Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, August 29, 2014

DUNIA YANGU-24


‘Usinitishe bwana, kama ni kwenda huko nitakwenda kwa hiari yangu mwenyewe, kwani nilishapanga kwenda huko ninapokwenda, sasa sijui huko unapotaka wewe niende ni wapi, au kuna sehemu gani nyingine unayotaka mimi niende, nieleze wewe nijue...’

Baby naomba tukutane Paradise hoteli, jioni, ukitoka kazini..

Mume wangu, leo ujitahidi kufika nyumbani mapema…’

Tuendelee na kisa chetu…..

                   ***************

Japokuwa Inspecta alikuwa meza moja na mdada mrembo au kama wamuitavyo mrembo Jembe lakini akili yake ilikuwa mbali kabisa, bado alikuwa akimuwazia mkewe, kwa kauli yake ya mwisho;

`….. mimi nitakuja huko huko unapokwenda kukutana na huyo aliyekuita....’.

‘Mhh, sasa akiamua kuja huku, ndio mwanza wa uhasama kwenye familia yangu na ndicho kitu sikitaki,…lakini mke wangu hawezi kuja huku na hata akija huku hawezi kufika hadi sehemu hizi maalumu, mmh, hata hivyo naomba  asije akachukua maamuzi ya kuja hapo hotelini…’akawa anawaza kwa mashaka.

‘Mungu nisamehe kwa hili maana nafanya hivi kwa nia ya kulipata hili kundi, na nikipata ushahidi wa kutosha nitalifkisha mbele ya sheria….’akazidi kuwaza, na mwenzake aliyekuwa mbele yake akiongea hili na lile, akawa sasa anamuangalia Insecta kwa mashaka akajua kuwa mwenzako hayupo hapo kiakili, akatulia na kumuangalia, akasema;

‘Hivi wewe upo hapa kweli…?’ akauliza huyo mwenzake

‘Kwanini…eeeh,  kwani unanionaje, mimi nakusubiria wewe uanze kunieleza ulichoniitia…’akasema Inspecta

‘Nafahamu hapo ulipo unamuwaza sana mke wako, hivi wewe umeolewa au umeoa, wakati mwingine kama mwanaume unatakiwa uwe na maamuzi yako mwenyewe, usikubali kuchungwa nyendo zako…hata hivyo unaweza kumdanganya kama upo kazini au sio…?’ akauliza

‘Kama wewe ni mke wangu ningalikufanyia hivyo, ungelifurahia, au ni mkuki kwa nguruwe…’akasema

‘Hahaha, ni mpaka, wewe mimi ni makini sana, ..lakini wakati mwingine haya lazima yawepo, hasaukikutana na warembo, kama mimi, kwani unanionaje mimi baby..?’ akauliza akisogeza kichwa chake, na kama isingelikuwa meza kuwa kati yako, yanglikuwa mengine.

‘Naomba ujiheshimu, mimi ni mume wa mtu…’akasema

‘Hahaha, mume wa mtu,..hapa,…ukiwa hapa hakuna cha mume wa mtu, unasikia, sitaki kusikia kauli hiyo, unanielewa lakini, usije ukajiharibia mwenyewe, hapa wewe ni mpenzi wangu,…fanya hivyo, kama unataka mambo yako yasifike usipotaka yafike…ok, baby, kunywa, kula raha ya dunia…nyie watu bwana, mnataka mpendwe vipi….’akasema
Wakati huyo binti anaongea akili ya Inspecta ilikuwa imeshahama, akiendelea kumuwazia mkewe, moyoni akasema;

‘Ila kwa jinsi nimjuavyo mke wangu…huyu mtu anaweza kufika huku, sasa kama kweli kaamua hivyo, itakuwaje, na kama kuja huku labda awe na mtu anamuongoza, yeye mwenyewe sizani kama anaweza kuingia humu ndani na kuanza kunitafuta, sasa kama kuna mtu anamuongoza, anaweza kuwa nani…?’ akajiuliza

‘Nahisi kuna jambo lipo nyuma ya haya yote, inawezekana yote ni mipangilio yao, na nispokuwa makini wanaweza hata kuivunja ndoa yangu…sikubali…., namfahamu mke wangu akiona jambo ni sahihi kwake, hasiti kuchukua maamuzi,..huyu mtu anaweza kufika hapa..sasa nifanyeje, hata ni lazima niondoke humu….’akawa anawaza

‘Vipi mpenzi mimi sikuelewi, naona sasa tufanye mengine ili nikuchangamshe….’akasema mdada na kunyosha mkono kushika mkono wa inspecta na kwa vile Inspecta alikuwa mbali kimawazo, kuguswa mkono wake na mkono laini wa huyu mwanadada, akajikuta akishituka, na kwa haraka akaondoa mkono wake na kushika gilasi ya kinywaji alichokuwa akinywa.

‘Nawaza mambo mengi sana, hata kichwa changu hapa hakipo sawa, unaweza kuniamia uliloniitia nini ili niwahi kuondoka, unajua nyumbani sijapaacha vizuri…’akasema

‘Wewe mwanaume wewe, ukiwa hapa na mimi sahau habari ya mkeo, ujue haya yote nafanya kwa ajilii ya kukusaidia wewe, jitahidi kuonyesha kuwa mimi ni mpenzi wako, vinginevyo, utakosa kila kitu, mimi sitaki kukumbusha mambo yako..’akasema mdada

‘Kwani unasubiri nini kuniambia, sawa nimejitahidi kutimiza wajibu wangu kama nilivyoahidi,  ndio maana nimekuja hapa vinginevyo, ningeliamua kutokuja kabisa, na hakuna angeliweza kunilazimisha, sasa mimi ninakupa nusu saa uniambie ulichoniitia au nondoke zangu…’akasema Inspecta kwa sauti ya kikazi zaidi

Kuna ujumbe uliingia kwenye simu ya mdada, na mdada akaishika simu yake akionyesha kukerwa, akaufungua ule ujumbe huku akisema;

‘Ndio mambo nisiyoyataka haya, watu tupo kwenye starehe zetu,wengine wanafikiria kusumbua,…..mmh’ akasema akisoma ule ujumbe, lakini Inspecta hakuwa na wazo lolote kuhusu anachokisome mdada, akawa anawaza jinsi ya kuondoka hapo tu.

‘Mhh baby mbona eeh, unajua naona tufanye hivi, ili usiniharibie siku, hebu kwanza inuka tucheze muziki, huo wimbo unananikumbusha mbali kweli…’akasema na kwa haraka akasimama na kwenda kumshika Inspecta mkono.

‘Simama baby tucheze…..eeh, my love, my sweetie….’akasema akishika kifuani, halafu akamshika Inspecta mkono kumuinua asimame

‘Mimi sitaki kucheza mziki, umenielewa lakini..’akasema Inspecta akijaibu kukwepa macho ya watu, akijua ni lazima kuna watu wanawaangalia.

‘Kwahiyo unataka kuniaziri sio, mimi nimesimama kwa mapenzi yangu kwako, wewe unakataa, ina maana gani, huoni watu wanatuangalia, inaonekana mimi ndiye nakutongaza…’akasema huyu kwa sauti, na Inspecta akajisikia vibaya

‘Unajua mimi naheshimika sana humu ndani…’akasema na Inspecta akainua uso, na kuangali huku na kule, ni kweli kuna wau walikuwa wakiwatupia jicho kwenye meza yao, yeye tangu mwanzo aliliona hilo, na alijua, kwa hisia zake ni kwa urembo wa huyo mdada.

Inspecta akasimama kwa shida, na wakashikana mikono kusogea kati kati ambapo kulikuwa na wau wengine walikuwa wakicheza wawili wawili, na mziki uliokuwa hewani ulikuwa ni wa taratibu, kwahiyo uchezaji wake ulikuwa wakukumbatiana, hapo Inspecta akasita, hakumsogelea mdada, akawa amenyosha mkono wacheze kimbalimbali, lakini mdada akijisogeza kwake, na kuweka mikono yake shingoni kwa Inspecta,..

Inspecta alijikuta akihema kwa shida, na hakuwa na jinsi akafanya kama alivyolazimika iwe akajitutumua mkuu, na kwa vile mambo hayo ya mziki anayajulia,basi akaonyesha kuwa naye hayupo nyuma.

Mdada akijua nini anachokifanya, hakuacha uchokozi, akilini akajua mambo yapo tayari, kutokana na huo ujumbe aliotumiwa, …..na hapo akajua afanye nini, kutokana na muda aliopewa…’akatulia akimuangalia Inspecta machoni, kwa yale macho yake, ambayo akimuangalia mwanaume, anagwaya

‘Alipomuona Inspecta haelekei, akaamua kufanya zaidi ya hayo, akawa amemkabili Inspecta kisawa sawa,…mikono ikawa inafanya mambo yake , macho, na sasa… na hapo Inspecta akazidiwa ujanja na kujikuta sasa anakwenda na wakati, mziki ukaendelea, pombe zikaanza kumchanganya , na Inspecta alipona hivyo,akasema;

‘Hivi kwanini msichana mrembo kama wewe unajizalilisha hivi?’ akauliza Inspecta

‘Hahaha, ina maana mimi hapa najizalilisha kwani kipi cha ajabu nilichokifanya mimi kwako, hivi mtu akijitoa mhanga kwa ajili ya mpenzi wake ni kujizalilisha, au ina maana sisi wanawake hatutakiwi kuonyesha mapenzi yetu kwa wanaume…eeh, acha hayo bwana…?’ akauliza

‘Hakuna cha mapenzi hapa, mimi nafahamu fika haya yote unayafanya kwa lengo maalumu umetumwa kunifanyia hivi, sijui ili iweje…’akasema Inspecta

‘Ili iweje, ….hahaha, kumbe unajua eeh, kwanini nifanya hivi kwako, ili iweje, huoni kama unajichanganya mwenyewe, je ina maana wewe hunipendi…ili iweje ni ili ujua kuwa kweli mimi nakupenda, au wewe hunipendi, ulichofanya siku ile ulikuwa unaigiza au..?’ akauliza

‘Mimi nina mke wangu, siwezi kupenda mtu mwingine na hilo walifahamu fika, nay ale ya sku ile ni mipango yenu ili kuninasa, hakuna zaidi ya hapo…’akasema Inspecta

‘Mkeo , mkeo…mkeo,..mmh, hivi wamuona mkeo wa maana sana, hivi ana uzuri gani Yule mwanamke, …ukilinganisha na mimi, eeh, hebu niambie ukweli, wewe wanionaj mimi, mkewe anaweza kukutenda haya ninayokutendea, hajui mapenzi…’akasema

‘Mke wangu anajiheshimu sana,ni kweli hawezi kuyafanya haya, kwani anajua nini maana ya mke…’akasema

‘Mhh, anajiheshimu, ungelijua usingelisema hivyo…’akasema

‘Ningelijua nini..?’ akauliza

‘Wewe hutujui sisi wanawake eeh, sisi wanawake tuna siri kubwa sana, nikuambie ukweli mkeo ni wakati mpo naye ndani, akitoka nje sio wa kwako,….mnajidanganya sana wanaume…unajua anachokifanya mkeo ukiwa kazini….’akasema

‘Hayo wasema wewe kwa vile hujaolewa, na kama ungekuwa kwenye ndoa ungelifahamuu fika kwanini nasema hivyo…’akasema Inspecta

‘Hahaha, unajua mkeo ni mara ngapi ameshawahi kuingia humu?’ akauliza na Inspecta akashituka na kuuliza

‘Lini ulimuona mke wangu humu?’ akauliza kwa hamasa, kwaza alihisi ni njama tu, lakini akataka kujua zaidi, huenda kuna kitu.

‘Kwanza ujue kuwa mimi ni keo pia, kuanzia siku ile ulipojitoa kwangu, ukanifuatilia nyumbani, na ukaonyesha pendo lako kwangu, kuanzia siku ile uelewe kuwa mimi ni mke wako, sijui utaniita nyumba ndogo, au mke mdogo, utajua wewe…’akasema

‘Wewe mwanamke hayo unayasema wewe mwenyewe, kwa mtindo huo, ina maana umeshaolewa mara ngapi…..ina maana kila mwanaume unayekutana naye kwa mambo yako anakuoa au siunakuwa umeolewa?’ akauliza

‘Usinitusi, uliwahi kuniona na mwanaume gani mwingine pale ulipofika nyumbani kwangu ulimuona mwanaume mwingine,…mimi sivyo kama unavyonifikiria, mengine nayafanya kikazi zaidi, lakini nalinda heshima yangu…’akasema kwa sauti ya kukasirika.

‘Hii ndio kazi yako sio, kujizalilisha na kulazimisha mapenzi kwa waume za watu ndio kazi hii…’akasema Inspecta.

‘Hahaha wewe waionaje, inalia kuliko kazi yako, kuliko kazi yoyote unayoifikiria, ..hahaha, eti ni kujizalilisha…’akasema na kutulia.

‘Nikuambie ukweli kama hii ni kazi, ni bora urudi kijijini ukalime tujue moja....kijijini ipo kazi nzuri tu ya kulima, na wanawake wa kule wanajiheshimu, wanaolewa kwa heshima..wewe unatumwa na wenzako ambao mwisho wa siku watakuja kukuruka mambo yakiharibika…’akasema na huyo mdada akakaa kimiya kwa muda.

‘Yamekuingia eeh, sasa anza kujitambua maana hilo ninalokuambia ni la ukweli, hilo kundi unalolifanyia kazi ipo siku litatambulikana na wewe utakuwa mmoja wao, uzuri wako, elimu yako na ujanja wako hautakusaidia kitu mbele ya sheria,…sheria itachukua mkondo wake, na wewe utafungwa, sasa utakuwa umepata nini..na hata hivyo, nikuulize, kwanini hamumuogopi mungu,…’akasema Inspecta alipomuona huyo mdada kautulia

Akamtupia jicho kumuangalia, hakujua mwenzake kamtegea, na wakati huo ndio ulikuwa muafaka kwake, akaanza kwa kucheka, na kusema;

‘Hahaha..unajua wewe ni mjinga kweli, usionione nimenyamaza kimiya ukafikiri ni maneno yako yameniingia, hakuna kitu kama hicho, nilikuwa nawazia mambo mengine, jinsi gani nitaweza kukuchukua uwe wangu, mimi na wewe tu, kama hivi…’akasema na kumshikilia kwa nguvu.

‘He-hebuuu mdada jiheshimu..’akasema lakini kabla hajamaliza neno, mdada akawa keshafikisha mdomo wake , kwenye mdomo wa Inspecta, na kuna mwako kama wa picha ukamulika sasa kwa mwanga kama taa imelekezwa kwake, na Inspecta akajua hiyo sio taa tu ya humo ndani, ni lazima kuna kifaa kinanakili hayo matendo yote, ni vifaa vya video vinachukua picha.

Inspecta akajitoa kwa mdada na mdada akawa anamung’ang’ania, lakini hatimaye Inspecta akajitoa na kurudi kukaa mezani, akatulia kwa muda, na mdada akamsogelea na kumshika begani, akasema;

‘Kwanini unanifanya hivyo mpenzi…’akasema

‘Mimi nataka kuondoka…’akasema Inspecta

‘Hahaha, unamuwazia mkeo sio, hahaha, ungelijua, kuwa mkeo naye yupo anastarehe na wa kwake,usingelisumbuka hivyo, hahaha….wanaume bwana, mnaiona wajaaaanja, hujui kuwa unayestarehe naye ni mwanamke, na kama sio wa kwako wa ndoa ujue ni mke wa mtu au mchumba wa mtu…hahaha, sasa nataka nikuambia ukweli…’akasema

‘Ukweli kuhusu nini?’ akauliza Inspecta.

‘Pamoja na yote niliyokufanyia, ni kweli nipo kikazi zaidi, na nashukuru umeshalijua hilo, ila mimi kutoka moyoni nimekupenda, sijui kwanini…nahisi naumia moyoni nikijua wewe ni mume wa mtu, lakini nitajitahidi kadri ya uwezo wangu, uwe wangu..hilo nakuahidi, ikishindikana basi nzi kufia kidondani ni ajali kazini…’akasema kwa sauti ya kulewa.

Inspecta japokuwa alikunywa, lakini alijaribu kujizuia, akawa anawaza hilo neno kuwa mke wake naye yupo kwenye starehe ina maaana kaamua kuja humo nini na yupo nani, huenda yupo na Inspecta mwenzake,..alipowaza hivyo, akahisi wivu, akahisi hasira, akaanza kumchukia rafiki, akaanza kujenga hisia kuwa huenda Inspecta mwenzake ndiye anamuhujumu mke wake, hapo kwa hasira akasimama kutaka kuondoka.

‘Unataka kwenda wapi?’ akauliza mdada

‘Naondoka zangu nyumbani….…’akasema

‘Uende kufanya nini, na wakai mkeo yupo naye anastereje na wake wa siku ya leo..’akasema

‘Mke wangu yupo nyumbani bwana…’akasema kwa hasira akitaka kuondoka, na Yule binti akacheka na kusema;

‘Hahahaha, mke wako yupo nyumbani una uhakika na hilo, hebu njoo huku nikuonyesha wapi alipo mke wako…’yule binti akamshika Inspecta mkono na kunza kumvuta waende huko anakopelekwa…

NB, Nitaishia hapa kwa leo, tutaonana sehemu ijayo
WAZO LA LEO: Katika maisha yako, usiweke tegemezi kwa mtu, kuwa huyu mwanaume huyu mwanamke, huyu rafiki, bosi muheshimiwa, nk ndiye tegemezi langu….na bila yeye hakuna zaidi, siwezi kupata, siwezi kuishi… yah, ndio wengine kwa vile ni mke wa mtu, au mume wa mtu unaweza kufanya hivyo,na kuamini hivyo, lakini ni vyema kumtegemea mola wako kuwa yeye ndiye tegemezi la kila kitu kuwa bila yeye, yote hayatawezekana, na kutoka kwake yeye, pekee ndiye anayeweza kumfanya huyo mwenzako awe tegemeo lako la kweli.

Nikuambie ukweli,mpende umpendaye, mtegemee umtegemeaye, pata upatacho, chuma uchumacho, lakini kwa mapenzi ya muumba, unaweza usiwe naye umpendaye, anaweza umpendaye asiwe na mapenzi na wewe, na zaidi  hayo huna muamala kwa mungu kuhusu maisha ya huyo umpendaye, ipo siku atakuaga, ataondoka,…


Sasa basi kuanzia leo, jitahidi kumtegemea mungu wako pekee, yeye ndiye apasaye kuabudiwa, na kutegemewa na kila mtu, kwani hana mshirika, kwake yeye yote yanawezekana, na yeye ndiye mwenye mapenzi ya kweli kwa waja wake.

Ni mimi: emu-threeNi mimi: emu-three

No comments :