Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, August 15, 2014

DUNIA YANGU-17Mlango ulipofunguka Inspecta akajikuta anaangaliana na binti mrembo uso kwa uso na na uvaaji wa huyo binti ni ule wa mtu huru, yupo nyumbani kwake, hana wasiwasi, binti alikuwa kigauni kinachoonyesha chepezi, kinachonyesha ndani kwa uwazi zaidi,..

‘Karibu mpenzi wangu nimekusubiri sana, natumai una ujumbe wangu, ingia ndani tafadhali, nilikuwa navalia kwa ajili yako, ...

Inspecta akiendelea kushika na mshangao mara..akahisi kapuliziwa kitu, kumbe ni madawa ya kumpoteza fahamu, na hakuweza kufanya lolote, akawa kanaswa,...

Inspecta akajua keshapatikana, hakuweza hata kujitetea, mwili wote sasa ulikuwa umelegea, akahisi kama anainuliwa juu kwa juu, na mara akahisi yupo kitandani, na kilichoendelea baadaye hakikujua,...alihisi kama anavuliwa nguo...;

Endelea na kisa chetu...


************

  Inspecta alifunua macho kwa shida na cha kwanza kukiona ni binti akiwa mbele yake, binti alikuwa kainua mikono akishika nywele zake, alikuwa kafunga taulo, na ilionekana kama katokea bafuni, akitikisa tikisa kichwa kuondoa maji yaliyokuwa kwenye nywele, na machoni kwa Inspecta ilikuwa kama unaona picha yenye mawingu, haionekanai vyema, yule binti akawa anasogea pale alipolala Inspecta, na alipokaribia yule binti akasema;....

‘Mpenzi umesha-amuka,nilikwenda kuoga mara moja, unajua tena, mimi nimechoka kweli, mmmh mapenzi yako ya jana sio ya kawaida,...mmmh kweli wewe si wa kawaida...hahaha...’akacheka kwa sauti ya kimahaba.

Inspecta macho yakawa sasa yanaona vyeme na kumuangalia yule binti kwa ufasha zaidi, na yule binti akaendelea kuongea

‘Nakuona hata wewe upo hoi, mmh, usiseme hujazoea mambo hayo mmh mpenzi, amka pasi, changamka, unashindwa na mimi bwana...unajua kuna maswala ya kazi ndio maana mimi nimekimbilia kuoga, mmh, hivi wewe kazni huendi...?’ akasema na kuja kukaa karibu na kitanda, na Inspecta aliposikia neno kazini, akajitutumia, hakuja ni saa ngapi, akainua kichwa kuangalia nje kwa kupitia dirishani

‘Kwani wewe ni nani...., kwani nipo wapi,...ni hivi sasa ni saa ngapi mmh, nipo wapi hapa...?’ akauliza akijaribu kufuta uso wake na kutuliza kichwa, kichwa kilikuwa kikimuuma, na alikuwa kama amelewa,

‘Oh, usijifanye hujui mpenzi, jana ulikuja kuniona, umesahahu,...oh, pole sana, amuka ukajimwagie maji, utajisikai vizuri tu, mimi najiandaa kuondoka nataka kuwahi kazini, ingelikuwa muda huu nimeshaondoka, lakini nimechelewa kwa ajili yako nisingeliweza kukuacha hivi hivi, nilitaka nihakikisha umeamuka, chai hiyo hapo mezani, kaoge unywe, au wewe unakunywa kitandani nikupe....?’akasema huyo binti

‘Wewe....mumenifanya nini, nyie watu....’Inspecta akasema na yule binti akacheka kidogo.

‘Hahahahaha...eti tumekufanya nini, wakati ulikuja mwenyewe, ...umesahau eeh, ..naona muda unakwenda, inuka ukaoge, halafu utapanga mwenyewe kuondoka, au utakaa hapa, nitakuja kukupitia baadaye, kwani kazini vipi...?’ akauliza

  Inspecta akajiatahidi kuinuka lakini mwili haukuwa wake,..n yule binti alipoona hivyo, akamshika akijaribu kumsaidia, na Inspecta akaweza kusimama huku akipepesuka, alismama pembeni ya kitanda akitumia kama kiegemeo...ndio hapo akajitambua kuwa yupo uchi, akachukua shuka na kujifunika,na yule binti alipoona hivyo akacheka, na kusema;

‘Sasa unajifunika nini, jana mbona hukufanya hivyo, ..ulitaka hata kunimeza,....hahaha, unalo hilo mpenzi...’akasema huku akimsaidia kusimama,

Inspecta akajaribu kujibaragua kumsukuma,asimshika, akilini bado hakuwa yeye, na akajikuta akitaka kudondoka akaangukia kitandani, hadi hapo hakuwa amejifahamu, akilini akawa anajiuliza ana nini, kuna nini kimempata, je alikunywa pombe jana yake, hakumbuki kufanya hivyo...

Yule binti akawa sasa kaingiwa na wasiwasi, alipomuona Inspecta hayupo sawa, nay eye alishaambiwa hicho alichpuliziwa kikisha Inspecta atakuwa sawa, na hakuna baya litakalompata, hakupenda mtu huyu wa serikali akutwe na baya akiwa mikononi mwake, japokuwa ni moja ya kazi zake,....

Yule binti akachukua maji, akamimina kwenye gilasi, na kumpa Inspecta, na Inspecta kwanza akasita kuyapokea, akiwa bado na mashaka, lakini kwa vile koo lilikuwa kavu na kweli alipoona yale maji, alihisi kiu, alihisi anahitaji maji, akaipokea ile gilasi yenye maji na kuyanywa yale maji kwa pupa, na akataka mengine, lakini yule binti akasema;

‘Hapana hutakiwi kunywa maji mengi kwa sasa...ukioga utasikia vyema....’akasema yule binti akichukua jagi lenye maji na gilasi na kutoka nalo, baadaye akarejea na kumuangalia Inspecta kwa macho yenye huruma, hakusema neno akatulia.

Inspecta sasa akawa anaanza kusjikia vyema, angalau sasa anajiona kama mtu, akaweza kutuliza kichwa na kujaribu kukumbuka, na taratibu akili ikaanza kukumbuka na matukio ya jana yakaanza kumrejea kichwani. Akainua kichwa kumuangalia yule binti, akamkumbuka vyema sasa, kumbe yeye ndiye chanzo cha haya yote.

 Yule binti bado alikuwa akimuangalia Inspecta kwa macho yaliyojaa huruma, na moyoni akawa anawaza maisha yake na hayo aliyoyafanya, kiundani hapendi, lakini ndio ajira yake, bila hivyo hatalipwa, akajaribu kujipa moyo kuwa yeye hana makosa, yeye anatimiza amri ya wakubwa zake...

‘Bafu ipo wapi...?’ akauliza Inspecta na kumfanya yule binti ashituke na yule binti akasema;.

‘Bafu ipo kwenye mlango huo hapo, ingia humo utakuta kila kitu, lakini unaweza kupumzika kama bado hujisikii vizuri, au kama bado una usingizi, endelea kulala, jisikie upo nyumbani....’akasema huyo binti akitabasamu.

‘Kwani mumenipa kitu gani, nahisi kulewa, wakati sikumbuki kunywa, mumeninywesha kitu gani nyie watu?’ akauliza Inspecta akimkazia macho yule binti.

Yule binti hakusema neno, alishaambiwa asije kuongea kitu chenye kumuweka hatiani, hiyo sio kazi yake, alipoona Inspecta sasa anaanza kuelewa kinachoendelea akatoka mle ndani, na kwenda kuingia kwenye chumba kingine.

Inspecta alipoona huyo binti kaondoka, akasimama, na akajinyosha na kujipa mazoezi kidogo, akajiona sasa yupo imara, akatoka pale kitandani na kuelekea bafuni...

Akiwa bafuni akioga, alijaribu kuwaza kitu gani kilitokea, lakini kumbukumbu yake ilipofika wakati anakutana na huyo msichana akiwa kavaa nguo za nusu uchi, akawa hakumbuki zaidi ya hapo, ila kuna namna anakumbuka kama alichukuliwa juu kwa juu hadi kwenye kitanda,...

‘Ndio nilifikishwa kitandani...hapo sikumbuki zaidi, walinifanya nini mimi....’akasema na hakuweza kukumbuka jingine, akashika kichwa na kutafakari, lakini akaona hataweza kupata ufumbuzi, ila alijua kuna kitu kimefanyika ambacho yeye hana ufahamu nacho.

‘Huu sasa ni mtego...kuna kitu kimepangwa, .....ni nani yupo nyuma ya haya yote, ni bosi wa huyu binti, ...na kama ni bosi wake, inawezekana ni yule mwanamke anayemiliki ile kampuni ya urembo......’akawa anajisemesha akilini, lakini hakutoa sauti.

‘Oh, naona nisiwaze zaidi hili ni swala la muda, najua hatima ya yote watafunguka tu, wenyewe wataniambia lengo lao ni nini, na hapo ndipo nitajua la kufanya ..’akamaliza kuoga, akajiangalia kwenye kiyoo,  na kujinyosha na alijiona sasa yupo tayari kwa lolote.

‘Hawa watu naona wamejipanga kunivunja nguvu, lakini sizani kama watafanikiwa, sitakata tamaa kabisa,..ngoja nione wana mipango gani...cha muhimu ni kuwa na tahahari, hii ni ishara mbaya, yaonekana hawa watu ni hatari na sijui ni akina nani, je ni hao waliomteka yule jamaa wa muhudumu wa hoteli, au ni kundi gani jingine, na kwanini na mimi wanifanyie hivi....’akawa anajiuliza.

Akarudi pale chumbani, akaona nguo zake zipo tayari, akazichukua na kuvaa,kila kitu kipo kama kilivyokuwa, akaangalia saa na kuona inakimbilia saa mbili na nusu, na muda kama huu mara nyingi yupo kazini, na simu yake iliyokuwa imezimwa, akaiwasha na ujumbe wa maneno ukaanza kuingia kwa wingi.

Akazipitia kwa haraka haraka, na nyingi zilitoka kwa Inspecta mwenzake, akielezea wapi yupo, kafikia wapi, ...na ujumbe mmoja ukamvutia huo ulitoka kwa namba ya mkewe akausoma kwa makini;

‘Nimerudi jana toka nyumbani sijakuona, ila nashukuru nimekuta ujumbe kuwa hutorudi leo nyumbani hadi kesho,..’

Halafu ukaja ujumbe mwingine kutoka kwa namba ya mke wake, nao unasema

‘Lakini mbona nina mashaka na huu ujumbe ni kweli umeandika wewe mwenyewe, haya maelezo ya mwisho yanasema kuwa kuna picha zitatumwa kwangu niziangalie kwa makini kuhusu wewe ulivyo,...wewe ulivyo, sielewi, kwani umekuwaje,...na hizo picha ni picha gani...oh, hata sielewi, ...’ujumbe ukakatika

Baadaye ukaanza ujumbe mwingine, na ukasema

‘Kwanini umezima simu yako, nakupigia hupatikani,... Hata hivyo usiwe na wasiwasi mimi mkeo nipo nyumbani....’ ukawa ujumbe wa mwisho kutoka kwa mke wake.

‘Picha zitatumwa..picha gani hizo , na kwanini zitumwe kwa mke wangu, ni nani kaandika huo ujumbe...ina inawezekana ni hawa hawa watu...ni nani hawa watu, ni lazima nimuulize huyu binti...lakini natakiwa niwe makini’ Inspecta akajiuliza na kabla hajatulia vyema mara simu ya humo ndani ya mezani ikalia.

Inspecta, akasita kuipokea, akaiangalia, ikiendelea kuita...na kabla hajaisogelea mara mlango ukafunguliwa na yule binti akaiendea ile simu na kuipokea, na akawa anasikiliza kwa muda, alikuwa ameshavalia mavazi yake ya kutokea; alipomaliza kusikiliza ile simu akasema;

‘Sawa nimekuelewa....’akairudisha hiyo simu sehemu yake na kumgeukia Inspecta, akasema;

‘Mimi nipo tayari kuondoka, kama na wewe upo tayari tunaweza kuongozana, au la, wewe pumzika, mimi nitakuja baadaye kukufuata, au unasemaje, ....?’ akauliza na Inspecta akawa anamuangalia tu, na yule binti, akasema;

‘Lakini nikichelewa usije kunilaumu, maana unafahamu foleni za Dar,ninaweza kusema nitakuja baadaye ikafika mchana...nikichelewa, ingia jikoni angalia humo kama kuna chochote kitakufaa kula,...mmh, na chai hiyo hapo ipo tayari, ningekunywesha mpenzi, lakini nisamehe kidogo, nawahi kazini yaani nimechelewa, unaweza kunywa mwenyewe mpenzi au sio..., mimi nina haraka kidogo samahani sana, ten asana, sio kawaida yangu....au kuna zaidi?’akasema akiangalia saa yake

Inspecta akashika kichwa akiwaza, akilini alijua humo sio mahali pema pa kuongea lolote kwa sasa, akilini alijua kuna jambo linaendelea, kwahiyo anatakiwa kuwa makini, akasema;

‘Sitaki kula chochote kwa sasa, ninachotaka ni kuondoka hapa....’akasema

‘Oh,haraka hivyo, ..au unaogopa umechelewa kazini, hayo maswala ya kazini kwenu, mmmh, nimeambiwa usiwe na wasiwasi nayo, mambo yameshawekwa sawa, nahisi wanajua kuwa umepitiwa na kilevi, hahaha ...’akasema na kucheka kwa dharau.

‘Unasema nini...nani kawaambia mtoe taarifa kama hizo kazini kwangu..mimi silewi, nyie ndio mumeniwekea kilevi, ...na ole wenu, kwanza nyie ni akina nani na mataka nini kwangu..?’ Inspecta akauliza kwa hasira.

‘Usikasirike mpenzi, ..nilikuwa nakutania tu, hutaniwi mpenzi, wao wanajua ni nini cha kusema kwa mabosi zako wasikuharibie kazi yako...unaonaeeh, kwahiyo unaweza kushinda hapa, nikirudi tutatoka kidogo, au..?’ akauliza

‘Mimi sio mpenzi wako tafadhali....’akasema Inspecta na yule msichana akashituka na kusema;

‘Mhh, jamani wajua mimi nakupenda sana, sahau yaliyopita, mwanzoni nilikuwa sijakuelewa, lakini ulivyotoka huko kote kunifuata, nimerizika kuwa kweli na wewe unanipenda,..nashukuru sana mpenzi,...yaani nikikumbuka ya jana sitaki tena kukuachia....’akasema na akaonyesha kama anawaza jambo la kumfurahisha na hapo Inspecta akashika kichwa na ndani kwa ndani alitaka kumbwatukia huyu binti, lakini akajipa subira kwani kwa jinsi ilivyo, kitakachoweza kumuokoa na hicho, subira na  kuwa muangalifu.

‘Mpenzi unaonekana mwingi wa mawazo, kama ni kuhusu huko kazini kwako wao wanajua kuwa unaumwa...na hata cheti kimeshaandaliwa kitaletwa muda si mrefu, kama utakihitajia...kwa tahadhari, maana nyie maaskari mna sheria kali, usijali, kila kitu kimewekwa sawa...’akasema akiangalia saa.

‘Kwanini mumenifanya hivyo, ni nini lengo lenu, mnafahamu mumefanya kosa kubwa sana, na mtakuja kujijutia...’akasema Inspecta.

‘Usijali mpenzi, halafu nimekumbuka, kwenye hiyo simu iliyopigwa wanasema mkeo amekuja, yupo nyumbani kwako, hivi kumbe una mke, kwanini hukuniambia, mimi nilijua wewe na mimi tu...jamani nyie wanaume ndivyo mlivyo...’akasema kwa sauti ya kudeka.

‘Tafadhali, achana na mimi, usiniletee hiyo lugha ya hadaa, sijawahi kuongea na wewe kuhusu mambo yenu mliyoyatunga,mimi sikujui nafahamu tu kama kibaraka wa...’Inspecta akatulia, na moyoni akasema natakiwa kuwa makini kwa kauli yangu, huenda wananipima nafahamu nini zaidi, akasema baadaye

‘Mimi..siwezi kuwa na mpenzi kama wewe, mnachofanya nyie ni aibu tupu...na kwanini binti kama wewe unajiingiza kwenye matatizo,....?’akasema Inspecta

‘Mpenzi hilo lisikutie wasiwasi, kwangu mimi tatizo ni hilo nililolisikia, kuhusu huyo mkeo...’akasema

‘Mke wangu kafanya nini...?’ akauliza Inspecta.

‘Ni kwanini hukuniambia kuhusu mke wako....unajua nimekupenda kweli, na mimi nilijua mimi ndiye mke wako mtarajiwa sasa oh, huyo mke wako katoka wapi, mbona unaniweka kwenye njia panda...’akasema

‘Huna haya kutamka maneno kama hayo, najua unaongea hivyo kwa maana yenu mumejipanga uongee hivyo ili ionekane kuwa kweli mimi nina mahusiano na wewe, ninachoweza kukuambia ni kuwa wewe na wenzako ni lazima muwajibike..hili litakuwa fundisho kwenu, labda kama sio mimi...’akasema inspecta na yule binti akacheka kidogo na kubenua mdomo kwa dharau akasema;

‘Mhh, naona wivu mie, kumbe nina mke mwenzangu ...mmmh..lakini usiwe na wasiwasi na mimi...’akatulia kidogo.

‘Mhh, unajua hawa wenzangu hawaelewi kuwa mimi nakupenda, eti wamesema wamemuambia huyo mke mwenzangu....wanadiriki kusema mke mwenzangu...wamenichefua kweli...’akatulia

‘Wivu ulinijia huwezi kuamini, kumbe wewe una mke , na mke wako kaja, nilishituka kweli,...mimi,nilijua ni mimi peke yako, wewe namimi , kumbe nina mke mwenza, mhh, hapo ipo kazi...lakini usijali mwenye kisu kikali ndiye mla nyama, au sio..sio umeona makali yangu...hawezi kunishinda mimi, au unasemaje mpenzi....’akasema huku akigusa gusa kwa kidole kwenye mawani yake.

‘Wewe unaweza kuondoka, siumesema unakwenda kazini kwako nenda bwana, naona unanichefua, ninaweza kufanya kitu kibaya nikaja kujilaumu..., mimi nitatumia usafiri wangu...’Inspecta akasema na sasa akasimama kutaka kuondoka....

‘Lakini usifanye haraka....’akasema na kumsogelea Inspecta ,na Inspecta akawa anajiuliza huyu binti anataka kufanya nini, akatulia kimuangali, na yule binti akamsogelea, taratibu akainua mikono na kupitisha shavuni kwa Inspecta, halafu akageuka kutembea kwa maringo, na huku akisema;

‘Sawa tutaona lini tena, unajua ni vyema tuagane kama wapenzi, ukifanya hivyo itaonekana mimi na wewe tuna ugomvi, kwani tuna ugomvi mpenzi...jana tu ulikuwa umetulia, leo umenibadilikia aah, haifai hivyo mpenzi..’akasema na kugeuka na kusogea karibu ya Inspecta, inspecta akasogea nyuma huku akiwa kakunja uso wa hasira

‘Mhh, usifanye hivyo mpenzi, tabasamu kidogo, kwani leo vipi, .....Ok, ok, see you later....’akasema huyo binti na kuanza kuondoka, akafanya mkono kuashiria busu la mbali, hakujali,...

Inspecta alijiuliza kwanini huyu binti anaondoka na kumuacha humo ndani,hajui kama akibakia humo ndani anaweza kupekua pekua na kugundua chochote au kuna mtego gani, inspecta akajua yote hayo ni mitego wao.

Yule binti alipoondoka, Inspecta akainua kichwa kuchungulia juu akaona kwa pembeni kuna kifaa, ni kadude kadogo, akajua kale kanawezekana ni kifaa maalumu cha kuchukulia matukio, akajua hivi sasa kuna watu wanamuangalia, na yote yaliyofanyika hapo yameshanakiliwa mahali...

Akatembea hatua chache mbele, kageuka, akaangalia huku na kule ,halafu akageuka kuelekea mlangoni na bila kugeuka nyuma tena, akauendea mlango, na kuufungua, akatoka nje na sasa akajiona yupo kwenye varanda ndogo inayotenganisha vyumba na ukuta mwingine, akawa anatembea kuelekea mlango wan je na wakati anapita akasikia sauti ikitokea kwenye vyumba.

Akawa sasa anatembea taratibu akitega sikio, na alihisi sauti, lakini hakujua inatokea kwenye chumba gani, akawa anasogea kwenye mlango akitega sikio ili kujua inatokea kwenye chumba gani, akakisogelea chumba kimojawapo, na kweli akasikia sauti ikitokea humo ndani, ni kama watu wanaongea.

Akatulia, kusikiliza, akajua humo kuna watu wanaongea, akahisi huenda ni wapangaji au ni washirika wa huyo mdada, alishajua kuwa huyo mdada hayupo peke yake, ni lazima ana washirika wake, hasa hao anaowaita mabosi...

‘Ngoja nigonge ,kama ni wapangaji nitawauliza ili nimjue vyema huyo mdada...’akasema
Kwa muda ule alishajiandaa kupambana na lolote hata kama ni washirika wake, akasogea pale kwenye mlango wa hicho chumba, akashika kitasa kuufungua mlango,hakutaka kugonga, na wakati ameshikilia hicho kitasa kutaka kufungua, mara akasikia sauti ikija upande wa pili, wa kile kivaranda, akageuka kuangalia.....

NB: Je inspecta kaona nini...kuna nini

WAZO LA LEO:Tunatakiwa kuhangaika ili kupata riziki yetu, kwani bila kuhangaika huwezi kufanikiwa,  lakini mihangaiko yetu iwe ya halali, sio kila kazi ni sahihi kuifanya kwa ajili ya kupata riziki zetu, kuna kazi nyingine hazistahili kwenye mienendo ya binadamu, na jamii husika. Zipo sheria za kidini na za maeneo tunapoishi.

Binadamu kama, binadamu ana akili ya utambuzi wa jema na zuri na yale mabaya yasiyostahili kwenye maisha ya mwanadamu ni vyema tukayaepuka hata kama yanaingiza kipato kikubwa. Ukiyafanya hayo yasiyostahili, hutakuwa na tofauti na mnyama, mnyama ambaye hajitambui, hana aibu,hajui sheria .


Na kwa ujumla aibu, adabu,stara, ndiyo hulka ya mwanadamu, usipokuwa na tabia hizo katika matendo yako ukaogopa kuwa hili ni baya nisitende, basi wewe huna tofauti ni mnyama asiye-elewa baya na zuri, yeye hufuata matamanio yake tu. Kwa vile mwanadamu ana akili ya kufikiri, basi uso wake umeumbwa na haya, na kwahiyo kila akitendacho, atakitenda kwa hekima, na asipofanya hivyo, kuna walakini ndani yake na matokea yake ni hasara. 

Ni mimi: emu-three

No comments :