‘Wewe unakula tu, unanenepeana hapa kama
nguruwe, huna faida yoyote humu ndani, tangu nikuoe, huna hata mimba ya
kusingizia, angalia wanawake wa rika lako wana watoto wangapi, wewe hata
wakutuma chumvi dukani hayupo…’akasema akionyesha uso uliojaa hasira.
‘Mume wangu lakini mimi sijapenda iwe hivyo…’nikajaribu
kujitetea lakini hakunipa naasi akaendelea kuongea
‘Hebu niambieuna faida gani humu ndani, nilikuoa
ili uje kula tu hapa, ni lazima nikutafutie mwenzako, atakayeleta matunda ndani
ya hii familia…’ akawa anasema baba yako huku akitaka kunipiga, mkono
wake ulikuwa mwepezi sana kupiga.
Mimi nikawa nalia tu, nikijaribu kuwaza kosa
langu hapo lipo wapi, kwani mimi nimependa iwe hivyo, hata mimi natamani sana
niwe na mtoto, nikamwambia mume wangu kwa upole;
‘Mume wangu hata mimi natakani tuwe na mtoto,
lakini mungu hajapenda, kwanini tusivute subira haya yote sikuyataka mimi,
kuzaa ni majaliwa ya mungu, na kama ikiwezekana twende hospitalini tukaone
tatizo lipo wapi….’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho yaliyoja hasira na
kusema;
‘Wewe una tatizo, unasema twende wapi
hospitalini, unataka kunipotezea muda wangu kwa kwenda kwa hao wadanganyifu, …huna
kwa ujumla juma kizazi, nimeshaangalia kwa wataalamu wanasema huna kizazi, …’akasema
na kupanda kitandani kulala.
‘Ina maana kumbe alikwenda kwa hao waganga
wao, akaambiwa hivyo, kwanini hakunishirikisha’ nikawa najiuliza
‘Ni muhimu nikaongee na mama yangu mzazni
huenda akanisaidia, lakini nitafikaje huko, wazazi wangu walishanipiga maruuku
kwenda nyumbani mpaka mume wangu anipe ruhusa, na taarifa ipelekwe kwanza…mmh,
sasa ni nani atanisaidia,’nilikesha nikiwaza huku nikisikiliza mikoromo ya mume
wangu maana yeye akilala hukoroma kama simba, nikawa usiku sipati usingizi ,
nikajiona mimi ni mtu wa shida tu, hadi kufikia kujuta kuzaliwa mwanamke.
‘Pamoja na hayo yote mateso, kashifa na kejeli,
sikukaidi wala kukiuka sheria za ndoa, nikavumilia hadi ikatimia miaka mitatu ndani
ya ndoa, fikiria miaka yote hiyo hakuna siku unaweza kusema leo nina raha na
mume wangu, kila siku kuna kosa linabuniwa, kila siku kuna kupigwa au kutukanwa,
kusimangwa, na miaka ikaenda sikuwa na
dalili yoyote ya mimba..’akasema mama
‘Miaka mitatu , utajitetea nini tena,
nilitumia dawa za miti shamba nilizopata kwa marafiki zangu lakini hakukuwa na
dalili ya mimba, hata mume wangu kuna siku anakuja na dawa anasema kunywa hizi
huenda ugumba utaondoka, lakini hakukuwa na dalili hiyo hadi wanafamilia
wakakubali kuwa mimi kweli ni mgumba, sizai kwahiyo nina mawili, aolewa mke
mwenza, au niondoke kwenda kwetu….
Mimi nilitamani sana kurudi kwetu, na
niliposikia kauli hiyo kutoka kwa mawifi kuwa ni lazima kaak yao atafute mke
mwingine au niondoke hapo, mimi
nikamwambia mume wangu kuwa nipo tayari kuachika nirudi kwetu kuliko kuendelea
kuwatia hasara, yeye akasema kwa dharau;
‘‘Nikurudishe kwenu, unajua nimekulipia ngombe
ngapi, unajua baba yako namdai kiasi gani, hapa hutoki, utakaa hapa ili nifidie
ngombe zangu na mali yangu,kama huzai basi utakuwa mfanyakazi wa hapa…na hivi
karibuni tu nitakuolewa mke mwenzako…’akasema bila hata aibu.
Haikupita muda akaolewa mke mwenza....
Tuendelee na kisa chetu
************
Kweli akaolewa mke mwenzangu,
na jinsi ilivypapangwa hadi kuolewa huyo mke sikushirikishwa, ilikuwa joni
naona msafara wa watu unakuja na ngoma, kuuliza kuna nini, mawifi wakacheka kwa
kejeli;
‘Hehehe sasa huna lako,
mwenzako anakuja kuwa malikia na wewe utakuwa kijakazi wake…’wakasema
‘Mna maana gani ina maana
mume wangu kaamua kuoa bila kunishirikisha..?’ nikauliza
‘Akushirikishe wwewe kama
nani, hayo ni maswala ya kifamila na yeye ni mume wako ana maamuzi yote, hujui
tatizo ni nini, tatizo ni wewe, ….’wakasema
Basi mimi moyoni japokuwa
nasononeka, nikasema ni aheri maana adha na mteso ya kupigwa na kunyanyapaliwa
zitapungua maana atakuwepo mwenzangu …lakini haikuwa hivyo.
Haikuwa hivyo kwani
alipoletwa huyo mkwe mwenza nikawa mimi ndiye mhudumiaji wake mkuu. Kazi zote
nafanya mimi , mwenzangu kujipamba na kumtumikia mume wake, na siku ya zamu
yangu mume akija ilikuwa ni karaha tupu, na nilitamani hiyo zamu yangu isiwepo
kabisa, lakini utaratibu wa zamu haukuweza kupingwa, ni lazima jae kwangu, siku
za zamu yangu.
Mungu ana miujiza yake
kwani hata huyu mke mwenza aliyeolewa ndani nyumba kwa mbwembwe na vifijo naye
akawa kama mimi , mwaka ukapita hakuna cha mimba wala mtoto, ikawa ngoma sawa.
‘Ina maana na huyu
hajapata mimba, nahisi kuna tatizo, sio
bure, maana mtoto wetu kaangaliwa ahna tatizo sasa kwanini hata huyu hashikimimba..’wakawa
wanalalamika wanafamilia
‘Hili linahitajika
kuangaliwa zaidi, tusije tukawa tunafuga tatizo,..huenda kuna jambo hapa, ni
lazima tuhangaike..’akasema mzee mmoja wa familia, basi mke mwenza yeye akaomba
kwenda kwao kwa muda, akitaka akaonge na wazazi wake akakubaliwa tofauti na
mimi.
Alikwenda kwao kwa muda
baadaye akarudi, na akarudi na mapya, nikazushiwa maneno kuwa mimi ndiye
niliyemfunga mke mwenzangu kizazi, ili asizae. Haya yaliletwa na wazazi wa mke
mwenzangu. Walisema walipoenda kwa mganga imegundulikana kuwa mimi ndiye
ninayezuia mwenzangu asizae kwasababu mimi ni mgumba.
‘Hayo yametoka wapi tena,…’nikauliza
‘Ndio hivyo, sasa
utatuambia ukweli kwanini unafanya hivyo, hatutaki uchafu kwenye hii familia,
kama una mambo yako ya kiuchawi ni bora uyaondoe haraka….’akasema wifi yangu
‘Huo uchawi nitautoa wapi,
na ina maana kama mnadai mimi ni mchawi hata wazazi wangu ni wachawi mnaweza
kuyaongea hayo mbele ya wazazi wangu?’ nikauliza
‘Ataongea huyo mtaalamu
akija kuutoa huo uchawi wako..tutamuita, na hapo ndipo utaumbuka, yawezekana
umenunua, wazazi wako hawajui…’wakasema
‘Hilo sasa sitaweza
kuvumilia kama hamnitaki kwanini mume wangu hataki kuniacha nikaondoka zangu
kwetu…’nikasema
‘Huwezi kuondoka mpaka
gharama za mahari yako zilipwe, na pia mpaka uhakikisha umetoa uchawi wako…’nikaambiwa
Ikawa mumewe naye akirudi
ulevini kama na ni zamu yangu huja na matusi, vurugu na hata kusema kuwa ugumba
wangu unasababisha hata mwenzangu asizae, nikamuuliza kwa vipi. Akasema ipo
siku nitajua tu, kwani dawa bado ipo jikoni.
Kutokana na hali hiyo yeye
nasikia aliamua kutoka nje ya ndoa ili kuona kuwa ni yeye mwenye matatizo au
kuna jambo jingine, siku moja nikamuuliza kuwa mzaha, mbona nimesikia kuwa
anatembea na wake wengine wa pembeni.
‘Kuliko kufanya hivyo , kwanini asiongeze mke mwingine ujaribu Bahati
yako kwingine kuliko kutembea nje ya ndoa…’nikamwambia kwangu mimi sikuona tatizo, hata wakiwa kumi ndio vizuri
nipate muda wa kujipumzikia.
‘Usiniingilie katika maisha
yangu, ninaanya nipendavyo, na huwezi kunizuia, ..na nitaamua jinsi gani ya kufanya mimi mwenyewe...'akasema kwa hasira
'Aaah mimi nilikuwa nakushauri tu,...wewe si kidume, basi oa mwingine, ...'nikawambia na akaniangalia kwa hasira nikajua kipigo kinakuja na nimejitakia mwenyewe, lakini akaguka na kuangalia pembeni , nahisi hata yeye ilikuwa inamkwaza, halau akasema;
'Unajua , nimeshaahamu kuwa wewe ndiye mbaya kwenye
hii familia, kwa vile wewe umejiona ni mgumba unataka kila mtu awe hivyo,...nimeambiwa kamwe sitaweza kuzaa na wewe, kwasababu wewe ni mgumba, huna kizazi, ...na kwahiyo wewe unachofanya ni kuwaharibia wenzako, sasa sikia dawa yako inachemka…’akasema
‘Unasema nini, ina maana hata
wewe unakubaliana na hilo kuwa mimi ni mchawi, je hayo unaweza kuyaongea mbele ya wazazi wangu?’ nikamuuliza
‘Wazazi wako watanifanya
nini mimi, kwanza nawadai ngombe zangu
nyingi tu, nawadai mali nyingi na pesa nyingi tu, …’akasema kwa nyodo.
‘Kwahiyo mimi ninakuwa
malipizo kwa mambo yenu, na mnadiriki kunisingizia mamboya uchawi,…’nikasema
kwa uchungu
‘Hilo utajua wewe
mwenyewe, na kama unataa nioe mke mwingine nitaoa tu, si ndivyo mnavyotaka,
nitaoa hata kumi, kwasababu nina mali ya kulipa mahari, lakini sio kwa shinikizo la mtu,
nitafanya hivyo kwa muda wangu…’akasema
Dua la mja mwema
hukubaliwa lakini kwa wakati mwingine sio anavyotaka yeye mwanadamu, mungu anajua mwenyewe wapi na wakati gani wa kukutimizia maombi yako,huwezi
ukaomba na kupata hapo hapo...unaweza ukaomba wee mpaka ukakata tamaa, na ukaja kupta muda usiotarajia kabisa.
‘Nikawa nahisi kuumwa, na
kawaida mimi sio mtu wa kuumwa umwa ovyo, kama nikumwa labda niwe nimeumia
shambani au kuteguka, lakini magonjwa ya homa tumbo kwangu ni nadara sana…nikashangaa
kuhisi hali hiyo, mara tumbo mara najisikia vibaya hili ikanipa mashaka sana.,
Mwanzoni nilihisi labda ni
kutokana na vipigo, huenda vimeniletea madhara mwilini, nikawa najitibia kwa
dawa za kienyeji, lakini hakukuwa na dalili za kupona, nikamwambia mume wangu ,
mume wangu akasema;
‘Ndio hayo, tabia ya uvivu
wako,…kwanini usitinywe dawa za miti shamba, unajua dawa za tumbo ni zipi,
unataka kutega kazi tu hapa,sitaki kusikia tena hiyo kauli ya kuumwa…’akaniambia
Mimi nilishayazoea maneno
yake, mwishowe nikaamua kwenda hospitalini.
Siku hiyo niliondoka kwa
kujiiba na kufika kituo cha matibabu….maana baba yako hakutaka kusikia naumwa,
anasema ni uvivu wangu , nasingizia tu ili kutega kazi,..nikaondoka kwa kisiri
hadi kituo cha matibabu…’akasema mama.
‘Nilifika kituoni,
nilipitia shambani kama kisingizio, na nikavuga vuga hadi mume wangu akawa kaondoka, kawaida yeye
huondoka mapema kupitia kwa marafiki zake,hapo nikaondoka, hadi kituo cha
hospitalini, nikamuelezea dakitari, na vipimo vikachukuliwa, kwa vile
nilichelewa kufika, nikaambiwa nirudi kesho kuja kuchukua vipimo.
‘Kesho tena,kwani
haiwezekani leo..’nikalamika
‘Hatuwezi kutoa majibu leo
mpaka kesho,na taratibu za hapa umezisoma vyema …’akasema huyo docta , ni
mzungu alifungua dispensary yake, na watu wanaipenda sana, na yeye anafahamu
sana Kiswahili na hata lugha yetu ya kienyeji, kwahiyo watu wanakimbilia kwake
kuliko kwenye hospitaliz za kawaida na gharama yake sio kubwa sana.
Basi , mimi nikamuitikia
tu kuwa nimezisoma wakati sijazisoma, kailini nikasema `mimi hapa nimefika kutibiwa
sio kuangalia taratibu zao..wazungu bwana, kila kitu taratibu, sheria..hawajui
watanzania hatujali hayo..’
Na kesho yake nikarudi, nilifika
mapema kidogo maana ilikuwa sio zamu yangu na niliskia mume wangu kasafiri,
kwahiyo niliondoka mapema na kumkuta dakitari. Dakitari akaniuliza
‘Mume wako yupo wapi,….?’
akaniuliza
‘Mume wangu, …unanichekesha
kweli, hata kuja hapa kutibiwa nimefanya kama kutoroka, hataki hata kusikia ninatibiwa
hospitali, yeye anaamini dawa ni za kienyeji tu…’ nikamwambia dakitari, na
dakitari akaniangalia usoni, akionyesha kitu kama mashaka, na nikahisi majibu
sio mazuri na sijui nina tatizo gani
Dakitari akasema;
‘Haya majibu yako ni
vyemaa angelikuwepo mume wako ili nyote myasikie na ikibidi na yeye pia apate kupimwa,
hiyo ndio inatakikana, na ndio taratibu zetu,…’akasema
‘Lakini yeye haumwi na
kama nilivyokuambia yeye haamini matibabu ya hospitalini, hatakubali kuja…’nikasema
‘Ni vyema urudi uje naye,
mwambie ni muhimu sana, na ni muhimu pia na yeye asikie majibu ya vipimo hivyo..yanataka
nyote wawili muwepo…unasikia haya nenda kamuite..tafadhali’ akasema. Mama
kusikia hivyo wasiwasi ukamwingia, akamuuliza dakitari;
‘Kwani nina ugonjwa gani
mbaya kiasi hicho mpaka na mume wangu awepo…?’ nikauliza.
‘Sijasema una ugonjwa
mbaya, hakuna ugonjwa mbaya,…ni muhimu sana hasa katika taratibu zetu za hapa haospitalini
mje wewe na mume wako…’akatulia
‘Nia yangu ni kuhakikisha
wote mnatibiwa, mnajua tatizo ni nini, au kuna matokeoa gani, kuna mambo tunataka kuyapiga vita, hasa hili
la kuja kutibiwa mke peke yake au mume peke yake…’akaangalia ile karatasi kama
anataka kusoma majibu ila akasita na kusema
‘Unajua piaa kuna magonjwa
yanahitajia muwepo wote wawili ili iwe rahisi kwetu kutoa maelekezo, na
matibabu pia…ndio maana nataka na mume wako awepo ili mpate majibu yenu kwa
pamoja, na matibabu pia, na pia ndio utaratibu wetu wa hapa hospitali…’akasema
dakitari.
‘Mungu wangu…’nikasema
huku nikiwa nimeshika kichwa kwa mikono yangu miwili..
‘Dakitari nimeshakuambia
kuja hapa nimefanya kujiiba…wewe hunielewi, mume wangu akisikia nimekuja huku
kutibiwa ataniua, na hata hivyo kwani kuna tatizo gani kubwa mpaka yeye awepo…..ina
maana nina ugaonjwa mbaya sana, au….oh, au nimeathirika, na hilo gonjwa la…ooh,
docta niambie kama ninao nijue moja….?’nikasema kwa wasiwasi maana nilishasikia
mengi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, nikajua ndio maana dakitari anaogopa kunipa
majibu yangu.
Docta akaniangalia kwa
mashaka, akainua karatasi ….
Naona kwa leo tuishie
hapa, tuwepo kesho kusikia nini majibu ya vipimo hivyo na kwanini dakitari
akashauri kuwa ni muhimu mumewe awepo!.
WAZO LA LEO: Ni vyema mke au mume anapoumwa, mkawa
mnahurumiana, mnasaidiana, na mkienda hospitalini muwepo pamoja, kwani mume na
mke ni kitu kimoja, na mmoja akiumwa ni sawa kama wote mnaumwa, lakini pia kuna
magonjwa ya kuambukizana, mkiwa pamoja ni rahisi sana tatizo hilo likatatuliwa kwa
haraka. Kumbukeni kiapo chenu cha ndoa kuwa mnaoana na kuwa kitu kimoja na mtakuwa
wote wakati wa shida na raha, kwahiyo kujaliana
wakati wa matatizo hasa ya ugonjwa ni moja ya masharti ya ndoa, na pia hujenga
mapenzi ya dhati.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment