Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 26, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-83‘Sikilizeni, huu sio utaratibu, lakini kutokana na hali isiyoweza kuzuilika, tumeona kuwa shahidi wetu wa awali ambaye alikuwa akiendelea kutoa maelezo ya ushahidi wake, asubirie kwanza,  ili tumpe nafasi mzee wetu huyu ambaye kutokana na hali yake hataweza kusubiria, tukae kimiya tumsikilize....’akasema hakimu akimuangalia mzee

Yule mzee alikuwa kakaa kwenye kiti chake huku akisoma makabrasha fulani aliyokuwa nayo mkononi, na nyuma yake kulikuwa na yule askari, akiangalia huku na huku kama kuhakikisha kuwa hakuna lolote baya dhidi yam zee huyo.

‘Mzee tunakupa hii nafasi japokuwa umetuvurugia utaratibu wetu, hilo unalifahamu vyema,lakini nina imani hicho unachikitaka kukiongea kinaweza kuziba hilo kosa...’akasema hakimu na yule mzee akatikisa kichwa kukubali

‘Sasa unaweza kuendelea na maelezo yako, na ili uweze kuongea kwa nafasi, hebu wakusaidie ukae vyema...’akasema hakimu na yule askari aliyekuwa nyuma yake, akamsogelea mzee kwa mbele, lakini mzee alimuashiria kuwa yupo sawa, na hakimu akaendelea kutoa maagizo

‘Wakili muendesha mashitaka, huyo naona ni mtu wako...au?’ akauliza hakimu, na wakili muendesha mashitaka, akasema;

‘Ndio muheshimiwa hakimu, naona ni mtu wangu,...lakini naona hahitajii kuongozwa, yeye anajua jinsi gani alivyojipangilia kutoa maelezo yake....’akasema wakili muendesha mashitaka, nahakimu akamgeukia mzee na kusema;

‘Haya mzee unaweza kuendelea, kutuambia yale yote uliyokusudia kutuambia, hatutaki kukuwekea pingamizi,...’akasema akiwaangalia wakili watetezi, ambao walionekana kuwa kimiya zaidi, na mzee akaanza kuongea kwa sauti ile ile, akasema;

‘Kundi hilo haramu lipo, na mimi nimepata bahati ya kuwa mmoja wa viongozi waliochaguliwa katika vitengo maalumu, sikuwa kiongozi mkubwa lakini nilipewa nafasi inayonifaa, nikapewa ulaji, ni nani anakataa ulaji eti jamani...’akasema na watu wakaguna, lakini wakakatisha kama vile kuna sauti imetoka ya kuwanyamazisha.

‘Mimi nilikuja kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kundi hilo baada ya kuonekana kuwa ninafaa, kwasababu nilishakuwa kwenye kundi la njaa kali, wakati nilikuwa mtu kwenye nafasi nzuri, na baadaye kutupwa kijijini, hohe hahe, na wanasema fainali uzeeni, na uzee wangu uliishia pabaya, mimi sikuwa fisadi..waulize niliowahi kufanyakazi nao,...hata hivyo, licha ya kupata huo ulaji, mimi pia nilikuwa na lengo langu..’akasema

‘Mimi nilichukuliwa kijijini ambapo nilishatupwa huko kusubiri siku yangu ya mwisho , maana katika utaratibu wa nchi zetu hizi za Kiafrika, hakuna jinsi ya kuwatunza wazee, ukistaafu, basi ujue lako, labda uwe ulikuwa na jina kubwa, mwanasiasa labda...lakini kama ulikuwa mtendaji wa hivi hivi, ujue unalo, utaishia kubezwa, kuwa ulikuwa hukutumia vyema meza yako,...na sana sana wanakutayarishia bima za mazishi yako,....’akawa kama anacheka.

‘Mimi nikiwa kijijini nilipata taarifa kuwa nahitajika kwenye kazi maalumu, sikuamini, na nikajua labda kuna mafao yangu yalibakia, au kuna lawama za madeni natakiwa kwenda kutoa ufafanuzi, lakini nilipofika nilikutana na jambo jingine kabisa, nikaambiwa kuwa kuna kazi maalumu ya kuweza kulifichukua tatizo, tatizo linalolalamikiwa kuwa kuna kundi baya...

‘Kundi gani?’ niliuliza na nikaambiwa jinsi gani watu wanavyolalamika kuwa kuna kundi limejijenga na kula mali ya umama, na kujiwekea himaya ya kificho...na maelezo mengi tu...

‘Ndugu zanguni, ndugu muheshimiwa hakimu, kundi hili lipo na kweli lilianzishwa lakini kutokana na uchunguzi wangu yote ni kutokana na hali mbaya ya kimaisha inayowakabili watu wengi,...’akasema na nikasikia watu wachache wakipiga makofi na hakimu akagonga rungu mezani na kukawa kimiya

‘Mimi siongei hili kwa nia ya kulitetea hili kundi, bali huo ndio ukweli, huwezi kumuajiri mtu kwa mshahara usiweza kukidhi mahitaji yake, akakufanyia kazi siku nzima, na baadaye anastaafu, hajui hata ataanzaje maisha yake, angalia wakulima wanalima kwa shida mwisho wa siku anapata nini, angalia mfanyabiashara anapata nini, kila anachopata kinanyakuliwa kwa kodi nyingi tu...

‘Angalia sisi tuliojituma kwa nia moja, kwa uzalendo, ni kitu gani tulikuja kukipata,...sasa hivi wale waliokuwa na majina mazuri watatupiwa mikoani, kuwa wakuu , nakadhalika, lakini hao ni wale waliokuwa na majina mazuri, je wale ambao hawana majina mazuri, lakini walifanya kazi pengine zaidi ya hao wenye majina mazuri wao wanapewa nini....

‘Japokuwa muasisi wa kundi hili alikuwa msomi,...lakini yeye alimuona baba yake alivyoteseka baada ya kuitumikia nchi yake kwa shida, akaingia vitani, na aliporudi kwenye vita ile ya nduli, alikuwa kama mwehu,...unajua mambo ya vita yalivyo, ni nini alikuja kukipata, ...mwehu atasaidiwa nini,..lakini bahati nzuri mtoto wake akapata msaada na elimu yake, kutoka kwa baba yake mdogo, akamsaidia akaenda nje kusoma, na huko ndipo alipokutana na wenzake wakabuni hilo jambo..

‘Yote hayo jinsi gani kundi lilivyoanzishwa, wahusika, viongozi wake, yapo kwenye nyaraka za siri zilizoibiwa...wapo watu wengi sana, na wengi wameunganishwa hata bila kujijua, wanatumika tu..hao mliowakamata ni chambo tu, ...mtakuwa mnawaonea bure, wapo wengi sana...’akasema

‘Siwatetei, na walichokifanya sio jambo nzuri, ila ninachotaka kusema ni kuwa, ili tupate raia wema, wazalendo, ni lazima tuwe na sheria ya kuwalinda raia, sheria ya kuwafanya wafaidi maliasili yao, sheria ya kuwawezesha wawe na maisha bora...ni muhimu sana twende na wakati, unaomjalia mzawa zaidi, angalieni mataifa ya nje wanavyofanya, ulaya na marekani, wewe muafrika ukifika kule unapewa nini..

‘Haya natoa mfano mdogo wa bima za uzeeni, mnajua thamani yake inakuwa haipo wakati mtu huyo anastaafu, wakati anakatwa hayo makato hela hiyo ilikuwa inalipa, lakini wakati anastaafu thamamani yake sio sawa na alipokatwa kwenye mshahara, je hili wanaliona, je hili lipo kwenye sheria ya kulinda thamani ya bima ya uzeeni...huo ni mfano tu mdogo.

‘Kama raia wataishi maisha bora, wakawa wanalindwa, mimi hapa sizungumzii kulindwa kiusalama, hilo la kiusalama linatelekezwa, mimi nazungumzia kulindwa kinafsi, mtu arizike,..akijua kuwa ninapata pato la halali kwa haki, kutokana na jasho langu...hebu angalieni malipo wanayolipwa watu wa nje wanapokuja kufanya kazi hapa nchini,lile ndilo pato halali la mfanyakazi, lakini kwanini alipwe yeye hivyo wewe ulipwe kiduchu...

'Jamani kiuadilifu ,hebu  linganisha na malipo ya hawa watu wawili, wanavyolipwa, unategemea nini hapa,...utaona dhuluma ilipojikita, hilo nililiweka wazi kwenye ripoti yangu, lakini ripoti hiyo iliwekwa kapuni....’akatulia

‘Upo ubaguzi mkubwa wa chini kwa chini, na ubaguzi huu unazaa chuki, ni moto uliofunikwa na majivu, mtu anaona kumbe mimi sithaminiki, kumbe kuna watu wanastahiki zaidi yangu mimi, kumbe mimi ni mkimbizi tu,kumbe mimi,hizi kumbe kumbe ni hatari, ndio zinazaa makundi,’

‘Kwahiyo nini tena unategemea hapo, mtu kama huyu aliyekuwa kijiweni, keshakata tamaa ya maisha, mtu kama huyu anayeona anadhulumiwa, anakuja kujenga dhana kuwa ili aishi vyema ni lazima aibe, ni lazina na yeye atafute mbinu za kuchukua chako mapema, akijaribu kidogo akafanikiwa ndio basi tena, moyoni anajenga dhamira,kuwa kumbe huo ndio mfumo wa maisha, kumbe unaweza kufanya lolote ili kutafuta namna nyingine ya maisha....

'Sasa huyu mtu ndio akutane na hawa watu wa hilo kundi, watu waliojipanga, watu wanaojua udhaifu wa binadamu keshamsomea binadamu na udhaifu wake, aje akutane na wabongo mwenye njaa kali,...hawa watu sio mchezo,wenyewe ukiwaona utahisi ni wacha mungu, waadilifu, wanajua jinsi gani ya kukupika na kukupakua, mwenyewe utakubali tu, na kufanya lolote lile watakalo kushawishi nalo...., hali hii jamani ni hatari.

‘Tunaweza kuibadili hii hali, mimi nina imani hiyo kabisa, na sio jambo la kuharakisha lakini kidogo kidogo tunaweza kuwafanya wazawa wakajiona na wao ni sehemu ya nchi yao...borosheni vipato vyao, na kuwe na sheria, ya kuwalinda,..ok, mishahara sio lazima iwe sawa, lakini kuwa na mafao ya kuweza kujikimu, kila mfanyakazi ni lazima awe na bima ya matibabu, usafiri wa kufika kazini, kodi ya nyumba, ...haya yawe kwa wote,na yawekwe kwenye katiba ...

‘Na pia ili haya yawezekane, huyu mtu kutoka nje, analipwa mamilioni basi tukate kidogo kwenye malipo yake kama kodi ya kuwapooza wazawa, kama analipwa mishahara mikubwa, basi kuwa na makato ya kumfidia huyu mzawa..tukifanya hivi tutajenga uwiano, tofauti iwe kwenye mishahara, lakini marupurupu yawepo ya kumkimu huyu mvuja jasho kutoka kwenye kodi ya huyu muheshimiwa sana...

' Maana sisi tunataka kuwavutia wawekezaji, lakini wasivutiwe kuja hapa kwetu kwenye kisiwa cha amani kwa mgongo wa wazawa..tuliangalie hili kwa makini, maana sisi sio malaika, kuwa tunaweza kuishi kwa amani miaka yote, tukavumilia, tukafunga mikanda kikomo cha matundu yake, amani inavurugwa na mambo madogo madogo tu, haya ya ubaguzi,...kuwagawa watu wakajiona sio sawa na wengine. Matabaka,ya kinchi, kijinsia, kirangi,kidini, kikabila, kiwenzetu, haya ni mabaya sana...

Chuki hazianzi mara moja kama mnavyofikiria nyie, chuki zinaanzia chini kwa chini, watu wanalalamika, hawasikilizwi, wakitokea viongozi wao wanaojaribu kuwatetea wanakamatwa, wanawekwa ndani, wanauliwa kiujanja...hivi tunakuza jambo tofauti na tunavyofikiria kuwa nguvu inasaidia,..haisaidii inapumzisha kwa muda, chuko zipo moyoni, zinasubiri nafasi...

‘Tukitumia nguvu, tukaona ndio njia muafaka, huku chanzo cha yote hayo kipo, kinajulikana, lakini kwa vile ni kwa masilahi yetu, hatutaki kuleta mabadiliko, tutazidi kuwajengea chuki wananchi, hasira visasi vinajijenga chini kwa chini, itafika muda watu watasema basi liwalo na liwe,...

'Mimi nimefanya utafiti mkubwa tu,  hayo ninayozungumza yapo makazini hasa makampuni wa watu binafasi ambapo kuna wafanyakazi wengi, kuna ubaguzi wa kipato, ukienda mitaani kuna ubaguzi wa maeneo, huku ni kwa wakubwa, nyie msioweza kujenga nyumba nzuri ondokeni,...mnamfukuza mzawa aliyewahi eneo hili likiwa pori, kwanini hao wakubwa wasiende kuanzisha makazi yao huko maporini...si wanauwezo..chungeni sana, vita vya kudai maeneo, chungeni sana umiliki wa ardhi kwa wasio wazawa ...hili ni balaa jingine tunajitakia

‘Mimi siwatetei wale wanaoanzisha makundi haramu, mimi siwatetei wale wanaoleta vurugu, ila naupinga utendaji mbovu, ambao ndio chanzo cha yote hayo,napinga ile hali za kuwabagua watu, wanaokuja wanapewa masilahi makubwa kuliko wazawa hata kama kazi wanayofanya ni moja, huu ni ubaguzi...wapeni haki zao stahiki kila mmoja bila kujali utofauti wao wa kiitikadi, kabila, utaifa ...tutaweza kufanikiwa kwa hilo

'Jamni , hilo linawezekana lakini ni mpaka hawa waheshimiwa, hawa watendaji wajishushe, na kuiona hiyo hali..tatizo watendaji wapo matawi ya juu, toka lini mwenye shibe akamjua mwenye njaa, haiwezekani...

'Kwahiyo kosa limejengwa na ile hali ya kujilimbikizia, huyu mkubwa anapata mshahara mnono, gari la bei mbaya, nyumba bora, bado anapewa mafungu mengine mengi zaidi ya mshahara wake, huyu wa chini,ana mshahara mdogo, bado hastahili kupata hayo mafungu mengine ya mrupurupu, anakatwa kodi, anapata shida ya usafiri, hana bima ya matibabu, gharama kubwa za ada za watoto...yaani pesa yote aliyolipwa inaishia njiani, basi tumuangalia na huyu namna gani tunaweza kumchangia katika gharama za kimaisha..

‘Jaribuni kujenga ubinadamu, jishusheni chini, muangalia hali halisi,punguzeni marupurupu kwa wakubwa na hizo punguzo wepeni walalahoi, hivi hamuwezi kukaa na kujiuliza huyu mtu anaishije, je ya huyu mtu itatulia vip kiakilii, hivi kwa hali kama hiyo huyu mtu atakuwa na uzalendo wa nchi yake..hilo halitawezekana, hata kama tutachonga rungu kubwa la dola, hawa watu watarubuniwa, na amani itakuwa na mashaka..

‘Mimi nikachukuliwa kuweza kulifichua hili kundi..nikapewa kazi ya kuzunguka, kutafiti, na  kupata maoni ya wananchi,..mwanzoni nilifanya vyema tu, nikakabidhi kazi yangu hiyo kwa wahusika, , mmmh, hutaamini, ilichukuliwa ikawekwa kapuni, mimi nikarudi kijijini kwangu nikiwa nimelipwa ahsante yangu, nikapaua kabanda kangu ili nipate sehemu ya kuanza umauti wangu..

Nayazungumza haya kwa uchungu mkubwa, kiukweli, kama mtu atakuwa muaminifu, akatumia mshahara wake bila mbinu nyingine yoyote, hawezi kujenga, nazungumzia wafanyakazi serikalini,....hutaamini mimi mpaka nastaafu nilikuwa na kabanda kabovu tu, ningewezaje kujenga kwa kipato nilichokuwa napata, mimi sikuwa mwizi,..nilikuwa mcha mungu, mchapakazi, muadilifu na faida yake ndio hiyo...

Nikiwa kijijini natafakari kile nilichokipata, nikajiwa na kijana, alikuwa kiongozi mpya wa kitengo nyeti tu, alikuwa kunitembelea, na katika mazungumzo yetu tukafikia kuelezea ile ripoti yangu niliyoipeleka huko kwa wahusika, kumbe na yeye alishaiona, na kumbe kuja kunitembelea likuwa na nia ya kuniingiza kwenye mtandao...

Mwanzoni sikujua, yeye alianza kwa kunisomesha, alianzia mbali, maisha yalivyo, hadi akafikia hatua niliyo nayo, baadaye akaniuliza;

‘Je mzee ina maana wewe umeshajiandaa kwenda peponi...’

‘Kwanini kijana..?’ nikamuuliza

‘Hivi wewe una njaa, umelima ukavuna, mazao yakachuliwa na wengine, utakuwa na moyo wa kuendelea kulima?’ akaniuliza

‘Siwezi, nitavunjika moyo...’nikasema

‘Mzee, sisi tunakupa nafasi nyingine,..pepo yako inaanzia hapa hapa duniani, umeteseka vya kutosha, umajituma vya kutosha, na kazi uliyoifanya ni nzuri sana, unawajali watu wako na nchi yako,sasa ni wakati wako wa kula, na wewe angalau uipate pepo yako, kuanzia hapa duniani....’akaniambia

‘Unajua hawa vijana wa siku hizi ni wasanii kweli kweli, wanajua kuitumia lugha kisanii, nilimuelewa ana lengo gani, lakini mimi nilijifanya sijui, ..baadaye akanisomesha, akanijenga ajuavyo yeye, na mwisho akasema;

‘Mzee, sisi tunakupa kazi ile ile...lakini sasa angalia masilahi yako,....angalia familia yako, ona wenzako, watoto wao wapo wapi, ona wenzako wamewekeza nini, na wewe unataka kufanya nini, hata hiyo pepo, itakuwa haina thamani wako kama nyuma umeacha familia inateseka, inanung’unika...

‘Huko nyuma umeacha, familia masikini, familia ambayo itakimbilia kuuza madawa ya kulevya, je kweli watakuwa na nafasi ...tunakupa nafasi, upate kipato usomeshe watoto wako, uwekeze ila familia yako ije ipate mahali pazuri hata pa kufanyia ibada, wakuombee, sio wawe wanakulaani kuwa mzee hukuwaachia kitu, ikifika muda wa kupeleka ripoti, unavunga vunga siku zinakwenda, ndivyo wenzako wanavyokula....’akatulia

‘Hebu niambieni, ni nani asiyetaka maisha bora, hebu niambieni ni nani asiyetaka watoto wake, familia yake, iishi maisha mazuri....tuweni wakweli, ...’akasema na watu waliokuwa wametulia wakaanza kunong’ona..na mzee akamuangalia hakimu na kusema;

‘Muheshimiwa hakimu hata wewe unayataka hayo maisha mazuri, ukumbuke ulikotoka, na sasa umefikia fmilia uzeeni, huna kitu, unajutia jinsi ulivyojitesa kwa nchi yako,na sasa umestaafu huna kitu,..sema ukweli wako na mungu wako anakuona,.....’akasema

`Sasa muheshimiwa hakimu naomba mtege sikio muone ni nini nilichokifanya, na kwanini hayo mauaji yalitokea...’akasema na hakimu akaangalia saa yake

NB: NIKUULIZE NA WEWE , je WEWE hutaki maisha bora, ?


WAZO LA LEO: Wafanyakazi ni sawa na familia yako nyumbani, wewe kama bosi, wewe kama muwekezaji, wewe kama muheshimiwa waangalie wafanyakazi wako kama unavyoiangalia familia yako nyumbani, kwa uadilifu na hekima, ukifanya hivyo, tija, na uzalishaji utaongezeka, lakini kama utakosa uadilifu katika utendaji wako, ukawabagua wafanyakazi wako kwa namna yoyote ile, haki ikawa haitendeki, tegemea kushuka kwa uzalishaji,..., na huo ndio mwanzo wa uvujifu wa amani. Amani ya kweli huanzia nyoyoni, punguzeni manung’uniko, kwa kuwa waadilifu kwenye sehemu zenu za kazi.

Ni mimi: emu-three

No comments :