Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, October 30, 2014

DUNIA YANGU-55


‘Bora upige simu huko hospitali, uthibitishe hilo, ni moja ya vitu alivyokuwa akiniuliza mkuu wetu wa kazi, hasa kuhusu mashahidi, …alihofia pia na hayo mambo ya kisiasa, na kiuchumi, ujue yeye anaangalia kote kote, na anawasiliana na wakuu wa nchi,….tumeongea naye mambo mengi tu, ana wasiwasi kuwa hao mashahidi wataitwa mahakamani washindwe kujielekeza na hapo itakuwa ni aibu kwetu...’akasema

‘Mkuu anaumwa, hawezi kujua afya za hao watu, hili ni jukumu letu, na wewe ndiye mwenye mamlaka kwa hivi sasa, je wewe unahisi halitawezekana hili, wakati sisi watendaji wako tumeshakuthibitishia, wewe upo kwa niaba yake, ina maana asipokuwepo na kazi hazifanyiki....’akasema Moto

‘Kazi zinafanyika, ili uone kuwa mimi nahangaika huku na kule kuhakikisha kazi zinafanyika hebu piga simu huko hospitalini, uhakikishe, ni muhimu sana, kama wapo tayari nitamuondoa wasiasi mkuu, ....’akasema na moto akapiga simu hospitalini

‘Je wale wagonjwa, tuliowaleta hapo wanaendeleaje?’ akauliza na kusikiliza kwa muda, halafu akasema;

‘Mbona hamkuniambia mumekaa kimia na mnajua hao ni watu muhimu mahakamani kesho..’akasema moto na kusikiliza kwa makini, baadaye akasema kwa mshangao

‘Ina maana, Msaidizi wa mkuu anajua, mlishamuambia, haiwezekani kwanini, hajaniambia, munengeniambia mimi kwanza, yeye alihitajika kujua kutoka kwangu, nini, alifika hapo...’akasema na kumgeukia msaidizi wa mkuu, halafu akakata simu

‘Mkuu kumbe uliambiwa kuhusu hali ya hao watu kuwa bado hawajagundua tatizo ni nini, wamepewa dawa ya kuwasaidia lakini hazifanyi kazi, wanasema hao watu bado wana hali mbaya, kumbe walishakuambia na ulifika huko,…lakini hukunipa hiyo taarifa..’akalalamika

‘Ndio maana nikataka uthibitishe wewe mwenyewe,…, hii ilikuwa ni kazi yako kuhakikisha hayo, unaona jinsi gani unavyopeleka mambo yako kwa pupa, ,…. Na ndio maana nilipoongea na mkuu wetu, akasema kwa hali hiyo inabidi tuahirishe hii kesi kwanza ili tuweze kupitai kwa pamoja hatua kwa hatua....’akasema

‘Kesi haitaahirishwa mkuu, kwasababu ya watu hao,ndio ni mashahidi muhimu sana, lakini wapo wengine,...kuna mashahidi wengine watasimama kabla yao na wao ni muhimu vile vile...’akasema Moto

‘Hao ni muhimu zaidi, ulisema mwenyewe kwenye kikao, na ni kweli ni muhimu zaidi, na ukiangalia afya zao zipo mashakani,….nielewe lengo langu hapo nini, agizo la mkuu, hao mashahidi afya zao, na ukamilifu wa kila kitu kinachohitajika mahakamani…’akasema

‘Kesi ipo pale pale mkuu…..

Tuendelee na kisa chetu

**************

Inspecta Moto akamsogelea Maneno pale alipolala, akamuinamia kusikiliza anataka kumuambia kitu gani, alichosikia na maneno haya kwa shida sauti ilikuwa ya kukwama kwama, kama mtu anayeongea kutoka usingizini;

‘Na-na-omba uni-ni-samehe rafiki yangu…nafahamu, nimekukosea sa-sana rafiki yangu, lakini usichoki-ki-kijua ni sawa na usiku wa giza, sikudhamiria..mmmh iwe hivyo, …’haya maneno aliyasikia kwa ukamilifu japo ni kwa sauti ndogo sana, akamuuliza

‘Sasa nikusamehe kwa lipi?’ akamuuliza

‘Kwa hali ilivyo,najua mimi nakufa, nasikia ikipita masaa..kama 120, tutakuwa hatuwezi kutibika tena,…na…na docta, hamjampata..huyo ndiye anaweza kuyaondoa haya madawa mwilini mwetu,….,na nia yao ni sisi tufe kabla ya kufika mahakamani, nahisi siku zetu zimeshafika, …ila nataka, ku-ku-ambia wazi ku-husu Mke wako…kanitokea, anaomba haki….anataka haki itendeke….’akasema kidogo kwa uelew mzuri

‘Mke wangu ?, kwanini anakuomba wewe haki..na haki ipi itendeke wakati ulisema alijiua mwenyewe?’ akamuuliza

‘Yah, ni hio, ila kwasasa, jamni mtafuteni docta haraka, Nataka nisimame mwenye-we mahakamani…..nataka nise-seme ukweli wote, nitu-tubu yote mbele ya mahakama, hata kama niku-ku-kufa nife tu, hata kama watafaya hayo wanayonitishia nayo, siogopi tena, siogopi kuchafuliwa hadharani tena, lakini, sa-sa..lakini siwezi mwili hauna nguvu….aaakh, …’akaanza kukoroma

Inspecta Moto akamuangalia msimamizi wa kesi, aliyekuwa nyuma yake , na msimamizi yule akatikisa kichwa cha kukata tamaa. Walifika hapo walipopewa taarifa kuwa Maneno ana kiu anataka kuwaambia.

‘Ni lazima kwa haraka huyu docta apatikane, kama alivyosema Maneno muda wa kuweza kutibiwa hawa watu, hitakiwi isizidi masaaa 120, unafikiri sasa yamebakia masaa mangapi, tangu walipopigwa hizo sindano,…lakini tukimpata huyu docta atajua jinsi gani ya kuwasaidia, hata kama hayo masaa yatakuwa yamekwisha…

‘Sasa tutampata wapi huyu mtu, maana sehemu zote, tumetafuta, na mke wake ndio huyo tumemshikilia tukijua kuwa tukifanya hivyo, atajileta mwenyewe, lakini haijawezekana, labda hawa wazazi wake watasaidia, hata tukiwaweka hewani kwenye radio na Tv, waongee kumsihi aje, inaweza kusaidia, lakini tunapigana na muda….’akasema Moto

‘Mimi nahisi huyu mtu hayupo nchini, anaweza kutumia njia nyingine na kupita mipaka, huenda keshavuka mipaka kwa hivi sasa,…’akasema

‘Hapana, hilo tumehakikisha kuwa hawezi kufanya hivyo, hawezi kupita mipaka ya nchi, najua kundi lao lina watu kila sehemu, lakini hata sisi tumeweza kuwaweka watu wetu waaaminifu sehemu zote hizo….hajaweza kuvuka mipaka ya nchi, atakuwa humu humu nchini,…’akasema Moto

‘Hebu subiri…..’Moto akasema na kuchukua simu yake, akapiga namba za nje, alitulia kidogo na baadaye alipempigia akawa hewani, akaiweka sauti kubwa ili muendesha mashitaka naye asikie anachoongea huyu binti.

‘Mrembo Jembe samahani kwa kukusumbua najua saa hizi umelala, …au nimekosea ..?’ akauliza

‘Ni kweli kabisa na kesho kuna mitihani, ..ooh, kuna nini tena huko jamani?’ akauliza

‘Samahani sana, kuna jambo limetutatizo, kwanza tunashukuru kwa mchango wako, umetusaidia hadi tumeweza kubaini chimbuko la hili kundi, na sasa tupo mbioni kuhakikisha mzizi wa mwisho unang’olewa,…najua kuna mambo mengi hata wewe ulikuwa huyafahamu,…’akatulia

‘Kwani mumeweza kumpata huyo docta, na..na yule mtaalamu wa mtandao, docta ndiye anaweza kumsaidia huyu mtaalamu wa mitandao, kutokana na madawa waliyomdunga nayo, hao wawili ndio watu muhimu kwenye kundi, ama kwa huyo kiongozi wao kwakweli sikuweza kumtambua ni nani hasa,..nilifanya kila njia sikuweza kabisa, hata Maneno mwenyewe hamfahamu..asije akawadangana…’akasema

‘Ninachotaka kujua kutoka kwako, huyu docta hana sehemu ambayo unaweza kuhisi kajificha huko kwani katoweka kabisa hatumuoni, hatujui kajificha wapi,..nakumbuka kuna siku ulisema uliwahi kwenda naye sehemu zake maalum anapotengenezea madawa….?’ Akaulizwa

‘Oh, sizani kama anaweza kwenda kujificha huko..lakini kajaribuni kuangalia huko,…sehemu nyingine ni kwenye saluni za mama urembo, mle kuna yumba vya siri, kuna watu walikuwa wakiingizwa huko kwa siri wakafichwa hata mwezi mzima hawajulikani walipo, ….ni swala la kujaribu au sio….’akasema mrembo jembe

‘Ok, tunashukuru sana..pole sana kwa usumbufu, ila ukumbuke kesho ndio kesi, na huenda tukakuhitajia kwenye mtandao, ikibidi lakini,…’akaambiwa

‘Hamna shaka mimi nipo pamoja na nyie, na nitashukuru sana kama kundi hilo litamalizwa kabisa ili na mimi niwe na amani, je Maneno amaweza kuongea chochote,…kuhusu mke wako?’ akauliza

‘Kaniambia mhh, kaomba samahani tu, ila, kasema ataongea mahakamani….’akasema

‘Ana mengi sana anayajua yeye hasa kuhusu mke wako,….moyo wangu hapa unaniuma kuona kwamba na mimi  japokuwa ilikuwa kikazi, lakini nilihusika kufanya mke wako ajiue..inaniuam sana..’akasema

‘Usijali,..haki itatendeka, mimi nina imani kuwa ubaya hauna mwisho mwema, na mara nyingi ubaya huishia kubaya, yote yana mwisho, na hili najua mwisho wake umeshafika, na mke wangu atatulia mahali pema peponi huko alipo…’akasema Moto, akionyesha hisia za huzuni usoni, na kukata simu, na muendesha mashitaka alipoona ule ukimia akasema;

‘Basi tusipoteze muda, watume vijana wako,au niwatume vijana wangu, kama vijana wako umeshawapa kazi nyingine…’akasema

‘Yote sawa….ngoja nifanya hivi….’akasema Moto na mara simu yake ikalia, akaangalia mpigaji, akaona ni mmoja wa vijana wake.

‘Nimbie kuna lolote jipya?’ akauliza na kusikiliza

‘Hakikisheni hakuna mtu kutoka hapo au kuingia, na usimwamini mtu yoyote, huyo ni mtu ni muhimu sana, najua hataweza kuamuka kutokana na hayo madawa, lakini hatuwezi kujua zaidi…unasikia, hakikisha kila saa moja unaingia kuhakikisha kalala….unasikia, usimwamini yoyote yule kuingia humo, tusije kuwajibika kwa kosa dogo…’akasema moto na kusikiliza kwa muda, halafu akasema;

‘Ni nani, msaidizi wa docta, anataka nini, hebu nipe niongee naye…..’akasema na mara kukatulia

‘Yes docta unasemaje?’ akaulizwa na Moto akawa anasikiliza, na baadaye akasema;

‘Ujue wewe ndiye utakayekuwa karibu na huyo mtu kama akihitajika, ..ujue mwenzako hayupo, na wewe unabeba dhamana yote, ujue lolote litakalotokea utabeba dhamana,hakikisha usalama wake

‘Sisi tunahangaika na kesi, na hii ni kesi kubwa, na wewe ulitakiwa ukamatwe kwa kuwashikilia hawa wagonjwa kwenye hospitali yako, sasa ili wewe ujikoshe kuwa ulikuwa huhusiki ni lazima ushirikiane na serikali, vinginevyo, na wewe utawajibika…’akaambiwa na Moto akawa anasikiliza kwa muda, sasa akaiweka hewani ili muendesha mashitaka naye asikie anachoongea huyo docta

‘Kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu wa vitisho….’akasema

‘Ujumbe gani huo, hakuna mtu wa kutuma ujumbe kwa hivi sasa, tumeshadhibiti kila sehemu, watu wa mitandao wote waliokuwa wakihusika tumeshawakamata, hakuna mwenye uwezo huo tena,…hebu angalia huo ujumbe umeandikwa lini,..?’ akaulizwa

‘Mhh, naona kweli sio ….tarehe za nyuma, mbona ndio naupata leo…’akasema

‘Unaonaeeh,  huo ujumbe uliwekwa hewani ili ufike kwako baadaye,..sizanii kama  kuna mtu mwingine anayefanya hiyoo kazi tena, wote wapo mikononi mwa polisi..’akaambiwa

‘Docta Chize mumeshamkamata?’ akauliza

‘Bado…lakini tupo mbioni unaweza kutusaidia kwa hilo kama kuna sehemu yoyote tunayoweza kumpata?’ akauliza

‘Kwakweli zaidi..hapana, lakini Mhhh…yes, ndio maana nataka tuonane haraka iwezekanavyo….’akasema na Moto akamgeukia muendedha mashitaka na kusema

‘Sawa wewe fanya hivyo, tuonane wapi unapohisi kunafaa…?’ akauliza na kukawa na ukimia fulani, Moto akasema;

‘Basi tunakuja huko huko hospitalini, tusubiri huko huko tunakuja….’akasema na kukata simu

‘Msaidizi wa docta Chize, ndiye huyo anasema tuonane naye, huenda anafahamu wapi alipo bosi wake, lakini nahisi kama anaogopa jambo, au keshawasiliana na mtu bosi wake, mimi naona twende tukaonane naye ….’akasema

‘Hapana watume kwanza vijana wako, inaweza ikawa ni mtego,…watume vijana wamchukue na yeye awe kwenye kundi la washitakiwa, naona hatuna haja ya kumuweka huru tena huyu mtu, wote tunaowashuku tuwakamate…’akasema msimaizi huyo wa kesi hiyo, na Moto akawapigia vijana wake simu waifanye hiyo kazi, na haikupita muda, taarifa ikaja; Inspecta akahakikisha simu inasikiwa na mwenzake

‘Inspecta Moto….’sauti ikaita kwenye simu

‘Nani mwenzangu?’ akauliza Inspecta Moto

‘Mimi ni docta Chize…..’sauti ikasema

‘Nikusaidie nini…’akasema Moto akimgeukia muendesha mashitaka na dole gumba hewani kuonyesha ushindi

‘Usalama wangu, na familia yangu, nasikia mumewakamata wanafamilia wangu, wakiwemo wazazi wangu….lakini mjue kuwa mimi nilikuwa natumiwa tu, kwanini mnawasumbua wazazi wangu, hiyo sio sahihi kabisa…..’akasema akionyesha kuhuzunika

‘Muhimu ni wewe kujitokeza, unafahamu kabisa kuwa hatupendi hilo, ila tunafanya kwa vile wewe umejificha, tuambie wapi ulipo kama kweli unawajali wazazi wako…’akaambiwa

‘Siwezi kuwaambia nipo wapi, maana nyie hamuwajui hao watu mnaopambana nao vyema, mitandao yote inasikilizwa, wana masikio mapana ya kusikiliza kila kitu  na macho makubwa ya kuona kila kitu..’akasema

‘Hakuna wakufanya hivyo tena, kila kitu tumeshakidhibiti, hilo nakuhakikishia….hatuna muda wa kupoteza tena, hii ni nafasi yako ya mwisho, jitokeze ujikoshe, utubu madhambi yako, na uwaweke wazazi wako kwenye moyo wa utulivu..’akaambiwa

‘Mkuu wako allinitumia ujumbe kuwa ananihitajia…lakini sikuweza kumuona, nina wasi wasi na usalama na afya yake, alkini pia naogopa usalama wangu, ni hatari tupu kwa hivi sasa je nyie mpo wapi?’ akauliza

‘Usijali,..hilo tumeshalishughulikia, hali ya mkuu wangu ipo kwa madocta sahihi,  inaendelea vyema, na yupo salama, usiwe na shaka naye, muhimu ni wewe kujitokeza…kwasababu ya hao watu uliowadunga madawa, unajua muda gani yanatakiwa yatolewe mwilini, ukichelewa, wakadhurika, ujue wewe ndiye muuaji wao…’akaambiwa

‘Najua, najua….ok, tutakutana mahakamani…’akasema na simu ikakatika. Moto akamgeukia Muendesha mashitaka na muendesha mashitaka akauliza

‘Unamwamini huyo mtu…?’ akauliza

‘Kwa hali ilivyo hivi sasa ni lazima tumuamini, unajua wazazi ni kitu kingine, huyu mtu anawajali sana wazazi wake,na ndio maana aliposikia kuwa hata wazazi wake wamekamatwa, akaamua kujitokeza, hata hivyo vijana bado wanamtafuta na atapatikana tu….’akasema Moto.

***********

Asubuhi kukapambuzuka, japokuwa wengine hawakulala kabisa wakihangaika huku na kule, kuhakikisha mambo yote muhimu yanapatikana, Inspecta Moto, alikuwa kaegemea kwenye kiti, ili angalau apate dakika tano za usingizi, alilala kidogo na ghafla akazindukana, na kusimama, akawa kama kakumbuka jambo;

Alisimama akajinyosha kuhakikisha mwili upo salama, akapiga simu kwa vijana wake kuhakikisha kuwa kila kitu kipo salama, halafu akatembea kuelekea ofisi ya muendesha mashitaka, kwani wote walikutana kwenye ofisi hiyo ya muendesha mashitaka, akafungua mlango wa ofisi yake, akamkuta mwenzake naye alikuwa akipata dakika tano za usingizi, na alipomsogelea tu jamaa huyu akainua kichwa na kusema;

‘Bado mapema bwana, hebu tupate usingizi kidogo, tunauhitajia sana huu usingizi…’akasema akipiga miayo

‘Kuna kitu kimenizindua, unakumbuka nilikuambia kuwa niliokota ‘external hard drive’  ipo kama simu, ina fanya kazi zote simu na pia inahifadhi kumbukumbu za komputa, unakumbuka eeh,….’akasema na mwenzake akatikisa kichwa kukubali

‘Nilijaribu kuitizama kwenye komputa ikakataa kufunguka,nikampelekea kijana wangu mmoja mtaalamu sana wa mambo hayo, kaishughulikia, na jana alinipigia simu kuwa sasa inaweza kuwaka, ila inahitajika ukarabati wa kimtandao na hilo litachukua muda, wa masaa kama kumi na mawili….’akasema

‘Sasa ya nini kwa hivi sasa, sioni kama itatusaidia kitu..?’ akaulizwa

‘Nimeota , mke wangu, akiwa na mama wa marehemu mmiliki wa hiyo hoteli, wameniambia kuwa kila kitu kipo kwenye hiyo ‘external hard drive’…unakumbuka ni wao walinielekeza kwenye ndoto kuwa niende pale nitakiona hicho kifaa, sasa wananiuliza nimekiangalia,…kabla sijawajibu ndio nikazindukana…’akasema

‘Lakini kama haifunguki, itasaidia nini kwa hivi sasa ujue saa tatu asubuhi tunahitajika mahakamani, kuna mambo ya kupitaia pitia kabla hatujasimama mahakamani, tuliza kichwa , achana na kitu kingine kipya…’akasema muendesha mashika akipiga miayo

‘Mimi naona hiyo kitu ni muhimu sana,…nina imani itakuwa imeshafunguka, nilimuambia ikiazna kufunguka natakiwa niione mwenyewe, sitaki mtu mwingine, aone kilichopo kabla yetu,…. ngoja nimpigia simu huyu kijana,mmmh, naona hapokei simu, hapana ni lazima nimuone, nahisi bado kalala …..’akasema akitembea kutoka nje

‘Sasa unakwenda wapi?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Nitarudi hoa nikichelewa tutakutana mahakamani….’akasema na kuondoka


WAZO LA LEO: Sio kila jambo la heri laweza kirahisi tu, kuna mambo mengine huja na mitihani yake, lakini mwisho wake huwa ni neema, na furaha kama utakuwa mvumilivu na kusimamia kwenye haki.Halikadhalika mambo ya ubaya, yana mvuto wake, usipokuwa makini unaweza kuzama kwenye giza nene, na mwisho wa ubaya ni kudahalilika, na kuumbuka, na kawaida majuto huja baadaye, kama utafanikiwa kujinasua. Tujitahidi sana kuwa makini katika matendo yetu, tusivutike tu kwa tamaa, tuangalia uzuri na ubaya wake kwanza.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Rachel siwa Isaac said...

Akhsaaante kwa wazo la leo..
kazi nzuri mtu wangu...
Pamoja Daima.