Akaanza kuhesabu ,
moja mbili , tatu, akasimama, lakini kabla hajafanya jambo, akahisi kitu
kikichoma upande wake wa kushoto,…ilikuwa ni sindani, iliyorushwa kama risasi,
ilikuwa imetokea dirishani, hakuweza hata kuigusa, ilifanya kazi mara moja,
akahisi giza likitanda usoni…. Akapoteza fahamu.
Endelea na kisa chetu.....
Inspecta
akafungua macho, na kuangalia huku na kule, aliona mazingira mageni kabisa, hata
hali ya hewa, ilikuwa ngeni kabisa, upepo, na milio ya ndege, akageuza kichwa
huku na kule, hakuweza kutambua moja kwa moja kuwa yupo wapi, na mara akasikia
sauti ya mtu akikaribia pale alipolala.
Alikuwa
msichana wa kama miaka kumi na tisa hadi ishirini na mbili,, alikuwa kashika
sinia lenye vifaaa ndani yake, kulikuwa na vikombe viwili na gilasi mbili na
chupa ndogo ndogo zikiwa na vitu ndani yake, na harufu kali yenye kukereketa
kooni ilisambaa
Yule
msichana akasogea hadi pale alipolala, akaweka ile sinia yenye hivyo vitu juu
ya kila kitanda , na yeye akakaa kwenye kiti kidogo cha mti, kilichokuwepo hapo pembeni ya kitanda, akasema;
‘Unajisikiaje
mgonjwa, naona fahamu zimerejea, niliambiwa ukiamuka nikupe hii dawa, ina
mchanganyiko wa virutubisho vingi mwilini,…kunywa ili upate nguvu, baba katoka
muda , alikwenda kujaribu kuulizia watu , au kujua kama kuna mtu anaulizia, kupotea
au kupatikana kwa mtu…’akasema.
‘Kwani
hapa nipo wapi…’akauliza Inspecta.
‘Huku
ni maeneo ya Bagamoyo,…’akasema.
‘Bagamoyo!!,
nimefikaje huku….?’ Akauliza kwa mshangao.
‘Uliokotwa
kwenye mtaro wa maji machafu barabarani, watu walijua umeshakufa, baba alifika
eneo akitokea kwenye shughuli zake, akaona vijana wakikugaua , siunajue tena,
vijana, waliona kuwa umekufa, kwahiyo wachukue kile ulicho nacho, Bahati baba
akawaona wakakimbia.
Baba
akakubeba na kukuleta hapa baada ya kugundua kuwa bado upo hai, akitumia ujuzi
wake wa uganga wa kienyeji, akagundua kuwa umedungwa sindano ya sumu, kwani
wewe ulikuwa wapi kwa mara ya mwisho na kilikutokea kitu gani…?’akaulizwa.
‘Mmmh,
mimi hata sijui kilitokea nini, ila nakumbuka kwa mara ya mwisho nilikuwa
nyumbani kwangu…’akasema.
‘Nyumbani
kwako ni wapi?’ akauliza huyo binti.
‘Dar-es-salaamu…’akasema.
‘Dar-es-salaamu,
Mhh, hapana haiwezekani, sasa umefikaje huku, au ulipatwa na ajali, ukapotewa
na fahamu, haiwezekani, utoke Dar-es-salaamu uje kuokotewa huku, tuliza kichwa
utakumbuka vyema…?’ akaulizwa huyo binti akionyesha wasiwasi.
‘Nina
uhakika kabisa nilikuwa nyumbani kwangu Dar, kwani hapa nimekaa muda gani,
alinileta lini baba yako hapa nyumbani kwenu, jana au leo, kwani sasa hivi ni
saa ngapi ?’ akauliza.
‘Leo
ni siku ya pili, …’akasema.
‘Khaaah!!,
siku ya pili, na nilipofika nilikuwaje?’ akauliza.
‘Ulikuwa
kama mfu tu…isingelikuwa baba kuwa mtaalamu wa kutoa sumu mwilini, sizani kama
ungelipona, kuna sindano walikudunga hapa kifuani, ikiwa na sumu, na sumu hiyo
hutembea pole pole mwilini, ni aina ya sumu ambayo baadaye mtu haweza kugundua
kuwa uliuwawa kwa sumu, hata wakikupima, kama ingelifanya kazi yake vyema, leo
ungakuwa na matatizo mengine…’akasema.
‘Oh,
ina maana hawa watu walitaka kuniua…!’akasema Inspecta kwa mshangao.
‘Lakini
sio kwa hapo , hapo, baba anasema, sumu hiyo, inafanya kazi polepole, itafika
muda utaanza kujisikia vibaya, wakikupima unaonekana una shinikizo la damu, na
ghafla unadondoka, unapoteza fahamu, na ndio inakuwa safari yako ka akhera….’akasema.
‘Oh,
najua sasa ni kweli, kumbe walitaka nife kama Muheshimiwa…’akasema Inspecta.
‘Ndio
nani hao, na huyo muheshimiwa ndio nani?’ kauliza yule binti.
‘Oh,
sasa nimejua hatari iliyopo mbele yangu,natakiwa niwe muangalifu,..kwahiyo sumu
hiyo haipo tena mwilini mwangu, una uhakika, baba yako kajifunzia wapi hiyo
kazi?’ akauliza.
‘Imeshanyonywa
yote…baba ni mtaalamu sana, watu wote hapa kijijini wanamfahamu ukiumwa na
nyoka mwenye sumu, au magonjwa mbali mbali mabaya, yeye anajua iba zake…,
hajaosema mahali kapewa ujuzi huo kutoka kwa mababu zake.’akasema
‘Unasema
sumu hiyo imenyonywa, imenyoywaje?’ akauliza
‘Unaona
lile jiwe pale jeusi, lile ni jiwe la sumu ya nyoka, pia jiwe hilo hilo huweza
kunyoya sumu iliyopo mwilini, inayokwenda kwa mishipa ya damu….’akasema.
Inspecta
akageuka kuliangalia lile jiwe, kilikuwa kipande kidogo chausi,…akajikagua
kifuani, kwa kujipapasa na vidole, na kugusa ile sehemu ambayo anakumbuka
alichomwa sindani, akapashika, hakuhisi maumivu, ila kulikuwa na uvimbe kidogo,
akajaribu kuinuka.
‘Usiinuke
kwanza subiri hivyo hivyo , mpaka baba aje, kuna kitu anatakiwa ufanyiwe kwanza,
lakini alisema kama ni dhararua, kuna hii dawa hapa unatakiwa unywe, ukisha
kunywa, itasfisha tumbo lote, kualizia sumu iliyopita tumboni, sas anikupe
kwanza au umsubiria baba kwanza aje…?’akasema huyo binti.
‘Umesema
baba yako ni mganga, na mama yako yupo wapi?’ akauliza inspecta akipewa dawa
kwenye kikombe, kwanza alisita kuinywa,lakini baadaye akapokea na kuinywa
haraka ilikuwa chungu sana…
‘Mama?…mmmh,
hayupo…’akasema huyo binti akisita, akasogea pembeni na kusema;
Nenda
chooni, hiyo dawa inafanya kazi mara moja, ….’akasema na Inspeca kweli alihisi
tumbo likikorogeka, akasimama na kwa haraka akatoka na kuelekea huko chooni, na
alichukua muda, aliporudi alikuwa akipepesuka, akamkuta yule binti akiwa
kashikilia kikombe, akasema.
‘Haya
ni maziwa, na asali, na dawa nyingine, baba alisema ukinywa hivi vitu vitatu,
utakuwa salama lakini ulale vile vile ulivyokuwa umelala….’akasema.
‘Umesema
mama yako hayupo, Kaenda wapi..?’ akauliza na yule binti akageuka kuangalia
pembeni, halafu akageuka kumuangalia Inspecta machoni, alionekana kubadilika
kama vile hakupenda kuulizwa hilo swali, akasema kwa sauti ya huzuni;
‘Amesafiri
mbele ya haki….’akasema kwa sauti ya huzuni,
‘Pole
sana, kwahiyo hapa unaishi wewe na baba yako tu?’ akauliza.
‘Wapo
ndugu zangu wengine, wamekwenda shambani,na mihangaiko mingine ya kimaisha,
siunajue tena huku ni kijijini, ni lazima mtu ujitume ili uweze kuishi, mimi
nimebakia hapa nyumbani kwa ajili ya kukuangalia wewe…’akasema.
Inspecta
akamuangalia yule binti, akagundua ni msichana mrembo, japokuwa anaishi maisha
ya dhiki, kama inavyoonekana, na usoni alionyesha dalili ya hekima, na huruma,
akamfananisha na mkewe, na hapo hapo akili yake ikakumbuka siku alipokutana na mrembo
kama huyo ambaye baadaye alikuja kuwa mkewe, alikuwa hivi hivi akiwa bado
msichana mdogo.
*****
‘Wewe
msichana unakwenda wapi?’ akamuuliza
‘Nakwenda
kuteka maji, kwanini unaniuliza na wewe ni nani?’ yule msichana akamuuliza
‘Mimi
ni binti Askari Kanzu…’akasema
‘Binti
Askari Kanzu…?’ akuliza kwa mshangao
‘Ndivyo
wanavyomuita baba yangu…’akasema
‘Ina
maana baba yako ni askari kanzu?’ akaulizwa
‘Anafanya
kazi polisi, sasa sijui kwanini wanamuita hivyo…’akasema
‘Nakwenda
kumuona mzee mmoja, anaitwa Majaliwa…ni askari polisi…’akasema
‘Ndiye
baba yangu huyo…’akasema
‘Oh,
sasa huko kisimani ni mbali, unaweza kunielekeza nyumbani kwenu..’akasema
‘Ngoja
nikupeleke…’akasema na akageuka, wakaongozana hadi nyumbani kwao, na hapo
wakasalimiana, na kuanza kujuana na huyo binti , kwani yeye alikaa hapo siku
mbili, alifika kujulia hali huyo mzee, kwake, alikuwa ni bosi wake.
Siku
mbili alizokaa hapo akajikuta yupo karibu sana na huyo binti, na akahisi
kampenda, lakini aliogopa akijua ni mtoto wa bosi wake, na siku anaondoka,
akasindikizwa na huyo binti.
‘Kwahiyo
utarudi tena?’ akauliza
‘Mhh,
nitakuja kumuangalia baba yako , kama anaendeleaje, kama akipona haraka, basi
sizani kama nitakuja huku tena, labda kuwa na jambo la kunifanya nije
huku…’akasema
‘Mhh,
nimekuzoea kweli, …sijui kwanini…’akasema huyo binti.
‘Usijali,
labda mungu kapanga iwe hivyo…ipo siku tutakutana tu, kwani wewe unasoma wapi?’
akaulizwa
‘Nimemaliza
chuo, na nsubiria kazi, kazi zenyewe mpaka kujuana, na baba kaema ni subiria
huku huku, ningelikuwa mjini ningelishapata kazi..’akasema
‘Kwani
wewe umesomea nini?’ akauliza
‘Unesi,..nilitaka
nisomee udakitari , lakini masomo hayakuniendea vyema, hata hivyo sikukata
tamaa, nikaona nisomee unesi, huko huko nitajiendeleza niwe dakitari..hata
hivyo napenda sana mambo ya urembo…’akasema
‘Ok,
nitaongea na baba yako nione tutakusaidia vipi…’akasema
‘Uongee
na baba, nakuona hunitakii mema, hapa tu nimekusindikiza kwa kujificha, hataki
kabisa nionekane na wanaume…’akasema
‘Kwa
kujificha, mimi nilijua baba yako kakuruhusu unisindikize…’akasema
‘Haya
kwaheri, safari njema,…’akasema na kurudi kwa haraka
Siku
baadaye akatembelea tena hapo nyumbani, na safari hii alifika na mshenga, na
ilikuwa kama ilipangwa, kwani binti huyo alishachumbiwa na watu wengi,
akawakatalia, lakini alipofika Inspecta, kipindi hicho alikuwa askari wa kwaida
tu, akakubaliwa, na baadaye wakafunga ndoa, na kuwa mke na mume.
************
`Nikikuangalia
unanikumbusha mbali sana, unanikumbusha marehemu mke wangu…’akasema Inspecta
kwa sauti ya huzuni.
‘Marehemu
mke wako!,..kwani mke wako amekufa?’ akauliza huyo binti kwa mshangao.
‘Mhh,ndio
kauwawa….’akasema akionyesha uso wa
huzuni
‘Mhh,
jamani, pole sana, alikufa kwa vipi, kwanini unasema kauwawa?’ akauliza
‘Wanasema
kajiua mwenyewe…’akasema Inspecta, akijaribu kujinyosha
‘Kwanini?’
akauliza akimuangalia Inspecta anavyopata taabu kujinyosha
‘Wanasema
hivyo, ila mimi siamini hivyo, …’akasema Inspecta
‘Kwanini?’
akauliza Inspecta
‘Baba
yako anarudi saa ngapi, maana nahisi mgongo unauma, kulala hivi ni kama
adhabu…’akasema Inspecta
‘Wewe
lala…nusa hii dawa hii itakusaidia ulale..’akasema na Inspecta akapokea dawa
kidogo ya unda aliyopewa na huyo binti, akallinusa na kupiga chafya mara moja
ya pili, akashikwa na usingizi.
Yule
binti alipoona mgonjwa kalala, akatoka nje, na kukutana na baba yake akiwa na
kikapu kikubwa kikiwa kimejaa majani na matunda matunda, na binti yake
akampokea baba yake, na kusema;
‘Baba
mgonjwa kazindukana, lakini kapitiwa na usingizi, nimemuacha ndani kalala….’akasema
‘Oh,
afadhali alale hivyo hivyo, maana huko mjini kuna taarifa kuwa kuna mtu wa
polisi kapotea,inasadikiwa kauwawa, na nilipoangalia kwenye gazeti, sura yake
inafanana kabisa na huyu mtu, huyu mtu ni polisi , anatafutwa sana…’akasema
‘Mhh,
baba lakini anaonekana ni mtu mwema, sasa tufanyeje?’ akauliza huyu binti
‘Hata
sijui, mwanzoni nilifikiria tumwambie aondoke, maana sitaki matatizo, lakini
unajua kuna watu wamemuona tukimchukua hapa kumuhudumia, ni lazima watawaambia
hao wanaomtafuta na watafaidika, hata hivyo nahisi kuna watu wanataka kumuua,
nawameshajua kuwa yupo hapa,… hajafa, sijui ninani kawaambia, ina maana sasa na sisi tupo matatani, ndio likanijia wazo….’akasema
‘Baba
mimi hata sikuelewi, …lakini baba ni bora, tumsaidie tu huyu mtu….hata hivyo
baba hao watu wamejuaje yupo hapa, wewe unasaidia watu wengi, wanakuja na
kuondoka, na huyo alikuja akaondoka kwanini tusifanye hivyo…?’akauliza huyo
binti
‘Watu
waliona tukimchukua akiwa katika hali gani, hakuna aliyemuona akiondoka …na kumbuka
binti yangu, siku hizi dunia ina macho, na masikio, inaona kila sehemu na
kusikia kila linaloongewa, huwezi jua….’akasema
‘Na
jana nimeota ndoto, nimemuota huyu mtu kuwa ni mtu mwema tu, ila kuna watu wanataka
kumuua kwasababu ya wema wake,… hata hivyo, tutafanyaje, maana tuispofanya sisi
,wenzetu watatuwahi, wawaonyesha hao watu, waonekane wao ndio wamafanya hiyo
kazi, na watalipwa…unaona hapo, mimi nionavyo tusiiachie hiyo neema,..’akasema
‘Mhh,
baba neema gani hiyo, ….’akasema huyo binti.
‘Nyota
ya huyo mtu inang’ara sana, lakini inaandamwa na watu wake wenyewe,…tena wa
karibu, alikuwa akiishi na watu lakini karibu wote ni adui zake …na
isingelikuwa ni nyota yake kuwa na nguvu sasa hivi alishakuwa marehemu….sasa
hapa tunatakiwa tujitahidi tuangalie kama neema hiyo tutaipata sisi,..
‘Baba,
kwani unataka kufanya nini, neema gani hiyo unayoizungumzia….?’akauliza
‘Kwenye
ndoto yangu nimeota kuwa huyu mtu, mke wake ameuwawa, katika kutafuta utajiri…’akasema
‘Ndoto
zako mara nyingi ni kweli…sasa huoni kuwa huyu mtu anadhulumuwa bure,
tunahitajika kumsaidia au sio baba?’ akauliza huyo binti
‘Ndio
hivyo..niliwazia sana hilo, nikasema labda tumwambie huyu mtu aondoke humu
ndani, lakini tukifanya hivyo, kuna watu walimuona watawaambia hao watu,
watapata pesa nyingi, sasa kwanini sisi tuliomuhangaikia, kwanini tusiwaambia
sisi tukapata hizo pesa,….pesa nyingi kweli, …mimi naona tujaribu Bahati yetu…’akasema
‘Kwahiyo
baba unataka kusema nini, nakumbuka ulisema uganga wako hautakiwi ufanye
dhuluma, hiyo baba ni dhuluma, au?’ akauliza huyo binti
‘Wewe
unataka tufe masikini, nimemsaidia huyu mtu kapona, je atatulipa nini, kama unavyoona
hana pesa kabisa, na kuna watu wanataka kutupa pesa nyingi tukiwaonyesha huyu
mtu, kwanini tusifanye hivyo….’akasema.
‘Baba….’akawa
analalamika huyo binti.
‘Wewe
nenda shambani,...hilo niachie mimi, niachie huyu kuna dawa nataka nimfanyie,
nimalize kazi yangu, hayo mengine nitajua la kufanya, na usije kumuambia mtu
yoyote na ukikutana na hao watu usiongee nao kabisa…’akasema.
Yule
binti akaondoka kwa shingo upande, hakuweza kupingana na baba yake, aliondoka
akiwa mnyonge sana. Aliatamani hata kulia,hata hivyo hakuwa na uwezo wa kufanya
lolote, akatembea taratibu kuelekea shambani, akimuacha baba yake akitengeneza
dawa zake.
Kwa
mbali kukawa na mngurumo wa gari likija kuelekea maeneo hayo, lilipofika tu
watu wenye silaha wakateremka kwa haraka na kuzunguka hiyo nyumba, na mmojawapo
aliyekuwa hana haraka akamsogelea yule mzee akiwa anaendelea na utengeneza dawa
zake.
‘Yupo
wapi huyu mtu….?’
WAZO LA LEO:Mara nyingi
inapofikia kwenye masilahi,ya pesa na mali watu hubadilika kabisa, mtu anaweza
kumsaliti hata mzazi wake, au mzazi akamsaliti mtoto wake, au ndugu kwa ndugu
wakakosana, yote hayo ni kwasababu ya mali au masilahi.
Tuepukane
na mitihani hii ya masilahi, na fitina zake maana mali, cheo utajiri ni kitu
cha kupita tu, bali utu na wema ndio hazina ya kudumu, muhimu, tupendane ,
tusaidiane, tulinde dhmana za watu tulizokabidhiwa za uongozi, kwani hicho ni
kiapo, tukiwa waadilifu, tukatenda wema na tukawa wakweli, mbona tutafanikiwa
kuliko kukubwa zaidi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment