Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, September 23, 2014

DUNIA YANGU-35


Yule binti akaondoka kwa shingo upande, hakuweza kupingana na baba yake, aliondoka akiwa mnyonge sana. Alitamani hata kulia,hata hivyo hakuwa na uwezo wa kufanya lolote, akatembea taratibu kuelekea shambani, akimuacha baba yake akitengeneza dawa zake.

Moyoni alishaingiwa na kitu, licha ya huruma, lakini alihisi kuingiwa na kitu kipya moyoni, hakutaka kuachana na huyo, alitamani awe karibu naye, sasa kusikia kuwa anataka kuchukuliwa na watu, na watu wenyewe huenda wana nia mbaya, akajihiis kuumua sana.

‘Sasa nifenyeje, kumuokoa huyo mtu..?’akajiuliza, na mara akasikia gari likija, akajificha kichakani,…na alipoona lile gari likikaribia nyumba yao akajua basi, huyo mtu keshachukuliwa, ..

‘Hata jina lake simjui…’akasema huku akiomba kwa mungu amsaidie huyo mu asichukuliwe.
Pale alipojificha alimuona baba yake aiendelea kutengeneza dawa zake, na hakuonyesha wasiwasi, akawaona watu wakitoka na silaha, na mtu mmoja akamsogelea baba yake na kwa sauti ya mbali akasikia yule mtu akimuuliza baba yake maswali.

Alikaa pale akiwa na wasiwasi, akijua watamzuru baba yake, Na mara akahisi kitu nyumba yake alipogeuka akazibwa mdomo..akajua na yeye keshakamatwa na hao watu wabaya.

Tuendelee na kisa chetu…

***********

‘Yupo wapi huyu mtu….?’

‘Kwani nyie ni nani?’ akauliza mzee.

‘Wewe mzee unakumbuka tuliongea wote kwenye simu ukasema kuna mtu wetu hapa, …’akasema.

‘Mliongea kwenye simu na mimi?’ akauliza kwa mshangao.

‘Mzee usitupotezee muda, sisi tumekuja kumchukua mtu wetu, na wewe tunakukabidhi chako…ujue sisi ni askari hatuna muda wa kupoteza hapa…’akasema huyo mtu akigeuka kutoa ishara kwa mtu aliyekuwa kabakia kwenye gari, na huyo mtu akaja akiwa na bahasha kubwa iliyotuna.

‘Unaona sisi hatutaki longo longo, humu kuna milioni kumi na tano, kama huyo mtu wetu yupo hapa, hii hapa ni zawadi yako yote….’akasema.

‘Ingieni ndani yupo kalala, lakini bado naendelea na matibabu yake hamuoni hapa ndio namtengenezea dawa yake…’akasema huyo mzee akiuangalia ule mfuko kwa hamasa.

‘Usijali, kama ni dawa zake tutazichukua atakwenda kuzitumia huko mbele kwa mbele, ni mu wetu tulijua ameshakufa, siumeona kwenye gazeti walivyoandika, …kuna watu wabaya walimteka nyara,..tunashukuru sana mzee umemponyesha,…’akasema lakini kabla hajamaliza mtu mmoja aliyeingia ndani akatoka na kusema;

‘Mbona hayupo, ….’akasema huyo mtu akiwa kashikilia silaha, na wenzake wakatoa na kutoa maneno hayohayo.

‘Mimi sielewi…maana asubuhi nilitoka kwenda kuzitafuta hizi dawa, nikamuacha akiwa kalala, na dawa nilizompa zausingizi asingeliweza kuamuka, ..nahisi basi kuna mtu kaja kamchukua, maana haiwezekani…’akasema huyo mzee akitaka kungia ndani.

‘Mzee usitupotezee muda wetu, hebu tuambie huyu mtu yupo wapi?’ akauliza huyo jamaa sasa akiwa kabadilika na akawa anamsogelea mzee kwa hasira.

‘Kwakweli kama hayupo huko ndani, siwezi kujua wapi alipokwenda, na haiwezekani dawa aliyotumia ina nguvu sana?’ akasema

‘Ulipoondoka ulimuacha humo ndani na nani…?’ akauliza

‘Nilimuacha peke yake, maaana nina uhakika kwa hizo dawa alizokunywa za usingizi asingeliweza kuinuka, …hizo dawa zina nguvu sana…’akasema akiogopa kusema alimuacha na binti yake.

‘Mzee unazikosa hizi pesa hivi hivi, na pia unajiweka katika mazingira magumu ya kuvunja uaminifu wako…’akasema huyo jamaa akiwa kashikilia ile bahasha akiichezesha chezesha mkononi.

‘Mimi nina uhakika yupo ndani, asingeliweza kuondoka, kwa hizo dawa..ngojeni nihakikishe..’akasema na kuingia ndani,na haikuchukua muda akatoka, na kusema

‘Kweli hayupo…sijui kaenda wapi, na sizani kama atakuwa katoka mwenyewe…haiwezekani….’akasema

‘Tafuteni kila mahali,…tusipomuona huyu mzee atawajibika, tutaondoka na kichwa chake…’akasema yule mtu na yule mzee aliposikia hivyo akasema

‘Kichwa changu kinahusu nini, mimi nimejitolea kuwaambia ukweli, ndio mnataka kulipa fadhila, kama kweli alikuwa mtu wenu mngelinishukuru kuwa nimemsaidia akapona, sasa mnataka kuniua,…’akasema

‘Kumdaidia kwako hakutusaidii sisi, ungelikuwa na maana kama huyo mtu angelipatikana, sasa ama kichwa chake ama  kichwa chako ndio maagizo tuliyopewa….’akasema

‘Kumbe nyie watu ni watu wabaya eeh, mnataka kuniingilia kwenye himaya yangu ..manataka kuingilia himaya ya Ndumba eeh, haya tuone….’akasema na kusogea pale kwenye dawa zake akatoa kichupa kidogo akatoa unga unga akarusha hewani na kusema maneno yasiyotambulikana.

Yule jamaa akawa anamuangalia tu kwa dharau mara kukatanda moshi mkubwa sana uliokuwa ukikereketa na yule jamaa na askari ambao walikuwa wakihangaika huku na kule, wakaanza kukohoa na kuanza kupepesuka..

‘Wewe mzee ndio umefanya nini…unatujaribu na uchawi wako, ngoja tuone uchawi na risasi ni kipi chenye nguvu, wewe ni lazima ufe…’yule jamaa akajaribu kuinua silaha kutaka kumlenga huyo mzee lakini hakuweza akadondoka chini…na wala jamaa wenzake waliokuwa wamerudi kutoa taarifa kuwa hawajamuona mtu wanayemtafuta wakakutana na huo moshi, wote wakadondoka chini.

Yule mzee kwa haraka akakusanya zile silaha zao na kuzipeleka nyuma ya nyumba na alipomaliza kufanya hivyo , akachukua kamba akawafunga wale watu na alipomaliza akaingia ndani na haikupita muda akatoka akiwa na mkoba wake begani…

Alipofika hatua chache akakumbuka jambo, akarudi na kuchukua ile bahasha kutoka kwa yule mtu akaangalia ndani kulikuwa na pesa nyingi tu ambazo hajawahi kuzishika maishani….

Akasogea hadi kwenye gari la hao watu akaliangalia, akakumbuka ujuzi wake wa kuendesha, lakini hakuwa na uhakika, hata hivyo hakujali akaingia na kuanza kuliwasha hilo gari, lakini hakuweza, na kabla hajakata tamaa mara akasikia sauti ya watu wakikohoa kwa mbalia

Alijua na hao watu wengine, walikuwa hawajarudi, akatoka kwenye lile gari na kuanza kukimbia, lakini sauti ya binti yake ikamfanya ageuke nyuma;

‘Baba…ni sisi…’akageuka na akatoa kichupa cha dawa, akawasogelea, walikuwa binti yake wakiwa na mgonjwa wao, akawapaka hiyo dawa puani, na kusema;

‘Unajua juendesha …?’ akamuuliza mgonjwa wao.

‘Ndio …’akasema Inspecta

‘Tuondokeni hapa haraka maana hapa kuna hatari…’

‘Kwani kumetokea nini?’ akauliza Inspecta ambaye bado alikuwa na mawenge mawenge kichwani

‘Hao watu walikuja kukuchukua wewe, na kauli yao ya mwisho ni ama kichwa chako au kichwa changu…’akasema

‘Sasa umewafanya nini?’ akaulizwa

‘Wanacheza na mizimu ya kwetu nimewafunga msukule, hapo hawawezi kuamuka mpaka nipende mimi mwenyewe,lakini nahisi kuna hatari hapa ni bora tuondoke haraka…’akasema

‘Twende wapi, maana hawa watu wana pesa watatusa hata kwa kutumia  ndege angani au mbwa wa polisi…’akasema

‘Kwahiyo tufanyeje…?’ akauliza huyo mzee

‘Tatizo ni wewe na familia yako je familia yako ipo karibu , je ukiondoka watakuwa salama?’ akaulizwa

‘Kuhusu familia yangu usiwe na wasiwasi nao, nitaikusanya huko mbele muhimu tuondoke hapa….’akasema

‘Ok sawa…’akasema Inspecta akijitutumua kusimama, akili sasa ilishakaa vyema,kutokana na dawa za huyo mzee aalizo mpaka tena puani, wakaingia kwenye gari na kuondoka, kuelekea huko shambani kulipokuwepo watoto wa huyu mzee, na kwa mbali kukawa na gari jingine likija kuelekea nyumbani kwa huyo mzee

****************
Wakati hayo yakiendelea Inspecta Maneno alikuwa kwenye chumba cha Inspecta Moto alikuwa akitafuta kitu, kitu ambacho ni muhimu sana kwake alikitafuta kila mahali hicho kitu bila mafanikio, mwisho akakata tamaa, na kusema;

‘Labda aliharibu ushahidi wote, kama alifanya hivyo, atakuwa kaniokoa,maana pale kuna kila kitu, kama mambo ya kiharibika natumia kama ni uchnguzi niliouwafanya, vinginevyo, …’akasema akitaka kutoka, na wakati huo simu yake ikawa inaita;

Akapokea bila kuangalia mpigaji, na sauti yenye wasiwasi ikasema

‘Hatukumpata, na tumewakuta watu wetu wamefungwa kamba, hawajiwezi, wameleweshwa madawa gani sijui, wapo kama wamepagawa…’akasema

What, haiwezekani…ina maana nyie na uaskari wenu wote mumeshindwa na mzee wa kijijini, lakini si mlisema kuwa mumeongea na mzee mmoja ambaye amesema kuwa anaye huyo mtu, na akakubali kuwaonyesha kwa malipo ya pesa ya zawadi tuliyotangaza…?’ ukauliza

‘Ndivyo ilivyokuwa lakini naona imekuwa tofauti….’akasema kwa sauti ya kukatika katika

‘Ni muhimu kulimaliza hilo zoezi sasa hivi…,maana kuna mambo yametokea, na kuna taarifa kuwa kesho kesi ya mauaji ya mke wa Inspecta inasikilizwa kwa mara ya mwisho, kama yeye hayupo,na walalamikaji hawapo itafutwa, lakini pia kesi nyingine imeletwa na watu wasiojulikana …..’akasema

‘Kesi gani hiyo kumshitaki nani?’ akaulizwa

‘Kuwa kuna kundi linalotishia amani, na ndilo linalohusika na haya yote yanatokea, kifo cha muheshimiwa, kifo cha mke wa Inspecta na mambo mengi tu …hii inaashiria kuwa kuna mtu keshajiandaa kupambana na kundi …’akasema

‘Sasa tutafanyaje?’ akaulizwa

‘Sisi hatuhusiki kwa hilo kwa sasa, au sio, sisi ni askari, …msimamo wetu ndio huo, lakini ili tufanikiwe, ni lazima kusiwe na ushahidi wowote wa kutukwaza sisi na ndio hapo tunahitajika kuondoa kila aina ya watu wanaotujua kuwa tunahusika kwa namna moja au nyingine, na mmojawapo ni huyo mtu, mtafuteni, na malizeni kazi…’akasema

‘Ndio…lakini sasa haonekani….’akasema

‘Kama haonekani ni bora mjimalize na nyie kabisa……mnasikia, kama hamtakuja na ushahidi kuwa huyo mtu ni maiti, ni bora nyie mpotee, …bosi hataki kusikia  makosa, keshatoa angalizo…’akasema

‘Sawa afande tutalifanyia hilo kazi, ila tunahitaji mshiko wetu kabisa, mwambie huyo bosi wako asiyeonekana  kuwa hatujalipwa mshiko wetu kwa kazi zilizopita,…..’akalalamika

‘Kazi kwanza …’akasema na kukata simu, akawa anaangalia juu ya kabati, alihisi kuona kitu…lakini…

Na muda huo huo akasikia gari likisimama nje, akachungulia dirishani, alikuwa mmoja wa wasaidizi wake wampya wa kitengo cha polisi, ambaye hawaivani kabisa, na hakujua kafuata nini hapo,na alishatakiwa kumfanya asalimi amri ya kundi, na harakati zilishaanza, lakini alikuwa bado hajawekwa sawa

‘Kwa haraka akafunga mlango wa chumba cha Moto, na kutoka nje kukutana na huyo askari mwenzake, akipanga ni kitu gani cha kumuambia.

 ‘Kumbe upo hapa mkuu, tumekutafuta na simu hupatikani, …’akasema

‘Nilikuwa nahakikisha, unajua huyu alikuwa rafiki yangu mkubwa kwahiyo nataka niwe na uhakika wa kila kitu, namalizia malizia uchunguzi wake kujirizisha, lakini nina uhakika huyu mtu kauwawa, sizani kama yupo hai…’akasema

‘Mkuu unahitajika makao makuu haraka….’akasema huyo msaidizi wake

‘Kuna nini tena…?’ akuliza kwa mashaka

‘Inspecta Moto kapatikana….’akasema

‘Eti nini….!’


WAZO LA LEO: Kauli ni kitu muhimu sana cha kuchunga, kauli inaweza kuzua jambo, jambo dogo likawa kubwa sana, au kauli hiyo hiyo ikamkwaza mwenzako, hata kumuumiza, na huenda hukuwa na nia mbaya, lakini kwa jinsi ulivyoitoa hiyo kauli, ikatafsiriwa vingine. Tunapoongea tujaribu kuangalia ni nani tunayeongea naye, na kwa wakati gani, na kauli zijaribu kuangalia matokea yake, na ili ufanikiwe hilo hebu jaribu kwanza kujiuliza je kama mimi ningeliambiwa hivyo ningelijisikiaje.

Ni mimi: emu-three

No comments :