`Kushoto, kulia, angalia juu, ehe, namna
hiyo…’ Alimsogelea yule binti mwanafunzi na kumpapasa kimahaba, kuanzia
shingoni hadi sehemu zote za mwili. Tabia kama hii aliipenda na kumpa raha , na
hali hii ilimfanya ajisahau kuwa yeye ni mwanamke , na pamoja na kujipenda,
kujiremba, kiusichana, lakini moyoni mwake alipenda sana kuwa kama mwanaume
Mawazo haya ya kuwa kama mwanaume humjia mara
kwa mara, hasa pale ananapowaona wasichana warembo, na alipoianza hii kazi,
akawa anapata nafasi ya kukutana na hao warembo, na hapo akawa anajifurahisha
kwa kujiigiza mwanaume...ila leo yupo kikazi zaidi, alikuwa akihitajia warembo
kwa ajili ya monyesho makubwa, kwa ajili ya kazi maalumu na mtu asiyempenda
kabisa katika maisha yake, lakini hakuwa na jinsi.
Alipokumbuka umuhimu wa maonyesho hayo,
akayaondoa haraka yale mawazo mabaya kichwani mwake na kuwaza kazi iliyopo
mbele yake. Alitakuwa kupata warembo maalumu kwa kazi maalumu,...kwa ajili ya
kufanikisha mambo ambayo hakuwa akiyafahamu undani wake.
Hapo akawa anawaza mengi, na mojawapo ni
kumsikitikia yule binti aliyekuwa akimshika shika, kwa kukubali kujiunga naye,
kwani pamoja na maonyesho haya, lakini pia kulikuwa na lengo baya ambalo lilipangwa dhidi yao, na
yote kwa ajili manufaa ya mtu ambaye kwake alimuona kama shetani
‘Mhh binti kama huyu ataniingizia mabilioni ya
mahela, kwanza mzuri , ana umbo la mvuto, kisomo si haba, kiingereza ndio
mwenyewe...lakini ningelijaliwa awe kwa msilahi yangu tu, ...anyway, mimi sijali sana’ akawa anajisemea
moyoni
`Umepita, nenda kaandikishe maelezo yako, kwenye chumba kile’ Alimweleza yule
binti huku bado akiendelea kumshikashika.
`Mwingine’ aliita kwa sauti kubwa, sauti ya ujasiri, hutaamini ndiye yule
aliyekuwa akimshikshika yule binti mrembo. Katika fani yake hii alijua nini na
wakati gani afanye nini. Kitu muhimu ni kuwa muelekevu kutokana na wakati, hata
sauti inatakiwa iendane na jambo lenyewe.
Mlango ulifunguliwa na aliyeingia hapo
hakuamini macho yake. Ilibidi ayaachie yale mafaili aliyokuwa ameyashika na
kudondoka chini...
‘Haiwezekani ni wewe...’akasema.
`Rose Mwelekevu... hatimaye umekuja mwenyewe...’akasema na yule binti
akamuangalia huku akionyesha kutokuwa na raha, alikunja uso, halafu,
akatabasamu.
‘Ndio nimekuja kufanya unachokitaka
wewe....’akasema
Alikumbuka
jinsi binti huyu alivyomsumbua kumpata. Huyu ni binti wa jirani yake, baba yake
ni mmoja wa matajiri pale mtaa wa Regent.
Ni binti wa geti kali, kasomeshwa majuu, na kumuingia ilikuwa kazi, lakini somo
alilompa huyu binti inaonekana lilimbadili, na inavyoonekana ameamua kuja
mwenyewe,
‘Nilijua ipo siku utakuja
mwenyewe.....’akasema na moyoni akiongezea kusema;
‘Na umekubali kuingia kwenye anga zake
umekwisha wewe na familia yako, sasa nimeua ndege wawili kwa jiwe moja...baba
yako na huyu shetani aliyenipa hii kazi nina usongo nao,...ipo siku, na nahisi
siku imeshatimia...’akasema kimoyo moyo, akimkumbuka baba yake huyu mtoto
ambaye alikuwa mwiba mkali kwake.
Baba yake huyu binti aliwahi kumchapa pale alipomkuta
akiwa mitaani na wavulana, hataisahau siku hiyo, kwani alichapwa vibaya sana,
na baadaye akapelekwa kwa wazazi wake, akachapwa tena, ni kipigo ambacho
hataweza kukisahau katika maisha yake,kilimuuma sana, akawa anamchukia sana
huyo baba, na hadi alipokuwa mkubwa, hakutaka hata kumsalimia.
‘Haya niambie nifanye nini?’ akauliza wakati
huo mawazo yake yalikuwa mbali, yakiwaza
siku alipokuwa akimsubiri huyu binti na
hakutokea, na bahati mbaya akakutana na baba yake, na baba yake alimkaripia
sana, akimuambia amesikia kuwa yeye ana kampuni ya kihuni yenye nia ya kuharibi
watoto wa wenzao
‘Mzee sivyo kama unavyofikiria, nia na lengo
langu ni kuwapa ajira wasichana wenzangu, wajishughulishe...’akasema
‘Sitaki kabisa kwa watoto wangu , ole wako
nisikie umemrubuni binti yangu nitahakikisha nimeharibu kabisa biashara zako...’akasema
‘Usijali mzee, mimi nafanya kazi kwa kufuata
sheria na taratibu za nchi...’akasema na huyo mzee akaondoka.
Akamuangalia yule binti na kusema;
‘Wewe umepita bila kupingwa, ingia pale ofisi
ukaandikishe mkataba wako...’akasema akilini akikumbuka siku mbaya kuliko zote,
siku ambayo inamfanya sasa hivi afanye hii kazi, ambayo japokuwa alikuwa
akiifanya kwa masilahi yake, lakini leo anaifanya kwa masilahi ya shetani
mmoja...
‘Huyu shetani ipo siku yake...’akajikuta
akisema kwa sauti, na yule binti akasikia na kugeuka kumuangalia
‘Sio wewe binti, kuna mtu mmoja namuwaza sana,
mtu huyo sitamsahau katika maisha yangu...’akasema
‘Ni nani huyo?’ akauliza huyo binti
‘Ni shetani mmoja hivi...’akasema na yule
binti akatabasamu na kueleka kwenye hiyo ofisi aliyoelekezwa
Katika kumbukumbu zake, siku hiyo aliiweka
kama siku mbaya kuliko zote, akawa anakimbuka siku hiyo alipokutana na shetani
mnywa damu za watu...
*********.
‘Ni shetani mmoja hivi....’akayarudia yale
maneno kimoyo moyo, akiikumbuka siku hiyo ya bahati mbaya...
Ilikuwa ni bahati mbaya na siku mbaya kwake.
Hakutarajia kukutana na huyu shetani tena katika maisha yake, kwani aliporejea
toka ng’ambo, ambapo moja ya misaada ya ya kufanikiwa kwenye kazi hiyo ya
urembo ilitoka kwa huyo aliyemuita shetani. Shetani huyo ndiye aliyemdhamini
kwenda kusoma Ulaya na Marekani ambapo huko alihitimu taaluma hiyo ya Urembo.
Tajiri huyu ambaye kwake ni shetani, alikutana
naye akiwa mitaani, na muda huo alikuwa akitafuta pesa, na haikuwa kazi rahisi
japokuwa alikuwa mrembo, hakupenda iwe hivyo, ila alijikuta akilazimika ili
apate pesa za kujikimu akiwa chuoni, pesa zake alizokuwa kapewa,ziliibiwa zote
pamoja na nguo zake, akabakia mweupe, sasa ataishije kwenye hicho chuo, akaona
ajaribu kazi ambayo hakuwa akiitaka lakini ilibidi ili aweze kuishi na
kuonekana mtu.
Basi katika kuhangaika hangaika siku moja
akakutana na tajiri huyu, na akapata pesa ambazo hakutarajia, na ikawa ndio
mwanzo wa kuwa buzi lake, akawa akilichuna kweli, na kwa jinsi alivyokuwa
akipewa pesa, na kutunzwa hata maswala ya shule akayasahau,chuo kikawa ni
kupoteza muda.
Siku moja alimtapeli huyo buzi dola
elifu kumi, akapotea jiji, na aliporudi kuchukua baadhi ya vitu vyake,
ilivyokuwa kaviacha, alikakamatwa na kwa mara ya kwanza akaingizwa ndani ya jengo
la kifahari la huyu tajiri, jengo hilo lilikuwa na vyumba vya chini kwa chini,
na siku hiyo akapelekwa ndani ya chumba ambacho hatakisahau,
Chumba hicho ambacho kipo chini ya ardhi,
kilinakishiwa kwa umaridadi wa hali ya juu, lakini pamoja na hayo kulikuwa na
kila aina ya vifaa vya utesaji, na akalazwa juu ya meza akiwa kafungwa mikono
na miguu kwenye meza, huku akavuliwa nguo na kubakia kama alivyozaliwa,
akaachwa hapo juu ya meza kwa dakika kadhaa.
Haikupita muda akaingia jamaa, pande la mtu,
jamaa huyo ni kama mnyama, mwili wote una manyoya, na kashupaa kama muinua
vyuma, alikuwa na sura kama ya nyani, macho yake yalikuwa yakitisha, binti huyu
hajawahi kuona mtu kama huyo kabla,...
‘Mungu wangu...’akasema akihisi mwili mzima
ukizizima kwa woga
‘Usijali, sina nia ya kukuumiza, ila nataka
kukuonyesha, jinsi gani ninavyoweza kukufanya pale mtu unapokiuka masharti
yangu, unakumbuka nilipokuchukua mitaani ulisema nini?’ akaulizwa na sauti
iliyokuwa ikitokea juu, lakini hakuweza kumuona aliyekuwa akiongea
‘Nisamehe bosi...’akasema huku akimuangalia
yule mtu aliyekuwa kasimama mbele yake, akiwa kavaa chupi tu.
‘Sihitajii maombi yako ya msamaha, mimi nataka
nikutengeneze, nimeona pamoja na mengine mengi unaweza kuwa mtu muhimu kwangu,
nahitajia kipawa chako, nakuhitaji uje kufanya kazi na mimi...’akasema
‘Kazi , kazi gani?’ akauliza
‘Kwanza nataka ukasome, nataka ukasomee hayo
mambo yako ya urembo, lakini ni zaidi ya huo urembo, nataka ukirudi uje
kufungua chuo cha warembo, na hao warembo watakuwa na kazi maalumu, utakuja
kuifahamu ukiwa huko masomoni...’akaambiwa
‘Niende kusoma nje..?’ akauliza akiwa haamini
‘Unashangaa, ....wengi niliwaambia hivyo
wakashangaa kama wewe,nawasubiri warudi, wapo wanasoma na wewe utakwenda
kusoma,ukirudi tutaanza kazi maalumu, nataka kutumia vipaji vya watu kwa nia ya
maendeleo zaidi ...’akaambiwa
Ni
kweli ilikuwa kama ndoto, lakini ikawa kweli, binti huyu kweli alipelekwa ulaya
kusoma..na alipofika huko hakupoteza muda wake, hakutaka kulirudia lile kosa
alilowahi kulifanya, akaisimamia vyema hiyo elimu, kwani ni jambo alilokuwa
akilipenda, alijifunza mambo mengi ya urembo, mavazi, na mambo mengi ya
wanawake,
Pia alijifunza kuhusu miili ya wanadamu, hisia
zao, akili zao,ujasiri, kujiamini, zaidi sana ni urembo, na kumjenga mwanamke
kimaumbile, akili na muoenekano, mafunzo hayo aliyofundishwa yalimjenga sana kiakili, na
kuwa jasiri zaidi, na huko ndipo alianza kujijengea hulka ya kuwa mwanaume-mwanamke...
Alirejea kinyemela, akijua huyo bosi keshamsahau na atakuwa kapata watu
wengine, maana masomo yake yalikuwa ya mwaka mmoja tu,
‘Mtu kama huyo anayependa wanawake, atakuwa
ameshanisahau,..na hata akiniona atakuwa ameshanisahau, nimejibadili sana,
kimaumbile , kitabia na kimwenendo,...cha muhimu sasa ni kuanzisha kampuni
yangu binafsi...’akajisemea na kweli akaweza kufanya hivyo, akaanzisha kampuni
yake ya mitindo na urembo.
Kutokana na ujuzi wake alioupata huko Ulaya,
aliweza kuliteka soko hilo la mitindo na urembo, na humo aliweza kufanya mambo
mengi aliyoyataka mwenyewe, na hata kuwarubuni mabinti kufanya biashara za
kujiuza, na kampuni yake ikakua kwa haraka, kutokana na shughuli zake, na haikupita
muda akaweka kasino la ndani kwa ndani.
Siku moja aliamua kutoka kwenye eneo lake na
kwenda kustarehe kwenye hoteli moja , akitafuta kubadili mazingira, na kupata
muda wa kuwaza mambo yake, alipofika kwenye hiyo hoteli,kwa vile ni mtu
mashuhuri akakaribishwa kwenye chumba maalumu, hakupenda kukaa huko, akasema;
‘Hapana leo nataka kujichanganya, nitakaa
pale...’akaonyesha meza moja iliyokuwa pembeni kabisa kwenye chumba hicho cha
hoteli, ni sehemu ya vinywaji na vyakula maalumu
‘Karibu sana bosi wetu,....’akakaribishwa, na
yeye akaenda kukaa kwenye hiyo meza, akaagiza alichopenda, na wakati anasubiria
vinywaji vyake na vitafunio vyake ambavyo ni nyamaa maalumu, mara akaja
muhudumu mwingine wa hiyo hoteli, akamwambia;
‘Kuna mgeni mmoja amefika anasema anataka kuja
kuonana na wewe...’akasema
‘Ni mgeni gani huyo mbona sina miadi na mtu
yoyote, na hata hivyo,leo sitaki kuongea na mtu nina mambo yangu ya kuwaza,
nataka upweke...nileteeni vinywaji vyangu, mwambieni hana nafasi ya kuongea na
mtu kwa sasa, kwanza ni nani huyo mtu?’ akauliza na kusema
‘Huyo mtu kasema ni muhimu sana, ...’ akasema
‘Hakuna mtu muhimu kwangu kwa sasa, naomba
unielewe hivyo, nahitaji kuwa peke yangu...’akasema kwa hasira
‘Samahani bosi, mimi nafikisha ujumbe tu, yeye
kasema ukimjua hutakasirika, kwani ni mtu muhimu sana kwako...’akazidi
kusisitiza yule muhudumu.
‘Kwanza ni nani huyo mtu ...?’ akauliza na
kabla swali lake halijajibiwa na huyo binti, mara kwa mbali akamuona mtu akija
kuelekea pale alipokuwa amekaa
‘Huyu ni nani...?’ akawa anajiuliza maana mtu
huyu alikuwa na suti kali ya bei mbaya, machoni kavaa mawani makubwa meusi ya
baei mbaya, nahisi hakutaka kujulikana sura yake, akawa anakuja kwa madaha
akionekana ni mtu tajiri sana, nyuma kulikuwa na watu , nahisi ni walinzi wake,
akawaonyeshea ishara ya kusubiri, ...akawa anakuja peke yake
Kwa jinsi alivyoonekana, huyu mdada akawa na hamu
ya kumuona sura yake, kwahiyo akamuashiria huyo muhudumu aondoke kwa mkono, na
yule muhudumu akaondoka, na akawa sasa anamsuburi huyo jamaa afike kwenye meza
yake.
Yule jamaa alipofika pale karibu kwenye meza, akasalimia
kwa kusema;
‘Samahani mpendwa, natumai sijakuvurugia siku
yako...’akasema na kugeuka kumuangalia muhudumu aliyekuwa anataka kuondoka,
akasema;
‘Nakushukuru sana muhudumu, unaweza kuendelea
na shughuli zako, hakutaharibika kitu...’akasema, na mdada akawa katulia akijaribu
kuikumbuka sauti hiyo ni ya nani, lakini hakuweza kukumbuka, maana alishakutana
na watu wengi wanaoongea hivyo, Kiswahili chenye lafudhi ya kizungu.
Yule mtu alipohakikisha yule muhudumu
kaondoka,yule mtu kwa taratibu akatoa mawani yake, na akafanya jambo la ajabu,
alipitisha kiganja cha mkono wake usoni, akatoa ngozi,....kumbe ni uso wa
bandia, na ana kwa ana akawa anaangaliana...na na
‘Oh, Di-amu, my God, ...’akasema huyu binti
akitaka kusimama ikiwezekana kukimbia, lakini hakuwa na jinsi, zaidi ya kunywea
na kusikiliza atakachoambiwa, akamtupia jicho tajiri huyu na tajiri huyu akawa
anamuangalia kwa tabasamu mdomoni
‘Ndio mimi, ..japokuwa spendi sana kuonekana
onekana,...na hii hoteli ni moja ya hoteli zangu kwahiyo usiwe na wasiwasi...’akasema
Ni kweli tajiri huyu ni nadra sana kuonekana
hadharani, wengi wanajua hayupo hapa nchini, huwezi hata kuona picha yake
kwenye gazeti au vyombo vya habari, leo alishangaa kumuona tajiri huyu
akimtokea mwenyewe. Mara nyingi akihitajia kitu au kufuatilia jambo huwa
anamtuma mfanyakazi wake anayemuamini.
Mdada
huyu akamuangalia huyu mtu kwa macho ya kujiiba iba kuhakikisha kuwa ni kweli ndiye
yule mtu, anayemfahamu. Ndio, ni yuleyule. Alikuwa yule yule jamaa, hazeeki,
mtanashati, na mpenda raha, bwana Di-amu. Jina hili lilikuwa kama jinamizi kila
alipolifikiria na mara nyingine alimuota na kumwita Damu, ikiwa na maana mtoa
damu za watu, au shetani mtoa damu za watu.
‘Ni mimi ...huamini eeh,?’akasema huyo mtu akitabasamu
na kumuangalia huyu mdada kwa kujiamini
‘Khaaa, siamini,....mbona nimesikia kuwa haupo
hapa nchini,...haya niambie unataka nini kutoka kwangu, au unahitajia nikulipe
gharama zako ulizotumia kwangu ....’akasema na huyo jamaa akacheka sana, na
kusema;
‘Eti unataka kunilipa gharama zangu, hivi
kweli unaweza kuzilipa, acha mzaha! Nikuulize ndivyo tulivyokubaliana wakati
nakutuma kwenda kusoma huko Ulaya?’ akauliza
‘Ulinisaidia sawa, sikatai na ninakushukuru
sana, lakini nimeona bora nianzishe kitu changu, ili niweze kusimama kwa miguu
yangu, na nikipata gharama zako nije kukulipa fadhila zako...’akasema
‘Mpendwa, hilo sio jibu la swali langu, mimi
nimekuuliza je hivyo ndivyo tulivyokubaliana wakati unakwenda kusoma huko
nje..., mimi sihitajii kurudhishwa hizo gharama, kabisa sihitaji, nafahamu sana
hizo ndizo shukurani zenu,....’akasema
‘Kwani nimefanya kitu gani kibaya, mimi
nilipofika, nilisikia haupo, upo, nikaona nisikae bure, nijishughulishe,
...kuna ubaya gani hapo...?’ akauliza
‘Na kauli zenu ni kama mlipanga, maana wenzako
wote niliwafanyia hivyo hivyo, na wote waliporudi wameanzisha makampuni yao, wakiwa
na kauli hizo hizo, na wamefanya hivyo wakihisi sitaweza kuwaona, hivi kweli
unaweza kujificha kwenye hili jiji, mnajidanganya....’akasema
‘Lakini mimi sijajificha, kila kitu changu
kipo wazi....’akasema
‘Ulitakiwa kuja angalau kunisalimia, halafu
uniambie malengo yako, nisingelikukatalia, lakini umeshaharibu, umeshanionyesha
jinsi gani ulivyo, japokuwa nafahamu ni ni ungelifanya,...’akasema
‘Kama ulifahamu kuna haja gani ya kuniuliza,
sioni ubaya wake, wewe nisubiri niweke mambo yangu sawa, nitakuja kwako tukae,
tuone unanidai shilingi ngapi, na mimi nitaangalia mahesabu yangu,...nitakulipa
tu...’akasema
‘Unajidanganya binti, wewe na wenzako
mumefanya hivyo mkijifanya sitawaona, nyie, hasa wewe umesahau kuwa mimi kwenye
jijini hili, na sehemu kubwa ya nchi, nina masikio na macho ardhini, unakumbuka
ulivyoniibia zile pesa ulipatikanaje,...mimi naweza kusikia kila kitu na kuona
kila kitu kinachoendelea kwenye hili jiji, kama kina masilahi na mimi..., kamwe
huwezi kujificha, labda ukimbilie vijijini ambapo sijawahi kuwekeza...’akasema
‘Lakini boo-si
nilifanya hivyo kwa nia njema kabisa...’akasema akitamka neno bosi kwa dharau,
hakutaka kumuita mtu mwingine bosi wakati yeye mwenyewe ni bosi wa kampuni
yake.
‘Najua kabisa, ...una nia njema ya kujiwekeza,
ili usije kufanya kazi na mimi, nakufahamu sana, kwa ujanja-ujanja wako, tabia
ya mtu haiwezi kujificha, lakini nikuambie ukweli mimi napenda sana hiyo tabia
yako japokuwa ni tabia mbovu...’akasema
‘Mimi sio yule binti wa mitaani tena,
najitambua na akili yangu imepevuka...amini hilo nakuambia...’akasema
‘Sawa, kama ingelikuwa hivyo, ungelionyesha
busara, kwa kuja kwangu angalau kunisalimia,...tusipoteze muda, mimi nataka kutumia huo ujanja ujanja wako, kwa
lile swal nililowahi kukuambia kabla hujaenda kusoma,...nataka tutumie ujuzi
wako, elimu yako, uzoefu wako, na kampuni yako, kufanya yale
niliyoyakusudia...’akasema
‘Boo-si
mimi kwakweli kwasasa sitaki kufanya kazi kwa mtu, sitaki kabisa kuwa mtumwa wa
mtu,....’akasema
`Sijasema uje kufanya kazi kwangu,...hapana wewe utaendelea na kazi zako, na
ndilo lengo langu, kila mtu ajishughulishe na kazi yake, ninachotaka kufanya ni
kuwekeza hisa zangu kwenye kampuni zenu, na humo tutaendelea kufanya yale
niliyoyapanga, ....’akasema
‘Natumai umenielewa, huwa sipendi kurudia
rudia, mimi ni mtu na wadhifa wangu, nina watu wananiangalia kama bosi wao,
iweje sasa niwe chini ya mtu mwingine, hapana hilo halitawezekana sitaki kabisa
kuchangia na mtu yoyote...’akasema
‘Mrembo, unajifanya umesahau fadhila zangu sio,
au ndio fadhila zenu za punda.Sikia binti najua mlivyo mkifanikiwa hamjali
wafadhili wenu, mnajiona mumefika. Sasa mimi natoa amri, sio ombi tena, na
nataka ulitekeleza, na kwa kuanzia, nataka unifanyie kazi moja kwa hivi
sasa...’akasema
‘Kazi!, kazi gani wewe mtu, naomba unielewe,
mimi ni bosi wa kampuni zangu huwezi kunutuma kazi yoyote, nimeshakuambia kama
ni gharama zako nitakulipa, naomba unielewe hivyo, sitaki kusumbuana na watu,
nina mambo yangu mengi ya kufikiria, ndio maana nilikuja hapa niwe peke yangu,
sasa umeniharibia yale yote niliyokuwa nikipanga kichwani...’akasema huku
akisimama kutaka kuondoka, lakini jamaa huyo akasimama, na kumuwahi wakawa
wameangaliana wakitoleana macho
‘Nimekuelewa kuwa wewe sasa ni bosi, ila
nataka hizi kadi za mualiko ziwafikie walengwa, na hakikisha wanafika kwenye
hoteli yangu ya Paradiso bila kukosa, pia na wewe ni mmoja wa waalikwa...’akasema
na kutoa bahasha kubwa na kuweka mezani
‘Kumbuka...ni muhimu sana, na hakikisha wote
wamefika...na wewe mwenyewe ukiwemo, vinginevyo, utanisahau katika maisha yako,
utapotea katika hii dunia, ....’ Sauti hiyo ilienda sambaba na mikono ambao ilishafika
begani kwake, kama wapenzi waliokuwa wakiongea, mkono huo mmoja ukawa ukitembea
kutoka begani ukashuka na kupanda na kumfanya binti huyu ahisi mwili
ukimsisimuka, akawa anakumbuka enzi zao na huyu buzi
Binti huyu aliduwaa, akageuka kuiangalia ile bahasha kubwa mezani, ambayo
huenda ndani yake kuna hizo kadi, hakutaka kabisa kuigusa, lakini alijua kuwa
kukataa kungelimuharibia kazi yake, kwani huyu jamaa akisema neno ujue kweli
atalifanya, na anaogopewa, hatanii...
Akukumbuka wasichana anaowajua waliopotea kimiujiza,na
kuna fununu kuwa aliowafanya wapotee ni huyu tajiri, japokuwa polisi hawakuweza
kulisibitisha hilo, kwani huyu mtu mwenyewe haonekani, na inajuliana yupo nchi
za nje.
Lakini yeye kama bosi wa kampuni yake hawezi
kufanya hiyo kazi,kwanini yeye ndio afanye hiyo kazi, kuna wahudumu, wanaweza
kuifanya hiyo kazi,huku ni kuzalilishana. Lakini akilini akasema, au nifanya tu
iwe namna nyingine ya kulipa fadhila...hata hivyo sipendi huyu mtu anione
mnyonge, nataka anitambue kuwa mimi sio yule binti wa mitaani tena..’ Alijisema
moyoni
Akainua mkono wake na kuondoa ule mkono wa
huyo bosi, uliokuwa unaendelea kumshika shika, akasogea karibu na ile meza akainama
kuichukua ile bahasha kubwa akiwa na dhamira ya kumrejeshea huyu jamaa na
kumwambia;
‘Go
to hell...’
Aliinama kuichukua ile bahasha pale mezani, na alipoishika, akainua kichwa
kumwangalia huyo tajiri , lakini hapakuwepo wala dalili yake, na macho yake
yalitua usoni mwa mtu ambaye alimfanya atake kutapika, na kujisikia
kichefuchefu.
Mtu huyu alimuona mara moja kwenye jumba la
kifahari la tajiri huyu, siku alipoweka mezani akiwa uchi, mtu huyu japokuwa
alikuwa kavaa suti kali, na kwanza machoni alikuwa kavaa kofia na mawani, na
baadaye akayatoa yale mawani, na kumuangalia huyo mdada...
Mdada alihisi mwili ukitikisika kwa
woga,...akikumbuka kazi ya huyu mtu ambayo ni kutesa watu, na kutoa roho za
wale wasiotii amri ya bwana wake. Mara nyingi akitumwa kwako ukiwa nje ya hilo
jengo lao ujue kuna mawili, kukupa onyo, au kuitoa roho yako. Na ukiwa ndani ya
jengo hilo hiutwa kwa ajili ya kukupa mateso au kuitoa roho yako. Huyu ndiye
mkono wa Diamu...
Huyu mdada alipomuona huyu mtu, kasimama mbele
yake, hakutaka hata kusubiri, woga ulimtanda, akataka kupiga ukelele, lakini
akajipa moyo, alichofanya ni kuichukua ile bahasha na kuanza kukimbia kutoka nje ya
hiyo hoteli, akimpita muhudumu akiwa na vinywaji alivyokuwa akimletea, muhudumu
alibakia kaduwaa...
NB Mambo ndio hayo,
WAZO
LA LEO: Zipo tabia za
kukera, na hazifai katika jamii, lakini wengine wanaona ni kawaida tu, sio
vyema kabisa, tunatakiwa kujifunza jinsi gani ya kuishi na watu kwa ustaarabu.
Kama wewe unapenda kelele, wengine hawapendi kabisa hizo kelele, wengine wana
matatizo ya kiafya, kelele kwao ni adha, lakini utawakuta watu wanafungulia
redio, au televisheni zao kwa sauti kubwa inakuwa kero,..unawaathiri wengine.
Tujaribu kuwa waungwana kidogo.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
mmmhhh ..kujua kusoma ni raha na pia utamu sana...utamuuuu
Post a Comment