Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, June 9, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-73


Kesi ikaahirishwa na wakati huo askari wa fanya fujo uone walishatanda kuzunguka hiyo mahakama, eti kuja kukabilia na vurugu zilizosababishwa na mdada, nahisi taarifa zilienda vibaya kuwa kuna watu wameleat vurugu mahakamani,...nikajiuliza hivi kweli hao askari wangeliingia humo ndani kipindi kile wangeliweza kumkamata mdada, kwa jinsi alivyokuwa, labda wangempiga risasi..

Nikawa najiuliza jinsi gani mdada alivyoweza kuniinua hewani na wakati keshajiandaa kunirusha, akaishiwa nguvu na kudondoka, na mimi akili ilishanipaa nilijua kuwa nimesharushwa, kumbe, ni kwa vile mdada aliniachia wakati yeye anadondoka.

Aliponiachia nilimdondokea , nikawa nimelala kichwa changu kikiwa tumboni kwa mdada, na wakati huo docta alikuwa ameshifika akiwa na sindani yake mononi tayari kumdunga mdada, lakini lipoona mdada katulia pale sakafuni, akasubiri, kidogo na mimi nikawa nimajiinua na kujikagua kama nipo sawa, nikasimama na docta akasema;

‘Haina haja ya kumpiga sindani,....’akasema na mimi nilipoona sina tatizo, nikawa nimesogea mbali na mdada, nikionyesha wasiwasi tayari kukimbia na docta alipoona nipo vile akaniambia;

‘Usiwe na wasiwasi hawezi kufanya kitu tena...’akasema huyo dakitari, na mara polisi wawili wa fanya fujo uone wakawa wameingia na vifaa vyao, dakitari akawaambia

‘Ni vyema mkaondoka tu, hawezi kufanya lolote, akiwaona mlivyo hivyo inaweza hali yake ikamrudi tena...’akasema na kiongozi wao akawa kama anakaidi akaja kumkabili mdada, akisema

‘Hivi kweli mtu huyu mmoja anaweza kuleta hizo vurugu, ..haiwezekani...’ akasema huyu askari, na wakati huo mdada akaanza kupata fahamu, akajiinua na kukaa vyema.

‘Waulize wenzako...’akasema docta akimaanisha awaulize askari polisi walioumia , wengine walishakimbizwa hospitalini, na yule askari wa fanya fujo uone akamuangalia mdada kwa dharau, akasema;

‘Huyu ni lazima twende naye mahabusu , hawezi kuizalilisha mahakama, huoni kuwa kafanya kitendo kisichokubalika, au kulikuwa na watu wengine wametumia mwanya huo kuleta vurugu…?’akasema kama anauliza

‘Hujafanya hayo kwa akili yake,amefanya hayo bila kujua alichokifanya, mimi ni dakitari bingwa wa mambo haya, ni vyema ukanisikiliza kuliko kutumia jaziba, na ni vyema tukafanya haya kwa ajili ya afya ya huyu binti, aliyoyapitia sio kusudio lake, anahitaji kupumzika, na nashauri sio vyema kumpeleka huko mahabusu, haitamsaidia yeye, mtazidi kumuumiza kisaikolojia…’akasema huyo dakitari.

Yula askari akamuangalia tena mdada halafu akageuka kuwaangalia wenzake, akawatolea ishara ya kuondoka, na kweli wakaondoka na kumuacha mdada akiwa na dakitari wake…
‘Kwani nimefanya nini docta..?’ akauliza mdada akiwa bado yupo kwenye mshangao, huku akiangalia huku na kule.

‘Naona walikushitua ubongo ukawa umechanganyikiwa tena,lakini nakuhakikishia kuwa haitatokea tena, kwani mara nyingi mshituko kama huu hutokea mara mbili ya tatu, inakuwa kubwa,…na inakuwa ndio ya mwisho, nina uzoefu na hilo, utapona kabisa sasa, na itafuta hatua nyingine uonane na dakitari wa maswala ya uzazi…’akasema

‘Hata sielewi,ina maana watu wametoka wote, kesi imeisha…’akauliza akageuka kuniangalia mimi

‘Mhh,imeahirishwa…’nikasema

‘Oh,hata sielewi,…nakumbuka nilikuwa natoa ushahidi,…halafu yule wakili akaanza kunifokea, oooh,sijui,kilichotokea baadaye, kichwa kilianza kuniuma, na ghafla akili sikujitambua tena,...mm huyo wakili yupo wapi, au nimemuumiza, mbona siwaoni, mawakili wengine, mmh, jamani hebu niambieni ukweli kumetokea nini…’akauliza

‘Mdada nafikiri ni bora ukapumzike kwanza, ili upate nguvu,hizi dawa ukizinywa zitakufanya ulale sana, na ukiamuka, utakuwa umetuliza kichwa chako,cha muhimu ni kukwepa mambo ya hasira…’akasema

‘Lakini mambo mengine yanaletwa na watu unaweza ukajizuia, lakini watu wasiojua tatizo lako ni nini wakakuchokoza..yule wakili aliambiwa hakusikia…’nikamtetea mdada

‘Kama alikuwa anabisha natumai sasa wamejionea wenyewe, sijui hakimu atasemaje,maana nilivyomuona sijui kama ataweza kusema usimame tena mahakamani kutoa ushahidi..’nikasema huku nikicheka

Mdada aliniangalia huku akikunja uso,nafikiri alikuwa akijaribu kuwaza jambo, au kujaribu kukumbuka hicho kilichotokea,halafu akasema;

‘Mimi nataka nisimamishwe tena kutoa ushahidi nataka niseme,ukweli wote bila kuficha, naona ndio wakati muafaka kila mmoja asema kila anachokijua ili hili tatizo lifikie mwisho,nimechoka na hili tukio, ….’akasema

‘Mimi nafikiriumeshasema kila kitu,kwani kuna ukweli gani uliobakia?’ nikauliza

‘Kuna mambo mengi yamejificha hapa, kufa kwa mtoza ushuru ni sehemu ndogo tu, lakini mara nyingi kunapotokea mauji kinachoangalia ni kile kifo, ni nani kamuua, …basi,lakini chanzo mpaka ikafikia…’akatulia kidogo, halafu akauliza

‘Mpelelezi yupo wapi, …ni muhimu ule ushahidi wote uwepo, nafahamu yeye anajua mengi sana, mimi naona ni muda muafaka mimi na yeye tukaweza kuungana na kulimaliza hili tatizo…’akasema mdada na kunifanya nimuangalia kwa mashaka.

‘Mdada unayaongea hayo kwa dhati kweli, au ….?’ Nikauliza

‘Unakumbuka tulipoitwa na mzee, baba mkwe wako, kuna jambo alilisema,kwakweli sikumuelewa huyo mzee, inaonekana kuwa huyo mzee anafahamu mambo mengi sana, mimi nimekuwa simuamini….’akasema

‘Kwanini…?’ nikauliza

‘Nataka nione naye kwanza, …..ni muhimu sana niongee naye na nikiongea naye, nataka nisimame tena kutoa ushahidi wangu, nataka nipambane na huyo wakili wao kwa hoja…yeye aliniandama kwa vitisho na kunishuku kuwa mimi ndiye niliyemuua mtoza ushuru,…ni lazima hili liwekwe wazi mbele ya mahakama…’akasema

‘Huwezi kuzidiwa tena, ukaleta fujo?’ nikauliza

‘Kwani mimi nilileta fujo…?’ akauliza akionyesha mshangao, na docta wake, alikuwa akimuangalia mdada kwa makini, akasema;

‘Mdada ni bora kwanza ukapumzike,…nataka kukupa dawa na hizo dawa ukizitumia, unatakiwa kulala, zitakusaidia sana….’akasema

‘Hapana docta, hili ninalotaka kulifanya halitakiwi kusubiri, nisipoliweka hili wazi mapema,jamii itanishuku mimi vibaya…nyie hamulioni hili,kuwa sasa hivi mlinzi haonekani tena muuaji, hiyo hatia imesukumwa kwangu...’akasema

‘Lakini…’nikasema na mdada akanikatisha.

‘Wewe huijui jamaii ilivyo,mara watu wengi wanapenda kuyachukulia mambo juu kwa juu bila kufanaya utafiti,na sijui huyu hakimu atakuwa na maamuzi gani, hebu niwaulize je hakimu alisema nini,…?’ akauliza

‘Alisema kesi imeahirishwa, hadii takapotajwa tena…’nikasema

‘Mhh, kwahiyo kauli hiyo aliitoa baada ya vurugu, …ina maana mimi nilisababisha kesi kusimama…hapana, lakini kwanini hawakumsimamisha yule wakili kuniandama kwa maswali yasiyo na ukweli…kuna nini hapa..?’ akauliza

‘Pale nahisi wengi walihisi wewe una mashetani, na yule wakili alikuwa akiyakemea,ili yakutoke,kwahiyo kukawa na kitu kama imani,wanavyoamini watu wengine….hata mimi niliona ajabu kwanini wakili yule alipokuwa akikiuliza maswali, na akaambiwa aache,hakuacha,akawa anaendelea tu, na hakukuwa na jitihada za kumsimamisha…’nikasema

‘Ngoja nionane na hawa watu wawili, hasa huyo mzee,aliyekuwa baba mkwe wako….’akasema na kuniangalia huku akionyesha tabasamu la kulazimisha pale alipotamka neno hilo `aliyekuwa..’, nahisi alikuwa na maana yake, nikasema;

‘Sizani kama watakuruhusu kumuona, shangazi hawezi kukupa nafasi hiyo..’nikasema

‘Hana ubavu wa kunizuia mimi, wewe utaona, mimi sio wewe….’akasema na akageuka kumuangalia docta na kusema

‘Tafadhali docta hili tatizo nataka liishe haraka iwezekanavyo,na likiisha nitakuwa mgonjwa wako kamili,ili nipone kabisa…sizani kama nitakuwa na kazi nyingine baada ya hii,nataka kupumzika, na mimi natamani kuwa mama wa nyumbani, hata kama siwezi kupata mtoto…’akasema na docta akatabasamu

‘Mhasibu, …’akasema mdada akiniangalia mimi machoni, mimi nikamuangalia, nay eye akasema;

‘Unakumbuka niliwahi kukuuliza swali, uje kunipa jibu baadaye, natumai sasac umeshapata jibu, kama una majibu yake natumai muda wa kuniambia umefika, kabla mimi sijachukua maamuzi mengine,…’akasema na mimi nilitaka kumuuliza swali gani, lakini yeye akaendelea kuongea, kwa kusema;

‘Mimi nafahamu henda hata wewe utakuwa na uwoga wa kuishi na mimi,baada ya kushuhudia yote yalitokea, kuwa labda mimi nina mashetani, nitakuwa nakusumbua, lakini kiukweli, mimi sina mashetani, docta huyu hapa anafahamu tatizo langu ni nini, na kaniahidi kuwa litakwisha….’akasema na docta akasema;

‘Hayo sio mashetani,…ni ugonjwa unaotokana na mashinikizo ya ubongo, kutokana na madhila aliyopambana nayo, ambayo yameanzia utotoni, na baadaye akaja kukabiliwa na mjanga ya kudhalilishwa, hadi kuharibiwa kizazi, …yote hayo yakajenga kitu kwenye ubongo wake, chuki, na kutaka kulipiza kisasi…’akasema docta

‘Docta ndio awe na nguvu za namna hiyo , aweze kuongea kama….mwanaume,ananguruma kama simba…hapana docta, mimi nahisi hayo ni mashetani…’akasema

‘Wewe utaona tu, hili ni swala la muda, tatizo ni kuwa tangu nianze kumuhudumia mdada ,sijapata nafasi ya kukaa naye kwa karibu kama nilivyomshauri, nilitaka yeye afuatilie masharti yangu,...nilitaka atulie...aachane na kazi za kumvuruga akili yake, lakini hakutaka, sasa inakuwa vigumu sana…’akasema docta

‘Au kuna watu wanataka iwe hivyo ili wakamilishe mambo yao kwa kukutumia hayo matatizo yake aliyo nayo….?’ Nikauliza na mdada akawa kama anawaza jambo na mara simu yake ikalia, ilikuwa kwenye mlio wa kunguruma tu, akaangalia na kusema;

‘Mzee anapiga sijui anataka nini….’akasema na kuipokea alisikiliza kwa makini bila kusema neno baadaye akasema;

‘Sawa mzee nitakuja kuonana na wewe…lakini iwe mara ya mwisho, nimeshakuelezea msimamo wangu, na nataka usiyahusishe haya na mambo binafsi,binti yako anatakiwa kukubali ukweli, yaliyotokea kwake ni bahati mbaya,….’akasema na kusikiliza kwa makini halafu akasema;

‘Kama ni hivyo sawa tutakuwa pamoja,na nikija hapo, sitaki kukutana na huyo shangazi,maana tutaishia kubaya mimi na yeye hatuivani, kama ni mambo ya uchawi,yeye ndiye mchawi,mimi sijui chochote kuhusu uchawi…’akasema na kutulia kusikiliza, halafu akasema

‘Yeye  ndiye anasema hivyo nakutangaza kwa watu hivyo,na mimi sina mashetani…hizo ni dhana za watu wenye imani hizo za kishirikina, mimi nina tatizo linalotambulikana kitaalmu na litakiwsha tu….’akasema

‘Sawa nitakuja mzee, muda sio mrefu, nipe dakika kumi, mimi sijambo, usiwe na wasiwasi na mimi, yah, yupo hapa, anasubiri kauli ya mahakama,...ndio yupo docta wangu, kutokana na yaliyotokea , natumai umeambiwa, …’akatulia kusikiliza halafu akasema

‘Ndio, nitakuja, nije na yeye, kwani yeye anahusikana vipi na hayo,sitaki kuwahusisha watu wengine, yeye na mimi ni maswala binafsi,…kwanini unataka nije na yeye?, hapana mzee ,kwanza ni lazima tuongee wawili, tukimaliza anaweza kuja mkaongea naye, hutakufa mzee, kwanini unasema hivyo, wewe sio mungu, na kuumwa sio kufa, haya mzee nakuja…’akasema mdada na kusikiliza kwa muda, halafu akakata simu na kusema;

‘Huyu mzee kachanganyikiwa, anasema anataka kusema ukweli wote, na hana muda mrefu wa kusubiri eti siku zake za kuishi zimekwisha,…naona keshakata tamaa ya maisha, …’akasema mdada na kunifanya mimi nianze kujilaumu, kwani huyo mzee kanisaidia sana, na kama kafikia hiyo hali ni muhimu niweze kuongea naye, ili angalau niweze kuonyesha huruma na fadhila zake,nikasema;

‘Ni muhimu nionane na huyo mzee…’nikasema

‘Ndivyo anavyotaka yeye hakujua kuwa umekamatwa tena, anataka mimi na wewe tuonane naye pamoja, lakini nijuavyo mimi ataanza kuingiza mashinikizo yake kwako kuhusu binti yake, yeye anampenda sana binti yake, hatakubali wewe utoe kauli ya kumkataa mbele yake,..’akasema mdada kwa sauti ya utulivu.

‘Na kwa hali aliyo nayo ukitoa kauli knyume na matarajio yake huenda itamuumiza sana, japokuwa shangazi yeye keshatoa maamuzi, sijui kwa huyo mzee, yeye ana kauli gani, sasa maamuzi ni yako...ila ,nikujuavyo wewe hutaweza kusema ukweli,…utakubali tu kumrizisha huyo mzee, na hilo mimi sitaweza kuvumilia, ni bora uje utoe kauli yako wakati mimi sipo,....’akasema kwa sauti ya huruma na sio kama yule mdada niliyemfahamu kabla.

‘Niliwahi kukuuliza kabla kuwa je upo radhi kuoa, na kuishi ukiwa huna mapenzi moyoni...uoe,kwa sababu tu ya baba mkwe, hukuwa na jibu la kujiamini, ukawa unasema eti kwa vile, ulifanya hayo makosa, kwahiyo...ooh, ...’akawa anatikisa kicha halafu akasema

‘Kiukweli,mimi sasa nimechoka, huenda ni vyema na mimi nikawa na maamuzi magumu, japokuwa nakupenda, japokuwa nilitarajia mengi kutoka kwako, lakini je mwenzagu unaweza kujiamini ukatoa maamuzi ya kutoka moyoni kwako kwa ujiamini japokuwa yataumiza wengine, sasa upo tayari kuyatoa majibu hayo kwa baba mkwe...'akasema

'Ila mimi sitaki uyatoe hayo nikiwepo, ili isije ikawa mimi ni sababu, hata hivyo, nikuonavyo huenda ukajibebesha zigo usilioweza kujitwika, ni bora mimi nianze, tukijaliwa basi au unasemaje…?’ akaniuliza

‘Mdada nilishakuelezea kwanini nimeamua kufanya hivyo, na ni vyema kwanza nikaongea na mzee nikajua msimamo wao....napenda sana niwe na wewe, kwani kiukweli moyo wangu kila mara unakuwaza wewe, sijui nitaishije bila ya wewe....’nikasema na mdada akawa kama analazimisha kutabasamu,

‘Mdada kiukweli mimi nataka wewe uwe karibu yangu wakati wote, kwa kipindi nilichojuana na wewe nakuona kama sehemu ya mwili wangu, lakini nitafanyaje sasa, sijui kwakweli mdada...’nikasema na nilijaribu kumuangalia docta kama anatusikiliza , lakini nilimuona akihangaika na mambo yake, na mimi nikaendelea kusema;

‘Mdada, hivi wewe huoni kuwa nitakuwa nimefanya unyama, nikitoa kauli ya kukataa mbele ya baba mkwe, na hali aliyo nayo kwasasa, wewe hujui niliyoyafanya kwa huyo binti yake huko nyuma, ni kweli ulikuwa ni ujana, unanisumbua, lakini nilifanya vibaya, na nikajifunga kwa kuahidi mbele ya wazazi wake kuwa nitamuoa...’nikatulia

‘Sasa naanza kujuta, najuta sana mdada kwa hayo niliyoyafanya , lakini nifanye nini kwa sasa,..nashindwa , na sijui kama nitaweza kumsaliti huyo mzee, kwa mambo mengi aliyonifanyia,...pia huyo binti yake ana mtoto wangu, hebu niambie mdada kama wewe ungelikuwa katika nafasi yangu au wewe ungelikuwa huyo binti ukafanyiwa hivyo ungelifurahi…’nikasema mdada alikunja sura na kusema;

‘Lakini wao wenyewe kwa kauli yao wamesema hawakutaki tena umchukue binti yao, wewe umekuwa chanzo cha matatizo kwa binti yao, na wameshataifisha mali zako, kutokana na mkataba mliowekeana...sasa ukiendelea kung’ang’ania sijui watakuelewa vipi, ...je ni kwamba unampenda huyo binti, au unataka tu kulipa fadhila...?’ akawa kama ananiuliza halafu akasema

‘Ok, mimi sijui, sasa hayo utajua wewe mwenyewe, kwasasa mimi nina mambo muhimu ya kufanya, nikiyamaliza kama hujanipa jibu, huenda tusionane tena...’akasema mdada

‘Una...’nikataka kusema kitu lakini nikashikwa na kigugumizi, na wakati huo mdada alikuwa amemgeukia docta, na docta akawa anafunga funga vitu vyake kuondoka, na alipoona mdada anamuangalia yeye akasema;

‘Hayo ni mambo yenu binafsi, nisingelipenda kuyaingilia, ila eeh, samahani kwa nitakalosema, kwani mimi kwenu ni mkubwa , na licha ya utaalamu wa udakitari lakini pia nina uzoefu wa maswala ya ndoa, kwahiyo sio vibaya nikachangia jambo hasa kwako wewe mhasibu, niyasema haya kwa nia njema, mhasibu, jaribu kuwa makini, hasa katika swala la ndoa...’akasema docta.

‘Mimi nimeshaoa, na kama ingeliwezekana kurudia nyuma, huenda ningelikuwa makini sana katika kuchagua mwenza wa maisha, nisingeliharakisha, sasa mimi nisingelipenda na wewe mhasibu ukaja kujijutia, kaa chini, panga,jiulize na ujipime, …akasema docta

‘’Nikuambie kitu kufunga ndoa ni pa-pa, utashangiliwa, sherehe nk, ...lakini maisha ya ndoa na wewe na mwenza wako, wenzako watakuwa hawapo tena, na hayo maisha ni safari ndefu,...’akasema huku akiweka mkoba wake begani.

‘Mimi nakumbuka wakati naoa,niliambiwa ndoa ni nusu ya imani yako,...kwa muda ule sikuelewa, maana akili ilikuwa na hamu ya kuingia kwenye chumba hicho cha ndoa, nikijua ni maisha rahisi tu, na kama nimekosea, nitamfunda mwenzangu maisha yataendelea ikishindikana si basi bwana nitaacha nitaoa mwingine,...ilikuwa hivyo, lakini sio rahisi kihivyo....’akasema docta

‘Kwanini walisema ndoa ni nusu ya imani,..ukiangalia kwa makini ndoa ni imani, maana unaoa, na unatakiwa ufuate masharti ya ndoa, kwa siri na kwa dhahiri, hiyo ni imani. Ni imani iliyokunga na hapo huna ujanja,..ukiiba uachepuka moyo unakusuta, mwenyewe unajihisi umefanya dhambi,..unaona hapo, imani .  Na ndio maana hapo unatakiwa ujipime,...

‘Unatakiwa ujipime kwasababu maisha ya sasa sio yale ya kale, ya akina baba,au babu zetu , hayo yalikuwa enzi zao, watu wanaoa, hata kama hawajuani, kinachohitajika kwa kipindi kile ni mwenza wa maisha, na maar nyingi wao walikuwa wakiangalia vigezo vya kijamii, ....lakini sio sasa, maisha ya sasa yana mitihani mingi, ndio maana kabla ya kuoa, unatakiwa ujipme kiukweli kama kweli unaweza kuishi ndani ya ndoa, ...usifuate mkumbo tu baba...’akasema na kutulia

‘Kwani hapo ukifanya makosa, ujue nusu hiyo ya imani ya maisha yako ambayo ni moja ya mihimili ya maisha ya ndoa itakuwa imevurugika, utakuja kujuta maisha yako yote …kwahiyo ni muhimu ukajiuliza wewe mwenyewe; je nipo tayari kuoa, na kama nipo tayari ni nani anafaa kuwa mke wangu,..’akatulia na huku mdada akiwa kashika shavu sijui alikuwa akimsikiliza docta au alikuwa akiwaza yake.

‘Nikuambie ukweli, kila mmoja ana mapendeleo yake, wengine wanaangalia sura, wengine wanaangalia mali, wengine hiki na wengine kile,. ...ukiambiwa uorozeshe hayo mapendeleo ya watu kuhusu mke au mume gani anayefaa kwake, huwezi kuyamaliza, lakini muhimu sana ni upendo wa kutoka moyoni...’akasema na kushika kifuani

‘Usifanye kosa hapo ukasema unaoa tu, eti wengine wanafanya hivyo kwasababu ya yale yaliyotokea nyuma kwa mfano unaoa kwa vile baba na rafiki yake wameshibana,au mlisoma wote, au...mwingine kwa vile baba mkwe alimfadhili, mwingine...’akatulia akionyesha mikono kwa ishara.

‘Hayo ninayokuambia yapo, lakini ukumbuke ndoa sio maisha ya muda mfupi, ndoa sio sehemu ya majaribio....itafika muda utakumbana na mitihani, vishawishi, utashindwa kuvumilia, na wakati huo mna watoto, unafikiri utafanya nini hapo...je kama ulioa kwa ajili ya fadhila, ndio basi tena, na sijui kama fadhila zinalipwa hivyo, ..hapana jaribu kufikiri zaidi….’ akasema

‘Mimi nakushauri, kabla hujatoa maamuzi ya nani umuoe, hebu chuja moyo wangu, hebu weka maisha yako mbele zaidi na ujaribu kuhisi kuwa upo na mke wako, anakufanyia hivi na vile, ...unaweza kuangalia maisha ya majirani zako,ndugu zako , hata wazazi wako,waliowahi kuoa, ikawa ni shule kwako....’akatulia

‘Kama nilivyokuambia wengine huwa wanaoa kwababu ya upendo,...hili ni muhimu sana katika ndoa, lakini upendo wa namna gani, mtu anaweza kupenda maumbile, mwingine sura, mwingine sauti..je hivyo vitu ni vitu vya kudumu,kama sio vya kudumu vikiisha utafanya nini, mtaachana?, ....angalia hapo kwa makini,...kwahiyo upendo nao una sura nyingi tu....’akaangalia saa yake na kumtupia jicho mdada, na mdada naye akawa anaangalia simu yake nafikiri alikuwa akisome kitu kwenye simu yake.

‘Sasa ndugu, sikutaka kukuingilia sana, ila kwa vile nimesikia mkiongea maswala ya ndoa,nikaona niwasaidie kwa hilo, kuwa kabla hujaoa au kuolewa fikirieni kwanza, kabla hujachagua mke au mume, angalia nafsi yako kwanza, inapenda nini, na huko mbeleni hicho unachokipenda kitakusaidia nini, lakini la muhimu ni upendo wa kweli, wa kutoka moyoni..’akashika tena kifuani.

‘Ukiwa hivyo ukawa unampenda mwenza wako na yeye akawa anakupenda mtafurahia sana ndoa yenu,kwani amani na upendo vitatawala ndani ya nyumba yenu, na mtapata kizazi bora, hata neema za riziki zitaongezeka....kumbuka ndoa ni sehemu ya kutuliza kichwa, ndoa ni sehemu ya kupendana , ndoa ni raha, na kamwe ndoa haikupangwa iwe ni karaha, kwahiyo ni muhimu umuoe mtu wa chaguo lako, mtu unayempenda, usichukue maamuzi kwa shinikizo fulani……’akasema

Mdada akawa katulia tu, na mimi nikawa naangalia chini nikishindwa la kusema chochote, halafu mdada akasema;

‘Docta naona kama niwaache, maana muda umetaradadi, ila ni muhimu nikamuone mzee, halafu baadaye nitakuwa na kikao na mpelelezi, naona kanitumia ujumbe wa kukubali kukutana na yeye, na kama mambo yatakwenda vyema, basi nitakuambia wapi nitakuwa tayari kwa matibabu yangu, nina imani kuwa safari hii nitatulia…’akasema na kuanza kuandoka, hakuniangalia..nikajihisi mpweke, nilitaka kumuita lakini sikuweza...

‘Hata mimi naondoka, sijui kama watakurudisha huko rumande au ndio dhamana imepita,....lakini mimi nakutakia kila laheri, usikate tamaa, na mimi nisingelipenda ukawa na pupa ya kuoa haraka kama hujajiweka sawa..usifuate shinikizo, acha haya yanayokukabili yapite, halafu ukitulia, mambo yatajileta...’akasema na kunishika mkono akawa kama ananikumbatia kidogo, alafu akawa anaondoka, nikasema;

‘Ahsante sana docta, ...’nikasema na sikuweza kusema zaidi nilihisi machozi yakinilenga lenga sijui kwanini,...

Nilibakia pale mahakamani nikiwa nimeduwaa,baadaye nikatoka, nikitarajia nitakumkuta mdada hapo nje, ili tuongozane, lakini sikuona gari lake, nikajua ameshaondoka, nikaingia kwenye gari langu na kuanza kuondoka ,moyoni nikiwa nawaza maneno ya docta;

..Ujue ndoa ni safari ndefu, na ndoa inakuwa nusu ya imani yako, ina maana ukikosea hapo tu, ujue nusu hiyo ya imani ya maisha yako ambayo ni muhimili muhimu wa ndoa yako utakuwa umeharibika, …kwahiyo ni muhimu ukajiuliza wewe mwenyewe je unaoa, kwasababu ya yaliyotokea huko nyuma, kama vile kulipa fadhila, au….’
Au unaoa kwa sababu ya upendo, na amani katika maisha yako ya baadaye, jiulize kwa makini maana ndoa ni upendo, ndoa ni ya raha, ndoa sio karaha, na ili uyapate hayo ni muhimu umuoe mtu wa chaguo lako, mtu unayempenda, usichukue hayo maamuzi kwa shinikizo fulani…

 NB: Darasa la ndoa kidogo,

WAZO LA LEO: Ni msimu mwingine wa ndoa, na wale waliojaliwa wapo mbioni au wanafunga ndoa.Ni muhimu sana, watu kabla ya kuingia kwenye kitengo hicho muhimu cha maisha,wakapitia darasa la ndoa, angalau mtu kujua ni nini maana ya ndoa, na ndani ya ndoa kuna nini, na natakiwa nifenye nini.


 Ndoa nyingi sasa ni maumivu, na hii ni kutokana na kuamua kabla ya kujifunza. Elimu ya ndoa ni muhimu sana, tujue, na tuwe na maamuzi ya uhakika, ili tukioa au kuolewa tuwe tumechagua mke au mume mwema, kwa ajili ya matunda mema.Tukumbuke ndoa ni raha, na haikutakiwa iwe ni karaha

Ni mimi: emu-three

No comments :