Mara akatokea binti mmoja
kwenye mlango wa ile kampuni, huku akiwa anaongea na simu, alitembea kwa
madaha, akionyesha tabasamu muruwa, na mara kwa mara alikuwa akinyosha mkono
mbele kama kuelekeza kitu,...na yule mlinzi alipomuona akasema;
‘Jembe hilo, unaliona
jembe...binti mrembo huyo hapo ndio keshajibadili kimtoko wa namna nyingine,
akiwa hivyo ndio asili yake anaelekea kwake,...huwezi kujua kuwa ni
yule yule aliyeingia muda mfupi uliopita , ila mimi nawafahamu hata wajibadili
vipi...’akasema yule mlinzi na Inspecta alikuwa kaduwaa, akimuangalia yule
binti hakuamini kuwa ni yule dada aliyeingia muda ule.
‘Hapana sio yeye, humo ndani kuna
majembe mangapi?’ akauliza kwa mzaha , macho yalikuwa hayabanduki kwa yule
binti.
‘Hahaha, mkuu, kuna jembe moja kwa
sifa, japo kikazi yapo mengi, huyo ndiye yule yule uliyekuwa ukimuongelea,...’akasema
na Inspecta akazidi kumuangalia kwa makini, akimkagua kutoka miguuni hadi
kichwani.
Huyo dada alikuwa
tofauti kabisa kutoka chini hadi juu, japo kimwili, walilandana na yule
aliyeingia kabla lakini kisura ni watu wawili tofauti, huyu wa sasa anaonekana
maji ya kunde kidogo,kichwani nywele za Kiafrika kidogo, sio kama za mzungu kama
alivyokuwa wakati anaingia, na kwa urembo mhh, huyu naona kama zaidi, ....
Inspecta akakagua
macho yake, kwani muda huo alikuwa hajavaa miwani, macho yake yalikuwa tofauti kabisa
na yale ya awali,...sasa nyusi sio nyingi kivile, ila juu kapaka wanja mweusi,
yaani we acha tu, Inspecta akagwaya...akashusha pumzi na kusema;
‘Una uhakika ndio
yeye..?’ akauliza huku akifuta macho kuthibitisha, na mlinzi akasema;
‘Hahaha, ndio yeye
ndiye mrembo jembe huyo, huyu anaweza kujigeuza kama kama kinyonga....ana
kipaji cha urembo na ubunifu ndio maana bosi wa kampuni hii anamtumia sana,
hilo ndio jembe lake la uhakika....’akasema huyo mlinzi, na mara kukapigwa
honi, na mlinzi akasema;
‘Samahani mkuu,
naona ni bora uondoke, sijui ni nani anataka kuingia...’akasema na Inspecta
akajisogeza kwa ndani kujificha, na mlinzi akielekea kufungua mlango, kwanza
akachungulia kwenye kidirisha na alipoona akanyosha kidole gumba kumuonyesha
Inspecta kuwa hakuna tatizo, na Inspecta akajitoa pale alipojificha, lakini
akiwa na tahadhari akaliangalia hilo gari linaloingia.
Mlango ulipofungulia
likaingia gari la njano, na likatembea taratibu karibu na pale aliposimama yule
binti, na kwa haraka akateremka jamaa mmoja na kuelekea upande wa pili wa
mlango, akamfungulia yule binti, na yule binti, akaingia kwenye hilo gari, na
hilo gari likaondoka taratibu.
‘Hilo gari ni la
kwake au la kazini?’ akauliza
‘Mkuu ndio maana
nakuambia ukiyachunguza ya hapa hutaamini kuwa dunia hii kuna watu matajiri,
hilo ni gari lake, yeye ana magari ya rangi tofauti tofauti, jekundu, njano,
kibluu na jeusi, na kila mara anabadili magari kutegemeana na toleo jipya,
...sijui wanapatia wapi pesa hawa watu...’akasema mlinzi
‘Wanauza madini au
madawa ya kulevya....’akasema akasema kama anauliza
‘Hapana mkuu, mimi
sijasema hivyo, ....sijawahi kuona biashara kama hiyo hapa, ...’akasema mlinzi
kwa sauti ya kuogopa.
‘Haya mimi natoka,
tutakuja kuongea zaidi, ....’akasema Inspecta
Inspecta akawapa
dakika mbili wale jamaa waliokuwa sasa wakingia barabara kuu , na yeye akapanda
pikipiki lake na kuanza kuwafuta taratibu kwa nyumba, na alihakikisha anaacha
magari kadhaa mbele yake.
Alipofika mbele
kidogo,akawasiliana na jamaa yake akimuelekeza gari ajaribu kuona gari hilo
linaelekea wapi, halafu amuambia, hakutaka kulifuata kwa muda mrefu akichelea
kugundulikana
Yeye alipofika njia
panda akaelekea sehemu nyingina, na mara akaja jamaa mwingine, ni mmoja wa watu
wake, akiwa na pikipiki aina nyingine, wakabadilishana pikipiki na Inspecta,
sasa Inspecta akawa na pikipiki ndogo ya kawaida, na moyoni akasema;
‘Ni lazima niwe
makini na hawa watu......’ huku akiendelea kulifuatilia hilo gari...
Endelea na kisa chetu..
**********
Akiwa anaelekezwa na mtu wake kuwa lile gari limeelekea wapi, na
yeye aliposikia hivyo, akaingia kwenye barabara ndogo, akaegesha pikipiki yake,
akaingia ndani kwenye nyumba moja anayoifahamu na humo alishaagiza nguo za tofauti, za kutokea akaingia na kubadili, na alipotoka hapo mtu mwingine, katoka kivingine,
akachukua pikipiki nyingine iliyoletwa abadaye, baadaye akaingia barabara za
kwenda Kawe
Alipofika Ubalozi wa Marekani akaelekea barabara zinazokwenda
Masaki, na kwa mwendo wa kasi kidogo akafika Namanga, na hapo akaliona lile
gari likiwa nje ya maduka ya hapo Masaki, na alimuona yule binti akiingiza vitu
kwenye gari, huku mwenzake naye akiwa kashikilia mifuko mwili, huku na huku, walionekana
walikuwa wakinunua bidhaa, yeye akaendesha pikipiki yake hadi eneo la hopitali
ya Macho, hapo akasubiri.
Baada kama ya nusu saa hivi
lile gari likaja likiwa na mwendo kasi kidogo, likapita pale aliposimama
Inspecta ambaye alikuwa kageuka kuangalia madukani, lakini mawani yake yalikuwa
yakionyesha kinachoendelea barabarani.
Wale jamaa walipopita , yeye akaliwasha pikipiki lake na kuanza
kulifuata lile gari, ilichukua muda kabla hajaliona kwa mbele, na walifuatana
hivyo, hadi wakafika Masaki mwisho, na lile gari likaingia barabara moja ndogo,
na geti likafunguliwa na hilo gari likaingia ndani.
‘Oh, kumbe anaishi hapa, sasa naona zoezi hili liishie hapa....’akasema
akitaka kugeuza pikipiki yake kurudi alipotoka lakini geti la huo mlango
likafunguliwa na mara lile gari la njano likatoka, likiwa na dereva peke yake ,
alipoona hivyo, akasema;
‘Ngoja nijaribu bahati, naweza kuteta kidogo na huyo binti, hata
akinigundua sio tatizo,..huenda nikagundua jambo.’akasema na kuelekea mlangoni,
akagonga na mlango ukafunguliwa na mlinzi, huyo mlinzi alikuwa kashikilia
chungwa mkononi, akasema;
‘Nikusaidie nini ndugu?’ akauliza huku akiweka chungwa mdomoni.
‘Nataka kuongea na huyo dada aliyeingia hapa sasa hivi, mimi ni
mfanyakazi wa kule ofisini kwake anapofanyia kazi, kuna barua hii hapa...nataka
kumpa lakini nina maagizo yake....’akasema Inspecta akitoa barua aliyokuwa
nayo, kiasi cha kumvunga yule mlinzi, na yule mlinzi akasema;
‘Ngoja kwanza..., unajua bosi ndio kaingia sasa hivi, hata
hajapumzika, nipe dakika tano tu kwanza ajiweke sawa, siunajua tena akina mama,
halafu nitampigia simu kumuuliza, akisema uende, mimi sina shida......’akasema
huku akiangalai saa yake.
‘Ila kwa tahadhari, hebu ingiza pikipiki yako ndani, hapo nje
hapaaminiki, unaweza kuibiwa ikawa ni tatizo kwangu, sitaki matatizo...’akasema
huyo mlinzi na Inspecta akaendesha pikipiki taratibu wakati geti linafunguliwa,
na akaingia ndani, akasogea hadi pale alipo mlinzi, na alitaka kuongea naye,
lakini yule mlinzi akasogea pembeni akawa anaongea na simu
Nyumba hiyo ni kubwa, ina ghorofa moja, juu na chini, naona
baadaye inaweza kuwa ofisi, na haijakaa kimuundo wa nyumba ya kuishi watu.
Majengo mengi maeneo haya yanageuzwa kutokwa nyumba za makazi kuwa ofisi. Na
wengi wanaomiliki majengo hayo sasa ni waliokuwa waheshimiwa, naona waliamua
kujiwahia mapema , majengo ya msajili ya enzi hizo,...chukua chako mapema.
Kuzunguka majengo haya kunamiti mingi mikubwa iliyopandwa enzi
hizo, na miti hii imechanua na kuweka vivuli, na kutengeneza mandhari nzuri ya
kupumzikia..na bustanis afi kabisa. Hivi ndivyo inavyotakwia sio kama huko
kwetu ambapo nyumba zimebanana, hakuna miti ya kuleta hew....’akawa anawaza
inspecta
Akashusha macho na kuangalia eneo la kuegesha magari hapo akaona
magari mawili, moja la kibluu na jingine jekundu, na kulikuwa na magari mengine
yameegeshwa kwa ndani zaidi, hapo Inspecta akajiuliza, ina maana magari yote
hayo ni ya huyu binti, au yamewekwa tu hapo.
Inspecta akakagua ile nyumba kwa macho ya haraka, na akahisi kama
kuna mtu anamchungulia kwa ndani japokuwa haikuonyesha, lakini kwa hisia zake
akahisi kama kuna mtu anamchungulia, kwahiyo akawa makini kuendelea na udaduisi
wake macho, na akahisi mwili ukimsisimuka, kwanza aljaribu kujipa moyo kuwa
huenda ni hali ya ubaridi na upepo wa miti, lakini ishara hiyo ilimusahiria
hatari.
Akageuka kuangalia kule alipo mlinzi, alitaka kuaga na kuondoka,
lakini mlinzi akamsogelea na kusema;
‘Ndugu unaweza kwenda, ila usimsumbue sana bosi wangu maana
kachoka...’akasema huku akicheka, na Inspecta akasema;
‘Usijali, ni barua na maelekezo kidogo tu halafu naondoka zangu,sitaki
kupoteza muda wangu, si yupo peke yake ...?’akasema na akauliza na yule mlinzi
akatikisa kichwa kukubali, hakusema kitu, na Inspecta, akatembea kuelekea kwenye
mlango, na alipofika mlangoni, ile hali ya hisia , mwili kusisimuka ikazidi,
kama angelikuwa muoga zaidi, kwa hali ile angeligeuza na kurudi, lakini akajipa
moyo, akabonyesha kitufe cha kuita, na alarm
ikasikika kwa ndani, baadaye mlango ukafunguliwa...Inspecta akagwaya...
Inspecta akajikuta anaangalia uso kwa uso na yule binti, na muda
huu alikuwa kavaa kagauni nusu uchi, na sehemu kubwa inaonyesha ndani kwa uwazi
zaidi,..na alikuwa kabadilisha mfumo wa nywele, na kuonekana tofauti kidogo, inspecta
hakutaka hata kuangalia zaidi alichovaa, akawa anaangalia uso kwa uso na huyo
binti, na huyo binti akawa anatabasamu, hakuonyesha wasiwasi, akawa anatabasamu
kwa kujirembua, akasema;
‘Karibu mpenzi wangu nimekusubiri sana, natumai una ujumbe wangu,
ingia ndani tafadhali, nilikuwa navalia kwa ajili yako, hii herein inanisumbua
kidogo....usiogope, umefika nyumbani mpenzi...siku nyingi eeh, nimekumisi
kweli...’akasema huku akiwa anatoa au kuvaa hereni sikioni, na alipomaliza akinyosha
mikono, na kwa haraka akambusu Inspecta na tendo hilo lilifanyika kwa haraka
bila Inspecta kujiandaa, ...
Inspecta kitu kikamgusa akilini, hii ni hulka yake, hasa
anapoingia kwenye mtego, na hiyo kauli ya ‘mpenzi,’ ikampa ishara ya kujihami,
akajua sasa yupo kwenye mtego, na asipofanya jambo, ataumbuka, akaweka mkono
wake mfukoni na kugusa simu yake, na kidole chake kikatafuta sehemu, akabonyeza
na huku akisema;
‘Hapana siwezi kukaa, nipo kazini, nimekuja mara moja kuongea na
wewe....’akasema
‘Nafahamu sana mpenzi, ni siku nyingi, tumekuwa tukiongea nawe, tukitafutana,
na hata mimi nimelifikiria sana hilo jambo, kwahiyo,...mmh, nipo tayari,
nakupenda sana mpenzi...leo nipo kwa ajili yako...na hii pete uliyonivalisha
leo nimeamua kuivaa rasmi...’akasema yule binti akiinua mikono hewani kama
kumkaribisha Inspecta wakumbatiane, huku akimsogelea, yule binti kwa haraka akashika
pua yake, na...
Inspecta akagwaya, akajua huo sasa ni mtego, akajiandaa kurudi
nyuma, lakini mara akahisi mkono ukitokea nyuma, na sauti ya psssss...,
ikasikika, harufu ya manukato, na akajua keshachelewa,hata hakuwahi kupandisha
mkono kushika puani, akahisi harufu kali ikipenya puani..na mkono ya yule binti
ikawa sasa imemkumbatia kwa mkono mmoja
na mmoja umeshika puani...
‘Fanya haraka itaniingia na mimi....’akasema huyo binti, na viungo
vya Inspecta vilikuwa vimelegea kama sio kushikiliwa angelianguka chini, lakini
kwa nyuma kulikuwa na mtu mwenye nguvu kamshikilia na kwa mbele yupo huyo
binti, akiwa kamkumbatia kama wapenzi wafanyavyo.
‘Haina shaka ondoa mkono puani, mtaalamu fanya vitu vyako....’akasikia
sauti ikisema
Inspecta akajua keshapatikana, hakuweza hata kujitetea, mwili wote
sasa ulikuwa umelegea, akahisi kama anainuliwa juu, na mara akahisi yupo
kitandani, na kilichoendelea baadaye hakikujua,...alihisi kama anavuliwa nguo,
na akapotelewa na kumbukumbu, kilichoendelea baadaye akawa hakitambui....alichosikia
badaye ni sauti kwa mbali ikisema;
‘Kumbe ni inspecta....’akapoteza fahamu
NB: Haya Inspecta kaingia kwenye mtego, je itakuwaje
WAZO LA LEO:Ushirikiano ni mnzuri
sana, hasa pale mnapokuwa na ajenda zilizo wazi, kila mmoja akaweka dhamira
yake ya kweli mezani kama walivyo wanandoa wa ukweli. Lakini kama ushirika huo
una ajenda ya siri, kila mmoja kadhamiria lake, kamwe hamtafanikiwa na kuuita
ushirikiano, na hili ni tatizo hasa kwa watendaji wanapofikiria masilahi yao
binafsi, kuliko masilahi ya ushirika wenyewe.
Na mfumo huu unakwenda hadi kwenye kutengeneza katiba, katiba ambayo
itaweka mambo yote wazi, bila kuweka mambo yenye kubabaisha kwa masilahi fulani.
Na hili litawezekana kama kila kundi, kila mtu atapewa nafasi kusema yake,
kuelewa ya mwenzake na mwisho wa siku kunatokea kitu kilichokubaliwa na
kukubaliana. Huu ndio ushirika wa kweli, na huo ndio mshikamano wa kweli wenye
muongozo wa kweli ambao mwisho wa siku hautawesa kuleta matatizo na msuguano.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment