Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, August 13, 2014

DUNIA YANGU-16


Mara akatokea binti mmoja kwenye mlango wa ile kampuni, huku akiwa anaongea na simu, alitembea kwa madaha, akionyesha tabasamu muruwa, na mara kwa mara alikuwa akinyosha mkono mbele kama kuelekeza kitu,...na yule mlinzi alipomuona akasema;

‘Jembe hilo, unaliona jembe...binti mrembo huyo hapo ndio keshajibadili kimtoko wa namna nyingine, akiwa hivyo ndio asili yake anaelekea kwake,...huwezi kujua kuwa ni yule yule aliyeingia muda mfupi uliopita , ila mimi nawafahamu hata wajibadili vipi...’akasema yule mlinzi na Inspecta alikuwa kaduwaa, akimuangalia yule binti hakuamini kuwa ni yule dada aliyeingia muda ule.

‘Hapana sio yeye, humo ndani kuna majembe mangapi?’ akauliza kwa mzaha , macho yalikuwa hayabanduki kwa yule binti.

‘Hahaha, mkuu, kuna jembe moja kwa sifa, japo kikazi yapo mengi, huyo ndiye yule yule uliyekuwa ukimuongelea,...’akasema na Inspecta akazidi kumuangalia kwa makini, akimkagua kutoka miguuni hadi kichwani.

Huyo dada alikuwa tofauti kabisa kutoka chini hadi juu, japo kimwili, walilandana na yule aliyeingia kabla lakini kisura ni watu wawili tofauti, huyu wa sasa anaonekana maji ya kunde kidogo,kichwani nywele za Kiafrika kidogo, sio kama za mzungu kama alivyokuwa wakati anaingia, na kwa urembo mhh, huyu naona kama zaidi, ....

Inspecta akakagua macho yake, kwani muda huo alikuwa hajavaa miwani, macho yake yalikuwa tofauti kabisa na yale ya awali,...sasa nyusi sio nyingi kivile, ila juu kapaka wanja mweusi, yaani we acha tu, Inspecta akagwaya...akashusha pumzi na kusema;

‘Una uhakika ndio yeye..?’ akauliza huku akifuta macho kuthibitisha, na mlinzi akasema;
‘Hahaha, ndio yeye ndiye mrembo jembe huyo, huyu anaweza kujigeuza kama kama kinyonga....ana kipaji cha urembo na ubunifu ndio maana bosi wa kampuni hii anamtumia sana, hilo ndio jembe lake la uhakika....’akasema huyo mlinzi, na mara kukapigwa honi, na mlinzi akasema;

‘Samahani mkuu, naona ni bora uondoke, sijui ni nani anataka kuingia...’akasema na Inspecta akajisogeza kwa ndani kujificha, na mlinzi akielekea kufungua mlango, kwanza akachungulia kwenye kidirisha na alipoona akanyosha kidole gumba kumuonyesha Inspecta kuwa hakuna tatizo, na Inspecta akajitoa pale alipojificha, lakini akiwa na tahadhari akaliangalia hilo gari linaloingia.

Mlango ulipofungulia likaingia gari la njano, na likatembea taratibu karibu na pale aliposimama yule binti, na kwa haraka akateremka jamaa mmoja na kuelekea upande wa pili wa mlango, akamfungulia yule binti, na yule binti, akaingia kwenye hilo gari, na hilo gari likaondoka taratibu.

‘Hilo gari ni la kwake au la kazini?’ akauliza

‘Mkuu ndio maana nakuambia ukiyachunguza ya hapa hutaamini kuwa dunia hii kuna watu matajiri, hilo ni gari lake, yeye ana magari ya rangi tofauti tofauti, jekundu, njano, kibluu na jeusi, na kila mara anabadili magari kutegemeana na toleo jipya, ...sijui wanapatia wapi pesa hawa watu...’akasema mlinzi

‘Wanauza madini au madawa ya kulevya....’akasema akasema kama anauliza

‘Hapana mkuu, mimi sijasema hivyo, ....sijawahi kuona biashara kama hiyo hapa, ...’akasema mlinzi kwa sauti ya kuogopa.

‘Haya mimi natoka, tutakuja kuongea zaidi, ....’akasema Inspecta
Inspecta akawapa dakika mbili wale jamaa waliokuwa sasa wakingia barabara kuu , na yeye akapanda pikipiki lake na kuanza kuwafuta taratibu kwa nyumba, na alihakikisha anaacha magari kadhaa mbele yake.

Alipofika mbele kidogo,akawasiliana na jamaa yake akimuelekeza gari ajaribu kuona gari hilo linaelekea wapi, halafu amuambia, hakutaka kulifuata kwa muda mrefu akichelea kugundulikana

Yeye alipofika njia panda akaelekea sehemu nyingina, na mara akaja jamaa mwingine, ni mmoja wa watu wake, akiwa na pikipiki aina nyingine, wakabadilishana pikipiki na Inspecta, sasa Inspecta akawa na pikipiki ndogo ya kawaida, na moyoni akasema;

‘Ni lazima niwe makini na hawa watu......’ huku akiendelea kulifuatilia hilo gari...

Endelea na kisa chetu..

**********
Akiwa anaelekezwa na mtu wake kuwa lile gari limeelekea wapi, na yeye aliposikia hivyo, akaingia kwenye barabara ndogo, akaegesha pikipiki yake, akaingia ndani kwenye nyumba moja anayoifahamu na humo alishaagiza nguo za tofauti, za kutokea akaingia na kubadili, na alipotoka hapo mtu mwingine, katoka kivingine, akachukua pikipiki nyingine iliyoletwa abadaye, baadaye akaingia barabara za kwenda Kawe

Alipofika Ubalozi wa Marekani akaelekea barabara zinazokwenda Masaki, na kwa mwendo wa kasi kidogo akafika Namanga, na hapo akaliona lile gari likiwa nje ya maduka ya hapo Masaki, na alimuona yule binti akiingiza vitu kwenye gari, huku mwenzake naye akiwa kashikilia mifuko mwili, huku na huku, walionekana walikuwa wakinunua bidhaa, yeye akaendesha pikipiki yake hadi eneo la hopitali ya Macho, hapo akasubiri.

 Baada kama ya nusu saa hivi lile gari likaja likiwa na mwendo kasi kidogo, likapita pale aliposimama Inspecta ambaye alikuwa kageuka kuangalia madukani, lakini mawani yake yalikuwa yakionyesha kinachoendelea barabarani.

Wale jamaa walipopita , yeye akaliwasha pikipiki lake na kuanza kulifuata lile gari, ilichukua muda kabla hajaliona kwa mbele, na walifuatana hivyo, hadi wakafika Masaki mwisho, na lile gari likaingia barabara moja ndogo, na geti likafunguliwa na hilo gari likaingia ndani.

‘Oh, kumbe anaishi hapa, sasa naona zoezi hili liishie hapa....’akasema akitaka kugeuza pikipiki yake kurudi alipotoka lakini geti la huo mlango likafunguliwa na mara lile gari la njano likatoka, likiwa na dereva peke yake , alipoona hivyo, akasema;

‘Ngoja nijaribu bahati, naweza kuteta kidogo na huyo binti, hata akinigundua sio tatizo,..huenda nikagundua jambo.’akasema na kuelekea mlangoni, akagonga na mlango ukafunguliwa na mlinzi, huyo mlinzi alikuwa kashikilia chungwa mkononi, akasema;

‘Nikusaidie nini ndugu?’ akauliza huku akiweka chungwa mdomoni.

‘Nataka kuongea na huyo dada aliyeingia hapa sasa hivi, mimi ni mfanyakazi wa kule ofisini kwake anapofanyia kazi, kuna barua hii hapa...nataka kumpa lakini nina maagizo yake....’akasema Inspecta akitoa barua aliyokuwa nayo, kiasi cha kumvunga yule mlinzi, na yule mlinzi akasema;

‘Ngoja kwanza..., unajua bosi ndio kaingia sasa hivi, hata hajapumzika, nipe dakika tano tu kwanza ajiweke sawa, siunajua tena akina mama, halafu nitampigia simu kumuuliza, akisema uende, mimi sina shida......’akasema huku akiangalai saa yake.

‘Ila kwa tahadhari, hebu ingiza pikipiki yako ndani, hapo nje hapaaminiki, unaweza kuibiwa ikawa ni tatizo kwangu, sitaki matatizo...’akasema huyo mlinzi na Inspecta akaendesha pikipiki taratibu wakati geti linafunguliwa, na akaingia ndani, akasogea hadi pale alipo mlinzi, na alitaka kuongea naye, lakini yule mlinzi akasogea pembeni akawa anaongea na simu

Nyumba hiyo ni kubwa, ina ghorofa moja, juu na chini, naona baadaye inaweza kuwa ofisi, na haijakaa kimuundo wa nyumba ya kuishi watu. Majengo mengi maeneo haya yanageuzwa kutokwa nyumba za makazi kuwa ofisi. Na wengi wanaomiliki majengo hayo sasa ni waliokuwa waheshimiwa, naona waliamua kujiwahia mapema , majengo ya msajili ya enzi hizo,...chukua chako mapema.

Kuzunguka majengo haya kunamiti mingi mikubwa iliyopandwa enzi hizo, na miti hii imechanua na kuweka vivuli, na kutengeneza mandhari nzuri ya kupumzikia..na bustanis afi kabisa. Hivi ndivyo inavyotakwia sio kama huko kwetu ambapo nyumba zimebanana, hakuna miti ya kuleta hew....’akawa anawaza inspecta

Akashusha macho na kuangalia eneo la kuegesha magari hapo akaona magari mawili, moja la kibluu na jingine jekundu, na kulikuwa na magari mengine yameegeshwa kwa ndani zaidi, hapo Inspecta akajiuliza, ina maana magari yote hayo ni ya huyu binti, au yamewekwa tu hapo.

Inspecta akakagua ile nyumba kwa macho ya haraka, na akahisi kama kuna mtu anamchungulia kwa ndani japokuwa haikuonyesha, lakini kwa hisia zake akahisi kama kuna mtu anamchungulia, kwahiyo akawa makini kuendelea na udaduisi wake macho, na akahisi mwili ukimsisimuka, kwanza aljaribu kujipa moyo kuwa huenda ni hali ya ubaridi na upepo wa miti, lakini ishara hiyo ilimusahiria hatari.

Akageuka kuangalia kule alipo mlinzi, alitaka kuaga na kuondoka, lakini mlinzi akamsogelea na kusema;

‘Ndugu unaweza kwenda, ila usimsumbue sana bosi wangu maana kachoka...’akasema huku akicheka, na Inspecta akasema;

‘Usijali, ni barua na maelekezo kidogo tu halafu naondoka zangu,sitaki kupoteza muda wangu, si yupo peke yake ...?’akasema na akauliza na yule mlinzi akatikisa kichwa kukubali, hakusema kitu, na Inspecta, akatembea kuelekea kwenye mlango, na alipofika mlangoni, ile hali ya hisia , mwili kusisimuka ikazidi, kama angelikuwa muoga zaidi, kwa hali ile angeligeuza na kurudi, lakini akajipa moyo, akabonyesha kitufe cha kuita, na alarm ikasikika kwa ndani, baadaye mlango ukafunguliwa...Inspecta akagwaya...

Inspecta akajikuta anaangalia uso kwa uso na yule binti, na muda huu alikuwa kavaa kagauni nusu uchi, na sehemu kubwa inaonyesha ndani kwa uwazi zaidi,..na alikuwa kabadilisha mfumo wa nywele, na kuonekana tofauti kidogo, inspecta hakutaka hata kuangalia zaidi alichovaa, akawa anaangalia uso kwa uso na huyo binti, na huyo binti akawa anatabasamu, hakuonyesha wasiwasi, akawa anatabasamu kwa kujirembua, akasema;

‘Karibu mpenzi wangu nimekusubiri sana, natumai una ujumbe wangu, ingia ndani tafadhali, nilikuwa navalia kwa ajili yako, hii herein inanisumbua kidogo....usiogope, umefika nyumbani mpenzi...siku nyingi eeh, nimekumisi kweli...’akasema huku akiwa anatoa au kuvaa hereni sikioni, na alipomaliza akinyosha mikono, na kwa haraka akambusu Inspecta na tendo hilo lilifanyika kwa haraka bila Inspecta kujiandaa, ...

Inspecta kitu kikamgusa akilini, hii ni hulka yake, hasa anapoingia kwenye mtego, na hiyo kauli ya ‘mpenzi,’ ikampa ishara ya kujihami, akajua sasa yupo kwenye mtego, na asipofanya jambo, ataumbuka, akaweka mkono wake mfukoni na kugusa simu yake, na kidole chake kikatafuta sehemu, akabonyeza na huku akisema;

‘Hapana siwezi kukaa, nipo kazini, nimekuja mara moja kuongea na wewe....’akasema

‘Nafahamu sana mpenzi, ni siku nyingi, tumekuwa tukiongea nawe, tukitafutana, na hata mimi nimelifikiria sana hilo jambo, kwahiyo,...mmh, nipo tayari, nakupenda sana mpenzi...leo nipo kwa ajili yako...na hii pete uliyonivalisha leo nimeamua kuivaa rasmi...’akasema yule binti akiinua mikono hewani kama kumkaribisha Inspecta wakumbatiane, huku akimsogelea, yule binti kwa haraka akashika pua yake, na...

Inspecta akagwaya, akajua huo sasa ni mtego, akajiandaa kurudi nyuma, lakini mara akahisi mkono ukitokea nyuma, na sauti ya psssss..., ikasikika, harufu ya manukato, na akajua keshachelewa,hata hakuwahi kupandisha mkono kushika puani, akahisi harufu kali ikipenya puani..na mkono ya yule binti ikawa sasa imemkumbatia kwa mkono mmoja  na mmoja umeshika puani...

‘Fanya haraka itaniingia na mimi....’akasema huyo binti, na viungo vya Inspecta vilikuwa vimelegea kama sio kushikiliwa angelianguka chini, lakini kwa nyuma kulikuwa na mtu mwenye nguvu kamshikilia na kwa mbele yupo huyo binti, akiwa kamkumbatia kama wapenzi wafanyavyo.

‘Haina shaka ondoa mkono puani, mtaalamu fanya vitu vyako....’akasikia sauti ikisema

Inspecta akajua keshapatikana, hakuweza hata kujitetea, mwili wote sasa ulikuwa umelegea, akahisi kama anainuliwa juu, na mara akahisi yupo kitandani, na kilichoendelea baadaye hakikujua,...alihisi kama anavuliwa nguo, na akapotelewa na kumbukumbu, kilichoendelea baadaye akawa hakitambui....alichosikia badaye ni sauti kwa mbali ikisema;

‘Kumbe ni inspecta....’akapoteza fahamu

NB: Haya Inspecta kaingia kwenye mtego, je itakuwaje

WAZO LA LEO:Ushirikiano ni mnzuri sana, hasa pale mnapokuwa na ajenda zilizo wazi, kila mmoja akaweka dhamira yake ya kweli mezani kama walivyo wanandoa wa ukweli. Lakini kama ushirika huo una ajenda ya siri, kila mmoja kadhamiria lake, kamwe hamtafanikiwa na kuuita ushirikiano, na hili ni tatizo hasa kwa watendaji wanapofikiria masilahi yao binafsi, kuliko masilahi ya ushirika wenyewe.


Na mfumo huu unakwenda hadi kwenye kutengeneza katiba, katiba ambayo itaweka mambo yote wazi, bila kuweka mambo yenye kubabaisha kwa masilahi fulani. Na hili litawezekana kama kila kundi, kila mtu atapewa nafasi kusema yake, kuelewa ya mwenzake na mwisho wa siku kunatokea kitu kilichokubaliwa na kukubaliana. Huu ndio ushirika wa kweli, na huo ndio mshikamano wa kweli wenye muongozo wa kweli ambao mwisho wa siku hautawesa kuleta matatizo na msuguano.

Ni mimi: emu-three

No comments :