Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 22, 2014

DUNIA YANGU-34


Akaanza kuhesabu , moja mbili , tatu, akasimama, lakini kabla hajafanya jambo, akahisi kitu kikichoma upande wake wa kushoto,…ilikuwa ni sindani, iliyorushwa kama risasi, ilikuwa imetokea dirishani, hakuweza hata kuigusa, ilifanya kazi mara moja, akahisi giza likitanda usoni…. Akapoteza fahamu.

Endelea na kisa chetu.....

Inspecta akafungua macho, na kuangalia huku na kule, aliona mazingira mageni kabisa, hata hali ya hewa, ilikuwa ngeni kabisa, upepo, na milio ya ndege, akageuza kichwa huku na kule, hakuweza kutambua moja kwa moja kuwa yupo wapi, na mara akasikia sauti ya mtu akikaribia pale alipolala.

Alikuwa msichana wa kama miaka kumi na tisa hadi ishirini na mbili,, alikuwa kashika sinia lenye vifaaa ndani yake, kulikuwa na vikombe viwili na gilasi mbili na chupa ndogo ndogo zikiwa na vitu ndani yake, na harufu kali yenye kukereketa kooni ilisambaa

Yule msichana akasogea hadi pale alipolala, akaweka ile sinia yenye hivyo vitu juu ya kila kitanda , na yeye akakaa kwenye kiti kidogo cha mti,  kilichokuwepo hapo pembeni ya kitanda, akasema;

‘Unajisikiaje mgonjwa, naona fahamu zimerejea, niliambiwa ukiamuka nikupe hii dawa, ina mchanganyiko wa virutubisho vingi mwilini,…kunywa ili upate nguvu, baba katoka muda , alikwenda kujaribu kuulizia watu , au kujua kama kuna mtu anaulizia, kupotea au kupatikana kwa mtu…’akasema.

‘Kwani hapa nipo wapi…’akauliza Inspecta.

‘Huku ni maeneo ya Bagamoyo,…’akasema.

‘Bagamoyo!!, nimefikaje huku….?’ Akauliza kwa mshangao.

‘Uliokotwa kwenye mtaro wa maji machafu barabarani, watu walijua umeshakufa, baba alifika eneo akitokea kwenye shughuli zake, akaona vijana wakikugaua , siunajue tena, vijana, waliona kuwa umekufa, kwahiyo wachukue kile ulicho nacho, Bahati baba akawaona wakakimbia.

Baba akakubeba na kukuleta hapa baada ya kugundua kuwa bado upo hai, akitumia ujuzi wake wa uganga wa kienyeji, akagundua kuwa umedungwa sindano ya sumu, kwani wewe ulikuwa wapi kwa mara ya mwisho na kilikutokea kitu gani…?’akaulizwa.

‘Mmmh, mimi hata sijui kilitokea nini, ila nakumbuka kwa mara ya mwisho nilikuwa nyumbani kwangu…’akasema.

‘Nyumbani kwako ni wapi?’ akauliza huyo binti.

‘Dar-es-salaamu…’akasema.

‘Dar-es-salaamu, Mhh, hapana haiwezekani, sasa umefikaje huku, au ulipatwa na ajali, ukapotewa na fahamu, haiwezekani, utoke Dar-es-salaamu uje kuokotewa huku, tuliza kichwa utakumbuka vyema…?’ akaulizwa huyo binti akionyesha wasiwasi.

‘Nina uhakika kabisa nilikuwa nyumbani kwangu Dar, kwani hapa nimekaa muda gani, alinileta lini baba yako hapa nyumbani kwenu, jana au leo, kwani sasa hivi ni saa ngapi ?’ akauliza.

‘Leo ni siku ya pili, …’akasema.

‘Khaaah!!, siku ya pili, na nilipofika nilikuwaje?’ akauliza.

‘Ulikuwa kama mfu tu…isingelikuwa baba kuwa mtaalamu wa kutoa sumu mwilini, sizani kama ungelipona, kuna sindano walikudunga hapa kifuani, ikiwa na sumu, na sumu hiyo hutembea pole pole mwilini, ni aina ya sumu ambayo baadaye mtu haweza kugundua kuwa uliuwawa kwa sumu, hata wakikupima, kama ingelifanya kazi yake vyema, leo ungakuwa na matatizo mengine…’akasema.

‘Oh, ina maana hawa watu walitaka kuniua…!’akasema Inspecta kwa mshangao.

‘Lakini sio kwa hapo , hapo, baba anasema, sumu hiyo, inafanya kazi polepole, itafika muda utaanza kujisikia vibaya, wakikupima unaonekana una shinikizo la damu, na ghafla unadondoka, unapoteza fahamu, na ndio inakuwa safari yako ka akhera….’akasema.

‘Oh, najua sasa ni kweli, kumbe walitaka nife kama Muheshimiwa…’akasema Inspecta.

‘Ndio nani hao, na huyo muheshimiwa ndio nani?’ kauliza yule binti.

‘Oh, sasa nimejua hatari iliyopo mbele yangu,natakiwa niwe muangalifu,..kwahiyo sumu hiyo haipo tena mwilini mwangu, una uhakika, baba yako kajifunzia wapi hiyo kazi?’ akauliza.

‘Imeshanyonywa yote…baba ni mtaalamu sana, watu wote hapa kijijini wanamfahamu ukiumwa na nyoka mwenye sumu, au magonjwa mbali mbali mabaya, yeye anajua iba zake…, hajaosema mahali kapewa ujuzi huo kutoka kwa mababu zake.’akasema

‘Unasema sumu hiyo imenyonywa, imenyoywaje?’ akauliza

‘Unaona lile jiwe pale jeusi, lile ni jiwe la sumu ya nyoka, pia jiwe hilo hilo huweza kunyoya sumu iliyopo mwilini, inayokwenda kwa mishipa ya damu….’akasema.

Inspecta akageuka kuliangalia lile jiwe, kilikuwa kipande kidogo chausi,…akajikagua kifuani, kwa kujipapasa na vidole, na kugusa ile sehemu ambayo anakumbuka alichomwa sindani, akapashika, hakuhisi maumivu, ila kulikuwa na uvimbe kidogo, akajaribu kuinuka.

‘Usiinuke kwanza subiri hivyo hivyo , mpaka baba aje, kuna kitu anatakiwa ufanyiwe kwanza, lakini alisema kama ni dhararua, kuna hii dawa hapa unatakiwa unywe, ukisha kunywa, itasfisha tumbo lote, kualizia sumu iliyopita tumboni, sas anikupe kwanza au umsubiria baba kwanza aje…?’akasema huyo binti.

‘Umesema baba yako ni mganga, na mama yako yupo wapi?’ akauliza inspecta akipewa dawa kwenye kikombe, kwanza alisita kuinywa,lakini baadaye akapokea na kuinywa haraka ilikuwa chungu sana…

‘Mama?…mmmh, hayupo…’akasema huyo binti akisita, akasogea pembeni na kusema;
Nenda chooni, hiyo dawa inafanya kazi mara moja, ….’akasema na Inspeca kweli alihisi tumbo likikorogeka, akasimama na kwa haraka akatoka na kuelekea huko chooni, na alichukua muda, aliporudi alikuwa akipepesuka, akamkuta yule binti akiwa kashikilia kikombe, akasema.

‘Haya ni maziwa, na asali, na dawa nyingine, baba alisema ukinywa hivi vitu vitatu, utakuwa salama lakini ulale vile vile ulivyokuwa umelala….’akasema.

‘Umesema mama yako hayupo, Kaenda wapi..?’ akauliza na yule binti akageuka kuangalia pembeni, halafu akageuka kumuangalia Inspecta machoni, alionekana kubadilika kama vile hakupenda kuulizwa hilo swali, akasema kwa sauti ya huzuni;

‘Amesafiri mbele ya haki….’akasema kwa sauti ya huzuni,

‘Pole sana, kwahiyo hapa unaishi wewe na baba yako tu?’ akauliza.

‘Wapo ndugu zangu wengine, wamekwenda shambani,na mihangaiko mingine ya kimaisha, siunajue tena huku ni kijijini, ni lazima mtu ujitume ili uweze kuishi, mimi nimebakia hapa nyumbani kwa ajili ya kukuangalia wewe…’akasema.

Inspecta akamuangalia yule binti, akagundua ni msichana mrembo, japokuwa anaishi maisha ya dhiki, kama inavyoonekana, na usoni alionyesha dalili ya hekima, na huruma, akamfananisha na mkewe, na hapo hapo akili yake ikakumbuka siku alipokutana na mrembo kama huyo ambaye baadaye alikuja kuwa mkewe, alikuwa hivi hivi akiwa bado msichana mdogo.

*****
‘Wewe msichana unakwenda wapi?’ akamuuliza

‘Nakwenda kuteka maji, kwanini unaniuliza na wewe ni nani?’ yule msichana akamuuliza

‘Mimi ni binti Askari Kanzu…’akasema

‘Binti Askari Kanzu…?’ akuliza kwa mshangao

‘Ndivyo wanavyomuita baba yangu…’akasema

‘Ina maana baba yako ni askari kanzu?’ akaulizwa

‘Anafanya kazi polisi, sasa sijui kwanini wanamuita hivyo…’akasema

‘Nakwenda kumuona mzee mmoja, anaitwa Majaliwa…ni askari polisi…’akasema

‘Ndiye baba yangu huyo…’akasema

‘Oh, sasa huko kisimani ni mbali, unaweza kunielekeza nyumbani kwenu..’akasema

‘Ngoja nikupeleke…’akasema na akageuka, wakaongozana hadi nyumbani kwao, na hapo wakasalimiana, na kuanza kujuana na huyo binti , kwani yeye alikaa hapo siku mbili, alifika kujulia hali huyo mzee, kwake, alikuwa ni bosi wake.

Siku mbili alizokaa hapo akajikuta yupo karibu sana na huyo binti, na akahisi kampenda, lakini aliogopa akijua ni mtoto wa bosi wake, na siku anaondoka, akasindikizwa na huyo binti.

‘Kwahiyo utarudi tena?’ akauliza

‘Mhh, nitakuja kumuangalia baba yako , kama anaendeleaje, kama akipona haraka, basi sizani kama nitakuja huku tena, labda kuwa na jambo la kunifanya nije huku…’akasema

‘Mhh, nimekuzoea kweli, …sijui kwanini…’akasema huyo binti.

‘Usijali, labda mungu kapanga iwe hivyo…ipo siku tutakutana tu, kwani wewe unasoma wapi?’ akaulizwa

‘Nimemaliza chuo, na nsubiria kazi, kazi zenyewe mpaka kujuana, na baba kaema ni subiria huku huku, ningelikuwa mjini ningelishapata kazi..’akasema

‘Kwani wewe umesomea nini?’ akauliza

‘Unesi,..nilitaka nisomee udakitari , lakini masomo hayakuniendea vyema, hata hivyo sikukata tamaa, nikaona nisomee unesi, huko huko nitajiendeleza niwe dakitari..hata hivyo napenda sana mambo ya urembo…’akasema

‘Ok, nitaongea na baba yako nione tutakusaidia vipi…’akasema

‘Uongee na baba, nakuona hunitakii mema, hapa tu nimekusindikiza kwa kujificha, hataki kabisa nionekane na wanaume…’akasema

‘Kwa kujificha, mimi nilijua baba yako kakuruhusu unisindikize…’akasema

‘Haya kwaheri, safari njema,…’akasema na kurudi kwa haraka

Siku baadaye akatembelea tena hapo nyumbani, na safari hii alifika na mshenga, na ilikuwa kama ilipangwa, kwani binti huyo alishachumbiwa na watu wengi, akawakatalia, lakini alipofika Inspecta, kipindi hicho alikuwa askari wa kwaida tu, akakubaliwa, na baadaye wakafunga ndoa, na kuwa mke na mume.

************
`Nikikuangalia unanikumbusha mbali sana, unanikumbusha marehemu mke wangu…’akasema Inspecta kwa sauti ya huzuni.

‘Marehemu mke wako!,..kwani mke wako amekufa?’ akauliza huyo binti kwa mshangao.

‘Mhh,ndio  kauwawa….’akasema akionyesha uso wa huzuni

‘Mhh, jamani, pole sana, alikufa kwa vipi, kwanini unasema kauwawa?’ akauliza

‘Wanasema kajiua mwenyewe…’akasema Inspecta, akijaribu kujinyosha

‘Kwanini?’ akauliza akimuangalia Inspecta anavyopata taabu kujinyosha

‘Wanasema hivyo, ila mimi siamini hivyo, …’akasema Inspecta

‘Kwanini?’ akauliza Inspecta

‘Baba yako anarudi saa ngapi, maana nahisi mgongo unauma, kulala hivi ni kama adhabu…’akasema Inspecta

‘Wewe lala…nusa hii dawa hii itakusaidia ulale..’akasema na Inspecta akapokea dawa kidogo ya unda aliyopewa na huyo binti, akallinusa na kupiga chafya mara moja ya pili,  akashikwa na usingizi.

Yule binti alipoona mgonjwa kalala, akatoka nje, na kukutana na baba yake akiwa na kikapu kikubwa kikiwa kimejaa majani na matunda matunda, na binti yake akampokea baba yake, na kusema;

‘Baba mgonjwa kazindukana, lakini kapitiwa na usingizi, nimemuacha ndani kalala….’akasema

‘Oh, afadhali alale hivyo hivyo, maana huko mjini kuna taarifa kuwa kuna mtu wa polisi kapotea,inasadikiwa kauwawa, na nilipoangalia kwenye gazeti, sura yake inafanana kabisa na huyu mtu, huyu mtu ni polisi , anatafutwa sana…’akasema

‘Mhh, baba lakini anaonekana ni mtu mwema, sasa tufanyeje?’ akauliza huyu binti

‘Hata sijui, mwanzoni nilifikiria tumwambie aondoke, maana sitaki matatizo, lakini unajua kuna watu wamemuona tukimchukua hapa kumuhudumia, ni lazima watawaambia hao wanaomtafuta na watafaidika, hata hivyo nahisi kuna watu wanataka kumuua, nawameshajua kuwa yupo hapa,… hajafa, sijui ninani kawaambia, ina maana sasa  na sisi tupo matatani, ndio likanijia wazo….’akasema

‘Baba mimi hata sikuelewi, …lakini baba ni bora, tumsaidie tu huyu mtu….hata hivyo baba hao watu wamejuaje yupo hapa, wewe unasaidia watu wengi, wanakuja na kuondoka, na huyo alikuja akaondoka kwanini tusifanye hivyo…?’akauliza huyo binti

‘Watu waliona tukimchukua akiwa katika hali gani, hakuna aliyemuona akiondoka …na kumbuka binti yangu, siku hizi dunia ina macho, na masikio, inaona kila sehemu na kusikia kila linaloongewa, huwezi jua….’akasema

‘Na jana nimeota ndoto, nimemuota huyu mtu kuwa ni mtu mwema tu, ila kuna watu wanataka kumuua kwasababu ya wema wake,… hata hivyo, tutafanyaje, maana tuispofanya sisi ,wenzetu watatuwahi, wawaonyesha hao watu, waonekane wao ndio wamafanya hiyo kazi, na watalipwa…unaona hapo, mimi nionavyo tusiiachie hiyo neema,..’akasema

‘Mhh, baba neema gani hiyo, ….’akasema huyo binti.

‘Nyota ya huyo mtu inang’ara sana, lakini inaandamwa na watu wake wenyewe,…tena wa karibu, alikuwa akiishi na watu lakini karibu wote ni adui zake …na isingelikuwa ni nyota yake kuwa na nguvu sasa hivi alishakuwa marehemu….sasa hapa tunatakiwa tujitahidi tuangalie kama neema hiyo tutaipata sisi,..

‘Baba, kwani unataka kufanya nini, neema gani hiyo unayoizungumzia….?’akauliza

‘Kwenye ndoto yangu nimeota kuwa huyu mtu, mke wake ameuwawa, katika kutafuta utajiri…’akasema

‘Ndoto zako mara nyingi ni kweli…sasa huoni kuwa huyu mtu anadhulumuwa bure, tunahitajika kumsaidia au sio baba?’ akauliza huyo binti

‘Ndio hivyo..niliwazia sana hilo, nikasema labda tumwambie huyu mtu aondoke humu ndani, lakini tukifanya hivyo, kuna watu walimuona watawaambia hao watu, watapata pesa nyingi, sasa kwanini sisi tuliomuhangaikia, kwanini tusiwaambia sisi tukapata hizo pesa,….pesa nyingi kweli, …mimi naona tujaribu Bahati yetu…’akasema

‘Kwahiyo baba unataka kusema nini, nakumbuka ulisema uganga wako hautakiwi ufanye dhuluma, hiyo baba ni dhuluma, au?’ akauliza huyo binti

‘Wewe unataka tufe masikini, nimemsaidia huyu mtu kapona, je atatulipa nini, kama unavyoona hana pesa kabisa, na kuna watu wanataka kutupa pesa nyingi tukiwaonyesha huyu mtu, kwanini tusifanye hivyo….’akasema.

‘Baba….’akawa analalamika huyo binti.

‘Wewe nenda shambani,...hilo niachie mimi, niachie huyu kuna dawa nataka nimfanyie, nimalize kazi yangu, hayo mengine nitajua la kufanya, na usije kumuambia mtu yoyote na ukikutana na hao watu usiongee nao kabisa…’akasema.

Yule binti akaondoka kwa shingo upande, hakuweza kupingana na baba yake, aliondoka akiwa mnyonge sana. Aliatamani hata kulia,hata hivyo hakuwa na uwezo wa kufanya lolote, akatembea taratibu kuelekea shambani, akimuacha baba yake akitengeneza dawa zake.

Kwa mbali kukawa na mngurumo wa gari likija kuelekea maeneo hayo, lilipofika tu watu wenye silaha wakateremka kwa haraka na kuzunguka hiyo nyumba, na mmojawapo aliyekuwa hana haraka akamsogelea yule mzee akiwa anaendelea na utengeneza dawa zake.

‘Yupo wapi huyu mtu….?’

WAZO LA LEO:Mara nyingi inapofikia kwenye masilahi,ya pesa na mali watu hubadilika kabisa, mtu anaweza kumsaliti hata mzazi wake, au mzazi akamsaliti mtoto wake, au ndugu kwa ndugu wakakosana, yote hayo ni kwasababu ya mali au masilahi.


Tuepukane na mitihani hii ya masilahi, na fitina zake maana mali, cheo utajiri ni kitu cha kupita tu, bali utu na wema ndio hazina ya kudumu, muhimu, tupendane , tusaidiane, tulinde dhmana za watu tulizokabidhiwa za uongozi, kwani hicho ni kiapo, tukiwa waadilifu, tukatenda wema na tukawa wakweli, mbona tutafanikiwa kuliko kukubwa zaidi.

Ni mimi: emu-three

No comments :