'Doctor kuna mgonjwa mmoja anataka kukuona’ sauti ya nesi ikasema.
Doctor Chize, aliinua uso
uliojaa kilevi, macho yalikuwa mazito kufumbua, hakutamani kufanya kazi yoyote siku
hiyo, japokuwa alihitajia pesa, lakini leo alitaka kunywa tu hadi hamu yake iishe,
ilikuwa siku ya furaha kwake, alikuwa keshaweka mambo yake sawa, na anataka
arudi huko majuu kufanya kazi, na kuishi huko huko.
‘Mwambie tumeshafunga, ...au hata mwambie nina mgonjwa mwingine,
mwambie chochote unachoweza, unaona leo sipo sawa, kwani msaidizi wangu hayupo
mpeleke huko kwake, leo sitaki kukutana na mgonjwa yoyote, leo ni siku yangu ya
furaha...’akasema na kucheua huku akijibaragua kujiweka sana.
Yule nesi wake akawa anamuangalia kwa macho ya huruma,
keshamfahamu bosi wake tabia yake, lakini mara nyingi hata alewe vipi, huwa
hakatai kuhudumia mgonjwa, alishangaa leo imekuwaje, hata hivyo alikumbuka
jinsi huyo mgonjwa alivyomsisitizia kuwa ni muhimu sana aonane na docta
mumiliki wa hiyo dispensary, kwahiyo akawa hana la kufanya zaidi ya kumsihi bosi
wake, kuwa huyo aliyekuja ana umuhimu sana.
‘Docta huyu mwanadada aanonekana ni tajiri, na anasema.....’
akaanza kumsihi bosi wake na docta akasema;
‘Nimeshakuambia umwambie kuwa leo sina muda wa kuonana na mgonjwa
yoyote hata awe nani, kama ni tajiri, mpeleke kwa msaidizi wangu, huyo ndiye
atakuwa bosi wenu, ....mimi nakwenda zangu Ulaya,...kwahiyo huyo atakuwa kila
kitu, unanisikia vyema,...’akasema docta kwa sauti ya kufoka, na nesi alitaka
kumjibu lakini akaghairi akataka kama kuondoka, lakini akawa kasimama
akimuangalia huyo docta.
‘Kwani huyo mgonjwa ni nani mbona unamshupalia sana kuonana na
mimi...una miadi gani na yeye ni mchumba wako, ni nani kwako?’ akauliza
alipokumbuka jambo, kuwa kweli alihitajia pesa kidogo kumalizia mambo yake
kabla hajaondoka, basi huenda hizo pesa atakazo lipwa haitakuwa na haja ya
kuingie kwenye mahesabu ya ofisi.
Akakumbuka pia kuwa kuna pesa inahitajika kwa malipo kadha wa
kadha pale alipopanga, pia kuna malipo ya kodi za serikali, na pango la hiyo
ofisi vyote hivyo vinatakiwa vilipwe kabla yeye hajaondoka, akawa anapiga mahesabu
yake kichwani, kujua anahitaji kuwa na shilingi ngapi,halafu akasema;
‘Aaah hizo pesa zitapatikana tu, hata hivyo kama kuna madeni
yatashindikana kulipwa, kazi hiyo itafanywa na msaidizi wake, kwahiyo
hahitajiki kuumiza kichwa zaidi tu....
‘Hahaha mimi sasa ni mtu wa majuu, hahahaha...’akawaza anacheka akikumbukia
enzi zake za msoto, na kumfanya nesi wake amuangalia kwa mashaka, na docta
alipoona huyo nesi bado kasimama hapo akasema;
‘Naona huyo mtu ni muhimu sana, hata mimi bosi wako hutaki
kunisikiliza au sio?’ akauliza
‘Sio hivyo bosi natumai mwenyewe ungemuona huyo mgonjwa,
usingelikataa kumuhudumia,...’akasema
‘Kwani yupoje,....unajua wewe nesi, unanifahamu sana, sijawahi
kumkatalia mgonjwa yoyote, lakini leo ni siku muhimu sana kwangu, mimi nimetoka
mbali sana, ...nimasota sana, sitaki mchezo kwenye kazi, ukiona nakataa jambo
ujue kuna sababu kubwa sana,.....’akasema
‘Nakufahamu sana, bosi wangu, lakini pia nafahamu jinsi gani
unavyowajali wagonjwa wako, najua nikimkatalia huyo mtu akaja kukutana na wewe
tena baadaye utakuja kunilaumu, ndio maana nakusihi kuwa ni muhimu umuone yeye
mwenyewe...’akasema
‘Hahaha, wewe nesi, unanikumbusha mbali sana, hapa nilipo nilikuwa
nawaza maisha yangu ya msoto, unajua kusota, basi mimi nilisota, hadi kugeuka
omba omba,..tumetoka mbali kwa kweli...’akasema huku anatabasamu na kichwani kumbukumbu
hizo za msoto, zikamjia kama njozi fulani;
***********
Alianza kukumbuka pale, alipofukuzwa kazi hospitali ya kubwa hapa
nchini kwa kujihusisha na wizi wa madawa na utoaji wa mimba isivyoruhusiwa.
Siku alipoitwa ofisini na kupewa barua ya kusimamishwa kazi eti kwa ajili ya
uchunguzi ya madai kuwa yeye anajihusisha na wizi wa madawa, na pia kuna kesi
ya kujibu polisi, alijua ndio basi tena taaluma yake ya udakitari ndio mwisho
wake, hakupewa hata nafasi ya kujitetea, hata hivyo angejitetea vipi wakati ni
kweli hayo yote aliyafanya.
Chamuhimu alichokiona ni jinsi ya kuwakwepa polisi, na ili
kufanikiwa hilo akawa kajichimbia uswahili ndani ndani, na huko akawa anatibu
watu kisirisiri, hata hivyo dawa alizokuwa nazo zikamuishia na matuzimi yake,
kodi ya nyumba vikawa vikubwa kuliko pato analilipata, akajikuta hana kitu
kabisa.
Siku moja aliamuka na kujikuta hana hata senti moja, siku hiyo
hataisahau katika maisha yake.
‘Hawa watu wamenitime kweli, maana wamenifukuza kipindi ambacho sikuwa
na pesa kabisa...’akasema akijalaumu
‘Lakini haya yote ni sababu ya yule mrembo...ole wake siku nikija
kukutana naye, nitahakikisha nakwenda polisi kwasababu nyingine...’akasema
Jamaa huyu kilichomuhaibu zaidi yeye ni mtu wa matumizi, japokuwa
alikuwa akipata pesa nyingi, kutokana na biashara yake hiyo haramu ya kuiba
madawa, na kwenda kuyauza kwenye maduka ya mitaani.
Alichokuwa akifanya ni kuwa, yeye kwa vile alikuwa ni mmoja wa
viongozi hapo hospitalini, alikuwa na mamlaka ya kuagiza kiasi kikubwa cha
dawa, na kudai kuwa zinapelekwa mahali kwingine, yeye mwenyeweanaingia bohari
ya madawa, anaongea na mtunza store, anapewa kiasi anachohitajia, anajua jinsi
gani ya kuandika.
Yeye hakuishia hapo, kwa vile alikuwa ni docta wa akina mama na
upasuaji, basi alianza tabia ya kuongea na wagonjwa waliokuwa na matatizo ya
kutaka kutoa mimba, akawa anawahudumia nje ya hiyo hospitali, na akajulikana
kwa kazi hiyo.
Alitarajia akiwa mitaani atafungua dispensary yake aendeleze hiyo
kazi, lakini aliogopa polisi, kwani alikuwa akitafutwa kwa kosa hilo hilo, na
akashindwa aifanyie wapi hiyo kazi, na kila siku akawa anasikia kuwa anatafutwa
na polisi, na hapo akashindwa kabisa kutoka.
Alikaa siku mbili hajui hata afanye nini, na mwishowe uzalendo
ukamshinda, akawa anapiga mguu kwenda kwa marafiki zake kwa siri, kuomba
msaada, kwani hali ilishaanza kumuendea vibaya, hakuwa mtu wa kubakia nyumbani
kabla alizoea kubadili bar leo hii keshi ile, na matumizi yake yalikuwa sio
haba.
Siku zikaenda na maisha yakazidi kuwa magumu, akaamua arudi kule
hospitalini ajaribu kuonana na marafiki zake, au kama anaweza kuongea na yule
mtunza store, ili awe kuchukua dawa, akiuza pesa watakuja kugawana naye,
akajipange vyema jisni gani ya kumshawishi. Siku hiyo alitaka afanye juu chini
ili biashara yake ya dawa, iweze kuanza tena;
‘Ni lazima niongee na mtunza store, mimi nafahamu siri zote za
pale hospitalini, na akijafanya kunikatalia nitamwambia nitamchomea na yeye,
maana tulikuwa tunashirikiana naye, nilimtetea kuwa yeye hahusiki kwa lolote,
sasa ni zamu yake kunilinda...’akasema huku akitembea kuelekea huko
hospitalini.
Akiwa njiani kuelekea huko, mara akamuona jamaa akitokea dukani,
jamaa huyo alikuwa kabeba mfuko, kuonyesha ametoka kununua kitu, na alikuwa
akieleka kwenye gari lake, alihisi kama anamfahamu, akaona ajaribu bahati yake,
alitaka apate angalau pesa kidogo ya nauli maana kutembea nako shughuli, akamsogelea,
na yule jamaa kwa muda huo alikuwa akifungua mlango wa gari lake.
‘Ndugu kama nakufahamu vile.....’akasema huku akinyosha mkono
kusalimiana na hauyo jamaa, na yule jamaa akasimama akimuangalia usoni kwa
mashaka, kwani dunia ya sasa imeharibika, unaweza kusalimiana na mtu kumbe ni
mwisi wa mazingaumbwe, na yule mtu akaonekana kumtambua, na haraka yule mtu
akasema;
‘Wewe si docta Chize, mmh, school
mate huyo, upo docta....’akasema huyo jamaa, akizidi kuonyesha mshangao
usoni, ni kweli huyo alikuwa mmoja ya watu aliosoma nao, na anakumbuka walikuwa
wakitaniana sana wakati wapo shuleni, wao wa masomo ya sayansi walikuwa
wakiwatania wa masomo mengine yasiyokuwa ya sayansi, kuwa masomo yao laini-laini.
Jamaa huyo waliachana kipindi yeye anakwenda kuchukua udakitari,
na hawakuweza kuwasiliana tena, na kwa mara ya mwisho walionana wakati jamaa
huyo alipofika hospitali ya Muhimbili akitaka kujaziwa fomu yake ya taarifa fulani
za kiafya, kwa ajili ya kufanikisha mambo yake, na walipokutana walitambulishana
na hawakuna na muda wa kuongea kila mtu alikuwa na haraka zake.
Leo wanakutaka tena, lakini kwa hali ambayo ilimtia mashaka huyo
mwenzake, hakutegemea kabisa kumkuta huyo dakitari katika hali hiyo, kachoka
ile mbaya, mijasho inamtoka kwa kutembea juani,....
‘Nakukumbuka kumbuka, hebu nikumbushe kidogo, tulikuwa wote wapi
vile....’akasema Chize, ni kweli kutokana na nakama za maisha na kazi yake ya
kukutana na watu wengi, akili yake ilishaanza kumsahau huyo jamaaa, na jamaa
akasema;
‘Wewe si ndio dakitari Chize, tuliwahi kusoma wote A-Level,japokuwa
wewe ulikuwa mchepua wa sayanasi, lakini vipi kulikoni, mbona upo mitaani huku
unaonyesha kuchoka sana, vipi umegomewa na wagonjwa nini...maana pale hospitalini
kwenu hapaishi migomo?’ akatania huyo jamaa
‘Kabla hatujaendelea na hayo maongezi, naomba unipoze koo, hapa nilipo
nina kiu, nina njaa, huwezi amini....’akasema docta.
‘Siamini, kwanini lakini, ...?’ akaulizwa huyo jamaa kwa mshangao
‘Kwanza fanya kama nilivyokuambia, naona wewe ni matawi ya juu, mmh,
nona una gari, umenawiri, mmh, nyie watu wa masomo laini laini, mnakula sana
nchi...’akasema
‘Acha utani wako, hakuna masomo laini-laini, hayo ni mambo ya
shule, ukiwa mitaani ni akili kichwani mwako...’akasema
‘Ni kweli, kama hivyo, naona umejilengesha mwenyewe,
nimeshakukumbuka vyema sasa, ulikuwa mtani wangu sana wewe...nakuona sasa upo
softi- softi, sisi tunaumiza kichwa nyie mnakula pesa ya nchi kilaini...sasa
nimekupata, ni lazima unisaidie, nisije kufa kwa njaa, je nikifa mimi docta mtatibiwa
na nani...’akasema huku akijua hapo keshapata chochote.
‘Sawa docta japokuwa nina haraka,lakini...mmmhh, pia nilikuwa nakuhitaji sana, sasa mhh naona
ni fursa pekee ya kukutana na wewe, nilikuwa natafuta mtu kama wewe....’akasema.
‘Sawa, kama kuna demu wako anataka kucholopoa.... wewe niwezeshe
tu, kazi rahisi tu, ni pesa yako tu..na mhali pa kujihifadhi maana hawa watu wa
magwanda njaa imewazidi, hawanipi nafuu....hawajui siku hizi kila mtu anafadii
mezani kwake....’akasema na jamaa yake akacheka, akijua huenda docta anamtania,
na akasema;
‘Docta bwana, huogopi kuharibu fani yako, ...haya twende pale
hotelini, mimi nitakununulia chakula nikuache ule maana nina mtu ananisubiria,
wewe ....’akasema na huyo jamaa akamkatiza na kusema;
‘Hapana,..huo ujanja wa mjini si utaki, nataka nakula na wewe upo
karibu, nimekuambia hawa watu wa magwanda na njaa zao wananimulika kila mhali
lakini ukiwepo karibu hawatanishuku....hata hivyo nina shida nyingine muhimu
sana nataka unitatulie, maana maisha sio mchezo, huwezi amini, chumba
nimeshafukuzwa, unaweza kuamini hilo docta mzima kama mimi nazalilishwa,
....’akasema na jamaa yule moyoni akasema;
‘Sasa nimeshampata huyu mtu kirahisi kabisa...kama hali yake
imefikia hivyo, basi naona ni bora nianzane naye na huyo mwingine nitakutana
naye baadaye...hapa nimeshapata mtu mwingine ....’ Akawa anasema kimoyo moyo huyo
jamaa na sasa akituma ujumbe wa maneno kwa mtu ambaye alitarajia kukutana naye,
kuwa kapatwa na dharura kwahiyo wakutane kesho
Kweli wakaondoka hapo na hadi kwenye hoteli iliyokuwepo karibu,
wakapata chakula, na jamaa anavyopenda kunywa, akaagiziwa kinywaji akanywa
‘Unajua rafiki yangu sijawahi kula hivi kwa miezi kadhaa
sasa...’akasema kilevi levi
‘Unafunga au?’ akaulizwa
‘Hahaha, wewe vipi bwana, mimi nifunge!,... hahaha, na wala sijui
kufunga ni nini, kwanini nigomee kula bwana, kama nina pesa, natumia,
....,,mimi namshukuru mungu kuwa sio bahili wa matumizi, nikiwa nazo nakula na
kusaza, na kinywaji ndio maji yangu...’akasema
‘Ndio maana unakuwa hivyo, maana hujui kupangilia matumizi yako,
hata uwe na pesa vipi kama huna mpangilio mnzuri wa kipato chako ni lazima
utaishiwa, unakumbuka ule usemi pesa bila daftari hupotea bila
habari...’akasema huyo jamaa
‘Achana na uswahili bwana, maisha yenyewe yapo wapi,..tumia ukiwa,
na wasaa, tumia ukiwa nazo, maana utakufa wenzako watakuja kutumia bila kusaza,
sasa utapata faida gani, mimi ni docta nimeona watu wakifa, wengine hata
hawastahili kufa, wanaacha utajiri wao nyuma...’akasema
‘Kufa kupo, lakini sio sharti la kutumia ovyo, haya niambie
ulikuwa na shida gani zaidi maana nina maongezi mengine...’akasema
‘Ndugu yangu, niseme huu mguu ni wako japokuwa sikutarajia
kukutana na wewe hapo barabarani...hapa nilipo sina pesa, unajua kuishiwa, basi
mimi ni mfano wa hao watu walioshiwa, na sio mfano, ila ni kweli nimeishiwa,
yaani hapa nimebakia mimi na mwili wangu tu,....’akasema akijiangalia.
‘Kwa vipi bwana docta, mbona nasikia unahudumia hata watu mitaani
wewe wanakufahamu sana kuwa ni docta bingwa, hapokuwa haujafikia kuitwa
hivyo...au sio wewe wanayekutaja docta Chizi, kwasababu ya kulewa, ukilewa ndio
unatibu vyema...’akasema
‘Unajua watu wakitaka kukutukana hawakuchagulii tusi, waache
waniite hivyo wapendavyo, lakini mimi bado Docta Chize.., ilimradi naingiza
mapesa..ila sasa wameniharibia, sasa wamenipata maana nipo kwenye mawe huwezi
amini...’akasema
‘Kwanini?’ akaulizwa.
‘Hawa wapuuzi walinisimamisha huko kazini nilipokuwa nimeajiriwa,
eti wanifanyie uchunguzi, na miezi mingi imeshapita, hawajaniita tena, sio ndio
kufukuzwa kazi huko...’akasema
‘Kwanini usiende kujitetea, wewe ni docta mzuri
watakusamehe...’akasema
‘Hivi kweli kuna Uzuri unaweza kukaa kwenye ubaya, hilo halipo,
hata uwe mnzuri,lakini kama una doa la ubaya, wewe sio mnzuri tena....ni ujanja
tu, huwezi kusema kitu kizuri kimefanya mabaya, hilo halipo ni propaganda na
kutokuelimika, mimi najijua mwenyewe...’akasema
‘Kwanini?’ akaulizwa
‘Kwanini, kwanini....we hujui, nikuambie, mimi nimesota sijwahi
kusota kihivi, maana hawa watu walinishitukizia, kabla sijajipiga mzinga wa
maana, kuna mzigo uliingia karibu nilishaupangia mahesabu yake, wakaniwahi
kabla sijafanya hivyo, unajua huku uraiani mzinga wa kikweli ni jinsi gani ya
kupata dili, ya kuingiza pesa, ....’akasema
‘Docta acha utani, wewe sio mtu wa kufanya hayo, ina maana ulikuwa
unafanya dili za kuingiza pesa kinyume na sheria, unakwiba..?’akaulizwa.
‘Hahaha, ndio maana nikakuambia kuwa huwezi kusema mimi ni mnzuri,
uzuri wangu una doa la ubaya, labda utafute jina jingine huo uzuri unaoutaja wewe,
hata hivyo yote ni maisha, unafikiri ningelifanya nini mimi kwa hali kama hiyo...’akasema
‘Kwani ilikuwaje?’ akalizwa
‘Unajua ukiwa kwenye nafasi yako ya kazi kuna mambo mengine
inabidi yafanyike tu vinginevyo hutaweza kujijenga, hutaweza kustarehe, na
starehe ni gharama, sijui ni nani aliwatonywa hawa watu, nilitaka nifanye vitu
vyangu halafu nipotee kwa muda,...wakaniwahi nikiwa sijajipanga vyema,...ila
safarini nyingine, kama watanirudisha, ni lazima nijipange, nitafanya kitu
wenyewe hawataamini, na hapo nitapotea kabisa...’akasema
‘Sasa kwanini walikufukuza, maana mimi hapo sijakuelewa,
hujaelezea kilichosababisha kwa wewe kufukuzwa?’ akaulizwa
‘Sijafukuzwa bwana, wamenisimisha eti kwa kisa la udokozi...wao
wanaita hivyo, eti nimekwiba madawa,....unajua kuna watu wanapesa zao,
wanahitaji dawa, na dawa zipo ningelifanyeje, nikaona dawa ni kutoa dawa,
nipate pesa....’akasema na huyu jamaa akavutiwa na sana na kauli hiyo.
‘Yah, hebu niambie ulifanyaje maana hapo ni muhimu sana, kutumia
akili kwa ajili ya kupata pesa hilo ni jambo kwangu muhimu sana, hebu nifafanulie
hapo kidogo...’akasema
‘Hao watu wanasema hawana pesa, sio kweli kuwa hawana pesa, ni
kwamba hawajui kuzitafuta hizo pesa...hebu niambie dawa zipo nyingi tu...halafu
hospitali kama hiyo ikose pesa, na wakati wateja wake ni wagonjwa,na wagonjwa
ni wengi sana, nikaona hawa watu wanahitajia fundisho dogo tu, nikawaonyesha
japo kwa siri, jinsi gani ya kutafuta pesa....’akasema
‘Ukafanyeje...?’ akaulizwa
‘Mbona unaniuliza kama polisi, usije ukawa shushu...’akasema
‘Hahaha, mimi na mambo hayo ni kama maji na mafuta, usiwe na
wasiwasi kabisa,mimi ni rafiki yako nimesoma na wewe siwezi kukutosa, wewe
niambie maana nahisi unaweza ukanifaa sana...’akasema
‘Ni hivi, eti wao wanaweka madawa mpaka yanaota ukungu, wagonjwa
wakifika, wanaambiwa hakuna dawa, hizo dwa wanamuwekea nani, nikaona hawa watu
hawanajijui,halafu wakanichagua mmoja wa viongozi wa bohari ya madawa,
nikacheka kimoyomoyo, nikisema kichaa kapewa rungu,...nikasema basi kama hakuna
dawa mimi nitakuwa nazo, ...nikawa nazibeba kilaini, na wagonjwa wakawa wanazipatia kwingine,
mitaani.....’akasema.
‘Na hilo la kucholopoa vipi,...?’ akauliza huyu jamaa akiona
anapoteza muda, na kile alichokitaka keshakifahamu.
‘Hahaha ina maana huyajui hayo,...ipo siku utanitafuta, ...Mimi ni
docta bwana, siunajua nimesomea nini, mambo ya kina mama kwangu ni rahisi sana,
kuna akina mama hawataki kuzaa, na ...’akasita na kuanza kuongea kwa sauti
ndogo
‘Unasikia ngoja nisije kukamatwa hapa, tuongee pole pole, unaye
msichana ana tatizo hilo....?’akasema akimsogelea huyo jamaa huku akiangalia
huku na kule, na jamaa akawa anashangaa kwanini docta anaogopa kuongea kwa
sauti.
‘Hapana kwasasa sina...’akasema
‘Unajua hii fani yetu wakati mwingine mshahara hautoshi,mimi kama
docta nahitajia kula vizuri, kulala vizuri, kunywa, kustarehe, ili kichwa
kitulie, sasa vyote hivyo ni gharama, na muda mwingi unakuwa kazini,unapambana
na matatizo ya watu, kichwa hakiwezi kuwa sawa, kama hutapata mahitajio hayo
muhimu...’akasema
‘Nakuelewa sana...’akasema huyo jamaa
‘Watu hawajui, kazi inayotumia kichwa inaumiza sana,..kuliko ya
mitulinga, ubongo unachoka haraka sana, na ili uufanye usiwe tatizo, basi
utimiziwe mahitajio muhimu, kama hayo niliyokutajia....’akasema
‘Sasa hawa jamaa wanaoitwa watawala, siwapendi hawa jamaa, meneja
utawala, meneja masihali, hamna kitu hapo, kazi yao kuongea tu, wengine
mnaumiza kichwa,...nikaona oke, kama ndio hivyo, na mimi nimjanja zaidi yao
nikawa napata vikazi kazi vya ziada, baada ya watu kunitonya, wakaniambia wewe
una utajiri, lakini hujijui tu...’akasema
‘Ehe...kweli wewe una kipaji kizuri, watu wanakusifia...’akasema
huyo jamaa
‘Ndio hapo nikaamuka, nikajua kumbe na uzuri wangu ninaweza pia kufanya
ubaya na ukakubalika, na nikajifunza jambo, usione watu wanapiga propaganda za
jambo nzuri kwa watu wabaya, ili tu lile jambo lionekane baya,...kweli mimi ni
docta mnzuri siwezi kukataa, lakini nina tamaa ya maisha mazuri, ndio maana
nikasoma sana, hilo siwezi kukuficha, kila mtu anahitajia hivyo, sasa kwanini
mimi nijidanganye, kamwe sikuweza kujidanganya...’akasema
‘Una maana gani?’ akaulizwa
‘Kuna hawa kina mama, eeh, nisisema akila mama, niseme hawa watu
kama nyie wenye pesa za bure, mumewapa watoto wa watu mimba,...maana wanaume jamani
mna dhambi sana nyie, mmmh, siwezei kujikataa, kuwa na mimi nimo, ila
ninachotaka kusema ni kuwa, watu kama nyie mnakuja kwangu kuomba niwasawazishie,
siwezi kukataa, ilimradi tu uwe na cash,
....sasa nikuambie kitu, kama unaye binti, msichana mwanamama, kapata mimba
isiyotegemewa, niletee, tutaelewana tu,....’akasema kwa sauti ndogo ndogo.
‘Kweli eeh, docta bwana, ina maana umefikia hapo, sasa...mmh, kwanini
usifungue hospitali yako...?’ akaulizwa
‘Sikiliza bwana, hayo ya hospitali yangu kwa sasa sio dili,nielewe
hapo, kuna tatizo, lakini kama nilivyokuambia wewe kama unaye usijali,mlete,....mimi
naitoa kirahisi tu, awe mwanafunzi au msichana wako atadunda, kama vile
hajawahi kupata mimba....’akatabasamu huku akitikisha kichwa kwa kujiamini.
‘Mhh, hiyo sasa kali...lakini nakuamini sana docta...’akasema.
‘Unajua mimi mwanzoni nilikuwa nawasaidia watu, unajua hilo ni
tatizo, likikupata utajua ugumu wake ulivyo, mimi nikawa natumia ujuzi wangu
kuwasaidia watu kama hao,... kuna watu wakanichomea mbovu....’akasema
‘Oh, wakakukushitaki au...?’ akaulizwa
‘Mhh, kitu kama hicho,usisikie kuna watu wana roho mbaya....lakini
bado naifanya kwa siri, wewe kama unaye mwanamke anataka kutoa au kusafishwa,
wewe nitakulipisha kidogo tu sio sana kama wengine..wewe ni rafiki yangu bwana,
unaona jinsi ulivyonifadhili leo....’akasema akiongea kwa sauti ndogo.
‘Hapana mimi sipo huko kabisa...hebu sasa nikuulize kwanini uogope
kufungua hospitali yako mwenyewe, ukajisajili rasimi, kwani hiyo ni fani yako na
watu wenyewe wanahitajia kufanyiwa hivyo...?’ akaulizwa
‘Kuna watu wabaya wewe wana
roho zao mbaya,...usiwaone wanapita mitaani wamependeza, wameniharibia, lakini,
hata hivyo nimeshamfahamu mbaya wangu ni nani, huyo jamaa nina usongo naye, ipo
siku atakuja kwenye anga zangu, nitamfundisha kulewa, hahahaha...’akasema na
kucheka na huyo mwenzake akaangalia saa yake, na docta alipoona hivyo akasema;
‘Nashukuru sana school mate
wangu, sasa cha muhimu ni wewe kunitafutia usafiri, nikalale nyumbani maana
nimechoka...nimetembea leo, nisingelikuona leo sijui ingelikuwaje..., unajua
kuchoka, hapa miguu inauma, kiatu chote kimakatika, yaani ni aibu kwa docta
kama mimi kuvaa hivi, lakini ipo siku...’akasema kilevi huku akijikagua
miguuni.
‘Usijali ndugu yangu ipo kweli, haina haja ya mimi kukutafutia
usafiri, mimi mwenyewe nitakupeleka nyumbani
kwako, nataka nihakikishe umefika nyumbani, maana ulivyolewa, unaweza ukapatwa
na ajali,...lakini sasa umesema umefukuzwa na baba mwenye nyumba au sio, sasa
unaishi wapi....?’akaulizwa
‘Hayo ya kuishi wapi niachie mwenyewe, ...unasema nimelewa,
hahaha, mimi nilewe,...hizo chupa nne tu nielewe, unanitania,...wewe kama
unataka kujilengesha tena, nichukue kwenye gari lako, nitakuambia wapi pa
kunishusha, ukinichunguza sana, hutaniweza...unasikia, wewe nitakuambia wapi
unipeleke, tukimaliza hapa, au unataka kuniagizia kinywaji kingine, maana mimi
baado kabisa...?’ akauliza huku akijilambalamba
‘Umeshalewa bwana docta, ila kuna kitu muhimu nataka kuongea na
wewe,ndio maana sitaki uelewe, nataka unisikilize kwa makini na unielewe, lakini
kama upo tayari kuongea, na sio swala la mambo yako, ni dili nyeti
kidogo,...’akaambiwa
‘Wewe sema usiogope....’akasema docta
‘Nataka tuongee ukiwa makini, lakini hapa nakuona umeshalewa, na
umesema umechoka na hili ninalotaka kukuambia ni muhimu...kutokana na wewe na
udocta wako, je upo tayari?’akaulizwa, na docta akamuangalia huyu mtu kwa macho
ya udadisi, akilini akajiulize asije akawa anaongea na shushu,akataka kusimama
kuondoka, lakini akasita, akasema;
‘Wewee, ... mimi ni mtoto wa mjini bwana, huwezi kunipata kirahisi, ngoja
niondoke zangu, kama umetumwa kunichunguza, hapa hupati kitu....’akasema akisimama kuondoka huku akipepesuka, na yule jamaa akamshika, na kusema;
‘Sikiliza Docta, mimi nimeshakujua vilivyo, kwahiyo ni vyema ukanisikiliza, tukaelewana, vinginevyo ....’akaambiwa na docta akabakia ameduwaa.
NB: Jamaa anataka waongee nini?
WAZO LA
LEO: Uwongo
na uzushi ni tabia chafu sana, siku hizi tabia hii imekuwa ni fani ya watu,
watu hawaogopi kuzisha uwongo, au kuutengeneza uwongo, ilimradi tu watu fulani
waonekane wabaya, na wao waonekane ni wazuri, hata kama ni kuua, hata kama
mzushiwa atafungwa, au kufukuzwa kazi, hawajali familia za wenzao, ilimradi
wanakipata wanachokitaka.
Jamani, uzushi, uwongo ni
jamii ya fitina, na fitina ni mbaya
sana, mfitinishaji ni mbaya kuliko hata mchawi. Tuache hii tabia kwani mfitinishaji
kalaaniwa, hadi hapo atakapojirekebisha na kutubu dhambi zake.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment