujua tu.Kwani tabia mbaya haijifichi ipo siku mbaya atafichuka.

 Kumbuka,  sio vizuri kushukiana ubaya kwa maneno ya kusikia tu, kwani sio kila atakyekuambia jambo ana nia njema kwako. 
Ni mimi: emu-three

No comments :